4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا الرِّبَا أَضْعَافًا مُّضَاعَفَةً وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴾
130.Enyi ambao mmeamini msile riba ziada juu ya ziada. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
﴿وَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ﴾
131.Na uogopeni moto ambao umeandaliwa makafiri.
﴿وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴾
132.Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemiwa.
﴿وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ﴾
133.Na harakisheni kuomba msamaha kwa Mola wenu na pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi imeandaliwa wamchao.
MSILE RIBA
Aya 130 - 133
MAANA
Enyi ambao mmeamini! Msile riba ziada juu ya ziada, Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
Wafasiri wametaja njia nyingi za kuiunganisha Aya hii na iliyo kabla yake. Nasi tumeshawahi kueleza mara nyingi kwamba miongoni mwa desturi ya Qur'an ni kuchanganya baadhi ya hukumu na hukumu nyingine. Zaidi ya hayo ni kwamba Aya zake zimeteremshwa kwa vipindi na kwa matukio mbali mbali. Wametoa dalili baadhi kwa Aya hii kwamba riba iliyo haramu ni riba iliyo maradufu. Ama isiyokuwa maradufu, basi si haramu; kutokana na neno ziada juu ya ziada. Ilivyo hasa ni kwamba riba ni haramu kwa mafungu yake yote na daraja zake zote. Umaradufu si sharti la ukatazo, isipokuwa ni kuonyesha vile walivyokuwa wakifanya riba wakati wa ujahiliya. Zaidi ya hayo, ni kuweko Hadith na kuweko 'ijma', kwamba riba chache ni haramu kama ilivyo nyingi. Chochote ambacho wingi wake ni haramu, basi uchache wake pia ni haramu; iwe ni riba au si riba, Mwenye Tafsir Al-Manar amerefusha ufafanuzi alipofasiri Aya hii. Mwisho akamalizia kuwa riba iko mafungu mawili: Fungu la kwanza, ni riba ya muda; kwa mfano kushindwa mtu kulipa deni lake katiTafsir ka muda wa deni, wakaafikiana mdai na mdaiwa kuwa aongeze muda wa kulipa na aongeze mali. Yaani kila unapozidi muda ndipo mali ya kulipa inavyozidi. Akaendelea kusema mwenye Al-Manar: "Aina hii ya riba ni haramu hiyo yenyewe".
Fungu la pili, ni riba ya ziada kwa mfano kutoa mtu shillingi 100 kwa kutaka kulipwa shillingi 110. Anasema mwenye Al-Manar kuwa riba hii, yenyewe sio haramu, isipokuwa ni haramu kwa sababu ya kufikia haramu; yaani kwa kuhofia kuwa riba ya muda ambayo ni haramu. Kwa maneno mengine ni kuwa riba ya muda ni haramu, kama lengo na riba ya ziada ni haramu kama njia ya kufikia lengo. Kisha akaendelea kusema: "Riba ya ziada ni halali kwa dharura, bali hata kwa kuwa na haja; kama alivyosema Ibn Al-qayyim." Hebu tuangalie maelezo yafuatayo:
(i) Imethibiti katika Qur'an na Hadith kwamba aina zote za riba ni haramu bila ya kutofautisha kuwa ni muda au la.
(ii) Kusema: "Bali kwa haja pia," ni katika kuteleza kwa kalamu. Kwani, ni dharura tu ndiyo ihalalishayo haramu, Ama haja hapana. Kuna tofauti kati ya haja na dharura, ni kwamba haja mtu anaweza asihitaji, japokuwa kwa kuivumilia. Ama dharura ni lazima kutekelezwa tu.
(iii) Dharura hapa haiwezi kupatikana kabisa. Si kwa mpokeaji wala kwa mtoaji. Mpokeaji riba, hana dharura yoyote, Kwa sababu anacho kitu cha kujisaidia japokuwa kwa siku moja (ndio maana akakopesha), ama yule mtoaji riba, ikiwa dharura imemfanya akope, basi haiwezi kumfanya atoe (yeye mwenyewe hana ndio maana akakopa). Na hilo si halali hata kama ataweka sharti, kwa sababu, sharti limebatilika. Na kama akichukua kwa nguvu, basi si halali kwa mchukuaji. Kwa sababu huko ni kula mali kwa batili.
(iv) Hebu tuseme, dharura inawezekana kwa anayepokea riba; itakuwa imeondoa hukmu tu, lakini maudhi hayajaondoka. Kwa mfano mwenye njaa ya kushikika akiiba mkate bila shaka atakuwa ameondokewa na hukmu ya kupata dhambi lakini maudhui ya kurudisha thamani ya mkate bado yapo. Yaani analo jukumu la kumlipa mwenye mkate atakapokuwa na uwezo. Na mwenye kuhalalisha kuchukua riba kwa dharura hawezi kuwajibisha kuirudisha kwa mwenyewe ikiondoka shida. Tumezungumza kwa ufafanuzi kuhusu riba katika Aya ya 275 Sura ya Baqara.
Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemiwa.
Hapa kuna ufahamisho wa mambo mawili: Kwanza, kula riba ni kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume. Pili: mtu hapati rehema ya Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote.
Na harakisheni kuomba msamaha kwa Mola wenu na pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi; imeandaliwa wamchao Mungu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kukataza kula riba, kuhadharisha na moto na kutoa mwito wa taqwa na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume; baada ya yote haya ameamrisha kufanya haraka mambo ya kheri ambayo yanawajibisha radhi ya Mwenyezi Mungu na pepo yake. Heri na mambo mema zaidi ni kuhurumiana, kusaidiana na kutoa mali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; kama itakavyoeleza Aya ifuatayo: Ama kauli Yake: Upana wake ni mbingu na ardhi; ni fumbo la ukubwa.
﴿الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ﴾
134.Ambao hutoa katika raha na shida na wazuiao ghadhabu na wenye kusamehe watu na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao hisani
﴿وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴾
135.Na ambao wakifanya jambo ovu au wakidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha wa dhambi zao, na nani anayesamehe dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu, na hawaendelei na waliyoyafanya hali wanajua.
﴿أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ﴾
136.Hao malipo yao ni msamaha utokao kwa Mola wao, na mabustani yenye kupita mito chini yake. Ni wenye kudumu humo na ni malipo mema ya wenye kutenda.
SIFA ZA WAMCHAO MWENYEZI MUNGU
Aya 134 - 136
MAANA
Mwenyezi Mungu amewasifu wanaomcha Yeye kwa sifa ambazo ni njema na ni bora hata kwa asiyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, sifa hizo ni kama hizi zifuatavyo:
I. AMBAO HUTOA KATIKA RAHA NA SHIDA
Utajiri hauwafanyi kuwa na pupa na tamaa ya mali na kufanya ubahili. Wala ufakiri hauwakatishi tamaa wakajiona kuwa wao wanastahiki kuchukua zaidi kuliko kutoa, Bali katika hali zote mbili kwao ni sawa wanatoa kiasi wanavyoweza. Hadith inasema: "Toeni sadaka japokuwa ni upande wa tende."
II. NA WAZUIAO GHADHABU
Hakuna kitu kifahamishacho zaidi nguvu ya imani na akili kubwa kuliko mtu kuimiliki nafsi yake na kuzuia ghadhabu. Ikiwa kumeza ghadhabu kuna uchungu na mashaka ya nafsi, lakini ni kinga ya masaibu mengi na matatizo. Imam Ali
katika kumuusia mwanawe, Imam Hasan
, anasema:"Meza ghadhabu, kwani mimi sikuona kinywa chenye utamu wa matokeo na ladha ya athari kuliko hicho"
III. NA WENYE KUSAMEHE WATU
Kumsamehe aliyekufanyia uovu kunashinda sana kuzuia ghadhabu. Kwa sababu mtu mara nyingi anaidhiki nafsi yake na kuzuia ghadhabu yake kwa msukumo fulani wa masilahi yake kama kujiepusha kujiingiza katika matatizo, ama kusamehe makosa ya watu huko ndiko kufanya hisani kuliko safi kabisa. Imam Ali
anasema: "Ikiwa unamuweza adui yako, ujaalie msamaha wako ndio shukurani ya kuwa na uwezo huo."
IV. NA MWENYEZI MUNGU HUWAPENDA WAFANYAO HISANI
Hisani inapatikana katika kila lenye manufaa ya kimaada au kimaana, iwe nyingi au chache, hata kama ni kusema: "Njia ni hii." Sheikh Al-Maraghi, katika kufasiri Aya hii, anasema: "Ametaja Baihaqi kwamba, mjakazi wa Ali bin Husein
alikuwa akimtilia maji ili atawadhe kwa ajili ya Swala. Birika ikamtoka mkononi na ikavunjika. Ali akainua kichwa chake; yule mjakazi akasoma Aya: "Na wazuiao ghadhabu." Akasema: "Nimezuia ghadhabu yangu."Akasoma tena mjakazi: "Na wenye kusamehe watu." Akasema: "Mungu akusamehe." Mjakazi akaongeza: "Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao hisani." Akasema: "Nimekuacha huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."
V. NA AMBAO WAKIFANYA JAMBO OVU AU WAKIDHULUMU NAFSI ZAO HUMKUBUKA MWENYEZI MUNGU NA KUOMBA MSAMAHA WA DHAMBI ZAO
Uovu ni kama kuingilia haki za wengine, nako ni kuovu zaidi na kukubwa. Kujidhulumu nafsi yake mtu, sio kuingilia haki za wengine, lakini kunaweza kuwa ni kuovu; kama vile ukafiri. Kwa hiyo kukutaja baada ya kutaja uovu ni katika hali ya kutaja ujumla baada ya kutaja mahsusi. Kwa vyovyote iwavyo, ni kwamba Mwenyezi Mungu husamehe madhambi yote na hughufiria kila dhambi; iwe kubwa au ndogo, Kwa sharti yakutaka msamaha; yaani toba ya kweli. Yaani hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) humsamehe mwenye kutubu na akajing'oa kutoka kwenye dhambi. Ama mwenye kung'angania kufanya dhambi naye akiwa anajua kuwa ni dhambi, hawezi kughufiriwa na Mwenyezi Mungu. Maana yake ni kwamba mwenye kufanya uovu kwa kutojua ubaya wake, basi ni mwenye kusamehewa.
Hao malipo yao ni Msamaha.
Mfano wa Aya hii umeshapita katika Sura ya Baqara Aya 25 na 266.
﴿ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ﴾
137.Hakika zimepita desturi nyingi kabla yenu, basi tembeeni katika nchi na muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.
﴿هَـٰذَا بَيَانٌ لِّلنَّاسِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةٌ لِّلْمُتَّقِينَ﴾
138.Huu ni ubainifu kwa watu na mwongozo na mawaidha kwa wamchao.
ZIMEPITA DESTURI
Aya 137 - 138
MAANA
Hakika zimepita desturi nyingi kabla yenu
Yametangulia maelezo kuhusu vita vya Uhud na walioshinda vita walikuwa ni washirikina. Kwa sababu wale waliokuwa wakilinda njia ya kupita adui waliiacha, adui akawazungukia kwa nyuma. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia katika Aya hii Masahaba wa Mtume Muhammad(s.a.w.w)
: Wajue habari za watu waliopita na yaliyowapata wale walioacha msimamo, ili wapate fundisho kwa hilo, na wasirudie tena waliyoyafanya katika Uhud ya kumwasi Mtume, kwa kuicha tupu njia ambayo waliamrishwa wabakie hapo vyovyote itakavyokuwa. Kwa hiyo, walipokhalifu, yaliwapata yalowapata umma uliotangulia ambao uliwakhalifu Mitume yao.
Basi tembeeni katika nchi na muangalie ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.
Makusudio sio kutembea hasa, bali ni kujua hali ya waliopita kwa njia yoyote ile. Hakuna mwenye shaka kwamba ni jambo la faida kwa mwenye akili kufanya utafiti wa hali za watu na kuchunguza sababu zilizowadhoofisha ili apate funzo na kuongoka kwenye lile lenye masilahi. Kwa ajili hii, ndio akasema Mtukufu wa ayasemayo:
Huu ni ubainifu kwa watu na mwongozo na mawaidha kwa wamchao.
Hii ni ishara ya kutaja desturi nzuri, ambazo mwenye kuzifuata hufaulu na mwenye kuziacha hupata hasara. Hapana budi ubainifu uwe kwa watu wote, ili iwe ni hoja kwa aliyeasi, na mwongozo na mawaidha kwa mwenye kumcha Mungu. Kwani hiyo ndiyo njia pekee inayopambanua baina ya mwasi na mtiifu. Lau si ubainifu kusingelikuweko na utiifu wala uasi.
USHENZI WA 5 JUNI
Mnamo mwaka 1387 A.H. watu wa Bahrain waliniita ili nikatoe mihadhara ya kidini kwa mnasaba wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Nilikaa kwao karibu siku 25 ambapo nilitoa mihadhara 20; na vijana walikuwa wakinitupia maswali mbali mbali. Siku moja nikajiwa na ujumbe wakasema: Tuzungumzie sababu za tukio la 5 Juni, bila ya mtazamo wa kidini. Nami ni kasema: Hakuna tofauti baina ya elimu na dini katika mtazamo wa kanuni na desturi inayotawala maisha. Kwani matakwa ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika viumbe vyake na waja wake yanakwenda kwenye desturi za kielimu zilizonyooka na sababu za kawaida; bila ya kutofautisha baina ya waumini au makafiri. Kwa mfano anayejua kuogelea, ataogelea mpaka ufukweni kwa amani hata kama ni kafiri, na asiyejua atazama hata kama ni Mumin, vile vile mwenye kujiandaa vizuri na adui yake atamshinda, ikiwa adui yake hayuko katika hadhari na maandalizi hata kama ni mlahidi.
Na mwenye kufanya uzembe akapuuza, basi hupata hasara hata kama ni katika mawalii na wakweli. Mwenyezi Mungu anasema kuwaambia Masahaba wa Mtume(s.a.w.w)
:
"Wala msizozane msije mkavunjika moyo na kupotea nguvu zenu"
(8:46) Imam Ali
anasema:"Hakika hao - akikusudia watu wa Muawiya - wameshinda kwa umoja wao kwenye batili. Na nyinyi - akiwakusudia watu wake - mmeshindwa kwa sababu ya kugawanyika kwenu kwenye haki yenu."
Kwa hivyo, haki haishindi kwa kuwa ni haki tu; na wala batili haishindwi kwa kuwa ni batili tu, bali kuna desturi katika maisha haya inayoendesha na kutawala jamii. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) haiondoi au kubadilisha mwendo wake; sawa na ilivyo katika desturi ya maumbile.
Kwa hali hiyo basi, hakuna ajabu kwa wazayuni kuteka sehemu ya ardhi yetu, wakisaidiwa na wakoloni, maadamu sisi tumeghafilika, tukiwa tumegawanyika katika vijinchi ambavyo havina umoja wowote zaidi ya neno 'Uarabu.' Hata hivyo, zamu ya kwanza inaweza kuwa kwa upande wa batili, lakini mwisho inakuwa kwa mwenye kusubiri na kumcha Mungu. Kwa sababu namna yoyote itakavyokuwa batili itakosa nguvu na sifa zitazoiwezesha kuendelea. Wakati wowote ule haki itakapopata wa kuipigania ambao wanaiamini na kujitolea mhanga kwa ajili yake, basi batili itatokomea tu. Jambo lenye matumaini ni kwamba waarabu hawakusalimu amri, bali misukosuko na kushindwa kumewakomaza. Wakoloni walifikiri kwamba urefu wa njia utawadhoofisha waarabu na kwamba kuzikalia kimabavu ardhi zao kutawafanya wanyenyekee. Lakini imeonekana kuwa wamekosea, na hakuna kitu kwa waarabu ila subira na bidii, iwe njia ni ndefu au fupi, nyepesi au nzito.
Unaweza kuuliza
: Umesema kuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu yanapita kwenye desturi iliyozoelekea; lakini mbona Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza watu wa Nuh kwa tufani, watu wa Hud kwa upepo usiozuilika, watu wenye ndovu aliwamwagia mawe ya udongo mkavu, na Madain ya Lut ikaigeuza chini juu, yote hayo ni kwa sababu ya kuasi tu na kuihalifu haki; kama ilivyoelezwa katika Kitabu chake Kitukufu.
Jibu
: Hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha matukio hayo ni maalum kupitia kwa Mitume waliotangulia tu na wala haikuendelea na kuenea kwa makafiri wote, kwa hiyo kutumia kipimo kwenye hilo ni nadra.
Swali la pili
: Kwa nini haki isishinde katika hali zote, maadamu Mwenyezi Mungu anaitaka na anawataka watu wa haki, akichukia batili na wafuasi wake?
Jibu
: Lau haki ingelishinda katika hali zote, watu wote wangelifuata kwa kupenda ushindi na kuchukia batili na ingelikuwa uzito kupambanua baina ya habithi ambaye anafuta haki kwa kukusudia manufaa na biashara, na mwema ambaye anafuata haki kwa njia ya haki na anayevumilia shida na matatizo. Zaidi ya hayo ni kwamba sababu hazijulikani ila baada ya kushindwa.
Pili
: lau matatizo angeyapeleka kwa wabatilifu daima na milele na kuwaepushia wenye haki, basi taklifa, thawabu na dhambi zingelibatilika vile vile. Kwa sababu kufuata haki katika hali hii kungelikuwa ni kwa nguvu na kushindwa, si kwa matakwa na hiyari. Kwa ufupi ni kwamba ni juu ya mwislamu kuizingatia vizuri maana ya Aya za Qur'an na kuzifanya ni kipimo cha itikadi yake, picha yake ya kushindwa na kushinda, na nguvu na udhaifu, na kwamba kila kimoja katika mawili hayo yana njia yake mahsusi.
﴿وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴾
139.Wala msidhoofike wala msihuzunike kwani nyinyi ndio mlio juu ikiwa nyinyi ni waumini.
﴿إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنكُمْ شُهَدَاءَ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴾
140. Kama mmepata jeraha, basi kuna kaumu wamekwishapata jeraha kama hilo, na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zamu. Na ili apate kuwajua Mwenyezi Mungu ambao wameamini katika nyinyi na afanye miongoni mwenu mashahidi, Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu.
﴿وَلِيُمَحِّصَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَمْحَقَ الْكَافِرِينَ﴾
141.Na ili awatakase Mwenyezi Mungu ambao wameamini na awaangamize makafiri.
MSIDHOOFIKE
Aya 139 - 141
MAANA
Wala msidhoofike wala msihuzunike
Katika mambo anayoyapa kimaumbile kiongozi mwenye hekima ni kuwepo kwa moyo shupavu katika jeshi lake, na kutokuwa na udhaifu au hofu katika nafsi zao. Kwa sababu kushinda hakutegemei nguvu tu, isipokuwa kabla ya lolote kwanza ni uthabiti na nguvu ya maazimio. Kwa hakika adui yako anaogopa zaidi kumpinga kuliko kumkabili kwako na silaha, Kwa sababu silaha hazina faida ikiwa hakuna uthabiti katika upinzani. Tumeyaona magazeti na kusikia Idhaa za kikoloni zinavyotawanya matangazo kwa ajili ya ukoloni na uzayuni kwa njia ya kupiga vita nafsi na kuuharibu uthabiti wa waarabu. Kujikomboa kimawazo, ndio nguzo ya kwanza ya kujitawala na kujikomboa. Qur'an imetuongoza kwenye hakika hii kwa kusema:"Wala msidhoofike wala msihuzunike"
Ama kusema:kwani nyinyi ndio mlio juu ikiwa nyinyi ni waumini
, ni kuonyesha kuwa Uislamu uko juu na wala hakuna kinachokuwa juu yake, ambaye uislamu umemakinika katika moyo wake, hawezi kulegea wala kufazaika hasa katika njia ya uislamu na kuinua haki isipokuwa anaweza kulegeza kamba katika haki zake zinazomhusu yeye, sio zinazohusu dini yake na itikadi yake.
Kama mmepata jeraha, basi kuna kaumu wamekwishapata jeraha kama hilo.
Yaani yaliyowapata siku ya Uhud kutoka kwa adui naye yalimpata siku ya Badr, lakini hakudhoofika bali alijiandaa na akaurudisha mpira kwenu.
Na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zamu.
Makusudio ya siku hapa ni nguvu; kwamba mara zinakuwa kwa hawa mara kwa wale. Kulikuwa na wakati nguvu zilikuwa kwa mali na watu tu. Lakini leo nguvu ni elimu na kukua viwanda. Kwa hiyo nchi isiyokuwa na elimu ni dhaifu, hata kama ina dhahabu nyeusi (petroli) au dhahabu ya njano. Na nchi yenye elimu ndiyo yenye nguvu hata kama ardhi yake ni tupu isiyokuwa na madini yoyote, Mnyonge inabidi amnyenyekee mwenye nguvu atake asitake, Zamani elimu ilikuwa Mashariki kwenye nchi za waislamu, kisha ikahamia Magharibi. Inawezekana kuwa waislamu wakawa juu kielimu na kiviwanda miaka ijayo, Nani ajuae? Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi
Na ili apate kuwajua Mwenyezi Mungu ambao wameamini katika nyinyi.
Jumla hii inaungana na jumla inayokadiriwa hivi. Na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zamu kwa hekima iliyopitisha zamu hii, Wala sio makusudio kwamba Mwenyezi Mungu hakuwa akiwajua waumini. Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri na yaliyofichika, isipokuwa makusudio ni kuidhihirisha elimu yake kwa waumini ili watu wajulikane na wapambanuke na wengineo. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: "Hakika mmoja wetu akijua kuwa kesho itafika atakuwa ameijua na ikifika pia atakuwa amekwishaijua. Kwa hiyo mabadiliko na matukio yanapatikana katika kile kinachojuliwa ambacho ni kesho sio yule anayejua. Hivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Yeye anamjua mumin na kafir kabla ya kudhihirika kwa watu, Wakijitokeza wanakuwa wamejulikana mbele za watu.
Na afanye miongoni mwenu mashahidi
Shahidi ni yule anayejitolea kufa kwa kuihami itikadi yake, kwa sababu yeye anayaona mauti ni furaha na kuishi na madhalimu ni majonzi, kama alivyosema bwana wa mashahidi, Hussein bin Ali
. Na Qur'an imejaa utukuzo wa mashahidi; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ﴾
"Basi hao wako pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa manabii na walio wakweli sana na mashahidi"
(4:69)
Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu
Kwa hiyo hawezi kumchagua yeyote katika wao kwa kufa shahidi
Na ili awatakase Mwenyezi Mungu ambao wameamini
Lengo la kuweko zamu ya siku ni kuwa mtu afaidike na majaribio na atakase nafsi yake na machafu. Imesemekana kuwa neno Mahhisa ni mitihani na majaribio ambayo yanadhihirisha hakika ya mtu.
Na awaangamize makafiri
Arrazi anasema: "Maana iliyo karibu zaidi ni kuwa makusudio ya makafiri hapa ni kikundi maalum katika wao, nao ni wale ambao wamepigana vita na Mtume(s.a.w.w)
siku ya Uhud, Tumesema hivyo kwa kujua kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuwaangamiza makafiri wote, bali wengi katika wao walibakia kwenye ukafiri wao" Maelezo haya ni sahihi ikiwa makusdio ya maangamizi ni adhabu ya duniani sio ya akhera.
﴿أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ﴾
142.Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu haja wajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?
﴿وَلَقَدْ كُنتُمْ تَمَنَّوْنَ الْمَوْتَ مِن قَبْلِ أَن تَلْقَوْهُ فَقَدْ رَأَيْتُمُوهُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ ﴾
143.Kwa hakika mlikuwa mkiyatamani mauti kabla ya kuyakuta; basi mmekwishayaona nanyi mwatizama.
THAMANI YA PEPO
Aya 142 - 143
MAANA
Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?
Aya hii imefahamisha wazi wazi kwamba uislamu una mfungamano mkubwa na amali njema hapa duniani na kwamba sharti ya kwanza ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kufuzu kwa radhi Zake na thawabu Zake ni jihadi, kujitolea, ukweli, ikhlasi, subira na uthabiti. Ama kujenga misikiti, sehemu za ibada, kufunga, kuswali na kusoma Qur'an na nyuradi, yote hayo na mengineyo sichochote ila ikiwa, ni nyenzo ya kazi itakayoleta manufaa kwa watu au itakayowakinga na madhara.
Aya hii tuliyonayo ambayo imefungamanisha kuingia peponi na jihadi na kuvumilia taabu zake, iko katika maana pamoja na Aya hizi zifuatazo:
﴿إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kwamba wapate pepo, wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wanaua na wanauwa. Ni ahadi iliyothibiti juu yake katika Tawrat na Injil na Qur'an"
(9:111) Na Aya nyingine ni:
﴿وَمَن كَانَ فِي هَـٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا﴾
"Na aliye kipofu katika (dunia) hii basi katika akhera atakuwa kipofu na aliyepotea zaidi njia"
(17:72)
Inatosha kuwa ni dalili ya mkato ya hayo kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾ وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ ﴿٤٠﴾ ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ ﴾
"Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya, Na kwamba amali yake itaonekana. Kisha atalipwa malipo yaliyo kamili"
(53: 39 - 41)
Miongoni mwa kauli za Imam Ali
ni:"Pepo imezungukwa na machukivu na moto umezungukwa na anasa, Nafsi zenu hazina thamani zaidi ya pepo, kwa hivyo msiziuzie (kitu kingine) ila hiyo tu"
Yameshatangulia maelezo katika tafsir ya Aya 155 katika Sura ya Baqara, kifungu 'Thamani ya pepo'
NEMBO ZA KIDINI
Nembo za kidini, ni kama sehemu za ibada na za kuswali zilizo takatifu, hilo halina shaka, bali ni dharura ya kidini, hapana budi kuwepo. Hakuna nchi yoyote au kikundi chochote ambacho kina msingi mmoja ila kitakuwa na nembo inayokionyesha kikundi hicho au nchi hiyo, na inayowaweka pamoja wafuasi wake. Lakini nembo peke yake si chochote, bali nembo ni lazima ifuatiliwe na vitendo na athari. Kwa hiyo Swala si kurukuu na kusujudu tu, bali Swala ni ile inayoiweka nafsi ya mwenye kuswali kujitakasa na maovu, wala muungano sio kuungana kusoma tahlili na takbira, bali ni kusaidiana tukiwa na ikhlasi ya lile ambalo lina kheri ya wote. Hivi sasa wengi wetu wamezifanya nembo za kidini ni vyombo vya kupoteza, na maficho ya miradi ya wakoloni na malengo ya uzayuni. Kwa sababu vyama vingi ambavyo vina majina ya kidini au ya kizalendo ni mashirika ya kijasusi ya nje. Na gharama zake zinatokana na faida itokayo katika mashirika ya mafuta. Lakini jambo la kutia moyo ni kuwa hayo yamefichuka kwa wote. Wenye ikhlasi hawaviamini wala hawashirikiani navyo isipokuwa wahaini wanaouza dini yao na nchi yao kwa shetani.
Kwa hakika mlikuwa mkiyatamani mauti kabla ya kuyakuta; basi mmekwisha yaona nanyi mwatizama
Msemo unaelekezwa kwa baadhi ya Sahaba wa Mtume(s.a.w.w)
, ambao kabla ya vita vya Uhud, walikuwa wakitamani kufuzu kwa kufa shahid, lakini mambo yalipowazidia, waliogopa, wakamwachia Mtume(s.a.w.w)
adui yake na adui yao. Baadhi ya Riwaya zinasema kuwa miongoni mwa Masahaba walikuwako waliokuwa wakisema: vikija vita tukiwa na Mtume(s.a.w.w)
tutapigana tu, walipotahiniwa na hilo hawakutekeleza ahadi. Ndipo Mwenyezi Mungu akawateremshia Aya hii, Makusudio ya kuona mauti ni kuona sababu zake kutoka kwenye mapambano ya mashujaa. Mwenyezi Mungu amewatahayarisha kwa Aya hii kutokana na vitendo vyao kuhalifu kauli zao.
MABADILIKO YA HULKA NA FIKRA
Kila mtu ana hali zake na mazingira yake yanayomuhusu. Hali hizi - aghlab - ndizo zinazotawala hulka na fikra zake, Kwa mfano mtu mnyonge anaiona mbaya zaidi dhulma kuliko mwenye nguvu. Na mwenye kukulia katika mazingira ya kuabudu masanamu hawezi kuona ubaya kuyatukuza, ila akiwa si mtu wa kawaida; kama vile Muhammad bin Abdullah, Kwani yeye kimaumbile yake tu alikuwa akichukia kila desturi mbaya ya watu wake. Mara nyingine hali ya mtu inaweza kubadilika na kuwa tajiri baada ya kuwa maskini, au kinyume chake. Basi hapo hulka zake na fikra zake zinabadilika kufuatana na mabadiliko hayo. Kwa hiyo dhati ya mtu inabakia na sifa yake ikiwa hali yake ya kijamii haikubadilika. Aghlabu hali ikibadilika na sifa za dhati nazo hubadilika. Tumewaona watu waliokuwa wakiwalaumu matajiri na maraisi, wakati wao ni mafukara wanaoongozwa, lakini mara tu walipopata mali na cheo wakavunja ahadi na kuwa wabaya zaidi ya waliokuwa wakiwalaumu jana.
Qur'an Tukufu imetilia mkazo nadharia hii kwa Aya hii tuliyo nayo, na pia Aya nyingine isemayo:
﴿وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٧٥﴾ فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ ﴾
"Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: akitupa katika fadhila zake, hakika tutatoa sadaka na tutakuwa miongoni mwa watu wema. Lakini alipowapa katika fadhila zake walizifanyia ubakhili na wakageuka na huku wakipuuza"
(9:75-76)
Mwenye akili na uzoevu huituhumu nafsi yake wala halitilii mkazo kwa mawazo kila linalomtokea, kwa kuhofia kuwa bendera inayofuata upepo; kama ambavyo mumin wa kweli anabaki kuwa thabiti katika tabu na raha; maneno yake hufuatana na vitendo vyake katika hali zote na yote huyaelekeza kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Yamekuja maelezo katika tafsir ya Aya isemayo:
﴿وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ فَمُسْتَقَرٌّ وَمُسْتَوْدَعٌ﴾
"Na yeye ndiye ambaye amewaumba katika nafsi moja kuna (iliyo) mahali pa milele na mahali pa muda"
(6:98)
kuwa, mahali pa milele ni imani iliyo thabiti, na mahali pa muda ni imani ya kuazima, na hakuna kitu kinachofahamisha imani potofu kuliko kugongana kauli na vitendo. Ndio maana zikawa kauli za Mitume na Maimamu watakatifu ndio vitendo vyao hasa. Na vitendo vya wanafiki viko mbali na kauli zao.
﴿وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴾
144.Hakuwa Muhammad ila ni Mtume; wamekwisha pita Mitume kabla yake. Je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma?. Na atakayerudi nyuma hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu atawalipa wenye kushukuru.
﴿وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَن تَمُوتَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ كِتَابًا مُّؤَجَّلًا وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ﴾
145.Na nafsi haiwezi kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyoandikwa ajali yake. Na anayetaka malipo ya dunia tutampa humo na anayetaka malipo ya akhera tutampa huko; na tutawalipa wenye kushukuru.
﴿وَكَأَيِّن مِّن نَّبِيٍّ قَاتَلَ مَعَهُ رِبِّيُّونَ كَثِيرٌ فَمَا وَهَنُوا لِمَا أَصَابَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَمَا ضَعُفُوا وَمَا اسْتَكَانُوا وَاللَّـهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ ﴾
146.Ni manabii wangapi waliopigana pamoja nao waumin wengi, nao hawakulegea kwa yale yaliyowasibu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika, wala hawakudhalilika, Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaosubiri.
﴿وَمَا كَانَ قَوْلَهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ﴾
147.Halikuwa neno lao, ila ni kusema: Ewe Mola wetu! Tughufirie dhambi zetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu na uimarishe miguu yetu na utunusuru juu ya watu makafiri.
﴿فَآتَاهُمُ اللَّـهُ ثَوَابَ الدُّنْيَا وَحُسْنَ ثَوَابِ الْآخِرَةِ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴾
148.Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na malipo ya akhera na Mwenyezi Mungu anawapenda watendao mema.
HAKUWA MUHAMMAD ILA NI MTUME
Aya 144-148
MAANA
Hakuwa Muhammad ila ni Mtume wamekwishapita Mitume kabla yake. Je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma?.
Aya hii inaashiria tukio maalum ambalo ni vita vya Uhud; limekwishaelezwa. Kwa ufupi ni kuwa Mtume(s.a.w.w)
aliwaamrisha wapiga mishale wasiondoke kwenye mlima kwa hali yoyote ile, ni sawa wawe waislamu wameshinda au wameshindwa. Lakini kundi kubwa la wapiga mishale walipoona kushindwa kwa washirikina katika muhula wa kwanza, waliziacha sehemu za nyuma za waislamu bila ya ulinzi na kuharakia nyara. Kwa hiyo washirikina wakawarudia waislamu: wengi wao wakauwawa na Mtume kujeruhiwa vibaya. Mnadi akanadi kuwa Muhammad ameuawa, watu wakamkimbia Mtume na akabakiwa na wachache tu, akiwemo Ali bin Abi Talib na Abu Dajana Al-ansari. Masahaba wengine wakasema: "Hatupati mtu wa kututakia amani kwa Abu Sufian?" wengine wakasema: "Lau Muhammad angelikuwa Mtume asingeuawa, rudieni dini yenu ya kwanza."
Qur'an imewakaripa walioshindwa, wenye shaka shaka ikiwaambia kuwa Muhammad ni Mtume aliye binadamu tu, anayefikisha risala ya Mola wake kwa waja wake, na anapofikisha, basi umuhimu wake umekoma. Na ujumbe wake haufungamani na utu wake wala haufi kwa kufa kwake, bali utabaki kwa kubakia Mwenyezi Mungu asiyekufa; sawa na Mitume wengine ambao walikufa au kuuwawa na ujumbe wao na mafunzo yao kubakia. Kwa maneno mengine, mwito haufi kwa kufa anayeutoa mwito huo; na misingi haiondoki kwa kuondoka watu. Mfano mzuri wa hakika hii ni yale yaliyoelezwa katika Tafsir Tabari kwamba mtu mmoja katika Mujahirina alimpitia mtu mwengine katika Ansari akiwa ametapakaa damu. yule Muhajir akasema: "Je, wajua kuwa Muhammad ameuawa?" Ansari akasema: "Ikiwa ameuwawa tayari amekwisha fikisha ujumbe, basi ipiganieni dini yenu"
Katika hiyo hiyo Tabari na vinginevyo imeelezwa kuwa Anas bin Annadhr alimpitia Umar bin Khattab na Talha bin Ubaidullah na watu wengine katika Muhajir na Ansar wakiwa wamesalimu amri. Anas akawaambia: "Mbona mmekaa? wakasema: Muhammad ameuawa. Akasema: Ikiwa Muhammad ameuawa, lakini Mola wa "Muhammad hakuuawa, na mtayafanyia nini maisha baada ya Muhammad, Basi piganieni lile alilopigania na kufeni kwenye lile alilolifia." Kisha akaendelea kusema: "Ewe Mola wangu! Hakika mimi nakuomba msamaha na waliyoyasema hawa na ninajitenga na waliyokuja nayo" Kisha akaukamata barabara upanga wake akapigana mpaka akauawa. (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie)
Ibn Al-Qayyim Al-Jawziy katika juzuu ya pili ya Zadul-Ma'ad uk. 253 anasema: Tukio la Uhud lilikuwa ni utangulizi na lawama kuhusu mauti ya Muhammad(s.a.w.w)
. Mwenyezi Mungu anawazindua na kuwakaripia kwa kurudi nyuma kwao, iwapo Mtume wa Mwenyezi Mungu atakufa au kuuwawa. Mwenye Tafsir Al-Manar akimnukuu mwalimu wake Sheikh Muhammad Abduh anasema: Neno 'mtarudi nyuma' linaenea katika kurtadi kwa kuacha dini na kuacha kuipa nguvu haki." Kisha akaongezea mwenye Al-Manar kwa kusema: hivi ndivyo ilivyo. Kwa hiyo basi, kurudi nyuma kulikokusudiwa katika Aya hii hakuishii kwenye Tawhid peke yake, bali kunaenea kuacha kazi ya haki aliyoiusia Mtume(s.a.w.w)
. Haya yanatiliwa nguvu na yaliyoelezwa katika Sahihi Bukhari Jz 9 kitabul-Fitan kwamba Mtume atasema siku ya kiyama: "Ewe Mola wangu! (Hao) ni sahaba zangu" Naye ataambiwa "Wewe hujui walizuwa nini baada yako" Hadith nyingine katika Hadith za Bukhari inasema: "wewe hujui walibadilisha nini baada yako?" "Hapo nitasema: Basi kuangamia ni kwa mwenye kuibadilisha (dini yake) baada yangu" Hakuna mwenye shaka kwamba makusudio ya kubadilisha hapa ni kuiacha sunna yake na kuhalifu kauli zake na sharia yake.
Na atakayerudi nyuma hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu
bali atajidhuru mwenyewe kwa kujiingiza katika machukivu na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na mwenyezi Mungu atawalipa wenye kushukuru
Ibnul-Qayyim katika Zadul-Ma'ad uk. 254 anasema: "Na wenye kushukuru ni wale waliojua thamani ya neema wakathibiti nayo mpaka wakafa au kuuawa. Ilidhihiri athari ya lawama hii na yakahukumu maneno hayo siku alipokufa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
, akartadi mwenye kurtadi kwa kurudi nyuma.
AJALI HAINA KINGA
Na nafsi haiwezi kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu - kama ilivyoandikwa ajali yake.
Aya hii iko katika maana ya Aya isemayo:
﴿فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ﴾
"Utakapofika muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia"
(7:34)
Maana ni kuwa uhai na kifo viko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwamba ajali imepangwa katika muda maalum anaoujua yeye; haiharakishwi wala haikawizwi. Ni sawa iwe sababu yake ni upanga, maradhi, uzee au mengineyo. Imam Ali
anasema:"Ajali inatosha kuwa ni mlinzi"
Akasema tena:"Ajali ni ngome imara."
Katika Aya hii kuna mahimizo ya Jihadi, kwa sababu ajali ipo tu, Na wala hakuna yeyote atakayekufa kabla ya kufikilia ajali yake, Hata akijipeleka kwenye maangamizi.
Unaweza kuuliza
: tunavyoshuhudia ni kuwa mauti yana sababu maalum: kama vile kuuliwa, kufa maji, majanga na mengineyo. Je hili si linakanusha kuwa ajali imepangwa kwa ujuzi wake Mwenyezi Mungu?
Hilo amelijibu Sheikh Muhammad Abduh- kama ilivyo katika Al-Manar - kwamba hakuna sababu za mauti zaidi ya ajali iliyokadiriwa na Mwenyezi Mungu. Kwani janga linaweza kuenea, lakini akafa kijana mwenye nguvu na akabaki mkongwe dhaifu, Ni majanga mangapi yaliyomwacha huyu ya kamuua yule. Na kama ingelikuwa sababu hizi zinawaenea wote, basi ingelithibiti athari yake kwa wote, bila ya kubakisha hata mmoja. Swali la pili: Kama ni hivyo basi inatakikana muuaji asiwe na majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu anasema:
﴿وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا﴾
"Na Mwenye kumua Muumin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atadumu na Mwenyezi Mungu amemghadhibikia na amemlaani na amemwandalia adhabu kubwa
(4:93).
Jibu
: Mwenye kuuawa amekufa kwa muda wake, na mwenye kuuwa anastahili adhabu, kwa sababu amefanya lililokatazwa na Mwenyezi Mungu hali alikuwa anaweza kujiepusha nalo na kumwacha aliyemuua, afe na sababu nyingine. Kwa maneno mengine ni kuwa hapa kuna mambo mawili:Kwanza
: Kila mwenye kufanya jambo la haramu kwa makusudi, ana jukumu.
Pili
: Mwenye kufanyiwa makosa ana muda wake maalum. Kwa hiyo hapo yamekuja mambo mawili katika maudhui moja, lakini kila moja lina hukumu yake na athari yake.
Na anayetaka malipo ya dunia tutampa humo na anayetaka malipo ya akhera tutampa huko: na tutawalipa wenye kushukuru.
Tamko la Aya linaenea kwa mambo yote na mfumo wa maneno unahusu jihadi. Maana yake ni kuwa mwenye kupigana kwa kutafuta faida na ngawira, si kwa kutaka thawabu za Mwenyezi Mungu na akauliwa, basi atakuwa amepata hasara ya dunia na akhera. Na kama akisalimika na jeshi likapata ngawira, atapata fungu lake na hatapata chochote katika thawabu za Mwenyezi Mungu, kama akipigana kwa kuinusuru haki na kuinyanyua dini atachukua fungu lake la ngawira na atastahiki malipo na thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Vilevile hata akikusudia mambo mawili pamoja, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ فَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ﴿٢٠٠﴾ وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿٢٠١﴾ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّمَّا كَسَبُوا وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴾
"Na kuna miongoni mwa watu asemaye: Mola wetu! Tupe katika dunia, na katika akhera hana sehemu yoyote. Na miongoni mwao yuko anayesema: Mola wetu! Tupe mema duniani na katika akhera (utupe) mema na utukinge na adhabu ya moto. Hao ndio wenye fungu katika waliyoyachuma na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu"
(2: 200-202)
Jihadi inaweza kuchukuliwa na makusudio mawili pamoja: dunia na akhera kinyume na Saumu, Swala, Hijja na Zaka. Kwa sababu hayo yote ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee yake ambayo yanaharibiwa hata na mchanganyiko mdogo.
KILA MTU ANA ALILOLINUIA
Mwenye kufuatilia Aya za Mwenyezi Mungu (s.w.t) na Hadith za Mtume Wake(s.a.w.w)
ataona kuwa nia ina athari kubwa katika kuhukumu kauli na vitendo vya watu. Mwenyezi Mungu anasema: "Anayetaka malipo ya duniani tutampa" Akasema tena:
﴿ن كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاءُ لِمَن نُّرِيدُ ﴿١٨﴾ وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا﴾
"Anayetaka (dunia) ipitayo upesi, tutamharakisha humo tunayoyataka na anayetaka akhera na akizifanyia juhudi amali zake na hali ya kuwa ni mu'min, basi hao juhudi yao ni yenye kushukuriwa"
(17: 18-19).
Vilevile amesema:
﴿يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾ إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴾
"Siku ambayo haitafaa mali wala watoto, isipokuwa mwenye kuja na moyo safi"
(26: 88-89)
Katika Hadith tukufu imesemwa hivi: "kila mtu ana alilonuiawatu watafufuliwa kulingana na nia zao. hakika amali (zote huzingatiwa) kwa nia Nia ya mtu ni bora kuliko vitendo vyake" Wala hapana ajabu, kwani moyo ndio msingi. Mapigo yake ndiyo yanayopeleka uhai wa mtu na kuzimika kwake ndiko kuzimika uhai, ndipo mahali pa imani na ukanushaji, hofu na matarajio, mapenzi na chuki, ushujaa na woga, ikhlas na unafiki, kukinai na tamaa na mengineyo katika mambo mazuri na mabaya. Hadith Qudsi inasema: "Haikunikunjua ardhi yangu wala mbingu yangu lakini moyo wa mja wangu mumin umenikunjua. Yaani umetambua ukubwa wa Mwenyezi Mungu.
Vitendo vyote hutendwa na kutengenezwa na moyo, kwa sababu ndio asili yake. Kwa hivyo basi mtu anaweza kujichagulia njia yake yeye mwenyewe kwa kuchagua malengo yake, kheri na shari anayachagua kuanzia mwanzo hadi mwisho, kama ambavyo sisi tunaweza kumhukumu kwa malengo anayojichaguliya mwenyewe. Watu wa nadharia (ya upatikanao) wanasema: haiwezekani kumhukumu mtu ila baada ya kupita hatua ya mwisho katika hatua za maisha yake.. maana yake ni kuwa wanalazimisha kutopitisha hukmu ila kwa waliokufa tu, Ama walio hai hawahukumiwi au kulaumiwaIngawaje hawa wanaodai hivyo akiwemo kiongozi wao Sartre, wanawahukumu walio hai.
Unaweza kuuliza
: Mara nyingi umeeleza - katika sehemu mbali mbali - kwamba vinavyozingatiwa ni vitendo na kwamba hakuna imani ila kwa takua na amali njema. Na haya si yanapigana na kauli yako ya hapa kwamba inayozingatiwa ni nia na malengo?
Jibu
: Nia, tunayoikusudia hapa ni nguvu ya msukumo na azimio linalotia mkazo ambalo haliepukani na kitendo. Hilo limeelezwa na Aya isemayo:
"... Na anayeitaka akhera na akazifanyia juhudi amali zake"
(17:19) Na nia hii iko katika hukmu ya kitendo, bali ni kitendo hasa, kama alivyosema Imam Jafar as-Sadiq
. kwa sababu ndiyo asili ya kitendo na ni chimbuko lake, Na asiyekusudia hatendi. Kwa hivyo basi thawabu za nia hii ni thawabu za kitendo. Ama nia ya uovu, yaani kuazimia kufanya uovu, ni haramu bila ya shaka yoyote. Na mwenye kuazimia hayo anastahiki adhabu, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) aweza kumuondoshea adhabu hiyo - kwa hisani yake - ikiwa hatofanya alilolinuiya, hata kama alilazimika kuliacha kwa nguvu. Hivyo, katika mtazamo wa Kiislamu, nia ya kheri ni kheri hata bila ya vitendo na nia ya shari si shari bila ya kitendo.
Ni Manabii wangapi waliopigana, pamoja nao waumini wengi, Nao hawakulegea kwa yale yaliyowasibu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika, wala hawakudhalilika, Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao subira.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwapa ushindi Waislamu katika vita vya Badr, wakiwa ni wachache na wanyonge, waliona kwamba kila vita watashinda maadamu wako na Muhammad(s.a.w.w)
, hivyo kushindwa kwa siku ya Uhud kukawa ni jambo wasilolitazamia. Wakawa na yale tuliyokwisha yaeleza. Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawapigia mifano wale waliolegea, wakadhoofika na kudhalilika na kutokuwa na subira siku ya Uhud, anawapigia mfano na wafuasi wa Mitume waliotangulia, ambao walikuwa na subira katika Jihadi, kuuliwa , kutekwa na kujeruhiwa, nao hawakukimbia, kama mlivyofanya nyinyi wafuasi wa Muhammad(s.a.w.w)
.
Na ilikuwa ni laiki yenu muwaigize, muwe na mazingatio kwa hali zao; jambo ambalo linatakikana kwa waumini wanaopigania dini yao na itikadi yao kwa nyoyo zao.
Halikuwa neno lao
, yaani wafuasi wa Mitume waliotangulia,ila ni kusema: "Ewe Mola wetu! Tughufurie dhambi zetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu na uimarishe miguu yetu na utusaidie juu ya watu makafiri.
Hawakutia shaka kabisa katika dini yao na Mtume wao kama yale waliyoyafanya maswahaba wa Muhammad(s.a.w.w)
siku ya Uhud. Hivi ndivyo anavyokuwa mu'min wa kweli, akijituhumu mwenyewe na kuona kuwa balaa zilizompata ni kwa ajili ya uzembe wake na kupetuka kwake mpaka katika amri za Mwenyezi Mungu, humuomba Mwenyezi Mungu msamaha na uongofu. Ama mu'min aliye kombokombo anamsukumizia Mungu na kusema: Mola wangu amenitweza.
Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na malipo mema ya akhera, na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaotenda wema.
Malipo ya Mwenyezi Mungu na pendo lake linatosha kuwa ni fahari na ni akiba ya akhera. Aya hii inafahamisha kwamba kunyenyekea na kujituhumu kunakurubisha kwa Mwenyezi Mungu na humwinua mwenye kunyenyekea na kumweka kwenye daraja ya juu.