5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO
﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴾
60.Je, huwaoni wale wanaodai kuwa wao wanaamini uliyoteremshiwa wewe na yalioteremshwa kabla yako, wanataka kwenda kuhukumiana kwa taghut na hali wameamrishwa wamkatae. Na Shetani anataka kuwapoteza upotevu wa mbali.
﴿وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا ﴾
61.Na wakiambiwa njooni kwenye yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kwa Mtume, utawaona wanafiki wanajizuia na kukupa mgongo.
﴿فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَاءُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا ﴾
62.Basi itakuwaje watakapopatwa na msiba kwa yaliyotangulizwa na mikono yao kisha wakakujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu (wakisema): Hakika sisi hatukupendelea ila wema na mapatano.
﴿ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَعْلَمُ اللَّـهُ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَعِظْهُمْ وَقُل لَّهُمْ فِي أَنفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا ﴾
63.Hao ni ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nyoyo zao. Basi achana nao na uwape mawaidha na uwaambie maneno yatakayoingia katika nafsi zao.
WANATAKA KUHUKUMIANA KWA UBATILIFU
Aya 60 - 63
MAANA
Je, huwaoni wale wanaodai kuwa wao wanaamini uliyoteremshiwa wewe na yaliyoteremshwa kabla yako, wanataka kwenda kuhukumiana kwa taghuti na hali wameamrishwa wamkatae.
Je huwaoni, ni msemo unaoelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w)
kwa njia ya swali ukiwa na makusudio ya kustaajabia hali ya wanafiki, walioficha ukafiri na kudhihirisha uislam na kuamini vitabu vya Mwenyezi Mungu. La kustaajabu ni kwamba wao wanajikadhibisha wenyewe; pale walipokataa kuhukumiwa kwenye haki na kwenda kwenye batili; pamoja na kuwa uislam umewaamrisha kujiepusha na upotevu na wabatilifu.
Mwenye Majmaul-bayan, anasema: aligombana yahudi na mnafiki katika waislam, yahudi akasema: "Tukahukumiwe kwa Muhammad" Kwa sababu alikuwa anajua kuwa Muhammad hakubali rushwa wala hafanyi dhulma. Mnafiki akasema: "Si yuko Kaabul-Ashraf," (yahudi) kwa sababu alijua kuwa Ka'ab anachukua rushwa na anadhulumu katika hukumu.
Pamoja na kuwa wafasiri hawathibitishi sababu ya kushuka Aya hii, hatuoni mfano unaofasiri makusudio ya Aya ulio wazi kuliko tukio hili aliolitaja mwenye Majmaul-bayan. Mnafiki alikataa kuhukumiwa na Mtume(s.a.w.w)
, kwa sababu anamkanusha yeye na dini yake. Ama yahudi anaamini uyahudi, lakini pamoja na hayo alikataa kuhukumiwa kwa yahudi mwenzake na akataka kuhukumiwa kwa Mtume(s.a.w.w)
pamoja na kuwa anamkanusha yeye na dini yake, Siri ilikuwa ni manufaa tu. Dhahiri hii haihusiki na yahudi tu, yeyote mwenye kupata manufaa katika dini au msingi wowote, haitakikani kumtegemea wala dini yake ila baada ya mitihani. Kwa sababu watu wengi wanakabidhiwa maelfu na kuishi vizuri, si kwa lolote ila kwa kuaminiwa tu. Huenda hao ndio wanaoambiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ﴾
" Na miongoni mwa watu kuna wanaomwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni. Ikiwafika kheri hutulia kwayo na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amepata hasara ya dunia na khera"
(22: 11)
Imam Ali
amesema: "Sifa ni baada ya misukosuko." Mtoto wake, Husein
naye anasema:"Watu ni watumwa wa dunia, dini iko juu juu tu ya ndimi zao. Wakipatwa na misukosuko huwa wachache wenye dini"
Mtume Mtukufu naye alikuwa akisema katika raha:"Sifa njema ni za mwenye kuneemesha mwenye kuzidisha." Na wakati wa shida husema: "Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu kwa kila hali."
Akionyesha kuwa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu yuko radhi kwa aliyokadiriwa hata katika hali hii; sawa na mtoto mwema anayebakia kumsafia nia mzazi wake hata katika hali ya kutiwa adabu. Na mjukuu wake Imam Zainul-abidin
alikuwa akisema miongoni mwa anayoyasema anapopatwa na shida:"Ewe Mola wangu! Ni ipi katika ya hali mbili ambayo nina haki zaidi ya kukushukuru? Ni ipi kati ya nyakati mbili ambayo ni bora zaidi kukusifu? Je ni wakati wa uzima uliponipa afya; au ni wakati wa ugonjwa uliponipata? Ewe Mola wangu! Jaalia kutoka kwangu kwenye ugonjwa kuwa ni msamaha wako na kusilimika kwangu na shida hii kuwa ni faraja iliyotoka kwako"
Na shetani anataka kuwapoteza upotevu wa mbali.
Hii ni dalili ya wazi kwamba shari inatokana na shetani si kwa Mwenyezi Mungu. Na kila fikra inayokupelekea kufanya shari huitwa shetani. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:Ambaye hutia wasiwasi katika nyoyo za watu katika majini na watu.
(114: 5 - 6)
Na kuna Hadith isemayo: "Shetani akikwambia: Ni wingi ulioje wa swala yako! Mwambie, kughafilika kwangu ni zaidi. Na akikwambia ni wingi ulioje wa mema yako! Mwambie maovu yangu ni zaidi. Na akikwambia ni wingi ulioje wa waliokudhulumu mwambie: Nilio wadhulumu ni wengi zaidi." Kwa dhahiri ni kuwa nafsi ndiyo inayompa picha mtu kwamba yeye ni mfanya ibada sana, mtenda mema na mwenye kudhulumiwa. Wala hahadaiki kwa ubatilifu huu ila mjinga.
Na wakiambiwa njooni kwenye yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kwa Mtume utawaona wanafiki wanajizuia na kukupa mgongo.
Kwa sababu wao hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Mtume wake wala kitu chochote isipokuwa dunia.
Basi itakuwaje watakapopatwa na msiba kwa yaliyotangulizwa na mikono yao.
Na msiba mkubwa zaidi kwa wanafiki ni kufunuka mambo yao na kufichuka siri yao hadharani, ambapo wanajulikana na watu kwa hiyana, uongo, vitimbi, hadaa, woga na utwevu.
Kisha wanakujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu (wakisema): Hakika sisi hatukupendelea ila wema na mapatano.
Wanamjia Mtume wakinyenyekea wakitoa sababu za uongo; na Mwenyezi Mungu, Mtume wake, na watu wanajua kwamba wanafiki ni waongo na kwamba wao wanafanya viapo vyao ni ngao ya fedheha na kuadhibiwa. Basi achana nao. Yaani wapuuze, usiwakubalie udhuru kwa sababu wao wanachukulia kukubali kwako huku katika malengo yao. Wala usiwaadhibu kwa sababu wametoa udhuru japokuwa kwa dhahiri. Na wape mawaidha na waambie maneno yatakayoingia katika nafsi zao. Mtume(s.a.w.w)
alikuwa akiwaamuru kumcha Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo wanahisi kuwa wao ni wakosaji na kwamba ni juu yao kujisafisha kwa kutubia. Huu ndio msingi wa uislamu kwa kila mwenye makosa, haumfanyii haraka kumwadhibu wala kumkatisha tamaa, bali hutumia njia zote za kumtengeneza. Mwenyezi Mungu anasema:
﴿ اذْهَبَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٤٣﴾ فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ﴾
"Nendeni kwa Firaun, hakika yeye amepetuka mipaka, Kamwambieni maneno laini huenda akawaidhika au ataogopa"
(20: 44)
Imam, Amirul-muminin
anasema:"Fakihi aliyekamilika ufakihi wake, ni yule asiyewakatisha tamaa watu na rehema ya Mwenyezi Mungu na asiyewavunja moyo kabisa na rehma ya Mwenyezi Mungu na kutowapa amani ya kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu."
Chimbuko la hekima hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿ قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ﴾
"Sema: enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu"
(39:53).
﴿ وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا ﴾
64.Na hatukumpeleka Mtume ila atiiwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Na lau kwamba wao walipojidhulumu wangekujia wakaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu na wakaombewa maghufira na Mtume, wangelimkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kutakabali toba na mwenye kurehemu.
﴿
فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴾
65.Naapa kwa Mola wako! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu katika yale wanayohitalifiana baina yao. Kisha wasione dhiki katika nyoyo zao kwa uliyohukumu na wanyenyekee kabisa kabisa.
﴿ وَلَوْ أَنَّا كَتَبْنَا عَلَيْهِمْ أَنِ اقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ أَوِ اخْرُجُوا مِن دِيَارِكُم مَّا فَعَلُوهُ إِلَّا قَلِيلٌ مِّنْهُمْ وَلَوْ أَنَّهُمْ فَعَلُوا مَا يُوعَظُونَ بِهِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ وَأَشَدَّ تَثْبِيتًا﴾
66.Na lau kama tungewalazimisha kuwa jiueni au tokeni katika miji yenu, wasingelifanya hilo isipokuwa wachache katika wao. Na lau kama wangelifanya yale waliyoagizwa, ingelikuwa heri kwao na uthibisho wa nguvu zaidi.
﴿ وَإِذًا لَّآتَيْنَاهُم مِّن لَّدُنَّا أَجْرًا عَظِيمًا ﴾
67.Na hapo tungewapa malipo makubwa kutoka kwetu.
﴿ وَلَهَدَيْنَاهُمْ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا﴾
68.Na tungewaongoza njia iliyonyooka.
﴿ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا﴾
69.Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema, Na hao ndio marafiki wema.
﴿ ذَٰلِكَ الْفَضْلُ مِنَ اللَّـهِ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ عَلِيمًا ﴾
70.Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu, Na anatosha Mwenyezi Mjuzi.
HATUKUPELEKA MTUME ILA ATIIWE
Aya 64 - 70
MAANA
Na hatukumpeleka Mtume ila atiiwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Unaweza kuuliza
: Habari hii ni kama kufafanua ufafanuzi. Kwa sababu kumtegemeza Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenyewe kunafahamisha kuwa amepelekwa ili atiiwe, vinginevyo kutegemezwa kusingelikuwa na maana, Basi je ubainifu una makusudio gani?
Jibu
: Makusudio ni kutoa hoja kwa wanafiki waliomwasi Mtume na kukataa kuhukumiwa naye. Hoja yenyewe ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewabainishia wanafiki na wengineo katika Aya hii kuwa kumwasi Mtume sio kumwasi yeye hasa, bali ni kumwasi Mwenyezi Mungu. Ambapo amekataa mambo yasipitie isipokuwa kwenye desturi yake, Na miongoni mwa desturi ni kufikisha hukumu zake kwa waja wake kupitia Mtume atokanaye na wao.
Kwa hiyo basi mwenye kumpinga katika anayoyafikisha miongoni mwa hukumu za Mwenyezi Mungu,atakuwa amempinga Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo natija ni kuwa wanafiki na kila anayemwasi Mwenyezi Mungu wanastahili adhabu. Kwa sababu wanamwasi na kumkhalifu Mwenyezi Mungu.
Na lau kwamba wao walipojidhulumu wangekujia wakaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu na wakaombewa maghufira na Mtume, wangemkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kutakabali toba mwenye kurehemu.
Wamejidhulumu pale walipojiingiza katika adhabu na maangamizi kutokana na dhambi walizozifanya. Wamemdhulumu Mwenyezi Mungu vilevile kwa kupetuka mipaka yake na kuasi amri zake. Pia wamemdhulumu Mtume kwa kuwa wao wamekataa hukumu yake na kuridhia hukumu ya ubatilifu na kumwonyesha kinyume na dhamira zao.
Pamoja na yote hayo bado Mwenyezi Mungu amewafungulia mlango wa toba. Ni juu yao basi kuuelekea na kutaka maghufira, Wakifanya hivyo atawaingiza kwenye rehema yake. Na wakitofanya, basi hawatapata wa kuwanusuru wala wa kumsaidia zaidi ya Mwenyezi Mungu.
Unaweza kuuliza
: kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu, Na wakaombewa maghufira na Mtume; inapingana na misi ngi ya kiislam ambayo inapinga kuwe na wasita baina ya Mwenyezi Mungu na watu?
Jibu
: Ni kweli kuwa hakuna wasita baina ya Mwenyezi Mungu na waja wake ila katika mambo yanayorudia kwenye haki yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumkosea Yeye.
Ama kukosea haki za watu, basi amri ni yao; na msamaha wake unaombwa kwao si kwengine. Na wanafiki walimwudhi Mtume na kumkosea haki yake. Hivyo ikawa hakuna budi katika toba yao ila kudhihirisha majuto kwake na kumwomba msamaha. Na kila unayemdhihirishia kinyume cha dhamira yako basi umemdhulumu na kumkosea. Bali lau mtu fulani alikudhania sifa nzuri usizo nazo na akakuamini kisha ukamfanya mjinga na tena ukamkimbia, basi wewe ni dhalimu.
Naapa kwa Mola wako! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu katika yale wanayohitalifiana baina yao.
Kwa sababu hukumu zote anazozitamka Muhammad, hazitokani na yeye, isipokuwa zinatoka kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na yeye Mtume ni mse- maji wake.
Kisha wasione dhiki katika nyoyo zao kwa uliyohukumu na wanyeyekee kabisa kabisa.
Maana yake ni kuwa wao hawatakuwa waumini mpaka wajue kwa yakini kwamba hukumu yake ni hukumu ya Mwenyezi Mungu hasa, na anayekupinga wewe ndio amempinga Mwenyezi Mungu. Ni muhali kwa Muumin wa kweli kuhisi dhiki kwa hukumu anayojua kuwa inatokana na Mwenyezi Mungu.
Ndio ni kweli muumin anaweza kutaka baina ya nafsi yake kuwa kula mchana mwezi wa Ramadhan kuwe halali, lakini pamoja na hayo anafunga na kujizuilia kula kwa kuhofia adhabu ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kali na ya mashaka zaidi ya kufunga. Na huenda nafsi yake ikamshinda na maasi, lakini yeye anavumilia na kuilaani, kwa sababu itakuwa imepuuza haki, Hii ndiyo imani hasa.
Na lau kama tungewalazimisha kuwa jiueni au tokeni katika miji yenu, wasingefanya hilo isipokuwa wachache katika wao.
Hakika dini ya Mwenyezi Mungu ina wasaa, nyepesi na ni bora na ya utengenefu. Haimkalifishi yeyote zaidi ya uwezo wake, bila ya manufaa yake ya kidini na ya kidunia. Mwenyezi Mungu anasema:
"Wala hakuweka mambo mazito katika dini"
(22: 78) Na amesema tena:
﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾
" Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika yatakayowapa uhai"
(8:24)
Unaweza
kuuliza
: Ikiwa mambo ni hivyo, basi hakuna wajihi wa kauli yake Mwenyezi Mungu (Na lau kama tungewalazimisha kuwa jiueni) kwa sababu hii ni amri ya lisilowezekana?
Jibu
: Hii ni kiasi cha kukadiria tu, na ndio maana limekuja neno "lau" linalofahamisha kuzuilika jambo kwa kuzuilika jengine. Makusudio ya kukadiria huku ni kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba wanafiki hawana udhuru kabisa katika kuzifanyia inadi hukumu zake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ambazo hakuna mashaka wala kujiangamiza, bali ni rehema kwao. Lakini pamoja na haya yote waliasi.
Ikiwa wanafiki wameasi na kuzigomea hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu pamoja na wepesi uliomo, basi katika Masahaba wa Mtume(s.a.w.w)
kuna ambao lau wangeliamrishwa kujiua wangelifanya. Nao Mwenyezi Mungu amewaelezea kuwa ni wachache. Miongoni mwa wachache hao ni Yasir na mkewe, ambao walikufa shahid katika adhabu kwa ajili ya Uislam.
Hao ni wazazi wa Ammar aliyeuliwa na kikundi kiovu siku ya vita vya Siffin. Alikuwa katika munajat akimwambia Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Ewe Mola wangu! Hakika wewe unajua lau ikiwa mimi ninajua kuwa kukuridhisha ni kukita upanga wangu huu kifuani mwangu na utokeze mgongoni mwangu, ningelifanya." Na lau kama wangefanya yale waliyoagizwa, ingekuwa heri kwao na uthibitsho wa nguvu zaidi.
Makusudio ya waliyoagizwa, ni kumtii Mwenyezi Mungu katika amri zake na makatazo yake,
﴿ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴾
"Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake hakika amefanikiwa mafanikio makubwa."
(33:71)
Makusudio ya kuthibitisha ni kuthubutisha imani. Imam Ali
anasema:"Katika imani kuna zilizo thabiti katika nyoyo na kuna zilizokaa kombo kwenye nyoyo kwa muda maalum."
Na hivi ndivyo alivyofasiri Imam as-Sadiq
kauli yake Mwenyezi Mungu:"Pako mahali pa kutulia pa kupita njia
(6:98)
Na hapo tungewapa malipo makubwa kutoka kwetu
Huu ndio ubainifu wa kheri katika kauli yake: "ingelikuwa kheri kwao" na kila malipo ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake ni kubwa, hata yakiwa machache, sikwambii akiyasifu kwa ukubwa.
Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume basi hao (watakuwa) pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na wasadikishaji na mashahidi na watu wema, Na hao ndio marafiki wema.
Aya hii ni kutilia mkazo Aya iliyotanguilia na kuhimiza imani na wema ambao utamfanya mtu kuwa ni rafiki wa Mitume, mashahidi na watu wema.
NI NANI WASADIKISHAJI?
Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Wasadikishaji ni wale walio na maumbile matakatifu, kiasi kwamba wao wanaipambanua haki na batili, heri na shari kwa kuiona tu."
Kauli hii iko karibu na kauli ya kisufi kwamba mtu akijitahidi na kuizowesha nafsi yake ataijua haki bila ya kujifundisha. Ilivyo hasa ni kufasiri wasadikishaje kuwa ni Maasum (walio hifadhiwa na makosa) waliokamilika na wanaokamilisha, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajaalia katika daraja ya pili kutoka Mitume bila ya kuweko kitu kingine. Na daraja hii haitakuwa kabisa kwa ambaye inajuzu kwake kukosea. Kwa sababu anayeweza kufanya makosa, hawezi kuwa mkamilifu wa mwengine kwenye ukamilifu wa uhakika. Bali atahitajia mkamilifu wa kihakika atakayemrudisha kwenye usawa. Na mkamilifu huyu ni Maasum.
Kwa maneno mengine wasadikishaji wako aina mbili:
Wa kwanza, ni yule asiyekusudia kusema uongo, lakini inawezekana kusema akakosa au kutatizika; kama mwenye kuelezea jambo mwenyewe akiamini ni mkweli katika anayoyaelezea, kisha ikabainika kwa habari yake si kweli. Hapo anakuwa mkweli katika makusudio yake na habari yake ni ya uongo, Haya hutokea mara nyingi.
Wa pili ni yule asiyekusudia uongo na wala hawezi kukosea, kiasi ambacho habari yake haikhalifu matukio kwa hali yoyote. Haya ndiyo makusudio ya wasadikishaji katika Aya hii na ya Wenye mamlaka katika Aya 59 ya sura hii. Kwa hiyo inakuwa makusudio ya wenye mamlaka na wakweli ni Ahlul -bait.
Vilevile Sheikh Muhammad Abduh amesema: "Makusudio ya mashahidi hapa ni watu wa uadilifu na wanaochunga haki, ambao wanaitilia nguvu haki kwa kuitolea ushahidi kuwa wao ni watu wa haki na kuwatolea ushahidi wabatilifu kuwa wao ni wabatilifu."
Hii ni kulifanyia taawili tamko lililo dhahiri bila dalili yoyote. Kwani inavyofahamika mashahidi ni wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu na haki. Ni kweli kuwa iko Hadith isemayo:Wino wa maulama ni kama damu za mashahid.
Na kwamba mwenye kufa katika njia ya haki, basi amekufa shahid, au ana thawabu za shahid, lakini kufa shahid ni jambo jengine na kuwa katika daraja ya kufa shahid ni jambo jingine. Ama watu wema ni wale ambao imekuwa njema itikadi yao na amali zao.
Imam Ali
amesema; "Kwa imani yanafahamika matendo mema na kwa matendo mema inafahamika imani"
Hakuna mwenye shaka kwamba kujua halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake kwa kujitahidi au kwa kufuata ni sharti la msingi katika wema. Kwa sababu kutojua huharibu itikadi na amali.
Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu.
Ndio! Radhi ya Mwenyezi Mungu, na kuwa na urafiki na Mitume, wakweli, mashahidi na watu wema, ni kutengenekewa kwa kweli na ni fadhila za kudumu, sio hizi starehe ziondokazo.
﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا خُذُوا حِذْرَكُمْ فَانفِرُوا ثُبَاتٍ أَوِ انفِرُوا جَمِيعًا ﴾
71 .Enyi mlioamini! Shikeni hadhari yenu, Tokeni vikosi vikosi au tokeni nyote pamoja
﴿ وَإِنَّ مِنكُمْ لَمَن لَّيُبَطِّئَنَّ فَإِنْ أَصَابَتْكُم مُّصِيبَةٌ قَالَ قَدْ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيَّ إِذْ لَمْ أَكُن مَّعَهُمْ شَهِيدًا﴾
72.Na hakika katika nyinyi kuna ambaye hukaa nyuma, na ukiwapata msiba husema: Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa kutokuwa nao.
﴿ وَلَئِنْ أَصَابَكُمْ فَضْلٌ مِّنَ اللَّـهِ لَيَقُولَنَّ كَأَن لَّمْ تَكُن بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُ مَوَدَّةٌ يَا لَيْتَنِي كُنتُ مَعَهُمْ فَأَفُوزَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴾
73.Na iwafikiapo fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu, husema - kama kwamba, hapakuwa na mapenzi baina yenu na yeye - laiti ningelikuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa.
CHUKUENI HADHARI
Aya 71 - 73
MAANA
Enyi mlioamini! Shikeni hadhari yenu
Aya hii ni miongoni mwa Aya za kuhimiza Jihad, zimetangulia Aya nyingi za namna hiyo na zijazo ni nyingi, Lakini Aya hii inawajibisha kutoka watu wote kwenye vita ikiwa iko haja, Umuhimu huu hasa unafahamisha maadui waliokuwa nao Waislamu wakiwapangia njama.
Na waislam hawaachi kuwa na wahasimu wanaowafitini na dini yao. Mpaka leo uislamu na waislamu wanaandamwa na makafiri na mataghuti. Kwa hiyo ni kawaida kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwahimiza waislam wawe na hadhari na kujua nguvu za uadui na maandalizi yake ya silaha.
Tokeni, vikosi vikosi au tokeni nyote pamoja
Tokeni, ni amri ya kutoka kwenda vitani; na kutoka kwa vikosi, ni vikosi maalum vya askari; na nyote pamoja ni jeshi pamoja na wengine kulingana na hali inavyotakikana. Makusudio ni kujiandaa kumkabili adui kwa nguvu zote na kutumia kila njia kuipinga dhulma na uadui; hata kama kujikinga kutapelekea umma wote kushiriki katika vita. Wakubwa kwa wadogo na waume kwa wake. Allama Hilli anasema: "Lau kuna haja ya kutaka msaada kwa wanawake basi itakuwa ni wajibu."
VITA VYA JANA NA LEO
Zamani vita vilikuwa vya wanaume tu na kuandaliwa na askari na vikosi. Ama leo, sayansi ndiyo imekuwa nguvu katika nyanja zote. Na panga na mishale zimebadilika kuwa mabomu, mizinga nyambiz i, vifaru na meli za kivita. Vile vile silaha za sumu na mitandao ya upelelezi wa anga, bara na baharini
kiasi ambacho hajui isipokuwa Mwenyezi Mungu na mabingwa katika elimu ya kuharibu na kuvunja.
Biashara ya vita haikutosheka na uvumbuzi wa elimu wa vifaa vya kuvunja na kuharibu, mpaka wameanzisha vyuo maalum vya elimu ya kuharibu na upangaji wa njama za mapinduzi, kuleta fitina na chuki na kuleta ghasia. Vilevile kupanga namna ya kueneza hofu na wasiwasi, kupuuza maadili na misimamo na kuamini mambo ya uzushi, na mengineyo yanayoandaa nguvu za kuwatawala wanyonge.
Hii ndiyo aina ya silaha anayotupiga nayo vita adui wa dini na wa ubinadamu, Basi tutajikinga naye vipi? Je, ni kwa matusi na shutuma? Au ni kuomboleza na kulia? Au ni kwa chuki. Hakuna jengine kwa tulivyo hivi sasa ila kumjua ni nani adui yetu na uwezo wake ukoje, na tujihadhari naye na mbinu zake; wala tusimwamini na chochote. Vile vile tujifunze kutokana na makosa yetu, tujiepushe na wahaini na tufanye bidii mkono kwa mkono kwa nguvu zetu zote katika nyanja zote. Kwa namna hii ndipo tutaweza kusimama kumkabili adui; angalau hali isiwe kama tulivyo sasa.
Wavietnam waliweza kuwang'oa wamarekani pamoja na nguvu nyingi walizozikusanya na mabilioni ya madola waliyoyatoa. Kabla ya Vietnam, Cuba ilijikomboa kutoka makucha ya wamarekani ingawaje ndilo taifa kubwa ulimwenguni, Na hivijuzi Korea ya Kaskazini imeteka nyara meli ya kijasusi na wala Amerika haiwezi kuitikisa.
Siri ya hayo - kwa nionavyo - ni kwamba mataifa haya yalikuwa na mwamko na mipango na yalisahihisha makosa yake wakaikata mikono ya wahaini na kuwatenga na uongozi na sehemu muhimu. Pia mataifa hayo yaliamini haki yake na misingi yake na kupuuza maisha katika kuipigania.
Wala haiwezekani kwa nguvu za ulimwengu wote kutawala taifa lenye nidhamu na mwamko, liwe la kivietnam au la kiarabu. Tofauti iko katika hali sio asili na katika mwamko na uthabiti katika wanachokiamini na kukiitakidi.
Na hakika katika nyinyi kuna ambaye hukaa nyuma
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria kwenye kikosi cha siri ambacho kinajiingiza katika safu za watu wema kwa makusudio ya kuharibu na kurudisha nyuma mapambano na uadui.
Unaweza kuuliza
: kuwa neno, katika nyinyi linaelekezwa kwa waumini, na wanafiki wako mbali zaidi na imani kuliko watu wengine. Sasa imekuwaje kuwafanya ni katika waumini?
Jibu
: Kwa sababu wao wanahisabiwa kuwa ni katika waumini kidhahiri, na wanachukuliwa kuwa ni katika wao, sawa na mtu anayechukuwa uraia wa nchi akiwa ni kibaraka. Hawa wapo kila mahali na kila wakati. Ukiwapata msiba husema: Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa kutokuwa nao.
Hii ni kuizungumzia hali ya mnafiki ambaye alikuwa akifurahi wanaposhindwa waislam katika vita ambavyo yeye hakuhudhuria pamoja nao. Kila mwenye kufurahi kwa kusalimika na balaa iliyompata ndugu yake katika njia ya Mwenyezi Mungu na kupigania kuinua dini, basi huyo ni mnafiki.
Unaweza kuuliza kuwa
: kauli yake Mwenyezi Mungu, amenineemesha, ni kukiri kuweko Mwenyezi Mungu, sasa imewezekanaje kumfanya ni katika wanafiki?
Jibu
: Yeye ameufanya unafiki kwa kudhihirisha uislamu na kumwamini Muhammad(s.a.w.w)
na kuficha kukanusha utume wake. Na hili halipingani na kumkubali Muumba. Si kila anayemwamini Mungu anamwamini Muhammad(s.a.w.w)
, Mwenyezi Mungu ameelezea kuwa kuna katika watu anayemwamini yeye Mwenyezi Mungu na wakati huo huo anamwamini mwingine, au atakayemkurubisha zaidi kwake.
﴿وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴾
"Na wengi wao hawamwamini Mwenyezi Mungu isipokuwa wao ni washirikina"
(12:106)
Na iwafikapo fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu, husema - kama kwamba hapakuwa na mapenzii baina yenu na yeye - laiti ningelikuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa. Baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea kuwa mnafiki hufurahi kwa kubaki kwake nyuma, kama waislamu wakishindwa, sasa anaeleza kuwa yeye anajuta kwa kuacha kujiunga nao wanapopata ushindi na ngawira. Kimsingi ni kuwa ambaye mambo yake ni hayo, si mwislamu kitu, hata kama anadai kuwa ni mwislamu. Na kama angelidhihirisha mapenzi baina yake na waislam angelitambua kwamba heri yao ni heri yake na shari yao ni shari yake.
Imekuwa mashuhuri Hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
:"Hakika waislam ni kama viungo vya mwili mmoja, na ni kama jengo moja, sehemu moja inasaidia nyingine; na kwamba asiyejishughulisha na mambo ya waislam si katika wao."
﴿فَلْيُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ الَّذِينَ يَشْرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا بِالْآخِرَةِ وَمَن يُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيُقْتَلْ أَوْ يَغْلِبْ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا ﴾
74.Na wapigane katika njia ya Mwenyezi Mungu ambao huuza maisha ya duniani kwa akhera, na mwenye kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, akauawa au akashinda, tutampa ujira mkubwa.
﴿وَمَا لَكُمْ لَا تُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ الظَّالِمِ أَهْلُهَا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ نَصِيرًا﴾
75.Na mna nini hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa katika wanaume na wanawake na watoto ambao husema: Ewe Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie mlinzi kutoka kwako.
﴿ الَّذِينَ آمَنُوا يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـه وَالَّذِينَ كَفَرُوا يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ الطَّاغُوتِ فَقَاتِلُوا أَوْلِيَاءَ الشَّيْطَانِ إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا ﴾
76.Wale walioamini wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na waliokufuru, wanapigana katika njia ya shetani. Basi piganeni na marafiki wa shetani; hakika hila za shetani ni dhaifu.
WANAOUZA UHAI WA DUNIA KWA AKHERA
Aya 74 -76
MAANA
Na wapigane katika njia ya Mwenyezi Mungu ambao huuza maisha ya duniani kwa akhera.
Uzuri wa yaliyosemwa katika kufasiri Aya hii ni haya yafuatayo: "Hakika Uislamu haupigani kwa ajili ya kupata ardhi au kuwatawala wakazi; haupigani kwa ajili ya kupata malighafi ya viwanda na masoko; au kwa ajili ya rasilmali zitakazozalishwa katika makoloni.
Uislam haupigani kwa ajili ya fahari ya mtu, nyumba, tabaka, dola, umma au watu fulani. Isipokuwa unapigana katika njia ya Mwenyezi Mung u kwenyeardhi na kumakinika njia yake katika maisha na ili mtu afaidike na njia hii na uadilifu baina ya watu huku ukimwacha mtu awe huru na mwenye hiyari katika itikadi ambayo atakuwa nayo.'
Natamani wakati ninasoma jumla hii (Uislamu haupigani kwa jili ya malighafi ya viwanda) niunganishe na jumla hii: 'na wala si kwa ajili viwanda vipakwe damu ya wasiokuwa na hatia, wanawake na watoto.
Na mwenye kupigana katika njia ya Mungu, Akauawa au akashinda, tutampa ujira mkubwa
Kila mwenye kuinusuru haki kwa njia ya haki na kufuata amri ya Mwenyezi Mungu peke yake, basi yeye ni mwenye kushukuriwa na mwenye kulipwa; ni sawa iwe ameshinda na akapata ngawira, au ameshindwa.
Wanahistoria, pamoja na kutofautiana misimamo yao, wameafikiana kuwa siri ya kuenea uislam ni itikadi ya Mtume(s.a.w.w)
na sahaba, kwamba wao ni wenye kupata faida katika hali yoyote, ya kuuliwa au kuua. Ikiwa ni kuuawa, basi mwelekeo ni peponi; au ikiwa ni kuua itakuwa tamko la haki limeinuka, na hili ndilo walilolitaka; kuongezea imani kwamba ajali yao ikifika haichelewi hata saa wala haizidi. Imani ya mtu ikifikia hatua hii hawezi kusimamishwa na kizuizi chochote.
Na mna nini hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa katika wanaume na wanawake na watoto.
Mtume(s.a.w.w)
alihama kutoka Makka kwenda Madina, na walihama pamoja naye wale walioweza na wakabakia wenye kushindwa, wakiwemo wanaume wanawake na watoto. Nao walikuwa wakipata adha kubwa kutoka kwa washirikina kwa ajili ya dini yao; na wala hawakuweza kujikinga wala kupata usaidizi, Kwa ajili hii ndio Mwenyezi Mungu akawaita 'wanaoonewa'. Walipokuwa hawana la kufanya, walimwelekea Mwenyezi Mungu na kusema:
Ewe Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie mlinzi kutoka kwako.
Mwenyezi Mungu ameifanya misukosuko ya wanyonge ni njia ya kuwahimiza jihadi waislam kuwaokoa ndugu zao wa dini, jamaa wanyonge walibakia Makka mpaka mwaka wa ushindi Mtume alipoingia Masjidul-haram wakiwa washindi, vigogo vya ushirikina vikasalimu amri na masanamu yakavunjwa. Uislamu ukatukuka na akawaneemesha wale walio wanyonge katika Makka na kuwafanya watukufu.
Wale walioamini wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na waliokufuru wanapigana katika njia ya shetani.
Katika Aya 71 Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameamrisha kutoka kwenda vitani vikosi au wote; katika Aya 74, ameamrisha kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu; katika Aya 75, amewahimiza kuwakomboa wanaoonewa, Katika Aya hii amegawanya wapiganaji kwenye mafungu mawili; waumini wanaopigana kwa ajili ya haki na uadilifu, na makafiri wanaopigana kwa ajili ya kutawala, kunyang'anya, na kudhulumu.
Hawa ndio wasaidizi wa shetani; na Mwenyezi Mungu amewaamrisha waumini wapigane na kuwatangazia vita na kuacha kufanya mapatano nao kwa namna yoyote ile. Kwa sababu kuwamaliza ndio heri na utengeneo wa ubinadamu, na kupatana nao ni shari na ufisadi.
Kwa ufupi ni kwamba Aya zote tulizozielezea na nyinginezo zinazohusu vita zina lengo moja tu, uimara na uthabiti katika kuwapiga vita wabatilifu na wenye kutaka kujichukulia faida. Aya za Jihadi zinatofautiana katika mfumo na ibara tu, lakini lengo ni moja.
Basi piganeni na marafiki wa shetani; hakika hila za shetani ni dhaifu.
Dhahiri ya Aya hii, ni kwamba wenye haki daima watawashinda wabatilifu, lakini aghlab hali inakuwa kinyume; je kuna siri gani?
Umetangulia mfano wa swali hili na jibu lake kwa ufafanuzi katika kufasiri Aya ya (3:137) kifungu cha Balaa la June. Lakini hapa tutajibu kwa mfumo mwingine, tuliojua kutokana na hotuba ya Imam Ali
katika Nahjul-balagha.
Ufupi wa jibu ni kuwa vijasumu vibaya haviishi na kukua isipokuwa kwenye takataka na uchafu, Hivyo hivyo shetani hapati mahali pa kutekeleza hila zake isipokuwa penye jamii mbaya. Hapa maandalizi yake hupata nguvu na kujaza nguvu zake. Katika kauli yake Imam, inadhihiri kuwa umuhimu wa Iblis unafaulu pale wanapokuwa katika jamii mafukara wenye shida na matajiri wajeuri, Imam anasema hivi:
"Yafahamu vizuri haya ! Ikiwa silaha ya shetani itakuwa na nguvu, vitimbi vyake vikaenea na uwindaji wake ukawa mwepesi tupa jicho lako popote unapotaka katika watu. Je, utaona zaidi ya fakiri mwenye mashaka au tajiri aliyebadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kuwa ukafiri au bakhili aliyefanyia haki ya Mwenyezi Mungu kuwa ndio ubakhili! au jeuri ila ni kama kiziwi Wako wapi wabora wenu na wema wenu? Wako wapi waungwana wenu na watoaji wenu?
Wako wapi wanaochunga haki katika chumo lao? - mpaka kufikia pale aliposema - kwa hali hii ndio mnataka kuwa karibu na Mwenyezi Mungu katika nyumba ya utukufu wake, na muwe ni watukufu wa vipenzi vyake mbele zake? Awalaani Mwenyezi Mungu wanaoamrisha mema na kuyaacha, na wenye kukataza mabaya na huyafanya"