9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI
﴿ يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا وَيَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلِ الْعَفْوَ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ ﴾
219.Wanakuuliza kuhusu ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo mna madhara makubwa na manufaa kwa watu, na madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Vilivyowazidia. Namna hii Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya mpate kufikiri.
﴿ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَىٰ قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَعْنَتَكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴾
220.Katika dunia na akhera. Na wanakuuliza kuhusu mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndiyo heri. Na kama mkichanganyika nao, basi ni ndugu zenu. Na Mwenyezi Mungu anamjua fisadi na mtengenezaji. Na kama angelitaka Mwenyezi Mungu angeliwatia katika dhiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu,Mwenye hekima.
ULEVI NA KAMARI
Aya 219 – 220
LUGHA
Limetumiwa neno Khamri, lenye maana ya kufunika, kwa maana ya ulevi, kwa sababu ulevi unafunika akili. Na limetumiwa neno Maysir, lenye maana ya wepesi, kwa maana ya kamari, kwa sababu chumo la kamari linakuwa jepesi bila ya jasho.
MAANA
Wanakuuliza kuhusu ulevi na kamari.
Waliuliza baadhi ya Waislamu kuhusu hukumu ya ulevi na kamari katika Madina; yaani zaidi ya miaka 13 tangu ulipoanza mwito wa Kiislamu. Hiyo inafahamisha kuwa hukumu ya pombe ilikuwa imenyamaziwa muda mrefu, kama zilivyonyamaziwa baadhi ya hukumu za haramu mpaka wakati wake maalum, kulingana na masilahi. Mara nyingine kubainisha hukumu kunataka hekima ya kuchukulia mambo pole pole. Inasemekana kuwa ubainifu wa hukumu ya pombe ulikuwa hivi, kwa sababu Waislamu walikuwa wameizoweya wakati wa Ujahiliya (kabla ya kuja Uislamu); lau wangelizuiliwa mara moja tu, ingelikuwa uzito kwao. Bali Mwenyezi Mungu aliwakumbusha Waislamu walipokuwa Makka kwamba katika jumla ya neema zake ni kwamba wao wanafanya ulevi na kupata riziki kutokana na tende na zabibu. Anasema Mwenyezi Mungu:
﴿ وَمِن ثَمَرَاتِ النَّخِيلِ وَالْأَعْنَابِ تَتَّخِذُونَ مِنْهُ سَكَرًا وَرِزْقًا حَسَنًا﴾
"Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza ulevi na riziki nzuri..."
(16:67)
Waliuliza baadhi ya Waislamu kuhusu hukumu ya pombe na kamari, Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kuwajibu: Katika hivyo madhara makubwa na manufaa kwa watu na madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Jawabu hili peke yake halitoshi kuwa ni dalili ya uharamu wa ulevi. Kwa sababu hakusema kuwa ni haramu; linafahamisha kawaida ya kujikinga na madhara ni bora kuliko maslahi, na muhimu inatanguliwa na muhimu zaidi. Lakini tukiangalia Aya isemayo:
﴿ قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ﴾
"Sema: Mola wangu ameharimisha mambo maovu yaliyodhihirika na yaliyofichika na madhara na uasi pasipo haki..."
(7:33)
Tukiiunganisha Aya hiyo na hii tunayoizungumzia tutapata dalili ya kuharimishwa ulevi waziwazi na kwa mkato. Kwa sababu natija inayopatikana ni kuwa ulevi ni madhara na madhara ni haramu, kwa hivyo ulevi ni haramu.
Hiyo ni pamoja na kuongezea Aya inayosema:
﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾ إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ﴾
"Enyi mlioamini! Hakika ulevi na kamari na masanamu na mishale ya kutizamia (ramli) ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu. Hakika Shetani anataka kuwatilia uadui na bughudha baina yenu kwa ulevi na kamari kuwazuilia na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na Kuswali. Basi je, mtaacha?"
(5:90 - 91)
Kwa hiyo kusema jiepusheni navyo ni amri ya kujiepusha, na amri inafahamisha wajibu. Na kusema basi je mtaacha! Ni kukataza, na kukataza kunafahamisha uharamu. Ndipo Waislamu waliposikia Aya hii wakasema: "Tumeacha."Ama ile Aya inayosema:
﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ﴾
"Enyi mlioamini msiikurubie swala hali mmelewa..."
(4:43)
ilishuka kabla ya Aya (5:90-91), ambazo zina uzito mkubwa. Tumeeleza kwamba huenda ilikuwa ni hekima ya kuchukulia mambo pole pole katika kubainisha uharamu, kwa vile kutoikurubia swala hali mme-lewa haina dalili yoyote ya kuonyesha uhalali wa pombe katika isiyokuwa swala. Tutafafanua Inshaallah tutakapofikia Aya hizo.
Zaidi ya hayo Waislamu wote tangu mwanzo hadi hivi leo wamekongamana kwa kauli moja tu! Kuwa ulevi ni katika madhambi makubwa, na kwamba mwenye kuuhalalisha siye Mwislamu. Na mwenye kuinywa kwa kupuuza ni fasiki na atapigwa (Had) viboko themanini. Imekuja Hadith Mutawatir kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
kwamba amelaaniwa mwenye kupanda mti wa (hiyo pombe), mwenye kuigema, mwuzaji, mnunuzi, mwenye kuhudumia wanywaji na mnywaji. Na imeelezwa katika baadhi ya hadith kwamba hakuna sharia yoyote ya mbinguni ila imekataza ulevi. Tumeyaeleza kwa ufafanuzi zaidi maudhui haya katika juzuu ya nne ya kitabu: Fiqhul Imam Jaffar Sadiq katika mlango wa vyakula na vinywaji.
Na madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake.
Makusudio ya ithm hapa ni madhara. Madhara ya pombe yanadhihirika katika mwili, akili na mali na vile vile kuacha kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kugom-bana na kufanya mambo yaliyoharamishwa.Wanahistoria wanasema kwamba baadhi ya walevi walizini na mabinti zao. Abbas bin Mirdas, alikuwa kiongozi wa watu wake, katika zama za Jahiliya (kabla ya Uislamu) alijiharimishia pombe yeye mwenye tu kwa maumbile yake. Alipoulizwa sababu, akasema: "Siwezi kuchukua ujinga kwa mkono wangu nijiingize mwenyewe, wala siko radhi asubuhi niwe bwana mkubwa wa watu na jioni niwe mpuzi wao." Daktari mmoja mashuhuri wa Kijerumani alisema: "Fungeni nusu ya mabaa na mimi ninawadhaminia kuwa hamtahitajia nusu ya zahanati na mahospitali na majela."
Ama kamari inaleta uadui na chuki na inazuia kutajwa Mwenyezi Mungu; kama ilivyoonyesha Aya tukufu, inaharibu tabia kwa kuzoeya uvivu na kutafuta riziki kwa ndoto tu! Pia inavunja majumba na inamtia mtu kwenye umasikini ndani ya saa moja tu. Inatosha kuwa haramu kamari, kule kuchukua mali bure bure tu.
Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Vilivyowazidia.
Yaani: Toeni vilivyozidi haja zenu na za familia yenu. Amri ya kutoa hapa ni ya suna sio ya wajibu, isipokuwa inakuwa wajibu kutoa kama zikithibiti sharti za khumsi na zaka. Tutaelezea kwa ufafanuzi, Inshaallah.
Aya hii ni kama Aya isemayo:
﴿ وَلَا تَجْعَلْ يَدَكَ مَغْلُولَةً إِلَىٰ عُنُقِكَ وَلَا تَبْسُطْهَا كُلَّ الْبَسْطِ فَتَقْعُدَ مَلُومًا مَّحْسُورًا ﴾
"Wala usifanye mkono wako ni wenye kufungwa shingoni mwako, wala usiukunjue ovyo ovyo utakuwa ni mwenye kulaumiwa mwenye kufilisika."
(17:29)
Imeelezwa katika Hadith kwamba mtu mmoja alikwenda kwa Mtume(s.a.w.w)
na kibonge cha dhahabu kama yai, akamwambia Mtume: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu chukua hii ni sadaka Wallah sina chochote zaidi ya hiyo." Mtume akaachana naye; kisha akamfuata tena na kurudia kumwambia, kisha Mtume akakichukua na kumrudishia mwenyewe akisema: "Mtu ananijia na mali yake naye hana kitu kingine chochote; kisha aombe watu! Hakika sadaka inatokana na kujitosha; chukua mwenyewe hatuna haja nayo." Iko Hadith pia kwamba Mtume(s.a.w.w)
alikuwa akiiwekea familia yake matumizi ya mwaka mzima.
Namna hii anawabainishia Mwenyezi Mungu Aya mpate kufikiri katika dunia na akhera.
Yaani Mwenyezi Mungu anawabainishia hukumu yake katika pombe na kamari, na hukumu yake katika vile ambavyo tunatakikana kuvitoa sadaka katika mali zetu kwa misingi ya maslahi yetu. Yeye haamrishi isipokuwa lile ambalo lina maslahi ya kidunia na askhera, na wala hakatazi isipokuwa lile lenye uharibifu.
Yatupasa kuuzingatia na kuuchunga uhakika huu tusimwasi Mwenyezi Mungu katika jambo lolote miongoni mwa amri na makatazo yake. Kwa hivyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu:"Mpate kufikiri katika dunia na akhera"
ni kwamba tufanye amali kwa ajili ya zote mbili (dunia na akhera) bila ya kuacha moja.
Na wanakuuliza kuhusu mayatima.
Wakati wa ujahilia (kabla ya Uislamu) watu walizowea sana kunufaika na mali za mayatima; pengine mtu aliweza kumwoa yatima au kumwoza mtoto wake kwa tamaa ya mali yake tu. Ulipokuja Uislamu, Mwenyezi Mungu alimterem-shia Mtume wake Aya hizi:
﴿ إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا﴾
"Hakika wale ambao wanakula mali ya mayatima kwa dhulma, hakika wanakula moto matumboni mwao..."
(4:10)
﴿ وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ﴾
"Wala msikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia ya wema kabisa..."(
6:152)
Basi ziliposhuka Aya hizo waliacha kuchanganyika na kuwasimamia mayatima. Hapo maslahi yao yakaharibika na maisha yao yakawa mabaya. Ndipo baadhi ya Waislamu wakauliza kuhusu hali hiyo. Likaja jawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
Sema: Kuwatengenezea, ndio heri.
Maana yake msijizuilie na kuchanganyika na mayatima na kuzikurubia mali zao, kama mnataka kuwatengenezea uzuri katika malezi yao, adabu zao na kusimamia mali zao. Bali hilo lina malipo na thawabu. Lenye kuharamishwa ni kuzifuja na kuzila mali zao.
Na kama mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu.
Kundi la wafasiri limesema: "Hii ni idhini kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa anayesimamia yatima kumshirikisha pamoja na familia yake katika kula na kunywa ikiwa hilo ni sahali kwa msimamizi na achukue kutoka katika mali ya yatima kiasi kile cha malezi.
Na Mwenyezi Mungu anamjua fisadi na mtengezaji.
Fisadi ni yule anayesimamia yatima ili afuje mali zake: Na mtengezaji ni yule anayesimamia mali ya yatima kwa maslahi ya yatima kwa dhati. Kwa hivyo kauli yake hiyo Mwenyezi Mungu ni kemeo kwa mwenye kutaka kufuja na kufanya ufisadi.
Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwatia katika dhiki.
Makusudio hapa ni kwamba Mwenyezi Mungu amehalalisha kuchanganyika yatima na familia ya msimamizi na kuchukua katika mali ya yatima thamani ya kile alichompatia posho, ili yasipatikane mashaka na uzito. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawatakia watu wepesi wala hawatakii uzito. Hapa inaonyesha kuwa si lazima kuwe na usawa wa kutopungua hata kidogo kati ya kile alichokula yatima pamoja na familia ya msimamizi na kile atakachochukua badali kutoka katika mali ya yatima. Kwani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) husamehe tofauti ndogo isiyoepukika, bali msimamizi anaweza hata kula katika mali kwa wema akiwa fukara. Hayo ni kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿ وَمَن كَانَ غَنِيًّا فَلْيَسْتَعْفِفْ وَمَن كَانَ فَقِيرًا فَلْيَأْكُلْ بِالْمَعْرُوفِ﴾
"...Na mwenye kuwa tajiri basi ajiepushe, na atakayekuwa mhitaji basi ale kwa kadri ya ada.
(4:6)
﴿ وَلَا تَنكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ حَتَّىٰ يُؤْمِنَّ وَلَأَمَةٌ مُّؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ وَلَا تُنكِحُوا الْمُشْرِكِينَ حَتَّىٰ يُؤْمِنُوا وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ أُولَـٰئِكَ يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَى الْجَنَّةِ وَالْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِ وَيُبَيِّنُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴾
221.Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi muumini ni bora kuliko mshirikina hata akiwa-pendeza. Wala msiwaoze wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa muumini ni bora kuliko mshirikina hata akiwapendeza. Hao wanaita kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaita kwenye Pepo na maghufira, kwa idhini Yake. Naye hubainisha Aya Zake kwa watu ili wapate kukumbuka.
MSIWAOE WANAOMSHIRIKISHA MWENYEZI MUNGU
Aya 221
MAANA
Aya hizi ni miongoni mwa Aya za hukumu, na zinaingia katika mlango wa ndoa. Kabla ya kuingilia madhumuni ya Aya, kwanza tutajaribu kufasiri neno. Nikah, Mushrikina, Amah, Neno: (Nikaha) lina maana mbili: Kufunga ndoa na kumwingilia mwanamke. Neno: Mushrikina (washirikina) imesemekana kuwa ni kila asiyeamini utume wa Muhammad(s.a.w.w)
. Kwa kauli hii watakuwa wanaingia watu wa Kitabu ambao ni Mayahudi, na Wakristo. Na inasemekana kuwa Qur'an haikusudii watu wa Kitabu, japo wanasema kuwa Issa ni Mwana wa Mungu na utatu wa Mungu. waliosema haya wametoa dalili kwa Aya hizi:
﴿ مَّا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَلَا الْمُشْرِكِينَ﴾
"Hawapendi waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu wala washirikina..."
( 2:105)
﴿ لَمْ يَكُنِ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ ﴾
"Hawakuwa, wale ambao wamekufuru katika watu wa Kitabu na washiririkina..."
(98:1)
Katika Aya hizo kuna viunganishi kati ya watu wa kitabu na washirikina, na kiunganishi kinafahamisha tofauti. Kwa sababu kitu hakiwezi kuunganishwa na kitu hicho hicho.
Neno: Amah (mjakazi) na Abd linatumiwa kwa mtumwa na hata aliyehuru. Unaweza kumwambia aliyehuru: "Ewe mjakazi wa Mwenyezi Mungu," vile vile mtumwa kwa sababu binadamu wote ni watumwa wa Mwenyezi Mungu. Maana ya Aya ni kuwa enyi Waislamu msioane na washirikina, bali oaneni na wanaotokana nanyi hata kama sio bora kama washirikina kwa umbo na tabia au kwa jaha na mali. Hao wanaiita kwenye moto. Yaani hao washiikina. hikima ya kukataza kuoana ni hiyo ya mwito wa motoni, na kwamba muungano wa kuiondoa unapelekea uharibifu wa itikaTafsir di na dini. Kwa ufupi unapelekea ufasiki na kupuuzwa hukumu ya Mwenyezi Mungu. Tunashuhudia hivi leo vijana wetu wengi wako katika hali mbaya kuliko makafiri na washirikina, kutokana na kudharau kwao, kuipuuza dini na kujivua kabisa katika athari za dini. Wanawalea watoto wao malezi yasiyokuwa ya dini wala ya tabia njema. Lau sikuwa walishuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na Muhammad ni Mtume wake, basi tungeliwafanyia muamala wa walahidi na washirikina.
Lakini kwa sababu ya tamko hili tu (la shahada), ndilo limehifadhi damu, mali na kusihi kuoana na kurithiana nao hata kama haya yanatokana na njia za taqlid na kurithi( [11]
).
Na Mwenyezi Mungu anaita kwenye pepo na maghufira.
Hapa kuna miito miwili:
• Mwito wa kwanza: Ni wa wanaoshirikisha - kufanya yale yanayoingiza motoni na kwenye ghadhabu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.)
• Mwito wa pili: Ni wa Mwenyezi Mungu - kufanya yanayoleta maghufira na kuingia peponi. Miongoni mwa hayo ni kuoa mwenye kuamini na wala sio mwenye kushirikisha. Hapana mwenye shaka kwamba wanaoamini ndio wanaoitika mwito wa Mwenyezi Mungu na wanapata maghufira yake na hatimae kuingia pepo Yake kwa idhini Yake; yaani kwa uongofu na tawfiki yake.
KUOA MWENYE KITABU (AHLUL-KITAB)
Wameafikiana Waislamu kwamba haijuzu kwa Mwislamu kuoa au kuolewa na asiyekuwa na kitabu; kama vile kuoa wale wanaoabudu masanamu, jua na moto, n.k. kwa ufasaha zaidi yule asiyeamini.
Vile vile haijuzu kumuoa au kuolewa na Majusi, hata kama imesemwa Majusi ni shabihi ya wenye kitabu. Wameafikiana madhehebu manne ya Ahli Sunna juu ya kusihi kumuoa mwenye kitabu, na wamehitalifiana Mafaqihi wa Kishia. Wengi wao wamesema kuwa haijuzu kwa Mwislamu kumuoa Yahudi au Mkristo. Na wengine wamesema inajuzu. Miongoni mwa Ulamaa wakubwa waliosema hivyo ni Sheikh Muhammad Hassan katika Jawahir, shahidi wa Pili katika Masalik na Sayyid Abul Hassan katika Wasilah, wamesema inajuzu. Na sisi tuko pamoja na rai hii kwa dalili hizi:
1. Dalili zinazohalalisha ndoa zimemtoa Mwislamu mwanamume kumwoa Mshirikina, na Mwislamu mwanamke kuolewa na mshirikina na mwenye kitabu. Kwa hivyo inafahamisha kuwa wasiokuwa hao inajuzukuoa.
2 Kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ ﴾
"Leo mmehalalishiwa kula vilivyo vizuri na chakula cha wale waliopewa kitabu ni halali kwenu na chakula chenu ni halali kwao na wanawake wasafi waumini na wanawake wasafi katika wale waliopewa kitabu kabla yenu..."
(5:5)
Kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu:Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa (zenu),
makusudio ya makafiri hapo ni washirikina sio wenye Kitabu. Kwa sababu Aya iliwashukia wanawake waliosilimu na kuhama na Mtume wakiwaacha waume zao washirikina; na mfumo mzima wa Aya unafahamisha hivyo. Aya yenyewe ni hii:
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا جَاءَكُمُ الْمُؤْمِنَاتُ مُهَاجِرَاتٍ فَامْتَحِنُوهُنَّ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِهِنَّ فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَاتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى الْكُفَّارِ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ وَآتُوهُم مَّا أَنفَقُوا وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَن تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ وَلَا تُمْسِكُوا بِعِصَمِ الْكَوَافِرِ ﴾
"Enyi mlioamini! Watakapowajia wanawake walioamini wanaohama, basi wafanyieni mtihani; Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi imani yao. Mkiwajua ni waumini basi msiwarudishe kwa makafiri. Hawa si halali kwa hao (wanaume makafiri) wala wao (wanaume makafiri) si halali kwao. Na warudishieni (waume zao) (mahari) waliyotoa. Wala kwenu si vibaya kuwaoa ikiwa mtawapa mahari yao (hao wanawake) kwenu. Wala msiwaweke katika kifungo cha makafiri..."
(60:10)
Pia ziko Hadith sahihi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) katika kusihi kumuoa mwanamke katika wenye kitabu, na haya tumeyafafanua zaidi katika juzuu ya tano ya kitabu. Fiqhul Imam Jafar Sadiq. Mlango yaliyoharamu, kifungu cha kutofautiana dini
﴿وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴾
222.Wanakuuliza kuhusu hedhi; waambie ni udhia. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi wala msiwakaribie mpaka watoharike. Wakisha toharika basi waendeni pale alipowaam-risha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubia na huwapenda wanaojitoharisha.
﴿ نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ وَقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُمْ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُم مُّلَاقُوهُ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴾
223.Wake zenu ni mashamba yenu. Basi yaendeeni mashamba yenu mpendavyo, na tangulizieni nafsi zenu; na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni kwamba mtakutana Naye, na wape habari njema wenye kuamini.
HEDHI
Aya 222 - 223
MAANA
Baada ya kumuuliza Mtume mtukufu(s.a.w.w)
kuhusu miezi mitakatifu, ulevi, kamari watakachotoa na mayatima; kisha walimuuliza kuhusu hedhi. Amesema Razi: "Imepokewa habari kuwa Mayahudi na Majusi walikuwa wakikaa mbali sana na wanawake wakati wa hedhi; Wakristo walikuwa wakiwaingilia bila ya kujali hedhi; na watu wa zama za Jahiliya (kabla ya Uislamu) walikuwa hawali, hawanywi, hawakai kitanda kimoja wala hawakai nyumba moja na mwanamke mwenye hedhi; kama walivyokuwa wakifanya Majusi na Mayahudi.
Wanakuuliza kuhusu hedhi; waambie ni udhia. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi.
Swali linahusu kuchanganyika na wanawake wakati wa hedhi, ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake mtukufu kuwajibu waulizaji kwamba: wajitenge na wanawake siku za hedhi; yaani wasiwaingilie. Imekuja Hadith inayosema;"Fanyeni kila kitu isipokuwa kuingilia tu."
Makusudio ya neno 'Adha' (udhia) ni madhara kwa kuwa ni uchafu na najisi.
Wala msiwakurubie mpaka watoharike.
Wamehitalifiana juu ya makusudio ya kutoharika kuwa je, ni kukatika damu tu bila ya kuoga au ni pamoja na kuoga? Yaani inajuzu kuingiliwa kabla ya kuoga au la? Wamesema Shia inajuzu kumwingilia hata kabla ya kuoga kwa vile ndio ufahamu wa tamko Tuhr watoharike. Ama kujitoharisha hiyo ni kazi ya wanawake ambayo inakuwa baada ya tohara (kwisha damu). Amesema Malik na Shafii: Haijuzu ila baada ya kuoga. Na wanasema Hanafi: Ikiendelea damu kwa muda wa siku kumi, inajuzu kumkurubia kabla ya kuoga, lakini ikakatika damu kabla ya siku kumi haijuzu mpaka aoge. Mwenye tafsiri ya Al Manar ameelezea juu ya ufafanuzi huu kwa kusema: "Huu ni ufafanuzi wa kushangaza.
"Wakishatoharika, basi waendeeni pale alipowaamrisha Mwenyezi Mungu.
Neno: pale ni uhakika wa mahali, kwa maana ya tupu ya mbele, kama inavyofahamika. Masuala ya hedhi na hukumu zake tumeyazungumzia kwa ufafanuzi zaidi katika kitabu Fiqhul Imam Jaffar Sadiq na kitabu Al Fiqhu ala Madhahibil Khamsa
Wake zenu ni mashamba yenu, Basi yaendeeni mashamba yenu mpendavyo.
Neno: Anna, Kulingana na sarufi (nahw ya Kiarabu) lina maana ya vyovyote, wakati wowote au popote. Zimekuja kauli nyingi kuhusu maana ya neno hilo Anna katika Aya hii: Kuna mwenye kusema: Ni kwa maana ya wakati wowote; yaani muwaendee (muwaingilie) wakati wowote usiku au mchana. Wengine wakasema ni kwa maana ya popote yaani mna hiyari ya kuwaingilia popote tupu ya mbele au nyuma. Vile vile kuna mwenye kusema ni kwa maana ya vyovyote; yaani hali yoyote kukaa, kulala, n.k.
Limesema kundi la wafasiri, miongoni mwao akiwa ni mwenye Tafsiri ya Al Manar ambaye ni miongoni mwa wanachuoni wa Kisunni na mwenye Tafsiri ya Bayanu Ssada ambaye ni miongoni mwa wanachuoni wa Kishia, kwamba Neno: shamba linafungamana na mazao na ni tupu ya mbele tu, ndiyo ambayo inaweza kuoteshwa mazao (Mtoto ). Kuongezea kuwa kuendea tupu ya nyuma ni udhia. Sisi tunaiunga mkono rai hii kwa sababu mbili: Kwanza, mazao hayapatikani isipokuwa kwa kupitia tupu ya mbele tu, kama walivyotaja wafasiri hao. Pili, kauli yake Mwenyezi Mungu "Waendeni pale alipowaamrisha Mwenyezi Mungu inaonyesha makusudio yake ni mbele baada ya kufasiri hayth kwa maana ya mahali.
Kuna baadhi ya Mafaqihi wa Kishia wanaojuzisha kumwendea mke nyuma lakini kwa makuruhu makubwa sana. Wengine wamedai ati kuwa hayo yanahusika na Shia tu! Na kwamba hawaafikiani na yeyote katika hilo; na inajulikana kuwa Razi (mwanachuoni wa kisunni) amenakili katika kuifasiri Aya hii kwamba, Ibn Umar na Malik walikuwa wakisema: "Makusudio ya Aya ni kujuzisha kuwaendea wanawake nyuma." Na Al- Hafidh Abu Bakr Al-Andalusi wa madhehebu ya Kimalik (Sunni) - aliyekufa mwaka 542 Hijriya - katika juzuu ya kwanza ya kitabu Ahkamul Qur'an ukurasa 73 chapa ya mwaka 1331 A.H.; alisema hivi ninamnukuu: Wamehitalifiana wanavyuoni katika kujuzu kumwendea mke nyuma, wengi wamejuzisha."
Ameyaeleza hayo Ibn Shaban katika Jimau nnis-wan wa Ahkamul Qur'an. Sunni Na akategemeza, riwaya nyingi kujuzu kwake, kwenye kundi tukufu la masahaba, na Tabiina na kwa Malik. Bukhari ametaja kutoka kwa Ibn Aun, kutoka kwa Nafi kwamba Ibn Umar alikuwa akisoma Sura ya Baqara mpaka alipoishia 'Anna shiitum' alisema: "Je unajua imeteremka kwenye nini?" Nikasema: "La." Akasema: "Imeshuka katika kadha na kadha"; yaani tupu za nyuma za wanawake.