18
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
SOMO LA KUMI NA NANE
MTAZAMO WA JUMLAWA TATIZO HILO
Mojawapo ya maswali ambayo mara nyingi yamevutia wanafikra wanaojihusisha na asili ya maisha ya mwanadamu na ambalo limekuwa mada kuu yenye ubishani usio na ukomo ni kama binadamu anayo hiari ya kuchagua malengo yake na kutekeleza matakwa yake katika matendo na shughuli zake zote - katika mambo yote ya maisha yake, yawe ni mambo ya kimaada au vinginevyo. Matamanio yake, mielekeo yake na dhamira ndio tu kipengele kinachotafuta maamuzi yake?
Au matendo yake na mwenendo wake yamelazishwa yake? Analazimika kwa unyonge kabisa kufanya matendo fulani na kufanya uamuzi? Je, binadamu ni kifaa kisicho na hiari mikononi mwa mambo yaliyo nje yake? Ili kuweza kuelewa umuhimu wa suala hili lazima izingatiwe kwamba katika ufumbuzi wake inategemea uwezo wetu kunufaika kikamilifu kutokana na uchumi, sheria, dini, saikolojia na matawi mengine yote ya elimu ambayo yanamchukua mwanadamu kama somo lao. Hadi tutakapogundua kama binadamu anayo hiari au hapana, sheria yoyote itakayoshauriwa kwa ajili ya mwanadamu katika elimu yoyote ile, itakuwa inatumika kwa kiumbe ambacho asili yake hatuijui. Ni dhahiri kwamba hakuna matokeo yanayopendeza yatakayopatikana.
Suala la hiari dhidi ya majaaliwa si tatizo la kitaaluma au kifalsafa pekee. Pia, linawahusu wote wale wanaopendekeza kwa binadamu kwamba ana jukumu ambalo anawajibu wa kulikamilisha na wakamtia moyo wa kufanya hivyo. Kwani kama hawataamini, angalau kwa ukamilifu kabisa, juu ya utashi huru, hapatakuwepo na msingi wa kuwapa thawabu watu wanaotekeleza wajibu wao na kuwaadhibu wale ambao hawatekelezi. Baada ya kujitokeza kwa Uislamu, Waislamu pia walitoa mazingatio maalum juu ya suala hili, kwa sababu falsafa ya maisha ya Uislamu ilisababisha suala hili kuchunguzwa kwa undani zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya hapo na mashaka yote yafafanuliwe. Kwani, kwa upande moja, suala hilo liliunganishwa na upweke wa Mwenyezi Mungu na, upande mwingine, liliunganishwa na sifa Zake za uadilifu na mamlaka.
Mabingwa wa fikra wa zamani na sasa wanaweza kugawanyika katika makundi mawili kuhusu suala la utashi huru dhidi ya majaaliwa. Kundi la kwanza linakataa kwa ushupavu hiari ya mwanadamu katika matendo yake, na kama matendo yake yataonyesha kudhihirisha dalili za uchaguzi wa hiari, hii ni kwa sababu ya makosa na mapungufu ya namna ya utambuzi wa binadamu.
Kundi la pili linaamini katika utashi huru na kusema kwamba mwanadamu anapata uhuru kamili wa kutenda katika nyanja ya matendo ya hiari; uwezo wake wa kufikiri na kuamua una athari nyingi na uko huru kutokana na vipengele vyote vilivyopo nje yake. Kwa kawaida, binadamu anapata uzoefu wa athari za ulazimisho kuhusiana na kuzaliwa kwake, pia kutokana na mambo mbalimbali yanayomzunguka na matukio anayokabiliana nayo wakati wa uhai wake. Matokeo ya hili yanaweza kuwa kwamba anaishia katika kuamini kwamba hakuna kitu kama utashi wa hiari. Aliingia dunia bila ya hiari na anaonekana kuwa anadhibitiwa kikamilifu na majaaliwa, akipeperushwa huko na huko kama kipande cha karatasi hadi mwishowe anaondoka hapa duniani.
Wakati huo huo, binadamu hutambua kwa wazi kabisa kwamba yuko huru na mwenye kujitegemea katika mambo mengi, bila ya aina yoyote ya ulazimishwaji au kuwekewa masharti. Mwanadamu anao uwezo na umahiri wa kupambana kikamilifu dhidi ya vikwazo na kuendeleza udhibiti wake wa maumbile kwa kutegemea uzoefu uliopita na ujuzi. Ukweli halisi na wenye madhumuni ambao hawezi kuukanusha ni kwamba kuna tofauti kubwa na halisi baina ya mishughuliko ya hiari ya mikono na miguu yake na utendajikazi wa moyo wake, ini na mapafu yake.
Hivyo, kwa kukubaliana na hiari, utambuzi na uwezo wake wa kuchagua, sifa ambazo ni ishara ya ubora wa ubinadamu wake na chimbuko la wajibu wake, binadamu anajua kwamba, ni kweli anao utashi huru katika mlolongo wote wa matendo yake na kwamba hakuna kipingamizi kinachozuia utekelezaji wa hiari yake au kutengeneza imani yake. Lakini, katika hali nyinginezo, mikono yake imefungwa na hana uwezo wa kuchagua: mambo yanaamuliwa na vitu vya kidunia au ulazimishwaji wa kisilika hali ambao unafanya thamani halisi ya maisha yake, na mengine ambayo yanalazimishwa juu yake na vipengele vilivyo nje yake.
Majaaliwa: Watetezi wa majaaliwa hawaamini kwamba binadamu yuko huru katika matendo ayafanyayo hapa duniani. Waamini majaaliwa wa kitheolojia kama ile madhehebu ya Kiislamu ijulikanayo kama Ashari ambalo linategemea maana ya nje ya Aya fulani za Qur'ani na hawasimami wakatulia na kutafakari kuhusu maana ya kweli ya Aya zote zinazohusika au namna ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu ili kuazimia kabla, wamehitimisha kwamba mwanadamu hana hiari ya namna yoyote ile.
Wao pia wanakanusha kwamba vitu husababisha athari na hawakubali kwamba visababishi vina kazi ya kufanya kwenye maumbile na uchimbukiaji wa viumbe vya kawaida. Wanakiona kila kitu kuwa ni athari ya moja kwa moja na zisizopatanishika za utashi wa ki-Mungu, na wanasema kwamba ingawa mwanadamu ana kiasi fulani cha hiari na uwezo mikononi mwake, havina athari juu ya matendo yake. Matendo ya wanadamu hayasababishwi na uwezo wao na hiari yao lakini husababishwa na utashi wa Mwenyezi Mungu, ambao hutoa athari zote kipekee.
Binadamu anaweza kuchangia kiasi fulani kwenye matendo yake anayoyafanya kwa lengo na nia yake, na kuchangia huku kunaleta matokeo ya kuvuma kwa matendo kama ni mema au mabaya. Mbali na haya, mwanadamu si chochote isipokuwa ni kiini kwa ajili ya utekelezaji wa utashi na mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Pia wanasema kwamba kama tukidhania kwamba mwanadamu anao utashi huru, tutakuwa tumepunguza uwanja wa mamlaka ya Mwenyezi Mungu na utawala wake. Uumbaji kamili wa Mwenyezi Mungu unahitajia kwamba hapana mtu atakayemkabili kama muumbaji, vivyo hivyo, imani katika misingi ya upweke wa Mwenyezi Mungu, kwa kufikiria mamlaka kamili tunayoyaweka juu Yake, lazima imaanishe kwamba viumbe vyote vilivyoumbwa, pamoja na matendo ya wanadamu, yameingizwa kwenye uwanja wa utashi hiari ya ki-Mungu.
Kama tunakubali kwamba mtu anatengeneza matendo yake mwenyewe, tutakuwa tunakanusha mamlaka ya Mwenyezi Mungu juu ya maumbile yote, jambo ambalo haliendani, baadaye, na sifa ya Mwenyezi Mungu ya muumba, kwani tungekuwa tuna mamlaka kamili katika uwanja wa matendo na kusingekuwepo na kazi iliyobakia ya Mwenyezi Mungu. Hivyo, imani katika utashi huru inachukuliwa kama yenye kuelekeza bila huruma kwenye ushirikina au kuabudu miungu wawili.
Kwa nyongeza, baadhi ya watu waifanya kanuni ya majaaliwa - ima kwa utambuzi au kwa kutotambua - kuwa kisingizio cha kufanya matendo kinyume na dini na maadili, na kufungua njia ya kuelekea kwenye upotofu wa kila aina katika nyanja ya imani na matendo. Washairi fulani wa kundi linaloamini kwamba anasa ndio msingi wa maisha, wamo ndani ya kundi hili, wanadhania kwamba kuazimiwa kabla kuwa ni kisingizio tosha cha wao kufanya dhambi na kutumaini, kwa njia hii, kuweza kukwepa yote haya; mzingo wa dhamira na tabia mbaya.
Mtindo huu wa fikra ya majaaliwa ni kinyume na kanuni ya uadilifu, kuhusiana na Mwenyezi Mungu na jamii ya binadamu. Kwa wazi tunaona uadilifu wa ki-Mungu ukiwa umedhihirika katika mpanuko wote katika maumbile yote, na tunaitukuza dhati Yake tukufu kabisa kama yenye sifa hii. Qur'ani inasema:
شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٨﴾
"Mwenyezi Mungu, na Malaika, na Wenye elimu, wanameshuhudia kuwa hakuna aabudiwaye ila Yeye tu, ni Mwenye kusimamia uadilifu, Hakuna aabudiwaye isipokuwa Yeye tu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima."(Imran:18)
Mwenyezi Mungu pia anaelezea usimamishaji wa uadilifu katika jamii ya wanadamu kuwa ni mojawapo ya madhumuni ya kuleta Mitume na anazungumzia kuhusu haja hii kwamba waja Wake wadumishe uadilifu:
لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ ﴿٢٥﴾
"Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani ili watu wasimamishe uadilifu .." (57:25). Katika Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu atawatendea waja Wake kwa kufuata misingi ya uadilifu vilevile, na hakuna hata mmoja ambaye atafanyiwa dhulma japo kidogo. Qur'ani inasema:
وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ﴿٤٧﴾
"Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote .." (21:47).
Sasa itakuwa haki kumlazimisha mtu kutenda jambo ambalo ni la dhambi na halafu kumwadhibu kwa hilo? Endapo mahakama yoyote ingetoa hukumu na kutoa adhabu chini ya hali kama hiyo, hakika hiyo ingekuwa ya kidhalimu. Kama tukikanusha kanuni ya uhuru na tusitoe kabisa kazi ya uhakika kwa hiari ya wanadamu, hakutakuwepo na tofauti yoyote baina ya binadamu na viumbe wengine wote waliobakia. Kwa mujibu wa wanaoamini katika majaaliwa, matendo ya tabia ya mtu hufanana ya yale ya viumbe vingine kwa vile yanasababishwa na mlolongo wa vipengele vilivyoko nje ya udhibiti wao, hiari yetu haina kwa yenyewe haina uwezo wa kusababisha athari.
Lakini ikiwa Mwenyezi Mungu anaumba matendo ya matakwa ya binadamu, kama Yeye ndiye Muumbaji wa udhalimu na dhambi, hata wa kule kujiwekea washirika Yeye Mwenyewe, tunawezaje kuelezea tabia kama hiyo kwa upande wa Dhati Kamilifu na Iliyotukuka? Kuamini katika majaaliwa kunabatilisha na kufuta kanuni za Utume na wahyi; ile dhana ya ujumbe wa ki-Mungu ambao ndio utumike kama chanzo cha utambuzi wa binadamu; fikra ya maamrisho ya makatazo, ya kigezo cha kidini na amri, ya sheria na kanuni za imani, na mafundisho ya kulipia matendo ya mtu. Kwani, pindi tutakapoamini kwamba matendo yote ya wanadamu hufanyika bila kufikiri (kama mashine), bila ya hiari au chaguo juu ya mhusika, hakutakuwepo na wajibu uliobakia kwa ajilai ya ujumbe wa Mitume ambao wametumwa kuja kumsaidia mwanadamu katika jitihada zake.
Ikiwa wajibu uliowekwa juu ya mwanadamu na maelekezo yaliyoelekezwa kwake hayana uhusiano wowote na utashi huru wake na uwezo wa kutii na kuwajibika, yatakuwa na umuhimu gani? Kama hali ya kiroho ya mwanadamu na matendo ya nje yatakuwa yaa- muliwe kimashine bila yeye kufikiria, juhudi zote zisizo na ukomo za wenye kufundisha maadili, kuikomboa jamii ya binadamu na kuielekezea upande wa ubunifu na maadili ya kiwango cha juu zaidi hazitakuwa na athari yoyote kabisa.
Juhudi zao hazitafaa kitu; hakuna faida kutumaini kiumbe ambacho kila kitendo chake kimekwisha kuamuliwa kiweze kubadilika. Lakini binadamu anawajibika juu ya uongofu wake au maangamizi yake na vilevile juu ya ule wa wengine; uchaguzi wake ndio unaounda hatima yake, na pindi anapojua kwamba kila kitendo anachofanya kina umuhimu wake, atachagua njia yake kwa uangalifu sana. Tegemeo lake juu ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu na radhi Zake litasababisha kufunguliwa kwa milango na madirisha ya uwezo kwa ajili yake.
Inawezekana kukanushwa kwamba kuchukulia imani katika ujuzi mkubwa wa Mwenyezi Mungu (Yeye amejua tangu mwanzo yale yote yanayofanyika hapa duniani, hakuna tukio lolote hapa duniani dogo au kubwa linalotokea bila Yeye kulijua kabla), Mwenyezi Mungu lazima ajue kabla juu ya ukatili, matendo maovu na dhambi ambazo binadamu hufanya, na kwa kuwa hutokea hata hivyo, nidhahiri wanadamu hawana uwezo wa kujizuia kufanya maovu hayo.
Tunajibu kama ifuatavyo: Ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu anatambua viumbe vyote, vidigo na vikubwa lakini, ujuzi huu haumaanishi kwamba mwanadamu analazimishwa katika yote anayofanya. Ujuzi wa Mwenyezi Mungu upo kwenye msingi wa kanuni ya kisababishi; haitumiki kwa viumbe au kwa matendo ya mwanadamu ambayo yapo nje ya mfumo huo. Ujuzi unaofanya kazi kwa namna ya chanzo na athari haihusishi ulazimishaji. Mwenyezi Mungu alikuwa anatambua mwelekeo wa siku zijazo wa matukio hapa duniani na alitambua kwamba wanadamu wangefanya matendo fulani kwa mujibu wa hiari zao huru. Zoezi la hiari huru ni sehemu ya mfululizo wa usababisho ambao huwaelekeza kwenye matendo yao, na ni wanadamu wenyewe ndio wanaoamua kufanya ama matendo mwema au maovu. Katika suala hili la mwisho, kwa kutumia vibaya utashi wao huru, wanasababisha uharibifu na ufisadi, hivyo endapo uovu na ukandamizaji unakuwepo katika jamii fulani, haya ni matokeo ya matendo ya wanadamu. Hayakuumbwa na Mwenyezi Mungu. Ujuzi wa Mwenyezi Mungu hauna athari juu ya chaguo la binadamu la wema au uovu.
Ni kweli kwamba katika upeo wa uhuru wa mwanadamu na uwezo wa kuamua, mambo fulani yanakuwepo - kama vile hali ya mazingira, hulka ya asili ya mtu, na mwongozo wa ki-Mungu - ambavyo huchukua wajibu mkubwa katika uchaguzi wake anaoufanya. Lakini wajibu huo umewekewa mipaka katika kuamsha matakwa, katika kutiwa nguvu na msaada wa hiari ya mwanadamu; haimlazimishi mtu kuchagua matakwa fulani. Kuwepo kwa vipengele hivi haimaanishi kwamba mwanadamu amefungiwa kwenye mfumbatio wao; kinyume chake, anao uwezo kamili ama wa kutii matakwa yaliyosababishwa na mambo ya nje au kuyakataa kwa kuyawekea mipaka au kuyabadilisha mwelekeo wao. Mtu anaweza kunufaika kutokana na mwongozo unaopatikana kwake kupitia umaizi na uoni wa dhahiri, unaotoa maumbo kwenye matakwa yake na kudhibiti au kuyarekebisha. Wingi wa misukumo ya kimaumbile mwanadamu aliyonayo ndani mwake kamwe haiwezi kuondolewa kabisa, lakini ni muhimu kuidhibiti na kuinyima fursa ya kwenda hovyo.
Natudhanie kwamba makanika mtaalamu anaikagua gari ndogo kabla haijatoka kuanza safari na anaona ya mbele kwamba motokaa hiyo haiwezi kwenda mbali zaidi ya kilomita chache kabla ya kusimama kwa sababu za dosari za kiufundi. Sasa, endapo motokaa hiyo itaanza safari na ikaharibika baada ya kwenda kilomita chache kama alivyotabiri fundi makenika, inaweza kusemekana kwamba yeye ndiye chanzo cha kuharibika huko kwa sababu amekutabiri hivyo? Ni dhahiri kwamba sivyo, kwa sababu hali duni ya matengenezo ya motokaa hiyo ndio ilikuwa sababu ya kuharibika, si ujuzi wa fundi makenika na utabiri aliofanya; hakuna mtu mwenye busara anayeweza kuuchukulia ujuzi wa fundi makenika kuwa ndio sababu ya kuharibika kwa gari hiyo.
Kwaw kutoa mfano mwingine: Mwalimu anajua maendeleo ya wanafunzi wake wanayoyafanya na anajua kwamba mwanafunzi mmoja hatafaulu katika mtihani wake wa mwisho kwa sababu ya uvivu wake na kukataa kujifunza. Pindi matokeo ya mtihani yatakapotolewa, ikadhihirika kwamba yule mwanafunzi mzembe kweli amefeli mtihani. Sasa, sababu ya matokeo kama hayo ni ujuzi wa mwalimu au uvivu wa mwanafunzi? Ni wazi kwamba ni uvivu wa mwanafunzi. Mifano hii imetuwezesha kuelewa, kwa kiwango fulani, kwa nini ujuzi wa Mwenyezi Mungu sio sababu ya matendo ya waja Wake.
Mojawapo ya athari zenye madhara za imani ya maqaadiru katika jamii ni kwamba inafanya kuwa rahisi zaidi kwa wakandamizaji wenye kiburi kuwakaba na kuwanyamazisha wanyonge na inakuwa vigumu zaidi kwa wanyonge kujitetea. Kutumia fikra ya majaaliwa kama kisingizio, mkandamizaji hukataa kuwajibika kwake na vurugu na matendo yake ya kikatili; anadai kwamba mkono wake ni mkono wa Mwenyezi Mungu na anazihusisha dhambi zake zote kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi - Mungu Ambaye Yupo na lawama na vipingamizi vyote. Wanyonge hulazimika kustahamili na kukubali lolote wanalofanyiwa na mkandamizaji, kwa sababu kupambana dhidi ya udhalimu wake ni kazi bure na jitihada za kuleta mabadiliko bila shaka zingeshindwa.
Makabaila na wahalifu wengine wakubwa katika historia wakati fulani wametumia fikra ya majaaliwa kuendeleza ukatili wao na ukandamizaji. Wakati familia ya Amiri wa Mashahidi, Husein bin Ali
ilipofika mbele ya Ibn Ziyad, mhalifu huyo mwovu alimwambia Zainabul Kubraa,
: "Umeona Mwenyezi Mungu alivyomfanya nduguyo na familia yake?" Zainab akajibu:"Kutoka kwa Mwenyezi Mungu sijaona kitu isipokuwa huruma na wema. Wamefanya kile ambacho Mwenyezi Mungu aliwataka wafanye ili kunyanyua makazi yao na walitekeleza wajibu ambao ulikabidhiwa kwao. Baada ya muda si mrefu wote mtakusanywa mbele ya Mola wenu na kuhesabiwa matendo yenu; hapo ndipo utaelewa nani ameshinda na nani ameokolewa."
Kuhusu suala la hiari huru na majaaliwa wayakinifu wamenasa kwenye ukinzani. Kwa upande moja, wanamuona mwanadamu kama kiumbe cha kimaada, kinachopatwa, kama ilivyo kwa ulimwengu wote, mabadiliko ya kimetafizikia na kuwa hawezi kutoa athari yake yeye mwenyewe; akikabiliwa na mambo ya kimazingira, ulazima wa kihistoria na hali iliyokwisha kuazimiwa, anakosa hiari. Katika kuchagua njia yake ya maendeleo, mawazo na matendo yake, yupo katika kutegemea maumbile. Mageuzi au maendeleo ya kijamii yoyote ni matokeo halisi pekee ya hali fulani ya kimazingira, na mwanadamu hana wajibu wowote wa kufanya humo.
Kwa mujibu wa uhusiano wa kimajaaliwa baina ya chanzo na athari zake, hakuna jambo linalotokea bila sababu yake tangulizi na utashi wa mwanadamu pia, anapokabiliwa na vitu na matatizo ya kinyenzo na kiuchumi ya mazingira yake na vipengele vya kiakili, anategemea sheria zinazobadilika, zikiwa kwa kweli, ni zaidi kidogo kuliko 'athari' zinazoizalisha. Mwanadamu analazimika kuchagua njia ambayo imeshurutishwa juu yake na matakwa ya mazingira yake na maudhui yake ya kiakili.
Hivyo, hakuna nafasi kwa ajili ya utashi huru na uchanguzi wa mwanadamu kujieleza yenyewe, na hakuna nafasi kwa ajili ya hisia za wajibu wa kimaadili na utofautishaji. Lakini, wakati huo huo, wayakinifu wanamfikiria mwanadamu kuwa na uwezo wa kuathiri jamii na ulimwengu, na hata wanaweka msisitizo zaidi kuliko madhehebu mengine katika nidhamu ya uenezaji na Kiitikadi ndani ya chama chenye mpango. Wanawakusanya watu ambao wameonewa na ukabaila kusimama kidete na kufanya mapinduzi ya nguvu na kujaribu kuwafanya wanadamu wabadilishe imani zao na kuchukua dhima tofauti na ile walikuwanayo hapo kabla - yote haya kwa kutegemea juu ya nguvu ya uchaguzi huru. Uhusishaji huu wa dhima kwa binadamu unapingana na mpango mzima wa uyakinifu wa mabadiliko ya kimetafisikia kwa vile unatangaza kwamba utashi huru upo hata hivyo.
Endapo wayakinifu wanadai kwamba kuwaamsha watu wanaokandamizwa na kuimarisha makundi ya kimapinduzi huongeza kasi ya kuanzisha kwa mpango mwingine mpya kutoka kwenye chimbuko cha ule wa zamani, hii itakuwa haina mantiki kwa sababu hakuna mapinduzi au mabadiliko stahilifu yanaweza kufanyika kabla ya wakati wake au kwa wakati mwingine mbali na ule unaostahili. Maumbile hufanya kazi yake yenyewe vizuri zaidi kuliko mtu yeyote, kwa mujibu wa mbinu ya mabadiliko ya kimetafisikia, kujihusisha kwenye propaganda na kutafuta kuhamasisha maoni ni uingiliaji usio halali katika kazi ya nguvu asili.
Inaweza pia kusemwa na wayakinifu kwamba uhuru unategemea katika kujua kanuni za maumbile ili kuweza kuzitumia kwa ajili ya malengo na makusudio fulani, sio katika msimamo huru mkabala na kanuni za maumbile. Lakini hii pia inashindwa kupata ufumbuzi wa tatizo, kwa sababu hata hapo baada ya mtu atapokuwa amejifunza sheria hizo na kuamua, kimsingi, kuzitumia kwa malengo maalum, suala linabakia la kama ni nguvu za asili na mata ndizo zinazoamua malengo hayo na kuyashurutisha juu ya mwanadamu au binadamu anayachagua hayo kwa hiari yake.
Kama mtu anaweza kuchagua, je, maamuzi yake ni tafakuri ya matakwa na hali ya maumbile au yanaweza kwenda kinyume nayo? Wayakinifu wamemfikiria mwanadamu kama kiumbe cha sura moja tu hivyo kwamba hata itikadi zake na mawazo ni matokeo ya maendeleo ya uchumi na mali na yanapaswa kufanyiwa tabaka la madaraja na uhusiano wa uzalishaji ndani ya jamii - kwa ufupi, yanaakisi picha makhsusi ya hali inayotokana na mahitaji ya vitu ya wanadamu.
Kama mambo yalivyo, ni kweli kwamba binadamu ana ukiumbe wa kimaada na kwamba uhusiano wa kimaada wa jamii na hali ya kiwiliwili, kijogorafia na ya kimaumbile vyote vina athiri juu yake. Lakini, mambo mengine, yanayotokana na asili muhimu ya mwanadamu na nafsi yake ya ndani pia yameathiri majaaliwa ya mwanadamu wakati wote wa historia, na haiwezekani kuyachukulia maisha ya kiakili ya mwanadamu kuwa yametiwa msukumo na mata pekee na uhusiano wa uzalishaji. Mtu kamwe hawezi kudharau wajibu muhimu uliofanywa na mambo ya kidini na maadili, na silika za kiroho, uchaguzi wa mwanadamu wa njia ya kufuata, utashi wake ndio haswa kiunganishi kimoja katika nyororo ya visababishi vinavyomuongozea kufanya tendo fulani au kutolitenda.
Hapana anayetia shaka kwamba mwanadamu analazimika kupatwa na athari za matendo ya maumbile na hisia zake, na/au kwamba nguvu ya historia na vipengele vya uchumi hutayarisha uwanja kwa ajili ya kutokea matukio fulani. Lakini matukio hayo si kiamuzi pekee cha historia na hayana wajibu muhimu wa kimsingi katika kuamua hatima ya mwanadamu. Hayawezi kumnyang'anya mwanadamu uhuru na uwezo wake wa kuamua, kwa sababu amesonga mbele mpaka kiasi kwamba anayo thamani ambayo, ikiwa nje ya maumbile inamwezesha yeye kupata utambuzi na hisia ya wajibu.
Si tu kwamba mwanadamu si mfungwa wa mata na uhusiano wa uzalishaji, anao uwezo na mamlaka juu ya nguvu asili na anao uwezo wa kubadili uhusiano wa mata. Kama vile mabadiliko katika vitu vya kimaada yanategemea kwenye sababu za nje, sheria fulani na kanuni zinakuwepo katika jamii ya binadamu ambazo zinaamua kiwango cha maendeleo cha taifa na uwezo, au kushindwa na kuanguka kabisa. Matukio ya kihistoria wala hayategemei dhana pofu ya majaaliwa au ya bahati mbaya; yanakuwa sawa na kanuni na mipango ya maumbile, ambayo miongoni mwao utashi ya mwanadamu unashika nasafi ya muhimu sana.
Katika Aya nyingi za Qur'ani Tukufu, ukandamizaji, uonevu, dhambi, na uovu yanaonyeshwa kubadili historia ya watu fulani, hii ikiwa ni kanuni iliyozingatiwa na jamii zote za binadamu.
وَإِذَا أَرَدْنَا أَن نُّهْلِكَ قَرْيَةً أَمَرْنَا مُتْرَفِيهَا فَفَسَقُوا فِيهَا فَحَقَّ عَلَيْهَا الْقَوْلُ فَدَمَّرْنَاهَا تَدْمِيرًا ﴿١٦﴾
"Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa." (17:16).
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ ﴿٦﴾ إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ ﴿٧﴾ الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ ﴿٨﴾ وَثَمُودَ الَّذِينَ جَابُوا الصَّخْرَ بِالْوَادِ ﴿٩﴾ وَفِرْعَوْنَ ذِي الْأَوْتَادِ ﴿١٠﴾ الَّذِينَ طَغَوْا فِي الْبِلَادِ ﴿١١﴾ فَأَكْثَرُوا فِيهَا الْفَسَادَ ﴿١٢﴾ فَصَبَّ عَلَيْهِمْ رَبُّكَ سَوْطَ عَذَابٍ ﴿١٣﴾ إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ ﴿١٤﴾
"Kwani hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya watu wa A'di? Na wa Iram wenye majumba marefu? Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi? Na Thamudi walichonga majabali huko bondeni? Na Firauni mwenye vigingi? Ambao walifanya jeuri katika nchi? Wakakithirisha humo ufisadi? Basi Mola Wako aliwapiga na mjeledi wa adhabu. Hakika Mola wako yupo kwenye mavizio anawavizia." (89:6-14).
Qur'ani pia inatukumbusha kwamba wanadamu wanaoabudu matakwa yao na kutii mielekeo yao ya upotofu, husababisha mengi ya majanga ya historia.
إِنَّ فِرْعَوْنَ عَلَا فِي الْأَرْضِ وَجَعَلَ أَهْلَهَا شِيَعًا يَسْتَضْعِفُ طَائِفَةً مِّنْهُمْ يُذَبِّحُ أَبْنَاءَهُمْ وَيَسْتَحْيِي نِسَاءَهُمْ إِنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ ﴿٤﴾
"Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbalimbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wa kike. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi." (28:4).
فَاسْتَخَفَّ قَوْمَهُ فَأَطَاعُوهُ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿٥٤﴾
"Basi aliwapumbaza watu wake, na wakamtii. Kwa hakika wao walikuwa ni watu wapotovu." (43:54).
Kiasi gani cha umwagaji wa damu, vita, uharibifu na vurugu vimesababishwa na uabudu matamanio yenye shauku kali na uchu wa madaraka! Wanadamu ambao ni kijenzi muhimu katika jamii, wanazo akili na utashi wa asili katika nafsi zao wenyewe, kabla ya kujumuishwa katika jamii, moyo binafsi haukukosa nguvu mkabala na moyo wa pamoja. Wale wanaodai kwamba mtu binafsi ameamuliwa kabisa katika matendo yake kikamilifu na mazingira ya kijamii wanadhania kwamba kompaundi achanishi ya uhakika ni muhimu ilazimike kuhusisha utengano wa sehemu katika umoja wa kitu kizima ili kuwezesha uhalisi mpya kutokeza. Njia mbadala pekee kwa hili, wao wanavyoamini, itakuwa ni imma kukanusha ukweli wa haki wa jamii kama mchanganyiko wa mtu mmoja mmoja na kukubali uhuru na kujitegemea wa mtu binafsi, au kukubali ukweli wa jamii kama mchanganyiko na kuacha kujitegemea na uhuru wa mtu binaf- si.
Haiwezekani kuunganisha matarajio haya mawili, wanashikilia hivyo. Sasa, ingawa jamii ina uwezo mkubwa zaidi kuliko mtu mmoja, hii haimaanishi kwamba huyo mtu mmoja analazimishwa katika shughuli zake zote za kijamii. Ubora wa maumbile muhimu ndani ya mwanadamu - matokeo ya maendeleo yake katika uwanda wa maumbile - yanampa yeye uwezekano wa kutenda kwa uhuru na kuasi dhidi ya udhia wa kijamii. Ingawa Uislamu unaweka mbele mwenendo na mamlaka kwa jamii, na vile vile kwa uhai na kifo, unamuona mtu binafsi kama mwenye uwezo wa kukataa na kupambana dhidi ya uovu uliopo katika mazingira ya jamii yake; hauoni kuwa katika hali za kitabaka yale mambo yenye kuamua, yanayoelekea kwenye kujitokeza imani zilizo na namna sawa miongoni mwa zile zilizoko chini yao.
Kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu yenyewe ni amri ya kuasi maagizo ya mazingira ya kijamii pale ambapo zinahusisha dhambi na uovu. Qur'ani inasema; 'Enyi mlioamini, kuweni imara katika imani zenu, kwa sababu upotovu wa watu wengine hauwezi kukulazimisheni kuingia kwenye upotvu.' Inaelezwa tena ndani ya Qur'ani Tukufu:
إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿٩٧﴾
"Hakika wale ambao wametolewa roho na Malaika hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao, Malaika watawauliza: Katika nini mlipoteza umri wenu? Watasema: Tulikuwa wanyonge ardhini. (Malaika) watasema: Je, ardhi ya Mwenyezi Mungu ilikuwa haina wasaa mkahamia humo? (ili mkayakimbia mazingira hayo; hivyo visingizio vyao havitakubaliwa) Basi hao makazi yao ni Jahannam, nayo ni marudio mabaya." (4:97).
Katika Aya hii, wale wanaojichukulia kama wamelazimishwa kuendana na hali ya jamii, wanalaumiwa sana na kisingizio chao cha kuwafanya washindwe kuwajibika kinakataliwa. Kwa binadamu kuendelea kimaadili na kiroho, kuwepo kwa utashi huru ndani mwake ni kwa lazima. Mwanadamu anayo maadili na maadili yanaweza kutegemewa kutoka kwake, hapo tu ambapo anakuwa huru. Tunapata uhuru wa binafsi na maadili pale tu tunapochagua njia inayoendana na haki na kukataa mwelekeo wa uovu ndani mwetu na mazingira yetu kwa njia ya jitihada zetu wenyewe. Kama tukienda kwa mujibu wa maendeleo ya kawaida au majaaliwa ya migongano ya kimantiki, tutakuwa tumepoteza maadili yote ya haiba.
Halafu, hakuna jambo linalomlazimisha mwanadamu kuchagua njia fulani katika maisha, wala nguvu ya kumshurutisha aache mojawapo. Mwanadamu anaweza kudai kutojitengeneza mwenyewe wakati anapobahatisha muundo wake kwa mujibu wa sheria zilizopo katika jamii au malengo yaliyoandaliwa kabla, lakini pale tu anapochagua mwenyewe, anaamua na kuwekeza juhudi zake mwenyewe.