TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17359
Pakua: 3458


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17359 / Pakua: 3458
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَن يَشَاءُ وَمَن يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ﴾

269.Humpa hekima amtakaye. Na aliyepewa hekima hakika amepewa heri nyingi na hawakumbuki ila wenye akili.

HEKIMA

Aya 269

MAANA

Neno Hekima hutumiwa kwa maana nyingi, kama vile maslahi; mfano: "Hekima ya kitu hiki ni jambo fulani." Maana nyingine ni mawaidha; mfano: Hekima ni kitu (anachotafuta) kilichompotea "mumin," Pia lina maana ya elimu na fahamu; kama anavyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

﴿وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ﴾

"Na hakika tulimpa Lukmani hekima ..." (31:12)

Maana nyingine ya neno hekima ni Utume, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ ﴾

"....Na tukampa hekima na kukata hukumu." (38:20)

Vilevile neno hili linatumiwa kwa maana ya elimu ya Falsafa. Msemaji mmoja amesema: "Hekima ni elimu ya Fiqh", mwengine amesema ni elimu zote za kidini, watatu akasema ni kumtii Mwenyezi Mungu tu.

Vyovyote ilivyosemwa au itakavyosemwa, ni kwamba neno hekima haliwezi kutoka kwenye maana ya usawa na kukiweka kitu mahali pake kwa kauli na vitendo. Kwa hivyo mwenye hekima ni yule anayekihukumu kitu na kukileta kwa mujibu wa akili na hali ilivyo, sio kwa mujibu wa mapendeleo na matakwa. Kitu hicho hawezi kukifanyia haraka kabla ya muda wake au kukizuilia na wakati wake au kukipeleka kombo na mipaka yake. Kwa hali hiyo basi, hekima haihusiki na mitume na mawalii tu au na wanafalsafa na wataalamu tu, bali kila mwenye kufanya vizuri amali yoyote na akaiweka sawa, basi huyo ni mwenye hekima katika amali hiyo; awe ni mkulima au mfanyakazi, mwajiri au mwajiriwa. Vilevile ni sawa awe ni muhuburi, malenga, hakimu au askari, n.k. Sharti la kwanza na la mwisho la hekima ni kuthibiti lengo la kitendo kiakili, kisharia, kidunia na kidini.

Hapana mwenye kutia shaka kwamba ambaye hekima ni mwongozi wake atakuwa mwema katika nyumba mbili (duniani na akhera). Imam Jaffar Sadiq(a.s) anasema:"Hakumneemesha Mwenyezi Mungu mja neema kubwa na tukufu zaidi kuliko hekima. Mwenyezi Mungu anasema:

"Na aliyepewa hekima hakika amepewa heri nyingi na hawakumbuki ila wenye akili"

Yaani hajui yeyote siri ya hekima aliyoitoa Mwenyezi Mungu, isipokuwa mwenye kumtakasia Mwenyezi Mungu nafsi yake.

Hekima ni uongofu, ni uthabiti wa vianzio vya mambo na ni kituo cha mwisho wa mambo."

Hapa inaonyesha kuwa kuna tofauti kati ya elimu na hekima. Elimu ni kujua mambo na mfungamano uliopo wa mambo hayo; vile vile kujua athari yake ya kheri au ya shari. Ama hekima inaamrisha akili kufuata usalama, kufuata dini iliyo sawa na kukitumia kitu mahala pake, palipoumbwa kwa ajili yake. Mfano elimu inatengeza chembechembe za bomu na kutengeneza maroketi, lakini haiangalii lengo lake, la kheri au la shari; wala haikatazi hili na kuamrisha lile. Lakini hekima haijishughulishi na utafiti wa mabomu na uvumbuzi wa maroketi hayo isipokuwa inaangalia matumizi ya maroketi hayo na kumwelekeza binadamu lile litakalo mfanya kupata kheri na ufanisi sio uovu.( [5] )

﴿وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴾

270. Chochote mtoacho, au nadhiri mnazoweka, basi Mwenyezi Mungu anakijua, Na madhalimu hawana wasaidizi.

﴿إِن تُبْدُوا الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاءَ فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَيُكَفِّرُ عَنكُم مِّن سَيِّئَاتِكُمْ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴾

271.Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; Na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafukara, basi hivyo ni bora zaidi kwenu na yatawaondokea baadhi ya maovu yenu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayoyatenda.

CHOCHOTE MTOACHO

Aya 270-271

MAANA

Tena amerudia Mwenyezi Mungu kutaja kutoa na kukutilia mkazo kwa kusema:

Chochote mtoacho au nadhiri mnazoweka basi Mwenyezi Mungu anakijua

Neno: kutoa linakusanya kila kinachotolewa; kiwe cha wajibu au suna, kingi au kichache cha utii au maasi na kisiri au kidhahiri. Maana ya nadhiri kilugha ni ahadi; na kisharia ni kujilazimisha mtu kutenda jambo fulani au kuliacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Tamko lake ni kusema yule mwenye kuweka nadhiri: "Ni juu yangu kufanya jambo fulani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, "Haitoshi kukusudia tu, bila ya kusema, wala kusema bila ya kumtaja Mwenyezi Mungu au kutaja mojawapo ya majina yake matukufu. Lau anasema: "Nimeweka nadhiri kufanya kitu fulani likiwa jambo fulani", hiyo haiwezi kuwa nadhiri kwa kutokuwa na jina la Mwenyezi Mungu.

Vilevile nadhiri haiwezi kuwa kabisa, ikiwa imefungamana na jambo la haramu au makuruhu. Wakati wa Mtume(s.a.w.w) mtu mmoja aliweka nadhiri ya kusimama tu bila ya kukaa wala kuwa kivulini, akiwa amefunga na asizungumze na mtu; Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema: "Mwamuruni azungumze akae kivulini na aendelee na Saumu yake." Maana ya "Mwenyezi Mungu anakijua" ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua lengo lolote la kutoa litakalokuwa na kulipatia malipo; ikiwa ni heri basi ni heri na kama ni shari basi ni shari tu.

Na madhalimu hawana wasaidizi

Makusudio ya madhalimu ni wote bila ya kuvua, wakiwa ni pamoja na wale wasiotoa chochote au wanaotoa vibaya au kwa ria. Vilevile wale wanaotoa kwa masimbulizi na adha au kuweka pasipokuwa mahali pake. Wengine ni wale wanaovunja ahadi na wasiotekeleza nadhiri. Wote hawa na walio mfano wao hawatakuwa na wasaidizi wala waombezi watakaowazuiilia na mateso ya Mwenyezi Mungu.

Kama mkizidhihirisha sadaka ni vizuri.

Yaani hakuna umakuruhu katika kudhihirisha sadaka maadam makusudio yake ni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Imam Jaffar Sadiq aliulizwa kuhusu mtu anayefanya jambo la kheri,watu wakamwona akafurahi. Imam akasema:"Hapana ubaya; kila mtu anapenda kuonekana na watu kwa kheri, ikiwa hakufanya hilo kwa ajili ya huko kuonekana."

Na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafukara, basi hivyo ni bora zaidi kwenu.

Hapana shaka kwamba kuficha sadaka ni bora kuliko kuidhihirisha, kwa sababu kunakuwa mbali na shubuha ya ria na kudhihirisha haja ya mafukara mbele ya watu. Huwa mara nyingine kudhihirisha sadaka kuna maslahi; kwa mfano ikiwa ni kwa kutaka kutoa mfano kwa wengine, hapo kudhihirisha kutakuwa bora zaidi. Inasemekana kuwa kuificha sadaka ya sunna ni bora kuliko kuidhihirisha; na kinyume chake kwa sadaka ya wajibu. Hatujui hoja ya ufafanuzi huu na Hadith ya "Sadaka ya siri inazima ghadhabu ya mola" inakusanya ya wajibu na suna; kama ambavyo Aya inakusanya fukara mwislamu na asiyekuwa mwislamu. Mafaqihi wametoa fatwa ya kutoa sadaka ya sunna kwa asiyekuwa mwislamu akiwa ni muhitaji kutokana na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu:"Kulinywesha kila ini la joto kuna malipo, Na yatawaondokea baadhi ya maovu yenu.

Neno: Min hapa ni baadhi, kwa sababu sadaka haifuti madhambi yote isipokuwa inafuta baadhi tu.

Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda

Maadam Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua siri, sawa na anavyojua dhahiri, basi siri ni bora, kwa sababu hilo liko mbali na ria, isipokuwa kama katika kudhihirisha kuna maslahi; kama kuwaonyesha mfano wengine ili watende. Na wenye ikhlasi wengi wanaficha sadaka zao; wanajitolea kwenye mambo ya kheri kwa majina ya watu wengine wema.

﴿لَّيْسَ عَلَيْكَ هُدَاهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَلِأَنفُسِكُمْ وَمَا تُنفِقُونَ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ اللَّـهِ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ﴾

272.Si juu yako kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye. Na mali yoyote mnayoitoa ni kwa kwa ajili ya nafsi zenu, wala hamtoi ila kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mali yoyote mnayoitoa mtalipwa kwa ukamilifu wala hamtadhulumiwa.

﴿لِلْفُقَرَاءِ الَّذِينَ أُحْصِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ ضَرْبًا فِي الْأَرْضِ يَحْسَبُهُمُ الْجَاهِلُ أَغْنِيَاءَ مِنَ التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴾

273.Ni kwa ajili ya mafukara waliozuiliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi. Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia. Utawafahamu kwa alama zao; hawaombi watu wakang'anga' nia. Na mali yoyote mnayoitoa, kwa hakika Mwenyezi Mungu anaijua.

﴿الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ سِرًّا وَعَلَانِيَةً فَلَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴾

274.Wale watoao mali zao usiku na mchana kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao; wala haitakuwa hofu juu yao wala wao hawatahuzunika.

SI JUU YAKO KUWAONGOZA

Aya 272- 274

MAANA

Si juu yako kuwaongoza,lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye.

Yametangulia maelezo katika Aya ya 26 ya Sura hii kwamba neno Huda (uongofu) linatuTafsir miwa kwa maana nyingi; miongoni mwayo ni ubainifu na (uongofu), hiyo ni kazi ya Mtume. Maana nyengine ni tawfiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kuandalia njia ya kufanya kheri; nyingine ni kuongoka, yaani kukubali nasaha na kuzitumia, huku kunategemezwa kwa mja. Pia neno hilo lina maana ya thawabu na mengineyo. Maana ya uongofu katika "Si juu yako kuwaongoza" ni kuongoka na kukubali nasaha; yaani, kuitumia kwao haki si juu yako wewe, isipokuwa ni juu yako kufikisha haki tu.

﴿فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ﴾

"... Basi juu yako ni kufikisha na juu yetu ni hisabu" (13:40)

Maana ya uongofu katika;"Lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye" ni tawfiki katika njia ya kheri.

Inasemekana kuwa sababu ya kushuka"Si juu yako kuwoangoza" ni kwamba waislamu walikuwa hawatoi sadaka isipokuwa kwa watu wa dini yao, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume Wake kwa Aya hii na akataka kuwabanishia waislamu wote kwamba kafiri haadhibiwi kwa sababu ya kufuru yake kwa kunyimwa riziki na kudhikishwa ili alazimike kuamini; na haifai kwa yeyote kufanya hivyo hata kama ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.

﴿أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ﴾

"...Basi je wewe utawalazimisha ili wawe waumini?" (10:99).

Aya inafahamisha kwamba sadaka ya sunna au ya wajibu inajuzu kuwapa wasiokuwa waislamu, lakini kauli ya Mtume(s.a.w.w) :"Nimeamrishwa kuchukua sadaka kutoka kwa matajiri wenu na kuitoa kwa mafukara wenu", inahusu sadaka ya sunna tu sio ya wajibu.

Na mali yoyote mnayoitoa ni kwa ajili ya nafsi zenu.

Huenda mtu akadhania kuwa kutoa ni hasara kwake na ni kuwanyima watoto wake na ndugu zake. Ndipo Mwenyezi Mungu akaondosha dhana hii, kwamba mwenye kutoa inamrudia yeye kheri na nafuu katika dunia na akhera. Katika akhera atapata malipo na thawabu. Ama katika dunia, Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Kutoa kunazuia mafukara kuwafanyia ubaya matajiri, kwa sababu mafukara wakiwa na dhiki, watakwenda kuwaibia matajiri, kuwaudhi na kuwanyang'anya. Kisha uovu wao huu unawaendea wengine; mara nyingine ufisadi huo huenea kwa ujumla na kuondoa raha na amani." Sijui kama Sheikh Muhammad Abduh ameitoa fikra yake hii kutoka vyama vya wafanyakazi ambavyo vimewaletea matatizo matajiri na kuwalazimisha kukubali haki nyingi za wafanyakazi.

Wala hamtoi ila kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Yaani: maadamu mnakusudia radhi ya Mwenyezi Mungu katika kutoa kwenu, basi Mwenyezi Mungu atakubali. Ni sawa muwe mumempa mwislamu au asiyekuwa mwislamu kwa sharti ya kuwa iwe ni mali nzuri sio mbaya. Pia kusiweko na masimbulizi na maudhi. Inasemekana kuwa Aya ina maana ya kukataza kwa njia ya kutolea habari; yaani msitoe isipokuwa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Na mali yoyote mnayoitoa mtalipwa kwa ukamilifu wala hamtadhulumiwa.

Hata kutoa kukiwa kwa asiyekuwa mwislamu, lakini hamtapunguziwa chochote katika malipo, ikiwa mliyempa ni muhitaji.

WATU WA SUFA (UPENUNI)

Kuna jamaa waliohamia Madina, wakiacha miji yao mali zao na watu wao. Hapa Madina hawakuwa na maskani yoyote wala jamaa na hawakuwa na nyezo za kujichumia maisha, wala hawakuweza kusafiri kutafuta riziki. Idadi yao ilikuwa watu mia tatu, wengine wanasema ni mia nne. Wakawa wako msikitini tu, wakiabudu na kuzilinda nyumba za Mtume. Pia walikuwa wakijifundisha Qur'an na kuihifadhi, jambo ambalo lilikuwa ni katika twaa bora zaidi, kwa sababu huko ni kuihifadhi dini. Wakati huo huo walikuwa wakitoka pamoja na Mtume katika kila vita. Walikuwa wakikaa upenuni mwa msikiti ndio maana wakaitwa watu wa upenuni (Ahlu Sufa). Mtume(s.a.w.w) , alikuwa akiwahimiza na kuwaambia:"Furahini enyi watu wa Suffa; yeyote atakayekuwa na sifa mlizo nazo nyinyi katika umma wangu, basi yeye ni katika marafiki zangu."

Hao ndio wanaofaa zaidi kupewa sadaka; Kwa sababu wao ndio walioshukiwa na Aya hii:

Ni kwa ajili mafukara waliozuiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi. Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia. Utawafahamu kwa alama zao; hawaombi watu wakang'ang'ania.

Mwenyezi Mungu katika Aya hii amewataja watu wa Sufa kwa sifa tano:-

1. Kujitolea kwa Jihadi na kutafuta elimu. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu "waliozuiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu", kwa sababu mvivu hawezi kuambiwa kuwa ameifunga nafsi yake katika njia ya Mwenyezi Mungu.

2. Kushindwa kuchuma: ndiyo makusudio ya kusema kwake: "Wasioweza kwenda huku na huko."

3. Kujizuia, Mwenyezi Mungu anasema: "Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia."

4. Kuonekana kuwa ni mafukara kwa hali yao tu, sio kwa sababu ya kuombaomba: ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Utawafahamu kwa alama zao."

5. Kuacha kuomba vilivyo mikononi mwa watu kwa kunga'ang'ania: Kwenye hilo Mwenyezi Mungu ameashiria kwa kusema "Hawaombi watu wakang'ang'ania". Tumetaja katika tafsiri ya Aya ya 177 katika Sura hii, kwamba kuomba bila ya dharura ni haram.

Wale watowao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao; wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

Mwenyezi Mungu ametaja hukumu ya kutoa katika Aya kumi na nne mfululizo, ya mwisho ikiwa ni hii ambayo ni muhtasari wa yaliyotangulia na kutilia mkazo fadhila ya kutoa katika nyakati zote, iwe ni usiku au mchana, na kwa siri au kwa dhahiri. Razi ametaja kauli nyingi katika sababu za kushuka Aya hii, miongoni mwa hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Ali bin Abu Twalib(a.s) alikuwa na dirham nne tu, akatoa kwa siri na nyingine kwa dhahiri, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii.

ZAKA

Zaka sio sadaka ya sunna, kwa sababu sadaka huitoa mwislamu kwa hiyari, wala haihitaji kufikia kiwango fulani na haina jengine zaidi ya kukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu peke Yake; na malipo yake yanaanzia maradufu ya kumi hadi maradufu ya mia saba na zaidi ya hapo, kiasi ambacho hakina mwisho kulingana na lengo la kutolewa kwake. Ama Zaka, ni faradhi, ni haki ya lazima katika mali ya kiwango fulani na hutolewa kwa anayestahiki. Ni ya tatu katika nguzo tano za uislamu ambazo ni: Shahada mbili, Swala, Zaka, Saumu na Hijja. Baadhi ya wenye ghera na uislamu wanaona kuwa Zaka ni mpango wa uchumi au ni utaratibu fulani wa kiuchumi wa kiislamu. Wengine wanaichukulia kuwa ni kodi ya mali za matajiri. Ukweli ni kwamba Zaka si kodi au mpango fulani wa kiuchumi. Kwa sababu sharti ya msingi ya kukubaliwa Zaka, ni nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, bila hivyo haikubaliwi kabisa. Na kodi au utaratibu wa kiuchumi hauzingati sharti hii.

Zaidi ya hayo, utaratibu wa kiuchumi, kwa maana ya kisasa, kwanza unaangalia nyezo za uzalishaji; kama vile ardhi, madini na viwanda. Mfumo wa kibepari unazingatia kuwa ni milki ya mtu binafsi anayeimiliki. Ama mfumo wa kijamaa unazingatia kuwa ni milki ya umma inayoongozwa na serikali. Na Zaka haiangalii haya kabisa, Ama kodi nayo inasimamiwa na kiongozi wa nchi katika kupatikana kwake na kuitoa; haiwezekani kwa mtoaji kwa hali yeyote kuacha kuitoa kwa kiongozi, ambaye ndiye mwenye uwezo wa kuitumia. Mafaqihi wote wanasema kuwa mwenye kumiliki mali anaweza kutoa Zaka bila ya idhini ya kiongozi, naye anaweza kuaminiwa, bila ya ushahidi wowote au kiapo, akisema kuwa amekwishatoa. Sasa Zaka na kodi ni wapi na wapi? Bali mafaqihi wamejuzisha kwa mkusanyaji Zaka kuitoa kwa mafukara yeye mwenyewe bila ya kuipeleka kwenye Baitul Mal (hazina ya Waislamu).

Imam Ali(a.s) alimwambia mmoja wa wanaokusanya Zaka:"Tumia mali uliyonayo kwa wenye watoto wanaohitaji na wenye njaa." Kwa dhahiri ni kwamba kodi haina matumizi haya kabisa. Mtu anaweza kusema: Faradhi ya zaka maana yake ni kukubali kwamba ufukara lazima uwepo, na kwamba uislamu unaukabili ufukara kwa sadaka, jambo ambalo natija yake ni kuweko tabaka ya utajiri na umasikini?

Jibu : Matumizi ya Zaka hayakufungika kwa fakiri na maskini tu, isipokuwa katika jumla ya matumizi yake ni maslahi ya umma, ambayo Mwenyezi Mungu ameyaeleza kwa ibara ya sabilillah (njia ya Mwenyezi Mungu) katika Aya nyingi. Kwa hiyo kama hakukupatikana fukara, basi Zaka hutumiwa katika njia hii. Kwa hali hiyo, Zaka hailazimishi kuweko fukara kwa namna yoyote, wala Zaka sio ikrari ya kusema ufukara ni chapa isiyoepukika.

Pili : wajibu wa jamii ni kuwatunza masikini ili wasiwe ombaomba na wazururaji. Jambo hili

linapatikana hata katika miji ya kijamaa ambayo haikubali utabaka. Tatu: Tutamfanyaje mgonjwa asiyeweza hata kununua dawa na mwenye njaa ambaye hana njia yoyote ya kupata chakula katika jamii inayoongozwa na ufisadi. Je tuache mpaka hali itakapokuwa nzuri na umasikini utakapoondoka? Au tuweke kanuni itakayodhamini maisha yao? Je, inawezekana kupatikana mabadiliko kwa msitari wa kalamu? bila ya kupitia vipindi vingi? Hakika Uislamu unapiga vita aina zote za unyonge,na Mtume(s.a.w.w) aliutolea mawaidha, Baadhi ya riwaya zinasema:"Ufukara unakurubia kuwa kufuru". "Mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko mnyonge" Ujumbe wa Mwenyezi Mungu una lengo la heshima ya mtu na utengeneo wake; na ufukara ni upungufu na madhila na ni mashaka na balaa, Kwa hivyo haiwezekani uislamu kuukubali. uislamu haukatai kuweko katika jamii tajiri na tajiri zaidi au mwenye nguvu na mwenye nguvu zaidi, isipokuwa unachokataa ni kuweko fukara na mnyonge. Uislamu haukuweka Zaka kwa ajili ya masikini tu kama inavyodhaniwa bali ni kwa kutatua matatizo mengi, ukiwemo umasikini kama upo. Vilevile utumwa, ambapo unapatiwa uhuru na mali ya Zaka. Matatizo mengine ni kuhudumia askari wanaopigana Jihadi, na mengineyo katika maslahi ya umma; kama vile kujenga shule, hospitali, barabara na miradi ya maji.

Tutaeleza ufafanuzi wa matumizi ya Zaka katika Sura ya (9:60) Inshallah. Lau tunakadiria kuwa mtu ataweza kupitiwa na wakati ambao hauna masikini na mahitaji yote ya umma yametoshelezwa, kiasi ambacho matumizi ya Zaka hayatapatikana kabisa, basi bila shaka itaachwa. Na wakati huo utafika tu; kama ilivyokuja Hadith katika Sahih Bukhari Juzuu ya 9 mlango wa Fitan; anasema Mtume(s.a.w.w) : "Toweni sadaka, utakuja wakati mtu atatemebea na sadaka yake asipate wa kuikubali." Zaidi ya hayo, uislamu umemwajibishia mtoaji Zaka wakati anapompatia muhitaji kutomuudhi na kutomvunjia heshima yake na asikwaruze hisia zake. Kwamba huko kutoa ni wajibu wake na ni deni ambalo hapana budi kulitekeleza. Kwa kutilia mkazo maana haya Qur'an inasema:

﴿وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ ﴿٢٤﴾ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ ﴾

"Na ambao katika mali yao iko haki maalum kwa ajili ya aombaye na anayezuilika kuomba." (70: 24 - 25)

Yamekwishatangulia maelezo katika tafsiir ya Sura hii Aya (262-263) kuhusu kuudhi, Pamoja na kuwa Uislamu umezishinda sheria zote za dini zingine na za kufanywa na watu kwa kuweka sheria hii ya Zaka sheria hii ya kibinaadamu ambayo hawakuigundua waweka nidhamu ispokuwa baada ya Uislamu kwa mamia ya miaka na kuiita 'dhamana ya jamii', pamoja na yote hayo jambo bora zaidi kuwapa wahitaji katika mtazamo wa kiislamu, ni kuwaandalia kazi inayonasibiana na uwezo wao ili wahisi thamani ya uhai. Mwenyezi Mungu humpenda mja wake mumin anayejishughulisha na kazi. Mwisho tunamaliza maelezo haya kwa kauli ya Imam Ja'far Asswadiq(a.s) :"Kila kiungo katika viungo vyako kina Zaka ya Mwenyezi Mungu: Zaka ya jicho ni kuzingatia na kulifumba na mambo ya haramu, Zaka ya sikio ni kusikiliza elimu na hekima, Zaka ya ulimi ni kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapa nasaha Waislamu, Zaka ya mkono ni kutoa na Zaka ya mguu ni kuhangaikia jihadi na kusuluhisha watu."

﴿الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا فَمَن جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَانتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّـهِ وَمَنْ عَادَ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

275.Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu. Hayo ni kwa sababu wanasema kuwa biashara ni kama riba. Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba. Na aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, akakoma, basi yake ni yaliyokwishapita na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele.

﴿يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ ﴾

276.Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri afanyae dhambi.

﴿إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾

277.Hakika wale walioamini wakafanya vitendo vizuri na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴾

278.Enyi mlioamini! Mcheni Mungu na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini.

﴿فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ ﴾

279.Na kama hamtafanya, basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu, basi haki yenu ni rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe.

﴿وَإِن كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَىٰ مَيْسَرَةٍ وَأَن تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴾

280.Na kama ana dhiki, basi angoje mpaka awe na uwezo. Na kama deni mkizifanya sadaka, basi ni bora kwenu ikiwa mnajua.

﴿وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴾

281.Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi ilipwe iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa.

Aya 275 - 281

MNASABA

Maudhui ya sadaka na riba yote ni mali, ingawa kuna tofauti ambayo ni: Sadaka hutolewa bila ya kutaka kurudishiwa; ni tohara, safi na dhamana. Ama riba ni kutoa kwa kutaka kurudishiwa mali pamoja na ziada; ni tamaa, uchoyo, uchafu, unyang'anyi na maangamizo. Kwa hiyo maudhui ni sawa, lakini hukumu na lengo ni kinyume kabisa. Ikiwa vitu hutajwa kwa mifano yake basi pia hutajwa kwa vinyume vyake, Ndio maana ikaja hukumu ya riba mara tu baada ya hukumu ya sadaka (Zaka). Kabla ya kuingilia kufasiri Aya, tutaanza kuonyesha riba inavyoeleweka katika sharia, dalili ya uharamu wake na yanayo sababisha uharamu.

NENO RIBA

Neno: 'riba' katika lugha maana yake ni ziada; kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu katika Sura (22:5). Katika sharia, riba inagawanyika kwenye mafungu mawili: Riba ya kukopesha na riba ya kuzidishiana katika bei. Maana ya riba ya kukopesha, ni mtu kumkopesha mwingine kitu chochote na kumlazimisha yule aliyemkopesha manufaa yoyote kwa sababu ya kumkopesha; kama vile kukopesha shillingi kumi kwa sharti ya kurudishiwa kumi na moja. Au kwa yasiyokuwa manufaa ya mali; kwa mfano mkopeshaji kumshurutisha aliyemkopesha amfanyie kazi fulani au amwazime kitabu au kitu chochote. Mtume(s.a.w.w) anasema:"Kukopesha kokote kunakovutia manufa ni haramu." Hapo hakutofautisha aina ya manufaa. Hata hivyo kama mkopaji akilipa deni pamoja na ziada ya ahsante, itafaa kwa mkopeshaji kuichukua. Mtume(s.a.w.w) alikuwa akilipa deni pamoja na ziada, akisema:"Bora ya watu ni yule anayewakopesha watu vizuri."

Inatakikana tuzingatie kuwa riba inathibiti katika kukopesha kwa kushurutisha ziada na manufaa kwa namna yoyote ile ya ziada, ni sawa iwe ziada ya kipimo cha mizani ujazo, urefu au idadi. Vilevile ni sawa iwe ni katika namna ya mali iliyokopeshwa au namna nyingine. Kwa maneno mengine riba ya kukopesha haina tofauti katika dhati ya kitu kwa kitu au manufaa.

Ama riba ya bei ni kuzidishiana kitu kil kile, na masharti yake ni mawili:

Kwanza: ni kupeana kwa ziada aina hiyo hiyo kwa jina lake la uhakika, kama kuuza ngano kwa ngano, au kuuza ngano nzima kwa unga wa ngano, kwa sababu unga umetokana na ngano nzima. Vilevile Wanga (nishaa) na unga, kwani vyote viwili vimetokana na asili moja ambayo ni ngano.

Dalili ya pili ni kuwa wanavyouziana viwe vinaweza kupimwa kwa ujazo au mizani tu. Kwa hiyo hakuna riba kwa vinavyouzwa kwa idadi; kama mayai. Inawezekana kuuzwa yai moja kwa mawili. Pia hakuna riba kwa kinachouzwa kwa kuonyeshana; kama nguo na wanyama. Kwa ufupi ni kwamba riba ni haramu katika deni kwa namna yoyote ile, na katika bei ni haramu kwa vinavyopimwa kwa namna yoyote, kwa sharti ya kuwa vyote viwili viwe ni jinsi moja. Hayo tumeyafafanua zaidi katika kitabu chetu Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq(a.s) Mlango wa Riba.

UHARAMU

Riba ni haramu kwa nukuu ya Qur'an, Hadith mutawatir na kongamano la Waislamu wote, tangu siku za Mtume(s.a.w.w) mpaka leo. Bali uharamu wake hauhitaji dalili, kwa sababu ni katika mambo yaliyo wazi; kama vile wajibu wa Swala na uharamu wa zina. Kwa sababu hiyo ndipo mafaqihi wakahukumu kwamba mwenye kukanusha uharamu wa riba, basi ni kafiri, kwa vile amekanusha dharura ya dini iliyothibiti. Kama ilivyo haramu kuchukua riba, pia ni haramu kuitoa. Hadith ya Mtume inasema:"Ameilaani Mwenyezi Mungu riba, mwenye kuila, mwenye kuuza, mwenye kununua, mwandishi wake na shahidi wake."

SABABU YA HARAMU

Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu, kwamba Yeye ndiye mwenye kuweka sharia ya halali na haramu, basi hawezi kutaka mengi zaidi ya wahyi katika kuharamishwa riba. Na kama ikitokea kuuliza sababu, basi haulizi kwa sababu ya kujikinaisha, isipokuwa ni kwa kutaka kufahamu tu; au kwa ajili ya kuwakinaisha wale walioelezewa na Aya hii:

﴿وَإِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَحْدَهُ اشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ وَإِذَا ذُكِرَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ ﴾

"Na anapotajwa Mwenyezi Mungu pekee yake, mioyo ya wale wasioamini akhera huchafuka, na wanapotajwa wale asiyekuwa yeye wanafurahi." (39:45).

Vyovyote iwavyo ni kwamba wametaja sababu kadha za kuharimishwa riba. Miongoni mwa sababu hizo ni kama ifuatavyo:- Kupingana na misingi ya kibinadamu; kama vile kufanyiana wema, kusaidiana na kuoneana huruma. Kuwa hiyo riba maana yake ni kula mali ya batili, Kwa sababu mwenye kula riba anaichukua bila ya kufanya lolote. Mtu anaweza kusema kuwa anayechukua riba hufanya kitu, kwa sababu mali yake anaitoa kwa aliyekopa ambaye anaitumia na kunufaika nayo. Kwa hivyo hali ya riba ni sawa na kukodisha ardhi, nyumba au mnyama.

Mtu akisema hivyo tutamjibu: Kuna tofauti kubwa kati ya kukodisha na riba, kwani mwenye kukodisha hana jukumu la kulipa kile alichokikodisha, kama kikifa au kikihariibika, isipokuwa kama yeye ndiye aliyesababisha. Lakini chenye kukopwa kikiharibika,basi mwenye kukopa atakilipa. Kwamba mwenye kuchukua riba hupata faida daima na mwenye kukopa hupata hasara; matokeo yake, matunda yote yanaishia kwa mchukuaji riba Baadhi ya maprofesa wa mambo ya uchumi wa Ulaya wameijua aibu hii. Miongoni mwa hao wataalamu ambao wameinukia katika nidhamu za riba, ni Dkt. Schacht, Mjerumani, Meneja wa zamani wa Benki alisema katika mhadahara alioutoa Damascus mnamo mwaka 1953:

"Tukifanya mahesabu tutajua kuwa mali yote katika dunia inaishia kwenye idadi ndogo sana ya wanaokula riba. Hiyo ni kwa sababu anayekopesha kwa riba, daima hupata faida katika kila kitu, wakati ambapo mwenye kudaiwa kwa riba anatazamia kupata faida na hasara; hatimaye ndipo mali yote inaishia kwa yule mwenye uhakika wa faida, Nadharia hii iko njiani kuthibitika. Kwani wenye mali humiliki maelfu ya pesa. Ama wenye milki wote, na wenye viwanda ambao wanakopa kutoka katika mabenki, n.k. hawana lolote isipokuwa ni waajiriwa tu, wakiwatumikia wenye mapesa ambao wanachukua matunda ya jasho lao." Kuna baadhi ya wataalamu wa kiuchumi waliothibitisha kwamba msingi na asili ya fikra ya riba unatokana na mayahudi, na watu wengine wamechukua fikra hiyo kutoka kwao, hayo hayako mbali, kwani historia ya mayahudi wa kale na wa sasa inathibitisha kuwa Mungu wao, dini yao heshima ya siasa yao ni mali tu peke yake haina mshirika; na njia yoyote ya kuleta mali ni tukufu, hata kama ni umalaya, ukuwadi, uasi, wizi, unafiki au ria na uovu wowote ule.

MAANA

Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu.

Shetani hamzugi yoyote, wala hana uwezo wowote wa kumfanya mtu kuwa mwenda wazimu. Isipokuwa hiyo ni tash'bihi na kuleta karibu ufahamu wa watu wanaosema kuhusu mtu aliiyepatwa na wazimu: "Amepagawa na Shetani." Maana ya Aya ni kwamba hali ya wanaofanya riba, ni sawa na hali ya mwenda wazimu ambaye amezugwa, katika matendo yake, na kuwa shaghalabalaghala. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibn Abbas kuwa watu wa riba watafufuka kutoka makaburini mwao kama wenda wazimu, hiyo itakuwa ndio alama yao kwamba wao ni wala riba.

Hayo ni kwa sababu wamesema kuwa biashara ni kama riba.

Wamehalalisha riba kwa kuleta falfasa ya kuwa biashara na riba zinafanana kwa njia zote; basi kwa nini riba nayo isiwe halali? Si mtu anaweza kuuza kitu cha thamani ya shilling tano kwa shilingi sita na kwamba mtu anaweza kuuza kwa bei ya taslim shilingi moja tu na kwa mkopo shiling mbili? Kwa hiyo, eti inatakikana kuweko na ruhusa ya mtu kutoa shilingi kumi mpaka mwezi ujao kwa shilingi kumi na moja. Mwenyezi Mungu anayajibu madai haya kwa kusema:

Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba.

Njia ya majibu hayo ni kuwa, kule kufanana kwa kidhahiri hakufanyi kuwa ndio kufanana kabisa. Kwani biashara ni kazi ya kibiashara yenye kutafuta manufaaa; mwuzaji anakuwa kati ya kupata faida na hasara, kwa hivyo faida yake ni mavuno ya taabu yake, na wala sio kula mali ya batil, ambapo riba ni faida tu na kuchukua ziada bila ya jasho, kwa hiyo inakuwa ni kula mali ya batili.

Kwa ajili hiyo ndio Mwenyezi Mungu akahalalisha biashara na akaharamisha riba.

Basi kutofautiana kihukumu ni dalili ya kutofautiana kihali na kinyume chake.

Na aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, kisha akakoma, basi yake ni yaliyokwisha pita.

Yaani aliyekuwa amechukua riba, kabla ya kuteremshwa Aya ya kuiharamisha kisha akaacha baada ya kuharamishwa,Pia yule mwenye kusilimu sasa ikiwa amechukua riba kabla ya kusilimu kwake, si wajibu kurudisha baada ya kusilimu. Aya hii ni sawa na ile inayosema:

﴿وَلَا تَنكِحُوا مَا نَكَحَ آبَاؤُكُم مِّنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ﴾

"Wala msiwaoe wake waliowaoa baba zenu, isipokuwa yale yaliyokwishapita ..." (4:22)

Kuacha kuchukulia mambo yaliyopita, kuko katika mambo mengi, hasa mambo ya mali. Wameeleza sababu kuwa ni kutoleta matatizo ya kiuchumi.

Na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu

Wametaja njia nyingi katika kufasiri ibara hii, kiasi ambacho akili haiwezi kutosheka, ambalo tumelifahamu sisi ni kuwa mwenye kuchukua riba bila ya kujua hukumu yake na akaacha baada ya kujua makatazo ya Mwenyezi Mungu kwa kumtii, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atamsaidia na kumtosheleza kwa halali yake. Kwa sababu ameacha haramu kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu; na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu atamtoshea.

Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele.

Maana yake ni kuwa wale ambao hawafuati amri ya Mwenyezi Mungu wala kuacha makatazo yake na kuendelea kula riba kwa inadi na kupuuza, basi watawekwa milele motoni. Kwa sababu mfano wa inadi hii hauwi isipokuwa kutokana na kafiri mkanushaji.

Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri afanyaye dhambi.

Yaani mwenye kula riba hutaka ziada katika mali yake, lakini riba kwa hakika ni kupungua mali na uchafu ulioharamishwa. Na haramu hutoa mali kutoka kwa aliye nayo na inafanya matumizi ya riba yawe kama matumizi ya mali ya kunyang'anya, zaidi ya hayo ni dhambi na adhabu. Kimsingi ni kuwa kila linalokuwa ni sababu ya kumkasirisha Mwenyezi Mungu na adhabu, basi ni uchafu na upungufu na ni amali ya shetani. Ama sadaka, inasafisha mali na kuitakasa na inaifanya thabiti miliki ya mwenye kutoa sadaka na Zaka. Vilevile inaleta radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu Yake. Huo ndio ukamilifu na ziada hasa. Kwa maneno mengine ni kwamba wingi, wa mali ya haramu ni uchache, na uchache wa mali ya halali ni wingi.Kafiri afanyae dhambi ni yule anayefanya inadi ya kula riba bila ya kushtuka na ni yule anayeendelea kufanya inadi ya kukataa kutoa Zaka, na kutoshtuka na vitendo vya Mwenyezi Mungu na kiaga chake.

Kwa kutegemea Aya hii, yafaa kusema kuwa waislamu wengi wakati huu ni makafiri wafanyao dhambi, kwa sababu ya kung'angania riba na kuacha kutoa Khums na Zaka.

Hakika wale walioamini wakafanya vitendo vizuri na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.

Aya hii iko dhahiri katika maana, haihitaji tafsiri, zaidi ya hayo tafsiri yake imekwishapita katika Aya ya 25 na 82 ya Sura hii. Isipokuwa ameirudisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ahadi hii kwa kufuatisha ahadi baada ya kiaga na kinyume. Kwa hiyo alipoelezea kiaga cha wanaofanya riba amefuatishia ahadi kwa watu wema.

Kwa ujumla Aya kwa dhahiri inafahamisha kuwa imani ya nadharia tu, bila ya vitendo si chochote.

Enyi mlioamini! Mcheni Mungu na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini.

Kusema: Acheni yaliyobaki katika riba kunafahamisha kuwa uharamu sio katika yale yaliyopita nyuma, kama tulivyoeleza.

Na kama hamtafanya, basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu Na Mtume Wake.

Na hakuna jambo linalowajibisha kutangaza vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa anayeng'angania kula riba ila, ni kwa kuwa yeye ni kafiri au yuko katika hukumu ya kafiri; hata kama kula kwake riba ni kwa kupuuza tu, si inadi. Lakini riwaya zilizopokewa kutoka kwa Masum zimegawanya kula riba katika mafungu mawili.

Kwanza : ni yule anayekula kwa kuifanya halali. Huyo ni kafiri bila shaka yoyote, kwa sababu amekana dharura ya dini. Imam Jaffar Sadiq(a.s) aliambiwa fulani anakula riba na anaita 'lubba" (kiini), akasema:"Nikimpata nitaikata shingo yake."

Pili : ni kula kwa kupuuza hukmu ya Mwenyezi Mungu pamoja na kuamini uharamu wake. Huyu atatakiwa kutubia mara ya kwanza na ya pili; kama akiendelea atauliwa. Imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) kuwa mwenye kula riba atatiwa adabu baada ya kubainika, akirudia atatiwa adabu, akirudia atauliwa. Imesemekana kuwa atauliwa mara ya nne.

Na mkiwa mmetubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe.

Yaani msimdhulumu mdaiwa kwa kumtaka zaidi ya rasilmali; wala msidhulumiwe kwa kupunguziwa rasilimali.

Na kama ana dhiki basi angoje mpaka awe na uwezo.

Kila mwenye kudaiwa riba, au isiyokuwa riba haijuzu kumdhiki ikiwa ana uzito; kama ambavyo pia haifai kwa mdaiwa kuchelewesha deni akiwa na uwezo. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Kama ambavyo si halali kwa mdeni wako kukucheleweshea deni akiwa na uwezo, vilevile si halali kwako nawe kumdhikisha akiwa na uzito"

Kiwango cha mwenye dhiki ni ambaye hamiliki chochote zaidi ya nyumba yake ya kukaa na vitu vyake vya dharura; kama nguo, vitabu na vyombo vya nyumbani vya lazima. Vilevile zana zake za kufanyia kazi zinazompatia chakula chake na cha familia yake na gharama yake ya siku moja. Vyote hivi si wajibu kuviuza kwa kulipa deni. Hayo tumeyataja kwa ufafanuzi katika kitabu 'Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq' mlango wa Muflis.

Na kama (deni) mkizifanya sadaka, basi ni bora kwenu ikiwa mnajua.

Hapana shaka kwamba kumsamehe deni mwenye dhiki ni fadhila katika dini, bali ni katika utii mkubwa. Kwani hilo ni kumfanya apumue na kuweza kutekeleza haja zake vizuri. Imekuja Hadithi: "Mwenye kumvumilia mwenye uzito au kumsamehe, Mwenyezi Mungu atampa kivuli siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli cha Mwenyezi Mungu."

Mafaqihi wameafikiana kwa kauli moja kuwa mwenye kukopa katika dharura ya halali, kisha akashindwa kulipa, atalipiwa deni lake kutoka katika hazina ya waislamu (Baitul Maal). Imam Jaffar Sadiq(a.s) anasema:"Mwenye kuchukua riziki hii kwa uhalali kwa ajili yake na ya watoto wake, ili airudishe baadae anakuwa kama mpigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Akishindwa kulipa na amkope Mwenyezi Mungu na Mtume wake"

Maana ya kumkopa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kwamba deni lake litalipwa kutoka katika hazina ya waislamu. Na hilo ni kuitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu. Qur'an imelieleza hilo kwa kusema:

﴿إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴾

"Sadaka hupewa: mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao na katika kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na wasafiri. Ni faradhi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima." (9: 60)

Kauli yake Mwenyezi Mungu "Ikiwa mnajua" ni kutilia mkazo kufanya kitu kwa kujua; yaani maadamu mnajua kuwa kumsamehe deni mwenye dhiki ni heri, basi ni juu yenu kufanya kwa kujua kwenu hili.

Imesemekana kuwa makusudio ya kujua ni kufanya; yaani mkiwa ni wafanya heri, basi litoeni sadaka deni kwa mwenye dhiki.

Maelezo haya hayako mbali, na kauli ya Imam Ali(a.s) anasema:"Elimu iko na matendo, mwenye kujua hufanya, elimu hubaki kwa kuifanyia kazi, vinginevyo huondoka." Wataalamu wengi wa kisasa hawaiti nadharia yoyote kuwa ni elimu mpaka wauone ukweli wake kwa kufuatishia na majaribio.

Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi ilipwe iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kukataza riba kwa mkazo na kuamrisha kumfanyia subira mdaiwa mwenye dhiki, au kumsamehe, katika Aya saba, kisha anafuatisha Aya anayowahofisha waasi na siku ya hisabu na malipo na adhabu yake. Katika Majmaul Bayan imeelezwa kuwa Aya hii ni ya mwisho kumshukia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na kwamba yeye aliishi siku 21 tu baadaye.