TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17360
Pakua: 3458


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17360 / Pakua: 3458
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿فَلَمَّا أَحَسَّ عِيسَىٰ مِنْهُمُ الْكُفْرَ قَالَ مَنْ أَنصَارِي إِلَى اللَّـهِ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ أَنصَارُ اللَّـهِ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَاشْهَدْ بِأَنَّا مُسْلِمُونَ﴾

52.Alipohisi Isa ukafiri wao alisema: "Nani watakuwa wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?" Wanafunzi wakasema: "Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemwamini Mwenyezi Mungu nawe shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.

﴿رَبَّنَا آمَنَّا بِمَا أَنزَلْتَ وَاتَّبَعْنَا الرَّسُولَ فَاكْتُبْنَا مَعَ الشَّاهِدِينَ ﴾

53.Mola wetu! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja na washuhudiao.

﴿وَمَكَرُوا وَمَكَرَ اللَّـهُ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ ﴾

54. Na wakapanga hila; na Mwenyezi Mungu akapanga hila; na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga hila.

NI NANI WASAIDIZI WANGU

Aya 52 - 54

HAKI NA MANUFAA

Hakuna yeyote mwenye akili timamu anayeweza kuipinga haki na kuitanguliza batili, isipokuwa kwa tamaa ya nafsi, au kutatizika katika fahamu yake, au kutojua dalili, au dosari katika utoaji dalili. Ni wazi kwamba dalili za manabii zimetosheleza kabisa kuthibitisha unabii wao katika pande zote, mpaka kufikia kuondoa makosa ya fikra na mikanganyo, kiasi ambacho hazibakishi dalili zao hoja yoyote ya kuipinga haki, isipokuwa inadi na kiburi. Yeyote mwenye kutafuta sababu iliyowafanya wapinzani kuwafanyia vitimbi mitume na kupinga ujumbe wao - baada ya kuona dalili na miujiza- ataona ni sababu ya manufaa ya kibinafsi na kupupia mali na jaha. Ushahidi wa hakika hii kutoka katika vitabu vya Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume, hauna idadi. Miongoni mwa mifano hiyo ni: Mataghuti wapenda anasa katika watu wa Nabii Hud, walipinga, si kwa lolote isipokuwa tu, aliwaambia:

Je, manajenga juu ya kila mwinuko ukumbusho wa upuuzi? Na mnajijengea majengo ya fahari ili mkae milele? Na mnaposhambulia, mnashambulia kwa jeuri (28:127-130)

﴿قَالُوا يَا شُعَيْبُ أَصَلَاتُكَ تَأْمُرُكَ أَن نَّتْرُكَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا أَوْ أَن نَّفْعَلَ فِي أَمْوَالِنَا مَا نَشَاءُ﴿٩١﴾وَلَوْلَا رَهْطُكَ لَرَجَمْنَاكَ﴾

Matajiri katika watu wa Nabii Shuaib walimtisha na kumwambia: "Ewe Shuaib hivi Swala zako zinakuamrisha tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu Lau si jamaa zako tungelikupiga mawe" (11: 87, 91)

Kosa lake tu, ni kuwa aliwaambia:

﴿وَيَا قَوْمِ أَوْفُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴾

"Na enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwapunguzie watu vitu vyao; wala msiwe waovu katika nchi mkafanya uharibifu" (11:85)

Qarun alikuwa tajiri sana katika watu wa Musa na ni mtu aliye karibu zaidi naye kiudugu, lakini pamoja na hayo alimfanyia uadui alipompa waadhi huu

﴿وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّـهُ إِلَيْكَ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴾

"Na ufanye wema kama alivyokufanyia wema Mwenyezi Mungu wala usitafute kufanya ufisadi katika nchi; hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafisadi." (28:77)

Abdalla bin Ubayya alikuwa ni katika viongozi na matajiri wa Madina. Mtume alipohamia huko, alipatwa na wivu; akamwambia Mtume maneno ya kutokubaliana naye. Sa'ad bin Ubada akamwambia Mtume: "Usiyatilie maanani maneno yake; kwani sisi tulikuwa tunataka kumpa Ufalme, naye anaona kuwa wewe umemnyang'anya."( [9] )*9 Yatosha kuwa ni dalili ya hakika hii, kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿كُلَّمَا جَاءَهُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنفُسُهُمْ فَرِيقًا كَذَّبُوا وَفَرِيقًا يَقْتُلُونَ﴾

"Kila alipowajia Mtume na lile ambalo nafsi zao halilipendi, wengine waliwakadhibisha na wengine wakawaua" (5:70)

Walimkadhibisha Bwana Masih (Yesu) na kujaribu kumuua, kwa sababu yeye aliwapa mwito wa mapenzi, uadilifu, usawa na kutolimbikiza dhahabu na huku wengine wana njaa na mahitaji. Miongoni mwa mafunzo yake ni: "Msilimbikize mali ardhini. Tajiri kuingia mlango wa mbinguni ni kama kamba nene kuingia kwenye tundu ya sindano."

MAANA

Isa alipohisi ukafiri wao

Kabla ya kuzaliwa nabii Isa, mayahudi walikuwa wakiamini Masih atakayekuja, Alipowajia na hoja na miujiza, walitofautiana; wakamwamini maskini na wanyonge ambao hawakuhofia kupoteza mali wala jaha, lakini matajiri na wenye jaha walimkanusha kwa kuhofia vyeo vyao na chumo lao; kama ilivyo kwa yeyote anayekuja kutengeza; awe mtume au si mtume, hata kama watamjua kuwa ni mkweli mwenye haki. Baadhi ya wafasiri wamekosea waliposema kuwa Mayahudi walimkataa Muhammad kwa vile ni Mwarabu wa kizazi cha Ismail, na kwamba kama angekuwa ni myahudi wa kizazi cha Is-haq(a.s) basi wangelimkubali! Mbona Isa alikuwa myahudi, lakini pamoja na hayo walimpiga vita na kujaribu kumuua na kutaka kumsulubu. Vilevile Muhammad waliompiga vita ni Mamwinyi wa Kiquraish. Siri ya hapa na huko ni moja tu, kupigania dunia na manufaa na wala sio ubaguzi wa kikabila. Vyovyote, itakavyokuwa, ni kwamba Isa alihisi watu wake waking'ang'ania ukafiri kwa inadi, na akapata tabu kutoka kwao; kama alivyopata tabu Muhammad (s.a.w.w.) kutoka kwa watu wake; ndipo Isa aliposema:

"Ni nani watakuwa wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu"

Yaani ni kina nani hao na wako wapi waumini wa kuinusuru na kuihami dini ya Mwenyezi Mungu, na ambao wataendeleza tabligh baada yangu? Kwani kila mwenye ujumbe hana budi kuwa na wasaidizi watakaomwamini na kumwakilisha kwa watu.

Wanafunzi wakasema: "Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, tumemwamini Mwenyezi Mungu nawe shuhudia kuwa sisi ni Waislamu. Mola wetu! Tumeamini uliyoyateremsha na tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia"

Kusema sisi ni waislamu ni dalili kwamba dini ya Mwenyezi Mungu ni moja tu tangu mwanzo hadi mwisho wa kikomo. Dini yenyewe ni uislamu ndiyo waliyokuja nayo mitume wote. Tofauti iko kwenye baadhi ya hukumu na sura ya ibada tu. Kwa hivyo basi, kila anayemwamini Mwenyezi Mungu, Vitabu Vyake na Mitume Yake, basi huyo ni mwislam, hata kama atajiita mkristo au yahudi. Ufafanuzi wa hilo umetangulia katika kufasiri Aya 19 ya Sura hii. Kauli ya wanafunzi: "Tuandike pamoja na wanaoshuhudia. " Ni dua yao kumwomba Mwenyezi Mungu (s.w.t) awajaalie katika fungu la waumini walioshuhudia umoja wa Mungu na kuwa na uaminifu, ili wafuzu yale waliyofuzu wenye ikhlasi wenye kuridhiwa; na wapate karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Katika tafsir nyingi imeelezwa kuwa wanafunzi walikuwa kumi na wawili. Baadhi ya wafasiri wametaja majina yao na kazi zao. Lakin sisi tunanyamaza kutokana na Hadith isemayo."Nyamazeni aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu"

MWENYEZI MUNGU NI MBORA WA WAFANYA HILA

Na wakapanga hila; na Mwenyezi Mungu akapanga hila; na Mwenyezi Mungu ni mbora wa wapanga hila.

Kuna Aya nyingi nyingine zinazofanana na Aya hii, kama zifuatazo:

﴿وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ ﴾

Na wanapanga hila; na Mwenyezi Mungu anapanga hila; na Mwenyezi Mungu ni mbora wa wapanga hila. (8:30.)

﴿وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴾

Na wakapanga hila na sisi tukapanga hila, na hali hawatambui (27:50).

﴿قُلِ اللَّـهُ أَسْرَعُ مَكْرًا إِنَّ رُسُلَنَا يَكْتُبُونَ مَا تَمْكُرُونَ ﴾

Sema: Mwenyezi Mungu ni mwepesi zaidi wa kupanga hila, hakika wajumbe wetu wanaandika hila mnazozipanga (10:21)

Makusudio ya hila kwa makafiri na wanafiki, ni vitimbi, hadaa, hiyana na kupanga njama. Ama hila ya Mwenyezi Mungu, makusudio yake ni kuzitangua hila na njama za wenye hila; kama ilivyosema Aya:

"Na hila mbaya hazimpati ila yule aliyezifanya" (35:43)

Katika Qur'an kuna sifa nyingi sana alizosifiwa Mwenyezi Mungu ambazo kwa dhahiri zinaonekana kuwa hafai kusifiwa nazo mfano: Mwenye shukrani, Mumin, Mwingi wa toba na Mwenye kiburi, Lakini ukiyafikiri vizuri maana yake, utayaona yako mahali pake. Maana ya Mwenye shukrani ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawalipa thawabu wenye kushukuru na watiifu. Mumin maana yake yeye ndio chimbuko la amani na salama. Mwingi wa toba, ni kwamba yeye anakubali toba za wenye kutubia. Na mwenye kiburi ni kwamba kila kilichomo ulimwenguni ni duni kwake yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa maana hayo, inatubainikia kuwa hila ni haramu ikiwa itakusudiwa kumdhuru mwengine; na itakuwa halali ikiwa itakusudiwa kujikinga na madhara ya mtu binafsi au mwengine.

Hebu tutaje mifano miwili ya kubatilisha hila za Makfiri na vitimbi vyao:

Mayahudi walipanga hila ya kumuua Isa(a.s) , lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaipan-gua njama yao, pale alipomfananisha Yahudha na Isa, yule myahudi aliyehimiza kuuliwa Isa, na akampaza Isa mbinguni. Maquraish kwa pamoja walipanga kummaliza Muhammad, kwa kumchagua kijana kutoka kila ukoo, wampige kwa panga zao akiwa amelala na damu yake iwe kwa wote. Lakini Mwenyezi Mungu akapangua hila zao, pale alipomwamuru kutoka Makka na Ali alale kitandani pake ili watu wafikirie kuwa Muhammad hajasafiri, walipovamia nyumba wakamkuta Ali ndiye aliyelalala kitandani.

﴿إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴾

55.Aliposema Mwenyezi Mungu: "Ewe Isa! Mimi nitakufisha, Na nikuinue kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru, mpaka siku ya kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nitahukumu baina yenu katika yale mliyokuwa mkihitalifania.

﴿فَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَأُعَذِّبُهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ﴾

56.Ama wale waliokufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na Akhera, na hawana wa kuwanusuru.

﴿وَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُوَفِّيهِمْ أُجُورَهُمْ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴾

57.Na wale walioamini na wakatenda matendo mema, atawalipa ujira wao, Na Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kudhulumu.

﴿ذَٰلِكَ نَتْلُوهُ عَلَيْكَ مِنَ الْآيَاتِ وَالذِّكْرِ الْحَكِيمِ ﴾

58.Haya tunayokusomea ni katika Ishara na mawaidha yenye hekima.

KUONDOKA ULIMWENGUNI

Aya 55 - 58

KUTOFAUTIANA KUHUSU ISA

Watu wametofautiana sana kuhusu nabii Isa. Wametofautiana kuhusu kupatikana kwake, tabia yake na hata kufa kwake; Kuna wanaosema kuwa hakuweko kamwe, na kwamba habari zake ni vigano tu, kauli hii ilijitokeza mnamo karne ya kumi na tisa (19) huko Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Ni kauli ya kipumbavu kabisa; kwani ni sawa na kusema kuwa hakuna ukristo wala uislamu unaomwamini Isa. Wengine wamesema ni Mungu, wengine wakasema ni binadamu, mayahudi nao wakasema kuhusu Isa na mama yake mambo ambayo yanaweza kuitingisha hata Arsh. Ama waislamu wametofautiana kama ifuatavyo: Wengi wamesema hakufa na kwamba yeye yuko hai kimwili na kiroho mbinguni au mahali pengine popote; na atatoka duniani wakati wa mwisho mwisho wa dunia. Kisha hapo ndipo Mwenyezi Mungu atamuua mauaji ya kihakika, Waislamu wengine wamesema kuwa yeye amekwisha kufa mauti ya kiuhakika na kwamba iliyopazwa ni roho yake tu, sio mwili. Tofauti hii ya Waislamu imetokana na kutofautiana dhahiri ya Aya; kama ifuatavyo:

﴿وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا ﴿١٥٧﴾ بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا﴾

"Na hawakumuuwa wala hawakumsulubu, lakini alifananishwa kwao, Na kwa hakika wale waliohitilafiana katika hayo wamo katika shaka nayo, hawana ujuzi nayo isipokuwa kufuata dhana tu; na hawakumuuwa kwa yakini, Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye hekima" (4: 157 - 158)

Dhahiri Aya hii kwa kuongezea Hadith za Mtume, zinayonyesha kuwa nabii Isa yuko hai.

Lakini Aya nyengine inayosema:

Uliponifisha wewe ukawa mchungaji juu yao" (5:117)

pamoja na Aya hii tuliyonayo. Maana yanayokuja haraka ni mauti. Na, maana ya dhahiri ni kuwa mimi nitakufisha na kukujaalia mahali patukufu kama ilivyo kuhusu Idris:

"Na tulimwinua daraja ya juu kabisa" (19:57)

Au kama ilivyo kuhusu mashahidi:

﴿وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ﴾

Wala usidhani wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu, bali wao wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao" (3:169)

Wale wanaosema kuwa Isa yuko hai kiroho na kimwili, wameleta taawili kuwa neno tawaffaytani na Mutawaffika (kufisha) kwa njia nyingi zenye nguvu zaidi ni ile inayosema makusudio ni kufananishwa na mauti, si mauti ya kihakika. Kwa sababu anapopaazwa mbinguni anakuwa hana mfungamano tena na dunia; kwa hiyo anakuwa kama maiti.

Ama wale waliosema kuwa amekufa kiuhakika wameleta taawili ya neno Hawakumuua kwamba mayahudi hawakuua msingi wa Isa na mafundisho yake kwa sababu ya kumuua na kumsulubu. Lakini waliletewa mawazo tu, ya kuwa wameyamaliza mafunzo yake lakini bado yamesimama tu na yatabakia mpaka siku ya ufufuo. Sisi tuko pamoja na kauli ya kwanza; kwamba Isa yuko hai, Mwenyezi Mungu alimwinua kwake baada ya kumkamilishia maisha yake duniani kwa namna isiyokuwa ya mauti. Tuko kwenye rai hii kwa kuangalia dhahiri ya Aya na yaliyopokewa kutoka kwa Sunni na Shia kwamba yeye bado yuko hai.

Lakini pamoja na hayo yote, sisi hatuoni faida yoyote ya kuhakikisha na kuangalia kwa undani kuhusu maudhui haya. Kwa sababu kuamini namna ya kubainika uhai wake hapa duniani, na kuinuliwa kwake si misingi ya dini wala misingi ya madhehebu. Pia si katika matawi yake, isipokuwa ni maudhui ya nje yasiyofungamana na maisha yetu si kwa karibu wala mbali. Mwenyezi Mungu kesho kamwe hatauliza watu kwamba Isa alikufa vipi, au vipi alivyoinuliwa, Tunachopaswa kuamini ni kuwa Isa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, naye ameumbwa kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba mama yake ni mtakatifu. Zaidi ya hayo utafiti wa maudhui haya hauishii kwenye yakini ya kujua aina ya kwisha maisha ya Isa au kuinuliwa kwake. Kwa hiyo lililo bora ni kumwachia Mwenyezi Mungu (s.w.t.)"( [10] )

Aliposema Mwenyezi Mungu: Ewe Isa! Mimi nitakufisha na nikuinue kwangu.

Baada ya mayahudi kung'ang'ania kutaka kumwua Isa na kupanga njama. Mwenyezi Mungu alimpa bishara ya kumwokoa na kuvunjilia mbali vitimbi vyao na kwamba atamkamilisha muda wake kwa njia ya kawaida; atamgurisha kwenye ulimwengu mwengine ambako hatapata adha ya mtu yeyote na wala hakuna utawala wa yeyote ispokuwa Mwenyezi Mungu, hayo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Nitakutakasa na wale waliokufuru.

Yaani nitakuweka mbali na uchafu wao na utangamano wao mchafu na shari wanayokutakia.

Na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru mpaka siku ya kiyama.

Makusudio ya kuwa juu hapa ni kwa kinafsi na kiukamilifu na wala sio kifalme na kimali. Hapana mwenye kutia shaka kwamba wale waliomwamini Isa ni bora kuliko waliomkadhibisha.

Kisha marejeo yenu ni kwangu niwahukumu katika yale mliyokuwa mkihitalifiana.

Hapa hapahitaji tafsir,kwani maana yaliyo dhahiri ndiyo yaliyokusudiwa. Zaidi ya hayo ni kwamba dhamir inaenea kwa wote waliohitalifiana kuhusu Bwana Masih katika sifa zake kila mahali na kila wakati.

Ama wale waliokufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na akhera na hawana wa kuwanusuru.

Adhabu ya akhera inajulikana, Ama adhabu ya duniani ni kwamba yeye (kafiri) ni tofauti na mwislam katika vipengele vingi vya sharia, kama vile kufaa kumsengenya kafiri, au kuwa kafiri anauliwa akimuua mwislam, lakini mwislam hauliwi kwa kumuua kafiri, bali hana hata fidia - kama walivyosema mafakihi wengi - isipokuwa akiwa dhimii; lakini fidia ya dhimii inatofautiana na ya mwislam kwa tofauti kubwa( [11] ).

Na ama wale walioamini na wakatenda matendo mema, atawalipa ujira wao; Na Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kudhulumu.

Katika Hadith imeelezwa kuwa dhalimu na mwenye kuridhia dhulma ni sawa. Imam Baqir(a.s) anasema:"Dhulma ni aina tatu: dhulma anayoisamehe Mwenyezi Mungu, dhulma asiyoisamehe Mwenyezi Mungu, na dhulma asiyoiacha Mwenyezi Mungu. Ama dhulma anayoisamehe ni ile ya kujidhulumu mtu mwenyewe kati yake na Mola wake. Dhulma asiyoisamehe ni ile ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Ama dhulma asiyoiacha ni kuwadhulumu waja"

Imam Ali(a.s) anasema:"Kumdhulumu mnyonge ndio dhulma mbaya kabisa"

Haya tunayokusomea ni katika ishara na mawaidha yenye hekima.

Haya ni ishara ya yale ambayo Mwenyezi Mungu amemwelezea Mtume wake kuhusu habari za mamake Maryam, Maryam mwenyewe na Zakariya. Vilevile Yahya, Isa, wanafunzi, wayahudi na wapinzani.

Maana yake ni kuwa tumekusomea ewe Muhammad habari hii ili iwe hoja na dalili kwa yule unayejadiliana naye kuhusu Isa n.k. Ama kuwa habari hizi ni hoja ya Muhammad, ni kwamba yeye hajui kusoma wala hakuna mtu anayemwambia hayo. Kwa hiyo inabaki kuwa kujua kwake habari hizi ni kwa njia ya wahyi tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Makusudio ya mawaidha yenye hekima ni Qur'an.

﴿إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ﴾

59.Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.

﴿الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُن مِّنَ الْمُمْتَرِينَ ﴾

60.Ni haki kutoka kwa Mola wako, basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.

﴿فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنفُسَنَا وَأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَتَ اللَّـهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ﴾

61.Na watakao kuhoji baada kukufikia elimu hii, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wana wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.

﴿إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْقَصَصُ الْحَقُّ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴾

62.Hakika haya ni maelezo ya kweli, na hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima .

﴿فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِالْمُفْسِدِينَ ﴾

63.Na wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu.

MFANO WA ISA NI KAMA WA ADAM

Aya 59 - 63.

MAANA

Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.

Wafasiri wanasema kuwa ujumbe wa Najran (Yemeni) ulimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Kwa nini unamshtumu sahibu wetu ?" (yaani Isa) Akasema: "Vipi?" Wakasema: "Wewe unasema kuwa yeye ni mja" Akasema: "Ndiyo yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu, na ni Mtume wake na ni tamko lake alilompelekea bikira Maryam" Wakamuuliza: "Je, umekwishaona mtu asiyekuwa na baba? "Ndipo ikashuka Aya: "Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam" Ikiwa riwaya hii ni sahih au si sahihi, lakini haya ndiyo maudhui ya Aya hii hasa. Kwa sababu wakristo walikuwa, na bado, wanaendelea kutoa hoja ya itikadi yao kuwa Isa ni Mungu, kwa vile amezaliwa bila ya baba. Lakini Mwenyezi Mungu ameivunja hoja yao hii kwa Adam; Ikiwa Isa ni mungu au mwana wa Mungu, kwa sababu ya kuzaliwa bila ya baba, basi Adam ndiye anayefaa zaidi kuwa Mungu, kwa sababu yeye amezaliwa bila baba wala mama. Hawakuijibu hoja hii, na wala hawatajibu mpaka siku ya mwisho.

Unaweza kuuliza kuwa inavyoonyesha kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu alimuumba kwa udongo ni kwamba Mwenyezi Mungu alimtengeneza Adam kwa ukamilifu; kwa maana ya kuwa kuumba kulitangulia kauli ya "Kun fayakun", kwa hiyo kulikuwa hakuna haja tena ya kauli hii kwa sababu maana yake ni kuumba kilichoumbwa; na maneno ya Mwenyezi Mungu hayafai kuwa hivyo. Jibu: Mungu alimuumba Adam kwa vipindi; miongoni mwa vipindi hivyo ni kwamba yeye alimuumba kwa udongo, kisha akatia roho. Kwa hiyo maana yanakuwa: "Ewe udongo! Kuwa mtu aliye na nyama, damu, hisia na utambuzi"

MITUME NA MAASI

Ni haki kutoka kwa Mola wako Yaani haya tuliyokuteremshia na kukufahamisha kuhusu Isa ni haki kutoka kwa Mola wako. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka. Unaweza kuuliza kuwa ni muhali Mtume kutilia shaka aliyoyatolea habari Mwenyezi Mungu. Kwa sababu shaka inapingana na imani, sikwambii isma. Sasa makatazo haya ni ya nini? Wafasiri wamelijibu swali hili kwa majibu mawili:

Kwanza : kwamba dhahiri inonyesha kuwa msemo unaelekezwa kwa Mtume, lakini makusudio ni wengine.

Pili : makusudio ni kuendelea Mtume na yakini. Njia zote mbili inabidi kuziangalia vizuri kwa sababu zinamaanisha kuwa haifai kwa Mwenyezi Mungu kuwakataza maasi mitume Yake. Ilivyo hasa ni kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuwakataza mitume maasi kwa vile kwanza hiyo ni amri ya mkubwa kwa mdogo.

Pili: Isma si maumbile na tabia ya mitume mpaka iwe ni muhali kuweko uwezekano wa kufanya maasi. Kama ni hivyo basi wasingekuwa na ubora wowote.

Wao wanaweza kufanya maasi, lakini hawafanyi maasi, Kwa hiyo basi inafaa kwa Mwenyezi Mungu kuwapa makatazo, lakini makatazo yawe yanatoka Kwake Mwenyezi Mungu tu, sio kwa mtu mwengine. Kwa sababu hakuna aliye zaidi ya Mtume isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu tu. Makatazo mengi yaliyokuja katika Qur'an yanachukuliwa kwa njia hii. Mfano kauli Yake Mwenyezi Mungu kumwambia kipenzi Chake Muhammad(s.a.w.w) :"Wala usiwatii makafiri." (33:48). Hatujui pengine wenyewe Mitume, walikuwa wakipenda makatazo haya kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), bali pengine walikuwa wakiyataka hasa; kama vile Mumin mwema anavyotaka kupata mawaidha na kukumbushwa Mungu kutoka kwa mjuzi.

MUBAHALA

Na watakaokuhoji baada ya kukufikilia elimu hii, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.

Hii ndiyo Aya inayojulikana kwa jina la Aya ya Mubahala (maapizano), nayo ni miongoni mwa Aya zilizo msingi wa kitabu. Kusudio la kwanza la Aya hii Tukufu ni kuimarisha dini na kuuthibitisha ujumbe wa Muhammad kwa njia ambayo elimu na wanavyuoni hawakuizoweya, na ambayo haiwezi yeyote isipokuwa Muumbaji wa ardhi na mbingu.

Lakini ni njia ambayo inafahamika kiwepesi kwa mtu yeyote, awe mjuzi au si mjuzi. Kisa chenyewe kwa ufupi ni kama ifuatavyo: Aya hii inafungamana na mwaka wa tisa tangu Mtume kuhamia Madina. Mwaka huo ulijulikana kwa jina la mwaka wa ugeni. Kwa sababu Mtume alipata wageni kutoka sehemu mbali mbali za Bara arabu kuja kutangaza utii wao kwake, baada ya Mwenyezi Mungu kuliinua neno la kiislamu na kuwapa ushindi waislam dhidi ya maadui zao.

Miongoni mwa ugeni alioupata Mtume, ulikuwa ni ujumbe wa watu sitini, wakristo kutoka Najran, Yemen. Inasemekana mlikuwa na wakubwa wao kumi na nne; akiwemo mkubwa wao na kiongozi wao, Abdul-Masih, mshauri wao, Ahyab akiwa na lakabu ya Sayyid na Askofu ambaye alitukuzwa sana na mfalme wa Roma, alimjengea kanisa na chuo na kumpatia mali na mshahara. Mtume akawapokea kwa takrima. Ulipofika wakati wao wa kuswali, waligonga kengele na wakaswali katika Msikiti wa Mtume kuelekea Mashariki. Masahaba walipotaka kuwazuiya Mtume aliwakataza kwa kusema: "Waacheni." Baada ya kutulia wageni hao, wakaanza kujadiliana na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuhusu Isa wakidai kuwa yeye ni Mungu mara nyingine yeye ni mtoto wa Mungu na mara yeye ni watatu katika watatu. Wakaleta dalili ambazo tumekwisha zitaja na jinsi zilivyobatilishwa.

Aliyezibatilisha dalili za wakristo ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, lakini kupitia kwenye ulimi wa Mtume(s.a.w.w) . Na, katika ugeni huo mlikuwa na maulama ambao ukweli hauwezi kujificha kwao; kama vile Abu Haritha ambaye alikuwa kiongozi wa dini wa msafara. Yeye alikuwa na ndugu anayeitwa Kurzi. Abu Haritha baada ya kusikia aliyoyasikia kutokana na hoja za Mwenyezi Mungu zilizo wazi, alimwambia ndugu yake kwa siri kwamba Muhammad ndiye yule Mtume tuliyekuwa tukimngojea Nduguye akamwambia: "Sasa wangoja nini nawe una yakini na ukweli wake?" Akamwambia: "Unajua, wafalme wametupa mali nyingi na wametutukuza sana, lau tukimwamini Muhammad watatuyang'anya kila kitu. Likamwingia moyoni hilo na akalificha; kisha akasilimu na kulisimulia." Ukweli wa riwaya hii hauhitaji dalili, kwa sababu hiyo yenyewe inafahamisha ukweli wake, na kiasi chake kinachukuliwa pamoja na riwaya hii; kama wanavyosema watu wa mantiki. Watu wengi waliokanusha haki na kuipinga, walifanya hivyo kwa sababu ya masilahi yao ya kibinafsi kama tulivyoelezea kwa ufafanuzi katika Aya ya 54 ya Sura hii.

Mtume aliujadili ujumbe wa Najran kuhusu Isa, na akajadiliana nao kwa hoja yenye kubatilisha uwongo na mantiki ya kisawasawa yasiyokubali kuongezewa chochote. Walipong'ang'ania upinzani, Mtume aliukata mjadala na kuwataka kufanya jambo jengine lisilofanana na mjadala, lakini litakalomaliza ugomvi mara moja na kumaliza ubishi wote. Aliwataka neno moja tu, ambalo hawezi kulikataa ila yule anayejijua kuwa ni mwongo. Tamko lenyewe ni 'Laana ya Mwenyezi Mungu iwe kwa waongo." Lakini tamko lenyewe litaambatana na muujiza ambapo utapanda ukelele kwenye kichwa cha mwongo na aone dunia yote ni moto. Zimekuja Hadith Mutawatir katika vitabu vya Hadith na Tafsir, kama vile Sahih Muslim na Tirmidhi, Tafsir Tabari, Razi, Bahrul-Muhit, Gharaibul-Qur'an, Rawhul-Bayan, Al-Manar, Maraghib na nyenginezo nyingi. Hadith hizo zinaeleza kuwa, Mtume alitoka akiwa amembeba Husein na kumshika mkono Hasan; Fatima na Ali wakimfuata nyuma akiwaambia nitakapoomba nyinyi itikieni amin.

Kiongozi wa kidini wa msafara akawaambia wenzake: "Enyi Manasara! Mimi ninaona nyuso ambazo, lau zitaomba jabali liondoke lilipo basi linaweza kuondoka. Kwa hiyo msiapizane nao msije mkaangamia" Kisha akasema: "Ewe Abul-Kassim tumeonelea tusiapizane na wewe." Akawaambia: "Basi silimuni," wakakataa; kisha wakasuluhishana watoe kodi. Msafara ukarudi mikono mitupu, ukiwa umeshindwa na kufedheheka. Baada ya tukio hili, walisilimu wengi na kuwazidishia waumini imani na uthabiti. Muhammad(s.a.w.w) aliwaleta vipenzi vyake kwenye Mubahala akiwa na hakika ya ushindi, kama kwamba uko mikononi mwake. Hakuna kitu kilichofahamisha uwazi na ukweli juu ya hoja ya utume wake kuliko tendo hili. Ni dalili iliyo wazi zaidi kuliko dalili ya mwangaza wa jua kuwa jua lipo. Sijui kama muujiza huu alikuwa nao Mtume mwengine yeyote. Ingawaje walikuwa wakiwaombea makafiri na kuitikiwa maombi yao.

Unaweza kuuliza: Mtume aliwataka baadhi ya makafiri waamini; waliposema:

﴿اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴾

"Ewe Mwenyezi Mungu! Kama haya ni haki itokayo kwako, basi tupige kwa mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu yoyote iumizayo."( 8:32).

Lakini pamoja na hayo haikuwatukia adhabu hiyo.

Jibu : Mazungumzo tuliyo nayo yanahusu maapizano, ambayo yanathibiti kwenye mahojiano na madai tu; vilevile hayajuzu ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu au mjumbe wake kuhofia kutojitokeza ukweli wa mkweli. Ama kauli ya makafiri (Tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni) hayo ya mvua ya mawe si katika maapizano, Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu ameahirisha adhabu yao mpaka siku ya kufufuliwa.

AHLUL BAIT

Katika aliyoyasema Razi kuhusu tafsir ya Aya ya Mubahala ni: "Imepokewa kuwa Muhammad(s.a.w.w) alipotoka akiwa katika kitambaa cheusi, alikuja Hassan (r.a) akamwingiza, akaja Hussein (r.a.) akamwingiza, kisha Fatima, kisha Ali (r.a..). Mtume akasema:

﴿إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu Ahlul bait watu wa nyumba ya Mtume na kuwatakasa kabisa kabisa." (33:33)

Anaendelea kusema Razi Jua kwamba riwaya hii - kama wailivyoafikiana usahihi wake watu wa tafsir na Hadith - inafahamisha kuwa Hassan na Hussein walikuwa watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu aliahidi kuwaita watoto akawaita, Hassan na Hussein(a.s) , kwa hivyo hilo limewajibisha kuwa ni watoto wake. Linalotilia mkazo hili ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na katika kizazi chake Daud na Suleiman na Zakariya na Yahya na Isa." (6: 84-85)

Inavyojulikana ni kwamba Isa ananasibishwa kwa Ibrahim kwa upande wa mama, sio wa baba.

Nimefanya utafiti mrefu wa maudhui haya katika kitab Fadhail Imam Ali (fadhila za Imam Ali) na nikaweka mlango maalum wa 'watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Hakika haya ni maelezo ya kweli, na hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu; na hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima, Na wakikataa, basi hakika Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu.

maneno haya ni ishara ya yaliyotangulia kuhusu Isa na kwamba yeye ni Mtume, wala si mtoto wa zina (wa haramu) kama wanavyodai mayahudi; wala pia siyo Mungu au mwana wa Mungu, kama wanavyodai wakristo. Asiyeamini uhakika huu basi achana naye ewe Muhammad, kwa sababu Mwenyezi Mungu anajua mfisadi na mpotevu na ana uwezo wa kumwadhibu.

﴿قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ ﴾

64.Sema: "Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu. Kwamba tusimwabudu yo yote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa waungu zaidi ya Mwenyezi Mungu Wakikataa, semeni: "Shuhudieni ya kuwa sisi ni waislamu.

﴿ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تُحَاجُّونَ فِي إِبْرَاهِيمَ وَمَا أُنزِلَتِ التَّوْرَاةُ وَالْإِنجِيلُ إِلَّا مِن بَعْدِهِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴾

65. Enyi watu wa Kitabu! kwanini mnabishana juu ya Ibrahimu, na hali Tawrati na Injili havikuteremshwa ila baada yake? Basi, hamfahamu?

﴿هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ حَاجَجْتُمْ فِيمَا لَكُم بِهِ عِلْمٌ فَلِمَ تُحَاجُّونَ فِيمَا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴾

66.Je, nyinyi ni wale mnaojadiliana katika lile mlilolijua, Mbona (sasa) mnabishana katika lile msilolijua? Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye, nyinyi hamjui (kitu).

﴿مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴾

67.Ibrahimu hakuwa myahudi wala mnaswara (mkristo), lakini alikuwa mwenye kuachana na dini potofu, na kushikamana na haki; wala hakuwa katika washirikina.

﴿إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَـٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ ﴾

68.Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahimu ni wale waliomfuata, na Mtume huyu na walioamini pamoja naye Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa waumini.

NJOONI KWENYE NENO LA USAWA

Aya 64 - 68

MAANA

"Sema enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu. Kwamba tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa ni miungu, zaidi ya Mwenyezi Mungu."

Mayahudi, wanaamini Tawrat, Wakristo wanaamini Tawrat na Injil, na waislam wanaamini Tawrat, Injil na Qur'an. Vitabu vyote hivi vitatu kwa pamoja vinakubali kuwa kuna mwenye kuutengeneza ulimwengu mwenye hekima, lakini wakristo wameingia ndani sana, wakamfanya Mungu kuwa na washirika, wakamnasibishia mtoto na wakawafanya maaskofu wao ni miungu wanaowahalalishia na kuwaaharamishia. Imepokewa Riwaya kuwa Adiy bin Hatim alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu chake kitukufu:

﴿اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ﴾

"Wamewafanya makasisi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Mwenyezi Mungu." (9:31).

Lakini wakristo hawawaabudu wanavyuoni na watawa" Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akasema: "Kwani si walikuwa wakiwahalalishia na kuwaharamishia, na nyinyi munakubali maneno yao?" "Ndiyo" Adiyo akajibu, Mtume akaongeza: "Basi ndio hivyo." Bado tukiwa katika karne ya ishirini tunasoma magazetini kwamba fulani amekutana na Baba (Mtakatifu) na akambariki. Vilevile makadinali na maaskofu wakuu, hutoa baraka. Ama Waislamu, wao wanaitakidi kwamba baraka haiwezi wala haitakuwa ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu:

Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu." (11:73)

Ama Mayahudi, walimkana Isa(a.s) na wakajaribu kumsulubu, wakamkana Muhammad(s.a.w.w) wakiwa wanajua ukweli wake.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَلَمَّا جَاءَهُم مَّا عَرَفُوا كَفَرُوا بِهِ فَلَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴾

"Lakini yalipowajia yale waliyokuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya makafiri" (2:89)

Mtume alijadiliana na watu wa Kitabu kwa mjadala mzuri, na akawapa aina kadhaa za dalili zilizowanyamazisha, lakini bado waling'ang'ania ukafiri. Kisha akawaita kwenye maapizano, lakini wao wakaona bora watoe kodi kwa unyonge, kuliko kuikubali haki. Pamoja na yote hayo alijitahidi ili waamini; kama ilivyo kawaida yake na kila mpinzani mpaka Mwenyezi Mungu akamwambia:

﴿وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ﴾

"Na wengi katika watu hawatakuwa wenye kuamini hata ukijitahidi vipi" (12:103)

﴿ن تَحْرِصْ عَلَىٰ هُدَاهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَن يُضِلُّ﴾

"Hata ukiwa na jitihada ya kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu hamuongozi yule anayepoteza" (16:37)

Kwa kutilia mkazo hoja kwa wapinzani na kuwadhihirishia hakika mbele ya Mtume na watu wote, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia kuwa aachane na kujadiliana nao na kuapizana nao,na afuatane nao na njia hii ambayo anaishuhudia kila mwenye akili kuwa ni haki na uadilifu, bali ni njia ya wazi. Njia yenyewe ni kuwaita kwenye lile linalokubaliwa na akili na vitabu vya dini kuwa nyote mlingane sawa katika kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee asiye na mshirika; na wala wengine wasiwaabudu wengine. Pia baadhi ya watu wasiwe juu ya wengine, Na hili ndilo neno la uadilifu.

"Wakikataa semeni: Shuhudieni kuwa sisi ni Waislamu"

Yaani kama hawakukubali hata dhahiri hii na kuwa na inadi ya ushirikina, basi achana nao, na wewe pamoja na wale waliokuamini waambieni, sisi ni Waislamu. Kuwashuhudisha makafiri kuhusu uislamu wa waislam, kuna faida mbili:

Kwanza : Kuwatambulisha makafiri kwamba wao hawawajali na ukafiri wao na kwamba Muhammad na walio pamoja naye wanaiamini haki na kuitumia hata kama watakufuru watu wa Mashariki na Magharibi.

Pili : Kuonyesha kuwa waislamu wanatofautiana na wengine kwa kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja pekee, wala hawafanyi baadhi kuwa waungu kinyume na Mwenyezi Mungu, au kuweko na yeyote mwenye mamlaka ya kuhalalisha, kuharamisha na kufuta madhambi; kama ilivyo kwa wasiokuwa waislamu.

Enyi watu wa Kitab! Kwa nini mnabishana juu ya Ibrahim, na hali Tawrat na Injil havikuteremshwa ila baada yake? Basi hamfahamu?

Qur'an imewajadili watu wa Kitabu kwa akili na mantiki, kwenye maapizano na kwenye neno la usawa - ambalo ni kumwamini Mungu peke yake. Kisha ikarudia tena mjadala na watu wa Kitabu; kama kawaida yake kulieleza jambo, halafu kueleza jengine hatimaye kulirudia lile la kwanza. Imerudia kuelezea kauli za watu wa Kitab na ubatilifu wake. Imetaja kauli ya mayahudi kwamba Ibrahim alikuwa myahudi na kauli ya manaswara kwamba Ibrahimu alikuwa mnaswara.

Qur'an Imejibu madai haya waziwazi, kuwa uyahudi ulitokea baada ya Musa, na baina ya Musa na Ibrahim kulikuwa na miaka elfu mbili. Unaswara nao ulizuka baada ya Isa na baina ya Isa na Ibrahim kuna miaka elfu; kama ilivyoelezwa katika Tafsir Rawhul bayan basi itakuwaje aliyetangulia awe katika dini ya aliyekuja nyuma? Basi hamfahamu? Kauli ya wayahudi na wanaswara inatukumbusha kichekesho kimoja wanachokisimulia walebanon : Kwamba watu wawili walikuwa wakisafiri pamoja. Walipokuwa wakizungumza mmoja akamuuliza mwenzake: ."Umewahi kuhiji Makka Tukufu?"

"Ndio, nimetekeleza Al-hamdulillah"

"Umeona Zamzam huko?"

"Ndio, ni msichana mzuri sana!"

" Vipi wewe, si msichana! Ni kisima cha maji bwana!

" Ah! Basi wamekichimba baada ya kuhiji mimi."

Hekaya za madhehebu na vikundi vilivyozuka baada ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) zinafanana kidogo na hoja za mtu huyo. Kila anayechukua dini yake kutoka kwa mtu yeye huwa ni aina hii isipokua kama itamthibitikia nukuu kutoka kwa Mtume Mtukufu(s.a.w.w) kama vile kuthibiti Hadith Thaqalayni ambayo imewajibisha kufanya ibada kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul Bait wa Mtume, Na ikavifanya sawa viwili hivyo. Tumeyafafanua hayo katika tafsir ya (2:39)

Je, nyinyi ni wale mliojadiliana katika lile ambalo mnalolijua. Mbona (sasa) mnabishana katika lile msilolijua na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye na nyinyi hamjui ( kitu).

Mtu anaweza akahusika kujua jambo fulani au maudhui fulani. Hapo anaweza kujadiliana na kubishana; na wala sio lazima awe yuko sawa katika maneno yake na mjadala wake wote, isipokuwa la muhimu ni kuwa awe anajua japo kwa ujumla. Ama kujadiliana na kubishana katika jambo asilolijua kabisa, basi ni ujinga na upumbavu. Watu wa Kitab wana dini yao wanayoitakidi; kwa hiyo kuna uwezekano wa kufanya mjadala unaohusiana na dini zao ijapokuwa kwa dhahiri lakini kufanya mjadala kuhusu dini ya Ibrahim hakuna njia yoyote hata kwa dhahiri, kwa sababu wao hawajui chochote.

-Ibrahim hakuwa myahudi wala mnaswara (mkristo) lakini alikuwa mwenye kuachana na dini potofu, na kushikamana haki, mwislamu wala hakuwa katika washirikina. Hakuwa myahudi kwa sababu, baina yake na Musa kulikuwa miaka elfu, wala itikadi yake haiambatani na dini ya kiyahudi, kwa sababu imegeuzwa sio ile aliyokuja nayo Musa(a.s) . Wala hakuwa mkristo, kwa sababu baina yake na Isa ilipita miaka elfu mbili wala itikadi yake haiambatani na itikadi ya dini ya kimasihi, kwa sababu imegeuzwa, siyo aliyokuja nayo Isa(a.s) . Ikiwa Ibrahim hakuwa mwislamu kwa maana iliyozoeleka, lakini alivyo yeye alikuwa mwislamu na imani yake inaambatana na imani ya uislamu. Kwa sababu, alikuwa akimwamini Mwenyezi Mungu na kumtakasa na shirk na kufananisha. Na huu ndiyo msingi wa asili ya dini ya Kiislam. Kwa hiyo, linabainika jibu la swali la atakayeuliza: Kwa nini Ibrahim ni mwislamu na Qur'an imeteremshwa baada yake? Umetangulia ufafanuzi kwamba Mitume wote walikuwa waislamu katika tafsir ya Aya ya 19 ya Sura hii.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Hakuwa katika washirikina, ni kuwapinga wanaswara waliosema kuwa Masih ni mtoto wa Mungu wayahudi waliosema na Uzair ni mtoto wa Mungu na waarabu waliokuwa wakiabudu masanamu, vikundi vyote hivi vitatu vilijihusisha na Ibrahim.

Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahim ni wale waliomfuata Mtume huyu na walioamini pamoja naye.

Yaani wenye haki ya kujinasibisha na dini ya Ibrahim ni wale walioitikia mwito wake au wale ambao itikadi yao inaambatana na yake; kama Muhammad na walio pamoja naye. Imamu Ali anasema: "Hakika watu walio karibu zaidi na manabii ni wale wanaojua zaidi waliyokuja nayo, kisha akasoma Aya hii akaendelea kusema: "Hakika mpenzi wa Muhamamd ni yule anayemtii hata kama yuko mbali naye kiudugu; na hakika adui wa Muhammad ni yule anayemwasi Mwenyezi Mungu, hata kama akiwa karibu naye Muhammad kiudugu"

Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa waumini, wale wanaomwamini Yeye bila ya kuwa na mshirika; na wala hawamtegemei yeyote kwa kuondolewa madhara na kutaka manufaa.

Hakuna kitu kinachofahamisha utukufu wa Imam Ali(a.s) , ikhlasi yake, na kuepukana kwake na malengo ya kidunia, kuliko kauli hii na kuacha kujiambatanisha na udugu ingawaje anajua kuwa yeye ndiye mtu wa karibu zaidi na Mtume kwa udugu. Yeye anategemea utukufu kutokana na nafsi yake na amali yake tu, na wala sio kutafuta asili na udugu au kwa kufunika mambo.

﴿وَدَّت طَّائِفَةٌ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَوْ يُضِلُّونَكُمْ وَمَا يُضِلُّونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ﴾

69.Kikundi katika watu wa Kitabu wanapenda kuwapoteza; wala hawapotezi ila nafsi zao, na hali hawatambui.

﴿يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَأَنتُمْ تَشْهَدُونَ ﴾

70. Enyi watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa Ishara za Mwenyezi

Mungu na, hali nyinyi mnashuhudia?

﴿يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَلْبِسُونَ الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴾

71.Enyi watu wa Kitabu! Mbona mnaichanganya haki na batili, na mnaficha haki na hali mnajua?

WANAJIPOTEZA WENYEWE

Aya ya 69 - 71

UISLAMU NI DINI YENYE NGUVU

Kikundi katika watu wa Kitabu wanapenda kuwapoteza, wala hawapotezi ila nafsi zao na hali hawatambui. Makusudio ya kikundi katika watu wa Kitab ni viongozi wa dini zao. Aya hii inaambatana kabisa na wahubiri wa kikiristo. Wao wanafanya kadiri wawezavyo wawaingize waislamu kwenye ukristo, Wakishindwa basi wanajaribu kuwapoteza na kuwatia shaka kubwa katika uislamu, ili wabakie bila dini. Kwa kufanya hivyo wanajifanyia ubaya wao wenyewe bila ya kutambua, Kwa sababu kuudhoofisha uislamu,. kama dini inayoelekeza kuweko Mwenyezi Mungu mpangaji mwenye hekima, kunamaanisha kushindwa dini zote na viongozi wake walio na fikra hiyo wakiwemo wakristo. Hii ndiyo tafsir ya hawapotezi ila nafsi zo na hali hawatambui.

Sijui ni kwa nini wafasiri hawayazingatii maana haya pamoja na uwazi wake, ambapo wamesema kuwa makusudio ya watu wa Kitab kujipoteza wao wenyewe, ni adhabu yao kesho kwa sababu ya kujaribu kuwapoteza waislam. Ama Sheik Muhammad Abdu na Razi, wamefasiri kujipoteza wao kuwa ni jaribu lao la kuwapoteza waislam bila kufanikiwa, kwamba hakuna mwislamu yeyote aliyekubali au kudanganyika na upotofu wao. Lakini usahihi hasa ni tulioueleza. Kudhoofisha uislamu ni kudhoofisha dini zote na watu wake. Vyovyote ilivyo uislamu pamoja na misingi yake una nguvu kiasi ambacho si rahisi kutingishwa na ukristo au na dini nyingine. Waabudu masanamu, milima na watu wa Kitabu wameingia kwa makundi katika uislamu kwa radhi yao na kukinai, wakiwemo wanavyuoni wao wakubwa. Sijui kama kuna Mwislamu wa kikweli kweli aliyeujua uislamu kiuhakika, ambaye ameuacha Uislamu.

Mwandishi wa kifaransa Henry Descarte anasema katika kitabu chake" Al-Islam sawani wa khawatwir," kifungu cha Uislamu Algeria anasema, ninamnukuu: "Tumeshuhudia Uislam ukionyesha nguvu zake na uhai wake kwa kupata waabudu mizimu wengi katika Afrika na kuwafanya ni jeshi moja chini ya bendera ya Qur'an na hakuna katika watu Waislamu anayeweza kwenda kwenye dini nyingine." Kwa mnasaba wa haya tunaleta kisa hiki kizuri cha kuvutia: Katika kumi la atatu la karne ya 20 kundi la wahubiri wa kikristo lilikwenda mji wa Amara ulioko Iraq ambao wakazi wake wote ni waislamu Shia. Jamaa hao walikwenda kwa lengo la kuwageuza wawe wakristo. Wakaanzisha mashule, na Zahanati, wakafanya matangazo na kuweka hafla wakamwaga mapesa. Mhubiri wao kila alipopanda jukwaani na kuelezea miujiza ya Yesu, Waislamu walikuwa wakipaza sauti" Salawatullah ala Muhammad wa Ali bayt Muhammad" (Rehema za Mwenyezi Mungu zimshukie Muhammad na watu wa nyumba ya Muhammad). Lilipokaririka hilo, walikata tama. Mapesa, shule,zahanati hazikulea manufaa yoyote kwao, wakarudi mikono mitupu. Enyi watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa ishara za Mwenyezi Mungu na hali nyinyi mnashuhudia?

Makusudio ya Ishara za Mwenyezi Mungu hapa ni dalili za utume wa Muhammad s.a.w.w ukweli wa Qur'an na utukufu wa mafunzo ya kiislamu. Enyi watu wa Kitab Mbona mnachanganya haki na batili na mnaficha haki na hali mnajua. Makusudio ya haki hapa ni yale yaliyowabainikia watu wa Kitabu kuhusu ukweli wa uislamu na nabii wake. baadhi ya watu wa kitabu walikuwa na bado wako wanaojaribu kuupaka matope uislamu na waislamu, wakimnasibisha Mtume pamoja na Qur'an uwongo na uzushi, kwa mfano wanadai kuwa Muhamamd anawalingania watu wamwabudu yeye kwa sanamu ya dhahabu, kwamba Muhammad alikuwa akipiga ngoma na nzumari na kwamba yeye ana ugonjwa wa kupagawa n.k. Yote ni chuki na kutojiamini.( [12] )

Dkt Zakiy Najib anasema katika kitabu chake Ayam fi Amrika kwamba yeye alipokuwa Amerika alihudhuria tamthilia iliyojaa dharau na kebehi kwa Quran na Uislam. Hiyo ndiyo nchi iliyoendelea ambayo inadai kuwa inabeba nembo ya dini na huku inatupa makombora kwa wanyonge kwa madai ya kupiga vita ulahidi.

﴿وَقَالَت طَّائِفَةٌ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ آمِنُوا بِالَّذِي أُنزِلَ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَجْهَ النَّهَارِ وَاكْفُرُوا آخِرَهُ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴾

72.Kikundi katika watu wa kitabu kilisema: Yaami nini yale waliyoteremshiwa wale walioamini mwanzo wa mchana na yakataeni mwisho wake, huenda wakarudi nyuma.

﴿وَلَا تُؤْمِنُوا إِلَّا لِمَن تَبِعَ دِينَكُمْ قُلْ إِنَّ الْهُدَىٰ هُدَى اللَّـهِ أَن يُؤْتَىٰ أَحَدٌ مِّثْلَ مَا أُوتِيتُمْ أَوْ يُحَاجُّوكُمْ عِندَ رَبِّكُمْ قُلْ إِنَّ الْفَضْلَ بِيَدِ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴾

73.Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu. Sema hakika uongozi hasa ni uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kuwa atapewa yeyote mfano wa mliyopewa nyinyi au wawahoji mbele ya Mola wenu. Sema hakika fadhila iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

﴿يَخْتَصُّ بِرَحْمَتِهِ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ﴾

74.Humhusisha husisha na rehema yake amtakaye.Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kubwa.

KUAMINI ASUBUHI NA KUKUFURU JIONI

Aya 72-74

MAANA

Kikundi katika watu wa Kitabu kilisema: Yaaminini yale waliyoteremshiwa wale walioamini, mwanzo wa mchana na yakataeni mwisho wake, huenda wakarudi nyuma.

Yaani warudi nyuma, Waislamu. Aya inaonesha hadaa na njama walizokuwa wakizifanya viongozi wa watu wa Kitabu. Wakidhihirisha uislamu Asubuhi na kurtadi jioni, ili angalau waweze kuzitia shaka baadhi ya nafsi dhaifu za waislamu, ziseme kuwa lau si kuwa wameona Muhammad si mkweli wasingelitoka katika uislamu baada ya kusilimu. Tafsir Al-Kashif: Juzuu ya Tatu 2. Sura Al-Imran Unaweza kuuliza; je, waliwahi kufanya hila zao hizi walizozipanga, au ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimpa habari Mtume wake na kuwafedhehesha kabla ya kuzitekeleza? Jibu: Inavyofahamisha Aya ni kwamba wao walisema. Ama kuwa walifanya baada ya kusema au hawakufanya; hayo yamenyamaziwa na Aya. Na, sisi vilevile tunayanyamazia yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo basi hakuna wajihi wowote wa waliyoyaeleza baadhi ya wafasiri kwamba wao waliswali Swala ya asubuhi pamoja na Mtume kisha wakarejea jioni na kuswali sala yao ili watu waone kuwa wao wameona upotevu, isipokuwa kama ni riwaya sahihi.

Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu.

Baadhi wameifahamu vibaya Aya hii na kuitolea ushahidi kuwa ni katika maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kwamba eti sio maneno ya mayahudi, bali hata nimemsikia mtu zaidi ya mmoja akisema Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikusudia kwa Aya hii kuwa tusimwamini yeyote isipokuwa aliye kwenye dini yetu. Ilivyo hasa ni kwamba Aya hii ni sehemu ya maneno ya wapinzani wenye vitimbi katika watu wa Kitabu. Mwenyezi Mungu ameyanukuu kwa kuwasimulia wao; yaani baadhi ya watu wa Kitabu waliwaambia wengine: "Silimuni mchana na mkufuru jioni." Vilevile wakasema:"Wala msimwamini ila yule anayefuata dini yenu."

Sema hakika uongozi hasa ni uongozi wa Mwenyezi Mungu.

Jumla hii imeingia kati, aliyoambiwa Mtume na Mwenyezi Mungu kabla ya kumalizika masimulizi. Makusudio yake ni kujibu jaribio la watu wa Kitab na hadaa yao ya kudhihirisha uislam, kisha kurtadi, ili kuzitia shaka baadhi ya nafsi dhaifu za wafuasi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Kwamba hadaa hii haina lolote. Kwa sababu uislam hauwezi kuondolewa au kuyumbishwa na vitimbi na hadaa. Mwenyezi Mungu anasema:

"Na ambaye ameongozwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumpoteza" (39:37)

Kuwa atapewa yeyote mfano wa mliyopewa nyinyi au wawahoji mbele ya Mola wenu.

Huu ndio mwisho wa masimulizi ya watu wa Kitabu hapa. Kwa ufupi ni kuwa viongozi wa watu wa Kitabu walikuwa wakiitakidi kwamba inawezekana Mwenyezi Mungu kumpeleka Mtume asiyekuwa mwisrail; na kwamba haukusimama kwao tu. Lakini baada ya kuja Muhammad(s.a.w.w) walidhihirisha hasadi na wivu, ati vitabu vyao na dini yao inawajibisha Mtume awe ni katika Bani Israil tu.

Walidhihirisha hayo wakiwa wanajua kuwa wao ni waongo tena wataaadhibiwa na kuhojiwa kesho mbele ya Mwenyezi Mungu, Wakaogopa haya yasiwafikie waislamu wasije wakapata nguvu. Kwa hiyo baadhi yao wakawaambia wengine: Tahadharini kusema mbele za waislam kwamba sisi watu wa Kitab tunaitakidi kuwa inawezekana kuletwa Mtume asiyekuwa mwisrail. Au kusema mbele ya waislam kuwa sisi tutahojiwa na kushindwa kesho kwa sababu ya kuficha kwetu haki na kuipinga. Kwa maneno mengine ni kwamba watu wa Kitabu hasa mayahudi walijua kabisa kuwa wao wako katika upotevu kwa sababu ya kumkadhibisha kwao Muhammad(s.a.w.w) na wakaogopa kuwafahamisha waislam hakika hii. Ndipo wakausiana kuficha upotevu wao na kuonyesha kuwa Mtume hawi na hatakuwa mwarabu.

Hii ndiyo tabia ya mayahudi tangu walipopatikana hadi leo na mpaka siku ya mwisho. Wanasema uongo huku wakijua kuwa wao ni waongo, wakijificha kwa kuleta mikanganyo, Lakini mara moja wanafedheheka. Wala Qur'an sio kitabu pekee kilichosajili makosa na uchafu wao, bali vitabu vyote vya kidini hasa Injil, vitabu vya historia, magazeti na idhaa; zote hizo zimekariri historia yao mbaya. Hii ndiyo siri ya kuwekewa vikwazo na kuteswa na uma mbali mbali; kuanzia Fira'un hadi Hitler. Hakuna taifa lolote duniani kuanzia zamani hadi sasa lililoungana nao isipokuwa Amerika tu, "Kwa sababu kufanana na kitu kunavutiana"

Sema hakika fadhila iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, Humpa amtakaye na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

Wafasiri wanasema makusudio ya fadhila hapa ni kuhusishwa utume; na kwamba kuko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humchagua kumpa utume yule anayefaa, awe mwisrail au mwarabu; na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu amekwishawajibu mayahudi waliotangaza kwamba Mungu hapeleki mtume isipokuwa kutokana na wao.

Haya ndiyo waliyoyasema wafasiri na wakatoa dalili kwamba mfumo wa Aya unafahamisha hilo. Kwa sababu uko katika mazungumzo ya watu wa Kitabu, madai yao ya uongo na hila zao.

Lakini tunavyoona sisi ni kuwa neno fadhila katika Aya linabaki katika ujumla wake; na kwamba linakusanya utume, hekima, uongofu, uislam na mengineyo. Linathibiti katika kujibu mayahudi; kama vile linavyothibiti kiujumla. Kwa sababu utume ni katika jumla ya mafungu ya fadhla.