11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO
135. Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa wa karibu. Akiwa ni tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi. Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu. Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo.
136. Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kabla. Na mwenye kumkakataa Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na vitabu vyake na siku ya mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali.
KUWENI IMARA NA UADILIFU
Aya 135 - 136
BAINA YA DINI NA WATU WA DINI
Sijaona Aya katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu inayoambatana na dini ila ninahisi umbali na tofauti iliyopo baina ya dini kama alivyoipanga katika Kitabu chake na dini kama tunavyoitekeleza sisi. Sisi tunazungumzia dini na kuitolea mwito kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba sisi hatuna lolote katika amri yake na ni watumwa wa dini, kama tulivyo watumwa wa Mungu.
Hayo ndiyo tuyatangazayo na kuyaeleza. Lakini dini tunavyoitangaza na tabia zetu tunazodai ni za kidini ni wapi na wapi! Na ni kinyume waziwazi. Na hii haifahamishi chochote zaidi ya kuwa sisi, kwa hakika na hali halisi ilivyo, ni wanafiki, Ni sawa tutambue hivyo au tusitambue.
Lau kama tutaifasiri dini kuwa Mwenyezi Mungu amelipa uwezo baraza la dini litunge sharia za halali na haramu, kama wanavyodai baadhi ya watu wa dini, basi hapo ingelikuwa dini inakwenda sambamba na tabia zetu. Ama tukisema kuwa dini ni ya Mwenyezi Mungu na inatoka kwa Mwenyezi Mungu, kisha tusiende sambamba na hayo katika tabia na vitendo vyetu, basi huo ni unafiki hasa.
Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili najamaa wa karibu.
Katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anasema:
﴿وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا﴾
"Na msemapo semeni kwa uadilifu hata kama ni jamaa wa karibu, Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu"
(6: 152)
Maana yake ni kuwa dini inatuhukumu sisi, baba zetu na watoto wetu; na kwamba ikitokea mgongano baina ya masilahi ya kiutu na dini, basi ni juu yetu kutanguliza ya dini; hata kama hili litapelekea kufa; kama alivyofanya Bwana wa mashahidi Husein bin Ali
Lau mtu atalinganisha hakika hii ya Qur'an na tabia zetu ataona kuwa sisi tunaathirika na masilahi yetu na masilahi ya watu wetu, kuliko masilahi ya dini. Na akiendelea kufanya utafiti zaidi ataamini kuwa kiini cha kwanza na cha mwisho cha dini kwetu ni masilahi na manufaa tu, si Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Hivi ndivyo tulivyo au ndivyo walivyo wengi katika sisi, lakini hatutambui hili wala kulizindukia; Kwa sababu ubinafsi umetawala akili zetu na ukatenganisha hali halisi zetu na nafsi zetu na kutuziba macho tusione haki. Pia imetupa ndoto ya kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni masilahi yetu hasa, vinginevyo si chochote.
Nayasema haya si kwa kumwekea nongwa yeyote au kuwa na msukumo wowote. Kwani mimi, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, sina haja na yeyote katika viumbe vyake Mwenyezi Mungu. Lakini hivi ndivyo ninavyohisi na wanavyohisi wengine wachunga haki.
Mimi nionavyo ni kuwa hakuna budi kuweko na marekebisho ya hisia hii; kama ambavyo ninaitakidi kuwa hakuna dawa ya ugonjwa huu ila kujituhumu sisi wenyewe; na ninaitakidi kuwa sisi ni wa kawaida tu kama wengine tuna hawaa na mapondokeo ambayo ni lazima tujihadhari nayo na tuyahalifu. Ninasema haya nikijua kuwa ni kama kupiga kelele za kutaka msaada jangwani. Kwa sababu ni kilio kutoka kwa nafsi zetu kwenda kwa nafsi zetu, ambazo ndizo adui mkubwa katika maadui zetu.
Akiwa tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anwastahiki zaidi.
Kila mtu katika wanadamu ana hali ya kukubali heri na shari wakati huo huo anaumbile la kuchagua heri kuliko shari, kiasi ambacho lau ataachwa na umbile lake, angelifanya lile analoitakidi kuwa ni heri; wala hawezi kuiepuka ila kwa sababu za nje ya dhati yake na maumbile yake.
Wanavyuoni wa elimu ya sifa za Mwenyezi Mungu wametolea dalili hakika hii kwamba mwenye akili lau atahiyarishwa baina ya kusema uongo apewe pesa, basi angelichagua ukweli kuliko uongo.
Kwa hiyo mwenye akili hasemi uongo ila kwa sababu; kama vile hofu, tamaa, kupendelea jamaa wa karibu, kuchukia adui, kuwahurumia mafukara au kujipendekeza kwa tajiri. Na amesema mkuu wa wasemaji;Akiwa
- wenye kushuhudiwa -ni tajiri au fukara, basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi.
Yaani kwamba yeye ni mwenye kurehmu zaidi mafakiri kuliko sisi na ndiye anayejua maslahi yake na maslahi ya tajiri. Sisi wajibu wetu ni kusema haki tu ni sawa iwe itawasaidia au la.
Ingawaje Mwenyezi Mungu hakutaja sababu zinazosababisha kupotoka zaidi ya kustahiki tajiri au kumuhurumia fakiri, lakini sababu ni ya kiujumla. Haki inapaswa kufuatwa hata kwa maadui wa dini.
Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu.
Yaani, mtakuwa watu wa uadilifu kwa kuacha hawaa na kwenda kinyume nayo. Imesemekana kuwa tafsiri yake ni kukadiria kuchukia kwa maana ya msifuate hawaa mkaacha uadilifu. Yaani nyinyi mnafuata mapenzi kwa kuchukia uadilifu na kwamba Mwenyezi Mungu amewakataza hilo, Lakini tafsiri ya kwanza ndiyo iliyo karibu zaidi.
UADILIFU
Wamehitalifiana mafakihi katika maana ya uadilifu na wakarefusha maneno. Kuna katika wao mwenye kusema, ni dhahiri ya uislam bila ya kudhihirisha ufasiki, Mwingine akasema, ni tabia iliyomo ndani ya nafsi inayopelekea kufanya wajibu na kuacha haram, wa tatu akasema, ni sitara na kujistahi, wa nne akasema ni kuacha madhambi makubwa na kutoendelea na madogo.
Katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Msifuate hawaa ili mfanye uadilifu."
Ni kuonyesha kuwa uadilifu ni kuhalifu hawaa. Amirul-muminin Ali
alimsifu ndugu yake, kwa Mwenyezi Mungu, katika aliyomsifu kuwa;"Alikuwa akijiwa ghafla na mambo mawili huangalia lipi lililo karibu zaidi na hawaa kisha akalikhalifu."
Na akasema:"Mwanzo wa uadilifu wake ulikuwa ni kukanusha hawaa ya nafsi yake."
Amesema Mjukuu wake, Imam Jafar as-Sadiq
:"Ama katika mafaqih atakayekuwa anaichunga nafsi yake, mwenye kuihifadhi dini yake, mwenye kukhalifu hawaa yake, mwenye kutii amri ya Mola wake basi ni juu ya watu kumfuata."
Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo.
Yaani msicheleweshe au kuacha kutoa ushahidi, Kisha akatoa tisho na kiaga kwamba mwenye kuyafanya hayo Mwenyezi Mungu anamjua na atamwadhibu.
Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kabla.
Mtu anaweza kuamini Muumbaji na kukanusha utume na vitabu vya Mwenyezi Mungu. Na anaweza akakubali utume wa baadhi na baadhi ya vitabu; au kukanusha kuwapo Malaika au Siku ya Mwisho.
Aya hii imebainisha nguzo za imani ambazo ni wajibu kuzikubali kila mwenye kuacha shirki na ulahidi na kuziamini zote sio baadhi ya sehemu zake. Nguzo zenyewe ni kumwamini Mwenyezi Mungu na mitume yake yote, vitabu vyake na Malaika wake na pia Siku ya Mwisho.
Kwa hiyo makusudio ya neno 'wale walioamini,' ni wale walioacha ushirikina na ulahidi. 'Na wale walioamini' la pili ni imani ya uhakika, sio kudumu imani na kuthibiti kwenye imani kama walivyosema wafasiri, Makusudio ya Mtume wake, ni Muhammad(s.a.w.w)
. Na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake ni Qur'an na Kitabu alichokiteremshia kabla, ni kila Kitabu cha Mwenyezi Mungu alichokiteremsha kabla ya utume wa Muhammad(s.a.w.w)
Na mwenye kumkakataa Mwenyezi Mungu na Malaika waake na vitabu vyake na Siku ya Mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali.
Aya hii ni dalili wazi kwamba kuamini ghaibu ni nguzo katika nguzo za Kiislamu na kwamba asiyeamini si Mwislamu. Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika sura 2: 285.
﴿إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا ثُمَّ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَّمْ يَكُنِ اللَّـهُ لِيَغْفِرَ لَهُمْ وَلَا لِيَهْدِيَهُمْ سَبِيلًا﴾
137.Hakika wale walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru, hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaghufiria wala kuwaongozea n jia.
﴿بَشِّرِ الْمُنَافِقِينَ بِأَنَّ لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴾
138.Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.
﴿الَّذِينَ يَتَّخِذُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ أَيَبْتَغُونَ عِندَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا﴾
139.Ambao huwafanya makafiri ndio marafiki badala ya waumini, Je wanataka kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.
HAWATHIBITI KWENYE UKAFIRI WALA IMANI
Aya 137 - 139
LUGHA
Asili ya neno Bishara ni habari njema za kufurahisha ambazo zinadhihirisha furaha katika ngozi bashar (bashar) ya uso, Mtu akimwambia mwenzake nakupa bishara basi anajua kuwa kuna jambo la kufurahisha. Halitumiwi neno hilo katika jambo la kuchukiza ila pamoja na kukutana na neno jingine, kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu: Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.
MAANA
Hakika wale walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru, hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaghufiria wala kuwaongozea njia.
Mtu anaweza kuamini dini yoyote miongoni mwa dini au itikadi yoyote katika itikadi, Hapo atashikilia na kujadiliana na watu wa dini nyingine au fikra nyingine kwa ajili ya dini yake. Kisha anasoma na kufanya utafiti ikambainikia makosa. Anaachana na fikra yake ya kwanza na kujiunga na watu wema ambao jana walikuwa ni katika maadui zake wakubwa.
Ni juu ya hawa kumkubali na kumpokea; wala hakuna haki yoyote ya kumwaibisha na kupinga mageuzi yake ya kufuata njia sahihi iliyomdhihirikia. Bali ni wajibu kumsifu na kumtukuza, kwa sababu mtu kuacha makosa ni utukufu na kuendelea nayo ni udhalilifu.
Hii ni ikiwa atathibiti na kudumu kwenye imani yake mpya. Ama akigeuka na kurudia sera yake ya kwanza, kisha akarudi tena, akarudia Akafanya hivi mara nyingi. Huyu ni waj ibu kumtoa na kumtupa. Bali ni wajibu kumwadhibu kwa adhabu kali. Hii ndiyo hali waliyokuwa nayo watu wa dini na wakuu wa madhehebu ya kisiasa tangu zamani na sasa. Kwa sababu kugeukageuka kwake huku kunafahamisha tu, kuwa yeye anafanya masihara na vitimbi na ni mzushi mwongo anayejiingiza katika ufisadi na upotevu na kuzidisha dhambi na upotevu kila anapoingia na kutoka.
Huyu na mfano wake ndio wanaokusudiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu anaposema: "Walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufu ru kisha wakazidi kukufuru" Kwa sababu ya mchezo huu na kujigeuzagueza, Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwasamehe maadam wanayumbayumba na kugeukageuka baina ya ukafiri na imani; wala kuwaongozea njia kwa sababu wamepotea njia kwa kuchagua uovu baada ya kuijua njia na kuifuata.
Kwa ufupi ni kwamba muumin ni yule anayethibiti kwenye imani yake hata hali ikigeuka vipi. Ama yule anayertadi mara kwa mara, basi yeye ana hali mbaya kuliko yule aliyethibiti katika ukafiri na ulahidi.
Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.
Razi anasema: "Mwenyezi Mungu ametumia neno 'bishara' kwa adhabu kwa istihzai sawa na msemo: 'salaam zako ni kipigo."
Ilivyo, ni kwamba mfumo wa Qur'an uko mbali na stihzai. La karibu zaidi ni kwamba makusudio ya bishara ni habari tu na inawezekana kulitumia neno hilo katika jambo la kuchukiza kwa kuambatana na jambo lenyewe; kama tulivyotangulia kueleza katika kifungu cha lugha.
Ambao huwafanya Makafiri ndio marafiki badala ya waumini, Je, wanataka kwao utukufu, basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.
Kila mmoja katika sisi anataka atajike katika maisha haya, Baadhi ya watu wanaweza kupupia kutaka umashuhuri kwa kufanya wema au kwa elimu. Lakini wengine hutaka utukufu na umashuhuri kwa kitu chochote kitakachokuwa; wanauza dini yao kwa shetani kwa ajili ya kupata umashuhuri; humfanya shetani ndio rafiki wa kumsikiliza na kumtii.
Ndipo hapa likaja swali la kusuta na kukanusha kutoka kwa Mola mtukufu kuwa je, wanataka utukufu kutoka kwa shetani na marafiki zake wadhalilifu. Je, utukufu unaweza kupatikana bila ya imani na takua? Uislamu kwa utukufu wake umedhalilisha dini zote, vipi utukufu utatafutwa kwa mwenye kuukanusha?
Waumini waliokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika kauli yake "badali ya waumini" ni wale ambao uislamu umetukuka kwa ajili yao. Kwa sababu wao wameutukuza na kuuweka juu kwa jihadi yao na kujitolea kwao mhanga. Tumezungumzia kuhusu kuwafanya marafiki makafiri katika tafsir (3: 28)
﴿وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ إِنَّكُمْ إِذًا مِّثْلُهُمْ إِنَّ اللَّـهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا﴾
140.Na amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki kwamba mtakaposikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na kuchezwa shere, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo hakika nyinyi mtakuwa mfano wao, Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote katika Jahannam.
﴿الَّذِينَ يَتَرَبَّصُونَ بِكُمْ فَإِن كَانَ لَكُمْ فَتْحٌ مِّنَ اللَّـهِ قَالُوا أَلَمْ نَكُن مَّعَكُمْ وَإِن كَانَ لِلْكَافِرِينَ نَصِيبٌ قَالُوا أَلَمْ نَسْتَحْوِذْ عَلَيْكُمْ وَنَمْنَعْكُم مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ فَاللَّـهُ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَن يَجْعَلَ اللَّـهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا﴾
141.Ambao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, huseme: Je hatukuwa pamoja nanyi. Na ikiwa Makafiri wamepata sehemu, husema: hatukuwa ni waweza wa kuwashinda tukawakinga na waumin? Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu siku ya kiyama na Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumini.
MSIKAE NAO MPAKA WAINGIE KATIKA UZUNGUMZI MWINGINE
Aya ya 140 - 141
MAANA
Na amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki kwamba mtakaposikia za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na kuchezwa shere, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine.
Aya hii ilishuka Madina, inawakumbusha waislamu Aya iliyoshuka Makka isemayo:
﴿وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴾
"Na unapowaona wale ambao wanaziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine; na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae baada ya kukumbuka pamoja na watu wadhalimu."
(6:68)
Ama sababu ya ukumbusho huu ni kuwa baadhi ya Waislamu - kama ilivyoelezwa Katika Tafsiri mbali mbali - walikuwa wakikaa katika vikao vya washirikina huko Makka waliokuwa wakingilia kumtukana Muhammad(s.a.w.w)
na kuicheza shere Qur'an. Waislamu wakati huo walikuwa wanyonge hawawezi kuwakanya; ndipo ikashuka Aya hiyo (6: 68), kuwahadharisha waislamu waepukane na washirikina na kuwaamrisha wasikae nao wanaposikia kufru na kuchezwa shere Aya za Mwenyezi Mungu.
Siku zikapita na waislamu wakahamia Madina; huko nako kulikuwa na mayahudi na wanafiki, waliodhihirisha uislamu na kuficha ukafiri. Baadhi ya waislamu wakarudia mwenendo wao wa kwanza, wakakaa na mayahudi na wanafiki waliokuwa wakiutusi uislamu na Mtume wake; ndipo ikashuka Aya hii, ambayo tunaifasiri, ili kuwakumbusha waislamu Aya ile iliyoshuka Makka na kuwaamrisha kujitenga nao.
Sababu yoyote ya kushuka Aya itakavyokuwa au wanaoambiwa, itakuwa Aya ni ya ujumla inayofahamisha wajibu wa kujitenga na kila mwenye kuingia katika mazungumzo ya batili. Wajibu huu hauhusiki na ambaye alikuwa akikaa na makafiri Makka au na wanafiki Madina tu, ingawaje iko katika kuhusika si kwa ujumla. Hadith inasema: "Upweke ni bora kuliko rafiki mwovu." Nyingine inasema: "Tahadharini na kukaa na maiti." Akaulizwa ni akina nani hao maiti? Akasema: ni kila mwenye imani potofu, dhalimu katika hukumu. Katika Nahjul Balagha imeelezwa: "Kukaa na watu wapuuzi kunasahaulisha imani na kumkurubisha shetani."
Hivyo hakika nyinyi mtakuwa mfano wao.
Mwenye kuridhia ukafiri ni kafiri, na mwenye kurdhia dhambi naye ana dhambi kwa namna yoyote atakayokuwa; kwa maafikiano ya mafakihi na Maulama. Imekuja Hadith Mutawatir isemayo: Mwenye kufanya dhulma, mwenye kumsaidia na mwenye kuiridhia ni washirika," hasa mwenye kuridhia ukafiri. Katika Nahjul-Balagha imeelezwa: "Mwenye kuridhia vitendo vya watu ni kamamwenye kuingia ndani yake na kila mwenye kuingia ana dhambi mbili: dhambi ya kutenda na dhambi ya kuridhia."
Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote katika Jahannam. Ambao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema; Je, hatukuwa pamoja nanyi? Na ikiwa makafiri wamepata sehemu, husema: hatukuwa ni waweza wa kuwashinda tukawakinga na waumin.
Aya hii inachora picha ya hali ya wanafiki wakati wa vita vya waislamu na washirikina. Kwa ufupi picha yenyewe ni kwamba wanafiki walikuwa wakitoka pamoja na waislamu katika kwenda vitani ili wakaharibu na kuchafua safu za waislam.
Wakati huo huo wanajionyesha kuwa wao wametoka kuwasaidia waislam; na kungoja, ikiwa ushindi ni, waislamu wakisema 'sisi tuko pamoja nanyi kwa hiyo sisi na nyinyi ni washirika katika ngawira.' Ikiwa ushindi ni wa washirikina husema, "sisi tulikuwa majasusi" Basi yako wapi malipo? Wanaishika fimbo kati kati.
Ufasaha zaidi niliousoma kuhusu wasifu wa wanafiki, ni ule aliousema Amirulmumiinin Ali
:"Wameiandalia kila haki batili, na kila msimamo upotofu, na kila mlango ufunguo, na kila usiku taa."
Hawa wapo kila siku na idadi yao inaongezeka katika miji ya kiarabu siku hadi siku, tangu ilipojitokeza dhahabu nyeusi (petrol). Wakafanya uzalendo kuwa ni nembo kama walivyojionyesha waislamu wakati wa Mtume. Wapigania ukombozi wakiwashinda wanyonyaji na walanguzi, wanafiki huwaambia: Je, hatukuwa pamoja nanyi? Na kama wanyonyaji wakifanikiwa huwaambia: Je, hatukuwazuia wapigania ukombozi wasiwafikie.
Unaweza kuuliza
: Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametumia ushindi kwa waislamu na kupata sehemu kwa makafiri?
Jibu
: Ushindi wa waislam ndio ushindi wa haki ambao unadumu na kubaki maadamu watu wake wanafuata desturi ya Mwenyezi Mungu na amri yake katika kujiandaa.
Kwa hiyo ikanasibu kuleta ibara ya ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ama ushindi wa batili ni ushindi wa muda usiodumu, unaondoka mbele ya watu wa haki, kama wakiungana kwa Jihadi. Walikwishasema zamani; "Dola ya batili ni saa moja na dola ya haki ni mpaka Kiyama."
Wala Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumin.
Mafakihi wameitolea dalili Aya hii kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuweka sharia inayofanya mamlaka au usimamizi wa asiyekuwa mwislamu kwa mwislamu; Na wameitolea hukumu nyingi; kama vile kuwa baba wa mtoto akiwa mwislamu na mama yake sio mwislamu, mama hana haki ya kumlea. Kwa sababu mtoto hufuata dini iliyo tukufu zaidi anayoifuata mmoja wa wazazi wawili na hukumu yake ni hukumu ya waislamu.
Hukumu nyingine ni kuwa haijuzu kwa mwislamu kuwausia watoto wake wasimamiwe na asiyekuwa mwislmau; na akifanya hivyo basi wasia umebatilika. Hukumu nyingine waliyoitoa katika Aya hiyo ni kuwa, baba anakuwa na usimamizi kwa watoto wake kama wana dini moja.
Ama wakiwa ni waislamu na baba si mwislam hatakuwa na usimamizi juu yao. Nyingine ni kuwa hukumu ya hakimu asiyekuwa mwislamu haitekelezwi kwa haki ya mwislamu, hata kama ni haki na mengine mengi.
﴿إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا﴾
142.Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye menye kuwahadaa. Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu. Wanajionyesha kwa watu Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.
﴿مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَٰلِكَ لَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَلَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ سَبِيلًا﴾
143.Ni vizabizabina baina ya huku na huko. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea huwezi kumpatia njia
WANAMHADAA MWENYEZI MUNGU NA ATAWALIPA KWA KUHADAA KWAO
Aya 142 - 143
MAANA
Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye menye kuwahadaa.
Makusudio ya kuhadaa kwao ni kule kuonyesha imani kwa Mtume na kuficha ukafiri, Kwa sababu mwenye kumhini Mtume ndio amemhini Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
﴿إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّـهَ﴾
"Hakika wale wanaokuunga mkono kwa hakika wamemuunga mkono Mwenyezi Mungu"
(48: 10)
Makusudio ya kuwa Mwenyezi Mungu anawahadaa ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaadhibu kwa hadaa yao na unafiki wao.
Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu.
Wataichangamkiaje na wao wanaikanusha? Hawatarajii thawabu kwa kuitenda wala adhabu kwa kuiacha; isipokuwa wanaitekeleza kwa kuwinda dunia tu na kuifanya ni nyanzo ya uchumi. Mwenyezi Mungu anasema:
"Kwa hakika hiyo Swala ni ngumu isipokuwa kwa wanyenyekevu"
(2:45)
Unaweza kuuliza
: Mtu akiswali kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na pamoja na hayo anapenda watu wamuone, ili wamhisabu katika watu wema au asituhumiwe kuwa aniipuuza dini. Je hii itakuwa ni ria?
Jibu
: Hapana! Maadamu msukumo wa kwanza ni wa amri ya Mwenyezi Mungu na radhi zake; mengine yanafuatia tu, Imam as-Sadiq
aliulizwa kuhusu mtu ambaye anafanya jambo la kheri, kisha akafurahi kwa kuonwa na mtu mwingine akilifanya jambo hili (nini hukumu ya mtu huyo)? Imam akajibu:"Hapana ubaya kwa hilo, ikiwa hakuifanya kwa hilo, kwani hakuna mtu asiyependa Mwenyezi Mungu amdhihirishie kheri mbele ya watu,.."
Wanajionyesha kwa watu.
Kwa sababu wao huswali kwa ajili ya kuwinda na kupata faida.
Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.
Yaani wakati wa kujionyesha kwa watu. Ama wakiwa peke yao, hawamtaji kabisa. Imam Jafar as-Sadiq
anasema: "Mwenye kujionyesha (ria) ana alama tatu: Anakuwa mvivu akiwa peke yake, anachangamka akiwa na watu na hupenda kusifiwa kwa asilolifanya."
JE WATU WOTE HUJIONYESHA
Unaweza kuuliza
: Hakuna yeyote anayedhihirisha ukweli wake kwa watu na kuwaambia kila analoitakidi, Ni nani anayeweza kumwambia kila mtu anayoyajua. Na akifanya hivyo, basi atahisabiwa katika wenda wazimu, bali ni nani ambaye - mara nyingine - hafanyi asiyoyapenda na kuyataka? Kisha utaziepuka vipi desturi na maadili ya jamii? Je, unaweza kumwambia mtu uliyekutana naye, ambaye humpendi, akakwambia 'natamani kukuona,' na wewe umwambie: nachukia kukuona? Na kama utamwambia hivyo je unavyoona wewe au waonavyo watu utakuwa uko sawa? Mwisho je watu wote wanafanya ria (kujionyesha), kwa sababu hawaitakidi yote wayasemayo; wala hawaamini yote wayafanyao?
Jibu
: Kuna tofauti baina ya Ria na Mudarat. Ria ni kudhihirisha unafiki na uzushi ili uwe pamoja na wema na wewe si katika wao.
Na Mudarat ni kuwa mpole na kutowachukilia na kuamiliana na watu bila ya kulenga chochote zaidi ya kutaka kuishi nao katika uelewano na maafikiano.
Ni kweli kuwa mara nyingine unafanya mambo kufuata desturi ya jamii; ukapongeza, kutoa rambi rambi au kutabasamu na kumheshimu mtu kwa jamala tu si kwa kuamini, lakini jambo hili ni salama halina tashwishi yoyote.
Wala halihisabiwi kuwa ni ria maadam kulifanya kwako kunaafikiana na jamii. Vilevile si wajibu juu yako kama utatokewa na kosa - hakuna maasum - kulitangaza kwa watu. Ndio ni wajibu kuwadhihirishia usafi sio makosa.
Vilevile ni kweli kuwa unasema uongo unapomwambia unayemchukia 'mimi nakupenda,' lakini ni uongo ulio katika masilahi na hulka njema. Mwenyezi Mungu anasema:"Na semeni na watu kwa uzuri"
(2: 83)
﴿أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ﴾
"Je hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri mizizi yake ni imara na matawi yake yako mbinguni"
(14:24)
﴿ اذْهَبَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٤٣﴾ فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ ﴾
"Nendeni kwa firaun hakika yeye amepetuka mpaka, Kamwambieni maneno laini huenda akaonyeka au akaogopa"
(20: 43 - 44)
Kuna Hadith isemayo: "Tamko jema ni sadaka, hupewa thawabu alisemaye, thawabu za wenye fadhila na ihsan." Hadith nyigine inasema: "Ameniamrisha Mola wangu kuwachukulia watu upole (Mudarat), kama alivyoniamrisha faradhi (wajib)."
Wamekongamana mafakihi kwamba uongo ni wajibu ikiwa utakuwa ni kutetea nafsi isiyo na hatia na kuiepusha na maangamivu. Na kwamba ukweli ni haram katika ufitini na usengenyaji. Kwa hiyo mfitini ni mkweli na msengenyaji ni mkweli, lakini wanashutumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele za watu
.
Baada ya yote hayo ni kwamba ria ya haramu ni ile ya kudhihirisha mambo asiyokuwa nayo mbele za watu; anajionyesha kuwa ana kheri ili apate hadhi ya watu wema na huku mwenyewe ni katika waovu wafisadi.
Ni vizabizabina baina ya huku na huko
, Mara wanajidhihirisha wako pamoja na waislamu na mara wako pamoja na makafiri; na wao hasa ilivyo nikuwa: hawako kwa hawa wala hawako kwa wale bali wako kwenye manufaa yao na tamaa zao; wanabusu mkono wowote wenye manufaa kwao uwe mchafu au msafi.
Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea huwezi kumpatia njia.
Yaani Mwenyezi Mungu anamwepuka na kumwachia mwenyewe kwa sababu ya inadi yake na kupinga kwake haki, Na ambaye mambo yake yako hivi, basi hatarudi kwenye uongofu.
Na hapana budi kuzingatia kuwa hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inasababisha kutomuacha mja wake; kama ambavyo mzazi hamwachi mtoto wake. Ila ikiwa mja mwenyewe ndiye aliyesababisha kuachwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya kumwasi; kama ambavyo mama anaachana na mwanawe kwa sababu ya kumwudhi sana.
Imetangulia Aya kama hii, herufi kwa herufi katika Sura hii. Aya 88 na tumeizungumzia kwa ufafanuzi kama ambavyo tulifafanua mafungu ya uongofu na upotevu katika kufasiri (2: 26)
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ أَتُرِيدُونَ أَن تَجْعَلُوا لِلَّـهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا مُّبِينًا ﴾
144.Enyi mlioamini! Msiwafanye Makafiri kuwa marafiki badala ya waumini, Je, mnataka awe nayo Mwenyezi Mungu hoja dhahiri juu yenu.
﴿إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا﴾
145.Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini mtotoni. Hutakuta kwa ajili yao msaidizi.
﴿إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَاعْتَصَمُوا بِاللَّـهِ وَأَخْلَصُوا دِينَهُمْ لِلَّـهِ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ وَسَوْفَ يُؤْتِ اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ أَجْرًا عَظِيمًا ﴾
146.Ila wale waliotubu na wakatengeza (mwendo wao) na wakashikamana na Mwenyezi Mungu na wakamtakasia Mwenyezi Mungu dini yao, basi hao watakuwa pamoja na waumini na Mwenyezi Mungu atawapa waumini malipo makubwa.
﴿مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ وَكَانَ اللَّـهُ شَاكِرًا عَلِيمًا ﴾
147.Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kupokea shukrani Mjuzi.
MSIWAFANYE MAKAFIRI KUWA MARAFIKI
Aya 144 - 147
MAANA
Enyi mlioamini! Msiwafanye Makafiri kuwa marafiki badala ya waumini.
Imetangulia Aya hii pamoja na tafsir yake katika (3:28)
Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyowazi juu yenu?
Kila asiyekuwa na ubainifu wa dini yake au kupomoka na njia ya uongofu baada ya kumbainikia, basi yeye mwenyewe amempa Mwenyezi Mungu hoja nzuri juu yake mwenyewe.
Hebu tusome dua hii:"Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika sisi tunakiri kwamba wewe huadhibu ila baada ya kusimamisha hoja. Vile vile tunakiri kuwa hoja imetusimamia, bali tunagwaya na kutetemeka kwa kuhofia mashiko yako na tunataka hifadhi yake kwa msamaha wako na utukufu wako. Kwa hiyo hakuna haja ya kusimama mbele zako kwa kuhukumiwa na kuhisabiwa au kuchunguzwa."
Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini motoni. Hutakuta kwa ajili yao msaidizi.
Kwa sababu adhabu iko kwa kiasi cha kosa, na hakuna kosa kubwa kuliko unafiki ambao umekusanya ukafiri na uongo. Yote mawili ni mama wa maovu.
Ila wale waliotubu na wakatengeneza (mwendo wao) na wakamtakasia Mwenyezi Mungu dini yao; basi hao watakuwa pamoja na waumini. Na Mwenyezi Mungu atawapa waumin malipo makubwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutoa kemeo na kiaga cha adhabu kali kwa wanafiki, anawaongoza kwenye toba, njia ya uokofu na kuokoka, njia pekee ya kutaka nusura na shufaa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hilo liko mikononi mwao na katika uwezo wao. Mwenye kuzembea, basi na ajilaumu mwenyewe. Hii ni hoja nyingine kwa kila mwenye dhambi, anayoiongezea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye hoja zake sahihi ambazo hazina idadi.
Tumeweka mlango mahsusi wa toba na wenye kutubia wakati wa kufasiri Aya 18 katika Sura hii.
Wafasiri wamerefusha maneno katika kubainisha tofauti katika viunganishi vilivyo katika Aya hii waliotubu, wakatengeneza (mwendo wao), wakashikamana na Mwenyezi Mungu na wakamtakasia Mwenyezi Mungu dini yao; Tuonavyo sisi ni kuwa neno toba linakusanya sifa zote hizi kwa ukamilifu wake; wala hatuoni tofauti ya kimsingi baina yao; isipokuwa yamekuja kwa kutilia mkazo kuonyeshwa yale waliyokuwa nayo wanafiki - kubabaika na kuasi, na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubali toba yao wala hatawaingiza katika hisabu ya waumini ila wakiwa na uthabiti na kuendelea na toba; na wao wakirtadi baada ya toba na wakatenda kama wanavyotenda, basi kurtadi kwao kutaongezea ukafiri wao, uzushi wao na ubabaikaji wao. Hakuna malipo ya kurtadi ila kifo duniani na adhabu chungu huko Akhera.
MWENYEZI MUNGU NA UNYENYEKEVU WA IMAM ZAINUL ABIDIN
Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini?
Kabisa hana haja! Yeye anajitosheleza na kila kitu katika dhati yake na sifa zake vinginevyo basi asingeweza kuumba; isipokuwa anapatiliza na kuadhibu kwa malipo yenye kulingana. Wala hamhitajii kiumbe katika kupatikana kwake na kubaki kwake na katika harakati zake zote.
Sasa msomaji hebu tusikilize unyenyekevu na utukuzo ulio katika munajat huu utokao kwa Imam Zainul Abidin: "Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika mimi ni mtu duni na mawazo yangu ni mepesi; wala adhabu yangu haiongezi chembe katika milki yako. Lau adhabu yangu ingelikuwa inazidisha kitu katika milki yako, basi ningekuomba univumilie na ningependa iwe hivyo kwako, lakini ufalme wako ni mkuu zaidi usioweza kuongezewa kitu na utiifu wa wenye kutii au kupunguzwa na maasi ya wenye dhambi."
Munajat huu sio alama tu ya kuonyesha upeo wa mapenzi na shauku juu ya wema wa Mwenyezi Mungu na utakatifu wake; kama wafanyavyo masufi, wala sio dua tu ya kuhofia adhabu ya Mwenyezi Mungu hata kama dhahiri ya maneno inafahamisha hivyo, isipokuwa ni maelekezo kwa kila mwenye nguvu anayetaka kuwakaba wanyonge wasio na uwezo na kwamba lililo bora kwa uwezo wake juu ya wanyong e ni msamaha, na wala sio kuadhibu na kutesa.
Nguvu haziwezi kuwa bora na kamilifu ila kwa kusamehe. Hakika kuhitajia au ukorofi ndio unaosababisha kumtesa asiyekuwa na kimbilio ila kwa mwenye nguvu. Na mwenye nguvu aliye mkamilifu hahitajii wanyonge, ni Mwenye kujitosheleza Mwenye kutakata na upungufu.
Baada ya yote hayo; hakika msamaha ni bora, sisi tuna haja nao na Mwenyezi Mungu ni muweza nao na wala hakuna zaidi kuliko Yeye. Kwa hiyo basi msamaha wake uko. Tunasema haya na sisi tukiwa miongoni mwa wanaomwogopa Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kupokea shukrani Mjuzi.
Anamjua mwenye kumtii na mwenye kushukuru na humlipa ujira wa watiifu wa wenye kushukuru. Tumemwamini Mwenyezi Mungu peke yake. Twanyenyekea tukimwambia Yeye (s.w.t) atuwafikishe kumshukuru na kumtii.
MWISHO WA JUZUU YA TANO
12
SHARTI YA KUCHAPA
au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini
ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini