1
TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS
MWANZO WA MAKALA
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Ifuatayo ni tarjumi na maelezo mafupimafupi ya Sura ya 10 ya Qur'ani Tukufu ambayo inaitwa Surat Yunus.
Jina la sura hii linatokana na jina la Nabii Yunus
, ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu aliyekuja baada ya Manabii: Nuh na Musa
.
AYA YA KWANZA NA YA PILI
Tunaianza basi darsa letu hili kwa aya ya kwanza na ya pili za sura hiyo ambazo zinasema:
الر تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ ﴿١﴾
1. Alif lam Ra. Hizi ni aya za kitab chenye hikima.
أَكَانَ لِلنَّاسِ عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ رَجُلٍ مِّنْهُمْ أَنْ أَنذِرِ النَّاسَ وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا أَنَّ لَهُمْ قَدَمَ صِدْقٍ عِندَ رَبِّهِمْ قَالَ الْكَافِرُونَ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ مُّبِينٌ ﴿٢﴾
2. Je ni ajabu kwa watu ya kwamba tumemfunulia wahyi mtu miongoni mwao kuwa: Waonye watu na wape walioamini habari njema ya kwamba watakuwa na cheo kikubwa mbele ya Mola wao?. Wakasema makafiri: "Hayakuwa haya ila ni kiini macho.
Kama tulivyowahi kueleza wakati tulipoizungumzia sura ya pili ya al Baqarah, ni kwamba kati ya sura zote 114 za quran tukufu, sura 29 kati yao zinaanza kwa herufi za mkato kama alif lam mim, hamim, yasin n.k. Na tukasema kuwa kwa kuwa aya zinazofuatia baada ya aya hizo mara nyingi huzungumzia adhama ya quran, baadhi ya wafasiri wanasema lengo lililokusudiwa katika kutanguliza aya hizo ni kutolewa changamoto kwa wasioiamini quran, kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha quran kwa kutumia herufi hizo, hivyo nanyi pia kama mnao uwezo teremsheni quran mfano wa hiyo.
Mojawapo ya sifa ambazo Mwenyezi Mungu ameitaja kuwa kimepambika nayo kitabu chake kitukufu cha quran ni hikima. Na hii ni kwa sababu hukumu za dini zilizokuja ndani ya kitabu hicho zimesimama juu ya hoja madhubuti na yale yaliyomo ndani yake ni mafunzo yenye hekima kubwa.
Baada ya kueleza hadhi na nafasi ya quran, katika aya ya pili Mwenyezi Mungu anabainisha nafasi na hadhi ya Mtume wake na kueleza kuwa watu wanatarajia kuona Mwenyezi Mungu akiteremsha Malaika kwa ajili ya kuwafikisha wao uongofu ,wakati kwa kuwa wao ni wanaadamu akili inahukumu kwamba Mtume atakayetumwa kwao lazima naye awe ni mtu kama wao, na anayezungumza lugha yao ili matendo na mwenendo wake wa maisha uweze kuwa kigezo kwao.
Kazi ya Mitume hao ni kutoa bishara njema kwa wafanyao mema na kuwaonya wale watendao mabaya. Lakini kutokana na baadhi ya wakati kuonyesha miujiza ya kuthibitisha ukweli wa unabii wao, baadhi ya watu wasiokuwa tayari kuiamini haki huwasingizia Mitume hao kuwa ni wachawi. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa quran ni kitabu imara na cha milele, kiasi kwamba kupita kwa wakati hakuwezi kupunguza hata chembe thamani na itibari ya kitabu hicho.
AYA YA TATU
Ifuatayo sasa ni aya ya 3 ya sura hiyo ambayo inasema:
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مَا مِن شَفِيعٍ إِلَّا مِن بَعْدِ إِذْنِهِ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٣﴾
3. Bila shaka Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Arshi. Yeye ndiye anayepitisha mambo yote. Hakuna muombezi ila baada ya idhini yake. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, basi Muabuduni yeye. Je hamkumbuki?.
Moja kati ya taratibu alizojiwekea Mwenyezi Mungu s.w.t ni kuumba ulimwengu hatua kwa hatua. Na ndiyo maana pamoja na kuwa na uwezo wa kuuumba ulimwengu na kila kiumbe wakati mmoja, Allah s.w.t aliamua kuziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita tofauti. Na hivyo ndivyo alivyojaalia pia katika maumbile ya viumbe wengine akiwemo binaadamu ambaye pia uumbwaji wake ni wa hatua kwa hatua, toka tone la manii, pande la damu na hadi mwishowe kufikia kiumbe kamili.
Kama tunavyoona kitoto kichanga kabla ya kuja duniani hupitisha kipindi cha miezi tisa tumboni mwa mama kikiwa katika umbo na hali tofauti hadi kuwadia wakati wa kuja duniani, hali ya kuwa kama angetaka, yeye Mola aliye Muweza wa kila kitu angeufanya uumbaji wote huo katika lahadha moja tu.
Baadhi ya yale tunayojifunza katika aya hii ni kuwa uumbaji wa ulimwengu umetokana na ratiba na wakati maalumu na si jambo lililotokea kwa sadfa tu. Aidha aya inatuonyesha kuwa ulimwengu ni kitu kinachofuata kanuni na malengo maalumu. Na sababu ni kuwa mumbaji wake ni mmoja tu.
AYA YA NNE
Darsa hii ya 306 inahitimishwa na aya ya 4 ambayo inasema:
إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ ﴿٤﴾
4. Kwake ndiyo marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika yeye ndiye aliyeanzisha viumbe na ndiye atakayewarejesha (baada ya kufa kwao) ili awalipe kwa uadilifu wale walioamini na kufanya vitendo vizuri. Na wale waliokufuru wao watapata vinywaji vya maji yanayochemka na adhabu inayoumiza kwa sababu ya kukataa kwao.
Aya iliyotangulia imeashiria uwezo wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi. Aya hii ya nne inazungumzia uumbaji wa mara ya pili wa viumbe, yaani kufufuliwa kwao siku ya kiyama; na katika kuliondolea shaka suala hilo inasema, hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu isiyo na shaka ambapo wale waliomwamini Mola wao wakatenda mema watapata jaza ya kheri, na wale waliomkufuru, malipo yao yatakuwa ni adhabu. Tabaan yote hayo yatafanyika kwa uadilifu ambayo ni miongoni mwa sifa kuu za Allah s.w.t
Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa falsafa ya kufufuliwa viumbe ni kuthibiti kwa uadilifu wa Mwenyezi Mungu mtukufu. Kwani dunia hii ndogo na ya kupita tunayoishi haitoshi kuwa ni mahali pa kuwalipa kiadilifu wale waliomwamini Allah na kutenda mema na pia kuwapa adhabu wanayostahiki wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na kufanya kila aina ya dhulma. Aidha aya inatuelimisha kuwa kama dunia na kila kilichomo ndani yake kimeumbwa kwa ajili ya mwanaadamu, huko akhera pia kuwepo kwa ulimwengu huo na neema na nakama zake vitakuwepo kwa ajili ya kutoa malipo kwa sisi wanadamu kutokana na yale yaliyotangulizwa na mikono yetu. Darsa ya 306 imefikia tamati.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa na mwisho mwema na kutunusuru na adhabu ya moto. Amin.
SURAT YUNUS 5-10
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa letu hii.
AYA YA 5 NA 6
Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na tunaianza kwa aya ya 5 na 6 za sura hiyo ambazo zinasema:
هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ مَا خَلَقَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ إِلَّا بِالْحَقِّ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ
5. Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyelifanya jua kuwa muanga, na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo(huo mwezi) ili mujue idadi ya miaka na hisabu (nyinginezo). Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki. Anazipambanua ishara (zake) kwa watu wanaotaka kujua.
﴿٥﴾ إِنَّ فِي اخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَّقُونَ ﴿٦﴾
6. Hakika katika mfuatano (wa daima) wa usiku na mchana ; na katika alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi ziko ishara kwa watu wanaomcha Mungu.
Baada ya aya za mwanzoni mwa sura hii kuashiria juu ya kufufuliwa, kama tulivyoona katika darsa iliyopita, aya hizi tulizosoma zinagusia sehemu ndogo tu ya madhihirisho ya adhama ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji kwa kuzungumzia nafasi ya jua na mwezi.
Uhai wa wanaadamu na sayari yenyewe ya dunia vinategemea nuru na joto litokanalo na jua kama ambavyo nuru ya kupendeza ipatikanayo kupitia kwenye mwezi huwa mithili ya mwanga wa kulalia kwa viumbe mbali mbali wakiwemo wanadamu na pia hutumiwa kama kurunzi ya kuongozea njia katika safari za majangwani na baharini za viumbe hao.
Lakini pia kama tunavyojua mwendo wa sayari ya dunia wa kulizunguka jua na ule wa mwezi wa kuizunguka dunia ndivyo vinavyotuwezesha kuwa na hesabu za siku na pia mwaka kulingana na kalenda ya jua yaani shamsia.
Aidha kutokana na mabadiliko ya umbo la mwezi kuanzia hilali hadi mwezi kamili, ndivyo tunavyoweza kupata pia hesabu ya miezi 12 kulingana na kalenda ya Hijria.
Aya zinamalizia kwa kutilia mkazo nukta hii kwamba yote hayo yaani mfumo kamili wa uumbaji vimefanywa kwa ajili ya kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ni wa haki na yote hayo ameyafanya kwa hikma kubwa na kwamba mabadiliko tunayoshuhudia kila siku ya kubadilika kwa usiku na mchana ambayo wengi wetu tunayachukulia kuwa ni kitu cha kawaida, ni dhihirisho la uwezo na hikma ya Allah s.w.t ambalo wanalidiriki na kulihisi wale wamchao yeye Mola Mwenyezi.
Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa idadi, hesabu na tarakimu ni vitu vyenye umuhimu katika maisha ya mwanadamu, na quran inatuonyesha kuwa kuhesabu masiku ya mwezi na mwaka kwa kutumia jua na mwezi ni miongoni mwa njia za kutumia kwa ajili ya kufanyia hesabu hizo.
Funzo jengine na ambalo ni la kuzingatiwa sana katika aya hizi ni kuwa haifai kwa muislamu kuvipita vivi hivi vitu vya kimaumbile vilivyomzunguka, kwani katika vitu hivyo anaweza kushuhudia kwa karibu adhama yake Mola Muumba.
AYA 7 NA 8
Zifuatazo sasa ni aya 7 na 8 ambazo zinasema:
إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ ﴿٧﴾
7. Hakika wale wasiotaraji kukutana nasi na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua kwa hayo, na walioghafilika na ishara zetu.
أُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمُ النَّارُ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨﴾
8. Hao makaazi yao ni motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
Baada ya aya zilizotangulia kubainisha ishara za kuwepo Allah s.w.t kupitia uumbaji wa mbingu na ardhi aya hizi zinasema wale walioghafilika na ishara hizo na kushindwa kuzidiriki ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu, uwezo wake na hikma yake huishia katika kuikumbatia dunia ya kupita wakidhani kuwa kila kitu kinaishia hapa.
Hivyo huwa hawafikirii juu ya kukutana na Mola wao siku ya Kiyama, na ndiyo maana mwisho wa watu hao unakuwa ni kwenda kutumbukizwa kwenye moto wa jahannam huko akhera.
Moja kati ya mafunzo muhimu tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa kughafilika na Kiyama na kuipaparikia dunia ndiyo mambo yanayomfanya mtu atumbukie kwenye ufuska na maasi.
AYA 9 NA 10
Darsa yetu tunaihitimisha kwa aya 9 na 10 ambazo zinasema:
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٩﴾
9. Hakika wale walioamini na wakatenda mema Mola wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya imani yao. Itakuwa inapita mito mbele yao katika mabustani yenye neema.
دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾
10. Wito wao humo utakuwa utakuwa: Subhanakallahumma! Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu. Na maamkiano yao humo ni salamun (Alaykum). Na wito wao wa mwisho ni: Alhamdulillahi Rabbil Aalamin" Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Wakati aya zilizotangulia zimebainisha hali ya adhabu itakayowapata wale walioamua kuiabudu dunia, aya hizi zinaashiria hali ya waumini watakaoingizwa peponi na kusema kuwa kupata uongofu wa Allah ndiyo hazina kubwa waliyokuwa nayo watu hao tabaan waliipata kutokana na kumwamini Mola wao na kufanya amali njema.
Kisha aya zinaashiria dua na dhikri za watu wa peponi na kusema kuwa utajo wa Subhanallah na Alhamdulillah ni miongoni mwa alama za watu hao, lakini kama tujuavyo dhikri hizo haziishii katika kuzitamka kwa ulimi tu bali mtu anatakiwa awe anaitakidi kwa dhati kuwa Allah s.w.t ametakasika na kila kasoro na upungufu, na ni kwa kufahamu hivyo ndipo mja humhimidi na kumshukuru kwa dhati Mola Mwenyezi kwa sifa zake zote za ukamilifu.
Aya hizi wapenzi wasomaji zinatuoyesha kuwa uongofu wa Allah ni kitu anachokihitajia katika lahadha ya uhai wake. Aidha aya zinatuonyesha kuwa maamkizi ya amani, ndiyo yatakayotawala katika anga ya peponi. Maamkizi ya amani yatakyotoka kwa Mwenyezi Mungu, yatakayotoka kwa Malaika, na pia watakayopeana watu wa peponi wao kwa wao. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa watu hao. Amin.