TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17417
Pakua: 3830


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17417 / Pakua: 3830
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

Mwandishi:
Swahili

4.SURA YA NNE: AN-NISAA

Sura hii imeshuka madina, ina Aya 176; ilishuka baada ya Sura Mumtahina (60).

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amewaumba kutokana na nafsi moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi hiyo, na akaeneza kutokana na hao wawili wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana na ndugu wa damu, Hakika Mwenyezi Mungu anawachunga.

AMEWAUMBA KUTOKANA NA NAFSI MOJA

Aya 1

LUGHA

Neno Zawj lina maana ya aliye na mwengine wa jinsi yake (jozi). Kwa hiyo mwanamke aliyeolewa ni jozi na mume aliyeoa ni jozi.

Mwenye Majmaul-bayan amenukuu kuwa katika Sura hii mna Aya mbili ambazo zimeshuka Makka nazo ni: 58 na 127 Imeitwa Sura ya wanawake, kwa sababu, imeanza kwa kuwataja wanawake na pia ina hukumu nyingi zinazofungamana nao.

MAANA

Katika Aya hii kuna mambo yafuatayo:

1. ENYI WATU! MCHENI MOLA WENU

Imesemekana kuwa msemo unawahusu watu wa Makka tu. Lakini ilivyo hasa ni kuwa unawaenea wote wanaokalifiwa na sharia, Kwa sababu dhahiri ya neno inawakusanya wote, wala hakuna dalili yoyote ya kuhusisha. Bali amri ya kumcha Mwenyezi Mungu inatilia mkazo kuwa inawaenea wote, Kwa sababu, wajibu wa Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu kujiepusha na maasi, hauhusiki na watu fulani.

2. AMBAYE AMEWAUMBA KUTOKANA NA NAFSI MOJA

Mwenye Tafsir Al-manar amemnukuu Sheikh wake Muhammad Abduh akisema: "Mwenyezi Mungu ameficha kuhusu nafsi aliyomuumbia mtu na ameileta kwa tamko Nakira (linaloenea). Kwa hiyo nasi tunaiacha kama ilivyofichwa. Pia Aya nyingine zinazomwambia mtu: "Ewe mwana Adam" haziondoi uficho huu. Wala hakuna kauli ya mkato kuwa watu wote ni watoto wa Adam.

Inatosha kusihi kuwa msemo uliwahusu watu miongoni mwao wana wa Adam waliokuwa wakati wa kuteremshwa msemo huo"

Yametangulia maelezo katika kufasiri kisa cha Adam mwanzo mwanzo mwa Sura ya Baqara, akisema kwamba katika ardhi kulikuweko na aina ya watu waliokuwa katika jinsi hii wakafanya ufisadi na wakamwaga damu." Kwa ufupi makusudio ya Sheikh Abduh ni kwamba Qur'an haithibitishi wala haikanushi kuwa Adamu ni baba wa watu wote; bali inawezekana kuweko na mababa kadhaa kwa watu, Adam akiwa mmoja wao. Na kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu "Enyi wana Adamu"Inafahamisha kuwa wale waliokuweko wakati wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) walikuwa ni watoto wa Adam na wala haifahamishi kila aliyekuwako na atakayekuwako ni kizazi cha Adam. Sisi tunamjibu, kwanza: Maamrisho na makatazo yaliyokuja katika Qur'an na Hadithi hayahusiki na aliyekuwepo wakati wa kutolewa, bali yanamkusanya kila aliyekuwepo na atakayekuwepo mpaka siku ya mwisho.

Kwa sababu kadhia la kisharia linamuhusu aliyepo na asiyekuwepo bila ya tofauti yoyote sawa na mfano wa kusema: "Atakayetimiza miaka ishirini basi ni lazima afanye jambo fulani. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ﴾

"Je sikuwaagiza enyi wanaadamu kuwa msimwabudu shetani ? Hakika yeye ni adui aliye wazi kwenu" (36:60)

Kauli hii inawaenea watu wote bila ya kumtoa hata mmoja, ni sawa wawepo wakati iliposemwa au la.

Pili : Maamrisho na makatazo katika Qur'an na Hadith ambayo wameelezwa wanadamu, ikiwa yanawahusu waliokuwa wakati wa Mtume(s.a.w.w) , sisi tusingelazimika nayo, na wala isingefaa sisi kuzitolea dalili juu ya hukumu yoyote miongoni mwa hukumu za Mwenyezi Mungu. Waislamu wote akiwemo Sheikh Abduh wanatoa hoja kwa Qur'an na Hadith za Mtume(s.a.w.w) bali ndio msingi wa kwanza wa kurejelea wa itikadi na sharia ya kiislam kwa dharura ya dini. Ikiwa taklifa inawahusu watu wote, basi watu wote watakuwa ni kizazi cha Adam. Kwa hiyo basi Sura ya 36 na Aya hii:

﴿ يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ﴾

"Enyi wanadamu asiwafitini shetani kama alivyowatoa wazazi wenu katika pepo." (7:27) na Aya:

﴿ وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ ﴾

"Na (kumbuka) Mola wake alipoleta katika wanadamu kizazi chao kutoka migongoni mwao." (7:172).

Na vile vile Aya isemayo:

"Na hakika tumewatukuza wanadamu" (17:70), zote hizi zinakuwa ni ubainifu na tafsiri ya nafsi moja; na kwamba makusudio ya nafsi ni baba yetu Adam bila ya shaka yoyote.

Ama kauli ya Sheikh Muhammad Abduh kuwa kulikuweko na watu wengine kabla ya Adam iko mbali na tunayoyaeleza. Kwa sababu maneno yako katika jinsi ya viumbe iliyobaki sio jinsi iliyokwishapotea, Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuambia kwa kauli yake:

"Enyi watu" na "Hakika tumewaumba kwa udongo" (22:5) Vilevile Aya:

﴿ إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ﴾

"Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa Adam; alimwumba kutokana na udongo," (3:59).

Aya hizi tukiziunganisha, natija itakuwa "Nyote mmetokana na Adam na Adam anatokana na udongo" kama inavyosema Hadith tukufu. Tatu: Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kwamba yeye amesema: "Mimi ni bwana mkubwa wa kizazi cha Adam." Je yuko mwislamu yeyote anayedhani tu au kufikiria kuwa Mtume alikuwa anakusudia aina maalum ya watu na sio watu wote? Swali hili hasa limwelekee Sheikh Muhammad Abduh.

3. NA AKAMUUMBA MKEWE KATIKA NAFSI HIYO.

Inassemekana kuwa herufi Min (katika) ni ya kuonyesha baadhi; na makusudio ni mkewe Hawa na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimuumba kutokana na ubavu wa Adam. Pia imesemekana kuwa alimuumba kutokana na ziada ya udongo wa Adam, kama zielezavyo riwaya nyengine. Ilivyo ni kuwa hakuna dalili ya kuonyesha baadhi, bali inawezekana kuwa ni ya kubainisha; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا﴾

"Na katika ishara zake ni kuwa amewaumbia wake zenu katika jinsi yenu. (30:21)"

Maana yake ni kuwa kila nafsi na mkewe wameumbwa katika asili moja ambayo ni mchanga kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ إِذَا أَنتُم بَشَرٌ تَنتَشِرُونَ﴾

"Na katika ishara zake ni kuwa amewaumba kwa udongo kisha mmekuwa watu wanaoenea" (30:20)

Ama kauli ya kuwa makusudio ya mke wake ni Hawa, haina dalili yoyote kutoka kwa Qur'an ambapo haikutajwa kabisa.

4. NA AKAENEZA KUTOKANA NA HAO WAWILI WANAUME WENGI NA WANAWAKE

Yaani na wanawake wengi pia. Haikutajwa sifa ya wengi kwa vile ile ya kwanza imefahamisha hii ya pili. Ajabu ni kauli ya Razi kwamba kwa kusifiwa wanaume kwa wingi, ni umashuhuri na kuonekana; kinyume na hali ya wanawake ambayo inakuwa ni kutokuwa mashuhuri na kufichika. Kauli hii ya Razi inafahamisha tu kuwa amehukumia tabia ya mwanamke kulingana na desturi za jamii anayoishi. Kimsingi ni kuwa desturi hizi hugeuka na kubadilika kutokana na wakati ulivyo. Kwa hiyo ni makosa kuchukua kipimo cha jumla kutokana na desturi maalum. Vyovyote itakavyokuwa maana yake iko wazi, ni kwamba mtu anazaliwa kutokana na mke na mume; na kutokana na wawili wao (mke na mume) ndio mamilioni yanaenea kizazi baada ya kizazi. Inasemekana kuwa ulimwenguni hivi sasa kuna watu zaidi ya Billioni tatu([9] ) .

5. NA MCHENI MWENYEZI MUNGU AMBAYE KWAYE MNAOMBANA NA NDUGU WA DAMU

Hii ni ishara ya yale wayasemayo baadhi yetu kwa mfano 'haki ya Mungu au haki ya mama. (Kuomba mtu afanye kwa haki ya mungu au ya ndugu (kizazi)) Makusudio ya amri ya kumcha Mwenyezi Mungu na udugu wa damu ni kutekeleza haki zetu kwao, Aya iko katika mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu."Ya kwamba unishukuru mimi na wazazi wako" (31:14). Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametuamrisha katika Aya hii kuogopa ghadhabu na adhabu yake, kuwafanyia mema ndugu wa damu, tusifanyiane kibri na tusidhulumiane. Kwa sababu wote ni wa asili moja. Amemalizia Mwenyezi Mungu kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu anawachunga. Haya ni makemeo na ni kiaga kwa yule anayeasi na kung'ang'ania uasi.

﴿ وَآتُوا الْيَتَامَىٰ أَمْوَالَهُمْ وَلَا تَتَبَدَّلُوا الْخَبِيثَ بِالطَّيِّبِ وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَهُمْ إِلَىٰ أَمْوَالِكُمْ إِنَّهُ كَانَ حُوبًا كَبِيرًا﴾

2.Na wapeni mayatima mali zao wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao kwa mali zenu; hakika hiyo ni dhambi kubwa.

MALI YA MAYATIMA

Aya 2

MAANA

Na wapeni mayatima mali zao.

Hapana budi yatima awe na mtu mwenye akili na mwaminifu atakayemlea na kuangalia mali yake kwa masilahi yake mpaka aweze kujitegemea na kujua baya na zuri. Aya hii inafungamana na mali za mayatima; inawaamrisha mawasii waichunge hiyo mali na wasiifuje; waitumie vizuri kwa ajili ya kuwalisha na wawape wenyewe watakapokuwa wakubwa.

Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri.

Makusudio ya kibaya hapo ni mali ya haramu na kizuri ni mali ya halali. Maana yake msile na kustarehe kwa mali ya yatima na mali zenu mkazibania. Ikiwa mtafanya hivyo, basi mtakuwa mmebadilisha lile ambalo ameliharamisha Mwenyezi Mungu (mali ya yatima) kwa zuri, lile alilolihalalisha (mali yenu). Aya hii iko katika mwelekeo wa Aya isemayo:

"Je,mnabadili vilivyo duni kwa vile vilivyo bora?" (2:61)

Wala msile mali zao kwa mali zenu; hakika hilo ni dhambi kubwa.

Makusudio yamsile hapo ni msitumie maana yake, msinufaike na mali za yatima kama mnavyofanya kwa mali zenu. Kwa sababu umuhimu wenu ni kuzichunga tu, na kuzitumia kwa masilahi ya mayatima. Na mkiligeuka hilo basi mtakuwa wakosaji wenye dhambi.

﴿ وَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تُقْسِطُوا فِي الْيَتَامَىٰ فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَلَّا تَعُولُوا ﴾

3.Na kama mkihofia kutowafanyia uadilifu mayatima, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili wawili na watatu watatu na wanne wane. Na mkihofia kuwa hamuwezi kufanya uadilifu, basi ni mmoja au wale ambao mikono yenu ya kuume imewamiliki. Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma.

﴿ وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً فَإِن طِبْنَ لَكُمْ عَن شَيْءٍ مِّنْهُ نَفْسًا فَكُلُوهُ هَنِيئًا مَّرِيئًا ﴾

4.Na wapeni wanawake mahari yao hali yakuwa ni zawadi. Kama wakiwatunukia kitu katika hayo mahari, basi kuleni kwa raha na kunufaika.

MKIHOFIA KUTOFANYA UADILIFU BASI NI MMOJA

Aya ya 3-4

NAHAU

Makusudio ya herufi Ma hapa ni wanawake, Wafasiri wamekanganywa kuhusu maana yake. Wengine wamefasiri kwa jinsi ya wanawake; wengine, kwa sifa na kuna wengine waliofasiri kwa kitu. Siri ya kubabaika kwao ni kauli ya watu wa Nahau kwamba herufi Ma ni ya kisichokuwa na akili na Man ndiyo ya mwenye akili. Lakini kimsingi ni kuwa Qur'an ni hoja juu ya watu wa Nahau, na wala watu wa Nahau si hoja juu ya Qur'an. Qur'an imetumia herufi Ma kwa mwenye akili katika Aya nyingi. Kama vile:

"Na (kwa) mbingu na aliyeziweka" (91:5)

Nyingine: "Wala nyinyi hamuabudu yule ninayemuabudu" Au kama ilivyotumia Man, kwa kisicho na akili. "Na wengine huenda kwa matumbo yao" (24:45)

Ndio ni kweli kwamba aghlabu ni kutumiwa Ma kwa kisicho na akili na Man kwa mwenye akili, lakini kuwa aghlabu ni kitu kingine na kutowezekana ni kitu kingine. Maunganisho ya wawili wawili na watatu watatu na wanne wanne, yamekuja kwa 'na' na wala sio 'au'. Kwa sababu kila mtu aweza kuwa na hiyari ya idadi anayotaka katika hii iliyotajwa. Lau ingeliunganishwa kwa au ingelikuwa maana yake atakayechagua wawili ndio hao hao, hawezi kuongeza, na mwengine aweze kuchagua watatu tu na pia mwengine achague wane.

MAANA

Na kama mkihofia kutowafanyia usawa mayatima, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili wawili na watatu watatu na wanne wanne.

Msingi wa kuoa wake zaidi ya mmoja hadi kufikia wane umethibitishwa kisheria kwa hukumu ya Qur'an na Hadith na ijmai kwa kauli na vitendo. Bali msingi huu unajulikana kuwa ni katika dharura za dini. Lakini haukuhalalishwa moja kwa moja, bali umewekewa masharti ya kuuhalalisha kwa dharura ya dini vilevile. Hapa kuna swali linalojitokeza; kwamba maana yaliyo wazi katika Aya hii ni kwamba mwenye kuogopa kutofanya uadilifu katika mayatima basi aoe wake wawili, watatu na wane, na kwamba akifanya hivyo hakutobakia dhuluma yoyote. Bila shaka, kama maana yangekuwa haya, ingekuwa sawa na maneno ya kubobokwa, kwani hakuna mfungamano wote kati yake, na Qur'an zimepambanuliwa Aya zake kutoka kwa Mwenye Hekima aliye Mjuzi?!

Jibu la swali hili liko wazi na ni jepesi, isipokuwa kutofautiana majibu ya wafasiri na kugongana kwao, kumemwacha msomaji gizani. Kwa ufupi ni kuwa maneno tangu mwanzo yanahusiana na waliousiwa (mawasii) mayatima, ambao ndio waliokusudiwa katika kauli ya "na wapeni mayatima mali zao wala msibadilishe kibaya kwa kizuri wala msile mali zao" Baada ya kuambiwa haya wenye kufungamana na mali ya yatima, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaambia mawasii jambo jengine litakalofungamana na ndoa ya mayatima ambalo ni "Kama mkihofia kutofanya usawa katika mayatima: Yaani katika ndoa ya mayatima. Neno 'ndoa' limefahamika kutokana na neno basi 'oeni' Huo ni mlango wa kuondoa cha kwanza kinachofahamishwa na cha pili; kama wasemavyo watu wa Nahau.

Kukadiria kwake ni: Ama mambo yanayohusu kuoa wanawake katika mayatima, basi ni juu yenu enyi mawasii, kama mkiwaoa msiwanyime haki zao. Na kama mkihofia kutowafanyia haki kwa kuangalia kuwa wao wako peke yao, hakuna yeyote atakayewatetea, basi waacheni na muoe wengine, Mwenyezi Mungu amewapa nafasi kwa mayatima kama vile alivyowahalalishia wengineo kuoa mmoja, wawili, watatu au wane. Lakini vilevile kwa misingi ya usawa na kama mkihofia kutofanya usawa kwa zaidi ya mmoja, basi oeni mmoja. Kwa maelezo hayo ndio maneno ya Aya yatakuwa yanaungana vizuri, sawa na kumwambia mwenzako. "Ikiwa huli aina hii, kwa sababu unakula sana na kuogopa kuvimbiwa, basi kula aina nyingine, lakini pia usile sana na utajitia kwenye madhara" Kila tamko tutakalo likadiria kwa maana hayo tuliyoyataja, basi yanakubalika nayo.

Imezoeleka kuwa Qur'an inafupisha maneno sana, na kuacha kutaja kila ambacho msomaji anaweza kukifahamu kwa ishara tu. Ikiwa yaonekana wafasiri watakuwa wanababaika, basi hiyo inafahamisha kuwa Aya hii ni ya mkato sana. (hivyo, inababaisha zaidi).

Mkihofia kutofanya uadilifu basi ni mmoja.

Makusudio ya usawa ni uadilifu (usawa) katika mavazi, mahali pa kuishi na mengineyo katika mambo ambayo yako ndani ya uwezo wa mtu. Ama yale ambayo yako nje ya uwezo wake; kama vile moyo kumpenda mmoja zaidi, basi hayalazimishwi usawa. Kwa hivyo basi, ndio tunapata tofauti kati ya Aya hii na ile isemayo:

﴿ وَلَن تَسْتَطِيعُوا أَن تَعْدِلُوا بَيْنَ النِّسَاءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ﴾

"Na hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake (wenu) hata mkijitahidi vipi" (4:129)

Makusudio ya uadilifu katika Aya kwanza ni uadilifu katika kukidhi mahitaji yake, na katika ya pili ni uadilifu wa mapenzi ya moyo.

Unaweza kuuliza : Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajibisha kutosheka na mke mmoja tu, ikiwa kunahofiwa dhuluma katika zaidi ya mmoja. Na kwa dhahiri ni kwamba hofu ya kinafsi mara nyingi hukosea kuliko kupata. Na tumewashuhudia wanaume wengi wanashindwa na matamanio na kuongeza wake halafu wanakabiliwa na matatizo, Kwa hiyo sharti hili si sawa.

Jibu : Mushkeli huu hauepukiki, kama tutakusudia kuhofia hali ya nafsi. Ama ikiwa ni kuhofia hali ya nafasi ya mtu na afya yake, kwamba yeye anaweza zaidi ya mmoja, basi swali halitokuwa na haja.Vitu vya kimaada vya kidhahiri inawezekana kuvidhibiti kwa wepesi; wala katika sheria ya kiislamu hakuna kukadiria hali mahsusi ya mtu anayetaka kuoa wake wengi; kama ilivyo hivi sasa katika baadhi ya miji ya kiislamu.

Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma.

Yaani kuwa na mke mmoja ni karibu zaidi na uadilifu na ni mbali zaidi na kufanya dhuluma. Hii ni ishara ya kuonyesha kuwa, ni juu ya mume kutosheka na mke mmoja, kwa sababu kuwa na zaidi ya mmoja kunaleta matatizo. Katika Tafsir Al-Bayadhawi amesema kuwa baadhi ya wafasiri wamefasiri neno la tau'uluu kutoka neno I'yal ulezi mwingi; kwa maana ya kuwa ni bora mume asioe wake wengi ili asipate tabu na mashaka kwa ajili ya hao wake na watoto, Mwenye Tafsir Al-Manar amesema kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Na amesema Imam Ali:"Ulezi mchache ni moja ya nafuu".

Wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni zawadi.

Makusudio ya zawadi hapa ni ile ambayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameilazimisha kwa mume. Maana yake ni wapeni wanawake mahari yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyalazimisha kuwa ni zawadi sio kununua starehe, Kwa sababu wote wawili wanastarehe.

Kama wakiwatunukia kitu katika hayo mahari yao, basi kuleni kwa raha na kunufaika.

Mahari ni mali ya mke, anaweza kuitumia vile anavyotaka, wala haifai mume au mtu mwengine yeyote kumwingilia kwenye mahari; kama asemavyo Mwenyezi Mungu: "Na mkawa mmempa mmoja wao chungu ya mali, basi msichukue kitu katika hiyo (mali)." Ila ikiwa atatoa ruhusa na kwa radhi yake sawa na mali nyingine.

NDOA YA MITALA (WAKE WENGI)

Uislamu umeweka sharia ya kuoa wake wengi kwa sharti. Hilo halina shaka, wala silo la kufanyiwa utafiti na Ijtihadi. Lakini mlango wa Ijthadi ulio wazi katika kufasiri sharti ya mwenye kutaka kuoa wake wengi, Mujtahid anaweza kusema: Makusudio ya kuhofia ni vile tu mume kufikiria kufanya dhuluma na kutofanya usawa kwa wake wengi. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Mujtahdii huyu itakuwa haiwezekani kuoa wake wengi isipokuwa kwa nadra. Kwa sababu mafikirio haya yako kwa wengi, na yanatiliwa mkazo na ufisadi tunauona katika majumba mengi yaliyo na mke zaidi ya mmoja. Qur'an pia imekwishalidokeza hilo kwa kusema "Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma." Yaani kutosheka na mmoja ni karibu na uadilifu na ni mbali na kufanya dhuluma. Kwa hiyo kufungamanisha kujuzu kuoa zaidi ya mke mmoja, na kusiwe na uonevu na ufisadi ni sawa na kufungamanisha na muhali (jambo lisilo wezekana) kulingana na inavyotokea mara kwa mara.

Jambo la kushangaza ni kwamba wale ambao wana uwezekano wa kuwafanyia uadilifu wake wengi na hali ya afya na mali zinawaruhusu, hawapendelei kuoa mke zaidi ya mmoja na wanaogopa hata kama wanatamani kufanya hivyo. Lakini wale ambao hawatarajiwi kufanya uadilifu kwa namna yoyote ile na kuharibu jamii na kizazi chao kwa kuoa wake wengi, hawa wanajipiga moyo konde kwa kuoa mke zaidi ya mmoja. Na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wanavyuoni wa kidini wanapitisha ndoa za watu hawa, bila ya kusita na hata kuuliza na kupata jawabu, kama kwamba kuoa mke zaidi ya mmoja kumehalalishwa hivi hivi tu, bila ya sharti lolote. Zaidi ya hayo, kuoa mke zaidi ya mmoja si katika wajibu wala sunna katika sharia ya kiislam, isipokuwa uislam umeruhusu kwa mambo maalum na masilahi mahsusi. Lakini maadui wa dini wamewachukulia wale vinukamito (wapendao kuoa sana) ambao hawajali masharti yoyote kuwa ni njia ya kutia ila na kuufedhehi uislam; kama ilivyo kawaida yao kutoa hoja kwa vitendo vya watu kuwa ndio vitendo vya dini na itikadi. Lau kama wangekuwa ni watu wa usawa basi wangelifanya kinyume, na kuitolea hoja dini juu ya watu wafanyao makosa na siyo dini.

Wakati uislam unashartiza mume asioe zaidi ya mke mmoja ila baada ya kuhakikisha kuwa hakutakuweko ufisadi na dhuluma, huko kwenye miji ya Ulaya na Marekani kuna baadhi ya miji wanawake mara nyingi wanatembea na waume wa nje wanaowataka bila ya sharti lolote tena pengine mumewe akiwa anajua. Zaidi ya hayo, bunge la Uingereza mwaka uliopita lilipitisha sheria ya kulawiti na ikaungwa mkono na baadhi ya wakuu wa dini; mji wote ukajaa furaha kwa kuwa wamewahi wao kuendelea na kuwa na mwamko wa kisasa.

Miongoni mwa maajabu ni kwamba Kusini mwa India na sehemu za mpaka wa Kaskazini wanaruhusu mke kuwa kwenye ndoa na zaidi ya mume mmoja; na utaratibu huu bado unaendelea hadi leo([10] ) .