3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE
﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَن تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾
116.Hakika wale ambao wamekufuru, haitafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyezi Mungu, na wao ndio watu wa motoni, wao humo watadumu.
﴿مَثَلُ مَا يُنفِقُونَ فِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَثَلِ رِيحٍ فِيهَا صِرٌّ أَصَابَتْ حَرْثَ قَوْمٍ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ فَأَهْلَكَتْهُ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِنْ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ﴾
117.Mfano wa wanavyovitoa katika maisha haya ya dunia ni kama mfano wa upepo wenye baridi kali uliofikilia shamba la watu waliodhulumu nafsi zao, ukaliangamiza, Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wanajidhulumu wenyewe.
UKAFIRI HAUFAI KITU
Aya 116 - 117
MAANA
Hakika wale ambao wamekufuru, haitafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyezi Mungu.
Amesema Razi na mwenye Tafsir Al-Manar: "Wametofautiana wafasiri katika makusudio ya ambao wamekufuru. Kundi moja likasema kuwa ni baadhi ya makafiri. Wengine wakasema ni makafiri wote. Ama tuonavyo sisi ni kwamba, makusudio ni kila mwenye kukhalifu haki na kuipinga kwa masilahi yake na ya watoto wake, na kuhofia mali yake na utajiri - vyovyote atakavyokuwa, Mwislamu au kafiri. Ni kweli kuwa tamko la Aya linawahusu makafiri lakini sababu inayowajibisha ambayo ni kutofaa kitu, inaenea kwa wote wanoikhalifu haki kwa msukumo wa hawaa zao; nao ndio wale aliowataja Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya kadhaa kuwa wameiuza haki kwa thamani duni.
Mfano wa wanavyovitoa katika maisha haya ya dunia, ni kama mfano wa upepo wenye baridi kali uliofikilia shamba la watu waliodhulumu nafsi zao, ukaliangamiza.
Yaani wale ambao wanachanganya utajiri wa halali na haramu na kuihalifu haki kwa ajili ya utajiri na kuutumia kwa ajili ya jaha, na starehe zao bila ya kujali dini au maadili, hakika matumizi ya hawa yameangamiza akili zao na kuharibu maadili yao, sawa na upepo wenye baridi kali unavyoangamiza shamba lililotayarishwa kuwa na mazao. Kama watapata faida siku chache kwa kustarehe na kutosheleza uchu wao, basi watakuwa wamejipatia hasara na kuziuza nafsi zao kwa shetani; na wao watapata adhabu ya milele huko akhera.
Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wanajidhulumu wenyewe, kwa sababu wamejiiingiza kwenye matamanio wao wenyewe kwa hiyari yao.
Imam Ali
anasema:"Watu duniani ni aina mbili: Mtu aliyeiuza nafsi yake ikamwangamiza (yaani ameiuza nafsi yake kwenye matamanio na hawaa zake), na mtu aliyeinunua nafsi yake akaiacha huru. (Yaani aliyeinunua nafsi yake na kuisafisha na matamanio)
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا بِطَانَةً مِّن دُونِكُمْ لَا يَأْلُونَكُمْ خَبَالًا وَدُّوا مَا عَنِتُّمْ قَدْ بَدَتِ الْبَغْضَاءُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ وَمَا تُخْفِي صُدُورُهُمْ أَكْبَرُ قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ الْآيَاتِ إِن كُنتُمْ تَعْقِلُونَ﴾
118.Enyi ambao mmeamini Msiwafanye wasiri wasiokuwa katika nyinyi, Hawazembei kuwaharibia, Wanapendelea yanayowapa mashaka. Imedhihiri chuki katika vinywa vyao, na wayafichayo vifuani mwao ni makubwa. Tumewabainishia ishara ikiwa nyinyi ni wenye akili.
﴿هَا أَنتُمْ أُولَاءِ تُحِبُّونَهُمْ وَلَا يُحِبُّونَكُمْ وَتُؤْمِنُونَ بِالْكِتَابِ كُلِّهِ وَإِذَا لَقُوكُمْ قَالُوا آمَنَّا وَإِذَا خَلَوْا عَضُّوا عَلَيْكُمُ الْأَنَامِلَ مِنَ الْغَيْظِ قُلْ مُوتُوا بِغَيْظِكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴾
119.Hivyo basi! Nyinyi ndio hao muwapendao hali wao hawawapendi, nanyi mwaviamini vitabu vyote, Na wakikutana nanyi husema: Tumeamini, na wanapokuwa faraghani huwaumia vidole kwa hasira. Sema: Kufeni na hasira zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyo vifuani.
﴿إِن تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ﴾
120.Ukiwagusa wema unawasononesha, na kama likiwapata baya wanalifurahia. Na kama mkisubiri na mkaogopa, basi hila zao hazitawadhuru kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka wayatendayo.
WASIRI WAOVU
Aya 118 - 120
MAANA
Katika Aya zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezungumzia kuhusu watu wa Kitabu, washirikina na wenye kurtadi ambao walikufuru baada ya kuamini kwao. Wote hao amewapa kiaga na akawapa hoja, kisha akaamrisha waislamu wamche Mwenyezi Mungu, washikamane na kamba yake na waamrishe mema. Baada ya yote hayo, sasa anawahadharisha waislamu wajiepushe na makafiri - ambao wanawadhamiria uovu waislamu na kuwatakia maangamizi - kwa kusema:
Enyi ambao mmeamini! Msiwafanye wasiri wasiokuwa katika nyinyi,
Hili kwa dhahiri ni katazo kwa waislamu kwa kila asiyekuwa katika dini yao bila ya kumvua yeyote. Hapo basi litakuja Swali hili: Ni maarufu kuwa viongozi wa dini katika mataifa yote wanaeneza kwa wafuasi wao roho ya uadui na ubaguzi, dhidi ya dini nyingine. Na hii Qur'an nayo inakwenda njia hiyo hiyo, ambapo inawaamrisha waumini kujitenga na wengine na kutoa tahadhari ya kuwafanya marafiki, Sasa kuko wapi kuvumiliana katika Uislamu? Je, kuna tofauti gani baina ya waislamu na mayahudi walioambiana: "Wala msimwamini ila mwenye kufuata dini yenu?"3:73
Jibu
: Aya haikuwatahadharisha Waislamu kujiepusha na wasiokuwa wao kwa kuwa si wafuasi; isipokuwa imewahadharisha na wale wanaowafanyia vitimbi. Hayo ndiyo maana wazi ya kauli yake Mwenyezi Mungu:Hawazembei kuwaharibia
; yaani wanajitahidi bila ya kufanya uzembe katika kuwadhuru na kuharibu mambo yenu. Na katika kauli yake: Wanapendelea yanayowapa mashaka. Pia kauli yake Mwenyezi Mungu:Imedhihiri,
Yaani kuitia ila dini yenu, Mtume wenu na Qur'an yenu.Na wayafichayo vifuani mwao ni makubwa kuliko yale yamiminikayo kwenye ndimi zao.
Vile vile miongoni mwa sifa za wale aliowahadharisha Mwenyezi Mungu ni: wanapokuwa faragha huwaumia vidole kwa hasira.
Na ukiwagusa wema unawasononesha na kama likiwapata baya wanalifurahia.
Sifa zote hizi, ndio sababu ziwajibishayo kuwakataza kuwafanya wasiri wenu, Kwa hiyo basi, kila mwenye sifa hizi ni wajibu kujitenga naye wala haijuzu kumfanya msiri; ni sawa awe ni mwislamu au si mwislamu. Hivi sasa tuko katika mwaka 1967, Mnamo tarehe 5 Juni mwaka huu, ukoloni umeileta Israel kufanya uadui katika ardhi za Waarabu baada ya kufagiliwa njia na makombamwiko waovu wanaonasibika na dini ya waislamu na kabila ya Waarabu. Na waovu hawa mbele ya Mwenyezi Mungu wana hatia kubwa kuliko walahidi na washirikina ambao hawawaudhi wengine.
Kwa hiyo suala hapa ni la ushari na hiyana, sio suala la ukafiri na kukosa imani.
Unaweza kuuliza
: Ingawa mambo ni hivyo, kwa nini Mwenyezi Mungu amesema, 'wasiokuwa katika nyinyi,' badala ya kusema katika wahaini walio wafisadi?
Jibu
: Aya ilishuka kwa sababu ya baadhi ya waislamu waliokuwa wakiungana na mayahudi kama walivyosema wafasiri. Kimsingi cha kuzingatia ni sababu iliyowajibisha sharia ya hukumu; sio sababu ya kushuka kwake. Kwa maneno mengine, ni kwamba hukumu itafuata dhahiri ya tamko, ikiwa hatujui sababu ya kushuka kwake. Ama tukiwa na yakini ya sababu yake basi hukumu itafuatia sababu, sio dhahiri ya tamko.
Tumewabainishia ishara ikiwa nyinyi ni wenye akili.
Makusudio ya neno ishara ni alama zinazo pambanua baina ya anayefaa kufanywa msiri, na habithi ambaye ni wajibu kujitenga naye.
Hivyo basi! Nyinyi ndio hao muwapendao hali wao hawawapendi,
Dhahiri ya msemo ni kuwa unaelekezwa kwa kikundi kinachojinasibisha na uislam, wala hauswihi kuelekezwa kwa waislamu wote, si katika wakati wa mwanzo wala mwengineo, Kwani haikutokea hata siku moja kwamba waislamu waafikiane kuwapenda makafiri. Sheikh wa wafasiri Tabari amesema na akafuatwa na wengi, kwamba waislamu kuwapenda wanaowachukia katika makafiri ni dalili kwamba uislam ni dini ya upendo na kuvumiliana. Huku ni kusahau kwa Tabari na akafuatwa na wengi, kwamba uislamu kabisa hauvumilii ufisadi na uhaini. Tuonavyo sisi ni kwamba suala sio la kuvumiliana, isipokuwa ni suala la hiyana na unafiki kutoka kwa baadhi ya wanaojinasibisha na uislamu, na wakati huo huo wakifanya ujasusi kwa waislamu kwa ajili ya maadui wa nchi na dini. Kama wafanyavyo leo vibaraka wa ukoloni wanaojulikana kwa jina la kikosi cha tano
askari wa kukodiwa n.k. Kwa sababu, wanauza dini yao na nchi yao kwa kila anayewapa pesa tu.
Nanyi mwaviamini vitabu vyote
, Herufi Alif na lam hapa ni ya jinsi; yaani mwamini kila kitabu kilichoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni sawa kiwe kimeteremshwa kwao au la. Nyinyi si kama wao wanaamini baadhi na kukanusha baadhi nyingine.
Na wakikutana nanyi husema tumeamini kwa ria na unafiki.
Haifai kwa mumin kufanya urafiki na mnafiki na mwenye ria (kujionyesha).
Na wanapokuwa faraghani huwaumia vidole kwa hasira.
Kuwaumia vidole ni fumbo la chuki zao na ukorofi wao kwenu. Hakuna kitu kinachomkasirisha adui kuliko fadhila na hulka njema, vile vile umoja na kupatana kwa undugu. Tangu zamani hadi sasa adui anajaribu kuwatawanya waislamu na umoja wao.
Sema: Kufeni na hasira zenu
.
Huu ni msemo wa kiarabu kwa mtu wanayamuombea abaki hivyo: Kama kusema; 'Kufa na ugonjwa wako' Yaani Mwenyezi Mungu akubakishe na ugonjwa wako. Kimsingi ni kwamba maneno haya huambiwa adui akiwa msemaji ana nguvu. Na hakuna nguvu kama umoja na kuungana.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyo vifuani
kila yanayompitia mtu na anayowazia moyoni mwake katika misukumo ya kheri na shari. Yaani Mwenyezi Mungu anajua chuki na ukorofi wao.
Ukiwagusa wema unawasononesha na kama likiwapata baya wanalifurahia.
Hiyo ni kawaida ya kila adui. Wafasiri wanasema, kumetajwa kugusa katika wema kwa kutambulisha kuwa kheri ndogo tu aipatayo Mwislamu, humsononesha adui. Na kumetajwa kupata katika uovu, kufahamisha kuwa kukiwa na baya kwa waislamu, basi maadui huzidi furaha. Huu ni ufasaha wa kuelezea uadui ulivyo mkubwa.Na mkisubiri
kwa twaa ya Mwenyezi Mungu na maudhi ya adui zakena mkaogopa
yaliyoharamishwa, na maasi,basi hila zao hazitawadhuru kitu.
Anayekuwa na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu huwa naye, na anayemcha Mwenyezi Mungu humpatia njia.
﴿وَإِذْ غَدَوْتَ مِنْ أَهْلِكَ تُبَوِّئُ الْمُؤْمِنِينَ مَقَاعِدَ لِلْقِتَالِ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴾
121.Na uliporauka asubuhi kutoka kwa ahli zako kwenda kuwaandalia waumini mahali pa kupigana. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia, mjuzi
VITA VYA UHUD
Aya 121
Aya hii na nyingine kadhaa zinazofuatia zilishuka kuhusu tukio la vita vya Uhud ambalo kwa ufupi ni kama ifuatavyo: Uhud ni jina la mlima ulioko Madina. Vita vya Uhud vilikuwa mnamo mwezi wa Shawwal (Mfungo mosi) mwaka wa tatu wa Hijra. Baada ya kuuawa magwiji wa Kikuraish katika vita vya Badr, Abu Sufian alipata nafasi na akawa ndiye Rais wa Makuraish. Akawa anampangia njama Mtume(s.a.w.w)
pamoja na washirikina, akaweza kukusanya jeshi la wapiganaji elfu tatu. Akaenda nalo hadi karibu na mlima Uhud. Na alikuwa yuko pamoja na mkewe Hind bint Utba (mamie Muawiya). Mtume(s.a.w.w)
naye akatoka na wapiganaji elfu moja, lakini Abdallah bin Ubayya, kiongozi wa wanafiki alitaka kuwavunja nguvu watu kwa kujitoa, wakamwitikia watu mia tatu; Mtume akabaki na mia saba. Abdallah bin Amr (baba wa Jabir Alansari) alijaribu kumzuia bin ubayya na azma yake hiyo, lakini hakufaulu. Na koo mbili za Ansari zikajaribu kumfuata bin Ubayya, lakini Mwenyezi Mungu akawahifadhi na wakathibiti pamoja na Mtume(s.a.w.w)
. Wao walikuwa Bani Salama katika Khazraj na Bani Haritha katika Aus.
Mtume(s.a.w.w)
akapanga mbinu ya mapigano, Akaweka wapiga mishale hamsini kwenye mlima nyuma ya jeshi la waislamu waliokuwa wakiongozwa na Abdallah bin Jubair, akawaambia, "nyinyi mtatuhami kwa upande wa nyuma, wala msiondoke hapo mlipo tukishinda au tukishindwa." Vita vilipochacha, Hind akawaongoza wanawake kupiga ngoma nyuma ya wanaume ili kuwachochea huku akiimba: Mkikabili tutawakumbatia na mazulia kuwatandikia, Na mkigeuka tutawakimbia mapenzi hatutawapatia Mtume(s.a.w.w)
alipomsikia akasema: Ewe Mwenyezi Mungu kwako nategemea na kwa ajili yako ninapigana. Tosha yangu ni Mwenyezi Mungu na bora ya mwenye kutegemewa ni Yeye Bendera ya Makuraish ilibebwa na Twalha bin Abu Twalha Al-Abdi kutoka ukoo wa Abdu Ddar, Imam Ali akamuua, bendera ikachukuliwa na Said bin Abu Twalha, akauawa na bendera ikaanguka, akaichukua Musafi bin Abu Twalha naye akauawa na Imam, mpaka wakauawa watu tisa katika ukoo wa Abdu Ddar. Wakavunjiliwa mbali washirikina na kushindwa, Waislamu wakawa wanaokota ngawira.
Wapiga mishale walipoona kushindwa kwa washirikina na ndugu zao waislamu wanakusanya ngawira, waliondoka pale walipowekwa na Mtume(s.a.w.w)
. Kiongozi wao Abdallah bin Jubair akawaambia: "Bakini sehemu zenu, mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Lakini walikataa na wakaenda kunyakua ngawira. Jubair akabaki na watu kumi tu. Khalid bin Al-Walid kuona hivyo aliwafuatia na kikosi cha washirikina. Wakawamaliza baada ya kupigana nao kiume, Makuraish walipoona alivyofanya Khalid waliwazingira Waislamu na kuwashambulia mpaka wakamfikia Mtume(s.a.w.w)
. Akapigwa jiwe na washirikina likamjeruhi jicho, uso wake ukarowa damu, akajeruhiwa mdomoni na vishikio viwili vya kofia ya chuma vikamwingia usoni, Hapo waislamu wakaanza kukimbia baada ya mtu mmoja kupiga kelele kuwa Muhammad ameuawa. Hakuna aliyebakia isipokuwa watu wachache wakiongozwa na Ali bin Abu Talib, Abu Dujana na Suheli bin Hanif wakipigana kiume kumkinga Mtume.
Hind akumuhadaa Wahshi amuue Muhammad au Ali au Hamza, Akamuua Hamza kwa mkuki wake. Hind akalipasua tumbo la Hamza akamtoa ini lake akalila, Tangu siku hiyo alibandikwa jina la 'Mla maini' Katika vita hivyo waliuawa washirikina 22 na Waislamu 70 walikufa shahid.
MAANA
Na uliporauka kutoka kwa ahli zako kwenda kuwaandalia waumini mahali pa kupigana.
Yaani, kumbuka ewe Mtume uliporauka kutoka nyumbani kwako kwenda kupanga sehemu watakayokaa wapiga mishale, wapanda farasi na waumini wengine uliokuwa nao.
﴿إِذْ هَمَّت طَّائِفَتَانِ مِنكُمْ أَن تَفْشَلَا وَاللَّـهُ وَلِيُّهُمَا وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴾
122.(Kumbuka) makundi mawili miongoni mwenu yalipodhamiria kufanya woga na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwanusuru, na kwa Mwenyezi Mungu na wategemee waumini.
MAKUNDI MAWILI
Aya 122
MAANA
Makundi mawili ni Bani Salama kutoka kabila la Khazraj na Bani Haritha kutoka Aus. Walikurubia kuathirika na harakati za Abdallah bin Ubayya, lau si kuwahiwa na nusura ya Mwenyezi Mungu. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwanusuru, Ni dalili ya mkato kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) huwapa tawfiki yake baadhi ya watu kinyume cha watu wengine. Kwa sababu Yeye hakuyaacha makundi hayo mawili yaogope na kukimbia. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa anapopasaidia, kama ambavyo ni Mjuzi zaidi anapoweka utume Wake.
﴿ وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ فَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾
123.Hakika Mwenyezi Mungu aliwanusuru katika vita vya Badr hali nyinyi ni madhalili. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.
﴿إِذْ تَقُولُ لِلْمُؤْمِنِينَ أَلَن يَكْفِيَكُمْ أَن يُمِدَّكُمْ رَبُّكُم بِثَلَاثَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُنزَلِينَ﴾
124.Ulipowaambia waumini: Je, haiwatoshi Mola wenu kuwasaidia kwa malaika elfu tatu wenye kuteremshwa.
﴿ بَلَىٰ إِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُم مِّن فَوْرِهِمْ هَـٰذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُم بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ ﴾
125. Ndio! Kama mkisubiri na mkamcha Mungu na wakawajilia katika wakati wao huu, atawasaidia Mola wenu na malaika elfu tano walio na alama.
﴿وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ لَكُمْ وَلِتَطْمَئِنَّ قُلُوبُكُم بِهِ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴾
126.Na Mwenyezi Mungu hakuyajaalia ila ni bishara kwenu ili mioyo yenu ipate kutulia. Na hapana nusra ila itokayo kwa M/Mungu Mtukufu, Mwenye hekima
﴿لِيَقْطَعَ طَرَفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَوْ يَكْبِتَهُمْ فَيَنقَلِبُوا خَائِبِينَ﴾
127.Ili apate kuliangamiza kundi katika waliokufuru au awadhalilishe, warejee hali ya kuwa ni wenye kuambulia patupu.
VITA VYA BADR
Aya 123 – 127
Mwenyezi Mungu katika Aya hizi, anawakumbusha waislamu vita vya Badr ambavyo vilimalizika kwa ushindi wa Waislamu. Badr ni kisima kilichoko baina ya Makka na Madina. Kilikuwa ni cha mtu aitwaye Badr, ndio kikaitwa jina lake. Msafara wa kibiashara wa Makuraish ulikuwa ukipitia hapo. Waislamu wakaamua kuukatiza msafara kwa kuushambulia. Msafara huo uliongozwa na Abu Sufyan, wakatoka wapiganaji washirikina kiasi cha elfu moja, wakiwa wamejiandaa tayari kuuhami msafara huu. Hapo vita vikaumana na waislamu walikuwa 313. Waislamu walipata ushindi mkubwa sana katika vita hivi na hasara kubwa kwa washirikina, vita hivi vilisikika Uarabuni kote. Tutarudia maelezo ya vita vya Badr Inshaallah tutakapofasiri Sura Anfal (8:7)
MAANA
Hakika Mwenyezi Mungu aliwanusuru katika Badr hali nyinyi ni madhalili. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.
Hii ni kuwakumbusha waislamu siku ya Badr kwa ajili ya taqwa ya nyoyo zao, wakati huo walikuwa wachache tena bila ya maandalizi ya nguvu. Ambapo idadi ya waislamu ilikuwa ni watu 313, wakiwa na farasi mmoja tu, washirikina walikuwa elfu moja na farasi mia moja, hata hivyo washirikina 70 waliuwawa na kutekwa 70. Waliobaki wakashindwa, Kusudio la kukumbushwa kwao haya ni kuwabainishia kwamba ushindi katika vita hauhisabiwi kuwa ndio ushindi wa mwisho, wala kushindwa katika vita hakuhisabiwi kuwa ndiko kushindwa kabisa, isipokuwa ushindi wa mwisho ni wa wenye uthabiti na wanaomcha Mwenyezi Mungu, wenye ikhlasi. Yamefahamisha uhakika wa hilo, matukio na vita vya zamani na vya sasa; hasa vita vya pili vya dunia ambavyo vilianza mwaka 1939 na kumalizika 1945.
Ulipowaambia waumini
hii ni kauli kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
siku ya Badr:
Je, haiwatoshi Mola wenu kuwasaidia kwa malaika elfu tatu wenye kuteremshwa.
Yaani wenye kuteremshwa kutoka mbinguni,
Ndiyo! Kama mkisubiri na kumcha Mwenyezi Mungu, na wakawajilia katika wakati wao huu, atawasaidia Mola wenu na Malaika elfu tano walio na alama.
Dhamiri ya wakawajilia inarudia washirikina, Yaani wakiwajia tena hao washirikina, Mwenyezi Mungu atawaletea malaika,
Neno Musawimina linatokana na Simau (alama), Yaani wana alama inayofahamisha.
Hakika kauli hii ya Mwenyezi Mungu imefahamisha ufahamisho usiokubali Taawili yoyote kwamba Mwenyezi Mungu, uliotukuka uwezo wake, aliwasaidia waislamu kwa Malaika katika baadhi ya vita vyao. Hadith nyingi zimefahamisha hilo. Wameafikiana waislamu kwamba Mwenyezi Mungu aliwateremsha Malaika siku ya Badr kuwanusuru waumini, wakatofautiana kuhusu kuteremshwa kwao siku ya Uhud, Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwateremsha Malaika siku ya Badr kwa ajili ya kuwasaidia waumini, lakini hatujui kama ulikuwa ni msaada wa kuonekana kama vile kupigana, au ni msaada usionekana kama vile kuwahofisha washirikina, na kuwapa utulivu waumini. Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wala hatuna wajibu wowote wa kufanya utafiti na kulichunguza hilo, kwamba hata tukifanya utafiti hatuwezi kufikia kwenye yakini. Hata hivyo ziko dalili zifahamishazo kwamba malaika huwa na sura za kibinadamu. Baadhi ya dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:
(i) Aliyoyaelezea Mwenyezi Mungu kuhusu ugeni wa Ibrahim
;
﴿وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ ﴿٥١﴾ قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴾
"Na wape habari kuhusu wageni wa Ibrahim, Hakika sisi tumetumwa kwa watu wenye makosa."
(15:51 & 58)
(ii) Wageni wa Lut walioelezwa katika Sura 11:77
(iii) Kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:
﴿فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا﴾
"Akajifananisha kwake kwa (Sura ya) binadamu aliye kamili"
(19:17)
(iv) Jibril alikuwa akimjia Mtume kwa Sura ya binadamu. Lakini malaika kuwa na sura ya binadamu hakulazimishi kwamba wao walipigana kwa ajili ya Waislamu, bali inawezekana kuwasaidia kwa njia nyengine isiyokuwa kupigana.
Unaweza kuuliza
: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema:
﴿لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ﴾
"Kwa hakika mimi nitawasaidia kwa malaika elfu moja watakaofuatana mfululizo"
(8:9)
Kisha katika Aya hizi tunazozifasiri, ametaja elfu tatu; Aya inayofuatia hiyo akataja elfu tano moja kwa moja. Je, Mwenyezi Mungu aliwasaidia kwa elfu moja kwanza kisha elfu tatu, baadae tano na hivyo kuwa tisa?Miongoni mwa yaliyojibiwa ni kwamba:
Mwenyezi Mungu aliwasaidia kwanza kwa elfu moja, kisha akaongeza elfu mbili, wakawa elfu tatu; tena akaongeza elfu mbili ikawa kwa ujumla ni elfu tano.
Mwengine amesema: Mwenyezi Mungu aliwasaidia waislamu siku ya Badr kwa malaika elfu moja. Kisha waislamu wakapata habari kwamba baadhi ya washirikina wanataka kuwasaidia Makuraish kwa idadi kubwa ya wapiganaji. Waislamu wakawa na hofu, na kuona taabu kwa sababu ya uchache wao, Ndipo Mwenyezi Mungu akawaahidi malaika elfu tano, ikiwa msaada utawajia Makuraish. Lakini kama ilivyosema Aya:"kama mkisubiri na mkamcha mungu na wakawajia katika wakati wao huu"
lakini msaada haukuwajia Makuraish. Kwa hiyo wakatosheka Waislamu na msaada wa elfu moja tu.
Na Mwenyezi Mungu hakuyajaalia ila ni bishara kwenu na ili mioyo yenu ipate kutulia.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasaidia kwa malaika au aliwaahidi msaada, ili nyoyo zenu zipate utulivu kutokana na wingi wa idadi ya adui zenu na wala msikate tamaa kwa uchache wa idadi yenu.
Ili apate kuliangamiza kundi katika wale waliokufuru au awadhalilishe, warejee hali ya kuwa ni wenye kuambulia patupu.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwasaidia kwa malaika kuua na kuteka nyara, au awafedheheshe kwa kushindwa na waambulie patupu bila ya kuwa na tumaini la ushindi.
﴿لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذِّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ ﴾
128.Huna lako jambo, au awatakabalie toba yao au awaadhibu, kwa sababu wao ni madhalimu.
﴿وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾
129.Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Humsamehe amtakaye na humwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mwenye kurehemu.
HUNA LAKO JAMBO
Aya 128 – 129
MAANA
Huna lako jambo
Huenda waislamu kwa sababu ya kumtukuza Mtume wa Mwenyezi Mungu, wakadhani kwamba ametia mkono katika yaliyotokea Badr au wangeshindwa. Ndipo Mwenyezi Mungu akayaondoa mawazo haya kwamba mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu peke Yake. Hakika Qur'an imesisitiza sana katika Aya kadhaa kwamba Muhammad(s.a.w.w)
ni mtoa bishara na muonyaji tu; ni mfikishaji wa hukmu za Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Sio mbali kuwa hekima ya kukaririka huku na kutilia mkazo ni kwamba waislamu wasiingie ndani sana kuhusu Mtume wao kama walivyofanya wakristo kumhusu Bwana Masih
.
Au awatakabalie toba yao au awaadhibu, kwa sababu wao ni madhalimu.
Kauli hii inaungana na ile iliyosema au awadhalishe, yaani amri yote ni ya Mwenyezi Mungu; ama awatakabalie toba watakaposilimu au awaadhibu waking'ang'ania ukafiri, kwa sababu wao wanastahili adhabu kwa dhuluma yao; yaani ukafiri wao.
Na ni vya Mwenyezi Mungu viliyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.
Ambaye ana ufalme wa mbingu na ardhi ni hakika kuwa na amri zote wala hakuna chochote anachoshirikiana na mwengine.
Humsamehe amtakaye na humwadhibu amtakaye.
Mara nyingi tumetaja kwamba akili inahukumu kuwa kafiri anastahili adhabu, lakini sio kuwa analazimika nayo; bali Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaweza kumsamehe. Kwa ajili ya hekima fulani hata kama anastahili adhabu; sawa na unavyomsamehe anayekufanyia uovu au kumsamehe unayemdai. Na rehema na usamehevu kutokana na Mwenyezi Mungu ndio zaidi kutokana na fadhila Yake na ukarimu Wake.