1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE
﴿قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا تَعْمَلُونَ﴾
98.Sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnazikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na hali Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya muyatendayo!
﴿قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ تَبْغُونَهَا عِوَجًا وَأَنتُمْ شُهَدَاءُ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴾
99.Sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu walioamini ? Mkaitafutia kosa na nyinyi mnashuhudia. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na muyatendayo
KUKANUSHA DALILI NA ISHARA ZA MWENYEZI MUNGU
Aya 98 -99
MAANA
Qur'an imejishughulisha sana na watu wa Kitabu, ikawateremeshia Aya kadha wa kadha zinazowakumbusha Tawrat na Injil na kuwaaibisha, kwa sababu ya kuzigeuza; ikawajadili kwa namna nzuri na kuwaelezea makosa yao mengi na dhambi zao. Miongoni mwa Aya hizo, ni Aya hizi mbili:
Ya kwanza ni
: "Sema:Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnazikanusha ishara za Mwenyezi Mungu
ambazo zimefahamisha Utume wa Muhammad(s.a.w.w)
; na kwamba Al-Kaaba ndiyo nyumba ya kwanza kuwekewa watu kwa ibada, pamoja na kuwa ishara hizo na hoja hizo ziko wazi kama jua, na hawezi kuzikanusha isipokuwa mwenye kiburi"
Ya pili ni
"sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu walioamini Mkaitafutia kosa?."
Hawakutosheka na kufanya ufisadi hao wenyewe, mpaka wakajishughulisha kuwaharibu wengine na kuwapoteza. Kwa hiyo wamechanganya upotevu na kupoteza, na ufisadi na kuwafanya wengine wawe wafisadi. Kila mfisadi anatamani na kufanya kadiri ya uwezo wake ili kuwe na mafisadi wengi kwa kutumia misingi ya Iblis aliposema:
﴿قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴾
"Kwa kunihukumu kupotea, basi nitawapambia katika ardhi na nitawapoteza wote"
(15:39)
Tusisahau ishara ya aina hii ya upole wa kuwaambia watu wa Kitabu, na kuwakumbusha vizuri kuwa wao ni watu wa dini na Kitabu, ili angalau waweze kusikia mawaidha na kuongoka.
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تُطِيعُوا فَرِيقًا مِّنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ يَرُدُّوكُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ كَافِرِينَ﴾
100.Enyi mlioamini! Mtakapotii kikundi katika watu wa Kitabu watawarudisha kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.
﴿وَكَيْفَ تَكْفُرُونَ وَأَنتُمْ تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ آيَاتُ اللَّـهِ وَفِيكُمْ رَسُولُهُ وَمَن يَعْتَصِم بِاللَّـهِ فَقَدْ هُدِيَ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴾
101.Na vipi mnakufuru na nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume wake mnaye? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi ameongozwa katika njia iliyonyooka.
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴾
102.Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekuwa waislamu.
﴿وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ﴾
103.Na Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane; na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu; na mlikuwa ukingoni mwa shina la moto naye akawaokoa nalo. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyozibainisha Aya Zake ili mpate kuongoka.
KUWATII MAKAFIRI
Aya 100 - 103
MAANA
Enyi mlioamini! Mtakapotii kikundi katika watu wa Kitabu, watawarudisha kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.
Katika Aya mbili zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewahadharisha watu wa Kitabu kuipinga haki pamoja na kuwazuia waumini na njia Yake Mwenyezi Mungu. Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawahadharisha waumini wasiwasikilize makafiri katika watu wa Kitabu wanaojaribu kuwapoteza waumini na kuwafitini na dini yao. Imepokewa Riwaya kwamba, sababu za kushuka Aya hii ni kuwa baadhi ya mayahudi walikusudia kuirudisha tena fitna iliyokuwepo baina ya kabila la Ansar na Khazraj wasiwe na umoja baada ya Mwenyezi Mungu kuwaweka pamoja kwenye Uislamu. Kwa hiyo, makafiri wakawa wanawakumbusha uadui na mapigano waliyokuwa nayo wakati wa ujahiliya. Hasa siku ya vita ya Bughat ambayo Aus na Khazraj waliuana, na ushindi ukawa wa Aus. Mori ukawapanda wakawa karibu wapigane kama si kuwahi Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
. Aya inafungamana na tukio hili, kama ambavyo inafungamana na jaribio la wahubiri wa Kikristo wakati huu; na majaribio yote ambayo baadhi ya watu wa Kitabu na wengineo katika kutawanya umoja wa waislamu na kuwaepusha na dini yao, uzalendo wao, na uhuru wao na kuwa windo la kila mnyang'anyi.
Haya ndiyo wayafanyao wakoloni wa Kimagharibi kwa waarabu. Na kazi hiyo hawaifanyi peke yao, bali wanashirikiana na vibaraka duni ambao wanawatii na kuwafuata; na waliokufuru dini yao baada ya kuamini na kuiuza nchi yao. Kwa hivyo basi, Aya inafungamana na vibaraka hawa na pia inafungamana na wanaohubiri fitina na ufisadi na wakapendelea ukafiri na upotevu. Ni sawa wawe ni katika watu wa Kitabu au wengineo; wa Mashariki na Magharibi. Vile vile, Aya hii inafungamana na wanawake wetu wanavyoiga wanawake wa kimagharibi katika kujiremba na kujipodoa, na vijana wetu katika kudharau dini na mwendo wa dini. Vile vile desturi zote za madhara na haramu tulizoziiga kutoka kwa wageni. Aya kwa dhahiri inakataza kuwatii makafiri katika kufuru na kurtadi. Lakini, linalosababisha hilo linaenea katika kila uigaji unaomkasirisha Mwenyezi Mungu na Mtume.
Na vipi mnakufuru na nyinyi mnaosomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake mnaye?
Yaani, haitakikani kwa Mwislamu kuathirika na kuwa katika upotevu wa wapotezaji, na kuwafuata makafiri katika desturi zao na hulka zao wakati ambapo yeye mwislamu anasoma Qur'an Tukufu na kumsikiliza Mtume Mtukufu, anayembainishia haki na kumuondolea kila shubha. Anasema Nidhamuddin Al-Hasan Muhammad Annaisaburi katika Tafsir, Gharaibul- Qur'an: "Ama Kitabu kitabaki milele. Na Mtume(s.a.w.w)
ingawaje amekwenda kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, lakini nuru yake imebaki, Kwa sababu, kizazi na warithi wake wanakaimu nafasi yake. Kwa sababu hii ndipo Mtume akasema:"Mimi ninawaachia vizito viwili ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu"
Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu, basi ameongozwa katika njia iliyonyooka.
Kushikamana na Mwenyezi Mungu ni kushikamana na dini; dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni uislamu, nayo ndiyo hasa njia iliyonyooka. Makusudio ni kuwa mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu kwa haki kabisa, hawezi wala hataweza kuuwacha uislamu kwa namna yoyote ya majaribio na hadaa zitakavyokuwa.
Unaweza kuuliza
: Imekuja Aya isemayo:
"Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka"
(11:56)
Na wewe unafasiri kuwa njia iliyonyooka ni uislamu, Kwa hiyo itakuwa Mwenyezi Mungu yuko kwenye dini ya kiislamu.
Jibu
: Hakika njia iliyoonyooka ikinasibishwa kwa mja, inakusudiwa uislamu. Ama ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu inakusudiwa uadilifu na hekima; yaani yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu anapanga mambo kwa uadilifu na hekima Yake.
Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekuwa waislamu
Kila mwenye kufanya ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, basi ndio amemcha Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha. Haya ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
"Mcheni Mwenyezi Mungu muwezavyo"
(64:16)
Kwa sababu, lisilowezekana halikalifiwi na sharia, Na kila lisilowezekana kukalifiwa, basi liko nje ya kumcha Mwenyezi Mungu. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu "Msife isipokuwa mmekuwa waislamu;" ni kukataza kuacha uislamu na kuamrisha kuwa imara nao mpaka siku ya kifo.
Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane.
Kamba ni maarufu; na makusudio yake hapa ni uislamu. Maana ya Aya nzima, ni kuwa maadam waislamu ni wafuasi wa dini moja, Mtume mmoja na Kitabu kimoja, basi ni juu yao wote kuuchunga mfungamano huu wa kidini ambao ndio wenye nguvu zaidi kuliko mfungamano wa nasaba, na kuwa na hima nao; wala wasigawanyike vikundi.
Unaweza kuuliza
: Je, mwito huu wa muungano wa kidini si aina ya ubaguzi wa dini?
Jibu
: Hapana, mwito huu wa mshikamano wa wafuasi wa dini moja ni sawa na mwito wa mshikamano wa wanachama wa chama kimoja, au wa wafamilia moja, Mshikamano huu haulazimishi kuwabagua wengine. Bali ni kinyume na hivyo katika uislamuu, ambapo unatoa mwito wa kuwapenda na kuwahurumia watu wengine bila ya kuangalia dini zao, fikra zao au kabila zao. Kwa hivyo basi undugu wa Kiislamu ni nguzo ya udugu wa kibinadamu.
Kwa ujumla ni kwamba kundi ambalo ni wajibu kusaidiana nalo, ni lile lililojikusanya na kusaidiana katika jambo lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na masilahi ya watu. Ama kukutana kusikokuwa na faida yoyote ya kuridhisha hakutakikani. Imam Ali
anasema:"Utengano ni kwa watu wa batili hata wakiwa wengi, Na kuungana ni kwa watu wa haki hata wakiwa wachahe."
Na hiyo ndiyo tafsir ya Hadith mashuhuri:"Msaada wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na wengi."
Yaani kuwahusu wanaojumuika na kusaidiana kwa jambo la haki. Ama ikiwa ni kwa jambo la batili; basi hawatakuwa na yeyote zaidi ya shetani.
Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu.
Mwenyezi Mungu anawakumbusha waislamu wa kwanza vile walivyokuwa na misukusuko ya vita, bughudha na vita vya kuendelea, kama vile vita vya Aus na Khazraj vilivyodumu kwa muda wa miaka mia moja na ishirini, kama ilivyoelezwa kwenye Tafsir Tabari. Basi Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zao kwa baraka ya uislamu mpaka wakawa ni ndugu wanaohurumiana na kunasihiana. Jafar bin Abu Talib katika mazungumzo yake na Najjash alimwambia: "Tulikuwa watu wa ujahilia (ujinga) tukiabudu masanamu, tukila mizoga, tukifanya maovu, kuvunja undugu, kumfanyia uovu jirani na mwenye nguvu akimuonea mnyonge. Tulikuwa hivyo mpaka Mwenyezi Mungu akatuletea Mtume atokanaye na sisi; tunayemjua nasaba yake, ukweli wake, uaminifu na usafi wake.
Akatulingania kwa Mwenyezi Mungu ili tumwabudu yeye peke yake na tuachane na kuabudu wasiokuwa Yeye - mawe na masanamu. Akatuamrisha kusema kweli, kutekeleza amana, kuunga undugu, kumfanyia wema jirani na kujizuia na haki za watu na damu (zao). Akatukataza kufanya maovu, kusema uongo, uzushi, kula mali ya yatima na kuwavunjia heshima wanawake wanaojistahi. Akatuamrisha tumwabudu Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote. Pia akatuamrisha kuswali, kutoa Zaka na kufunga"
Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto naye akawaokoa nalo
Yaani mlikuwa karibu na moto wa Jahannam, kwa ukafiri wenu, Mwenyezi Mungu akawaokoa nao kwa baraka ya Muhammad(s.a.w.w)
.
﴿وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴾
104.Na liwepo miongoni mwenu kundi lenye kulingania kwenye heri, na kuamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio wenye kufaulu
KUAMRISHA MEMA
Aya 104
Makusuido ya heri hapa ni uislamu, na mema ni kumtii Mwenyezi Mungu, na maovu ni kumwasi. Maana yanayopatikana ni kwamba hapana budi kupatikane kundi la watu litakalowalingania wasiokuwa waislamu kwenye uislamu; kwenye lile linalomridhisha Mwenyezi Mungu, analolilipa thawabu na kuacha lile linalomkasirisha analoliletea adhabu. Tamko kutokana na nyinyi katika Aya hii inafahamisha wajibu wa kuamrisha mema kwa njia ya kutosheana (kifaya). Yaani, wakilisimamia hilo baadhi, utakuwa wajibu umewaondokea wengine, Wala si lazima kuwa mwenye kutekeleza umuhimu huu, awe mwadilifu. Hapana, si hivyo, kwa sababu mbili:
Kwanza
: kwamba sharti ya hukumu ni sawa na hukumu yenyewe, haithibiti ila kwa dalili wala hakuna dalili ya sharti ya uadilifu hapa; si kutoka katika Qur'an, Hadith au kutoka katika akili.
Pili
: hukumu ya kuamrisha mema haitegemei maasi au utiifu wa mwengine katika hukumu. Mafakihi wengi wameshartisha wajibu wa kuamrisha mema kuwa mwenye kuamrisha awe atakuwa salama, kiasi ambacho hatapata madhara yoyote kwa kuamrisha mema na kukataza maovu. Lakini sharti hili haliingi sehemu zote, kwani, kupigana na anayetupiga kwa ajili ya dini yetu na nchi yetu ni wajibu, ingawaje tunafahamu kwamba, kwa kawaida kupigana huleta madhara.
Inafaa kwa kila mtu kuyatoa mhanga maisha yake, akiwa na yakini kwamba kujitoa mhanga huku kuna maslahi ya umma. Faida ya watu na nchi ni muhimu na adhimu zaidi kuliko maisha yake, bali hilo linashukuriwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa watu. Kuna Hadith isemayo:"Jihadi bora zaidi ni tamko la haki mbele za Sultan dhalimu."
Kwa ufupi ni wajibu kukinga madhara yakiwa hayatakuwa na faida yoyote. Vyenginevyo, itajuzu kuyavumilia; kama inavyojuzu kwa mtu kukata kiungo kibovu katika viungo vyake kwa kupigania uhai wake na kuhofia kumalizika. Zaidi ya hayo, mifumo inaathari zake, Baadhi ya mifumo inaifukuza haki na kumsababishia mtu matatizo. Na mingine inalazimisha fikra kwa msikilizaji bila ya kujitambua. Mwenye akili na hekima anafanya kulingana na hali ilivyo ya taratibu au ya nguvu.
Firaun alikuwa na ukomo wa Usultani na kupetuka mipaka; Musa na Harun hawakuwa hata na msaidizi, lakini pamoja na hayo waliamrishwa kumlingania kwenye haki. Lakini kwa njia ya upole. Hata Muumba wa ulimwengu, (ambaye limetukuka neno lake) mara nyingine amewaambia waja wake kwa vitisho na kusema:
"Hakika nyinyi hamtanusuriwa nasi"
(23:65) Mara nyingine hutumia upole na kusema:
﴿أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾
"Je, hampendi Mwenyezi Mungu awasamehe na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu."
(24:22)
Kwa ujumla kutangaza mwito wa uislamu kwa watu, na waislamu kuamrishana mema na kukatazana mabaya, ni katika nguzo za uislamu. Kwa hiyo kunawajibisha kuwapo kwa kikundi kitakachosimamia umuhimu huu, sawa na kulazimika kuwapo uongozi utakaosimamia amani na nidhamu, wafanya kazi wa viwandani, wakulima na wengineo ambao wanachangia maisha.
Huu ni msingi wa kila dini, kila dhehebu na kila fikra. Kwa sababu, hiyo ndiyo njia nzuri ya kueneza mwito, kupata ushindi na kuwazuia maadui. Angalia jinsi watu wa siasa na uchumi wanavyotilia umuhimu vyombo vya habari, kuvikuza na kuvitolea mamilioni ya mapesa na kufanya mizinga na habari kuwa bega kwa bega. Hawakufanya hivyo ila ni kwamba wametambua, kutokana na uzowefu wao, kwamba habari ni silaha yenye nguvu kuliko mizinga na mabomu. Mmoja wa wakuu wa mapatano alisema baada ya kufaulu kwao katika vita vya ulimwengu: "Tumeshinda katika vita kwa mabomu ya karatasi." Yaani magazeti.
Unaweza kuuliza
: kwamba unawezaje kuziunganisha Aya hizi mbili: "Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kwenye heri na wanaoamrisha mema na kukataza maovu." Na Aya isemayo:
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ﴾
"Enyi mlioamini! Jiangalieni nafsi zenu hatawadhuru aliyepotea ikiwa mmeongoka"
(5:105)
Ambapo ya kwanza imefahamisha wajibu wa kuamrisha mema na ya pili imefahamisha kutokuwepo wajibu huo kutokana na neno "Jiangalieni nafsi zenu."
Jibu
: Makusudio ya Aya ya pili, ni kwamba mwenye kutekeleza wajibu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya, hatadhuriwa na upotevu wa aliyepotea wala upinzani wa mpinzani, maadamu yeye anaetekeleza wajibu wake tu,
"Hakika ni juu yako kufikisha tu, na juu yetu ni kuhisabu"
(13:40)
Swali la pili
: kuna Hadith mashuhuri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
isemayo: "Mwenye kuona katika nyinyi uovu, na auondoe kwa mkono wake, akishindwa, basi (auondoa) kwa ulimi wake, akishindwa basi ni kwa moyo wake na hilo ni katika udhaifu zaidi wa imani." Mpangilio huu unapingana na ilivyo desturi ya sharia, kiakili na kimazoweya; kwamba kuondoa uovu kunaanzia kwa ulimi halafu ndio vita. Sasa kuna wajihi gani wa kauli hii ya Mtume?
Jibu
: Kuna tofauti kubwa sana baina ya kuondoa uovu na kukataza uovu, kwani kukataza uovu aghlabu ni kabla ya kutokea uovu wenyewe; ni kama vile kukinga, kama kuona kuwa mtu fulani anafikiria kuiba, ukamkataza kufanya wizi huo, Ama kuondoa uovu, kunakuwa baada ya kutokea uovu wenyewe. Kwa mfano umejua kuwa mtu fulani ameiba mfuko wa mtu mwengine, hapo ukiwa unaweza kumnyang'anya na kumrudushia mwenyewe, basi ni wajibu kwako kulifanya hilo wewe mwenyewe, ikiwa kuna uwezekano wa kumyang'anya mwizi; na wewe usiweze kupata madhara. Kama hukuweza ni wajibu kwako kumwamrisha mwizi aurudishe kwa mwenyewe na kumkataza kuuzuwia. Kama utashindwa na vishindo vya mwizi, basi usikiridhie kitendo chake - baina yako na Mola wako. Kwa hivyo maudhui ya Hadith ni kugeuza uovu, si kukataza uovu
.