14
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
SOMO LA KUMI NA NNE
MAONI KUHUSU UADILIFU WA MWENYEZI MUNGU
Tatizo la uadilifu kama mojawapo ya sifa za Mwenyezi Mungu limekuwa na historia yake iliyo dhahiri. Madhehebu mbali mbali za Kiislamu zimeshikilia maoni tofauti kuhusu suala hili, wakilitafsiri kwa mujibu wa kanuni zao bainishi. Baadhi ya Sunni ambao hufuata maoni ya mwanateolojia Abul-Hasan Ash'ari hawaamini katika uadilifu wa Mwenyezi Mungu kuwa ni suala la imani na wanakanusha kwamba uadilifu unatimizwa na matendo ya ki-Mungu.
Hata hivyo, kwa maoni yao, Mwenyezi Mungu humtendea mtu fulani, na adhabu yoyote au thawabu Anazompa, bila kuzingatia ni nini angeonekana kustahili kupewa, itawakilisha uadilifu na wema kamili, hata kama itaweza kuonekana si haki ikipimwa katika viwango vya kibinadamu. Hawa Ash'ari, kwa hiyo hutofautisha sifa ya Mwenyezi Mungu ya uadilifu mbali na matendo Yake na kwa hiyo, wanafikiri chochote kinachohusishwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni haki. Kama anampa thawabu muadilifu na kumwadhibu mkosaji, huu ni uadilifu, na ndivyo itakavyo kuwa kwa kinyume chake; bado ingekuwa kwenye nyanja yake pana ya uadilifu Wake.
Madai yao kwamba maneno yenyewe hasa 'uadilifu' na 'udhalimu' hayana maana yanapotumiwa kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka yanakusudiwa kunyanyua dhati ya Mwenyezi Mungu takatifu hasa kufikia upeo wakuvuka mipaka. Lakini hakuna mtu mwenye mawazo kamili atakayeziona dhana hizi za juu juu na pungufu kuwa na uhusiano wowote na uvuka mipaka wa Mwenyezi Mungu. Kwa kweli, wanahusisha ukanusho wa mpango hapa duniani, wa kanuni ya uababishaji katika mpango wa jumla wa dunia na katika tabia na matendo ya watu binafsi.
Wafuasi wa al-Ash'aria wanaamini hata hivyo, kwamba taa ya akili yenye mwanga mkali, huzimika wakati wowote inapokabiliwa na utambuzi na matatizo ya dini, kwamba haiwezi kumnufaisha mwanadamu au kuangaza njia yake. Madai haya wala hayaendani na mafundisho ya Qur'ani wala maudhui ya Sunna. Qur'ani inaona kupuuza akili ni namna ya upotovu na inarudia kuwataka watu watafakari na kuzingatia ili waweze kujifunza elimu bora zaidi na imani za kidini. Wale wanaoshindwa kunufaika kutokana na taa hii angavu iliyomo ndani mwao wanalinganishwa na hayawani. Qur'ani inasema:
إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ ﴿٢٢﴾
"Hakika ya viumbe wabaya zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale viziwi na mabubu ambao hawatafakari." (8:22)
Mtume wa Uislamu anasema:"Mwenyezi Mungu amemwekea kila mtu walinzi wawili: mmoja ni wa nje yake, wajumbe wa Mwenyezi Mungu, na mwingine wa ndani, uwezo wake mwenyewe wa akili".
Wafuasi wa Mutazilite na Shia wanapingana na al-Ashari na madhehebu yake. Kati ya sifa zote za Mwenyezi Mungu, wao wamechagua uadilifu kuwa kama kanuni ya imani yao. Kwa kutegemea uthibitisho wa mapokezi au wa kihekima, pia wamepinga na kukataa kama isiyoendana na kanuni ya uadilifu, mafundisho ya athari za hatima ya ki-Mungu na kudra ya matendo ya mtu (kabla hajayafanya). Wanaamini kwamba uadilifu ndio msingi wa matendo ya Mwenyezi Mungu, katika mpangilio wa ulimwengu na katika kuanzisha sheria. Kama vile ambavyo matendo ya mtu yanavyoweza kupimwa kwa mujibu wa kigezo cha wema na uovu, matendo ya Muumbaji pia yanatakiwa kupitishwa kwenye kigezo cha namna hiyo hiyo. Kwa kuwa mantiki ya akili huamua kwamba uadilifu ni wa kutukuzwa kiasili na udhalimu kiasili ni wa kulaumiwa, basi lengo la kuabudiwa ambalo sifa zake ni pamoja na akili isiyo na ukomo na mawazo hakiwezi kamwe kufanya kitendo ambacho mantiki inakiona hakiruhusiwi.
Tunaposema kwamba Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, ina maana kwamba dhati Yake yenye kujua kila kitu na bunifu haifanyi kitu ambacho ni kinyume cha busara na manufaa. Dhana ya hekima, inapotumiwa kwa Muumbaji haimaanishi kwamba Yeye huchagua njia bora ya kufikia malengo Yake au kurekebisha mapungufu Yake, kwani ni mwanadamu tu ambaye anayetakiwa kutoka kwenye upungufu kuelekea kwenye ukamilifu. Anachotaka Mwenyezi Mungu kuwafanya viumbe waondoke kutoka kwenye mapungufu na kuwasukuma kwenda kwenye ukamilifu na malengo ya asili ya dhati zao. Hekima ya Mwenyezi Mungu ni pamoja na hili; kwamba kwanza hupandikiza aina ya upendeleo wake kwenye kila kiumbe, na halafu baada ya kukipa uhai juu yake, hukisukuma kuelekea kwenye ukamilifu wa uwezo wake kupitia utekelezaji zaidi wa ukarimu Wake.
Halafu, uadilifu una maana pana, ambayo kwa kawaida inajumuisha kuepuka ukandamizaji na matendo yote ya kipumbavu. Imamu Jafar as- Sadiq
anasema katika kuelezea uadilifu wa Mwenyezi Mungu:"Uadilifu katika suala la Mwenyezi Mungu maana yake ni kwamba usihusishe jambo lolote kwa Mwenyezi Mungu ambalo kwamba kama ungelifanya wewe lingekusababishia kulawamiwa na kukosolewa."
Kwa mwanadamu, ukandamizaji na aina zote za shughuli za kidhalimu ambazo huzifanya, bila shaka, hutokana na ujinga na upungufu katika umtambuzi na kuhitaji kulikoungana na uduni wa hulka, pia wakati mwingine ni kuakisi kwa chuki na uadui, kunakochomoza kutoka kwenye nafsi ya ndani kabisa ya mwanadamu kama cheche.
Ni watu wengi sana ambao huchukizwa na ukandamizaji na uovu wao wenyewe. Hata hivyo, kwa sababu ya kutokujua kuhusu matokeo ya mwisho ya matendo yao, wanaendelea mara kwa mara, kufanya udhalimu na kujichafua wenywe kwa aina zote za matendo ya fedheha na uovu. Wakati mwingine mwanadamu anahisi kwamba anataka kupata kitu ambacho yeye mwenyewe hana njia au uwezo wa kukipata. Hii ndio sababu ya msingi ya maovu mengi. Hisia za kuhitaji, njaa na ulafi, mtu kuwa na tamaa ya kuumiza au kutawala - yote haya ni mambo ambayo huongozea kwenye tabia ya ugomvi.
Chini ya ushawishi wao, wanadamu hukosa udhibiti wa kujizuia. Huweka juhudi zake zote katika kutimiza matakwa yake na kukiuka masharti yote ya kimaadili, huanza kukaba makoo ya wanaogandamizwa. Dhati ya kipekee ya Mwenyezi Mungu, ile nafsi isiyo na ukomo, imeepukana na tabia na mipaka ya aina hiyo, kwani hakuna kinachofichikana kwenye elimu Yake bila ya mipaka, na haiingii akilini kwamba apatwe na udhaifu wa kutokuwa na uwezo kuhusiana na kitu chochote -Yeye, wa Tangu na Tangu, ambaye nuru Yake ya milele inagawa uhai na riziki kwa vitu vyote na Ambaye anawahakikishia mwenendo wao, namna zao mbalimbali na maendeleo.
Dhati stadi ambayo inakusanya viwango vyote vya ukamilifu haina haja ya kitu chochote ambacho kwamba kama hakipo kitatia hali ya wasiwasi ndani Yake Anapopatwa na kukihitajia. Nguvu na uwezo wake bila shaka hazina mipaka na hazipungukiwi na chochote hivyo kwamba anaweza kusababishiwa kupotoka kutoka kwenye njia ya uadilifu na kumfanyia uovu mtu au kulipiza kisasi ili kutuliza moyo wake au kufanya kitendo kisichostahili na kiovu. Hakuna hamasa yoyote ya tabia ya udhalimu inayoweza kupatikana kwa Mwenyezi Mungu, na kwa kweli dhana za ukandamizaji na udhalimu hasa hazitumiki kwa dhati, Ambayo ukarimu na huruma yake vinavienea vitu vyote na Ambaye utakatifu wa dhati yake unaonekana dhahiri katika maumbile yote.
Qur'ani inakanusha mara nyingi mawazo yote ya udhalimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumchukulia Yeye katika utukufu Wake kwamba ameondokana kabisa na matendo yote mabaya. Qur'ani inasema:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٤﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu kitu chochote; lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao." (10:44).
Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu Anajitenga Mwenyewe na fikra yoyote ya udhalimu, jambo linachukiza kwa wanadamu, na badala yake analirudisha kwao wenyewe.
Kwa nyongeza, inawezekanaje kwamba Mwenyezi Mungu awaite wanadamu kwenye uadilifu na usawa ambapo wakati huo huo achafue mikono Yake kwa matendo ya kidhalimu? Qur'ani inasea:
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٩٠﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu na hisani, na kuwapa jamaa, na anakataza uchafu na uovu na dhulma. Anakuwaihidhini ili mpate kukumbuka." (16:90).
Uislamu unathamini sana uadilifu hivyo kwamba endapo kundi moja la Waislamu linataka kupotoka kwenye njia ya uadilifu na kuanza kujihusisha na ukandamizaji, lazima wazuiwe, hata kama hili litahusisha vita. Haya ndio maagizo ya Qur'ani:
وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ ﴿٩﴾
"Na ikiwa makundi mawili katika waumini yanapingana, basi yapatanisheni. Na ikiwa moja kati yao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki." (49:9).
Jambo la kuvutia linalojitokeza kutoka kwenye Aya hii ni kwamba mpatanishi amepewa maagizo kumuelekeza kuhakikisha, pale anapofanya usuluhishi, ugomvi uishe kwa mujibu wa uadilifu, bila kuonyesha huruma kwa yule mchokozi. Inaweza kutokea, katika hali ambapo vita vimeanzishwa kwa malengo ya uchokozi, kwamba mpatanishi anajaribu kumaliza ugomvi kwa kusisitiza juu ya huruma na kutoyaangalia makosa, na hatimaye, anashawishi upande mmojawapo wa wagomvi kuacha madai yake kwa manufaa ya upande wa pili. Utaratibu huu wa huruma, ingawa una uhalali ndani yake, unaweza kuzidisha moyo wa uchokozi ulikuwepo tayari kwa wale walionufaika kwa kuanzisha vita. Kwa kweli ni jambo la kawaida kumridhisha mchokozi katika hali kama hizi kwa kumpatia tahafifu.
Ingawa kusamehe madai kwa hiari, lenyewe ni jambo la kupendeza, katika hali kama hiyo, linaweza kuwa na athari mbaya katika fikra za mchokozi. Lengo la Uislamu ni kung'oa matumizi ya nguvu na udhalimu kutoka kwenye jamii ya Ki-Islamu na kuwahakikishia Watu wake kwamba hakuna mtu anayeweza kupata kitu chochote kwa uchokozi na mabavu.
Kama tukitazama utaratibu wa maumbile, tunaweza kuona kwamba upo uwiano mkubwa na mpana mno miongoni kwa viumbe vyote vya kimaada. Hali hii, inadhihiri kwenye ukawaida wa Atomu, haraka ya elektroniki, mzunguko wa sayari, na kusogea kwa viumbe vyote. Inaonekana kwenye madini na kwenye nyanja ya mimea na chanikiwiti, kwenye uhusiano sahihi uliopo baina ya viungo vya kiumbe hai, katika ulingano miongoni mwa vijenzi vya ndani ya atomu, katika uwiano miongoni mwa maumbo makubwa ya angani na nguvu zao za mvutano zilizokokotolewa vizuri.
Aina zote hizi za ulingano na uwiano, pamoja na kanuni zingine sahihi ambazo sayansi bado inatafuta, kuzigundua, zinatoa ushahidi wa kuwepo kwa mpangilio usiokanika katika ulimwengu, ambao unathibitishwa kwa mlinganyo wa kimahesabu. Mtume wetu mkweli ameuelezea kuhusu uadilifu huu wa jumla na uwiano mpana - ukweli kwamba hakuna kisicho sawa au kilichoko nje ya sehemu yake - kwenye tamko hili fupi na fasaha: "Ni uwiano halisi na mpachano ambao unaendesha dunia na mbingu."
Qur'ani inayahusisha maneno yafuatayo na Musa
na Mtume wetu:"Akasema: Mola wetu Mtukufuni yule aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa."
(20:50).
Katika sentensi hii fupi, Musa anamfafanulia Firauni jinsi dunia ilivyoumbwa pamoja na mpangilio na uzuri wake, ambavyo ni miongoni mwa ishara za Mwenyezi Mungu. Lengo lake Musa lilikuwa ni kumkomboa Firauni kutoka kwenye fikra zake potofu na kumsaidia kutambua kuwepo kwa mpango wa adilifu na mtukufu uliowekwa ulimwenguni.
Mojawapo ya kanuni zinazotawala maumbile bila kuzuilika, kwa hiyo ni mpangilio na uadilifu, na vitu vyote, kwa sababu ya kuwa chini ya kanuni na taratibu za maumbile, vipo katika mlolongo wa mageuzi kuelekea kwenye ukamilifu ambao ni mahsusi kwa kila kimoja chao. Ukengeukaji wowote kutoka kwenye mkondo huu wa jumla wa mpangilio na uhusiano ulioandaliwa juu yake utasababisha utatanishi na ghasia. Wakati wowote panapotokeza hali isiyo ya kawaida kwenye maumbile, vitu vyenyewe huonyesha athari, na vitu vya ndani au nje hujitokeza kuondoa vikwazo vya maendeleo na kuanzisha upya ule utaratibu unaohitajika kuendelea kwenye njia ya kwenye ukamilifu.
Mwili unaposhambuliwa na viini na mambo mengine ya maradhi, chembechembe za damu nyeupe huanza kuvidhoofisha, kwa mujibu wa kawaida isiyozuilika. Dawa yoyote itakayoagizwa na daktari ni kipengele cha nje ambacho kinazisaidia chembe chembe nyeupe katika kazi ya kudhoofisha viini vya maradhi na kuanzisha upya uwiano mwilini. Mwisho kabisa, haiwezekani kwamba Mwenyezi Mungu, Ambaye upendo Wake niwa milele na Ambaye kwa ukarimu hutoa fadhila Zake kwa waja wake, afanye kosa lolote dogo sana la kidhalimu au tendo lisilofaa. Jambo hili ndilo ambalo hakika Qur'ani inaelezea ifuatavyo:
اللَّـهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ قَرَارًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٤﴾
"Ni Mwenyezi Mungu aliyekufanyieni ardhi kuwa ni mahala pa kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndio Mwenyezi Mungu, Mola Wenu. Na ametukuka Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote." (40:64).