8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI
﴿كَانَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً فَبَعَثَ اللَّـهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ وَمَا اخْتَلَفَ فِيهِ إِلَّا الَّذِينَ أُوتُوهُ مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ فَهَدَى اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا لِمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِهِ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴾
213.Watu wote walikuwa wa mila moja. Basi Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii watoao bishara na waonyao. Na pamoja nao akawateremshia kitabu kinachoshikamana na haki ili kihukumu baina ya watu katika yale waliohitilafiana. Na hawakuhitilafiana katika hayo ila wale waliopewa Kitabu, baada ya kuwafikia ubainifu, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu akawaongoza kwenye haki walioamini katika yale waliyohitilafiana kwa idhini yake. Na Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye kwenye njia iliyonyooka.
WATU WOTE WALIKUWA MILA MOJA
Aya 213
LUGHA
Mwenyezi Mungu amelitumia tamko Umma katika kitabu chake, kwa maana nyingi, kama vile Mila Mwenyezi Mungu anasema:
﴿إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً﴾
"Hakika mila yenu hii ni mila moja."
(21:92)
Au kwa maana ya kundi - Mwenyezi Mungu anasema:
﴿وَمِمَّنْ خَلَقْنَا أُمَّةٌ يَهْدُونَ بِالْحَقِّ ﴾
"Na katika wale tuliowaumba wako watu wanaoongoza kwa haki tu...
(7:181). Pia limekuja kwa maana ya muda; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
﴿وَلَئِنْ أَخَّرْنَا عَنْهُمُ الْعَذَابَ إِلَىٰ أُمَّةٍ مَّعْدُودَةٍ ﴾
"Na kama tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliokwisha hisabiwa..."
(11:8).
Vile vile kwa maana ya Imam anayefuatwa - Mwenyezi Mungu anasema:
﴿إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ ﴾
"Hakika Ibrahim alikuwa mfano (wa kufuatwa) mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu..."
(16:120).
Ama makusudio ya neno Umma katika Aya hii tunayoifasiri, ni mila.
MAANA
Kauli za wafasiri zimegongana katika kuelezea maana ya aya hii. Razi ameifafanua kwa kiasi cha kurasa saba. Ama mwenye Tafsir Al-Manar ameifafanua kwa kurasa ishirini na mbili na kumwacha msomaji wa kawaida patupu, bila ya kuambua chochote. Na sisi, kama kawaida yetu, tumo katika njia yetu ya kumfanyia wepesi yule msomaji wa kawaida, kwa kiasi kile kitakachoafikiana naye. Kwa hivyo ufafanuzi wake ni kwa uwazi na ufupi, ili aweze kuangalia vizuri Aya za Mwenyezi Mungu kwa wepesi na kuathirika nafsi yake. kama kunakuwa na maudhui muhimu, tunayaeleza katika kifungu cha peke yake.
Watu wote walikuwa mila moja.
Yaani walikuwa wa umbile ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu na ambalo Mtume(s.a.w.w)
ameliashiria kwa kusema:"Kila anayezaliwa huzaliwa kwenye fitra (umbile la usawa)."
Mwenye Majmaul Bayan anasema: "Masahaba wetu wamepokea kutoka kwa Imam Abu Jaffar al Baqir, kwamba:kabla ya Nuh(
( [9]
)watu walikuwa mila moja ya umbile alilowaumba Mwenyezi Mungu, si wenye kuongoka wala kupotea; Mwenyezi Mungu akawapelekea Mitume"
.
Kwa hivyo maana yake ni kwamba wao walikuwa ni wenye kuabudu kulingana na akili zao bila ya uongofu wa Mitume wala sharia.
Kisha wakajiliwa na mawazo na fikra ambazo ziliwapeleka katika tofauti ya itikadi na rai, hatimaye kwenye uadui. Kwa hivyo wakagawanyika vikundi vikundi baada ya kuwa ni wa mila moja. Mwenyezi Mungu akawapelekea Mitume na kitabu kinachosema kweli na kinachohukumu mizozo yao.
Haya ndiyo maana yaliyo wazi ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Basi Mwenyezi Mungu akawaleta Manabii watoao bishara na waonyao.
Na pamoja nao akawateremshia kitabu kilichoshikamana na haki ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitalifiana. Hapa inatubainikia kwamba katika maneno kuna jumla iliyokadiriwa ambayo ni:"Watu walikuwa wa mila moja kisha wakahitalifiana,
Linalofahamisha hilo ni kauli inayosema:"Ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitalifiana."
Na hilo linatiliwa nguvu na kauli hii:
﴿وَمَا كَانَ النَّاسُ إِلَّا أُمَّةً وَاحِدَةً فَاخْتَلَفُوا﴾
"Na watu hawakuwa isipokuwa wamila moja; kisha wakahitalifiana..."
( 10:19).
Na hawakuhitilafiana katika hayo ila waliopewa kitabu, baada ya kuwafikia ubainifu, kwa sababu ya uhasidi baina yao.
Yaani: Watu ambao walikuwa ni umma mmoja, kisha wakahitalifaina na Mwen-yezi Mungu akawapelekea Mitume, watu hao pia walihitalifiana katika Mtume alieyepelekwa; wengine waliamini na kusadiki na wengine wakakufuru na kukadhibisha baada ya kusimama hoja na dalili wazi za mkato. Hakuna sababu yoyote ya kukadhibisha huku isipokuwa uhasidi na kuhofia manufaa yao ya kibinafsi na uadui.
Ndipo Mwenyezi Mungu akawaongoza kwenye haki walioamini katika yale waliyohitalifana kwa idhini yake.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewafikisha wenye nia njema kwenye imani ya haki aliyokuja nayo Mtume; na imani hiyo ni kwa amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Kwa hiyo makusudio ya idhini ni amri.
Na Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye kwenye njia iliy onyooka.
Katika kufasiri Aya ya 26 ya Sura hii kifungu cha uongofu na upotevu, tumetaja maana ya uongofu ambayo miongoni mwake ni: Kukubali mtu nasaha na kuzitumia; na hayo ndiyo makusudio yake hapa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaafikisha watu wema kukubali nasaha na kufanya vitendo vya haki na heri.
TOFAUTI KATI YAWATU
Kulipatikana kutofautiana kati ya watu tangu Qabil alipomuua nduguye Habil; kunaendelea hadi leo na kutabaki hadi siku ya mwisho. Kutofautiana hakuhusiki na watu wa dini tu; kama wanavyodai wasiojua hakika ya mambo. Kwani tunaona kutofautiana kusikokuwa kwa dini kumefikia kugeuka maneno na kuwa vita vya kumalizana. Ugomvi kati ya dola za kibepari kumepelekea vita vya Atomic. Bomu lilitupwa Hiroshima kwa wanawake na watoto na dola ya kibepari dhidi ya dola nyingine ya kiberi pia. Na kugawanyika mwelekeo kwa dola za kijamaa kunaeleweka. Vile vile dola za Kiafrika na Kiesia zinatofautiana kulingana na upande wa wanyonyaji wanaozinyonya. Ama kutofautiana kwa dola za Kiarabu matokeo yake ni kupatikana Israil ndani ya nchi yao na hatimaye kusalimu amri mnamo tarehe 5 June, 1967.
Hali yoyote iwayo, kutofautiana kuna sababu nyingi, kama vile: Kutofautiana katika malezi na maendeleo, katika tabia na akili na kutofautiana kunakotokana na mgongano wa masilahi na manufaa ya kiutu. Tofauti inayotokana na maendeleo, akili na tabia inaweza kurekebishwa kwa kufanya yale yanayoafiki misingi iliyothibitishwa na elimu na majaribio. Lakini tofauti zinazotokana na kugongana kwa manufaa ya kiutu hazina dawa isipokuwa kumzuwia adui kwa nguvu. Maelezo yetu haya, ni kukamilisha tuliyoyasema katika kufasiri Aya ya 113 kifungu cha "Kila mmoja anavutia dini yake."
﴿أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ ﴾
214.Au mnadhani kuwa mtaingia Peponi na hali hamjajiwa na mfano wa wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara, na wakasukwasukwa hata akasema Mtume na wali-oamini pamoja naye: Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu.
KUINGIA PEPONI
Aya 214
MAANA
Au mnadhani kuwa mtaingia peponi na hali hamjajiwa na mfano wa wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara.
Hakika Aya hii tukufu inamwelekea kila mwenye kuamini haki, akaitumia na akailingania. Inasema waziwazi kwamba desturi ya Mwenyezi Mungu kwa wanaoinusuru haki, ni kuitolea thamani yake wao wenyewe, watu wao na hata mali zao. Vile vile kuvumilia adha na kuwa na subira juu ya masaibu na shida. Waliokuwa kabla yenu walipambana na aina za maudhi wakasubiri; Je, nanyi mtasubiri kama walivyosubiri? Au nyinyi mnataka kuingia peponi bila ya kuilipia thamani. Na mwenye pepo hiyo amekataa isipokuwa thamani yake iwe ni imani, ikhlas na kuvumilia hofu, njaa na upungufu wa mali na nafsi!
Yamekuja maelezo katika khutba mojawapo ya Nahjul Balagha: "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
alikuwa akisema: Hakika pepo imezungukwa na machukivu na moto umezungukwa na anasa; na jueni kuwa hakuna katika twaa ya Mwenyezi Mungu isipokuwa huwa machukivu na hakuna katika maasi ya Mwenyezi Mungu isipokuwa anasa. " Kwa faida zaidi ni vizuri msomaji arudie tuliyoyataja katika kufasiri Aya ya 155 kifungu 'Thamani ya pepo.'
Na wakasukwasukwa hata akasema Mtume na walioamini pamoja naye: Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini?
Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini, ni swali kutoka kwa Mtume na waumini, linaloleta picha ya misukosuko na shida walizozipata kutoka kwa maadui wa haki na makundi ya batili Maana kwa ujumla ni kwamba walionusuru haki, waliotangulia, walipatwa na shida na wakaingia katika misukosuko mpaka wakadhani kwamba nusura imechelewa, hivyo wakaitaka ije haraka kwa kusema: Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini? Mwenyezi Mungu naye akawajibu kwa kusema: Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu.
Aya hii iko katika mwelekeo wa Aya isemayo:
﴿حَتَّىٰ إِذَا اسْتَيْأَسَ الرُّسُلُ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا جَاءَهُمْ نَصْرُنَا ﴾
"Hata Mitume walipokata tamaa, wakadhani ya kwamba wamekadhibishwa, msaada wetu uliwajia..."
(12:110)
﴿يَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلْ مَا أَنفَقْتُم مِّنْ خَيْرٍ فَلِلْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا تَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴾
215.Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri yoyote mtakayotoa ni kwa ajili ya wazazi wawili na akraba na mayatima na masikini na mwana njia. Na kheri yoyote mnaoufanya Mwenyezi Mungu anaujua.
WATOE NINI?
Aya 215
MAANA
Wanakuuliza watoe nini?
Msemo unaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w)
.Sema: Kheri yoyote mtakayotoa ni kwa ajili ya wazazi na akraba na mayatima na masikini na mwananjia.
Makusudio ya neno kheri hapa ni mali. Wazazi wawili ni baba, mama, babu na bibi, kwa sababu wao wanaingia katika jina la wazazi wawili. Ndugu ni akraba wa karibu wa mtoaji, yatima ni asiyekuwa na baba, na mwana njia ni yule aliyeishiwa njiani na kushindwa kufika kwa watu wake na wala hana chakula.
Unaweza kuuliza kuwa: dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa watu waliuliza aina ya kitakachotolewa sio nani wa kumpa. Na jibu ni la matumizi sio la aina, sasa je, imekuwaje?
Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya jawabu ni kumzindua muulizaji kwamba yeye anatakikana kuuliza nani wa kumpa, sio nini atoe. Razi amemnakili Qafal kwa jibu jingine; nalo nikuwa hata kama swali liko kwa tamko la Ma (nini) lakini kilichoulizwa ni nani wa kumpa sio cha kutoa, kwa sababu cha kutoa kinajulikana.
Sheikh Muhammad Abduh ameyatilia mkazo hayo kwa kauli yake: "wasomi wa fani ya mantiki ndio waliosema, swali la Ma linahusika na aina na jinsi..." Lakini waarabu wanatumia kwa aina. Qur'an haiko katika mfumo wa Aristotle na mantiki yake, isipokuwa iko katika mfumo wa lugha ya Kiarabu ulio waziwazi. Jibu hili lina nguvu kuliko la kwanza ingawaje natija ni moja. Swali la pili: Je kuwapa waliotajwa katika Aya hii, ni wajibu au sunna?
Jibu
: Ni wajibu kwa wazazi kuwalisha watoto, na watoto kuwalisha wazazi ikiwa upande mmoja una uwezo na mwengine hauna uwezo wa kujilisha wenyewe. Kutoa huku hakuhisabiwi kuwa ni zaka. Ama mayatima na wasa-firi, inajuzu kuwapa kutokana na zaka ya wajibu; kama vile ambavyo inajuzu kuwapa wote sadaka ya sunna. Na sadaka ya suna hupewa kila mwenye kuhitajia, awe Mwislamu au si Mwislamu, kwa sababu kuna malipo katika kumnywesha kila mwenye ini la joto (kiu); kama ilivyoelezwa katika Hadith.
﴿كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴾
216.Mmeandikiwa kupigana (vita) nalo ni (jambo) la kuchukiza kwenu. Na huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu, na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
﴿يَسْأَلُونَكَ عَنِ الشَّهْرِ الْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَكُفْرٌ بِهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ اللَّـهِ وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ وَلَا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ إِنِ اسْتَطَاعُوا وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾
217.Wanakuuliza juu ya kupigana (vita) katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita katika (miezi) hiyo ni (dhambi) kubwa. Na kuzuilia watu na njia ya Mwenyezi Mungu na kumkufuru na (kuwazuilia) Msikiti Mtakatifu na kuwatoa humo wenyewe ni kukubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni kubwa zaidi kuliko kuua. Wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika dini yenu, kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi atakayertadi, kisha akafa hali ya kuwa kafiri, basi hao zimepomoka amali zao duniani na akhera. Na hao ndio watu wa motoni, humo watakaa milele.
﴿إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ يَرْجُونَ رَحْمَتَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾
218.Hakika wale walioamini na wale waliohama na wakafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye kutaraji rehema ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu.
MMEANDIKIWA KUPIGANA VITA
Aya 216 - 218
MAANA
Mmeandikiwa kupigana vita.
Mmeandikiwa hapa ni kwa maana ya mmewajibishiwa zilivyo Aya kadhaa zenye neno hilo. Mwenyezi Mungu amewajibisha vita kwa Waislamu si kwa kuwa vita vinapendeza au vinatakiwa mara kwa mara. Pia si kwa ajili ya kupanua nchi na kutawala au kunyonya mataifa mengine, isipokuwa au Mwenyezi Mungu amewajibishia kwa ajili ya kuinusuru na kuitetea haki. Kwa sababu haki pekee, ni fikra na nadharia tu. Ama kuifuatilia na kulazimiana nayo kunahitaji kazi ngumu, ambayo kwanza ni kuilingania kwa hekima na kwa njia iliyozoeleka. Kama haikuwezekana, basi ni wajibu kuitekeleza haki kwa nguvu. Nadharia yoyote isiyotegemea nguvu za kiutekelezaji, basi kuwepo kwake na kutokuwepo ni sawa.
Ni kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawajibisha, katika Aya hii na nyinginezo, kupigana jihadi na kila adui wa haki, ikiwa hakuna faida kwake kumwamrisha mema na mawaidha mazuri. Lau si nguvu za kiutekelezaji, basi nguvu za kisheria zingekuwa ni maneno yanayosemwa mdomoni na kuandikwa tu.
Nalo ni (jambo) la kuchukiza kwenu. Na huenda mkachukia kitu nacho ni heri kwenu, na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamujui.
Wafasiri wanasema kwamba masahaba wa Mtume walichukia vita, kwa sababu ni tabia ya mwanaadamu kuona uzito kujiingiza katika jambo litakalomwangamiza. Lakini wakati huo huo wanaitikia amri ya Mwenyezi Mungu kwa kutaka radhi Yake; sawa na mgonjwa anayekunywa dawa kwa kutaka kupona. Na Mwenyezi Mungu akawazindua kwa kauli yake: "Huenda mkachukia kitu nacho ni heri kwenu" kwamba matunda ya vita na jihadi yanawarudia wenyewe na sio Mwenyezi Mungu.
Huu ndio ufupi wa waliyoyasema wafasiri. Na dhahiri ya Matamshi inakubaliana nayo, lakini tukiwaangalia masahaba wenye ikhlasi na ushujaa katika jihadi, kujitolea kwao kwa ajili ya dini na jinsi dini ilivyotawala hisia zao. Vile vile jinsi walivyopuuza uhai kwa kutaka kufa mashahidi mpaka ikawa anayeokoka vitani na kurudi salama anajiona ni mwovu tukiangalia yote haya na kuyatia akilini mwetu, wakati wa kufasiri Aya hii, tutaona kuwa, haielekei kwa masahaba kuchukia vita, na kwamba hapana budi kufasiri Aya kwa maana nyingine itakayochukuana na matamko.
Kwa ufupi maana ni kuwa masahaba walikuwa wakiogopa kuwa Uislamu utamalizwa na washirikina kutokana na idadi yao kuwa kubwa na ya Waislamu kuwa ndogo; kwamba wao wataangamia kusibakie atakayeunusuru Uislamu, na mwito wa Kiislamu uende bure. Kwa hiyo walikuwa wakihofia Uislamu, sio nafsi. Ndipo Mwenyezi Mungu akawabainishia kuwa vita mnavyoitiwa na kuvichukia ni bora kwenu na kwa ajili ya Uislamu, na kwamba kukaa tu, kutapelekea kumalizwa nyinyi na Uislamu; na nyinyi hamjui hakika hii, lakini Mwenyezi Mungu anajua, kwa sababu kwake halijifichi lolote. Aya iko katika mwelekeo wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ يَغْلِبُوا أَلْفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ﴾
"Ewe Mtume! Wahimize walioamini waende vitani. wakipatikana kwenu watu ishirini wanaosubiri watawashinda mia mbili. Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watawashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana wao ni watu wasiofahamu."
(8:65)
Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana (vita) katika (miezi) hiyo ni dhambi kubwa.
Yamekwishapita maelezo katika kufasiri Aya ya 192 na inayofuatia hiyo:Na kuzuilia watu na njia ya Mwenyezi Mungu na kumkufuru na (kuwazuilia) msikiti mtakatifu na kuwatoa humo wenyewe ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Waarabu walikuwa wakijizuilia kupigana katika miezi mitukufu ambayo ni Dhul-Qaada, Dhul-Hijja, Muharram na Rajab (mfunguo pili, mfunguo tatu, mfunguo nne na mfunguo kumi). Mtume naye akaithibitisha ada hii, kwa sababu inapunguza shari na umwagikaji damu. Kwa ujumla Uislamu umethibitisha kila ada nzuri au isiyokuwa mbaya iliyokuwa wakati wa Jahilia. Hata hivyo Waarabu waliokuwa wakiitukuza na kuitakasa miezi hii, walivunja miiko yake na wakatangaza kupigana vita na Mtume katika mwaka wa sita Hijriya; wakamzuwia pamoja na masahaba zake kuzuru nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu na kumfitini mwenye kusilimu;
wakawa wanamwadhibu kwa aina aina ya adhabu kwa muda wa miaka kumi na tatu; kama walivyofanya kwa Bilal, Suhaib, Khabbab na Ammar bin Yasir pamoja na baba yake na mama yake. Lakini Waislamu wanapotaka kujikinga au kulipiza kisasi kwa washirikina, basi washirikina huanza kupiga mayowe kwa propaganda za upotevu, kwamba Waislamu wamevunja miko. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawabainishia kuwa makosa waliyoyafanya wao kwa Waislamu ni makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kupigana katika miezi mitukufu. Na kwa ajili hii Waislamu wamehalalishiwa kupigana na washirikina mahali popote na wakati wowote watakapowapata kwa kuchukua kisasi.
Na fitina ni kubwa zaidi kuliko kuua.
Yaani kuwafitini Waislamu na dini yao, mara nyingine kwa kuwaadhibu na mara nyingine kujaribu kuwatia shaka katika nyoyo zao, ni mbaya zaidi kuliko kupigana katika miezi mitukufu.
Wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika dini yenu, kama wakiweza.
Lengo la washirikina ni kutobakia athari yoyote ya Uislamu duniani. Na ni kwa ajili hii tu, ndio wanapigana na Waislamu, na wanaendelea kupigana nao. Basi kama Waislamu wakichukia kupigana na washirikina, lengo la maadui litatimia.
Roho hii ya kikafiri ya kiadui, inaendelea mpaka leo popote pale penye harufu ya Uislamu; inaendelea katika nafsi za wengi katika mashariki na magharibi. Sababu ya kwanza ya uadui kwa Uislamu ni utu wake, uadilifu wake na kuzuia kwake dhulma na ufisadi. Kwa sababu hiyo ndio wanawakusudia na kila shari na kuwapiga vita kwa nyenzo mbalimbali. Vile vile kuwafitini kulingana na hali ilivyo. Kwa hiyo ni juu yetu kuzinduka na maadui hawa na kuwapiga vita kwa silaha ile ile wanayotupiga nayo.
Na yeyote katika atakayertadi, kisha akafa hali yakuwa kafiri, Basi hao zimepomoka amali zao katika dunia na Akhera Na hao ndio watu wa motoni, humo watakaa milele.
Hii ni hadhari kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mwenye kuwaitikia maadui na kutoka dini yake, basi mtu huyo amepata hasara ya duniani na akhera na mwisho wake ni Jahannam ambayo ni marejeo mabaya. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kisha akafa hali yakuwa kafiri," inafahamisha waziwazi kwamba mwenye kurtadi (kutoka) katika dini, akitubia kabla ya kufa, Mwenyezi Mungu huikubali toba yake na huondokewa na adhabu; na akili inakubaliana na hilo. Lakini mafaqihi wa kishia wamesema: Ikiwa ni mwanamume na kutoka kwake kukawa kunatokana na kuzaliwa; kisha akatubia, basi ataondokewa na adhabu ya akhera tu, ama ya duniani ambayo ni kuuliwa itakuwapo. Kama kukiwa kutoka kwake kunatokana na mila basi hatauawa.
Katika ufafanuzi huu wametegemea riwaya za Ahlul bait
( [10]
).
Maana ya kupomoka amali zao katika dunia ni kuwa wao watafanyiwa muamala wa kikafiri kuongezea kustahiki kuuawa. Ama kupomoka amali zao huko akhera, ni adhabu na mateso. Hakika wale walioamini na wale waliohama na wakafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye kutarajia rehema ya Mwenyezi Mungu. Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutaja hali ya washirikina na waliotoka katika Uislamu na kutaja adhabu yao, amefuatishia kutaja waumini na malipo yao.
waliohama (Muhajirina) ni wale kutoka Makka kwenda Madina pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na waliofanya jihadi ni wale waliotoa juhudi zao katika kuunusuru Uislamu na kupigana na maadui zake.
IBADAYA MWENYE KUTUBIA BAADA YA KURTADI (KUTOKA KATIKA UISLAMU)
Mwenye kutoka katika Uislam (murtadi) akitubia na akarudi katika Uislamu kabla ya kufa, Mwenyezi Mungu humkubalia toba yake kwa hukumu ya kiakili na kwa dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
"Kisha akafa hali yakuwa kafiri"
alipounganisha kupomoka amali na kufa katika hali ya kafiri. Hapo basi yanakuja maswali mawili: Swali la Kwanza: Je, ibada zake kama vile swala, Hijja, Saumu na Zaka, zitasihi baada ya kurudi kwenye Uislamu? Mafaqihi wa Kisunni wameafikiana kuwa zinasihi na kukubaliwa. Mafaqihi wa Kishia wameafikiana kwamba zinazokubaliwa ni za yule wa mila, na wamehitalifiana katika wa kuzaliwa. Wengi wao wamesema hazisihi kwa hali yoyote na kwamba Uislamu wake baada ya kuutoka, haumfai na chochote katika dunia kabisa, bali atatendewa muamala anaofanyiwa kafiri;isipokuwa Uislamu wake utamfaa akhera tu, kwa kuondokewa na Adhabu. Lakini wahakiki wa mambo katika Shia wamesema, bali zinasihi ibada zake, na utamfaa Uislamu wake na atafanyiwa muamala wa Kiislamu. Nasi tuko pamoja nao.
Swali la Pili: Je, Murtadi akirudi katika Uislam atalazimika kulipa ibada zake alizozifanya wakati alipokuwa Mwislamu kabla ya kurtadi. Hanafi na Maliki wamesema, atalazimika kulipa. Na Shafii amesema hatalazimika.
Ama Mafaqihi wa Kishia wamesema kuwa zinasihi ibada za mwenye kutubia baada ya kurtadi, wao wanasema mtu halipi chochote alichokifanya wakati ni Mwislamu, isipokuwa atalipa yaliyompita wakati wa kutoka Uislamu (kurtadi).
KUPOROMOKA
Mu'utazila wamesema kuwa thawabu za Mumin mtiifu zinaanguka zote kwa maasi yatakayofuatia; mfano hata mwenye kuabudu umri wake wote, kisha akanywa tama moja tu la pombe, basi ni kama ambaye hakumwabudu Mwenyezi Mungu kabisa. Vile vile twaa inayofuatia inaondoa madhambi yaliyotangulia; na hayo ndiyo maana ya kupomoka amali. Shia Imamiya na Ashari wameafikiana kuwa hakuna kuharibika; wakasema kila amali ina hisabu yake inayoihusu; wala twaa haifungamani na maasi, nayo hayafungamani na twaa, bali atakayefanya wema (hata) uzani wa sisimizi atauona. Mwenye kufanya uovu na wema akiwa muumini Mwenyezi Mungu ataupima wema wake na uovu wake. Ikiwa wema utazidi, atakuwa kama ambaye hakufanya uovu, kwa sababu wingi unafuta uchache. Ikiwa yote ni sawa, basi atakuwa kama ambaye hakutokewa na lolote.
Kupomoka kuko mbali sana na maana haya; maana yake hasa ni mwenye kufa akiwa kafiri baada ya kuwa Mwislamu, ukafiri wake huu utakuwa unafichua amali zake alizokuwa akizifanya wakati wa kusilimu, kuwa hazikuwa katika njia inayotakikana tangu mwanzo; sio kwamba alistahiki thawabu kisha zikafutwa, bali hili ni katika upande wa kuzuwia sio kuondoa; yaani thawabu hazikuwepo.