TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17269
Pakua: 3413


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17269 / Pakua: 3413
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

Mwandishi:
Swahili

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SITA

﴿إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا أَن يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَافٍ أَوْ يُنفَوْا مِنَ الْأَرْضِ ذَٰلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنْيَا وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴾

33.Hakika malipo ya wale wanaopigana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya ufisadi katika ardhi, ni kuuawa au kusulubiwa au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho au kuhamishwa katika nchi. Hii ndiyo fedheha yao katika dunia, na Akhera watapata adhabu kubwa.

﴿إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن قَبْلِ أَن تَقْدِرُوا عَلَيْهِمْ فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾

34.Ila wale waliotubia kabla hamjawatia nguvuni. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

MALIPO YA UFISADI

Aya 33 - 34

MAANA

Hakika malipo ya wale wanaopigana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya ufisadi katika ardhi.

Makusudio ya kupigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kuwafanyia uadui watu. Kwani kuwafanyia uadui watu ndiko kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa sababu hii, ndipo ikawa adhabu yake ni haddi[14] katika haddi za Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya mwenye kufanya ufisadi, ni kila mwenye kuchomoa silaha kwa ajili ya kuwahofisha watu kwa kupiga, kuuwa, kunyan'ganya au kuvunja heshima. Iwe kwa Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu, bara au baharini, usiku au mchana na mjini au porini. Iwe ni kwa upanga, bastola, fimbo au jiwe, mradi tu ikiwa ni kuchafua amani ya watu wenyewe, mali zao au heshima yao.

Kosa hili linazalisha makosa mengi; kama kuvuruga amani, kudharau sharia, kumwaga damu, kunyakua mali na hata kuvunjia heshima. Kwa ajili hiyo ndio Mwenyezi Mungu akafanya malipo yake, ni yale aliyoeleza kwa kusema kwake:

Ni kuuawa au kusulubiwa au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho au kuhamishwa katika nchi. Hii ndiyo fedheha yao katika dunia na Akhera watapata adhabu kubwa.

Aya imeeleza adhabu nne.

1. Kuua. Kumeelezwa kwa tamko la kusisitiza, kwa maana ya kuwa ni lazima. Lau kama jambazi ataua mtu; kisha wasimamizi wa aliyeuawa wakasamehe, basi msamaha huo hauzingatiwi. Aliulizwa Imam Jafar as-Sadiq(a.s) unaonaje, ikiwa wasimamizi wa aliyeuawa wakichukua fidia na kumwaacha, itafaa? Akasema:La, ni lazima auawe.

2. Kusulubiwa msititizo wake ni kama katika kuuliwa. Namna yake ni maarufu kwa watu.

3. Kukatwa mikono na miguu kwa mabadilisho; yaani ukikatwa mkono wa kushoto, utakatwa mguu wa kulia. Usisitizo wake ni zaidi kuliko usisitizo wa kuuwa na kusulubu, Kwa sababu ya kukaririka kukata.

4. Kuhamishwa mji ulio mbali na mji wake, ambapo atahisi ugeni na kufukuzwa. Abu Hanifa anasema makusudio ya kuhamishwa ni kutiwa jela. Mwenye Al-Manar ameeleza juu ya kauli hii kwa kusema: "Hii ni kauli ya kustaajabisha sana."

Madhehebu yametofautiana katika utekelezaji wa hukumu hizi. Je zitatekelezwa kwa hiyari (kuchagua yoyote) au ni kuangalia kiasi cha kosa na adhabu yake inayolingana.

Shia Imamiya wamesema kuwa neno au kwa dhahiri linafahamisha hiyari. Kwa hiyo ataachiwa hakimu kutekeleza lile litakaloondoa ufisadi na litakalo kuwa na masilahi katika kuuwa, kusulubu, kukata au kuhamisha. Kauli hii iko karibu na ya Malik.

Shafii amesema kuwa: adhabu hii itatofautiana kulingana na kosa. Mwenye kuua tu atauawa, mwenye kuuwa na kuchukua mali atauliwa na kusulubiwa baada ya kuuawa kwa siku tatu. Mwenye kuchukua mali tu bila ya kuua, atakatwa kwa mabadilisho, mwenye kuwatisha wapita njia tu, bila ya kuua au kuchukua mali, atahamishwa.

Hanafi amesema kuwa akichukua mali na kuua, basi hakimu atakuwa na hiyari, akitaka atamkata kwa mabadilisho au amuuwe bila ya kumsulubu, na akitaka anaweza kumuuwa na kumsulubu. Namna ya kusulubu, ni kusulubiwa akiwa hai na tumbo lake litatobolewa kwa mkuki mpaka afe; na hatasulubiwa zaidi ya siku tatu.

Ila wale waliotubia kabla hamjawatia nguvuni. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Akitubia mkabaji watu njiani yeye mwenyewe kabla ya kushikwa, basi adhabu imemwondokea; kwa sababu hekima ya adhabu ni funzo la kutofanya tena, Kwa hiyo, akijizuia itakuwa hakuna wajibu uliobakia. Na huu ni ukweli wa mfano wa ubinadamu ulioko katika sharia za kiislamu.

Kwa hakika ni kuwa toba kabla ya kutiwa nguvuni mwenye hatia, inamwondolea adhabu tu, lakini haki ya watu ni lazima ailipe. Akinyanganya mali, basi ni lazima airejeshe au thamani yake au mfano wake akiwa ameiharibu. Na kama akiuwa, basi ni juu ya wasimamizi wa aliyeuawa kumuua wakitaka.

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ وَجَاهِدُوا فِي سَبِيلِهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴾

35.Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikia mfanye juhudi katika njia yake ili mpate kufaulu.

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لِيَفْتَدُوا بِهِ مِنْ عَذَابِ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَا تُقُبِّلَ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴾

36.Hakika wale waliokufuru lau wangekuwa na yote yaliyomo duniani, na mengine kama hayo, ili watoe fidia ya kuepukana na adhabu ya siku ya Kiyama, yasingelipokelewa kwao; na wana wao adhabu iumizayo

﴿يُرِيدُونَ أَن يَخْرُجُوا مِنَ النَّارِ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنْهَا وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ ﴾

37.Watataka watoke motoni, lakini hawatatoka humo, na wana wao adhabu inayodumu.

TAFUTENI NJIA YA KUMFIKIA

Aya 35-37

MAANA

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikia na mfanye juhudi katika njia Yake ili mpate kufaulu.

Kumcha Mwenyezi Mungu, kutafuta njia ya kumfikia (wasila) na kufanya juhudi katika njia Yake yote haya ni ibara yenye maana moja au ni maana yanayooana, kwa sababu kumcha Mwenyezi Mungu ni kuacha machukivu yake na kutafuta njia ya kumfikia ni kupata radhi zake.

Na juhudi inakusanya yote mambo mawili, Njia bora ya kumfikia Mwenyezi Mungu ni kuwapenda watu na kuwahudumia.

Niliwahi kusoma maneno kwenye Kitabu kimoja kikubwa yanayosema: "Ni muhali kwa asiyependa watu kujua hakika ya watu." Nasi tunaongezea: "Ni muhali kumpenda Mungu kwa asiyependa watu"

Hakika wale waliokufuru lau wangekuwa na yote yaliyomo duniani, na mengine kama hayo, ili watoe fidia ya kuepukana na adhabu ya siku ya Kiyama.

Mtu anajitolea milki yake yote ili apone ugonjwa na maumivu katika maisha haya; je kwa moto wa Jahannam itakuwaje.

Yasingelipokelewa kwao; na wana wao adhabu iumizayo.

Anakubali fidia yule anayehitajia, Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini, sasa anahitajia nini.

Watataka watoke motoni, lakini hawatatoka humo, na wana wao adhabu inayodumu.

Hii ni kauli wazi ya mkato kuwa mwenye kumpinga Muumba au akamwabudu mwingine, atakaa milele motoni. Aya nyingine inasema:

﴿كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا أُعِيدُوا فِيهَا وَقِيلَ لَهُمْ ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ﴾

"Kila watakapotaka kutoka humo watarudishwa mumo humo na wataambiwa: Onjeni adhabu ya moto ambayo mlikuwa mkiikadhibisha" (32:20)

Kuna makosa mengine ambayo hayatofautiani na kumkufuru Mwenyezi Mungu kwa dhambi na adhabu; kama vile kunyan'ganya vyakula vya umma na nyenzo za maisha na kuua.

﴿وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴾

38.Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao; ni malipo ya yale waliyoyachuma. Ndiyo adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

﴿فَمَن تَابَ مِن بَعْدِ ظُلْمِهِ وَأَصْلَحَ فَإِنَّ اللَّـهَ يَتُوبُ عَلَيْهِ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾

39.Mwenye kutubia baada ya dhuluma yake na akatengenea, basi hakika Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

﴿أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَيَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

40.Je, hujui kuwa Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na ardhi? Humwaadhibu amtakaye na humsamehe amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.

MWIZI MWANAMUME NAMWANAMKE IRABU

Aya 38 – 40

IRABU

Dhahiri ya neno 'Mikono yao' ni kuwa mikono yote miwili ikatwe, lakini dhahiri hii inaachwa kutokana na Hadith na Ijmai, kama ambavyo ujumla wa mwizi mwanamume na mwizi mwanamke unaachwa.

MAANA

Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao ; ni malipo ya yale waliyoyachuma. Ndiyo adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya adhabu, ni adhabu ya duniani. Kadiri zitakavyotofautiana sharia za Mwenyezi Mungu na za duniani katika kupinga aina ya kosa na adhabu na sharti za kuitekeleza, lakini zitaafikiana kuwa lengo ni kumkanya mkosaji kwa kuchunga amani na masilahi.

Imam Ali(a.s) anasema:"Watawala ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, wa kukinga aliyoyaharamisha katika ardhi yake" Wala haitiliwi manani kauli ya baadhi ya mafakihi kuwa lengo la adhabu, ni kuondoa adhabu ya akhera tu. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa rehema na mwadilifu wa kukuchanganya adhabu mbili kwa kosa moja.

Kukatwa mkono kuna masharti yafuatayo:-

1. Chenye kuibwa kiwe katika hifadhi na mwizi akitoe humo. Kwa mfano; mtu akiiba gari iliyofungwa ndani ya gereji, atakatwa na kilichoibwa kitarudiswa kwa mwenyewe. Na mwenye kuiba njiani au isiyofungwa ndani ya gereji, basi hakatwi mkono, bali ataaziriwa kwa namna atakayoona hakimu (kadhi) na kilichoibwa kitarudi kwa mwenyewe, wala hakuna kinyume cha hivyo.

2. Wameafikiana kuwa hakuna kukatwa mkono ila kitakachozidi robo dinari. Abu Hanifa amesema, ni dinari kamili.

3. Mwizi awe ni baleghe; kutokana na Hadith:"Imeondolewa kalamu kwa mtoto mpaka abaleghe, na kwa mwenda wazimu mpaka apone, na kwa aliyelala mpaka aamke." Malik anasema: "Hakuna tofauti baina ya mtoto na mkubwa."

4. Mwizi awe na akili; kutokona na Hadith hiyo iliyotangulia.

5. Wameafikiana kuwa baba hakatwi mkono kwa kuiba mali ya mwanawe; kwa Hadith:"Wewe na mali yako ni wa baba yako." Madhehebu manne na baadhi ya Shia wamesema kuwa: mama ni kama baba.

Hanafi, Shafi na Hambal, wamesema: hakatwi mkono mume au mke kwa kuiba mali ya mwenzake.

Malik amesema: hakatwi ikiwa ameiba ndani ya nyumba wanayoishi; vinginevyo atakatwa.

Shia wamesema: atakatwa kwa hali yoyote ile, ila akiiba posho yake na ya watoto wake.

6. Wizi usiwe katika mwaka wa njaa. Akiiba mwenye njaa chakula kwa namna ambayo amekosa budi ila kuiba, hatakatwa.

Ama namna ya kukatwa mkono, yameafikiana madhehebu manne kuwa: atakatwa kiganja kuanzia sehemu ya kiwiko.

Shia wamesema: vitakatwa vidole vya kiganja cha kulia, na kitaachwa kiganja na dole gumba. Kuna maelezo mengi yanayoambatana na utafiti huu, tunayaachia vitabu vya Fiqhi, kama vile Fiqhul imam Jafar as-Sadiq J.6.

Mwenye kutubia baada ya dhuluma yake na akatengenea, basi hakika Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Sunni wamesema: toba ya mwizi haimuondelei haddi (adhabu).

Shia Imamiya wamesema: akitubia kabla ya kuthibiti wizi kwa hakimu, basi hana haddi. Wameafikiwa juu ya hilo.

Mwenye Tafsir Al-Manar aliyesema: "Ikiwa wizi utafananishwa na ukabaji watu njiani, basi kauli ya kuwa haddi haipo, ni dhahiri, ikiwa mwizi atatubia kabla yakufika kwa hakimu"

Wameafikiana wote kwamba toba, haiondoi haki ya mwenye kuibiwa; Kwa hiyo ni lazima mali irudishwe ikiwa ipo na irudishwe badali ikiwa haipo.

Je, hujui kuwa Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na ardhi? Humwadhibu amtakaye na humsamehe amtakaye.

Msemo huu unaelekezwa kwa kila mwenye kuisikia Qur'an, sio kwa Mtume peke yake. Ndani yake mna ubainifu kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyeumba ulimwengu na binadamu, na kwamba yeye hafanyi ila lililo na heri na masilahi kwa waja wake.

Akimwaadhibu amtakaye katika wakosaji basi amefanya hivyo kwa kumpa malezi na kuwasalimisha watu na shari yake, Na, akimsamehe amtakaye katika waja wake waliotubia, basi anafanya hivyo kumhimiza kujitengeza.

﴿يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ لَا يَحْزُنكَ الَّذِينَ يُسَارِعُونَ فِي الْكُفْرِ مِنَ الَّذِينَ قَالُوا آمَنَّا بِأَفْوَاهِهِمْ وَلَمْ تُؤْمِن قُلُوبُهُمْ وَمِنَ الَّذِينَ هَادُوا سَمَّاعُونَ لِلْكَذِبِ سَمَّاعُونَ لِقَوْمٍ آخَرِينَ لَمْ يَأْتُوكَ يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ مِن بَعْدِ مَوَاضِعِهِ يَقُولُونَ إِنْ أُوتِيتُمْ هَـٰذَا فَخُذُوهُ وَإِن لَّمْ تُؤْتَوْهُ فَاحْذَرُوا وَمَن يُرِدِ اللَّـهُ فِتْنَتَهُ فَلَن تَمْلِكَ لَهُ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَمْ يُرِدِ اللَّـهُ أَن يُطَهِّرَ قُلُوبَهُمْ لَهُمْ فِي الدُّنْيَا خِزْيٌ وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴾

41. Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wanaofanya haraka kukufuru miongoni mwa wale wasemao kwa vinywa vyao, tumeamini, hali nyoyo zao hazikuamini.

Na miongoni mwa Mayahudi kuna wasikiao sana uwongo wasikiao kwa ajili ya watu wengine wasiokufikia, wanayageuza maneno kutoka mahali mwake; wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni, na msipopewa haya basi tahahadharini.

Na ambaye Mwenyezi Mungu anamtakia fitna huwezi kumpatia chochote mbele ya Mwenyezi Mungu

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao; wana fedheha duniani na Akhera watakuwa na adhabu kubwa.

﴿سَمَّاعُونَ لِلْكَذِبِ أَكَّالُونَ لِلسُّحْتِ فَإِن جَاءُوكَ فَاحْكُم بَيْنَهُمْ أَوْ أَعْرِضْ عَنْهُمْ وَإِن تُعْرِضْ عَنْهُمْ فَلَن يَضُرُّوكَ شَيْئًا وَإِنْ حَكَمْتَ فَاحْكُم بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴾

42.Wasikilizao sana uwongo walao sana haram. Basi wakikujia, hukumu baina yao au achana nao, na ukiachana nao, hawatakudhuru na chochote. Na ukiwahukumu basi hukumu baina yao kwa uadilifu; hakika Mwenyezi Mungu anapenda wadilifu.

﴿وَكَيْفَ يُحَكِّمُونَكَ وَعِندَهُمُ التَّوْرَاةُ فِيهَا حُكْمُ اللَّـهِ ثُمَّ يَتَوَلَّوْنَ مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَمَا أُولَـٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ ﴾

43.Watakufanyaje hakimu nao wanayo Taurat yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanakataa; na hao si wenye kuamini.

WASIKILIZAO SANA UWONGO

Aya 41 – 43

MAANA

Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wanaofanya haraka kukufuru, miongoni mwa wale wasemao kwa vinywa vyao, Tumeamini, hali nyoyo zao hazikuamini.

Huu ni msemo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake(s.a.w.w) akimpoza moyo na mambo ya wanafiki na Mayahudi, Kwa sababu mwisho hautakuwa wao.

Jumla hii inahusika na wanafiki. Kwa sababu kuamini kwa mdomo bila ya moyo ndiyo hakika ya hali yao.

Kukatazwa kuhuzunika ni kukatazwa na kulazimiana nako na kutoathirika nalo; Kwa sababu binadamu hana hiyari nalo, Ni nani mwenye akili anaye hiyari kujihuzunikia? Lakini inabaki kutawala akilini na kwa ajili ya dini.

Mtume Mtukufu(s.a.w.w) anasema:"Jicho linalia na moyo unahuzunika, wala hatusemi yanayomchukiza Mola."

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wanafiki aliashiria kwa Mayahudi, kwa kusema:

Na miongoni mwa Mayahudi kuna wasikiao sana uwongo, wasikiao kwa ajili ya watu wengine wasiokufikia.

Tena yamerudi mazungumzo kwa Mayahudi. Katika Aya hii kuna habari walizozitegemea wafasiri, ambazo ufupi wake ni kuwa, Taurat ilieleza wazi wajibu wa kurujumu[15] mzinifu. Ikasadifu wakati wa Mtume(s.a.w.w) mwanamume na mwanamke, katika mamwinyi wao, akazini.

Baadhi ya Mayahudi wakaona uzito kumrujumu. Wakatuma ujumbe kwa Mtume kumwuliza hukumu ya mzinifu. Wakawaambia wale wajumbe, akitoa fatwa kurujumu kataeni, na akifutu vinginevyo basi kubalini.

Mtume akawapa fat-wa ya kurujumu. Wakakataa wakidai kuwa Taurat haina hukumu ya kurujumu. Alipowatolea hoja, mmoja wa maulama wao, alikiri kuwa hukumu ya Taurat ni kurujumu; sawa na alivyosema Muhammad; na kwamba Mayahudi wameihusisha hukumu ya kurujumu kwa walalahoi tu na kutandikwa viboko kwa mamwinyi.

Kwa hiyo makusudio ya 'wasikiao uwongo' ni kwamba Mayahudi wanakubali uwongo kutoka kwa wanafiki na kutoka kwa baadhi yao.

Na, makusudio ya 'wengine wasiokufikia' ni wale waliotuma ujumbe kwa Mtume na wala wasije wao wenyewe.

Wanayageuza maneno kutoka mahali mwakekwa kuweka viboko mahali pa kurujumiwa.

Maana ya jumla hii yametangulia katika kufasiri (2:75).

Na vile vile imetangulia kwa herufi katika (4:45).

Wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni na msipopewa haya basi tahadharini.

Yaani walisema wale waliotuma ujumbe, kuwa Muhammad akifutu isivyokuwa kurujumu kubalini na akifutu kurujumu basi kataeni.

Na ambaye Mwenyezi Mungu anamtakia fitina, huwezi kumpatia chochote mbele ya Mwenyezi Mungu.

Wametofautiana wafasiri kuhusu makusudio ya fitna. Ashaira, yaani Sunni, wamesema ni ukafiri; na maana yake ni kuwa: mja yeyote ambaye Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa kafiri na mpotevu, basi hakuna yeyote awezaye kumzuia. Ashaira wamepondokea kwenye tafsiri hii, wakiongozwa na Arrazi, kwa vile wao wanajuzisha kwa Mwenyezi Mungu kumtakia mtu ukafiri na kumfanya awe kafiri, kisha amwadhibu.

Shia na Mu'tazila wamesema, makusudio ya fitna katika Aya hii ni adhabu; na maana yanakuwa ni kwamba ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumwaadhibu, basi hakuna yeyote atakayeweza kuzuwiya adhabu. Wamesema hivyo, kwa vile wao hawaoni kwa Mwenyezi Mungu amfanyie mtu jambo kisha amwadhibu nalo.

Tuonavyo sisi kuhusu tafsiri ya Aya hii ni kuwa: Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwakataza Mayahudi uongo, kugeuza, vitimbi na hadaa, na akawaahidi adhabu wakihalifu, lakini wao waliendelea kuwa na inadi wala hawakujali makatazo wala kinga. Ndipo Mwenyezi Mungu akaachana nao na wala asiwazuiye na fitna.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anatoa mwongozo na nasaha kwa watu, katika mambo yanayohusiana na vitendo vyao, na wala sio kuwalazimisha kwa nguvu. Hilo amelisisitiza Mwenyezi Mungu kwa kusema kwake.

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao.

Yaani hakutaka kuwategemezea utoharifu wa nyoyo na utakatifu wa nafsi. Bali amewahiyarisha katika hilo. Kwa kuzingatia haya, ndio imesihi kunasibisha fitna kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Tumeyafafanua hayo katika kufasiri (4:88)

Wasikiao sana uwongo, walao sana haram.

Amelikariri hilo Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kushutumu sana na kukanya sana hayo. Haramu ni mali ya haramu, kama riba na mfano wake. Kosa zaidi ya riba ni mali zinazochukuliwa na wakoloni na vibaraka wao, ili wananchi wabakie masikini na kuomba chakula kwa wale waliowanyang'anya vyakula vyao na mali zao.

Basi wakikujia, hukumu baina yao au achana nao, Na ukiachana nao, hawatakudhuru chochote. Na ukiwahukumu basi toa hukumu baina yao kwa uadilifu, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.

Huu ni ubainifu wa wadhifa wa hakimu Mwislamu, akiwahukumu watesi wasiokuwa Waislamu. Wameafikiana mafakihi kuwa ikiwa si katika walio katika dhima (chini ya himaya ya Kiislamu), basi hakimu atakuwa na hiyari akitaka atawahukumu na asipotaka atakataa; ataangalia masilahi.

Na wametofautiana mafakihi, ikiwa ni katika watu walio katika dhima. Mwenye Al-Manar katika upande wa Sunni, amesema ni wajibu kwa hakimu kuwahukumu. Na wamesema mafakihi wa Kishia, bali atakuwa na hiyari, akitaka atahukumu akitaka hatawahukumu.

Na kama akiamua basi ni wajibu juu yake kuhukumu kwa hukumu ya kiislamu, si kwa hukumu ya dini yao; kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:'Na ukiwahukumu basi hukumu baina yao kwa uadilifu.'

Ikiwa mmoja wa mahasimu wawili ni Mwislam na mwingine si Mwislam, basi ni wajibu kwa hakimu kukubali madai na kuhukumu kama vile alivyosema Mwenyezi Mungu, kwa maafikiano ya Waislamu wote.

Watakufanyaje hakimu, nao wanayo Tawrat yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanakataa.

Mayahudi walitaka kuhukumiwa kwa Mtume(s.a.w.w) kuhusu mzinifu; alipowahukumu walikataa hukumu yake baada ya kumteua kuwa hakimu. Bora wasingemfanya hakimu tangu mwanzo.

Lakini kumkubali kuwa hakimu, kisha wakatae hukumu yake ni jambo la kushangaza. Hii ni pamoja na kuwa wao wanajua kwa yakini kuwa Mtume(s.a.w.w) atahukumu kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu iliyo katika Tawrat.

Na hao si wenye kuamini.

Yaani hakuna la kushangaza katika kuikataa hukumu ya Mtume baada ya kumridhia kuwa hakimu na baada ya kuhukumu kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu wao hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Tawrat kwa imani ya kweli; isipokuwa wanaamini hawaa yao na matakwa yao. Na kila asiyeridhia haki na hukumu yake, basi hayuko katika imani ya kweli awe Yahudi au Mwislam.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴾

"Naapa kwa Mola wako! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu katika yale wanayohitalifiana baina yao. Kisha wasione dhiki katika nyoyo zao kwa uliyohukumu na wanyeyekee kabisa kabisa" (4:65)

﴿إِنَّا أَنزَلْنَا التَّوْرَاةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ يَحْكُمُ بِهَا النَّبِيُّونَ الَّذِينَ أَسْلَمُوا لِلَّذِينَ هَادُوا وَالرَّبَّانِيُّونَ وَالْأَحْبَارُ بِمَا اسْتُحْفِظُوا مِن كِتَابِ اللَّـهِ وَكَانُوا عَلَيْهِ شُهَدَاءَ فَلَا تَخْشَوُا النَّاسَ وَاخْشَوْنِ وَلَا تَشْتَرُوا بِآيَاتِي ثَمَنًا قَلِيلًا وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ﴾

44.Hakika tuliteremsha Tawrat yenye uongozi na nuru, ambayo kwayo Manabii waliojisalimisha na watawa na wanazuoni, waliwahukumu mayahudi; kwani walitakiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Nao walikuwa mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu bali niogopeni mimi. Wala msiuze Aya zangu kwa thamani chache. Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio Makafiri.

USIWAOGOPE WATU

Aya 44

MAANA

Hakika tuliteremsha Tawrat yenye uongozi na nuru.

Kila Kitabu alichokiteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume yake, basi ni mwangaza unaoongoza kwenye haki na kheri. Tawrat ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu alichomteremshia Musa(a.s) , ni mwongozo na nuru.

Ama Tawrat ya sasa haikutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu iko mbali na kuwa ni mwangaza na nuru na kuwa ni haki na heri.

Mafunzo yake yanasimamia ubaguzi na kugawa watu; yanawafanya Mayahudi kuwa ni taifa teule la Mwenyezi Mungu; inawahalalishia kuyapiga vita mataifa mingine, kuuwa watu, kuwachinja wanawake na watoto, kunyakuwa mali zao na kuikalia miji yao.

Angalia Kitabu cha Waamuzi 20: 13 – 14.

Ambayo kwayo Manabii waliojisalimisha na watawa na wanazuoni waliwahukumu Mayahudi; kwani walitakiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Yaani mitume waliokuja baada ya Musa, kama vile Daud, Suleiman, Zakariya na Yahya walikuwa wakiwaongoza Mayahudi kwa hukumu ya Tawrat ambayo ni uongozi na nuru; wakiwahalalishia halali na kuwaharamishia haramu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu; 'Manabii waliojisalimisha maana yake ni kuwa mitume wa Mwenyezi Mungu walijisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, wakawahukumu Mayahudi kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu si kwa matakwa yao wala kwa ijtihadi yao au mapenzi yao; kama walivyofanya Mayahudi wakati wa Mtume, Muhammad(s.a.w.w) kumtaka awahakumie mzinifu vile watakavyo wao.

Vilevile watawa wa kiyahudi, maulama wao na makadhi wao, waumini wenye ikhlasi walikuwa wakihukumu yale waliyoyajua na kuyahifadhi kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Nao walikuwa mashahidi juu yake.

Maana ni kuwa watawa na maulama walikuwa wakikitumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala hawakipingi. Hapana mwenye shaka kuwa mwenye kuitukuza kauli na akaitumia, anakuwa ameitolea ushahidi kwa kitendo kabla ya kauli, kuwa ni haki na sawa.

Basi msiwaogope watu bali niogopeni mimi. Wala msiuze Aya zangu kwa thamani chache.

Mwenye kuijua hukumu ya Mwenyezi Mungu hawezi kuhalifu ila kwa mambo mawili. Ama kwa kuhofia cheo chake kuondoka au kuwa na tamaa ya mali. Mwenyezi Mungu ameliashiria la kwanza kwa kusema:'Basi msiwaogope watu, bali niogopeni mimi'

Na la pili ameliashiria kwa kauli yake: 'Wala msiuze Aya zangu kwa thamani chache.' Yaani, Enyi Maulama wa Kiyahudi! Fanyeni lile mnaloliona ni haki wala msiogope lawama na wala msibadilishe kwa tamaa ya rushwa.

Ikiwa msemo huu kwa dhahiri yake unaelekezwa kwa maulama waliobadilisha hukumu ya mzinifu ya kurujumiwa kuwa ya viboko, basi kwa uhakika unamhusu kila mwenye kujaribu kugeuza kwa kuhofia au kwa tamaa.

Kwa ufasaha zaidi wa kutafsiri Aya hii ni kauli ya Ali, Amirul-muminin(a.s) katika kuwasifu mawalii wa Mwenyezi Mungu:"Kwa ajili yao kimesimama Kitabu na kwa ajili ya Kitabu wamesimama, hawaoni matarajio zaidi ya wanayotarajia wala hofu zaidi ya wanayohofia"

Yaani hawamtaraji zaidi ya Mwenyezi Mungu wala hawamwogopi isipokuwa yeye.

Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya inayofuatia hii (45) anasema:"Basi hao ndio Madhalimu," katika Aya 47, anasema:"Basi hao ndio Mafasiki." Katika Aya hiyo tutabainisha kupatikana sifa ya ukafiri, dhuluma na ufasiki kwa mmoja.