4
TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS
SURAT YUNUS 50-56
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Karibuni katika mfululizo huu wa 316 wa darsa la quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus.
AYA ZA 50 NA 51
Tunaianza darsa yetu kwa aya za 50 na 51 ambazo zinasema:
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُهُ بَيَاتًا أَوْ نَهَارًا مَّاذَا يَسْتَعْجِلُ مِنْهُ الْمُجْرِمُونَ ﴿٥٠﴾
50. Sema: Mwaonaje ikikufikieni hiyo adhabu yake usiku au mchana, basi kwa nini wenye makosa wanaitake ije haraka?
أَثُمَّ إِذَا مَا وَقَعَ آمَنتُم بِهِ آلْآنَ وَقَدْ كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ ﴿٥١﴾
51. Tena Je! Ikishatokea mtaiamini? Ndio sasa tena? Na nyinyi mlikuwa mkiihimiza.
Aya hizi zinatoa jibu kwa wale wanaokanusha kufufuliwa kwa viumbe ambao walikuwa wakisema, hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu itatokea lini? Ndipo Bwana Mtume akatakiwa awajibu kuwa hivi nyinyi mnaoharakisha mteremshiwe adhabu, kama adhabu hiyo itakushukieni ghafla iwe ni mchana au pengine usiku mkiwa mmelala, mtafanya nini wakati huo? Je mtaweza kupata pa kukimbilia au kuwa na nguvu za kuizuia isikupateni? Kama mnadhani pia kwamba ikiwa mtaiamini haki pale mtakapoanza kuona ishara za kuteremka adhabu na kuwa imani yenu hiyo itaweza kukufaeni, basi dhana yenu hiyo ni batili, kwani pale itakaposhuka adhabu milango ya toba itafungwa na hivyo imani katika lahadha hiyo haitokuwa na taathira yoyote.
Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuamini mtu wakati hatari iko mbele ya macho yake hakuna thamani yoyote, kwani imani ya aina hiyo si ya hiyari wala ya kuitakidiwa moyoni, bali ni imani inayotokana na khofu ya lisilo budi.
AYA YA 52
Ifuatayo sasa ni aya ya 52 ambayo inasema:
ثُمَّ قِيلَ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا بِمَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ ﴿٥٢﴾
52. Kisha waliodhulumu wataambiwa: Onjeni adhabu ya kudumu. Kwani mtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyachuma?
Katika aya zilizotangulia lilizungumziwa suala la adhabu ya Mwenyezi Mungu ya hapa duniani inayowashukia kwa ghafla waovu na waliomkufuru Mola Aliyetukuka.
Aya hii ya 52 inaashiria adhabu ya milele itakayowapata waovu hao siku ya Kiyama kwa sababu ya dhulma waliojitendea wao wenyewe na kuwatendea wanadamu wenzao.
Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa katika mafundisho ya Uislamu mpaka wa dhulma hauishii katika kutenda dhulma kwa wengine tu, lakini hata madhambi anayoyafanya yeye mwenyewe mtu yanahesabika pia kuwa ni dhulma, kwani ufanyaji dhambi huo ni sawa na mtu kujidhulumu nafsi yake na pia kuwafanyia dhulma Mitume wa Allah ambao walitaabika na kupata mashaka mengi kwa ajili ya kuhakikisha uongofu utokao kwa Allah unawafikia waja wake.
Aidha aya inatuelimisha kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuwa ya kiadilifu kulingana na amali zake mwenyewe mja, bila kuzidishiwa kitu.
AYA ZA 53 NA 54
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 53 na 54 ambazo zinasema:
وَيَسْتَنبِئُونَكَ أَحَقٌّ هُوَ قُلْ إِي وَرَبِّي إِنَّهُ لَحَقٌّ وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٥٣﴾
53. Na wanakuuliza: Je! ni kweli hayo? Sema: Ehe! Naapa kwa Mola wangu! Hakika hayo ni kweli nanyi hamuwezi kumshinda (Mwenyezi Mungu).
وَلَوْ أَنَّ لِكُلِّ نَفْسٍ ظَلَمَتْ مَا فِي الْأَرْضِ لَافْتَدَتْ بِهِ وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٥٤﴾
54. Na lau kuwa kila nafsi iliyodhulumu inamiliki kila kilichomo duniani, bila shaka ingelitoa vyote kujikombolea. Na watakapoiona adhabu watajitahidi kuficha majuto yao. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu nao hawatodhulumiwa.
Baada ya aya zilizotangulia kuelezea juu ya ushukaji wa adhabu ya Allah kwa waovu hapa duniani na ile itakayowapata huko akhera, aya hizi zinasema musiwe na shaka yoyote juu ya kushuka kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwani ahadi ya Mola itathibiti tu. Pamoja na kwamba yote aliyokuwa akiyatamka Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w)
yalikuwa ni hakika na kweli tupu, lakini kutokana na uzito wa suala la kufufuliwa viumbe, hapa anaapa kwa jina la Mola Mwenyezi kuthibitisha kwamba kujiri kwa siku hiyo ya Kiyama hakuna chembe ya shaka, na wala hakuna atakayeweza kuikwepa siku hiyo au kuweza kukabiliana na adhabu yake.
Kwa hakika adhabu ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama itakuwa kali na nzito kiasi kwamba, kila muovu atakuwa tayari kutoa mali na utajiri wote uliopo duniani ili aweze kuokoka na adhabu hiyo.
Lakini hiyo itabaki kuwa ni ya laiti ambayo haileti, kwa sababu kujuta wakati huo kwa yale aliyoyatanguliza mtu hakutosaidia kitu kwani mahakama ya Mwenyezi Mungu itatoa na kutekeleza hukumu kwa waja wote kwa msingi wa uadilifu.
Funzo mojawapo tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mahakama ya Mwenyezi Mungu si utajiri wala nguvu na uwezo wa kidunia vitakavyoweza kumsaidia mtu. Ni imani safi na sahihi, na amali njema zilizofanywa kwa ikhlasi, ndivyo vitakamvyomfaa mja siku hiyo.
AYA ZA 55 NA 56
Darsa hii ya 316 nahitimishwa na aya za 55 na 56 ambazo zinasema:
أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَلَا إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٥﴾
55. Jueni kuwa hakika vyote vilivyomo katika mbingu na katika ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Lakini wengi wao hawajui.
هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٥٦﴾
56. Yeye ndiye anayefufua na anayefisha. Na kwake mtarejeshwa.
Sababu kuu inayowafanya wanaokufuru na kukanusha juu ya kuwepo kwa siku ya Kiyama ni shaka yao juu ya uwezo wa Allah s.w.t Hivyo aya tulizosoma zinasema kuwa ni nini ikakupitikieni kwamba Mwenyezi Mungu hana uwezo wa kuwafufua waliokufa na kuwalipa kwa waliyotenda? Kwani hamujui nyinyi kuwa kila kitu ni milki yake yeye, na yeye ndiye Muumba na Mmiliki wa ulimwengu, na kwamba uhai wenu na mauti yenu viko mikononi mwake yeye? Kama mnayakubali hayo, yawaje basi mnakuwa na shaka juu ya kiyama?
Aya hizi wapenzi wasomaji zinatuelimisha kuwa mmiliki halisi wa kila kitu ni Mwenyezi Mungu s.w.t, na umiliki wa wanaadamu kwa kitu chochote kile ni wa kupanga tu. Na ndiyo maana siku ya kiyama wale waliokufuru hawatokuwa na chochote cha kuweza kutoa kama fidia ili waweze kuokoka.
Aidha aya zinatuonyesha kuwa uwezo wa Allah wa kutawala kila kitu ni ithbati tosha ya uwezo wake wa kutekeleza kila anachoahidi. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii huku tunamwomba Mola atujaalie kuwa miongoni mwa wale watakaopata radhi zake na pepo ya milele, na atulinde na ghadhabu zake na adhabu ya moto, amin
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
SURAT YUNUS 57-61
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.
AYA ZA 57 NA 58
Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 317 tunayoianza kwa aya za 57 na 58 ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾
57. Enyi watu Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa waumini.
قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ ﴿٥٨﴾
Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehma yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya.
Roho ya mwanadamu wapenzi wasomaji kama ulivyo mwili wake huzongwa na mashaka na magonjwa mbali mbali ya kinafsi na hivyo nayo pia huhitajia dawa. Maradhi ya kiroho kama vile kiburi, ghururi, ubakhili, uhasidi na riya, kama hayatopatiwa dawa huweza kumfanya mtu aishie kwenye ukafiri na unafiki na kumtoa kwenye njia ya uongofu.
Na kwa hivyo quran kutokana na mawaidha na maonyo yake ya mara kwa mara huweza kumkinga mtu na kumwezesha kuepuka madhambi mbali mbali. Kwa upande mwingine kwa kubainisha adhabu iliyoandaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waovu, kitabu hicho cha mbinguni humzindua na kumtanabahisha mwanadamu na matendo yake maovu ili achukue hatua ya kuisafisha na kuitakasa roho yake. Ni wazi kwamba nafsi zilizo safi ndizo zinazoweza kupata taufiki ya kuufikia uongofu wa Allah (s.w.t).
Hivyo Mola Mwenyezi anamtaka Mtume wake awaeleze waumini kwamba rasilimali bora kabisa kwao ni hiyo imani yao kwa kitabu cha Allah na kushikamana kwao na kitabu hicho, na kwa kweli wana kila sababu ya kufurahia kupata neema hiyo kubwa na si kupaparikia vyeo na utajiri wa kidunia.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa quran ndiyo ponya na dawa bora kabisa kwa nyoyo zenye maradhi na nafsi zilizo chafu kimaadili.
Aidha kutokana na aya hizi tunabaini kuwa quran ndiyo hazina na kito chenye thamani kubwa zaidi kuliko utajiri wa aina yoyote ile wa kidunia. Kwa hakika fukara hasa ni yule mtu aliyekosa mafundisho matukufu ya kitabu hicho, hata kama atakuwa amejikusanyia mali na kila aina ya utajiri.
Na kinyume chake tajiri na aliye mkwasi hasa ni yule anayeishi maisha ya kiquran hata kama kwa mtazamo wa kimaada na kidhahiri hatokuwa na mali wala utajiri wowote.
AYA ZA 59 NA 60
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 59 na 60 ambazo zinasema:
قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ لَكُم مِّن رِّزْقٍ فَجَعَلْتُم مِّنْهُ حَرَامًا وَحَلَالًا قُلْ آللَّـهُ أَذِنَ لَكُمْ أَمْ عَلَى اللَّـهِ تَفْتَرُونَ ﴿٥٩﴾
59. Sema: Je! Mwaonaje zile riziki alizo kuteremshieni Mwenyezi Mungu, nanyi mkafanya katika hizo nyengine haramu na nyengine halali. Sema:Je! Mwenyezi Mungu amekuruhusuni, au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?.
وَمَا ظَنُّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّ اللَّـهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَشْكُرُونَ ﴿٦٠﴾
60. Na nini dhana ya wanaomzulia Mwenyezi Mungu kwa Siku ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu, lakini wengi wao hawashukuru.
Aya zilizotangulia zimezungumzia rehma na uongofu wa quran. Zikiendeleza yale yaliyokuja katika aya hizo aya hizi zinasema yule ambaye amejiweka mbali na quran hutumbukia kwenye mkumbo wa kufuata mambo ya uzushi na kubuni na kanuni zisizo na mashiko, ambayo yenyewe ni chanzo cha masaibu na matatizo mbali mbali yanayowatinga watu katika maisha yao. Kama ilivyo katika aya nyingine, quran tukufu inaashiria hapa tabia waliyokuwa nayo washirikina ya kujiharamishia kula wanyama wa miguu mine na baadhi ya mazao ya kilimo na badala yake wakivichukua vitu hivyo na kuviweka nadhiri kwa ajili ya masanamu yao.
Katika aya tulizosoma quran tukufu inawaambia washirikina hao kuwa riziki yenu nyinyi inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na hivyo ni yeye ndiye mwenye haki ya kuamua kipi kiwe halali na kipi kiwe haramu kula, na wala sio nyinyi; vinginevyo muonyeshe kama mumepata idhini kutoka kwake yeye Allah s.w.t ya kufanya hayo, hali ya kuwa nyinyi hamjapewa haki hiyo.
Hivyo basi mjiandae kwenda kujieleza siku ya Kiyama kuhusu uzushi na uwongo huo mliojitungia.
Aya zinaendelea kubainisha kuwa neema za Mwenyezi Mungu kwa waja ni kielelezo cha fadhila na ukarimu wake Mola lakini wanaadamu si washukurivu wa neema hizo ambazo huwaondokea kutokana na kuzusha kwao aina kwa aina za mambo ya upotofu na yasiyo na msingi.
Baadhi ya mambo tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa neema zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo ni yeye ndiye mwenye haki ya kuhalalisha na kuharamisha vitu, na si wanadamu kutokana na utashi na matamanio yao ya kinafsi wajiamulie watakavyo kuhalalisha hiki na kuharamisha kile.
Aidha aya zinatutaka tuelewe kuwa aliye na mamlaka ya kuweka sheria kwa ajili ya wanadamu ni Allah pekee, na hivyo sheria yeyote inayotungwa na wanadamu ikakinzana na sheria yake ni bidaa na haina itibari.
AYA YA 61
Aya ya 61 ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hiyo inasema:
وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦١﴾
61. Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Quran, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi.
Aya hii inaashiria elimu isiyo na mpaka ya Allah s.w.t iliyo na utambuzi wa hali na harakati zote za mwanadamu, na kuelewa kila tendo litendwalo, liwe kubwa au dogo, la siri na la dhahiri, linalojiri kila mahala na katika kila sekunde, iwe ni katika ulimwengu wa mbinguni au wa ardhini na kuyahifadhi yote hayo katika lauhim mahfuudh.
Kwa hakika matendo yote ya waja, mbali na kushuhudiwa moja kwa moja na yeye Mola Karima yanaandikwa na kuhifadhiwa pia na malaika wake ambao huwa pamoja na waja ili kushuhudia na kuyanakili mazuri yote na mabaya yote wanayotenda.
Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa matendo yetu yote bali hata yale yanayotupitikia akilini na katika nafsi zetu yanashuhudiwa na kujulikana na Mwenyezi Mungu sw pamoja na malaika wake. Na kwa kweli hakuna chochote kinachofichika kwao.
Wapenzi wasomaji darsa yetu ya juma hili inaishia hapa. Tunamwomba Mola atulinde na hatari ya kuhalalisha vile alivyoviharamisha yeye na kuharamisha vile vilivyohalalishwa na yeye Mola Karima. Amin.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.