TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17435
Pakua: 3869


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17435 / Pakua: 3869
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

Mwandishi:
Swahili

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تُطِيعُوا الَّذِينَ كَفَرُوا يَرُدُّوكُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ فَتَنقَلِبُوا خَاسِرِينَ﴾

149.Enyi ambao mmeamini! Mkiwatii ambao wamekufuru watawarudisha nyuma mtageuka kuwa ni wenye kuhasirika.

﴿بَلِ اللَّـهُ مَوْلَاكُمْ وَهُوَ خَيْرُ النَّاصِرِينَ ﴾

150.Bali Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wenu naye ndiye bora wa wasaidizi.

﴿سَنُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ بِمَا أَشْرَكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ وَبِئْسَ مَثْوَى الظَّالِمِينَ ﴾

151.Tutatia hofu katika nyoyo za ambao wamekufuru kwa sababu ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia hoja; na makazi yao ni motoni nayo ndiyo makazi mabaya ya wadhalimu.

MKIWATII AMBAO WAMEKUFURU

Aya 149-151

LUGHA

Makusudio ya neno sultan ni hoja, limetumika neno hilo kwa vile hoja ina nguvu za kuikinga batili.

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Mkiwatii ambao wamekufuru watawarudisha nyuma,

Sheikh Maraghi katika kufasiri Aya hii anasema: "Makusudio ya 'ambao wamekufuru' ni Abu Sufyan, kwa sababu yeye ndiye mzizi wa fitina." Kila mtu, awe na haki au batili, anataka watu wote wawe upande wake. Tofauti ni kwamba twaa ya mbatilifu ni hasara na madhara. Na twaa ya mwenye haki ni faida na manufaa, kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawahadharisha waumini na makafiri.

Bali Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wenu naye ndiye bora wa wasaidizi.

Mu'min hafikirii kumtii kafiri na kumpenda wala hababaishwi na hadaa zake au kumfanya ni mlinzi, isipokuwa Mungu tu peke yake ndiye anayemnusuru na maadui.

Na ambaye Mwenyezi Mungu ndiye msaidizi wake, hatahitajia rafiki wala msaidizi mwingine.

Tutatia hofu katika nyoyo za ambao wamekufuru kwa sababu ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia hoja.

Yaani, enyi waislamu! Msiwaogope washirikina kwa sababu ya wao kuwashinda katika vita vya Uhud, kwani Mwenyezi Mungu atatia hofu katika nyoyo zao kutokana na nyinyi, kwa sababu wao wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika bila ya dalili yenye mwelekeo, isipokuwa ni kwa kufuata tu.

Inasemekana kuwa Abu Sufian na washirikina wenzake walipoondoka Uhud kuelekea Makka, walisema: "Tumefanya vibaya sisi; tumewaua mpaka wakabakia wanyonge halafu tukawaacha, tuwarudieni! Tuwamalize" Walipoazimia hivyo Mwenyezi Mungu akawatia hofu, mpaka wakaacha yale waliyoyakusudia."Ni sawa sababu hii iwe ndiyo ya kushuka Aya au la,lakini tamko la Aya halikatai hayo.

﴿وَلَقَدْ صَدَقَكُمُ اللَّـهُ وَعْدَهُ إِذْ تَحُسُّونَهُم بِإِذْنِهِ حَتَّىٰ إِذَا فَشِلْتُمْ وَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَعَصَيْتُم مِّن بَعْدِ مَا أَرَاكُم مَّا تُحِبُّونَ مِنكُم مَّن يُرِيدُ الدُّنْيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ الْآخِرَةَ ثُمَّ صَرَفَكُمْ عَنْهُمْ لِيَبْتَلِيَكُمْ وَلَقَدْ عَفَا عَنكُمْ وَاللَّـهُ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ﴾

152.Na hakika Mwenyezi Mungu aliwatimizia miadi yake mlipokuwa mkiwaua kwa idhini yake, mpaka mlipolegea na kuzozana katika amri na mkaasi, Baada ya kuwaonyesha mliyoyapenda. Kuna katika nyinyi wanaotaka ulimwengu na kuna katika nyinyi wanaotaka akhera. Kisha akawaepusha nao ili awafanyie mtihani na amekwisha wasamehe, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye hisani kwa waumini.

MWENYEZI MUNGU AMEWATIMIZIA

Aya 152

MAANA

Na hakika Mwenyezi Mungu aliwatimizia miadi yake mlipokuwa mkiwaua kwa idhini yake.

Bado maneno yanaelekezwa kwa Masahaba wa Mtume waliokuwa katika Uhud. Mtume alikuwa amekwisha waahidi kuwa ushindi ni wao siku hiyo kama wakifuata amri. Na Mwenyezi Mungu ametekeleza ahadi ya aliyoyasema kupitia kwa Mtume wake. Hilo ni kuwa Mtume(s.a.w.w) aliwaweka wapiga mishale kwenye mlima kuwalinda waislamu kwa nyuma, akawausia kutoondoka hata kama wakimwona adui anadonwa na ndege. Na akawaahidi ushindi kwa sharti hili. Wapiga mishale walikuwa hamsini.

Vita vilipoanza wapiga mishale wa mstari wa mbele waliwadunga washirikina na Masahaba wengine wakawa wanawapiga kwa panga zao na kuwauwa haraka haraka mpaka washirikina wakashindwa. Na hii ndio maana ya 'mlipokuwa mkiwaua kwa idhini yake' Yaani mnawaua kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Katika Tafsir ya Ibn Jarir Tabari na Maraghi na wengineo imetajwa kwamba, Talha bin Uthman mshika bendera ya washirikina aliye maarufu kwa kamanda, alisimama akasema: "Enyi watu wa Muhammad! Nyinyi mnadai kuwa Mwenyezi Mungu atatuharakisha motoni kwa panga zenu na zetu. Je nani aliye tayari nimharakishe peponi kwa upanga wangu au aniharakishe motoni kwa upanga wake? Akajitokeza Ali bin Abu Talib(a.s) akampiga na kumkata mguu, akaanguka na kuwa uchi, Talha akamwambia Ali, "Muone Mungu ewe binamu!" Ali akamwacha; na Mtume akapiga takbira, Masahaba wakamwuliza Ali, "Kitu gani kilichokufanya usimmalize?"

Akajibu : "Amenilalamikia kwa jina la Mwenyezi Mungu." Hii ndiyo hulka ya Ali, moyo wake una upole hata kwa adui yake ambaye alikuwa tayari kumuua.

Mpaka mlipolegea na kuzozana katika amri na mkaasi baada ya kuwaonyesha mliyoyapenda.

Baada ya washirikina kuanza kukimbia - ambapo walikuwa elfu tatu - bonde lilikuwa limejaa ngawira na huku wenzao wakiziokota, walinzi waliingiwa na tamaa na wakazozana, baadhi yao wakasema: "Twangoja nini hapa?" wakajipurukusha na wasia wa Mtume na alivyowatilia mkazo kubaki. Kiongozi wao Abdallah bin Jubair akawaambia. "Bakini wala msikhalifu amri ya Mtume(s.a.w.w) " lakini wengi wao wakaondoka kwenda kuokota ngawira na kumwacha kiongozi wao akiwa na watu wasiozidi kumi.

Kwenye uasi huu na mzozano Mwenyezi Mungu ndio anaashiria kwa kusema: "Mpaka mlipozozana katika amri na mkaasi" Ama kusema kwake: baada ya kuwaonyesha mliyoyapenda, ni ishara ya kushindwa washirikina na ngawira zao. Khalid bi Al-Walid (aliyekuwa akipigana dhidi ya Mtume) akiwa pamoja na Abu Sufiyan, alipoona ngome iko tupu alichukua nafasi hiyo pamoja na kikosi cha washirikina kwenda kuwashambulia wapiga mishale waliobaki. Hawa walipigana kishujaa mpaka wote wakauwa shahidi na ngome ya nyuma wa waislamu ikawa tupu. Washirikina wakarudi uwanjani na kuwazingira waislamu kutoka mbele na nyuma, wengi wakauawa na kujeruhiwa, Mpira ukawageukia. Hii ndiyo natija hasa ya ugomvi na mizozano.

Kuna katika nyinyi watakao ulimwengu.

Hao ni wapiga mishale ambao waliacha sehemu zao kwa tamaa ya ngawira.

Na kuna katika nyinyi watakao akhera.

Hao ni wale waliobakia sehemu zao pamoja na kiongozi wao Abadallah bin Jubair mpaka wakafa mashahid,

Kisha akawaepusha nao.

Yaani kuwarudishia makafiri baada ya kuwa nyinyi mmewashinda, kwa sababu ya kuzozana kwenu na kuasi kwenu.

Ili awafanyie Mtihani

Yaani, amewafanyia mtihani ili aonekane mwenye uthabiti katika imani na uvumilivu na ampambanue mwenye ikhlasi na mnafiki.

Na amekwisha wasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye hisani kwa waumini.

Ni mara nyingi mtu hukosea kwa kuchanganyikiwa, kisha akarudia uongofu wake. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu humsamehe kwa yale yaliyopita. Lakini mwenye kurudia ataadhibiwa na Mwenyezi Mungu.

﴿إِذْ تُصْعِدُونَ وَلَا تَلْوُونَ عَلَىٰ أَحَدٍ وَالرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ فِي أُخْرَاكُمْ فَأَثَابَكُمْ غَمًّا بِغَمٍّ لِّكَيْلَا تَحْزَنُوا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا مَا أَصَابَكُمْ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴾

153.(kumbukeni) mlipotoka mbio wala hamumtizami yeyote na hali Mtume anawaita nyuma yenu. Akawalipa majonzi kwa majonzi ili msihuzunike kwa mliyoyakosa wala kwa yaliyowasibu, Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

﴿ثُمَّ أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّن بَعْدِ الْغَمِّ أَمَنَةً نُّعَاسًا يَغْشَىٰ طَائِفَةً مِّنكُمْ وَطَائِفَةٌ قَدْ أَهَمَّتْهُمْ أَنفُسُهُمْ يَظُنُّونَ بِاللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ ظَنَّ الْجَاهِلِيَّةِ يَقُولُونَ هَل لَّنَا مِنَ الْأَمْرِ مِن شَيْءٍ قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّـهِ يُخْفُونَ فِي أَنفُسِهِم مَّا لَا يُبْدُونَ لَكَ يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ وَلِيَبْتَلِيَ اللَّـهُ مَا فِي صُدُورِكُمْ وَلِيُمَحِّصَ مَا فِي قُلُوبِكُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴾

154.Kisha baada ya majonzi akawateremshia utulivu, usingizi uliofunika kundi katika nyinyi, na kundi jingine limeshughulishwa na nafsi zao, wakimdhania Mwenyezi Mungu dhana ya kijinga isiyo ya haki. Wakisema: je, tuna chochote katika jambo hili? Waambie mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu, Huficha katika nafsi zao ambalo hawakudhihirishii wewe. Husema: lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusingeliuawa hapa. Waambie: lau mgelikuwa majumbani mwenu, wangetoka ambao wameandikiwa kuuawa wakaenda katika maangamivu yao na ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu na ayasafishe yaliyomo nyoyoni mwenu, Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani.

﴿إِنَّ الَّذِينَ تَوَلَّوْا مِنكُمْ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ إِنَّمَا اسْتَزَلَّهُمُ الشَّيْطَانُ بِبَعْضِ مَا كَسَبُوا وَلَقَدْ عَفَا اللَّـهُ عَنْهُمْ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ حَلِيمٌ﴾

155.Hakika wale waliogeuka siku yalipokutana makundi mawili, shetani ndiye aliyewatelezesha kwa baadhi ya waliyoyafanya, na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Maghufira, mpole.

MKAWALIPA MAJONZI KWA MAJONZI

Aya 153-155

MAANA

(Kumbukeni) mlipotoka mbio wala hamumtizami yeyote na hali Mtume anawaita nyuma yenu.

Msemo unaelekezwa kwa wale walioshindwa siku ya Uhud naye anawakumbusha walivyowaogopa washirikina na kukimbia kwao bila ya kumwangalia yeyote, na bila ya kuitikia mwito wa Mtume(s.a.w.w) wakati alipokuwa anawaita, akiwa amesimama nyuma yao huku akisema:"Njooni enyi waja wa Mwenyezi Mungu Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu Atakayerudi Pepo ni yake"

Alifanya hivyo Mtume ili awatulize kuwa yeye yuko hai, baada ya mtu mmoja kupiga kelele kwamba Muhammad ameuawa, na nyoyo za waislamu kutaharuki.

Akawalipa majonzi kwa majonzi.

Mtume aliwaamrisha wapiga mishale wasiondoke kwenye jabali kwa hali yoyote, wakaasi na kukhalifu amri yake. Mtume(s.a.w.w) akapata majonzi kwa hilo, Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawalipa wao majonzi ya kushindwa badala ya majonzi ya Mtume.

Majonzi ya kwanza ni yale waliyoyapata Masahaba walioshindwa, na majonzi ya pili ni yale aliyoyapata Mtume.

Inasemekana kuwa majonzi yote mawili waliyapata Masahaba, na kwamba majonzi yalikuwa mengi; kama vile kuuawa ndugu zao, kushindwa na washirikina na majuto ya kuasi kwao.

Ili msihuzunike kwa mliyoyakosa,

Ambayo ni manufaa na ngawira.

Wala kwa yaliyowasibu.

Ambayo ni majeraha na kushindwa. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaonyesha uchungu wa kuuliwa na kushindwa ili mjizoeze muweze kuvumilia shida na mashaka, na kuwa na subira juu ya twa'a ya Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote itakavyokuwa natija, wala msihuzunike kutokana na kukosa ngawira au masaibu yaliyowapata. Yametangulia maelezo kwamba wapiga mishale waliacha sehemu zao kwa tamaa ya ngawira, jambo ambalo lilisababisha kushindwa kwa waislamu. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu anatanabahisha kuwa wachukue funzo kutokana na kushindwa huku na wala wasimkhalifu tena Mtume.

Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

Maana yako wazi, na makusudio ni kuhimiza twa'a na kukaripia maasi.

Kisha baada ya majonzi akawateremshia utulivu, usingizi.

Waliokuwa pamoja na Mtume siku ya Uhud wamegawanyika sehemu mbili, kuna wale waliokuwa waumini wa kweli walioona uhakika kuwa uislamu utashinda tu, na kuwa Mwenyezi Mungu ataudhihirisha kuliko dini zote, kwa vile Mtume amewaelezea hilo, Ama kushindwa katika vita moja au zaidi hakuwatoi katika uislamu. Ambao walikuwa wakiitakidi hivi ndio wanaoambiwa: 'kisha baada ya majonzi akawateremshia utulivu' - usingizi. Kulala wakati wa misukosuko ni neema kubwa inayosahihisha masaibu mengi,

Uliofunika kundi katika nyinyi.

Ni kundi hili hili tulilolitaja ambalo watu wake walikuwa na busara katika imani. Kundi la pili, katika waliokimbia siku ya Uhud, ni wanafiki ambao Mwenyezi Mungu amewataja kwa sifa hizi zifuatazo.

1). NA KUNDI JINGINE LIMESHUGHULISHWA NA NAFSI ZAO

Kundi hili halifunikwi na usingizi ili wapate mfazaiko. Wafasiri wamesema watu hao ni Abdullah bin Ubayya, Mut'ib bin Qushairy na wafuasi wao. Aya hii inafahamisha kwamba imani kamili inahitaji mtu kujishughulisha na mambo ya waislamu, asipofanya hivyo huyo ni mpungufu wa imani. Kuna Hadith isemayo: "Asiyejishughulisha na mambo ya waislamu basi si mwislamu."

2). WAKIMDHANIA MWENYEZI MUNGU DHANA YA KIJINGA ISIYO YA HAKI

Kila anayekata tamaa kwa rehma ya Mwenyezi Mungu au akamdhania Mwenyezi Mungu kwamba amefanya yasiyotakikana kuyafanya ameleta dhana ya kijinga. Miongoni mwao ni wale waliosema siku ya Uhud, kwamba Muhammad angelikuwa Mtume, asingeshindwa na washirikina, hawajui au wanajitia kutojua kuwa vita ni kushinda na kushindwa na kwamba mambo huangaliwa mwisho wake.

3). WAKISEMA: JE, TUNA CHOCHOTE KATIKA JAMBO HILI?

Yaani hatuna chochote, na Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kuwajibu kuwa hamna chochote kwa ajili yenu wala kwa mwengine, isipokuwa ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake:

"Waambie mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu"

Sisi letu ni kusikiliza na kutii tu. Aya hii iko katika mfano wa Aya ya

128 ya Sura hii.Huficha katika nafsi zao uongo na unafikiambalo hawakudhihirishii wewe kama vile kuwa wao husema,lau ingelikuwa tunalolote katika jambo hili tusingeliuliwa hapa.

Yaani, lau tungelikuwa na kitu katika jambo hili tusingelitoka kwenda kupigana, na kama tungelitoka tungelipigana vizuri bila ya kuuliwa yeyote hapa; yaani, katika Uhud.

Kauli ya wanafiki kusema: 'Je tuna chochote katika jambo hili?' Kisha kusema: 'Lau tungelikuwa na kitu katika jambo hili.' Inafanana na mtu anayesema: 'Sina pesa, lau ningelikuwa nazo ningelifanya hivi na hivi.'

Waambie lau mngelikuwa nyumbani mwenu wangetoka ambao wameandikiwa kuuawa wakaenda katika maangamivu yao.

Hili ni jibu la aliyesema: 'Lau tungelikuwa na kitu tusingeliuawa.' Njia ya majibu ni kwamba, hadhari haiondoi kadari na kwamba mpangilio hauzuwii makadirio, ni sawa jambo la vita liwe lenu au lisiwe, Umekwisha tangulia ufafanuzi katika kufasiri Aya ya 145 ya Sura hii, kifungu 'Ajali imeandikwa.'

Na ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu na ayasafishe yaliyomo nyoyoni mwenu, Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani.

Hekima ya janga la siku ya Uhud ni upambanuzi wa kutambua mumin na mnafiki na kudhihirisha hakika yao kwa watubiao kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyo katika nyoyo. Kwa hivyo, mu'min anazidi imani kwa misukosuko na vile vile kwa malipo na thawabu, Na mnafiki anafichuka.

SIRI YA KUSHINDWA

Zaidi ya hayo yote ni kwamba lau mtu angeliishi maisha yake yote bila ya matatatizo na shida yoyote, ingelikuwa ni jambo la kushangaza katika akili za watu. Matatizo ndiyo yasafishayo nafsi na kuzikomaza, na kuvumilia shida kunamfikisha mtu kwenye malengo yake. Uzoefu umeonyesha kuwa hakuna mpinganaji yoyote au mwanasiasa, mfanya biashara, mwanachuoni, mwana fasihi, mfanyi kazi, au mkulima, aliyefanikiwa katika malengo yake, isipokuwa kwa uthabiti na kuvumilia shida. Lau tutafanya utafiti ili tujue siri ya kutofaulu katika maisha, tutaona kuwa ni udhaifu, kuhofia urefu wa njia na kutovumilia tabu na matatizo. Nayasema haya nikiwa mimi mwenyewe nimefanya majaribio kutokana na uvumilivu nimefikia ambayo sikuwa hata nikiyaota Al-hamdulillah. Nimejaribu nikawa na yakini kuwa subira inafanya miujiza na kwamba werevu bila ya subira na uvumilivu haufai chochote.

Hakika wale waliogeuka siku yalipokutana makundi mawili, shetani ndiye aliyewatelezesha kwa sababu ya baadhi ya waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu amekwishawasamehe; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, mpole .

Wengi wamesema kuwa Aya hii inawahusu wapiga mishale walioamrishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) wabakie sehemu zao ili kuwakinga waumini kwa upande wa nyuma, kisha wakaondoka wakidhania kuwa washirikina wameshindwa. Lakini Aya haikuwataja wapiga mishale na wengineo walioshindwa siku ya Uhud. Hata hivyo kuenea kwake kunahusu waumini na wala si kwa wanafiki, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, amekwisha wasamehe kwa sababu Mwenyezi Mungu hawasamehi wanafiki wananong'ania unafiki wao ambao ni mbaya zaidi kuliko ushirikina wa waziwazi. Kwa ufupi ni kwamba aliyeshindwa siku ya Uhud hana shaka na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, isipokuwa alikimbia ama kwa tamaa au kutokua na subira na mshikamano, na mengineyo ambayo hawezi kujiepusha nayo asiyekuwa Masum, na ambayo hayana mfungamano na unafiki au shaka yoyote. Haya aliyasamehe Mwenyezi Mungu, hata kama ndiyo yaliyoleta yaliyotokea. Imesemekana kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu: Shetani ndiye aliyewatelezesha, kwa baadhi ya waliyoyafanya; ni kwamba Shetani aliweza kuwatelezesha kwa sababu ya dhambi walizozifanya kabla ya Uhud. Lakini haya ni kiasi cha kudhani tu. Lililo karibu zaidi ni kwamba kufanya, hapa ni ishara ya pupa yao na kutokuwa na subira. Shetani alipoona hivi akaitumia nafasi na kuwahadaa kuwa wameshinda na kuwapofua kuwa mambo ni salama. Na wafasiri wote, watu wa sera na historia wameafikiana kuwa Imam Ali bin Abu Talib(a.s) alikuwa ni mmoja wa waliobaki bila ya kukimbia.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ كَفَرُوا وَقَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ إِذَا ضَرَبُوا فِي الْأَرْضِ أَوْ كَانُوا غُزًّى لَّوْ كَانُوا عِندَنَا مَا مَاتُوا وَمَا قُتِلُوا لِيَجْعَلَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ حَسْرَةً فِي قُلُوبِهِمْ وَاللَّـهُ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴾

156.Enyi mlioamini msiwe kama wale waliokufuru na wakawasema ndugu zao, waliposafiri katika nchi au walipokuwa vitani: lau wangelikuwa kwetu wasingekufa na wasingeliuawa; ili Mwenyezi Mungu ayafanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu anahuisha na kufisha na Mwenyezi Mungu anaona mnayoyatenda.

﴿وَلَئِن قُتِلْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَوْ مُتُّمْ لَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَحْمَةٌ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴾

157.Na kama mkiuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkifa, basi maghufira na rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

﴿وَلَئِن مُّتُّمْ أَوْ قُتِلْتُمْ لَإِلَى اللَّـهِ تُحْشَرُونَ﴾

158.Na kama mkifa au mkiuawa, nyote mtakusanywa kwa Mwenyezi Mungu.

MSIWE KAMA WALE WALIOKUFURU

Aya 156-158

MAANA

Enyi mlioamini msiwe kama wale waliokufuru.

Tamko la ambao wamekufuru, ni la kiujumla, linamkusanya kila kafiri; awe mnafiki au kafiri wa wazi wazi, bali wafasiri wengi wamesema; makusudio hasa ni wanafiki,

Na wakawasema ndugu zao.

Yaani: walisema waliyoyasema kwa ajili ya ndugu zao waliokufa.

Waliposafiri katika nchi au walipokuwa vitani; lau wangelikuwa kwetu wasingelikufa na wasingeliuawa.

Wanafiki walikuwa wakiyategemeza mauti ya msafiri kwenye safari na yule mwenye kuuawa vitani kwenye vita hivyo, sio kwa kuwa yameandikwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amewakataza waumini kusema mfano wa maneno haya. Kwa sababu ndani yake mna kuitikia mwito wa hadaa za wanafiki na matamanio yao. Ikiwa hawatayasema hayo na kuyategemeza mauti ya anayekufa safarini au vitani kwa Mwenyezi Mungu, basi watakuwa wamevipinga vitimbi vya wanafiki kwao wenyewe na kuwapatisha hasara. Makusudio ya udugu hapa ni kiujumla, yaani ndugu wa nasaba au kushabihiana katika itikadi na tabia.

Ili Mwenyezi Mungu ayafanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao

Yaani, Mwenyezi Mungu amewakataza waumini kujifananisha na wanafiki kwa kauli na vitendo. Kwa sababu kujifananisha huku kunawafurahisha na kunathibitisha makusudio yao. Na kukosa kufanya hivyo kunawasumbua na kuwakasirisha.

Na Mwenyezi Mungu anahuisha na kufisha.

Ajali zote ziko kwenye uwezo wake, wala si kwa sababu ya vita au safari. Kwani anaweza kusalimika na yule aliyekaa mjini akafa. Hili ndilo jibu la kauli ya wanafiki, kuwa safari na vita vinasababisha mauti.

Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda

Hili ni himizo la kumtii Mwenyezi Mungu na ni tishio la anayewaiga makafiri na wanafiki kwa kauli na vitendo.

Na kama mkiuliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkifa basi maghufira na rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

Kila mwenye kuipigania haki au nafsi yake kwa upanga wake au kalamu yake au ulimi wake na akauawa, basi ameuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Vilevile kupigania maisha na elimu au chochote kinachowafaa watu na akafa, basi amekufa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na kila mwenye kufa au kuuawa, katika njia ya Mwenyezi Mungu amewajibikiwa kusamehewa dhambi na kupanda daraja katika dunia na akhera. Kauli yake Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yale wanayoyakusanya ni kwamba lililo bora kwa mumini ni kuathirika na linalodumu kuliko linaloisha ambalo ni starehe na anasa.

Na kama mkifa au mkiuawa, nyote mtakusanywa kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ndio mwisho wa binadamu awe amefariki dunia kwa kuuawa au kwa sababu yoyote ile. Hapo ndipo penye malipo ya (matendo) yaliyopita, ikiwa kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari. Mwenye akili anajiandaa na siku hii wala hawezi kufanya mchezo.

﴿فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَوَكِّلِينَ﴾

159. Kwa sababu ya rehma itokayo kwa Mwenyezi Mungu, umekuwa mpole kwao, lau ungelikuwa mkali mwenye moyo mgumu bila shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe na uwaombee maghfira na ushauriane nao katika mambo, Utakapoazimia, basi mtegemee Mwenyezi Mungu, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wamtegemeao.

﴿إِن يَنصُرْكُمُ اللَّـهُ فَلَا غَالِبَ لَكُمْ وَإِن يَخْذُلْكُمْ فَمَن ذَا الَّذِي يَنصُرُكُم مِّن بَعْدِهِ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴾

160.Akiwasaidia Mwenyezi Mungu hapana wa kuwashinda. Na kama akiwaacha basi ni nani atakayewasaidia baada yake? Na wategemee kwa Mwenyezi Mungu waumini.

KAMA UNGEKUWA MKALI

Aya 159-160

MAANA

Kwa sababu ya rehma itokayo kwa Mwenyezi Mungu, umekuwa mpole kwao.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu alikuwa akiwambia Masahaba wa Mtume(s.a.w.w) ; katika Aya hizi, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake mtukufu(s.a.w.w) . Yametangulia maelezo kwamba Waislamu walikwenda kinyume na amri ya Mtume(s.a.w.w) siku ya vita vya Uhud, na natija ilikuwa ni kushindwa wakamwacha Mtume kwenye shida, ambapo vita iliuma mchanga mpaka Mtume akajeruhiwa na maadui, akavunjwa meno ya mbele, ukachanika uso wake na ukawa unachuruzika damu. Wakati huo akiwa bado na uthabiti pamoja na watu wachache, akaita wale wanaokimbia lakini wasimwitike. Baada ya kwisha vita waislamu walirudi kwa Mtume(s.a.w.w) , lakini Mtume hakuwalaumu ingawaje walikuwa wakistahili hivyo. Bali aliyapuuza, akawapokea na akazungumza nao kwa upole. Haukuwa upole huu ila ni rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ikiwa Mwenyezi Mungu amemsifu Mtume wake kuwa ni mvunja ghadhabu kwa watu wake pamoja na ubaya wao, basi itakuwa yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu ni zaidi. Imam Ali anasema, katika kumsifu Mwenyezi Mungu: "Ghadhabu haimshughulishi kuwacha rehma yake." Na katika dua zilizopokewa imesemwa: "Ewe ambaye rehma yake imetangulia ghadhabu yake."

Kisha Mwenyezi Mungu anabainisha hikma ya upole kwa Mtume wake mtukufu kwa kusema:

Lau ungelikuwa mkali mwenye moyo mgumu bila shaka wangelikukimbia , na maadui wangelikucheka na ujumbe kwako usingelitimu na kuenea. Kwa hakika makusudio ya kutumwa Mtume ni, kuongoza viumbe kwenye haki, nao viumbe hawawezi kumsikiliza isipokuwa yule mwenye upendo ambaye nafsi zao zinamtegemea, na nafsi haitegemei isipokuwa kwa aliye na moyo rahim; kama moyo wa Muhammad(s.a.w.w) ambao ulikunjuka kwa watu wote hata kwa wanyama. Alisema kuhusu wanyama: "mnapochinja chinjeni vizuri, anoe mmoja wenu kisu chake na ampe raha anayemchinja" Akasema tena: "Kuna malipo katika kumhudumia kila mwenye ini la joto. "Hakika Mwenyezi Mungu alimsamehe Mumis kwa sababu alimwokoa mbwa asife na kiu"

Basi wasamehe katika mambo yanayokuhusu wewe ambapo walikuacha wakati wa dhiki na shida mpaka ukajeruhiwa.Na uwaombee maghufira katika haki inayomhusu Mungu Mtukufu pale walipomwasi na kuacha vita. Kauli yake hii Mwenyezi Mungu inafahamisha kimaana kuwa Yeye amekwisha wasamehe na kuwaghufuria, vyenginevyo asingemwamrisha Mtume wake hilo.

Na ushauriane nao katika mambo.

Arrazi anasema: Maulama wengi wamesema kuwa alif na lam hapa sio ya kijumla bali ni mahsusi tu, na kilichohusishwa katika Aya hii ni vita na kupambana na maadui. Kwa hivyo ushauri unahusika na vitu tu." wengine wakasema kuwa inakusanya mambo yote ya kidunia. Kisha Razi akimnukuu Shafi anasema; kuwa mshawara hapa ni mapendekezo, sio wajibu, na kwamba hekima ya ushauri ni kuzituliza nyoyo zao tu. Kauli hii iko karibu na uzingatio. Kwa sababu, Maasum hawezi kutaka mwongozo kwa asiyekuwa Maasum.

Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba dini kwa itikadi yake na sharia yake ni wahyi bila ya kuweko rai ya yeyote, hata Mtume mwenyewe ni mfikishaji tu na wala sio mtunga sharia. Na Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume wake: "Huna lako jambo.." (3:128) "Wewe ni muonyaji tu."(79:45).

Utakapoazimia, basi mtegemee Mwenyezi Mungu.

Yaani ukiazimia kufanya jambo kutokana na ushauri au usiokuwa ushauri, basi litekeleze kwa kufanya maandalizi kwa kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu katika kufaulu na kushinda.

Akiwasaidia Mwenyezi Mungu, hapana wa kuwashinda.

Msaada wake Mwenyezi Mungu Mtukufu unakuwa pamoja na kutekeleza sababu alizozijaalia Mwenyezi Mungu kuwa ni njia ya kufikia ushindi, ambazo pamoja na kumtegemea Mwenyezi Mungu, ni kukamilika maandalizi ambako Mwenyezi Mungu amekudokeza pale aliposema:"Na waandalieni nguvu muwezavyo" (8:60)

Na kama akiwaacha ni nani tena atakayewasaidia baada yake?

Mwenyezi Mungu huwaacha wale ambao hawana mjumuiko wa kheri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

"Wala msizozane, msije mkalegea na kupoteza nguvu zenu" (8:46) Kwa ufupi ni kwamba kukamilisha maandalizi bila ya ikhlas hakuna faida yoyote, kama ilivyokuwa kwa Waislamu siku ya vita vya Hunain:

﴿وَيَوْمَ حُنَيْنٍ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُم مُّدْبِرِينَ ﴾

"Na siku ya Hunain, ulipowapandisha kichwa wingi wenu, lakini haukuwafaa kitu, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawaje ni pana, kisha mkageuka mkarudi nyuma." (9:25)

Kama ambavyo ikhlas nayo bila ya maandalizi haifai kitu, Mwenye kutekeleza yote mawili (maandalizi na kumtegemea Mwenyezi Mungu), basi hana wa kumshinda. Kwa sababu Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye; "panga na utawakali"

SIRI YA UTUKUFU WA MUHAMMAD

Abdullah, baba yake Mtume, alisafiri kwenda Sham (Syria ya sasa) kibiashara wakati mama yake akiwa na mimba yake. Katika safari ya kurudi, Abdullah aliwapitia wajomba zake wa ukoo wa Najjar waliokuwa Madina, akaugua huko na kufariki. Kwa hivyo akafariki akiwa fakiri bila ya kumwachia mwanawe kitu chochote zaidi ya ngamia watano, kondoo wachache na mjakazi wa kihabeshi aliyekuwa akiitwa Ummu Ayman ambaye alikuwa ni mmoja kati ya walezi wake. Mtume(s.a.w.w) alizaliwa Makka mwezi wa Rabi-ul-Awwal (mfungo sita), mwaka wa ndovu, sawa na mwezi wa Agosti 570 A.D. kama ilivyotajwa.

KUNYONYESHWA KWAKE NA MALEZI YAKE

Mtume alinyoyeshwa na Thuwayba kisha akanyonyweshwa na Halima Saadiya. Mama yake alifariki akiwa na miaka 6 na babu yake alifariki akiwa na miaka 8. Kisha akalelewa na ami yake, Abu Talib na akamkinga hadi pumzi yake ya mwisho. Aliishi naye miaka 42. Mtume aliishi miaka 63 ambayo 53 aliimalizia Makka na 10 Madina.

WASIFU

Kiumbo alikuwa si mrefu si mfupi, alikuwa na kichwa kipana. Uso wa duara na mpana. Nyusi zake zilikuwa ziko karibu kuungana, katikati yake palijitokeza mshipa, ambao anapokasirika hufura na kuwa mwekundu. Vilevile alikuwa na macho meusi na kope ndefu. Pua iliyochongoka, mwenye meno mazuri, ndevu nyingi na kifua kipana. Pia alikuwa na mikono mirefu, na alikuwa na weupe uliochanganyika na wekundu, na alikuwa na mwili mkakamavu. Akasirikapo, uso wake huiva na anapohuzunika mara nyingi hushika ndevu zake. Alipokuwa akizungumza huashiria kwa kiganja chake chote na anapostaajabu hukigeuza. Anapozama katika mazungumzo hupiga dole lake gumba la kushoto kwenye kiganja chake cha kulia. Akiona jambo linalomchukiza alikuwa akigeuza uso wake na anapochemua (kupiga chafya) hujifunika. Alikuwa akicheka mpaka yakaonekana magego yake na alikuwa mwingi wa tabasamu.

Alikuwa hakatai chakula kinachopatikana wala hakalifishi kinachokosekana, Na kama hapati chakula, huvumilia mpaka kufikia hatua ya kufunga jiwe tumboni mwake kwa sababu ya njaa, Alikuwa anaweza kukaa mwezi mzima bila ya kupata mkate. Siku moja alimtuma mtu kwenda kumkopea kwa myahudi mmoja, yule myahudi akakataa na akasema: "Muhammad hana shamba wala mifugo, ni nani atakayelipa?" Vilevile Mtume hakuwa na kanzu, juba au shuka zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Pia hakuwa na viatu zaidi ya jozi moja. Alikuwa na mkeka anaoulalia usiku na kuukalia mchana, mpaka akafanya alama mbavuni. Na alikuwa na mto wa ngozi uliojazwa ndifu. Wakati wa kulala alikuwa akiweka mkono wake chini ya shavu lake na hulalia upande wake wa kulia. Alikuwa akijishonea viatu na kanzu yake inapopasuka, na alikuwa akipanda punda. Ingawaje utajiri wa Bara-arabu ulikuwa kwenye madaraka yake lakini alikuwa akitoa kila kinachomfikia akiwa ni mtu asiyeogopa ufukara, kama alivyosifiwa na bedui mmoja.

MTUME NA UFUKARA

Lakini yote hayo hayana maana kwamba yeye alikuwa akiupenda ufukara na kuuridhia. Hapana! Bali alikuwa akiomba kuhifadhiwa nao na akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Ninataka hifadhi kwako kutokana na ufukara, uchache wa mali na udhalili. Na ninataka hifadhi kwako na kushindwa na uvivu. Na ninataka hifadhi na kudhulumu au kudhulumiwa" Mtume hakuwa akiupenda ufukara na kuuridhia, lakini maadamu alikuwa akiishi katika jamii fakiri, basi njia bora ni kuishi upande wa ufakiri na kuwa sawa nao katika ulaji, mavazi na mahali pa kuishi. Wala hakuna kosa kubwa na dhulma kuliko kuwa kiongozi ameshiba na raia wake mmoja ana njaa. Amirul-Muminiin Ali anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu amewafaradhishia Maimamu waadilifu kujipima kwa kuwa sawa na watu ili maumivu ya ufukara yasimwathiri yakammaliza." Amesema tena: "Je, nitosheke kuitwa Amirul-Mu'miniin (Kiongozi wa Waumini) na wala sishirikiani nao katika hali ngumu ya maisha."

UTARATIBU WA MWITO WAKE

Kwanza aliwaonya jamaa zake walio karibu, Hapo ni wakati iliposhuka Aya:"Na waonye jamaa zako walio karibu." (26:214) Basi akawafanyia chakula na akawaalika. Miongoni mwa maneno aliyowaambia ni, "Ni nani atakayekuwa msaidizi wangu katika jambo hili, awe ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu?" wote wakanyamaa isipokuwa Ali bin Abu Talib aliyesema: "Mimi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Basi akamshika shingoni kwake akasema: "Huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu, kwa hiyo msikilizeni na mumtii." Watu wakanyanyuka huku wakicheka na kumwambia Abu Talib: "Umeamrishwa umsikilize na umtii mwanao mwenyewe!" Kisha Mtume akawalingania watu wake - Waarabu, kisha akamlingania kila mtu wa mwanzo hadi wa mwisho. Mwenyezi Mungu anasema;"Na hatukukutuma ila kwa watu wote" (34: 28) Ama Mitume wengine walipelekwa kwa watu wao tu au watu wa zama zao tu. Ndio maana Nuh, Ibrahim, Hud, Swaleh, Musa na wengineo, walikuwa wakiwaambia watu wanaowalingania kwenye imani kwa kutumia neno: "Enyi watu wangu." Ama Muhammad(s.a.w.w) aliwaambia watu wote wa kila zama na kila miji, wa aina tofauti na lugha tofauti, kwa kusema:"Enyi watu! Mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu nyote." (7: 158) Pia Mtume aliwaandikia barua wafalme wa duniani, akiwemo Kisra na Kaizari na akawatumia ujumbe wake akiwalingania kwenye imani kuhusu risala yake.

SIRI YA UTUKUFU WAKE

Muhammad(s.a.w.w) alikuwa ni mwanaadamu; yeyote atakayemsifu kwa sifa ya muumbaji, mwenye kuruzuku, basi atakuwa amemkufuru Mwenyezi Mungu. Lakini watu wote kuanzia Adam mpaka mtoto wake wa mwisho, sio kama Muhammad, mtukufu zaidi katika wao, ni yule atakayethibitishwa utukufu na ubora wake na Muhammad. Ni sawa awe amethibitishiwa kwa nukuu na kuelezwa jina au kwa sifa ya kijumla, kama kusema: mbora wa watu ni yule anayewanufaisha zaidi watu. Ama siri ya utukufu wa Muhammad ni kwamba yeye alikuwa akibeba matatizo ya watu wote. Alikuwa pamoja na mayatima na wajane na kuwatekelezea mahitaji yao. Hakuna yeyote awe rafiki au adui ila atamshughulikia na kumhurumia, kumpa usaidizi. Maneno yangu haya hayatokani na ushabiki au malezi na mazingira la! Bali yanatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:"Na hatukukutuma wewe ila ni rehma kwa viumbe." (21:107) Maana yake ni kuwa huruma zake, na kushughulikia kwake watu hakuko kwa jamaa zake, au marafiki zake tu bali kumeenea kwa watu wote, maadui na marafiTafsir ki, kama maji na hewa. Watu walimvunja meno, wakamjeruhi uso, lakini alisema: "Ewe Mwenyezi Mungu waongoze watu wangu hakika wao hawajui." Hakutosheka kuwaombea uongofu lakini aliwatakia udhuru kwa ujinga wao na kutofahamu.

Hakuna ajabu ikiwa Muhammad hakukasirika kwa ajili ya nafsi yake au kuzuia nafsi yake na anasa za dunia, isipokuwa ajabu ni kufanya kinyume na hivyo. Tabia hiyo ni lazima kwa yule aliyepelekwa kwa ajili ya kutimiza tabia tukufu na kuwalingania watu wote kumsadikisha na kuamini risala yake. Wala hakuna maana ya kusadikisha isipokuwa kusadikisha uadilifu na wema, wala kumwamini yeye isipokuwa kuamini haki na utu, sio yeye mwenyewe. Siku moja mtu mmoja alimwita hivi: "Ewe bwana wetu, mtoto wa bwana wetu, Mbora wetu na mtoto wa mbora wetu!" Mtume akasema: "Asiwachezee shetani, mimi ni Muhammad mja wa Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, Wallahi sipendi wanitukuze zaidi ya cheo changu." Masahaba zake walikuwa wanapomuona hawamsimamii ingawaje ni kipenzi chao, kwa sababu walikuwa wanajua kuwa hapendi kusimamiwa. Pia alikuwa akichukia kutembea na mtu akiwa nyuma yake, hivyo humshika mkono na kumvuta ubavuni mwake ili watembee pamoja, Hii ndiyo hulka ya Muhammad(s.a.w.w) . Ndio ni kweli kuwa watu wote si kama yeye, lakini hulka zake ndio kioo cha hakika ya uislamu. Yeyote mwenye kulingania uislamu na asifuate mwendo wa Mtume wake, basi ni mdanganyifu, ni sawa atambue hivyo au asitambue au hata akijiona, na watu wakimwona yeye ni mtukufu zaidi.

﴿وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَغُلَّ وَمَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴾

161.Na Mtume hawezi kufanya hiyana. Na mwenye kufanya hiyana, atayaleta yale aliyoyafanyia hiyana siku ya kiyama, kisha italipwa kila nafsi iliyoyachuma, wala hawatadhulumiwa.

﴿أَفَمَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَ اللَّـهِ كَمَن بَاءَ بِسَخَطٍ مِّنَ اللَّـهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴾

162.Je, aliyefuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungu ni kama aliyestahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na makazi yake ni jahannam. Hapo ni mahali pabaya pa kurejea.

﴿هُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِمَا يَعْمَلُونَ﴾

163.Wao wana daraja mbele ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyaona yale wanayoyafanya

﴿لَقَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ﴾

164.Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao, anayewasomea Aya zake na anayewatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima. Na hakika kabla ya hapo walikuwa katika upotofu wa dhahiri.

MTUME HAFANYI HIYANA

Aya 161-164

MAANA

Na Mtume hawezi kufanya hiyana.

Imesomwa herufi 'ya' kwa fataha kwa mweko wa fail (mtendaji) kwa maana ya kuwa Mtume hafanyi hiyana katika ghanima na vinginevyo kama wanavyodhani wajinga. Pia imesomwa kwa dhumma, kwa mweko wa maful (mtendwa), kwa maana ya kuwa haifai kwa yeyote kumhini Mtume katika ghanima. Katika tafsir nyingi, imeelezwa kuwa lililowafanya watu wa kikosi cha mishale kuondoka sehemu yao kuiacha tupu ngome ya nyuma ya waislamu siku ya vita vya Uhud, ni kuwa wao walihofia kuwa Mtume hatawagawia ghanima, wakifikiria kuwa anayechukuwa kitu basi ni chake. Mtume akawaambia: "Hivi mwadhani kuwa sisi twafanya hiyana? Ndipo ikashuka Aya. Tamko la Aya halikatai maana haya, hata mfumo wa Aya pia unakubali, kwa sababu bado ni katika tukio la Uhud. Vyovyote iwavyo, lile ambalo tunalifahamu kwa ujumla, bila ya kuangalia sababu za kushuka, ni kwamba Ma'asum hawezi kufanya hiyana, kwa sababu ni mkweli, kwa kuwa yeye ni mkweli, hawezi kusema uongo, isipokuwa kama sio mkweli, na tamu ni tamu tu, haiwezi kuwa chungu isipokuwa kama utaviita vitu kwa kinyume, jambo ambalo linabatilisha upimaji wa mambo.

Na mwenye kufanya hiyana, atayaleta yale aliyoyafanyia hiyana siku ya kiyama, kisha italipwa kila nafsi iliyoyachuma.

Yaani, mwenye kufanya hiyana na kuiba kitu kesho (siku ya kiyama) atakuja na dhambi ya alivyovifanyia hiyana na atapata aliyoyachuma bila ya kupungua chochote na atafedheheka mbele ya watu wote. Imesemekana pia kuwa atakuja na kitu chenyewe kilichoibwa, Kwa mfano mwenye kuiba ngamia, siku ya kiyama atakuja amebeba ngamia shingoni mwake. Hayo yamesemwa kwa kutegemezwa kwenye Hadith ndefu ya Mtume(s.a.w.w) Kama Hadith itakuwa sahih, basi itakuwa ni fumbo la kubeba madhambi ya maasi, sio kuchukua kitu chenyewe hasa. Na Aya hii iko katika mwelekeo wa Aya isemayo:

﴿ مَن يَعْمَلْ سُوءًا يُجْزَ بِهِ وَلَا يَجِدْ لَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴾

"Mwenye kutenda uovu atalipwa kwa uovu huo, wala hatapata asiyekuwa Mwenyezi Mungu wa kumlinda wala wa kumsaidia" (4:123)

UISLAMU UNAFANYA MAAJABU

Mwenye kufuatilia historia ya uislamu, ataona kwamba mafunzo ya Qur'an na Hadith yamefanya kazi yake na kuathiri katika nafsi za waislamu wengi, mpaka yakatokea makundi yanayoendelea na hulka njema, ambazo Mtume ametumwa kuzitimiza. Mwanajeshi wa kiislamu wa kawaida anaweza kupata nyara yenye thamani kubwa kutoka kwa adui na akaileta kwenye hazina ya waislamu bila ya kuhisi chochote rohoni mwake. Ibn Athir katika Tarikh anasema: Waislamu walipoteka Madain, kamanda wa jeshi alikuwa Saad bin Abi Waqqas. Yeye alimweka Saad bin Umar bin Muqrin kukusanya nyara na ngawira akawa yeye ndiye anayekabidhiwa. Mwanajeshi mmoja akamjia na sanamu mbili ili azichanganye kwenye ngawira. Moja ilikuwa ni farasi wa dhahabu aliyepambwa kwa zumaridi na yakuti na juu yake kuna mtu aliyevishwa taji la johari. Sanamu ya pili ilikuwa ni ya ngamia wa fedha aliyepambwa kwa yakuti akiwa na lijamu ya dhahabu iliyozungushwa johari. Hizi zilikuwa sanamu za Kisra alizokuwa akiziweka kwenye taji lake.

Yule anayekusanya mali alipoziona, alishikwa na mshangao akasema: "Hatujaona kitu kama hiki, mali yote tuliyonayo haifikii hii hata haikaribii pia." Kisha akamuuliza yule askari: "Wewe ni nani?" akasema: "Sikwambii wala simwambii yeyote asije akanisifu, lakini mimi namsifu Mwenyezi Mungu peke yake, nataraji thawabu zake na wala sitaki kitu kingine zaidi yake" Kisha akajiondokea. Yule mkabidhiwa akamfuatafuata na kumuuliza kwa watu mpaka akamjua kuwa ni Amir bin Abdu Qays.

Masimulizi haya unaweza kuyaona kama ngano tu, lakini Uislamu ukipata moyo mwema, basi hufanya maajabu sawa na ilivyo mbegu bora ya rutuba katika ardhi. Ama ardhi isiyo na rutuba haileti mazao bora, hata kama mbegu bora na mvua ikawa nyingi, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا﴾

"Na nchi nzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake na nchi mbaya haitoi ila kwa taabu" (7:58)

Je, aliyefuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungu ni kama aliyestahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na makazi yake ni Jahannam. Hapo ni mahali pa baya pa kurejea.

Aya hii inafanana na ile isemayo:

﴿أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ﴾

"Je, tuwajaalie wale walioamini na wakatenda amali njema kuwa sawa na wafanyao uharibifu katika ardhi…"? (38:28)

Amirul Mu'minin Ali(a.s) anasema: "Kuna tofauti kubwa kati ya amali mbili, amali ambayo inaondoka na kubaki taabu yake, na amali ambayo taabu yake inaondoka na kubaki malipo yake" Anaendelea kusema:"Haki ni nzito lakini ni nzuri na batili ni hafifu lakini ni balaa. Ni mwisho gani mbaya kuliko ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu ya moto"

Wao wana daraja mbele ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyaona yale wanayoyafanya, Dhamir ya wao inawarudia wenye kufuata ya kumridhisha Mungu.

Maana yake ni kuwa watiifu wanatofautiana katika twa'a kati ya wale, wanaopigana jihadi wao wenyewe na wale waliokaa wasiokuwa na madhara. Vilevile waasi wanatofautiana katika maasi na katika makosa. Kwa hivyo ikawajibika hawa kutofautiana adhabu na wale katika thawabu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumin kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao anayewasomea Aya zake na anayewatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima. Na hakika kabla ya hapo walikuwa katika upotofu wa dhahiri.Umepita mfano wa Aya hii katika Sura ya Baqara Aya 129.

Kwa hali yoyote ile ni kwamba Aya hii imekusanya mambo yafuatayo:

1) Mtume ni hisani kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa viumbe; Kwa sababu Mtume huwatoa ujingani kuwapeleka kwenye ujuzi, kutoka kwenye udhalili kwenda kwenye utukufu na kutoka kwenye maasi na adhabu kwenda kwenye twa'a na thawabu.

2) Hisani hii imezidi kwa Waarabu hasa kwa sababu Muhammad(s.a.w.w) anatokana nao, wanajifaharisha naye kwa umma zote.

3) Yeye amewatakasa na uchafu wa shirk, masanamu, vigano, uzushi, kuiga kunakodhuru na ada mbaya.

4) Anawafundisha Kitabu, yaani Qur'an ambayo imewapa umoja, kuhifadhi lugha yao na kuwahimiza elimu, na tabia njema. Vilevile Mtume amewafundisha hekima, ambayo ni kuweka mambo mahali pake. Inasemekana kuwa makusudio ya hekima ni Fiqh.

5) Tafsir bora ya Aya hii ni yale maneno aliyoyasema Jafer bin Abu Talib kumwambia Najash wa Uhabesh, "Ewe mfalme, sisi tulikuwa ni watu wajinga, tukiabudu masanamu, tukila nyamafu na kufanya mambo mabaya. Vilevile tulikuwa wavunja undugu, kumfanyia ubaya jirani, na mwenye nguvu alikuwa akimwonea mnyonge. Tulikuwa hali hiyo mpaka Mwenyezi Mungu akatuletea Mtume atokanaye na sisi. Tunayemjua nasaba yake, ukweli wake, uaminifu wake na usafi wake. Akatulingania kwa Mungu mmoja peke Yake. Tukavua yale tuliyokuwa tukiyaabudu sisi na baba zetu, miongoni mwa mawe na masanamu. Akatuamrisha kusema kweli, kutekeleza amana, kuunga udugu, kumfanyia wema jirani na kujizuiliya na mambo ya haramu na kumwaga damu. Vilevile alitukataza mambo maovu, kuzulia, kula mali ya yatima na kuwatusi wanawake wanaojistahi. Na akatuamrisha kumwabudu Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote. Pia akatuamrisha kuswali, kutoa zaka na kufunga" Kwa ufupi Muhammad(s.a.w.w) ndiye aliyeleta maendeleo kwa waarabu ya kiutu na ya kimataifa, lau si yeye waarabu wasingekuwa na historia yoyote wala jambo lolote la kutambuliwa.