TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 18782
Pakua: 3492


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 18782 / Pakua: 3492
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

Mwandishi:
Swahili

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASYHIF JUZUU YA TANO

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّوا أَيْدِيَكُمْ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَخْشَوْنَ النَّاسَ كَخَشْيَةِ اللَّـهِ أَوْ أَشَدَّ خَشْيَةً وَقَالُوا رَبَّنَا لِمَ كَتَبْتَ عَلَيْنَا الْقِتَالَ لَوْلَا أَخَّرْتَنَا إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ قُلْ مَتَاعُ الدُّنْيَا قَلِيلٌ وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّمَنِ اتَّقَىٰ وَلَا تُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴾

77.Je, huwaoni wale ambao wameambiwa: Zuieni mikono yenu, na msimamishe Swala na mtoe Zaka. Walipolazimishwa kupigana, mara kundi moja katika wao wakawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu au kwa hofu zaidi; na wakasema: Ewe Mola wetu! Kwa nini ukatufaradhia vita usituahirishie muda mchache! Waambie: Starehe ya duniani ni chache, na akhera ni bora kwa wenye kumcha Mungu wala hamtadhulumiwa hata kidogo.

ZUIENI MIKONO YENU NA SIMAMISHENI SWALA

Aya 77

MAANA

Mwanzo wa kulingania Mtume(s.a.w.w) kwa Mwenyezi Mungu, alilingania akiwa Makka. Wenye nguvu wakamzuia, wakihofia masilahi yao. Wakamwita mwenda wazimu, mchawi na mwongo, Lau si ami yake Abu Twalib kumhami, wangelimmaliza, Waliposhindwa naye, waliingilia kuwatesa wanaomwamini. Na Mtume alikuwa akiwaamuru kuwa wavumilivu na kuizuia mikono yao, kwa sababu ya wingi wa adui na uchache wa wasaidizi.

Maudhi na vikwazo vya washirikina vilipoziidi kwa waumini wanyonge, kikundi kimoja kilisema kumwambia Mtume(s.a.w.w) "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; tupe idhini ya kupigana na washirikina." Akasema: "Nimeamrishwa kufanya subira." Na Mtume alikuwa akiwapa matumaini sahaba zake ya kuenea waislam na kuondoka utawala dhalimu.

Baada ya kupita miaka 13 Makka tangu kuanza mlingano, Mtume alihama kwenda Madina na wakahama pamoja naye wanaojiweza katika waislamu, wakiwemo wale waliotaka idhini ya kupigana na washirikina wa Makka, Idadi ya waislam ilipoongezeka wakawa wanaweza kujilinda. Mwenyezi Mungu akawaamrisha kupigana Jihadi na washirikina ili kujikinga na shari yao.

Kwa sababu hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ilihukumia kupita mambo kwa desturi yake na sababu zake; na kutoenea dini yake ispokuwa kwa nyezo za kiubinadamu na kutolazimisha dini kwa nguvu za kiungu; kama inavyonyesha mvua na tufani.

Mambo yalipoiva wakaanza kuogopa wale waliokuwa na hamasa ya kupigana na washirikina walipokuwa Makka kabla hawajaruhusiwa vita. Hii ndiyo hali ya wanaopandwa na mori kwa hisia za mapenzi bila ya kufikiri na kuwaza, wanapandwa na mori na hamasa ya kupigana mpaka wanarukwa na akili; ambapo utekelezaji wake ni kujiua. Lakini inapofikia haja ya kupigana na kuwa ni lazima, basi huanza kurudi nyuma kwa woga.

Si lazima watu wa namna hii wawe ni wanafiki au wasiokuwa na uhakika wa dini yao. Wanaweza kuwa ni katika wanyonge wanaohofia mauti na kuathirika na uhai kwa kuhofia kufa shahid katika njia ya haki.

Aya hii tuliyonayo imeonyesha kikundi cha waislamu waliokuwa na hamasa ya kupigana walipokuwa Makka kisha wakaogopa walipokuwa Madina. Tumetangulia kueleza utangulizi huo, kabla ya kuanza kufasiri Aya hii ili yawe wazi makusudio yake.

Je huwaoni wale ambao wameambiwa: Zuieni mikono yenu, na msimamishe Swala, na mtoe Zaka.

Makusudio ya, wale ambao; ni wale waliokuwa na haraka ya vita na hamasa walipokuwa Makka. Na kauli yake Mwenye zi Mungu "wameambiwa" ni ishara ya kwamba Mtume aliwaamuru kufanya subira na kujizuia kupigana, na kufanya lile waliloamriwa ikiwemo kuswali na kutoa Zaka.

Walipolazimishwa kupigana, mara kundi moja katika wao wakawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu au kwa hofu zaidi.

Yaani, zilipokamilika sababu za waislam kupigana baada ya kuhamia Madina, na kukawa na haja sana waliamrishwa kufanya hivyo, lakini wale waliokuwa na haraka walichukia kwa kupenda uhai na kuwa na woga wa kukabiliana na adui na kuogopa kuteseka.

Kusema kwake na wakawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu au kwa hofu zaidi ni fumbo la kuwa hofu imefikia kikomo.

Na wakasema: Ewe Mola wetu! Kwa nini ukatufaradhia vita, usituahirishie muda kidogo

Walitaka muda kwa kupenda sana anasa za dunia. Na mwelekeo wao wa hili kwa kunyenyekea, unaonyesha kumwamini kwao Mungu. Ilivyo ni kuwa kuasi amri ya Mwenyezi Mungu kwa mauti, hakufahamishi kuwa ni ulahidi; kama ambavyo kuhiyari mauti kuliko kuwa dhalili hakufahamishi kumwamini Mungu.

Tumewaona walahidi wengi wakihiyari kufa kuliko kuishi na madhalimu; kama ambavyo tumewaona waislamu wengi wanajiingiza kwenye vifungo vya udhalili na utumwa, wao wenyewe na watu wao.

Waambie starehe ya duniani ni chache.

Makusudio ya uchache hapa ni kutodumu na kuondoka haraka. Na kila starehe za dunia zitakwisha zaidi ya kuwa zimechanganyika na wasiwasi na machukivu.

Na akhera ni bora kwa wenye kumcha Mungu.

Akhera ndio mwisho wa yote; uchache wa neema yake ni bora kuliko neema za dunia zote; kama ambavyo uchache wa adhabu yake ni mkubwa kuliko adhabu ya dunia yote. Mwenye akili ni yule ambaye anathamini kitukufu cha kudumu, hata kama kitakuja baadaye, kuliko kitu duni kinachokwisha ingawaje ni cha sasa hivi.

﴿أَيْنَمَا تَكُونُوا يُدْرِككُّمُ الْمَوْتُ وَلَوْ كُنتُمْ فِي بُرُوجٍ مُّشَيَّدَةٍ وَإِن تُصِبْهُمْ حَسَنَةٌ يَقُولُوا هَـٰذِهِ مِنْ عِندِ اللَّـهِ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَقُولُوا هَـٰذِهِ مِنْ عِندِكَ قُلْ كُلٌّ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ فَمَالِ هَـٰؤُلَاءِ الْقَوْمِ لَا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ حَدِيثًا﴾

78.Popote mtakapokuwa yatawafika mauti na hata mkiwa katika ngome madhubuti. Na likiwafikia zuri wao husema: Hili linatokana na Mwenyezi Mungu. Na likiwafika baya husema: Hili linatokana na wewe, Sema: Yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, Basi wananini watu hao hata hawakaribii kufahamu maneno.

﴿مَّا أَصَابَكَ مِنْ حَسَنَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ وَمَا أَصَابَكَ مِن سَيِّئَةٍ فَمِن نَّفْسِكَ وَأَرْسَلْنَاكَ لِلنَّاسِ رَسُولًا وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا ﴾

79.Jema likufikalo linatokana na Mwenyezi Mungu na ovu likufikalo linatokana na wewe mwenyewe. Na tumekupeleka kwa watu kuwa ni mjumbe, na atosha Mwenyezi Mungu kuwa shahidi.

POPOTE MTAKAPOKUWA YATAWAFIKA MAUTI

Aya 78 - 79

MAANA

Popote mtakapokuwa yatawafika mauti na hata mkiwa katika ngome madhubuti.

Umetangulia mfano wake wakati wa kufasiri 3: 145 kifungu 'Ajali imeandikwa.'

Likiwafikia zuri wao husema: Hili linatokana na Mwenyezi Mungu na liki- wafika baya, husema hili linatokana na wewe.

Kila alionalo mtu ni zuri, husema ni zuri na kulifuatishia na neno heri ambalo mtu hulipendelea na kulitamani. Na kila alionalo mtu ni baya, husema ni baya, na kuliufuatishia na neno shari ambalo mtu hujiepusha nalo na kulikataa.

Kheri inaweza kuwa ya watu wote; ka ma vile rutuba na fanaka ambayo haimhusu mtu au kundi pekee. Na mara nyingine huwa inamhusu mtu; kama ufanisi wa mtu baina yake na familia yake. Vilevile shari inaweza kuwa ni ya kiujumla; kama vile ukame na ughali wa vitu; au kuwa ni ya mtu binafsi; kama vile kuwa mke mwovu na watoto wake.

Makusudio ya uzuri katika Aya hii ni kheri ya kimaumbile ambayo inaenea kwa wote; kama vile mvua na mfano wake. Na ubaya ni shari inayoenea kwa wote; kama vile kahati na mengineyo. Kwa sababu washirikina walipokuwa wakipata neema; kama vile mvua, husema; Mwenyezi Mungu ametukirimu. Na wakipatwa na adhabu; kama vile kahati, husema: Hii imesababishwa na Muhammad; sawa na vile walivyokuwa wakisema wana wa Israil, ambao Mwenyezi Mungu amewaelezea kwa kusema:

﴿فَإِذَا جَاءَتْهُمُ الْحَسَنَةُ قَالُوا لَنَا هَـٰذِهِ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَطَّيَّرُوا بِمُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ﴾

"Unapowafikia uzuri husema: Huu ni kwa ajili yetu. Na ukiwafikia ubaya humnasibishia ukorofi Musa" (7:131)

HAIWEZEKANI KUONGEZA ZAIDI YA ILIVYO

Sema: Yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hili ni jibu la anayenasibisha wema kwa Mwenyezi Mungu na uovu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kwani kahati, mvua, matatemeko na madini vyote hivi na vinginevyo ni katika athari na mambo ya lazima kwa maumbile.

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyeleta maumbile, Kwa hiyo heri ya maumbile na shari yake inanasibishwa kwenye maumbile na kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kupitia kuleta kwake maumbile, Yeye ambaye umetukuka utukufu wake, ndiye sababu ya sababu.

Unaweza kuuliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu hakuyafanya maumbile bila ya shari, kwa namna ambayo heri itatakata na kila tatizo na waja wapate raha, wasiwe na tabu?

Swali hili au mushkeli huu umetolewa tangu maelefu ya miaka iliyopita, Zaradasht amejaribu kulitatua kwa kusema kuwa kuna waungu wawili Mungu wa heri (Mozad) na Mungu wa shari (Ahriman).

Wengine wamesema: Hakika Mwenyezi Mungu ameyaumba maumbile haya mkiwa ndani yake mna heri na shari, lakini wakati huo akaumba akili itakayolinganisha maumbile haya kwenye heri yake na utengenevu wake.

Ikiwemo huu ugunduzi ambao umefanya kitu cha mbali kiwe karibu, ukasahilisha jambo zito, yakatengenezwa mawingu ya mvua, na vimbunga vikajulikana kabla ya kutokea na mengineyo yasiyokuwa na idadi.

Amesema Abid Zahid: Hakuna budi na shari ili waasi waadhibiwe, lakini jibu hili linakanushwa na ushahidi uliopo na Qur'an. Kwa sababu desturi ya maumbile haimuhurumii muumin wala dhaifu na matetemeko ya ardhi hayamtengi mwema na mwovu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:

﴿ وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً﴾

Na iogopeni adhabu ambayo haitawasibu waliodhulumu nafsi zao katika nyinyi, peke yao. (8:25)

Kuna wengine waliosema: Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye na sisi hatujui kitu, Ashaira wamesema swali hili linarudishwa lilivyo. Kwa sababu vitendo vyake Mwenyezi Mungu Mtukufu, havisababishwi kwa malengo fulani. "haulizwi alifanyalo".

Katika kitab Asfar cha mwanachuoni mtukufu aliye mashuhuri kwa jina la Mulla Sadra kuna maelezo, kwa muhtasari: Ni jambo lisilowezekana kuweko ulimwengu usiokuwa na shari. Kwa sababu ulivyo ulimwengu wa kimaumbile kwa mujibu wa hali yake hulazimika kuweko na heri na shari, nguvu na udhaifu na upole na ugumu. Vinginevyo isingewezekana kabisa kuweko ulimwengu; kama isivyowezekana kwa bingwa wa ujenzi kujenga ngome madhubuti kwa udongo tu.

Hilo ni kwamba ni muhali kuweko kitu bila kuweko na vitu vinavyopingana ambavyo daima vinakuwa katika mvutano na msukumano wa daima.

Katika hali hii ndipo yanapatikana maumbile kama vile vimbunga, joto, baridi, mvua, ukame na mengineyo ambayo athari zake za kimaumbile ni heri yake na shari yake. Katika hali hii ndipo mambo lazima yawe katika hali mbili tu. Ama kusiweko ulimwengu ama uweko ukiwa na heri yake na shari yake.

Hii ndio maana ya msemo mashuhuri: "Haiwezekani kuzidisha zaidi ya ilivyo," kama ambavyo inaafikiana kwa ukamilifu na kauli ya wanasayansi kuwa katika kila maumbile kuna sehemu ya nguvu ya sawa na ya kutengua.

Kwa hivyo basi, inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema; Kwa nini Mwenyezi Mungu hakuumba ulimwengu usiokuwa na shari, ni sawa na mwenye kusema: kwa nini Mwenyezi Mungu hakuumba moto usiokuwa na joto, theluji isiyokuwa na baridi, akili isiyokuwa na utambuzi, uhai usiokuwa na harakati au mauti yasiyokuwa na kutulia.

Kwa maneno mengine swali hili linafanana na mtu aliyepagawa anayesema: Kwa nini kitu kikawa hicho hicho na hakikuwa kingine. Katika hali hii ndipo tunapata siri ya undani katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Basi wana nini watu hao hata hawakaribii kufahamu maneno.

Kwa ufupi ni kuwa si Muhammad(s.a.w.w) wala mwingineo mwenye athari yoyote, ya heri au ya shari katika maumbile. Iko riwaya mashuhuri kutoka kwa Mtume kwamba alisema wakati jua liliposhikwa, alipokufa mtoto wake Ibrahim: "Jua na mwezi ni alama katika alama za Mungu, zinakwenda kwa amri yake na kumtii yeye tu, hazishikwi kwa sababu ya kifo cha yeyote au uhai wa yeyote."

Jema likufikalo linatokana na Mwenyezi Mungu na ovu likufikalo linatokana na wewe mwenyewe.

Unaweza kuuliza : Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya ya kwanza ameutegemeza ubaya na uzuri kwake Yeye tu, kwa kusema yote yatoka kwa Mwenyezi Mungu; na katika Aya ya hii ametegemeza mema kwake na mabaya kwa binadamu, Je kuna wajihi gani?

Jibu : Tumetanguliza kueleza katika Aya ya kwanza kwamba makusudio ya uzuri katika Aya ya kwanza ni heri ya maumbile na ubaya ni shari ya maumbile, na kwamba yote mawili ni dhahiri ya maumbile ambayo ni katika utengenezaji wa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo ikasihi kuyanasibisha kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa mazingatio haya. Ama makusudio ya uzuri katika Aya ya pili ni kuokoka mtu katika maisha haya kidini na kidunia.

Na makusudio ya uovu ni kutofanikiwa kidini na kidunia. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekunasibisha kuokoka - katika kuangalia ibara ya wema - Kwake Yeye kwa kuangalia kuwa yeye amempa uzima na utambuzi na akaamrisha kufanya amali kwa ajili ya manufaa ya duniani na akhera. Kwa hiyo akifuata na kufanya amali akafikia kufaulu, hunasibishwa kwake Mwenyezi Mungu. Kwa sababu yeye ndiye aliyemwezesha na akampa ala za kufanyia kazi hiyo tena akamwamrisha. Ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:Jema likupatalo linatoka kwake .

Vilevile inawezekana kunasibisha kuokoka kwa mtu. Kwa sababu yeye ameacha uvivu na kupuuza akajitahidi na kufanya, Hakuna dalili katika Aya kwamba mtu hana athari kabisa katika kufaulu kwake. Ama kupuuza na kufanya uvivu na asifikie popote kwa sababu ya kupuuza kwake na uzembe, hakuwezi kunasibishwa kwa yeyote zaidi yake yeye mwenyewe.

Kwa sababu ni yeye aliyejiingiza kwa chaguo lake ovu la kupuuza. Kwa kuzingatia hivi ndipo Mwenyezi Mungu akasema: "Na ovu likufikalo linatoka kwako." Wala haiwezekani kwa hali yoyote kutofaulu kwa mtu kunasibishwe na Mwenyezi Mungu. Kwani Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, amemwamrisha mtu kufanya na kumhimiza baada ya kumpa zana zote zihitajikazo.

﴿ مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا﴾

80.Mwenye kumtii Mtume, basi amemtii Mwenyezi Mungu; na mwenye kukataa, basi hatukukupeleka kuwa mlinzi juu yao.

﴿ وَيَقُولُونَ طَاعَةٌ فَإِذَا بَرَزُوا مِنْ عِندِكَ بَيَّتَ طَائِفَةٌ مِّنْهُمْ غَيْرَ الَّذِي تَقُولُ وَاللَّـهُ يَكْتُبُ مَا يُبَيِّتُونَ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا﴾

81.Na wanasema: 'Tunatii' na wanapotoka kwako kundi moja katika wao huenda njama usiku kinyume cha yale wayasemayo, Na Mwenyezi Mungu anaziandika njama zao. Basi achana nao na mtegemee Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa ni mwenye kutegemewa.

﴿ أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا﴾

82.Je, hawaizingatii Qur'an? Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangelikuta ndani yake tofauti nyingi.

HATUKUKUPELEKA KUWA MLINZI JUU YAO

Aya 80 - 82

MAANA

Mwenye kumtii Mtume, basi amemtii Mwenyezi Mungu

Imetangulia tafsir yake katika Aya 59 ya Sura hii,

Na mwenye kukataa, basi hatukukupelekea kuwa mlinzi juu yao.

Kazi ya Mtume inaelezwa na tamko la jina lenyewe; kama ambavyo tamko la jua linavyoelezea maana yake. Ama hisabu ya mateso, ni kazi ya Mwenyezi Mungu, si ya Mtume:

Hakika ni kwetu sisi marejeo yao. Kisha ni juu yetu sisi hesabu yao (88:25 - 28)

Tumezungumzia kwa ufafanuzi maudhui haya katika kufasiri (2:270)

Na wanasema: 'Tunatii' na wanapotoka kwako kundi moja katika wao huenda njama usiku kinyume cha yale wayasemayo, Na Mwenyezi Mungu anaziandika njama zao.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa waislamu kwa ujumla wao walidhihirisha utii kwa Mtume(s.a.w.w) , lakini wao si wote waliokuwa na ikhlasi katika waliyoyadhihirisha, Bali katika wao kulikuwa kuna kikundi kinachomhadaa Mtume na kula njama usiku kinyume na wanayoyadhihirisha. Aya hii ni jawabu tosha kwa wale wanaodai kuwa masahaba wote ni waadilifu na kwamba kusuhubiana na Mtume tu kunamfanya mtu awe msafi wa kila kitu.

Basi achana nao na mtegemee Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa ni mwenye kutegemewa. Msemo unaelekezwa kwa Mtume, ukiwa na maana kuwa hekima inapelekea kutowafichua makafiri na kuwataja majina yao, Watafichuka wenyewe. Mfano wa Aya hii ni kama Aya ya 63 ya Sura hii hii.

MAYAHUDI NA MUUJIZA WA QUR'AN

Je hawaizingatii Qur'an? Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangelikuta ndani yake tofauti nyingi.

Katika kufasiri (2: 23-5) chini ya kifungu 'Siri ya muujiiza wa Qur'an; tumeonyesha siri hii kwa njia ya ujumla. Kwa sababu ufafanuzi utamaliza kitabu chenye ukubwa wa juzuu hii.

Baada ya kwisha kufasiri tumegundua siri za muujiza ambazo hawakuzinduka nazo wanavyuoni wa kiislam waliotangulia; hata wale waliotunga vitabu mahsus katika muujiza wa Qur'an. Hiyo sio kama imetokana na uzembe, la! Isipokuwa maajabu na siri za Kitabu cha Mwenyezi Mungu haziishi.

﴿ قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا﴾

"Sema lau bahari ingelikuwa ni wino kwa (kuandika) maneno ya Mola wangu, bila shaka bahari ingelikwisha kabla ya kwisha maneno ya Mola wangu. Hata kama tungelileta (bahari) kama hiyo kuongezea." (18:109)

Na amesibu kutokana na matamko haya kila mmoja kwa kadiri unavyomsaidia wakati wake na kipawa chake. Kwa sababu zama ni kiungo muhimu katika kufichua maana ya Qur'an na siri zake. Ibn Abbas anasema: "Katika Qur'an kuna maana yatakayofasiriwa na wakati."

Miongoni mwa maana hayo ni yale yaliyoonyeshwa na Aya ya 53 ya sura hii: "Au wao wana fungu katika Ufalme? Basi hapo wasingewapa watu hata kitobwe cha kokwa ya tende"

Tumetaja katika kufasiri Aya 46 utabiri wa Qur'an kuhusu fedheha ya Mayahudi na madhambi yao, wakipata Ufalme. Baada ya karne kumi na tatu utabiri huu umethibitika. Hii ni dalili ya mkato ya utume wa Muhammad(s.a.w.w) na ukweli wa ujumbe wake.

Huu ndio muujiza tulioukusudia kusema kuwa wanavyuoni na wafasiri hawakuzinduka nao. Kwa sababu Mayahudi wakati huo walikuwa wakitawaliwa, hawakuwa na chochote, si katika Palestina wala penginepo.

Katika jumla ya dalili za kuwa ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wangelikuta ndani yake tofauti nyingi."

Miongoni mwa tofauti hizi ni kutokuwepo mpangilio na kunasibiana katika maneno ya watu ki mfumo na kifikra.

Hakuna mwanachuoni mwanafasihi au mtu yeyote ila kutakuwepo na kutofautiana nguvu na udhaifu katika ibara zake na fikra zake. Ama Qur'an iko katika daraja moja katika ufasaha wa mpangilio wake na ukubwa wa maana zake.

Siri ya hilo ni kuwa binadamu ana hali na matatizo yanayotofautina na kubadilika kwa nyakati mbali mbali bali hata kwa kitambo kidogo tu. Na yeye binadamu anafuatana nazo, wala hawezi kuepukana na hilo kwa hali yoyote ile. Kusema kwake Mwenyezi Mungu, Tofauti nyingi, ni ishara ya kuwa mageuzi ya binadamu kulingana na hali yake ni mengi sana yasiyo na idadi.

Tofauti hii inatufasiria tofauti katika mfumo wa binadamu na fikra yake. Ama dhati takatifu ni moja katika kila kitu milele na milele, haibadiliki kwa hali wala kwa matatizo. "Vipi yatampita Mwenyezi Mungu yale aliyoyapitisha; na yamrudie yale aliyoyaanzisha; na yamzukie yale aliyoyazusha? Ingekuwa hivyo, basi dhati yake ingelitofautiana, na kuwa kwake kungegawanyika;" kama anavyosema Imam Ali(a.s) .

Huyu ndiye anayetufasiria kufuatana na kunasibiana katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, madhumuni na utendaji kazi wake, kuanzia Alifu mpaka Ye.

﴿ وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا ﴾

83.Ikiwajia habari ya amani au ya hofu huitangaza. Na lau wangeirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache tu.

SIRI YA VITA NA KUVITANGAZA

Aya 83

MAANA

Ikiwajia habari ya amani au ya hofu huitangaza

Walikuwepo katika Masahaba wa Mtume - kama ilivyo katika kikundi au kikosi chochote - wakweli na wanafiki, mashujaa na waoga, wenye nguvu na wadhaifu katika imani, na wenye akili wanaoangalia mambo kulingana na matukio, na wajinga wasiozingatia mambo wala kupima mwisho wake. Qur'an imewaelezea hawa wote, mara nyingine kwa uwazi na mara nyingine kwa ishara.

Wafasiri wameafikiana kwamba Aya hii imeshuka juu ya wale waliokuwa wakisikiliza habari za amani au za hofu, ambazo zilikuwa zikufungamana na nguvu za askari wa kiislam, basi huzitangaza kwa watu. Kisha wafasiri wakatofau tiana katika kuwaelezea hao watangazaji: Je, ni wanafiki au ni wale waumini wa juu juu wadhaifu? Kila kikundi kikasema kutokana na vile ilivyotiliwa nguvu kwao.

Ama sisi haikuwa na nguvu kwetu kauli ya kukusudia wanafiki wala wanyonge. Kwa sababu yote yanayofahamishwa na dhahiri ya Aya ni kuwa miongoni mwa jamaa waliokuwa karibu na Mtume(s.a.w.w) , wakifikiwa na habari ya amani au vita, huizungumzia na kuifuchua kwa watu.

Hakuna kitu kinachodhuru amani ya ndani na ya nje kuliko kufichua siri za kiaskari, hasa ikiwa watangazaji wenyewe wamepata habari juu juu. Kwa sababu habari nyingi wanazitengeneza maadui na kuzisambaza kwa makusudio ya kufaidika nazo na kueneza fitina na hofu katika safu za waislamu.

Na lau wangeirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao.

Dhamiri ya 'wenye mamlaka katika wao' inawarudia waislam. Ama dhamiri ya 'wenye kupeleleza katika wao' wafasiri wametofautiana. Kuna mwenye kusema kuwa inarudia wale waliotangaza habari ya amani au vita. Wengine wakasema kuwa inawarudia wenye mamlaka.

Hilo ndilo lililo dhahiri, Makusudio ya wenye mamlaka ni wale ambao Mtume(s.a.w.w) anaowaamini kwa ujuzi wao wa kidini na kielimu, na ambao Mwenyezi Mungu amewakusudia aliposema:"Yeya ndiye aliyekusaidia kwa nusura yake na kwa waumini." (8: 62)

Maana yake ni kuwa ingelikuwa bora kwa wale waliotangaza waliyoyasikia katika habari za vita kuacha kuziingilia habari zilizowafikia na wazielezee kwa Mtume na wenye ujuzi katika Masahaba wake, ni wao tu wanaojua habari za vita na mbinu zake na kuvitoa vitu kutoka katika machimbuko yake na kuvirudisha kwenye mashina yake.

Kwa hiyo kauli yake wangelijua wenye kuchunguza katika wao, maana yake ni kwamba wenye ujuzi wanajua hakika ya habari za kutangazwa na lengo lake. Kwa sababu wao ndio wanaofichua hakika kutoka katika chimbuko lake la kwanza na kufanya lile linalowajibisha hekima na masilahi. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache tu.

Makusudio ya fadhila za Mwenyezi Mungu na rehema yake ni kuteremshwa Qur'an na utume wa Muhammad(s.a.w.w) ; na maana yake ni, lau si Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake, mngelibaki juu ya ukafiri na upotevu isipokuwa wachache tu, katika nyinyi; Mfano Qas bin Saida, Waraqa bin Nawfal, Zaid bin Amr na wengine ambao walimwamini Mungu peke yake kwa hisia safi za ndani kabla ya Mwenyezi Mungu kumtuma Muhammad(s.a.w.w) . aina hii ya waumini wanaitwa Hanafiya. Na Hanif, kwa Waarabu, ni yule aliye katika dini ya Ibrahim(a.s)

﴿فَقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ لَا تُكَلَّفُ إِلَّا نَفْسَكَ وَحَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَكُفَّ بَأْسَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَاللَّـهُ أَشَدُّ بَأْسًا وَأَشَدُّ تَنكِيلًا﴾

84.Basi pigana katika njia ya Mwenyezi Mungu; haikalifishwi ila nafsi yako tu, Na wahimize waumini, Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulizi ya waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ni mkali zaidi wa kushambulia na mkali zaidi wa kuadhibu.

HAIKALIFISHWI ILA NAFSI YAKO

Aya 84

MAANA

Basi pigana katika njia ya Mwenyezi Mungu; haikalifishwi ila nafsi yako tu, Na wahimize waumini.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja katika Aya 77 kuhusu wale walioogopa kupigana wakasema; "Ewe Mola wetu kwa nini ukatufaradhia vita…"

Na katika Aya ya 81 wakadhihirisha twaa na kuficha uasi wakasema 'Tunatii' na wakala njama dhidi ya yale waliyoyasema, Akataja katika Aya ya 83 wale waliota ngaza habari za vita na siri zake. Baada ya kutaja yote hayo ndipo akamwamrisha Mtume wake kupigana jihadi, kuitetea haki na kuwahimiza waislamu kupigana jihadi pamoja naye na kuachana nao wale walioachana naye. Kwa sababu yeye hana jukumu wala kukalifishwa na matendo ya mwingine; isipokuwa matendo ya nafsi yake tu. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Haikalifishwi ila nafsi yako tu.

Siyo maana yake kuwa pigana peke yako tu, kama hakupigana pamoja na wewe yeyote; kama ilivyosemwa. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amemkataza Mtume na waislam kupigana, wakati wa mwanzo mwanzo wa kutanganza dini; na aliwaamrisha wasubiri na kuvumilia maudhi ya washirikina walipokuwa Makka. Kwa sababu kupigana wakati huo kulikuwa ni sawa na kujiua. Na hakuwamrisha jihadi ila baada ya kuhama kwenda Madina; wakawa sasa wanaweza kukabiliana na adui. Sasa ikiwa hali ni hiyo, itakuwaje Mtume aamrishwe kupigana akiwa peke yake.

Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulizi ya waliokufuru

Huenda hapa ni ya uhakika, kwa sababu ni katika maneno ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu havunji ahadi. Makusudio ya waliokufuru ni wakuu wa Kiquraish ambao wamemtoa Mtume(s.a.w.w) Makka na kuandaa jeshi la kumpiga vita mara nyingi. Na Mwenyezi Mungu alitekeleza ahadi yake, alimnusuru mja wa ke na akavishinda vikosi vya washirikina akiwa peke yake.

﴿ مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقِيتًا ﴾

85.Mwenye kuunga mkono jema, hupata fungu katika hayo, na mwenye kuunga mkono baya hupata hisa katika hayo; na Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu.

﴿وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا﴾

86.Na mnapoamkiwa kwa maamkuzi, basi itikieni kwa yaliyo bora au mrejeshe hayo hayo; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhisabu kila jambo.

﴿اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ لَيَجْمَعَنَّكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ حَدِيثًا﴾

87.Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye. Kwa yakini atawakusanya siku ya Kiama, halina shaka hilo na ni nani msema kweli katika maneno kuliko Mwenyezi Mungu?

KUUNGA MKONO NA MAAMKUZI

Aya 85 - 87

MAANA

Mwenye kuunga mkono jema hupata fungu katika hayo, Na mwenye kuunga mkono baya, hupata hisa katika hayo

Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa kuuunga mkono jema ni kuhimiza kupigana, na kuunga mkono baya ni kuvunja moyo wa kupigana. Kila mwenye kuhimiza na mwenye kuvunja moyo ana malipo ya kampeni yake na athari zake. Hilo ni katika kila kuunga mkono jambo la heri na kuunga mkono jambo la shari. Kuna Hadith isemayo: "Mwenye kuanzisha desturi nzuri atakuwa na malipo sawa na ya yule anayeifanya na mwenye kuanzisha desturi mbaya atakuwa na malipo sawa na ya yule anayeifanya."

Uislamu unapongeza kila tendo zuri, liwe litafuatwa na mwingine au limefanywa na mlahidi au hata bila ya nia ya kitendo chenyewe. La muhimu ni kuwa liwe linaweza kuitwa heri, bora, jema, zuri au mfano wa hayo. Tumelielezea suala hilo katika kufasiri 3: 144 kifungu 'Kila mtu ana alilolinuia,' Pia katika 3: 178 kifungu 'Kafiri na amali ya heri.'

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza juu ya kila kitu.

Yaani ana uweza wa kutulipa kila mmoja anavyostahiki humpa thawabu mwenye kuunga mkono mema na kumwadhibu mwenye kuunga mkono maovu.

Na mnapoamkiwa kwa maamkuzi, basi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au mrejeshe hayo hayo. Uislamu umelifanya neno 'Tawhid' kuwa ni nembo ya itikadi yake; na umefanya Salaam kuwa ni maamkuzi yanayohusiana nao, kuonyesha kuwa mwelekeo wake katika maisha ni kueneza amani (salaam) na kuusimamisha uadui.

Kuongezea kuwa maana ya neno lenyewe Islam ni kuusalimisha uadilifu na wema na heri na amani. Zaidi ya hayo Salaam ni katika majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴾

"Yeye ndiye Mwenyezi Mungu hapana mola isipokuwa Yeye tu; Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Jabbar, Mkubwa. Mwenyezi Mungu yuko mbali na hao wanaomshirikisha naye" (59:23)

Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuhisabu kila jambo.

Ana hisabu kuacha kuitikia salaam na mengineyo katika kuacha haramu na kutenda mambo ya wajibu.

Mafakihi wametoa dalili kwa Aya hii kuhusu wajibu wa kuitikia salaam, ama kwa mfano huo huo, yaani kumrudishia salaam aliyekuamkia kwa herufi hizo hizo bila ya kuongeza au kupunguza; kwa mfano kuongeza: Wa rahmatullah nk. Kuitikia salaam ni 'wajib ainy' (wajibu wa mtu mwenyewe) kama ikielekezwa kwa mtu maalum.

Na 'wajibu kifaya', kama ikielekezwa kwa watu wengi; kwa maana kama baadhi wakiitikia, imetosheleza kwa waliosalia; vinginevyo wote watalaumiwa na kustahiki adhabu. Kuna Hadith isemayo: "Kuamkia ni Sunna na kuitikia ni wajib."

Wafuasi wa Abu Hanifa wamesema makusudio ya neno Tahiya katika Aya ni kukirimiwa kwa mali. Mwenye kukupa zawadi kitu, basi ni juu yako kumpa zawadi ya kiasi alichokupa au zaidi[11] .

NJIA MBALI MBALI ZA KUTHIBITSHA MAREJEO (UFUFUO)

Uislamu umeipa kipaumbile misingi ya mwanzo ya uislamu na kuithibitisha kwa mifumo mbali mbali. Misingi hiyo ni kumwamini Mungu, Mitume na Siku ya Mwisho. Katika kitabu cha kwanza cha Tafsir Kashif, umewekea kila moja misingi hiyo mlango: Wa kwanza, tumeuzungumzia kwa anuani ya Tawhidi katika kufasiri 2: 21, wa pili, tumeuzungumzia kwa anuani ya 'Leteni Sura mfano wake' katika kufasiri 2: 23, na wa tatu, tumeulezea kwa anuani ya 'vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu' katika kufasiri 2: 28.

Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an yenye hekima zinazoelezea ufufuo, atakuta aina nyingi, miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:

1. Kutolea habari kutokea Kiyama:

﴿يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴾

"Siku itabadilishwa ardhi hii kuwa ardhi nyingine na mbingu; nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja, Mwenye nguvu." (14:48)

2. Kuelezea pamoja na kusisitiza kwa kiapo na kuondoa shaka; kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo: Kwa yakini atawakusanya siku ya Kiama, halina shaka hilo.

3. Kutolea dalili uwezekano wa ufufuo kwa kuumbwa mbingu na ardhi:

﴿أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ بَلَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

"Je, hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu - aliyeziumba mbingu na ardhi na hakuchoka kwa kuziumba - Ana uwezo wa kuwafufua wafu? Ndio, hakika Yeye ni muweza wa kila kitu" (46:33)

4. Kutoa dalili kwa kuumbwa mimea:

﴿وَاللَّـهُ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَسُقْنَاهُ إِلَىٰ بَلَدٍ مَّيِّتٍ فَأَحْيَيْنَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا كَذَٰلِكَ النُّشُورُ ﴾

"Na Mwenyezi Mungu ndiye anayepeleka pepo ziyatimue mawingu na tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa na kwayo tukaihuisha ardhi baada ya kufa kwake; kama hivyo ndivyo kufufuliwa." (35:9)

5. Kutoa dalili kwa kuumbwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu:

﴿فَسَيَقُولُونَ مَن يُعِيدُنَا قُلِ الَّذِي فَطَرَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ﴾

"Hapo watasema: Ni nani atakayeturudisha? Sema: Ni yule aliyewaumba mara ya kwanza" (17:51)

Kutoa dalili kwa ushahidi uliotokea. Miongoni mwa matukio hayo ni haya yafuatayo: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwafisha jamaa katika wana wa Israel kisha akawafufua Qur'an yaeleza juu ya hilo

﴿وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَىٰ لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْكُمُ الصَّاعِقَةُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ ﴿٥٥﴾ ثُمَّ بَعَثْنَاكُم مِّن بَعْدِ مَوْتِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴾

"Na mliposema: 'Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi,' Yakawanyakuwa mauti ya ghafla na hali mwaona. Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru." (2: 55 - 56)

Mtu mmoja katika wana Israel alifufuliwa baada ya kuuliwa:

﴿فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا كَذَٰلِكَ يُحْيِي اللَّـهُ الْمَوْتَىٰ وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ﴾

"Tukasema: Mpigeni kwa baadhi yake (huyu ng'ombe), Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anawaonyesha dalili zake ili mpate kufahamu." (2:73)

Vilevile Mwenyezi Mungu alimfufua Uzair baada ya kufa kwake:

"Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua " (2: 259)

Pia Mwenyezi Mungu aliwafufua ndege wane wa Ibrahim baada ya kuwakatakata na kuwaweka mafungu:"kisha waite, watakujia mbio" (2:260)

Na aliwafufua watu wa pangoni baada ya kuwafisha miaka 309:

"Namna hii tuliwafufua ili waulizane baina yao" (18: 19)

Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ﴾

"Na hakika tumewapigia watu mifano ya kila namna katika hii Qur'an ili wapate kukumbuka." (39:27)

Je, atakumbuka mjinga anayefahamishwa yule ambaye hashindwi na kitu chochote na yule asiyeweza kitu chochote? Vipi ataamini mnafiki siku watakayotukuzwa wakweli na kudhalilishwa wanafiki? Wala sijui ni madhara gani watakayopata jamii au watu kwa kuamini siku atakayopambanuliwa mwema na mwovu na mahakama watakayokuwa sawa watu wote mbele ya haki na uadilifu?