TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17270
Pakua: 3413


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17270 / Pakua: 3413
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SITA

﴿وَكَتَبْنَا عَلَيْهِمْ فِيهَا أَنَّ النَّفْسَ بِالنَّفْسِ وَالْعَيْنَ بِالْعَيْنِ وَالْأَنفَ بِالْأَنفِ وَالْأُذُنَ بِالْأُذُنِ وَالسِّنَّ بِالسِّنِّ وَالْجُرُوحَ قِصَاصٌ فَمَن تَصَدَّقَ بِهِ فَهُوَ كَفَّارَةٌ لَّهُ وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

45.Na tuliwaandikia humo ya kwamba nafsi kwa nafsi na jicho kwa jicho na pua kwa pua na sikio kwa sikio na jino kwa jino na majeraha yana kisasi, Lakini atakayesamehe, basi itakuwa kafara kwake. Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.

﴿وَقَفَّيْنَا عَلَىٰ آثَارِهِم بِعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ التَّوْرَاةِ وَآتَيْنَاهُ الْإِنجِيلَ فِيهِ هُدًى وَنُورٌ وَمُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ التَّوْرَاةِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةً لِّلْمُتَّقِينَ ﴾

46.Na tukamfuatishia Isa bin Maryam katika nyao zao kuyasadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Tawrat, na tukampa Injil ndani yake mna mwongozo na nuru, na isadikishayo yaliyo kabla yake katika Tawrat, na mwongozo na mawaidha kwa wenye takua.

﴿وَلْيَحْكُمْ أَهْلُ الْإِنجِيلِ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فِيهِ وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴾

47.Na watu wa Injil wahukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu. Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio mafasiki.

MTU KWA MTU

Aya 45 - 47

MAANA

Na tuliwaandikia humo ya kwamba nafsi kwa nafsi na jicho kwa jicho na pua kwa pua na sikio kwa sikio na jino kwa jino na majeraha yana kisasi.

Aya hii ni miongoni mwa Aya za hukumu, na maudhui yake ni kisasi, Katika Fiqh ya kiislamu kuna mlango mahsusi. Hukumu hii, mtu kwa mtu, iliteremshwa katika Tawrat na sheria ya kiislamu haikuifuta.Yametangulia maelezo ya kisasi katika kufasiri (2:178)

Lakini atakayesamehe basi itakuwa kafara kwake.

Yaani mwenye kukosewa akimsamehe mkosa, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) ataujaalia msamaha huo ni kafara ya dhambi zake.

Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.

Maelezo yatakuja katika Aya inayofuatia;

Na tukamfuatishia Isa bin Maryam katika nyao zao kuyasadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Tawrat.

Dhamir katika kuwafuatishia inawarudia mitume, Yaani tulimtuma Isa baada ya mitume waliokuwa wakihukumu kwa Tawrat, na yeye akaithibitisha kwa kauli yake na vitendo vyake. Amenukuliwa katika Injil yao kuwa yeye alisema: "Mimi sikuja kuitangua Tawrat bali nimekuja kuitimiza," (Mathayo 5:17) yaani nizidishe hukumu na mawaidha.

Na tukampa Injil, ndani yake mna mwongozo na nuru.

Ni hali ya kila Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Mitume wa Mwenyezi Mungu. Injil aliyoisifu Mwenyezi Mungu kwa uwongozi na nuru ni Injil ile iliyotamka Tawhid (umoja wa Mwenyezi Mungu), ikakanusha utatu na ikathibitishia utume wa Muhammad(s.a.w.w)

Na isadikishayo yaliyo kabla yake katika Tawrat.

Ambayo inaamrisha uadilifu na hisani; wala sio kuua na kunyang'anya.

Na mwongozo na mawaidha kwa wenye takua.

Unaweza kuuliza : kuwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameisifu Injil aliyoiteremsha kwa Isa kwa uwongozi na nuru; tena akaisifu mara ya pili kwa uwongozi na mawaidha kwa wamchao Mwenyezi Mungu; sasa kuna wajihi gani wa kukaririka sifa za uwongozi katika Aya moja?

Jibu : Neno mwongozo la kwanza limekuja kusifu hali halisi ya Injil hiyo yenyewe tu bila ya kuangalia kuitumia, na neno mwongozo la pili ni la kusifu kuitumia; yaani Injil hii atanufaika nayo na kuwaidhika na mawaidha yake yule amchaye Mwenyezi Mungu; sawa na kusema: Ananufaika na mwangaza mwenye macho! Imam Ali(a.s) amesema:"Huenda mwenye elimu akauliwa na ujinga wake na elimu anayo, isimfae kitu."

Tunarudia tena kuwa makusudio ya Injil katika Aya ni Injil ambayo inamwepusha Mwenyezi Mungu na mtoto na kukana Uungu wa Isa(a.s) na kubashiria utume wa Muhammad.

Na watu wa Injil wahukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu.

Watu wa Injil ni Wakristo, watu wa Tawrat ni Mayahudi na watu wa Qur'an ni Waislamu. Mwenyezi Mungu amememwamrisha kila mwenye dini na kuamini Kitabu katika vitabu vya Mwenyezi Mungu, basi akitumie na kushikamana na hukumu zake.

Yeyote mwenye kwenda kinyume, basi atakuwa ni mzushi mwongo, awe Yahudi, Mkristo au Mwislam, hayahusu kundi fulani; wamehusishwa kutajwa watu wa Injil kwa vile mazungumzo ni yao.

UKAFIRI, UFASIKI NA DHULUMA

Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio mafasiki.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema katika Aya iliyotangulia, 44: "Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio Makafiri." Katika Aya ya 45 amesema: "Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu." Na katika Aya hii amesema: "Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio Mafasiki."

Sifa zote tatu zinasifu hali moja. Wafasiri wametofautiana katika wajihi na taawili; nasi tunaziacha kauli zao kwa kuepuka kurefusha kurasa.

Ama rai yetu ni kama ifuatavyo:- Hakika dini ni itikadi na sharia. Itikadi ni sifa za moyoni, nayo ina misingi yake ambayo ni kumwamini Mwenyezi Mungu na sifa zake, na kuamini Vitabu vyake, Mitume yake, Malaika wake na Siku ya Mwisho. Na sharia ni amali inayoambatana na kauli na vitendo.

Tamko la Ukafiri likitamkwa peke yake bila ya kuambatana na jingine; kama kusema: fulani ni kafiri, basi itaeleweka kuwa yeye anakana misingi ya kiitikadi yote au baadhi.

Ikisemwa: Fulani ni fasiki, itafahamika yeye anakubali dini kwa misingi yake na matawi yake, lakini anapuuza tu na kuaacha kutenda sharia zote au baadhi. Hii ni ikiwa matamko yote mawili yametajwa peke yake bila ya kutegemezwa kwenye kitu chochote. Ama ukitegemezwa ufasiki kwenye itikadi, kama kusema: Fulani ni fasiki wa itikadi, basi makusudio ya ufasiki hapo yatakuwa ni ukafiri. Hiyo imetumiwa katika Qur'an pale Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema.

﴿وَلَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكَ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ وَمَا يَكْفُرُ بِهَا إِلَّا الْفَاسِقُونَ﴾

"Hakika tumekuteremshia ishara zilizo wazi, na hawazikufuru ila mafasiki" (2:99)

Na kama neno ukafiri likitegemezwa kwenye amali na si katika itikadi, basi makusudio yake yatakuwa ni ufasiki. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

﴿وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴾

"Na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea. Na atakaye kufuru basi Mwenyezi Mungu si muhitaji wa viumbe" (3:97)

Mwenyezi Mungu amemsifu na ukafiri mwenye kuacha Hijja pamoja na kuwa anaamini misingi yote. Kwa hiyo hapo makusudio ya ukafiri yanakuwa ni ufasiki.

Ama neno dhuluma, inajuzu kulitumia kwa ukafiri na ufasiki, kwa sababu kafiri na fasiki anakuwa ameidhulumu nafsi yake kwa kuitia katika adhabu jambo isiloliweza. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:"Na waliokufuru ndio madhalimu" (2:254)

Na akasema tena:"Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule afichaye ushahidi alionao utokao kwa Mwenyezi Mungu" (2:140)

Kuficha ushahidi kwa ujumla hakuwajibishi ukafiri kwa maafikiano ya Waislamu wote.

Kwa hali hii inatubainikia kuwa ukafiri ufasiki na dhulma ni maneno yaliyokuja katika Qur'an kwa maana moja. Kwa hiyo basi, inafaa kusifiwa nayo asiyehukumu kwa aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu.

Makusudio ni kutilia mkazo, makemeo kwa asiyehukumu kwa haki, ni sawa awe amehukumu kwa batili au aliacha kuhukumu.

Vile vile anaambiwa hayo yule aliyehukumiwa kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu akaacha kutekeleza.

Kwa mnasaba huu, tunaashiria kuwa mafakihi wameafikiana kuwa mwenye kukana hukumu ya kisharia iliyothibiti kwa Ijmai ya Waislamu wote; kama vile wajibu wa Swala na uharamu wa zina basi yeye ni kafiri; na mwenye kuihalifu lakini anaikubali, basi ni fasiki.

﴿وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ الْكِتَابِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ فَاحْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ عَمَّا جَاءَكَ مِنَ الْحَقِّ لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِي مَا آتَاكُمْ فَاسْتَبِقُوا الْخَيْرَاتِ إِلَى اللَّـهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴾

48.Na tumekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Kitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao kwa kuacha haki iliyokufikia. Na kila (Umma) katika nyinyi, tumeujalia sharia yake na njia yake. Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka, angewafanya umma mmoja, lakini ni kuwajaribu katika hayo aliyowapa. Basi shindaneni katika mambo ya kheri, marejeo yenu nyote ni kwa Mwenyezi Mungu; naye atawaambia yale mliyokuwa mkihitilafiana.

﴿وَأَنِ احْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ وَاحْذَرْهُمْ أَن يَفْتِنُوكَ عَن بَعْضِ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ إِلَيْكَ فَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمْ أَنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُصِيبَهُم بِبَعْضِ ذُنُوبِهِمْ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ لَفَاسِقُونَ ﴾

49.Na hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate mapenzi yao. Nawe jihadhari nao wasije wakakutia kwenye fitna ukaacha baadhi ya yale aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu. Na kama wakikengeuka, basi jua kwamba Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi katika watu ni wafasiki.

﴿أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ ﴾

50.Je wanataka hukumu za Kijahiliya. Na ni nani aliye mzuri zaidi kwa hukumu kuliko Mwenyezi Mungu; kwa watu wenye yakini.

KILA UMMA NA SHARIA YAKE

Aya 48 - 50

MAANA

Na tumekuteremshia Kitabu kwa haki kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Kitabu na kuyalinda.

Makusudio ya Kitabu kilichotajwa kwanza ni Qur'an na Kitabu kilichotajwa mara ya pili ni jinsi ya vitabu vyote vya Mwenyezi Mungu; ikiwemo Tawrat, Injil n.k.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja Tawrat na Injil, na Musa na Isa(a.s) , amefuatishia kutaja Qur'an na Muhammad(s.a.w.w) .

Ameisifu Qur'an kwa sifa mbili:

Kwanza : kwamba hiyo inasadikisha vitabu vyote vilivyoteremshiwa Mitume.

Pili : kuwa ni mlinzi wa wa vitabu vilivyotangulia. Maana ya ulinzi wa Qur'an kwa Tawrat na Injil ni kwamba: inashuhudia kuwa vitabu viwili hivyo ni haki na ukweli na inatolea habari, misingi na hukumu zilizopotoshwa ndani yake, ili mtu apambanue ya asili na ya kuongezwa ambayo viongozi wa dini wameyanasibisha kwa Mwenyezi Mungu kwa uzushi na uwongo.

Basi hukumu baina yao (yaani Mayahudi) kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao.

Kimsingi ni kuwa Mtume(s.a.w.w) hahukumu ila kwa haki, wala haghafiliki na dogo au kubwa, na ni muhali kufuata matamanio ya viumbe. Vipi isiwe hivyo na kauli yake na vitendo vyake ni kipimo cha kupimia haki na uadilifu. Lau tukikadiria kutokea mlaghai anayejaribu kumhadaa Mtume kwa kujionyesha, na Mtume akurubie, kuhadaika kwa kuzingatia kuwa yeye ni mtu, basi hapo Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamlinda kwa msaada wake na kumfahamisha haki halisi kabla ya kutokea chochote cha mlaghai. Mwenyezi Mungu anasema:

"Na kama tusingelikuimarisha ungelikuribia kuwaelekea kidogo" (17:74)

Unaweza kuuliza : Maadamu mambo yako hivyo, kwa nini Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake aliye Maasum hivi?

Jibu :Kwanza , tumekwisha bainisha katika sehemu zilizotangulia kuwa maneno yakitokea kwa mkubwa haiangaliwi hali na cheo cha anayeambiwa. Hilo litaangaliwa ikiwa maneno yametoka kwa aliye sawa na anayeambiwa au mdogo zaidi yake.

Pili : hakika Mwenyezi Mungu (swt) anajua kuwa maulama waovu katika umma wa Muhammad(s.a.w.w) wataboresha hukumu potofu kwa vijisababu vya kishetani. Ndipo akamwambia Mtume wake Mtukufu maneno haya, kumhadharisha na wanaochezea dini kwa kufuata mapenzi ya watawala.

Na kila (umma) katika nyinyi, tumeujaalia sharia yake na njia yake.

Dhamir katika nyinyi inawarejea watu wote au makundi matatu (Mayahudi, Wakristo na Waislamu). Na sharia ni hukumu za kimatendo wanazozifuata binadamu kwa kumtii Mwenyezi Mungu na kutaka radhi zake na malipo yake. Kwa hakika hasa ni kuwa neno halienei zaidi kuliko neno 'Dini', kwa sababu dini inakusanya sharia na misingi ya itikadi.

Maana ya njia, ni njia iliyo wazi; yaani Mwenyezi Mungu amejaalia kila umma sharia iliyo wazi isiyokuwa na mkanganyo wowote.

Aya hii, ni kauli wazi kuwa sharia ya Mwenyezi Mungu haikuwa moja kwa watu wote na wakati wote; na kwamba wakati ulioupita ilikuwa ya muda maalum; na kwamba dini zinaafikiana na kuwa moja katika misingi ya itikadi tu, si katika sharia.

Utauliza ; Ikiwa mambo ni hayo, kwa nini sharia ya kiislamu imehusika na hukumu na kuendelea?

Hawezi kujua jibu la swali hili ila yule aliyesoma sharia za kiislamu, ambapo ataziona zimesimama kwenye misingi thabiti; ni muhali kubadilika kwa kubadilika zama na hali. Kwa sababu, zinaoana na mwanadamu akiwa ni mwanadamu, si akiwa ni wa zamani au wasasa. Mfano wa hayo ni kama ifuatavyo:-

Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi ila uweza wake, 'Kila mtu ni mwema mpaka uthibiti ubaya wake.' 'Suluhu ni bora', 'Inajuzu wenye akili kujithibitisha wenyewe', 'watu wako kwenye masharti yao,' Haddi hukingwa na shubuha,' 'Hapana madhara wala kudhuriana,' 'Dharura inahalalisha haramu,' 'Yakini haivunjwi ila na yakini mwenzake.' Kinga ni bora kuliko kuponya' 'Dhara haiondolewi na dhara mwenzake,' 'Asiyekuwepo anahoja mpaka aje' na mengineyo katika misamiati ya fiqh ambayo mafakihi wameiorodhesha katika mijalada ya vitabu vya fiqh. Kwa hiyo misingi hii ni muhali kuweza kugeuka ila litakapogeuka umbile la binadamu.[16]

Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka, angewafanya umma mmoja.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatofautisha watu na viumbe wengine kwa kuwafanya kuwa na mwelekeo wa ujinga na ujuzi, kuwa nyuma na kuen delea na kwa kufanya heri na shari; Kisha akamkataza hili akamwamrisha lile.

Kwa hiyo natija ya mwelekeo huu, amri na makatazo, ni kutofautiana watu, katika kuutumia mwelekeo huu, na katika kumtii Mwenyezi Mungu na kumwasi.

Lau Mwenyezi Mungu angelitaka asingempa mtu kipawa hiki, na kama angelifanya hivyo, basi watu wote wangelikuwa katika hali moja tu, sawa na wanyama, ndege na wadudu, wanajiendea tu hawajui heri wala shari au kufaulu au kufeli.

Lakini ni kuwajaribu katika hayo aliyowapa.

Yaani Mwenyezi Mungu ametupa kipawa hiki, akatuamrisha na kutukataza ili atufanyie mtihani: Ni nani mzuri wetu wa matendo? Ingawaje yeye anajua siri na dhamiri, lakini hamlipi mtu ila kwa amali wala hamwadhibu ila baada ya maonyo.

Basi shindaneni katika mambo ya kheri. Marejeo yenu nyote ni kwa Mwenyezi Mungu; naye ataawambia yale mliyokuwa mkihitilafiana.

Yaani akiwa Mwenyezi Mungu amempa binadamu kipawa hiki, na akaweka sharia mbali mbali kwa umma, ili yadhihirike matendo anayostahiki mtu kupata thawabu, basi ni juu yetu wote kuharakia mambo ya heri, kwa sababu ndiyo makusudio ya kwanza ya sharia. Na yeyote atakayefanya tofauti za sharia ndio chombo cha kuleta chuki na uadui, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) kesho atamhisabu na kumlipa atakachostahiki.

Na hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate mapenzi yao. Nawe jihadhari nao wasije wakakutia kwenye fitna ukaacha baadhi ya yale aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu.

Aya hii ni kuikariri Aya iliyoitangulia. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa iliyoitangulia ilishuka katika kuhukumiana Mayahudi katika zina, na hii imeshuka katika kuhukumiana katika kuua.

Lakini hakuna dalili yoyote katika mwelekeo huu wala mwengineo ulioko katika baadhi ya vitabu vya tafsir.

Tumebainisha katika kufasiri Sura (2:47) kwamba Qur'an inatumia kukaririka, kwa sababu ni njia yenye nguvu ya kueneza jambo. Zaidi ya hayo ni kwamba dhamir katika 'mapenzi yao' inawarudia Mayahudi. Ni katika njia ya Qur'an kulikariri na kulisisitiza jambo linalowahusu Mayahudi zaidi kuliko jambo jingine.

Na hii inafahamisha tu kuwa Mayahudi ni umma wa shari katika hali zote. Historia yao ya zamani na sasa inalishuhudia hilo. Hakuna yeyote anayewaona kuwa si washari ila watu wa shari tu. Hakika hii imedhihiri, kwa maana yake, kwa wote baada ya tukio la 5 Juni 1967.

Na kama wakikengeuka, basi jua kwamba Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao.

Yaani wakikengeuka na hukumu ya Mwenyezi Mungu, basi kutawaletea hizaya na balaa.

Unaweza kuuliza : kwa nini Mwenyezi Mungu amesema: "kwa baadhi ya dhambi zao" na wala asiseme 'kwa dhambi zao.' Je, hii inamaanisha kuwa Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa baadhi ya dhambi na nyingine atawasamehe?

Jibu : Kauli yake Mwenyezi Mungu kwa 'baadhi ya dhambi zao,' ni ishara ya kupinga kwao hukumu waliyohukumiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Maana yake ni kuwa; "Ewe Mtume! Kupinga kwa Mayahudi kusikuzuie kuhukumu, kwani Mwenyezi Mungu atawadhibu kwa dhambi yao."

Na hakika wengi katika watu ni wafasiki.

Fasiki ni yule anayemwasi Mwenyezi Mungu katika hukumu moja miongoni mwa hukumu zake. Watu wengi wako hivi, bali ni watu wote; isipokuwa wachache lakini neno wengi hutumika katika wingi na sio kinyume.

Je wanataka hukumu za Kijahiliya?

Kila hakimu anayehalifu hukumu ya Mwenyezi Mungu, basi amehukumu hukumu za kijahiliya, awe katika wakati wa Jahiliya au baada yake.

Na ninani aliye mzuri zaidi kwa hukumu kuliko Mwenyezi Mungu, kwa watu wenye yakini.

Hapana mwenye shaka kwamba kila hukumu yenye masilahi fulani kwa watu, basi hiyo ni hukumu ya Mwenyezi Mungu, ni sawa iwe imeelezewa na kauli wazi mahsusi ya Qur'an au Hadith au iwe haikuelezea. Na kila yenye madhara fulani kwa watu, basi Mwenyezi Mungu ni muhali kuiridhia.

Hata haki ya Mwenyezi Mungu inaondoka ikiwa italeta madhara. Inatosha kuwa ni dalili, kuwa kila hukumu inayonufaisha watu ni ya Mwenyezi Mungu, kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾

"Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anopowaita katika yale yatakayowapa uhai." (8:24).

Kwa sababu maana yake ni kuwa kila mwito wa uhai ni mwito wa Mwenyezi Mungu na wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

NAHW

wametofautiana wafasiri katika maana ya herufi 'lam' katika neno; kwa watu wenye yakini. Baadhi wamesema kuwa ni kwa maana ya mbele ya, yaani kwao watu wenye yakini. Wengine wakasema ni ya ubainifu.

Ilivyo hasa ni ya kuhusisha, kama vile kusema; Pepo ni kwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, kwa sababu, wenye yakini peke yao ndio wanaohukumu na kuitumia hukumu ya Mwenyezi Mungu.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴾

51.Enyi mlioamini! Msiwafanye kuwa marafiki Mayahudi na Manaswara; wao kwa wao ni marafiki. Na miongoni mwenu atakayewafanya urafiki nao, basi huyo ni katika wao, Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

﴿فَتَرَى الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ يُسَارِعُونَ فِيهِمْ يَقُولُونَ نَخْشَىٰ أَن تُصِيبَنَا دَائِرَةٌ فَعَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَ بِالْفَتْحِ أَوْ أَمْرٍ مِّنْ عِندِهِ فَيُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا أَسَرُّوا فِي أَنفُسِهِمْ نَادِمِينَ ﴾

52.Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema: Tunaogopa yasitusibu majanga. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake, wakawa wenye kujuta kwa yale waliyoyaificha katika nafsi zao.

﴿وَيَقُولُ الَّذِينَ آمَنُوا أَهَـٰؤُلَاءِ الَّذِينَ أَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ إِنَّهُمْ لَمَعَكُمْ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَأَصْبَحُوا خَاسِرِينَ ﴾

53.Na watasema walioamini: Hivi hawa ndio wale walioapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vigumu, ya kwamba wao wako pamoja nanyi? Zimepomoka amali zao na wamekuwa wenye hasara.

MAYAHUDI NAWAKRISTO MSIWAFANYE KUWA MARAFIKI

Aya 51 - 53

MAANA

Enyi mlioamini! Msiwafanye kuwa marafiki Mayahudi na Manaswara.

Neno rafiki limefasiriwa kutoka neno walii ambalo hapa lina maana ya rafiki au msaidizi, Dini ya kiislamu iko wazi kwa dini zote na jinsi zote.

Hakuna tofauti baina ya mweusi na mweupe wala baina ya mwarabu na asiyekuwa mwarabu wala baina ya Mwislamu na asiyekuwa Mwislamu katika usawa mbele ya kanuni.

Mtu yoyote, vyovyote atakavyokuwa, ana haki ya kuishi huru na kwa amani, yeye na mali yake, Wala hakuna haja ya kumchunga yeyote maadamu hawaudhi wengine.

Akikeuka mipaka na akafanya ufisadi, atahukumiwa. Mwislamu akimfanyia uovu asiyekuwa Mwislamu, ni wajibu wetu sisi Waislamu kumwadhibu na kujitenga naye. Myahudi au Mkristo akiufunga mkono wake na asituudhi, basi tutamnyooshea mkono wa heri na wema, hata kama anakana utume wa Muhammad na Qur'an. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ ﴿٨﴾ إِنَّمَا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ قَاتَلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَأَخْرَجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ وَظَاهَرُوا عَلَىٰ إِخْرَاجِكُمْ أَن تَوَلَّوْهُمْ وَمَن يَتَوَلَّهُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

"Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia hisani na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini, wala hawakuwafukuza katika nchi zenu, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao uadilifu.

Isipokuwa Mwenyezi Mungu anawakataza kuwafanya marafiki wale wanaopigana nanyi katika dini, na wakawafukuza katika nchi zenu na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu, na wawafanyao marafiki, basi hao ndio madhalimu" (60: 8 - 9)

Tukiziunganisha Aya hizi ambazo zimewahimiza Waislamu kuwafanyia wema na hisani watu wa mataifa yote na wa dini zote, ambao hakuwafanyia uadui Waislamu, pamoja na Aya hii tunayoifasiri, tukizichanganya katika mazungumzo mamoja, basi maana yake yanakuwa: Enyi mlioamini! Msiwafanye mawalii Mayahudi na Wakristo, kama wakiwafanyia uadui na kuwapiga vita. Ama wakiwa na usalama, basi tangamaneni nao kwa wema.

Muishi nyote kwa kujuana na kuzoeana; bali muwafanyie wema na uadilifu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anapenda uadilifu na wema kwa viumbe vyake vyote, wanomwamini na wanaomkufuru; kwa sharti moja tu, kutomfanyia ubaya yeyote.

Kwa sababu watu wote ni wa Mungu, na anayependeza zaidi kwake ni yule awanufaishaye zaidi watu wake Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo mbele ya Mwenyezi Mungu, utengamano mzuri na mtu yeyote ni kujizuia na kumfanyia uovu na kumwudhi. Ama mwenye kukanusha na akakufuru, basi ni juu yake kufuru yake.

Umetangulia ufafanuzi kuhusu aina za urafiki na kafiri na hukumu zake katika kufasiri (3:30)

Kwa mnasaba huu tunaishiria kuwa kuchukia kwetu Mayahudi sisi Waislamu hakuna sababu nyengine ila kwamba wamepigana nasi nchini mwetu, waliwatoa wanawake wetu na watoto wetu; kama ambavyo sababu ya kwanza na ya mwisho ya kuchukia kwetu na uadui wetu kwa Amerika na Uingereza na mataifa mengineyo, katika mataifa ya kikoloni yanayosaidia Israil, ni kuwa mataifa haya yamesaidia kutolewa Wapalestina nchini kwao. Kwa mara nyingine tunarudia anavyotuambia Mwenyezi Mungu;

﴿إِنَّمَا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ قَاتَلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَأَخْرَجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ وَظَاهَرُوا عَلَىٰ إِخْرَاجِكُمْ أَن تَوَلَّوْهُمْ وَمَن يَتَوَلَّهُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

"Isipokuwa Mwenyezi Mungu anawakataza kuwafanya marafiki wanaopigana nanyi katika dini, na wakawafukuza katika nchi zenu na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu, na wawafanyao marafiki, basi hao ndio madhalimu" (60: 9)

PETROLI NA MAYAHUDI NAWAKRISTO

Wao kwa wao ni marafiki.

Wafasiri wamekongamana kuwa makusudio yake ni baadhi ya Mayahudi ni marafiki wa baadhi ya Wakristo, na wala sio Makusudio kwamba kila kundi ni rafiki wa kundi jingine. Kwa sababu, makundi hayo mawili yana uadui zaidi kuliko uadui uliopo baina ya Wakristo na Waislamu. Kwani Mayahudi wanamzulia Maryam na zina na Waislamu wanamtukuza na kumtakasa na kila aibu.

Hakuna mwenye shaka kwamba wafasiri wametoa maana haya kutokana na wakati walioshi, ambapo hakukuwa na mashirika ya kimataifa ya petroli wala taasisi za ulanguzi na ulafi wa kunyonya mali za wananchi.

Ama leo baada ya kuweko mashirika hayo na taasisi hizo, wenye mashirka hayo, Wakristo wameona kuwa Mayahudi ndio njia bora ya kutegemea kuunga mkono ulanguzi wao na tamaa yao.

Kwa ajili hii wakaweka taifa la Kiisrail ndani ya Palestina na wakalisaidia na kulihami, wakalipangia njia za kufanyia uchokozi na kujipanua, wakaliahidi kusimama upande wake katika Umoja wa mataifa na Baraza la usalama, wakalifunga kwenye milki yao na kuzunguka kwenye sayari yao.

Kwa hiyo Israil ikawa inatekeleza mipango ya kikoloni na kufuata amri za kiuadui, baada ya kugundua kuwa uhai wake uko kwenye rahani ya kusikiliza na kutii amri za wakoloni na kutekeleza mipango yake, vinginevyo litakimbiwa na kutawalishwa taifa jingine.

Ikiwa wakoloni wameweka tamaa yao kwenye makucha ya waisrail, basi tunamtegemea Mwenyezi Mungu na kujiandaa na vita ili kurudisha haki iliyoporwa.

Na miongoni mwenu atakayewafanya urafiki nao basi huyo ni katika wao pamoja nao.

Yaani mwenye kuwafanya marafiki Mayahudi na Wakristo walio na uadui na Uislamuu basi yeye yuko katika hukumu yao, atahisabiwa hisabu yao na kuadhibiwa adhabu yao, Kwa sababu, 'mwenye kuwaridhia watu, basi yeye ni katika wao.' Aya hii ni dalili mkato kuwa vibaraka wa wakoloni wanaolinda masilahi ya wakoloni, wana makosa zaidi na hatari zaidi kuliko wakoloni wenyewe, au angalau ni kama wakoloni wenyewe. Kwa sababu wao ndio nguzo ya unyoyaji wao na uadui wao.

Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao. Inaonyesha, kutokana na mfumo wa Aya, kuwa hilo ni tukio halisi lililotokea. Kwa ufupi ni kuwa baadhi ya wanafiki, wenye maradhi nyoyoni mwao, walikuwa wakifanya urafiki na Mayahudi ambao walikuwa waki Tafsir ficha uadui kwa Uislamu na Waislamu na kuwaeleza mapenzi yao. Wakilaumiwa juu ya hilo husema: Unajuwaje pengine mambo yatageuka na Waislamu wawe wanyonge na nguvu iwe kwa Mayahudi na washirikina, kama hatukujipangia, tangu sasa na kuwaunga mkono, tutapata hasara na majanga.

Hii ndio maana dhahiri ya kauli yake Mungu Mwenyezi kwa Mtume:Wakisema: Tunaogopa yasitusibu majanga.

Na hivi ndivyo walivyo wazabizabina, wanajitia huku na kule, ili watakao shinda wawaambie sisi tulikuwa nanyi. Kwa maneno mengine ni kwamba wanafiki wako na wote kwa midomo, na kumbe hawana ila matamanio yao.

﴿يَحْلِفُونَ لَكُمْ لِتَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِن تَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَرْضَىٰ عَنِ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ﴾

"Wanaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi wala wao si katika nyinyi, bali wao ni watu wanaoogopa" (9:56)

Yaani wanahofia nafsi zao na masilahi yao.

Unaweza kuuliza : kwanini amesema wanakimbilia kwao na wala asiseme wanawakimbilia.

Jibu : Kusema 'kwao' ni kusisitiza, Kwa sababu mwenye kuingia katika kitu anatulizana ndani yake zaidi. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake, wakawa wenye kujuta kwa yale waliyoyaficha katika nafsi zao. Makusudio ya ushindi, ni Waislamu kuwashinda Mayahudi na Washirikina.

Na makusudio ya jambo jingine litokalo kwake ni kudhihirisha waliyo nayo wanafiki na kuwadhalilisha hao wanafiki na kuwafedhehesha. Maana ni kuwa wanafiki walijipangia kuwa maadui wa Uislamu, kwa kudhani kwamba Waislamu watafikwa na majanga kutoka kwa makafiri. Lakini mambo yalipogeuka na janga likawapata maadui wa Uislamu, walijuta wanafiki, lakini hakutafaa kujuta kwao! Na watasema walioamini: Hivi hawa ndio wale walioapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vigumu, ya kwamba wao wako pamoja nanyi?

Mwenyezi Mungu alipoudhihirisha ushindi wa Waislamu kwa maadui zao, wanafiki hawakuweza kuficha uchungu wao, midomoni mwao na nyusoni mwao. Waumini wakastaajabu kutokana na hali ya wanafiki ilivyofichuka, wakaambiana.

Hivi hawa si ndio wale waliokuwa wakiapa kwa nguvu jana kuwa wao wako nasi? Ni mahodari sana wa uwongo na ria. Zimepomoka amali zao na wamekuwa wenye hasara.

Arrazi na mwenye Al-Manar anasema inawezekana jumla hii kuwa ni katika maneno ya Mwenyezi Mungu na inawezekana kuwa ni katika maneno ya waumini. Lakini ilivyo hasa haiwezekani kuwa ni maneno ya Mwenyezi Mungu kabisa. Kwa sababu, mfumo wa Aya unafahamisha kuwa ni katika maneno ya waumini na wala sio habari inayoanza upya kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Maana yake nikuwa baada ya waumini kustajabia hali ya wanafiki na aibu yao walisema: Zimebatilika amali za wanafiki walizokuwa wakituonyesha, kama vile Saumu, Swala n.k. na wala hawakupata chochote katika thawabu. Wamekuwa wenye hasara duniani, kwa vile wamedhalilika, na wamepata hasara akhera kwa adhabu kali waliyoandaliwa.

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَن يَرْتَدَّ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ يُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴾

54.Enyi mlioamini! Atakayeritadi dini yake miongoni mwenu, basi Mwenyezi Mungu atawaleta watu anaoawapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa waumini, wenye nguvu juu ya makafiri, wenye kufanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anayelaumu. Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa, mwenye kujua.

WANYENYEKEVU KWA WAUMINI WENYE NGUVU KWA MAKAFIRI

Aya 54

MAANA

Enyi mlioamini! Atakayeritadi dini yake miongoni mwenu, Kuritadi ni kuwa kafiri baada ya kuwa Mwislamu.

Tumemtaja Murtadi na mafungu yake katika kufasiri (2:217).

Kukataza kuritadi, baada ya kukataza kufanya urafiki na maadui wa dini, kunatambulisha kuwa kufanya urafiki huko kunasababisha kuritadi. Kuna Hadith isemayo:"Lau mchungaji atachunga kandokando ya ugo, hataweza kuwadhibiti mbuzi wake kuingia ndani" Watu wa sera na wanahistoria wanasema, kuwa watu watatu waliritadi na kudai utume, wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , baada ya kuwa Waislamu.

Wa kwanza ni As-wad Al-Ansi, alidai utume katika Yemen na akawatoa wajumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) huko, Aliuawa siku moja kabla ya kufa Mtume(s.a.w.w) .

Wa pili ni Musaylamatul Kadh-dhab. Alidai Utume na akamwandikia Muhammad(s.a.w.w) hivi:"Kutoka kwa Musailama, Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwenda kwa Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ama baada ya hayo, mimi ni mshirika wako katika jambo hili na ardhi baina yetu iko nusu kwa nusu" Aliuawa wakati wa Abubakr. Watatu ni Twalha bin Khuwalid alidai utume, kisha akarudi kwenye Uislamu.

Ama Sajah ni mwanamke aliyedai utume wakati wa ukhalifa wa Abubakar na akaolewa na Musailama. Katika ndoa hii Abdalla alitunga shairi hili: "Saja na Musaylama wamekwisha kupatana, waongo wa duniani tena ni waongo sana."

Unaweza kuuliza : kuwa baadhi ya masheikh hawana sharti za mujtahid (uongozi) alizozikusudia Imam Ali(a.s) aliposema:"Mwenye kuichunga nafsi yake, mwenye kuihifadhi dini yake, mwenye kukhalifu hawaa yake, na mwenye kutii amri ya Mola wake"

Lakini pamoja na hivyo wanadai kuwa ni manaibu wa Maasum, na kwamba kuwapinga ni kumpinga Mwenyezi Mungu. Je, hukumu yao ni sawa na ya Muislama, Kwa sababu wote wanamzuilia Mwenyezi Mungu?

Jibu : atakuwa kama Musailama kwa masharti mawili:

Kwanza : kudai unaibu wa Maasum naye anajua kuwa yeye ni mzushi mwongo na kwamba yeye hastahiki.

Pili : kutoona kuwa ijitahidi na uadilifu ni sharti za msingi za unaibu wa Ma'sum na huku anajua kuwa ni wajib kwa hukumu za kimsingi za dini. Kukadiria huku kuko mbali sana, kwa sababu mwenye kudai unaibu wa Maasum anajiona kuwa ni katika watu waadilifu na wenye kujitahidi hata kama hamtii Mola wake na kuhalifu hawaa yake.

Hakuna mwenye shaka kwamba huyu anatofautiana na Musailama kwa upande wa kuritadi, lakini anaungana naye katika upande wa uwongo na ghururi.

Kimsingi ni kuwa elimu na ghururi ni vitu viwili tofauti visivyokutana, sawa na uwongo na uadilifu. Kwa sababu ghururi inamtenga mtu wake na hali halisi ilivyo, na kumpeleka kwenye ulimwengu wa dhana na ndoto, Na atakayekuwa hivi, hawezi kuongoka kwenye usawa, Basi atawaleta Mwenyezi Mungu watu.

Wametofautiana wafasiri kuhusu waliokusudiwa katika neno 'watu' Arrazi amenukuu kauli sita, Mwenyezi Mungu hakuwataja majina yao, bali amewashiria kwa sifa zao.

Kwa hivyo, kila mwenye sifa tano, zilizotajwa katika Aya, basi ndiye aliyekusudiwa, Sifa zenyewe ni:-

1. Anaowapenda nao wanampenda.

Mwenyezi Mungu kumpenda mja wake, ni kumwinua kesho na kumneemesha kwa pepo na radhi. Ama pendo la mja kwa Mwenyezi Mungu, haliepukani na kuwapenda waja wa Mwenyezi Mungu, sawa na ambavyo kuipenda haki hakuepukani na kuwapenda wanaoitumia, na kuichukia batili kusivyoepuka na kuwachukia watu wa batili.

2. Wanyenyekevu kwa waumini.

kwa sababu kumnyenyeka mumini ni kuitakasa na kuitukuza imani na ikhlasi na sio mtu mwenyewe. Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake:"Na uinamishe bawa lako kwa yule anayekufuata katika walioamini" (26:215).

Ilivyo ni kuwa wao hawakustahiki heshima hii ila kwa imani na ikhlasi yao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

3. Wenye nguvu juu ya makafiri. Kwani kuwa na nguvu juu yao ni kuwa na nguvu kwa itikadi na misingi. Mfano wa Aya hii ni ile isemayo:"Wenye nguvu kwa makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao." (48:29)

Aya hii na ile isemayo "Na uinamishe bawa lako", zinatuongoza kwenye hakika mbili:

Kwanza , kila mwenye kuwanyeyekea matajiri na wenye nguvu walio mataghuti na kujitukuza kwa mafukara waumini, basi hana chochote katika dini, hata kama akisimama usiku na akifunga mchana.

Hakika ya pili : msimamo wa maadili mema katika Uislamu sio unaotakiwa huo wenyewe isipokuwa Mwenyezi Mungu ameuamrisha kwa ajili ya watu na wala hakuwaamrisha watu kwa ajili yake. Kuanzia hapo, kunyenyekea wenye kiburi ni uduni na kuwanyenyekea wanyenyekevu ni utukufu. Imamu Ali anasema:"Ni uzuri ulioje wa matajiri kuwanyenyekea mafukara kwa kutaka yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu, na uzuri zaidi kuliko huo ni mafukara kuwabeza matajiri kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu"

4. Wenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kila tendo la kutekeleza haja au kuondoa dhuluma, basi ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kuna hadith isemayo:"Mtume alikuwa amekaa na baadhi ya Sahaba zake wakamwangalia kijana wa miraba mine, wakasema angalia huyu! Lau ujana wake na nguvu zake angezitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu." Mtume akasema:"Ikiwa anaihangaikia nafsi yake ili asiombe watu, basi hiyo ni njia ya Mwenyezi Mungu; ikiwa anawahangaikia wazazi wake wadhaifu au ndugu (zake) wadhaifu ili awatosheleze, basi hiyo ni njia ya Mwenyezi Mungu na ikiwa anahangaikia kwa kutaka kujifakharisha ili aonekane ni tajiri basi hiyo ni njia ya Shetani"

5. Wala hawaogopi lawama ya anayelaumu. Hakika ya imani haidhihiri ila wakati wa misukosuko. Ndio ushindani sahihi wa imani ya mumini, anakanusha maovu kwa kumridhisha Mola wake na dhamira yake, Ama yatakayotokea hayajali. Hii ndiyo nembo ya wenye ikhlasi hawaogopi lawama ya mwenye kulaumu; au kama asemavyo Mtume wa rehema; "Ukitonikasirikia sitajali." Chimbuko la matatizo ya ulimwengu leo, kuanzia vita vya Vietnam mpaka vya Mashariki ya kati, na kuanzia serikali ya kibaguzi ya Rhodesia[17] na Afrika kusini hadi tatizo la wamarekani weusi katika Amerika, chimbuko lake ni kunyamazia haki tu, katika magazeti na idhaa, na katika Umoja wa mataifa na Baraza la usalama, kwa kuhofia wafalme wa dhahabu nyeusi (petroli) na wahami wao waliokodishwa.

Kwa hiyo basi, kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu inatoa picha hai ya mwenye dini na malengo anayopasa kuyaendea na kujitolea mhanga kwayo.. Limebaki swali hili jepesi: Je, baada ya haya mtu anaweza kusema kuwa dini ni mambo ya ghaibu na kuswalia maiti tu?" Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye.

Tumeona kwa hisia kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hataki kumpa fadhila zake ila mwenye kwenda kulingana na sababu na desturi ambayo ameiwekea nidhamu ya ulimwengu Yeye ambaye kwake hekima imetukuka. Lau angelitaka tutembee bila ya miguu, tufanye kazi bila ya mikono na tuone bila macho asingelikuwa na haja ya kuumba chochote katika hivyo. "Na ameumba kila kitu akakikadiria kwa kipimo (chake)" (25:2)

TATIZO LA MAADILI

Anasema Nietzsche, mwenye falsafa ya upeo wa juu zaidi wa Binadamu: "Hakuna kitu kinachoitwa, thamani ya maadili. Kwa hiyo uhuru, uadilifu na usawa ni maneno tu waliyoyatengeneza wanyonge ili kuzuia kutawaliwa na wenye nguvu. Marks naye anasema kinyume na hayo:

Maana yake, kwa wote wawili, ni kuwa neno thamani halina mshiko isipokuwa ni hawaa na masilahi tu ya dhati; na maadam hawaa haiafikiani na utu na upeo wake basi matamko hayo yatakuwa ni uwongo na unafiki. Sisi tunaamini kwamba chimbuko la thamani ni masilahi, lakini ni masilahi yanayotokana na asili ya binadamu kama binadamu, si kutokana na tabaka aliyo na kundi aliloko. Hapana mwenye shaka kwamba masilahi haya yanaafikiana na binadamu na upeo wake, Ndipo yakaitwa thamani ya binadmau sio ya tabaka.

Kwa hiyo basi yanakuweko kwa kuweko binadmau mwenyewe, wala hayaondolewi na mnyonyaji au atakayeyageuza kulingana na matakwa yake. Vinginevyo, basi isingefaa kuwagawanya watu, mwenye haki na mbatilifu anayebadilisha maneno na mwenye ikhlasi na mnafiki anajifunika ngozi ya watu wema. Zaidi ya haya hakuna katika historia ya binadamu au jamii yoyote iliyowahi kusema: Fanya utakavyo kwa sababu wewe huna jukumu lolote, ukiua au ukiiba, Ndio kuna madhehbu mbalimbali ya kupanga thamani ya maadili, ambayo hatuna nafasi ya kuayataja. La muhimu ni kuyaeleza, kama ilivyo katika mtazamo wa kiislamu. Kalamu za wenye ghera zimeandika mpango wa kiislamu kuwa una lengo la kuweka mtu mwema katika jamii njema.

Lakini mpango huu unahitaji mpango, Kwa sababu, msomaji hafahamu kitu wazi atakachokuwa nacho wakati wa kufuatilia na kutekeleza, Kwa kuepuka matatizo hayo, kwanza tutaanza kutaja baadhi ya mifano, kisha tutoe, katika dalili zake, mpango ulio wazi unaowezekana kutekekelezwa kila siku, Uislamu umeamrisha ukweli, utekelezaji ahadi, kujitolea, kunyenyekea, uvumilivu, kusamehe n.k.

Lakini uwajibikaji wake katika hayo umewekewa mpaka ambao haifai kuukiuka kwa hali yoyote ile. Mpaka wenyewe ni kuwa uwajibikaji huo usisababishe kwenda kinyume na lengo liliokusudiwa.

Ukweli ni wajibu maadamu uko kwenye masilahi ya binadamu, lakini kama ukileta dharau, kama vile kumpa adui siri za kiulinzi au kunakili maneno kwa kukusudia fitina, basi hapo ukweli utakuwa ni haramu. Uwongo ni haramu isipokuwa kuutumia katika vita na adui wa dini na wa nchi, katika kusuluhisha wawili na kuhifadhi mtu asiyekuwa na hatia na mali.

Kutekeleza kiapo ni wajibu maadamu muapaji hapati manufaa yoyote kutokana na kiapo chake, vinginevyo ataacha, kutokana na hadith isemayo" Ukipata heri kutokana na kiapo chako basi kiache" Kutoa mali sabili ni kuzuri, lakini ikiwa mwenyewe ataihitajia basi haifai.

Uvumilivu unatiliwa nguvu, lakini haufai kwenye dhulumu na tabia mbaya. Na kusamehe ni fadhila, lakini hakufai ikiwa ni sababu ya kuleta vurugu na kuendeleza utendaji makosa.

Kwa hivyo basi, imetubainikia kuwa thamani ya maadili katika Uislamu hupimwa na masilahi yatakayopatikana au kukinga madhara. Maana yake ni kuwa thamani hiyo iko kwa ajili ya binadamu, na wala sio kuwa binadamu yuko kwa ajili ya hiyo thamani, ili aiabudu. Thamani ya kimaadili ni ile inayodhibiti matumizi ya mtu katika kuleta masilahi yake na masilahi ya jamii au kutodhurika nayo au kumdhuru mtu mwingine. Unaweza kuuliza: Ni kipi kitakachodhibiti kupambanua manufaa na madhara. Tunajibu kwa ufupi: Mdhibiti ni hisia za ujumla kwamba hili linadhuru na hili ni la manufaa. Hisia zikiona tu basi 'kwisha maneno' hakuna swali wala jawabu, kwa sababu hisia za ujumla ndio msingi wa dhati.