TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS 0%

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS Mwandishi:
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

Mwandishi: Radio ya Kiswahili Tehran Iran
Kundi:

Matembeleo: 12567
Pakua: 3162

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 10 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12567 / Pakua: 3162
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

Mwandishi:
Swahili

7

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

YUNUS 79-86

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran.

AYA ZA 79 NA 80

Hii ni darsa ya 321, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus tunaianza darsa yetu kwa aya za 79 na 80 ambazo zinasema:

وَقَالَ فِرْعَوْنُ ائْتُونِي بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ ﴿٧٩﴾

79. Na akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi.

فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنتُم مُّلْقُونَ ﴿٨٠﴾

80. Basi walipokuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyotaka kuvitupa.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa as alitakiwa na Mola wake aianze kazi yake ya kulingania La ilaha illa llah kwa kumwendea Firauni na kumtaka aikubali tauhidi yaani kumuabudu Mungu mmoja wa haki na pia kuwakomboa Bani Israil na madhila ya Mafirauni.

Aya tulizosoma zinasema Firauni, ambaye hakuwa na uwezo wa kukabiliana na huja na burhani alizopewa na Musa(a.s) alianza kuutuhumu muujiza alioonyeshwa na Nabii huyo kuwa ni uchawi na hivyo kutoa amri ya kuitwa wachawi wake wote ili kukabiliana na muujiza huo wa Mtume wa Allah Musa(a.s) .

Lakini Nabii Musa ambaye hakuwa na chembe ya shaka kuwa haki iko upande wake aliwataka wachawi wa Firauni wafanye kila walichonacho cha uchawi na mazingaombwe yao ili watu wajionee wenyewe na kuamua. Hivyo miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa mataghuti wa kila zama huamua kuwatumia vibaya wataalamu na taaluma zao ili kuweza kufikia malengo yao maovu.

Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa Mitume walikuwa na yakini na risala waliyokuwa wakiilingania, na juu ya kupata nusra na msaada wa Allah sw.

AYA ZA 81 NA 82

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya za 81 na 82 ambazo zinasema:

فَلَمَّا أَلْقَوْا قَالَ مُوسَىٰ مَا جِئْتُم بِهِ السِّحْرُ إِنَّ اللَّـهَ سَيُبْطِلُهُ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُصْلِحُ عَمَلَ الْمُفْسِدِينَ ﴿٨١﴾

81. Walipotupa, Musa alisema: Mliyoleta ni uchawi; Mwenyezi Mungu sasa hivi ataubatilisha. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu.

وَيُحِقُّ اللَّـهُ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na Mwenyezi Mungu ataithubutisha haki kwa maneno yake, ingawa watachukia hao wabaya.

Kama ilivyoelezwa pia katika suratu Shuaraa, wachawi wa Firauni walitupa kamba zao na vifimbo vyao, na kutamka kuwa kwa utukufu wa Firauni tunaapa kuwa sisi ndio washindi. Hakika ni kuwa wachawi wa Firauni hawakufanya chochote kubadilisha kamba na vifimbo vyao, bali walifanya kiini macho tu na hivyo watu wakahisi kana kwamba vifimbo na kamba hizo zilikuwa zinaonyesha harakati za kutambaa.

Na ndiyo maana Nabii Musa aliwatangazia kinagaubaga kuwa Mwenyezi Mungu atauanika hadharani ubatili wa uchawi wao huo na kuithibitisha haki mbele ya macho ya watu.

Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa hata kama batili itarembwa na kupambwa kwa kila namna ya urembo mwishowe itabainika na kutoweka tu.

Nukta nyingine ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa nia na njama ya mustakbirina ya kutaka kuizima nuru ya haki haiwezi kufaulu na kusimama mbele ya irada ya Allah s.w.t ambaye ameahidi kuwa nusra na msaada wake hautoacha kuwafikia wale waliosimama upande wa haki.

AYA YA 83

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 83 ambayo inasema:

فَمَا آمَنَ لِمُوسَىٰ إِلَّا ذُرِّيَّةٌ مِّن قَوْمِهِ عَلَىٰ خَوْفٍ مِّن فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِمْ أَن يَفْتِنَهُمْ وَإِنَّ فِرْعَوْنَ لَعَالٍ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الْمُسْرِفِينَ ﴿٨٣﴾

83. Hawakumuamini Musa isipokuwa baadhi ya vijana wa kaumu yake kwa kumuogopa Firauni na wakuu wao, wasiwatese. Kwani hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi. Na kwa yakini alikuwa miongoni mwa (maasi) waliopita mpaka.

Katika awamu ya kwanza ya kazi yake ya kulingania laa ilaha illa llah, Nabii Musa(a.s) alimwendea Firauni na wasaidizi wake kisha katika awamu ya pili akakabiliana na wachawi na kuwashinda

Ama katika hatua ya tatu aliwafuata watu wa Bani Israil ambapo mwanzo wake ni vijana wa kaumu hiyo ndio waliomuamini.

Tabaan vijana hao nao waliamini pamoja na kwamba walikuwa wakikabiliwa na mateso na madhila ya Firauni.

Miongoni mwa yale tunayojifunza na kutokana na aya hii ni kuwa tabaka la kwanza kumwamini Musa katika Bani Israil lilikuwa ni tabaka la vijana, na hii ni kwa sababu nyoyo ya za vijana huwa safi na bongo zao huwa pia hazijakomazwa na fikra za kitaasubi. Halikadhalika aya hii inatuonyesha kuwa hata katika mifumo inayotawaliwa na mafirauni, mtu anaweza kujivua na upotofu wa mfumo huo na kushikamana na njia ya haki ya akina Musa(a.s) .

AYA ZA 84, 85 NA 86

Darsa ya 231 inahitimishwa na aya za 84, 85 na 86 ambazo zinasema:

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ ﴿٨٤﴾

84. Na Musa akasema: "Enyi kaumu yangu Ikiwa nyinyi mumemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye kama nyinyi ni Waislamu kweli.

فَقَالُوا عَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٨٥﴾

85. Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ee Mola wetu. Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na hao watu madhalimu.

وَنَجِّنَا بِرَحْمَتِكَ مِنَ الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٨٦﴾

86. Na utuokoe kwa rehama yako na hao watu makafiri.

Katika kukabiliana na mateso makali na maudhi na madhila ya akina Firauni, Nabii Musa(a.s) aliwataka watu wa kaumu yake watawakal kwa Mwenyezi Mungu na kuwaonyesha kuwa kutawakkal na kumtegemea Allah tu na kusalimisha muislamu mambo yake yote kwa Mola wa haki ni sharti la imani ya kweli. Nao wale waliokuwa wamemuamini kikweli kweli Musa as waliyasikiliza mawaidha hayo waliyopewa na Mtume wao na kusema, sisi hatuna kimbilio wala egemeo jengine ghairi ya Allah sw na hivyo tunamuelekea yeye na kumwomba atulinde na shari ya madhalimu na makafiri.

Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa wakati wa masaibu na misukosuko Mola Mwenyezi huwa ndiye tegemeo pekee la mja muumini, na kwa kweli kwa kumtegemea yeye Mola aliye Muweza wa kila kitu na kujisalimisha kwake kwa kushikamana na maamrisho yake na kujiepusha makatazo yake, mja huweza kufaulu katika kukabiliana na misukosuko yoyote inayomkuta.

Aidha kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa dua na kushtakia hali yake mja kwa Mola, ni miongoni mwa njia za kumnasua mja na mazonge. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu ya juma hili na kumwomba Mola aijaze subra ndani ya nyoyo zetu, athibitshe imani zetu na atunusuru na kila fitna inayoweza kutuweka mbali na dini yetu. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

YUNUS 87-92

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran.

AYA YA 87

Hii ni darsa ya 322, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 87 ambayo inasema:

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ وَأَخِيهِ أَن تَبَوَّآ لِقَوْمِكُمَا بِمِصْرَ بُيُوتًا وَاجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ قِبْلَةً وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٧﴾

87. Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi ya kwamba: Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu zielekeane, na mshike Sala na wabashirie Waumini.

Ili kuijenga tena jamii ya Bani Israil, baada ya kuikomboa na madhila ya Firaun, Nabii Musa(a.s) aliamriwa na Mola wake kuwakusanya watu wa kaumu yake mahali pamoja na kwa msaada wao kujenga nyumba kwa ajili ya makaazi yao.

Nyumba hizo zilitakiwa ziweko mahali pamoja zikiwa zimeelekeana na si kutawanyika huku na huko ili iwe rahisi kwao kujumuika pamoja kwa ajili ya kupanga na kuchukua maamuzi mbali mbali ya kijamii, na pia endapo Firauni atataka kuwaangamiza waweze kusimama pamoja na kukabiliana naye.

Baadhi ya wafasiri wa quran wanasema, kutokana na kutolewa amri ya sala katika aya hii, muradi uliokusudiwa hapa juu ya neno qibla ni kuzijenga nyumba zao hizo kwa namna ambayo zitakuwa zimeelekea upande wa kibla ili wakiwa ndani ya nyumba zao waweze kutekeleza ibada zao. Pamoja na hayo maana hiyo ni ya kiistilahi, na kimsingi makusudio ya neno qibla kilugha ni maana hiyo hiyo ya kuelekeana.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa mojawapo ya sifa za Mitume ilikuwa ni kuwafikiria watu na hivyo kila wakati wakichukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuwasaidia watu wa kaumu zao.

Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kushughulika na masuala ya kimaada na kimaisha kusitughafilishe na utekelezaji wa sala na kumwabudu Mola wetu. Kutekeleza kwa pamoja yote hayo ndiko kutakakotufanya tupate rehma na baraka za Mola Karima.

AYA ZA 88 NA 89

Zifuatazo sasa ni aya za 88 na 89 ambazo zinasema:

وَقَالَ مُوسَىٰ رَبَّنَا إِنَّكَ آتَيْتَ فِرْعَوْنَ وَمَلَأَهُ زِينَةً وَأَمْوَالًا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا رَبَّنَا لِيُضِلُّوا عَن سَبِيلِكَ رَبَّنَا اطْمِسْ عَلَىٰ أَمْوَالِهِمْ وَاشْدُدْ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُوا حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٨٨﴾

88. Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na watu wake wakubwa mapambo na mali katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanapoteza watu na Njia yako. Mola wetu! Ziangamize mali zao na zifunge nyoyo zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu.

قَالَ قَدْ أُجِيبَت دَّعْوَتُكُمَا فَاسْتَقِيمَا وَلَا تَتَّبِعَانِّ سَبِيلَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٨٩﴾

89. Mwenyezi Mungu akasema: Maombi yenu yamekubaliwa. Basi simameni sawasawa, wala msifuate njia za wale wasiojua.

Katika kuendelea na utekelezaji wa jukumu alilopewa na Mola wake la kupambana na Firaun, Nabii Musa(a.s) alimwomba Allah s.w.t auangamize utajiri uliopindukia mpaka aliokuwa nao Firaun na kutomruhusu aendelee kufanya ufisadi na uharibifu, pamoja na kutumia vibaya nguvu na mamlaka aliyokuwa nayo kutokana na utajiri na neema za kimaada alizoruzukiwa na yeye Mola Karima; mali na neema ambazo alikuwa akizitumia kwa ajili ya kupotosha watu na njia ya Mwenyezi Mungu.

Nabii Musa aliomba dua hiyo kwa Mwenyezi Mungu pale ilipofika hadi akawa hana matumaini tena kwamba Firauni ataamini na kuikubali haki.

Allah s.w.t aliitakabalia dua ya Mtume wake, na hivyo akamtaka Mussa as na watu wake wao wenyewe kwanza wasimame sawa sawa na kushikamana na njia ya Mola wao; kwani sharti mojawapo la kutakabaliwa dua ni waumini wenyewe kwanza kuwa wameshikamana barabara na njia ya uongofu. Na ndiyo maana kwa mujibu wa hadithi ni kwamba ilichukua muda wa miaka arubaini tokea Nabii Musa alipoomba dua ya kumwapiza Firauni hadi taghuti huyo alipoangamizwa kwa kugharikishwa baharini.

Aya hizi pamoja na mambo mengine zinatufunza kwamba, kuwa na utajiri wa mali tu si kipimo cha kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu amemjali na kumpenda mja. Kwani katika dunia hii, hata makafiri nao wamepewa neema nyingi za kimaada.

Halikadhalika aya zinatuonyesha kuwa pamoja na sisi kumwomba Mola awaangamize madhalimu, sisi wenyewe pia tujihimu na kutekeleza wajibu wetu ipasavyo.

AYA ZA 90, 91 NA 92

Darsa ya 322 inahitimishwa na aya za 90, 91 na 92 ambazo zinasema:

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٩٠﴾

90. Tukawavusha bahari wana wa Israili, na Firauni na askari wake wakawafuata kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipokuwa anataka kuzama akasema: "Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliyemuamini Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa wanaonyenyekea.

آلْآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ ﴿٩١﴾

91. Ala! Sasa (unaamini hayo)? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa mafisadi!.

فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ ﴿٩٢﴾

92. Leo basi tutakuokoa kwa kuuweka mwili wako, ili uwe ishara kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na ishara zetu.

Aya hizi wapenzi wasomaji zinabainisha jinsi dua iliyoombwa na Nabii Musa as ilivyotakabaliwa, na kueleza kuwa pale jeshi la Firauni lilipoamua kukuandameni nyinyi kwa lengo la kukuangamizeni, sisi tulikufungulieni njia katika mto Nile na kukupitisheni salama usalimini. Ama Firauni na jeshi lake wao tuliwagharikisha kwenye mto huo na tukaamua kukiibua kutoka majini kiwiliwili cha Firauni tu peke yake, ili hilo liwe funzo na ibra kwa wengine.

Nukta yenye kutoa mguso hapa ni kuwa ule utabiri wa Nabii Musa tuliouona katika aya iliyotangulia ulithibiti na kuwa kweli, kwani wakati Firauni alipoiona adhabu ya kugharikishwa imemkabili hapo alitamka kwa unyenyekevu kuwa amemwamini Mola wa haki waliyemuamini Bani Israil.

Lakini wapi! jibu alilopata ni kuwa, hivi sasa wakati mauti yamekukabili ndiyo unatubia na kuiamini haki.

Hayo ni majuto matupu yaliyopitwa na wakati na majuto ni mjukuu. Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa katika kupambana na mataghuti, tutawakal na kumtegemea Mwenyezi Mungu tu, kwani yeye hatotuacha mkono bali atatufungulia njia ya faraja hata pale tutakapkuwa katika hali ngumu kabisa ya misukosuko.

Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa, kama sisi tutasimama imara na bila kutetereka katika njia ya laa ilaha illa llah mataghuti hawatokuwa na jengine la kufanya ghairi ya kupiga magoti na kusalimu amri, na kupata jaza ya maovu yao.

Aidha aya zinatuonyesha kuwa kuna umuhimu wa kuzitunza na kuzihifadhi athari na turathi za watu waliotangulia zinazoonyesha uwezo wa Allah sw, ili ziwe funzo na mazingatio kwetu sisi na watakaokuja baada yetu. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii, kwa kumwomba Allah atuwafikishe kutubia makosa yetu mara tu tunapoteleza, na kupata maghufira na msamaha wake kabla ya kufikwa na mauti. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmallahi Wabarakaatuh.

8

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

YUNUS 93-97

Bismillahir Rahmanir Rahim. Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo huu wa 323 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus.

AYA YA 93

Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 93 ambayo inasema:

وَلَقَدْ بَوَّأْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مُبَوَّأَ صِدْقٍ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ فَمَا اخْتَلَفُوا حَتَّىٰ جَاءَهُمُ الْعِلْمُ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٩٣﴾

93. Na hakika tuliwaweka Wana wa Israili makazi mazuri, na tukawaruzuku vitu vizuri. Nao hawakukhitalifiana mpaka ilipowafikia ilimu. Hakika Mola wako atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitalifiana.

Katika aya hii Mwenyezi Mungu s.w.t ameashiria neema kadha wa kadha alizowapa Bani Israil na kusema kuwa baada ya miaka na miaka ya kutangatanga na kutokuwa na pa kukaa tuliwapa Bani Israil eneo lenye hali nzuri kabisa ya hewa, na lenye rutuba na ustawi huko Sham na kuwaruzuku riziki zilizo bora kabisa.

Lakini badala ya kushukuru kwa hayo na kuwa watiifu wa kushikamana na maamrisho tuliyowateremshia wakaanza kufarikiana na kutengana na kila mmoja akaamua kufuata njia yake. Hivyo kila mmoja atatakiwa kuja kuutolea maelezo mwenendo huo muovu aliokuwa nao atakaposimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu siku ya Kiyama.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa katika mafundisho ya Mitume, mbali na kuzingatiwa suala la kuwalea na kuwajenga watu kiroho na kimaanawi, yanazingatiwa vile vile mahitaji yao ya kimaada kwa kuwapa uhuru, fursa na suhula za kimaisha za kupatia riziki safi na za halali.

Aidha aya hii inatuonyesha kuwa hitilafu na mifarakano hutokana na kujiweka mbali watu na mafundisho ya mbinguni na hilo huwa sababu ya kuondokewa na neema za Mola wao.

AYA ZA 94 NA 95

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 94 na 95 ambazo zinasema:

فَإِن كُنتَ فِي شَكٍّ مِّمَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ فَاسْأَلِ الَّذِينَ يَقْرَءُونَ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكَ لَقَدْ جَاءَكَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ ﴿٩٤﴾

94. Na kama unayo shaka juu ya hayo tuliyokuteremshia, basi waulize wasomao kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia haki kutoka kwa Mola wako. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.

وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ فَتَكُونَ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٩٥﴾

95. Na kabisa usiwe miongoni mwa wale wanaozikanusha ishara za Mwenyezi Mungu usije ukawa miongoni mwa wenye khasara.

Aya hizi wapenzi wasomaji zinawahutubu wale waliokuwa na shaka kama yale aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w) ni maneno ya haki au la na kuwaambia kwamba ikiwa mtavirejea vitabu vya mbinguni vilivyotangulia mtaona humo bishara na alama za Mtume Muhammad(s.a.w.w) Mbali na hayo mtashuhudia pia kuwa zimezungumzwa na vitabu hivyo hatima za kaumu nyingi zilizotangulia zilizotajwa pia ndani ya Quran kama vile bani Israil, na hivyo kukubainikieni kwamba hii Quran pia ni kitabu cha haki kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu s.w.t

Ni wazi kuwa kama shaka yenu itaondolewa baada ya kubaini hayo na kutambua kuwa Quran ni kitabu cha haki, kukadhibisha kwenu kitabu hicho baada ya kubainikiwa na hayo kutakuwa ni kwa madhara yenu yenyewe kutokana na kujinyima fursa ya kuufikia uongofu hapa duniani.

Ijapokuwa kidhahiri matamshi ya aya hizi wapenzi wasomaji yanaonekana kumhutubu Bwana Mtume, lakini ni wazi kwamba si yeye anayesemezwa hapa, kwa sababu ni jambo lililo muhali na lisiloingia akilini kwamba Bwana Mtume awe na shaka na wahyi alioteremshiwa na Mola wake.

Hivyo anaowahutubu Allah katika aya hii ni mushirikina na Ahlul Kitab, lakini kama ilivyo katika aya nyingi za Quran lugha iliyotumika inaonyesha kuwa mhutubiwa ni bwana Mtume wakati kumbe mlengwa hasa ni watu wengine wa kawaida.

Pamoja na mambo mengine aya hizi zinatuelimisha kuwa shaka na hati hati ni vitu vya kawaida vinavyoweza kumtokea kila mtu. La muhimu ni kujivua na hali ya shaka kwa kurejea kwa maulamaa na wanazuoni wa kidini na kufikia kwenye daraja ya utambuzi kamili na yakini.

Funzo jengine tunalopata hapa ni kuwa endapo mtu ataendelea kubakia katika hali ya shaka na kutochukua hatua ya kuiondoa shaka aliyonayo si hasha akajikuta anaishia kwenye kukadhibisha na kuikataa moja kwa moja haki.

AYA ZA 96 NA 97

Aya za 96 na 97 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hizo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ حَقَّتْ عَلَيْهِمْ كَلِمَتُ رَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٩٦﴾

96. Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwisha thibitika juu yao hawataamini.

وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٩٧﴾

97. Ijapokuwa itawajia kila ishara mpaka waione adhabu inayoumiza.

Watu wamegawika makundi matatu katika suala la namna wanavyoamiliana na ukweli wa mafundisho ya dini.

Kundi la kwanza ni la wale wasioitambua haki na wala hawajishughulishi kutaka kuijua.

La pili ni la wale ambao haki hawaijui lakini wanaamua kufanya juhudi za kuitafuta hadi kuifikia. Ama kundi la tatu ni la wale ambao wameitambua haki lakini kwa kuwa inagongana na maslahi yao ya kimaada ya hapa duniani, hawako tayari kuifuata.

Aya tulizosoma zinawalenga watu wa kundi hili la tatu ambao nyoyo zao zimepiga weusi na kufanya kutu kutokana na inadi na ukaidi wao na ambao hakuna tena matumaini ya nyoyo zao kubadilika na kuiamini haki. Watu wa aina hii huwa ni katika wale walioghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu; kwani hawawi tayari kuamini na kujisalimisha kwa Mola wao kama haijafikia hatua ya kuiona adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa macho yao.

Tatizo la watu hao si kutopewa hoja za kiakili wala kutoonyeshwa muujiza, ambao hata kama wataonyeshwa pia hawatouamini. Tatizo lao ni kwamba hawaa na matamanio yao ya nafsi hayawaruhusu kuungama kile ambacho wamepata utambuzi wake.

Hivyo kama tutaona watu wengi hawaiamini haki, hilo lisitufanye tukautilia shaka ukweli wa maneno ya Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo. Bali tuelewe kwamba kuna watu ambao nafsi zao zimekubuhu kwa maovu na kuharibika kimaanawi kiasi kwamba hakuna chochote kile cha kuweza kuwaathiri wakabadilika.

Watu hao ni mithili ya mpira ambao kama utautupa baharini hakuna hata moja la maji litakalopenya na kuingia ndani yake. Hali ambayo ni matokeo ya kuziba kwa mpira tu vinginevyo bahari iko pale pale na maji yake yako kwa ajili ya kila mtu.

Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa tusiwe na matumaini kwamba watu wote wataiamini haki, bali tujue kwamba maovu na madhambi ni mambo yanayofanya utandu juu ya moyo wa mtu unaomfanya asiwe tayari kuikubali haki.

Nukta nyingine ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa iko siku hata wale waliotopea katika kukadhibisha haki watabaini hakika hiyo lakini wakati huo watakuwa wamechelewa na kuikubali kwao haki wakati huo hakutowasaidia kitu.

Darsa ya 323 imeifikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwafikisha kuifuata na atuonyeshe batili na kutupa taufiki ya kuiepuka. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

YUNUS 98-100

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa darsa ya quran.

AYA YA 98

Hii ni darsa ya 324, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 98 ambayo inasema:

فَلَوْلَا كَانَتْ قَرْيَةٌ آمَنَتْ فَنَفَعَهَا إِيمَانُهَا إِلَّا قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَىٰ حِينٍ ﴿٩٨﴾

98. Kwa nini usiwepo mji mmoja ukaamini na imani yake ikawafaa isipokuwa kaumu Yunus? Waliamini na sisi tukawaondolea adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia, na tukawasterehesha kwa muda.

Kama ambavyo tumewahi kuashiria katika darsa zetu za huko nyuma, ni kwamba utaratibu aliojiwekea Allah s.w.t kuhusiana na waja wake ni kuwapa fursa na muhula wa kutubia madhambi yao na kutenda amali njema ili kufidia waliyoyatanguliza huko nyuma.

Lakini pia kama tulivyowahi kueleza ni kwamba mlango wa toba uko wazi madamu mtu bado hajafikia lahadha ya kufikwa na mauti au kuteremkiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Kwani kutubia katika lahadha mbili hizo au kuiamini haki katika wakati huo hakuwi na faida yoyote kwa mtu, na sababu ni kwamba imani na toba ya lahadha hizo hutokana na khofu ya mauti na adhabu na si kwa hiyari yake mtu.

Suala hilo la fursa na muhula wa kutubia na kuiamini haki hauishii kwa mtu binafsi tu, bali Allah ameuweka pia kwa kaumu na umma mzima wa watu. Kwa upande wa kaumu, ni ile ya Nabii Yunus tu(a.s) ndiyo ambayo watu wake walipoiona adhabu waliiamini haki na kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, naye Mola Mrehemevu akaikubali imani yao na kuwapa fursa nyingine.

Historia inasimulia kwamba baada ya miaka mingi ya kazi ya tablighi aliyoifanya Nabii Yunus(a.s ) kuwalingania watu wake lailaha illa llah ni watu wawili tu ndiyo walioukubali wito wa uongofu.

Akiwa katika siku za mwisho za uhai wake, na kutokana na kukata tamaa kwa watu wake kuiamini haki, Mtume huyo wa Allah aliwaapiza watu wa kaumu yake na kisha akaamua kuondoka na kwenda zake.

Kama ilivyo kawaida ni kwamba dua za Mitume huwa hazirudi, na kwa hivyo ilipasa watu wa kaumu yake wateremkiwe na adhabu.

Hata hivyo mtu mmoja mtambuzi na mwenye hekima kati ya wale wawili waliomuamini Mtume huyo alipoona Nabii Yunus ameshatoa tamko la kuwaapiza watu wake waliokataa kuamini haki aliwaendea watu hao na kuwaambia: "Sasa subirini mshukiwe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, la kama mnataka mpate rehma zake Mola basi tokeni nje ya mji, na mutenganishe baina yenu na watoto wenu wadogo ili sauti za vilio vya watoto na za maombolezo ya mama zao waliotenganishwa nao ziweze kupanda na kusikika, na nyote pamoja mtubie kwa mliyoyafanya huko nyuma na kumwomba maghufira Allah s.w.t

Asaa kwa njia hiyo mkaweza kusamehewa. Hivyo watu hao wakaufuata wasia huo na hivyo adhabu haikuteremshwa tena, naye Nabii Yunus akarejea kwa watu wake.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na ayah ii ni kuwa miongoni mwa kaumu zilizopita, ni kaumu ya Yunus tu ndiyo iliyotubia kwa wakati na kabla ya kushuka adhabu na toba yao ikapokelewa na kuamini kwao kukakubaliwa.

Funzo jengine tunalopata katika ayah ii ni kwamba hatima na majaaliwa ya watu yako mikononi mwao wenyewe, na hivyo kwa kuomba dua na kushtakia waja hali zao hiyo inaweza ikawa sababu ya kuzuia balaa lisiwashukie na rehma za Mola ziwamiminikie.

AYA YA 99

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 99 ambayo inasema:

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَآمَنَ مَن فِي الْأَرْضِ كُلُّهُمْ جَمِيعًا أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٩٩﴾

99. Angelitaka Mola wako wangeliamini wote waliomo katika ardhi. Je wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe waumini?.

Moja ya kati ya mambo ambayo Mwenyezi Mungu sw amejifunga nayo mwenyewe ni kuwafikishia waja wake uongofu. Hata hivyo Mola Mwenye hikima hakutaka watu waiamini haki kwa nguvu na kulazimishwa.

Bali ametaka waamue kwa hiyari yao waja, ima kuiamini au kuikufuru haki. Tabaan baada ya kuchagua kwa hiyari yake mtu ima kuamini au kukufuru ajiweke tayari pia kwa jaza na malipo atakayopata kutokana na chaguo lake.

Kwa kuzingatia kwamba sifa moja kubwa ya Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w) kama ilivyoelezwa na quran ni kwamba alikuwa na hamu kubwa ya kuona watu wa umati wake wanaiamini haki na akiumia na kuungulika mno kwa kuwaona wamezama katika dimbwi la upotofu, lakini kwa kuwa Allah s.w.t ametaka imani ya waja itokane na hiyari yao hivyo anamhutubu Mtume wake kwa kumwambia kwamba pamoja na hamu kubwa uliyonayo usifikirie kuwafanya watu waumini hata kwa kuwateza nguvu, kwani lau Mola wako angetaka iwe hivyo wanaadamu wote wangeiamini haki.

Moja ya nukta za kuzingatiwa katika ayah ii ni kuwa imani huwa na thamani inapotokana na hiyari ya mtu, ama ikiwa itatokana na kulazimishwa haiwezi kuwa na faida kwa mtu.

AYA YA 100

Darsa ya 324 inahitimishwa na aya ya 100 ambayo inasema:

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَن تُؤْمِنَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ وَيَجْعَلُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ ﴿١٠٠﴾

100. Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasiotumia akili zao.

Kama tujuavyo, watu hawalazimishwi kuiamini haki, na kuamini kwa kulazimishwa hakuna thamani yoyote.

Pamoja na hayo ni taufiki ya Mola ndiyo inayoufanya moyo wa mtu uikubali na kuiamini haki kwa hiyari na ukunjufu. Kwani ni yeye ndiye anayetukamilishia suhula zote kuanzia za kutufikia uongofu wenyewe kupitia kwa Mitume wake, pamoja na kutupa akili timamu ya kuchanganua na kupambanua zuri na baya, la kheri na la shari na lile la kimantiki na lisiloingia akilini.

Hivyo mtu asije akaingiwa na ghururi na kumpitikia kwamba ni uhodari wake ndio uliomfanya kuitambua haki na kuifuata. Na kwa hakika kila mtu anapojiona amepata taufiki ya kushikamana barabara na kamba ya uongofu, basi amshukuru sana Mola wake na kuomba taufiki ya kudumu katika kushikamana na mambo ya kheri. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

9

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

YUNUS 93-97

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 101

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 325 tunayoianza kwa aya ya 101 ambayo inasema:

قُلِ انظُرُوا مَاذَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿١٠١﴾

101. Sema: Angalieni yaliyomo mbinguni na kwenye ardhi! Na ishara zote na maonyo hayawafai kitu watu wasioamini.

Katika aya zilizotangulia tulisema kuwa kutotumia watu akili zao na kutotafakari juu ya alama na ishara za uwezo wa Allah ndiyo sababu ya watu kukufuru na kuikana haki.

Aya tuliyosoma inatilia mkazo suala la kutadabari na kubainisha kuwa, kutafakari na kuzingatia kwa kina madhihirisho ya uumbaji wa Allah ni utangulizi wa kumfikisha mtu kwenye imani thabiti na sahihi.

Kwa upande mwingine kama tulivyosisitiza katika darsa iliyopita na nyingine kadhaa, imani lazima itokane na hiyari ya mtu na si kwa kulazimishwa na kutezwa nguvu, na ndiyo maana aya hii ya 101 inasisitiza juu ya kutafakari ili kwa kupitia njia hiyo ya uelewa na ufahamu mtu aiamini haki na kuweza kudumu na imani aliyonayo.

Bila shaka utafiti sahihi na wa kutafuta ukweli juu ya chungu ya maajabu yaliyomo katika mbingu na ardhi na ulimwengu mzima wa uumbaji humfanya mwanaadamu atambue adhama ya Mola wake na hivyo kunyenyekea na kujisalimisha kwa Muumba asiye na mshirika.

Pamoja na hayo bado wanakuwepo watu ambao licha ya kushuhudia ishara za adhama ya Mola Muumba huamua kuikana na kuikataa haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa kutafakari na kutadabari juu ya uumbaji ni njia inayoweza kutumiwa na kila mtu kwa ajili ya kumjua Mwenyezi Mungu.

AYA YA 102

Ifuatayo sasa ni aya ya 102 ambayo inasema:

فَهَلْ يَنتَظِرُونَ إِلَّا مِثْلَ أَيَّامِ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِهِمْ قُلْ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Basi je wanagojea jingine ila kama yaliyotokea siku za watu waliopita kabla yao? Sema: Basi ngojeni! Nami ni pamoja nanyi katika wanaongojea.

Katika aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu amewataka wapinzani wa haki kutafakari na kuzingatia kwa makini ishara za kuwepo Muumba wa ulimwengu katika mbingu na ardhini.

Aya tuliyosoma hivi punde inasema wale ambao hawako tayari kutafakari juu ya hayo basi wajiweke tayari kukabili siku ngumu za mashaka na adhabu. Kwani utaratibu aliouweka Allah kuhusiana na uma au jamii za watu mbali mbali ni kwamba kama ilivyo kwa watu mmoja mmoja, majaaliwa na hatima ya jamii nzima ya watu hutegemea mwenendo wa akthari ya watu walioko katika jamii hiyo.

Kama wengi wao watakuwa ni watu wema basi jamii nzima huwa na muelekeo wa kutengenea hata kama watu wachache kati yao watakuwa mafasiki; la kama wengi wao watakuwa ni waovu basi jamii nzima itatumubukia kwenye ufisadi na kupatwa na mwisho mbaya hata kama ndani yake baadhi ya watu watakuwa ni waja wema.

Historia ya kaumu zilizopita kama zile za Manabii Nuh, Lut na Hud as ni uthibitisho juu ya kutobadilika kwa utaratibu huo wa Allah s.w.t Hivyo bwana Mtume anatakiwa na Mola awaeleze Mushirikina wa Makka kwamba kama nao pai wataamua kusimama dhidi ya risala ya haki watafikwa na hatima sawa na iliyowapata watu wan kaumu hizo.

Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa ni historia ya waliotangulia ni funzo na ibra kwa wanaofuatia.

AYA YA 103

Ifuatayo sasa ni aya ya 103 ambayo inasema:

ثُمَّ نُنَجِّي رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا كَذَٰلِكَ حَقًّا عَلَيْنَا نُنجِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Kisha sisi huwaokoa Mitume wetu na walioamini. Ndio kama hivyo, inatustahiki kuwaokoa Waumini.

Ikiendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia kuhusiana na watu kupatwa na adhabu ya papa hapa duniani, aya ya 103 ya suratu Yunus inasema kwa kuwa hailaiki katika uadilifu wa Allah kuwachanganya wema na wabaya katika adhabu, hivyo kila kaumu inayofkia hatua ya kustahiki kufikwa na adhabu ni wale walio waovu na wale waliokuwa hawayajali maovu yanayotendeka katika jamii ndio wanakaopatwa na adhabu ya Allah, ama wale walio waumini Mwenyezi Mungu atawaokoa na adhabu hiyo.

Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa wale walio waumini wa kweli Mwenyezi Mungu huwalinda na adhabu hata ya hapa duniani, japokuwa watakuwa wakiishi katika jamii ya watu mafasiki.

AYA YA 104

Ifuatayo sasa ni aya ya 104 ambayo inasema:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِن كُنتُمْ فِي شَكٍّ مِّن دِينِي فَلَا أَعْبُدُ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِنْ أَعْبُدُ اللَّـهَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٤﴾

104. Sema: Enyi watu ikiwa nyinyi mnayo shaka katika dini yangu basi mimi siwaabudu mnaowaabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu. Lakini mimi ninamwabudu Mwenyezi Mungu anayekufisheni. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waumini.

Baada ya aya ziliowahutubu washirikina na kuwabainishia ipi itakuwa hatima yao, aya hii inamtaka Bwana Mtume awaambie watu hao kuwa kama wanadhani kwamba wewe utayumba na kutia shaka katika kufuata njia yako ya haki na pengine kukushawishi ulegeze msimamo katika itikadi yako basi wape jibu zito na la wazi kwamba hutomwabudu mwingine yeyote ghairi ya Mola wako Allah s.w.t na katu hutoyatukuza msanamu yao hayo wanayoyaabudu. Waambie kwamba mimi ninamwabudu Mungu ambaye mauti yangu na yenu yako mikononi mwake na hamuwezi nyinyi abadani kuyakwepa hayo wala hayo masanamu yenu pia hayana uwezo wa kukuepusheni na kifo.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa shaka inayotiwa na wengine juu ya haki hata kama watakuwa wengi namna gani isituyumbishe katika kufuata njia ya uongofu.

Aidha aya inatuonyesha kuwa aliye na ustahiki wa kuabudiwa ni yule ambaye uhai wetu na mauti yetu yako mikononi mwake.

AYA ZA 105 NA 106

Darsa ya 325 inahitimishwa na aya za 105 na 106 ambazo zinasema:

وَأَنْ أَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٥﴾

105. Na uelekeze uso wako kwenye dini ya kweli wala usiwe katika washirikina.

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ ﴿١٠٦﴾

106. Na wala usiwaombe wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Ukifanya hivyo basi utakuwa miongoni mwa waliodhulumu.

Katika kuwatangazia watu na hasa washirikina yale aliyoamriwa na Mola wake, Bwana Mtume anabainisha katika aya hizi kuwa ni wajibu kuifuata na kushikamana nayo njia iliyonyooka na kuepuka kila aina ya upotofu. Ama kinyume chake, itikadi ya mushirkina imejaa upotofu na mambo ya uzushi chungu nzima na muhimu zaidi ni kuwa hivyo vinavyoabudiwa na washirikina hao yaani masanamu, havina uwezo wa kumdhuru wala kumnufaisha mtu kwa lolote.

Hivyo anayevielekea na kuviabudu vitu hivyo huwa ameidhulumu nafsi yake na pia kuifanyia dhulma dini ya haki ya mbinguni.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini ya kufuata ni ile inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu. Aidha aya zinatuonyesha kuwa kila mwenye akili na busara hufanya kitu ambacho ima kitamletea manufaa au kumuepusha na madhara.

Lakini kama tujuavyo masanamu na miungu wengine wengine wote bandia hawana uwezo wa hayo.

Kwa haya machache basi tunaifunga darsa yetu hii kwa kumwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki na kutuwafikisha kumwabudu yeye kwa ikhlasi. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

YUNUS 107-109

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 107

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 326 na ya mwisho inayozungumzia sura hiyo tunayoianza kwa aya ya 107 ambayo inasema:

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿١٠٧﴾

107. Na kama Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara, basi hapana wa kukuondolea ila yeye. Na akikutakia kheri basi hapana awezaye kurudisha fadhila zake. Huzifikisha kwa amtakaye katika waja wake. Naye ni Mwingi wa Kusamehe na Mwingi wa Kurehemu.

Katika aya ya mwisho tuliyoisoma katika darsa iliyopita Allah s.w.t alimtaka Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w) asimame imara na kuwatangazia kinagaubaga washirikina kuwa njia yake yeye ni ya tauhidi, na wala hatolegeza msimamo kwa sababu ya kuwavutia ao washirikina waukubali Uislamu.

Aya tuliyosoma inaendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia na kumwambia Bwana Mtume na Waislamu kwa jumla kwamba, elewa kuwa kheri yoyote utakayopata au dhara yoyote itakayofika iko mikononi mwa Mola wako Allah s.w.t, na hakuna yeyote ghairi ya yeye aliye na uwezo wa kukupa kheri au kukupokonya neema yoyote uliyopewa na yeye Mola. Kama ambavyo bila ya ridhaa yake Mola, hakuna mtu yeyote awezaye kukudhuru, kama ambavyo endapo Mwenyezi Mungu s.w.t atataka dhara yoyote ile impate mja hakuna yeyote aliye na uwezo wa kumkinga mja na dhara hiyo.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa mushirikina na makafiri waelewe kwamba kukataa kwao kuiamini haki hakutawawezesha kutoka nje ya irada ya Allah s.w.t, na kwa hakika kile alichoandika Mola kiwafike ndicho kitakachotokea. Aidha aya inatuelimisha kuwa kheri na neema azipatazo mja zinatokana na ihsani na fadhila zake Mola na wala si kwa kustahiki mja.

AYA YA 108

Ifuatayo sasa ni aya ya 108 ambayo inasema:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَكُمُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا وَمَا أَنَا عَلَيْكُم بِوَكِيلٍ ﴿١٠٨﴾

108. Sema: Enyi watu haki imekwisha kukujieni kutoka kwa Mola wenu. Basi anayeongoka, anaongoka kwa faida ya nafsi yake, na anayepotea, anapotea kwa khasara ya nafsi yake. Na mimi si mlinzi juu yenu.

Katika aya hii ambayo ni moja kabla ya aya ya mwisho ya suratu Yunus Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w) anawahutubu watu wote kwa jumla kwamba mimi nina jukumu la kukufikishieni wito wa wahyi wa Mola wangu na kukulinganieni kuifuata njia yake tu; na wala sina haki ya kukulazimisheni muukubali wito huo.

Kila mmoja kati yenu anaweza kuamua kwa hiyari yake kuukubali uongofu na kuongoka, au kuukana na kupotoka. Lakini jueni kwamba kuamini kwenu na kukufuru kwenu hakuna tofauti yoyote kwa Mwenyezi Mungu s.w.t wala mimi Mtume wake, na kwa hakika kama ni kupata faida au madhara na hasara, hilo litakurudieni nyinyi wenyewe.

Kwani Mwenyezi Mungu yeye ni mkwasi wala hahitaji chohcote kwenu, nami pia nimetimiza wajibu wangu wa kukulinganieni na kukufikisheni risala ya uongofu kutoka kwa Mola wenu, na hivyo sina dhima yoyote juu ya kuamini au kutoamini kwenu.

Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ameondoa dhima kwa waja wake kwa kuwaonyesha na kuwabainisha njia ya haki. Kufuata au kutofuata hilo liko katika hiyari ya waja wenyewe.

Nukta nyengine ya kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa jukumu la maulamaa na wale wafanyao tablighi ya dini ni kuwaelimisha na kuwaonyesha njia watu na si kuwalazimisha waikubali na kuifuata.

AYA YA 109

Darsa ya 326 na sura yetu ya Yunus inahitimishwa na aya ya 109 ambayo inasema:

وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَاصْبِرْ حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّـهُ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ ﴿١٠٩﴾

109. Na (nimeambiwa): Fuata yanayofunuliwa kwako kwa Wahyi. Na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na yeye ndiye mbora wa mahakimu.

Aya hii ya mwisho ya sura hii inasisitiza kwa mara nyingine juu ya kushikamana barabara na njia ya haki ya risala ya wahyi utokao kwa Mola Muumba, kwanza kabisa ikimuelekea bwana Mtume mwenyewe na kisha waumini kwa jumla, kwa kuwataka waendelee kuwa na subra hadi ushindi wa haki dhidi ya batili.

Kama inavyojulikana mataghuti na madhalimu hufanya kila vitimbi na njama ili kuwakwamisha waumini wa kweli wasiweze kushikamana na kamba ya lailaha illa llah kama inavyostahiki.

Na ndiyo maana aya inawataka waumini kusimama kidete dhidi ya njama hizo na kuvumilia tabu na mashaka yote yatakayowapata katika njia hiyo. Alaa kulli haal Mwenyezi Mungu s.w.t anaona kila kinachofanywa na waja wake wote, na siku itafika ambapo atahukumu baina yao kwa uadilifu. Lakini hata hapa duniani pia, pale waumini wanaposimama kidete kukabiliana na madhalimu, mwishowe hupata nusra ya Allah na haki kuishinda batili. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa watu wana hiyari ama kuamini au kukufuru, hata hivyo kukufuru kwao kusitufanye sisi tukaingiwa na shaka katika kufuata njia ya uongofu ya kushikamana na maamrisho ya Mola wetu na kujiweka mbali na makatazo yake. Wapenzi wasomaji.

darsa ya 326 imefikia tamati na kuhitmisha pia tarjumi na maelezo ya sura ya kumi ya Yunus.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atuwafikishe kuyatekeleza kivitendo yale yote tuliyojifunza ndani ya sura hii, Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS