TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17416
Pakua: 3830


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17416 / Pakua: 3830
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

﴿الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ عَهِدَ إِلَيْنَا أَلَّا نُؤْمِنَ لِرَسُولٍ حَتَّىٰ يَأْتِيَنَا بِقُرْبَانٍ تَأْكُلُهُ النَّارُ قُلْ قَدْ جَاءَكُمْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِي بِالْبَيِّنَاتِ وَبِالَّذِي قُلْتُمْ فَلِمَ قَتَلْتُمُوهُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴾

183.Wale ambao wamesema: Hakika Mwenyezi Mungu ametuahidi kuwa tusimwamini Mtume yeyote, mpaka atuletee kafara itakayoliwa na moto. Sema: Hakika waliwajia Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo waziwazi na kwa hayo mliyosema basi mbona mliwaua kama mu wa kweli?

﴿فَإِن كَذَّبُوكَ فَقَدْ كُذِّبَ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ جَاءُوا بِالْبَيِّنَاتِ وَالزُّبُرِ وَالْكِتَابِ الْمُنِيرِ﴾

184.Kama wakikukadhibisha, basi hakika wamekadhibishwa Mitume kabla yako waliokuja na hoja waziwazi na vitabu vya waadhi na kitabu chenye mwanga.

KAFARA NA MOTO

Aya 183-184

MAANA

Wale ambao wamesema: Hakika Mwenyezi Mungu ametuahidi kuwa tusimwamini Mtume yeyote, mpaka atuletee kafara itakayoliwa na moto.

Kila mwongo anadai kuwa ni mkweli, na anaupamba uongo wake kwa uzushi na tuhuma, hata wale wanaotajirika kwa vita na kuvichochea ili viwanda vyao vifanye kazi, wanadai kuwa wanawaua watu wasio na makosa, watoto na wanawake ili kuleta amani. Haya ndiyo mantiki ya kila mpinga haki na uadilifu kwa kuhofia chumo lake na manufaa yake. Kwa hiyo hakuna geni kwa Mayahudi kumzulia Mwenyezi Mungu na kumwambia Muhammad(s.a.w.w) kuwa hatukuamini, kwa sababu Mwenyezi Mungu ametuamrisha kutomsadiki anayedai Utume mpaka atuonyeshe muujiza wa kutoa kafara yetu na iteketezwe na moto utokao mbinguni. Na Mayahudi waliomwambia Muhammad kauli hii, ndio hao hao waliosema kufuru ya kuwa Mwenyezi Mungu ni fukara na wao ni matajiri.

Sema: Hakika waliwajia Mitume kabla yangu kwa hoja waziwazi na kwa hayo mliyosema basi mbona mliwaua kama mu wa kweli?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwamrisha Mtume wake Mtukufu kuwakatalia maneno yao na kuwajibu kwa matukio ya kihistoria kwa kuwaambia, wakale wenu waliwataka Mitume waliotangulia muujiza huu muutakao nyinyi, wa kushuka moto kutoka mbinguni, akaudhihirisha Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo hawakuwaamini, bali waliwaua. Na nyinyi mko radhi na vitendo vya wa kale wenu. Walivyokuwa wao ndiyo mlivyo nyinyi kwa inadi. Lau mngelikuwa mwatafuta ukweli, mngelimwamini Muhammad(s.a.w.w) baada ya kuwaletea hoja ya Utume wake.

Kama wakikukadhibisha, basi hakika wamekadhibishwa Mitume kabla yako waliokuja na hoja zilizo wazi wazi na vitabu vya waadhi na kitabu chenye mwanga.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume Mtukufu(s.a.w.w) , lengo lake ni kumpa moyo kwa masaibu yaliyowapata wenzake waliotangulia. Sera yao ilikuwa ni kukabiliana na kupingwa na wenye inadi katika watu waovu, kama wana wa Israil na wanaofanana nao, hata ingawaje walionyesha hoja kwa kila mkadhibishaji na mpinga haki. Makusudio ya hoja zilizo waziwazi ni miujiza iliyo wazi inayofahamisha ukweli wa waadhi; mawaidha ya Mtume na hekima zao, na kitabu chenye mwanga ni Tawrat, kwa yanayomuhusu Muhammad na sifa zake. Na kwa kuwa Aya zilikuwa zikibainisha mambo yao. basi hao ndio waliosema: Mwenyezi mungu ni fukara na kwamba Mwenyezi Mungu amewaahidi wasimwamini Mtume mpaka awajie na kafara

﴿كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ﴾

185.Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtatekelezewa malipo yenu siku ya Kiyama, Mwenye kuepushwa na moto akatiwa peponi, basi huyo amefuzu. Na hayakuwa maisha ya dunia ila ni starehe idanganyayo.

﴿لَتُبْلَوُنَّ فِي أَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ وَلَتَسْمَعُنَّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَمِنَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا أَذًى كَثِيرًا وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا فَإِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴾

186.Kwa hakika mtapata misuko suko katika mali zenu na nafsi zenu na mtasikia udhia mwingi kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na kwa washirikina. Na mkisubiri na mkamcha mungu basi hayo ni miongoni maazimio.

KILA NAFSI ITAONJA MAUTI

Aya 185-186

KILA NAFSI ITAONJA MAUTI

MAANA

Kila nafsi itaonja mauti

Ni glasi inayozunguka kwa kila mtu, awe mwema au muovu. mfalme au kabwela, Haiwezekani wala hakuna njia yoyote ya kuyakimbia mauti. Lile wanalofikiria madaktari ni kujaribu kurefusha maisha ya mtu tu, sio kukinga mauti. Jaribio la mwisho walilifanya madaktari la kurefusha maisha mwaka 1967, ni kupachika moyo mwengine wa mtu anayekaribia kufa, anatolewa moyo na kuwekwa kwa mwenye moyo mgonjwa baada ya kutolewa. Lakini jaribio hili halikufanikiwa, ingawaje lilifanyika mara kwa mara. Kukawa na mzozo kwa madaktari wakubwa wakasema hilo ni kosa lisilosameheka. Kwa sababu haiwezekani kuhakikisha kuwa yule anayetolewa moyo kweli angekufa baada ya muda mfupi? Kwani kifo hutokea kwa namna tofauti; kama vile kuzimia muda mrefu na kukosa kuvuta pumzi, wala hakuna njia ya kujua hali hii baina ya kifo na uhai. Mara ngapi madaktari wamethibitisha kifo, kisha wagonjwa wakarudiwa na uhai.

Jana nimesoma katika gazeti moja kwamba kikongwe mmoja Mmisri alizimia, watoto wake wakaita madaktari, wakathibitisha bila ya wasiwasi kwamba amekufa, baada ya kutangaza kifo, kutoa matangazo ya tanzia, kuchimba kaburi na watu kuhudhuria mazishi, alifungua macho yake na akawaambia watu waliokuja: "Nendeni kwenye shughuli zenu Mungu awalipe." Ikiwa madaktari wameshindwa kuurefusha umri wa mtu na hata kumjua kama amekufa au ni mzima, basi kumkinga na mauti ndio hawawezi kabisa.

Bila shaka mtatekelezewa malipo yenu siku ya kiyama

Hakuna malipo duniani kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) isipokuwa mtu atalipwa malipo kamili siku ya kiyama.

Wafasiri wengi wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) humpa mtu sehemu ya malipo ya amali yake baada ya mauti kabla ya Kiyama, kisha humalizia malipo yake Siku ya Kiyama, Kwa hivyo hapo ndipo unatimia utekelezaji kwa ukamilifu. Na wamedai kuwa neno Tuwaffauna linafahamisha hilo. Ama sisi hatufahamu neno hilo zaidi ya lilivyoelezwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

"Na hakika sisi tutawatekelezea fungu lao bila ya kupunguzwa" (11:109).

Kauli hii haifahamishi kugawanywa, si kwa mbali wala karibu. Ndio, iko Hadith isemayo:"Hakika kaburi ni bustani katika mabustani ya pepo au ni shimo katika mashimo ya moto." Lakini hili ni jambo jengine na kufahamisha kugawanywa malipo ni jambo jengine.

Mwenye kuepushwa na moto akatiwa peponi basi huyo amefuzu.

Bali hata mwenye kuepushwa na moto na asitiwe peponi pia atakuwa amefuzu. Wanafalsafa wengi wamepanga kuwa 'kutokuwa na maumivu ni raha' na 'kutokuwa na uovu ni wema'

Na hayakuwa maisha ya dunia ila ni starehe idanganyayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesifu kuwa ni starehe inayohadaa, kwa vile mtu anahadaika nayo, au kwa sababu mtu akimiliki kitu basi inatokea kujidanganya. Imam Ali(a.s) anasema:"Dunia inadhuru, inadanganya na inapita."

Kwa hakika mtapata misuko suko katika mali zenu na nafsi zenu, na mtasikia udhia mwingi kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na kwa washirikina.

Hii ndiyo thamani ya haki na pepo. Ni mapambano machungu pamoja na wabatilifu, ni subira kutokana na tuhuma zao na uzushi wao, na kujitolea mhanga kwa nafsi na mali. Kadiri mtu anavyokuwa na nguvu katika dini yake ndivyo mitihani yake inavyozidi na kuwa mikubwa. Hilo ni kwa kwa sababu umuhimu wa watu wa haki unaleta machukivu kwa wabatilifu, kwani hakuna kupatana wala kupakana mafuta baina ya haki na batili. Watu wa batili walikuwa na bado ni wengi na wenye nguvu. Nao hawawezi kuwanyamazia maadui zao katika itikadi na misingi. Ni nani ajuaye kuwa unambughudhi na kumchukia, kisha akukubalie na kukunyamazia? isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mola wako? Kwa sababu hiyo ndipo ikawa historia ya Mitume na viongozi wazuri ni ya vita na jihadi pamoja na washirikina na wafisadi. Ama mitihani ya nafsi na mali na mengineo ni natija ya kila vita.

Makusudio ya wale waliopewa Kitabu kabla yenu ni mayahudi na manasara. Na waliofanya ushirikina ni Warabu waliotangaza vita na MtumeNa mkisubiri kutokana na jihadi ya wabatilifu na misukosuko inayowapata namkiogopa Mwenyezi Mungu katika yanayopasa kumwogopa, basi hayo ya kuwa na subira kutokana na misukosuko na kuogopa yaliyoharamishwa,ni miongoni mwa mambo ya kuazimia.

﴿وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَتُبَيِّنُنَّهُ لِلنَّاسِ وَلَا تَكْتُمُونَهُ فَنَبَذُوهُ وَرَاءَ ظُهُورِهِمْ وَاشْتَرَوْا بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَبِئْسَ مَا يَشْتَرُونَ﴾

187.Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi na wale waliopewa Kitabu, lazima mtakibainisha kwa watu wala hamtakificha. Wakakitupa nyuma ya migongo yao na wakakiuza kwa thamani ndogo. Basi ni mabaya waliyoyauza.

KAZI YA WANAVYUONI

Aya 187

MAANA

Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi na wale waliopewa Kitab, lazima mtakibainisha kwa watu wala hamtakificha.

Serikali huanzisha vituo na kumpangia kila mtu kazi yake na pia huchukua ahadi kwa kila mfanya kazi kwamba ataitekeleza kwa uaminifu na kuwa ataadhibiwa yule atakayevunja miiko. Mwenyezi Mungu ameumba binadamu, akamwamrisha lile lililo na kheri naye na akamkataza lile lililo baya kwake na linalomdhuru. Na amewachagua Mitume ili wafikishe hukumu zake kwa waja wake, akawaamuru wachukue ahadi ya Mwenyezi Mungu na kila wanayemfikishia hukumu hizi kwamba nao wazifikishe kwa watu.

Kwa hivyo, mwanachuoni wa dini ni mfanyikazi wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) wa kubainisha yaliyoteremshiwa Mitume. Yeyote atakayeficha kitu, basi yeye atakuwa na jukumu la kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, sawa na mfanyikazi wa serikali anavyoulizwa kama hakutekeleza wajibu wake. Hayo yameelezwa katika Aya kadhaa walizozitaja wanavyuoni katika mlango wa kuamrisha mema na kukataza mabaya. Kama vile:

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ﴾

Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha, katika hoja na uwongofu; baada ya Sisi kuyabainisha kwa watu Kitabuni, hao anawalaani Mwenyezi Mungu na wanawalaani wanaolaani (2:159)

Na Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kuinyamazia haki ni shetani bubu" Sikwambii mwenye kuisaidia batili. Vilevile aliulizwa kuhusu jihadi ipendezayo zaidi kwa Mwenyezi Mungu, akasema: "Neno la kumpa ukweli kiongozi dhalimu." Imam Ali(a.s) naye akasema:"Mwenyezi Mungu hatawaadhibu wajinga kwa kutojifundisha mpaka awaadhibu wenye elimu kwa kutoelimisha."

Haya yanaenea kwa wote, sio kwa wenye elimu tu, au watu wa dini au wasio na dini, au kwa mashinani au matawii, la! Ni kazi ya kila mtu, Kauli ya Mwenyezi Mungu: "Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi" inaenea kwa wote. Kwa sababu waliopewa Kitabu wanaingia mayahudi,manasara na waislamu. Bali Qur'an ndicho Kitabu Kitukufu, kama ambavyo wajibu wa kubainisha na uharamu wa kuficha unaingia katika Utume wa Muhammad(s.a.w.w) . na mengineyo katika misingi ya dini na matawi yake. Wengine wakasema inawakusanya mayahudi na manasara tu, kwa sababu wao walificha dalili za Utume wa Muhammad(s.a.w.w) zilizo katika Tawrat na Injil. Lakini ilivyo ni kuwa inaonyesha kuenea kwa kukosekana dalili ya kuhusika.

Wakaitupa nyuma ya migongo yao.

Kutupa kitu nyuma ya mgongo ni fumbo la kuacha kukitilia manani, kama ambavyo kukikodolea macho ni fumbo la kukitilia maanani.

Na wakakiuza kwa thamani ndogo basi ni mabaya waliyoyauza.

Kila anayeificha haki kwa kuathirika na mambo ya kidunia bila ya kuangalia ya akhera, basi atakuwa amemuuzia shetani dini yake kwa thamani ndogo. Wengine hawatosheki na kuificha haki tu, bali wanakigeuza kitabu na Hadith kwa tamaa ya ukubwa na utajiri, na hawa ndio wanaolaaniwa na Mwenyezi Mungu na pia wenye kulaani.

﴿ لَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَفْرَحُونَ بِمَا أَتَوا وَّيُحِبُّونَ أَن يُحْمَدُوا بِمَا لَمْ يَفْعَلُوا فَلَا تَحْسَبَنَّهُم بِمَفَازَةٍ مِّنَ الْعَذَابِ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴾

188.Usiwadhanie kabisa wale ambao wanafurahia mambo waliyoyafanya na wakapenda kusifiwa kwa wasiyoyafanya - usiwadhanie kabisa kuwa wataokoka na adhabu, na wana wao adhabu iumizayo.

﴿ وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

189.Na ufalme wa mbinguni na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye uwezo juu ya kila kitu.

KUSIFIWA KWA WASIYOYAFANYA

Aya 188-189

MAANA

Furaha si haramu, Ni nani asiyefurahi akipata jambo la kheri au kuokoka na shari? Bali kufurahi kwa ajili ya kheri ya watu inaonyesha ukweli wa nia na furaha njema. Mtume(s.a.w.w) alifurahi kwa sababu ya kuwasili binamu yake Jafar bin Abu Talib kutoka Uhabeshi, akambusu na akasema: "Sijui ni jambo gani kati ya mawili litakalomshinda mwenzake kwa furaha, ni kwa kuwasili Jafar au kwa kuiteka Khaibar?!" Furaha isiyotakikana ni ile iliyo na msukumo wa mifundo, kufurahia matatizo ya wengine na majivuno, au kufurahi mtu kwa sababu amenyang'anya, akaua au kufanya ufisadi bila ya kuadhibiwa au kulaumiwa, au kufurahi kwa sababu ya kufanya hila na hadaa ili asifiwe na sifa asizokuwa nazo, na mengineyo ambayo tunayashuhudia huku na huko.

Baada ya utangulizi huu tunaelezea kwa ufupi kauli zinazohusu Aya hii:

Usiwadhanie kabisa wale ambao wanafurahia mambo waliyoyafanya na wakapenda kusifiwa kwa wasiyoyafanya, usiwadhanie kabisa kuwa wataokoka na adhabu, na wana wao adhabu iumizayo.

Yasemekana kuwa Aya hii ilishuka kwa wanavyuoni wa Kiyahudi ambao walificha jina la Muhammad na sifa zake zinazopatikana katika Tawrat, na wakati huo huo wanapenda wasifiwe kuwa ni wa kweli, na kwamba wao wako kwenye mila ya Ibrahim(a.s) Na ikasemekana kuwa ilishuka kwa ajili ya wanafiki, waliokuwa wakihepa kuungana na Mtume(s.a.w.w) katika vita kwa kutoa sababu za uongo na Mtume alikuwa akionyesha kuwakubalia. Hilo liliwafurahisha sana na kupenda kusifiwa kwa wasiyoamini.

Kauli yenye nguvu ni kuwa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja wale waliochukua ahadi kuwa wasifiche haki, na wakaitupa ahadi, ndipo akawataja katika Aya hii kwamba wao wamefurahi kwa tendo lao hilo wakapenda kusifiwa kuwa ni wa kweli na wenye haki, na hali wao wako mbali nayo kabisa. Kadiri watakavyoendelea katika upotevu wao hawatatoka katika mamlaka ya Mwenyezi Mungu na uwezo wake, wala hawataokoka na adhabu yake. Vipi isiwe hivyo,"Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu" Kwa tafsir hii wanaingia katika Aya hii Mayahudi na Manasara walioficha yanayomhusu Muhammad(s.a.w.w) na wanafiki katika Waislamu walioficha ukafiri na kudhihirisha imani.

Unaweza kuuliza : kwa nini Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, 'usiwadhanie' baada ya kwisha kusema usiwadhanie ambao'

Jibu : imekaririka hapa kwa sababu ya kuondoa mikanganyo baada ya maneno marefu. Matumizi haya yameenea siku hizi katika maandishi na idhaa.

Swali la pili : Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema: "Usiwadhanie kuwa wataokoka na adhabu." Na kisha akasema: "Na wana wao adhabu iumizayo." Pamoja na kuwa jumla ya kwanza inaitoshelezea ya pili.

Jibu : hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anatofautisha kati ya jumla mbili, kwa sababu ya kwanza imefahamisha kwamba wao si wenye kuokoka na adhabu bila ya kubainisha adhabu yenyewe kama ni hafifu au ni kali, ndipo akabainisha katika jumla ya pili kuwa ni katika aina ya adhabu iumizayo. Kama vile kusema: "Nakupenda tena nakupenda sana.'

﴿ إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ﴾

190.Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kutofautiana usiku na mchana, ziko ishara kwa wenye akili.

﴿ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴾

191.Ambao humtaja Mwenyezi Mungu katika hali ya kusimama, na kukaa na kulala, na wanafikiria umbo la mbingu na ardhi. Mola wetu hukuviumba hivi bure, Utukufu ni wako, basi utuepushe na adhabu ya moto"

﴿ رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴾

192.Mola wetu! Hakika wewe ambaye utamwingiza motoni utakuwa umemfedhehesha na hawatakuwepo wasaidizi kwa ajili ya madhalimu.

﴿ رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ ﴾

193.Mola wetu! Hakika sisi tumemsikia mwenye kulingania anayelingania kwenye imani kwamba: mwaminini Mola wenu nasi tukaamini. Mola wetu! Tusamehe madhambi yetu na na utufutie makosa yetu na utufishe pamoja na watu wema."

﴿ رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴾

194.Mola wetu! Na utupe uliyotuahidi kwa Mitume yako, wala usitufedheheshe siku ya kiyama. Hakika wewe huvunji ahadi"

﴿ فَاسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ فَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَأُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأُوذُوا فِي سَبِيلِي وَقَاتَلُوا وَقُتِلُوا لَأُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَأُدْخِلَنَّهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ثَوَابًا مِّنْ عِندِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عِندَهُ حُسْنُ الثَّوَابِ﴾

195.Akawakubalia Mola wao kwamba mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, ni nyinyi kwa nyinyi. Basi wale waliohama na wakafukuzwa katika majumba yao na wakaudhiwa katika njia Yangu na wakapigana na wakauawa, bila shaka nitawafutia makosa yao na nitawaingiza katika mabustani ambayo hupita mito chini yake. Ndiyo malipo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo mema.

MWENYEZI MUNGU NA WENYE AKILI

Aya 190-195

MAANA

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kutofautiana usiku na mchana, ziko ishara kwa wenye akili.

Tulionyesha dalili za kutosha za kiakili juu ya kuweko Mwenyezi Mungu (s.w.t) wakati wa kutafsiri Aya ya 22 na 164 ya Sura Baqara, Nayo iko katika maana ya Aya hii tuliyo nayo. Kwa vile hapa ni mahali pake, tutarudia kuyaeleza maudhui hayo kwa ufupi na kwa namna nyingine. Njia nzuri ya kumjua Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni njia ambayo anaitolea dalili Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu kuweko kwake. Kwa ufupi ni kuangalia mwenye akili kwenye ulimwengu na kufikiria kwa undani maajabu Yake na siri iliyomo ya mipangilio na maajabu kadhaa. Utaona kuwa kila kilichopo kinafahamisha makusudio na malengo, kwa kuwekwa mahali panaponasibiana na kuwa katika mpangilio wa ulimwengu na mwendo wa maisha.

Kutokana na misingi hii miwili (hisia na akili), inapelekea kabisa kujua sababu ya kwanza inayosifika na uhai, elimu, uweza na hekima ya hali ya juu. Nimewasikia watu wengi wakisema kuwa watu wote, hata walahidi, wanakubali kuwa iko sababu ya kwanza, isipokuwa waumini huiita Mwenyezi Mungu na wengine huiita maada au nguvu asili, kwa hiyo tofauti iko katika majina tu. Lakini hilo ni kosa kubwa na ni kuleta shubha. Kwa sababu waumini wanaamini kuweko sababu hiyo, inayothibitishwa na akili sio kwa hisia, na kwamba sababu hiyo inasifika kwa sifa ya ujuzi, uweza, hekima na uadilifu. Ama wengine wanasema kuwa inaonekana kwa macho na kuguswa kwa mkono na kwamba hiyo ni kipofu na kiziwi. Kwa hiyo tofauti ya kauli mbili hizo ni mbali zaidi ya mbingu na ardhi.

Ambao humtaja Mwenyezi Mungu katika hali ya kusimama na kukaa na kulala na wanafikiria umbo la mbingu na ardhi. Mola wetu hukuviumba hivi bure, utukufu ni wako; basi utuepushe na adhabu ya moto.

Makusudio ya kusimama, kukaa na kulala kwa ubavu ni kwamba wao wako katika twa'a ya Mwenyezi Mungu wakati wowote. Makusudio ya kufikiria umbo la mbingu na ardhi ni kuwa wanamkubali Mwenyezi Mungu (s.w.t) Ama kumyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutaka kinga na adhabu ya moto, ni dalili ya uchaji Mungu na imani. Arrazi anasema: "Aina za kuabudu ni tatu: Kusadikisha kwa moyo, kuthibitisha kwa ulimi na kutenda kwa viungo" Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu 'wanamtaja Mwenyezi Mungu' inaonyesha ibada ya ulimi, 'katika hali ya kusimama kukaa na kulala kwa ubavu' inaonyesha ibada ya viungo, na kauli yake, na 'hufikiria umbo la mbingu na ardhi;' inaonyesha ibada ya moyo na fikra na roho. Na mtu ni mkusanyiko wa hivi vitu vitatu. Kama ulimi utazama kabisa katika dhikri (utajo), viungo vikawa vinatenda na akili ikazama katika kufikiria, basi hapo ndipo atakuwa ameingia katika ibada kwa mwili wake wote"

Hakuna mwenye shaka kwamba kumtaja Mwenyezi Mungu, kumwamini na kumwabudu ni vizuri, lakini vizuri zaidi ya kumtaja kwa ulimi, kusimama usiku, kuswali na kufunga mchana, ni kufanya kazi kwa ajili ya watu na kujitolea katika maslahi ya umma. Na kila atakayetaka matukufu kutoka kwa Mwenyezi Mungu bila ya kujitoa mhanga huku, pamoja na kuwa na uwezo, basi atakuwa anatafuta kuthaminiwa bila ya thamani. Kwa mnasaba wa kauli yake Mwenyezi Mungu. 'Mola wetu hukuviumba hivi bure' tutaonyesha kauli za Sunni wanaosema kuwa haifai kuleta sababu ya vitendo vya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na makusudio au lengo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hapaswi na jambo lolote wala hakuna ubaya kwake wa kitu chochote. (Al- Mawafiq J. 8 uk. 202)

Sheikh Abu Zuhra katika kitab Madhahibul Islamiyya, anasema; "Wamesema Ashaira. Yaani sunni, kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba vitu si kwa sababu yoyote" Shia wanasema kuwa vitendo vyote vya Mwenyezi Mungu Mtukufu vina sababu ya maslahi ya watu au ya utaratibu wa ulimwengu, kwa kuwa yeye ni mjuzi mwenye hekima. Wakatoa dalili ya Aya hii, "Mola wetu hukuviumba hivi bure"

Pia inawezekana kuwajibu Sunni kwa kauli yao na vitendo vyao wala sio kwa Aya au riwaya. Kwamba wao wanafanya makisio na kuchukulia uzuri na maslahi yanayosababisha upole wa Mwenyezi Mungu katika kuwaangalia viumbe na kutengeneza vizuri hali zao, katika maisha yao ya duniani na akhera. Pia wanachukua asili ya hukumu za kisharia ya Mwenyezi Mungu kwa kukisia na kuonelea kuwa ni vizuri. Vilevile wametunga vitabu mahsusi katika kubainisha hekima ya Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na makatazo yake. Maana ya hayo yote ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu haamrishi wala hakatazi isipokuwa kwa lengo sahihi na sababu yenye hekima.

Mola wetu! Hakika Wewe ambaye utamwingiza motoni, basi utakuwa umemfedhehesha.

Na sisi tunakutii kwa kutaka radhi Zako na kuepuka fedheha hii. Hivi ndivyo anavyokuwa mumini, anaweka mbele thawabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Kwa hiyo anatii kwa kuogopa adhabu na kutumaini thawabu. Imamu Ali(a.s) amesema: akiwasifu Waumini: "Wao na pepo ni kama walioiona wakiwa humo wanastarehe. Na wao na moto ni kama waliuona wakiwa ndani yake wanaadhibiwa. Ama anayemwabudu Mwenyezi Mungu kwa dhati yake tu, sio kwa kutumaini pepo Yake au kuogopa moto wake, huyo ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwanafunzi wake Imam Ali."

Na hawatakuwepo wasaidizi kwa ajili ya madhalimu.

Kila msaidizi wa batili katika dunia hii na ambaye ana haki za watu, basi yeye ni dhalimu, na itakapofika Siku ya haki na uadilifu hatakuwa na msaidizi. Mawaidha fasaha kabisa katika maudhui haya ni khutba ya Mtume alipohisi kukaribia mauti alisema: "Enyi watu ambaye nimemchapa mgongoni mwake, huu hapa mgongo wangu, na ambaye nimemchukulia mali yake hii hapa mali yangu, na achukue wala asiogope kumwekea nongwa, Kwani hiyo siyo hulka yangu. Isipokuwa nawataka mchukue haki zenu tu kama ziko kwangu, au kisasi ili nikutane na Mola wangu nikiwa na nafsi njema" Maelezo zaidi yako katika tafsir ya Aya 160 ya Sura hii kifungu cha 'Muhammad na hulka njema'

Mola wetu hakika sisi tumesikia mwenye kulingania anayelingania kwenye imani kwamba muaminini Mola wenu, nasi tukaamini

Hii ndio hali ya kila mwenye kuitafuta haki kwa njia ya haki anaufungua moyo wake kwa mwito wa haki na anaikubali mara tu anapoisikia kutoka kwa yoyote; sikwambii akiwa ni bwana na Mitume na mwisho wa Mitume.

Akawakubalia Mola wao kwamba mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke.

Yanayozingatiwa ni matendo, sio nasaba ya mtendaji au kabila yake, wala si kwa jinsia yake, awe mwanamume au mwanamke. Wote ni sawa katika uislamu. Huu ni uthibitisho wa haki ya mwanamke na utukufu wake. Ni nyinyi kwa nyinyi mwanamume ni baba wa mwanamke na mwanamke ni mama wa mwanamume, na kila mmoja ni kaka wa mwengine na mume wa mwengine; wote wanatokana na asili moja; wote mnatokana na Adam na Adam anatokana na mchanga. Kuna Hadith isemayo: "Wanawake ni ndugu baba mmoja mama mmoja wa wanaume." Yamekwishatangulia maelezo zaidi katika tafsir ya (2:228)

Basi wale waliohama na wakafukuzwa katika majumba yao na wakaudhiwa katika njia yangu na wakapigana na wakauawa, bila shaka nitawafutia makosa yao na nitawaingiza katika mabustani ambayo hupita mito chini yake. Ndiyo malipo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu na kwake Mwenyezi Mungu kuna malipo mema.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuyafungamanisha malipo na matendo mema na wala sio kwa jinsia, amebainisha kuwa matendo ambayo yatapata nyongeza ya thawabu ni kama haya yafuatayo.

1. Kutoka mumini kwa hiyari yake katika mji wake ambao hawezi kusimamisha dini kwenda mji mwengine anaoweza kufanya hivyo. Kwa sababu ya Aya hii na Aya isemayo:

﴿إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَسَاءَتْ مَصِيرًا﴾

"Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: Tulikuwa wanyonge katika ardhi." Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkaweza kugura humo. Hao makazi yao ni jahannam, nayo ni marejeo mabaya kabisa." (4:97)

Kwa sababu ya Aya mbili hizo, mafakihi wametoa fatwa ya kuharamisha kukaa mtu mnyonge katika mji wa kikafiri ambao hawezi kutekeleza faradhi na nembo za Kiislamu, wakawajibisha kwake kuhamia mji wa waislamu ili kuweza kutekeleza yale yaliyo wajibu kwake isipokuwa kama atashindwa kuhama. Jambo la kusikitisha siku hizi ni kuhusu vijana wetu wa Kiislamu wenye uwezo, wanakazania kwenda Amerika na Ulaya, si kwa jengine ila kwa kufuata ufuska, zinaa na ulevi.

2. Kutolewa waumini kwa nguvu majumbani mwao, kama washirikina wa Kiquraish walivyowafanyia wale waliomwamini Muhammad(s.a.w.w) na kama walivyofanya waisrail kwa wapalestina.

3. Kuudhiwa katika njia ya haki. Hakuna yeyote anayeifuata ila ataudhiwa. Imeelezwa katika Hadith kwamba mtu hujaribiwa kwa kiasi cha dini yake. Ikiwa katika dini yake ni nzito basi huzidi mitihani na ikiwa ni nyepesi basi pia atajaribiwa kwa kiasi chake. Wala hakuna kitu kikubwa zaidi kwa malipo mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kuvumilia maudhi kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu na kuwa na subira. "Ewe Mwenyezi Mungu tujaalie katika wenye kuvumilia"

4. Kujitoa mhanga katika njia ya haki. Wote hawa Mwenyezi Mungu atawafutia maovu yao na zaidi ya hayo atawapa thawabu itakayofanana na utukufu wake na cheo chake. Kukaririka neno malipo na utukufu ni kuonyesha kuwa malipo yake hayana mfano, kama ambavyo utukufu wake hauna mfano.

﴿لَا يَغُرَّنَّكَ تَقَلُّبُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي الْبِلَادِ﴾

196.Kusikuhadae kabisa kuzungukazunguka, kwa wale ambao wamekufuru katika miji.

﴿مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴾

197.Ni starehe ndogo. Kisha makazi yao ni Jahannam ni mahali pabaya pa kushukia.

﴿لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نُزُلًا مِّنْ عِندِ اللَّـهِ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ لِّلْأَبْرَارِ﴾

198.Lakini wale waliomcha Mola wao watapata mabustani ambayo hupita mito chini yake. Watakaa humo milele, Ndiyo makaribisho yatokayo kwa Mwenyezi Mungu, na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema.

WALIOKUFURU NA WENYE TAQWA

Aya 196-198

MAANA

Maana ya matamshi ya Aya zote tatu yako wazi. La muhimu ni kubainisha makusudio kwa ujumla. Wafasiri wengi wamesema kuwa kafiri anaishi maisha ya hapa duniani kwa raha, lakini mwisho wake huko akhera ni balaa na mashaka. Na mu'min anaishi kwa mashaka na dhiki, na mwisho wake ni mzuri. Na kwamba "Dunia ni jela ya mu'min na ni pepo ya kafiri." Tulivyofahamu sisi kutokana na Aya hizi ni kwamba zimeeleza tofauti baina ya wale walioathirika na dunia yao kuliko dini yao, na wala wasifanye kazi yoyote isipokuwa kwa maslahi yao ya kibinafsi, kama vile mayahudi na wanaofanana nao, na wale ambao wameitanguliza dini yao kuliko dunia yao kwa hali yoyote itakayokuwa.

Kundi la kwanza Mwenyezi Mungu ameliita makafiri kwa sababu wao wanaikufuru haki wala hawaipi uzito wowote. La pili ameliita wanaomcha Mwenyezi Mungu, kwa sababu linajiepusha na machukivu yake na maasia yake. Hakuna mwenye shaka kwamba mtu anayefanya tendo lolote kwa ajili ya dunia, akaipa kipaumbile na akahalalisha ya haramu kwa ajili ya dunia, basi takataka zote zitamwangukia, kama tunavyoshuhudia. Kinyume na mwenye kufanya zuhudi katika haramu na akathirika na njaa na kujinyima. Makusudio ya kuzunguka zunguka katika miji ni kupata kwao neema za dunia. Huenda wakadhani kwamba dhahiri ya neema na starehe za wabatilifu ni kheri kwao, na kwamba dhahiri ya kujinyima kwa watu wa haki ni shari. Ndipo Mwenyezi Mungu akaiondoa dhana hii, kwamba ni kinyume cha hivyo. Kwa sababu neema ya wabatilifu ni starehe chache, kisha waingie katika Jahannam ambayo ni marejeo mabaya. Na kwamba shida ya wenye haki itaondoka, kisha itakuja neema ya milele na raha ya daima.

﴿وَإِنَّ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَمَن يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْهِمْ خَاشِعِينَ لِلَّـهِ لَا يَشْتَرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴾

199.Na hakika miongoni mwa watu wa Kitabu wako wanaomwamini Mwenyezi Mungu na yaliyoteremshwa kwenu na yaliyoteremshwa kwao, kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawaziuzi Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hao wana ujira wao kwa Mola wao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴾

200.Enyi ambao mmeamini! Fanyeni subira na mvumilie na muwe imara na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.

WAUMINI KATIKA WATU WA KITABU

Aya 199-200

LUGHA

Imesemekana kuwa neno Isbiruu na Saabiruu yana maana moja. Pia imesemekana kuwa Isbiruu lina maana ya kuvumilia adha ambayo haikusababishwa na mtu; kama maradhi, na Saabiruu ni kuvumilia adha inayotokana na mwengine.

MAANA

Na hakika miongoni mwa watu wa Kitabu wako wanaomwamini Mwenyezi Mungu na yaliyoteremshwa kwenu na yaliyoteremshwa kwao, kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawaziuzi Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hao wana ujira wao kwa Mola wao.

Makusudio ya yaliyoteremshwa kwenu ni Qur'an na yaliyoteremshwa kwao ni Tawrat na Injil. Aya inamhusu kila aliyemwamini na atakayemwamini Muhammad(s.a.w.w) katika waliopewa kitabu, na wala haimhusu Najjash au Abdallah bin Salam tu, kama ilivyosemekana, kwa sababu tamko linawanea wote, wala hakuna dalili ya kuwa ni mahsusi. Ikiwa Mwenyezi Mungu anaweza kumkubalia anayemwamini Muhammad katika watu waliokuwa hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Kitabu, basi uwezekano wa kumkubalia mtu wa Tawrat na wa Injil ni zaidi. Hasa kwa kuzingatia kuwa mtu anaacha dini yake, jambo ambalo ni gumu sana kwa mtu kuweza kuacha dini aliyoizoea na kuirithi.

Enyi ambao mmeamini! Fanyeni subira na mvumilie na muwe imara na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufaulu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamalizia Sura ya Al-Imran kwa Aya hii ambayo imekusanya taqwa ya Mwenyezi Mungu na amri ya kuwapiga jihadi maadui zake. Yamekwishatangulia maelezo kwa ufafanuzi kuhusu subira wakati wa kufasiri Aya ya 155 ya sura ya Baqara katika kifungu cha subira na kifungu cha aina ya malipo ya subira.

TAQWA

Nasi tunaihitimisha Sura hii tukufu kwa muhtasari kuhusu taqwa. Aliulizwa Imam Jafar As-Sadiq(a.s) kuhusu Taqwa, Akasema:"Ni asikose kukuona Mwenyezi Mungu pale alipokuamrisha na usiweko katika yale aliyokukataza." Kwa hiyo hapana budi katika taqwa kujua hukumu za Mwenyezi Mungu na kuzitumia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu ilimu bila ya matendo ni hoja kwa mtu, na matendo bila ya ilimu ni kama kutembea bila ya kutumia njia. Kwa msingi huu, taqwa inakuwa ndiyo dini, ndiyo hulka na ndiyo msingi wa mambo. Mtume(s.a.w.w) anasema: "Msiseme Muhammad ni wetu, Wallahi! Marafiki zangu sio nyinyi wala si wengine isipokuwa wale wamchao Mwenyezi Mungu." Amesema tena: "Asiyekuwa Mwislamu, wakisalimika watu na mkono wake na ulimi wake, yuko karibu zaidi na Muhammad(s.a.w.w) kuliko yule anayenasibika na uislamu, lakini asijizuie na kuwaudhi watu." Zimekuja Aya kadhaa katika Qur'an kwamba kufuzu na kuokoka kesho ni kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu peke yao. Katika ngano za watu wa kale kuna hekaya inayoishiria ukweli huu: Hapo zamani za kale paliondokea mtu mmoja aliyekuwa akipenda sana kusema: sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote na mwisho ni wa wamchao Mwenyezi Mungu. Iblis alikasirika sana na hali hii. Hivyo akamtumia mmoja wa mashetani zake.

Akaenda na kumwambia: Sema, mwisho ni wa matajiri. Yule mtu akasema: Hapana, mwisho ni wa wamchao Mwenyezi Mungu. Walipozidi kubishana waliafikiana waamuliwe na mtu watakayemuona kwanza, na atakayeshindwa akatwe mkono. Mara wakakutana na mtu mmoja wakamweleza, akasema: Mwisho ni wa matajiri, sio wa wamchao Mwenyezi Mungu" Yule mtu akakatwa mkono.

Yule mtu akaendelea kuyakariri maneno yake, sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote na mwisho ni wa wamchao. Shetani akamjia mara ya pili na kumwambia: Hukupata funzo? Je unataka tuamuliwe tena? yule mtu akajibu: Ndio akatokeza mtu mwengine akahukumu kuwa mwisho ni wa matajiri sio wa wamchao Mwenyezi Mungu. Yule mtu akakatwa mkono wa pili.

Licha ya hayo, yeye aliendelea kuyakariri yale maneno kuliko mara ya kwanza. Shetani akarudi tena akasema: Hivi sasa atakayeshindwa atakatwa kichwa. Yule mtu akakubali akasema: Naam. Mara wakakutana na mpanda farasi mmoja wakataka waamuliwe, naye baada ya kuelezwa kisa yule mpanda farasi akachukua upanga na kumdengua kichwa shetani huku akisema huu ndio mwisho wa wafisadi.

Kisha Mwenyezi Mungu akamrudishia yule mtu mikono yake kama ilivyokuwa; yakathibiti aliyokuwa akiyasema. Lakini hii ni baada ya subira na uvumilivu na kukatwa mkono wa kuume na kushoto. Ni muhali kwa mtu kufikilia malengo bila ya kuwa na subira na kuvumilia taabu na mashaka.