TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA
KIMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA
KIMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA
KIMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED
KUPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI
Sura Ya Tano: Al - Maidah
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI
Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.
Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.
Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.
Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.
Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).
Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.
Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo,vile vile kutaja nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika; kama vile Afrika ya kusini, Zimbabwe nk, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.
Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.
Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.
Mwisho
: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.
MAKOSA YA CHAPA
Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.
Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.
Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama" badala ya "Fawqahum yawamal qiyama" Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.
Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: " Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"
Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.
Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.
Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin
:"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."
Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubaliayale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH
1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA
﴿لَتَجِدَنَّ أَشَدَّ النَّاسِ عَدَاوَةً لِّلَّذِينَ آمَنُوا الْيَهُودَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا وَلَتَجِدَنَّ أَقْرَبَهُم مَّوَدَّةً لِّلَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ قَالُوا إِنَّا نَصَارَىٰ ذَٰلِكَ بِأَنَّ مِنْهُمْ قِسِّيسِينَ وَرُهْبَانًا وَأَنَّهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ﴾
82.Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa walio amini ni Mayahudi na washirikina. Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanao sema: Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi.
﴿وَإِذَا سَمِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَى الرَّسُولِ تَرَىٰ أَعْيُنَهُمْ تَفِيضُ مِنَ الدَّمْعِ مِمَّا عَرَفُوا مِنَ الْحَقِّ يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاكْتُبْنَا مَعَ الشَّاهِدِينَ﴾
83.Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa Mtume, utaona macho yao yanamiminika machozi kwa sababu ya haki waliyoitambua, wanasema: Mola wetu tumeamini tuandike pamoja na wanaoshuhudia
﴿وَمَا لَنَا لَا نُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَمَا جَاءَنَا مِنَ الْحَقِّ وَنَطْمَعُ أَن يُدْخِلَنَا رَبُّنَا مَعَ الْقَوْمِ الصَّالِحِينَ﴾
84.Na kwa nini tusimwamini Mwenyezi Mungu na haki iliyotujia, na hali tunatumai Mola atuingize peponi pamoja na watu wema?
﴿فَأَثَابَهُمُ اللَّـهُ بِمَا قَالُوا جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ﴾
85.Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyosema, Bustani zipitazo chini yake mito, Humo watakaa milele, Na hayo ndiyo malipo ya wafanyao mema.
﴿وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ﴾
86.Na wale waliokufuru na kuzikanusha Aya zetu, hao ndio watu wa motoni
UADUI WA MAYAHUDI NA URAFIKI WAWAKRISTO
Aya 82 - 86
MAANA
Hakika utawakuta walio maadui zaidi kuliko watu wengine kwa walioamini ni mayahudi na washirikina.
Yaani mayahudi na washirikina ndio waliokuwa maadui zaidi kwa Waislamu. Mara nyingi watu wameitolea ushahidi Aya hii, kuwa dini ya kikristo iko karibu zaidi na Uislam kuliko dini ya kiyahudi. Hilo ni kosa ikiwa inakusudiwa dini ya kiyahudi na ya kikristo kabla ya kugeuzwa. Kwa sababu dini kwa Mwenyezi Mungu na Mitume wake ni moja tu kwa upande wa itikadi na msingi yake. Na kama ikikusudia baada ya kubadilishwa, basi zote mbili ni sawa (Ukristo na Uyahudi) hakuna yenye afadhali.
Usahihi ni kuwa uhasama wa mayahudi na washirikina katika Uislam unatokana na mgongano baina ya mwito wa kiislam na tabia iliyokuwa imeshika kasi katika Bara arabu mwanzo wa utume. Tabia hiyo ilikua ni mashindano ya kupora mali na watumwa. Vilevile riba, ghushi na mengineyo ya kutumia nguvu na utapeli. Tabia hii iliambukiza wafanyibiashara wa kigeni, kama walivyoambukizwa viongozi wa kiyahudi waliokuwa wakimiliki viwanda na biashara ya ndani.
Ukaja mwito wa Muhammad(s.a.w.w)
unaohimiza uadilifu na kukataa dhuluma na unyonyaji wa aina zote, na kuzuia unyonyaji wa mayahudi na washirikina. Kutokana na hali hiyo ndipo pande zote mbili zikakutana na kukubaliana kwa pamoja kujiepusha na dini na itikadi na kuungana mkono kupigana na Muhammad(s.a.w.w)
, adui wa wote wawili.
Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa uadui wa mayahudi na washirikina kwa waislam, ulikuwa ni kwa msukumo wa kidunia na wala sio wa kidini, lakini mayahudi walijificha nyuma ya pazia la dini kwa kujionyesha na unafiki; sawa na wafanyavyo leo watu wanaotafuta chumo la haramu. Zaidi ya hayo ni kuwa mayahudi na washirikina wanashirikiana katika ubaguzi. Lakini washirikina pamoja na ujahili wao walikuwa na moyo usiokuwa mgumu, wakarimu na wenye fikra huru zaidi ya mayahudi. Ndio maana wengi wao wakamwamini Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
na ni mayahudi wachache tu ndio waliomwamini Muhammad.
NI NANI WALIO KARIBU NAWAISLAMU KIMAPENZI
Na utawakuta walio karibu zaidi kwa mapenzi na waumini ni wale waliosema sisi ni wanaswara.
Baadhi wanaichukulia Aya hii na iliyo baada yake ni chombo cha kukoroga mambo, kwamba Uislamu unaelemea mojawapo ya majeshi mawili hivi sasa. Jambo hili ndilo lililotufanya tufafanue Aya hizi nne kwa namna ambayo haitaacha nafasi kwa wale wanaobadilisha mambo.
Hakika mwenye kuziangalia vizuri Aya hizi, hawezi kuwa na hata chembe ya shaka kuwa zinakamilishana na kwamba haifai kabisa kuifasiri moja pekee yake bila ya kuichanganya na wenzake.
Nazo ziko wazi kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuwafanya bora manaswara, kwa ujumla, kuliko makundi mengine katika kuwa karibu kiurafiki, si kwa umbali wala karibu.
Isipokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikusudia kikundi maalum kutoka manaswara (wakristo) kwa dalili ya kuwa yeye hakuishia hapo tu bali aliendelea kusema: "Hayo ni kwa sababu wako miongoni mwao makasisi na watawa, na kwamba wao hawafanyi kiburi." Tena akaendelea kusema: Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa mtume, utaona macho yao yanamiminika machozi kwa sababu ya haki waliyoitambua; wanasema: "Mola wetu! Tumeamini basi tuandikie pamoja na wanaoshuhudia"
Maana yake ni kuwa miongoni mwa manaswara (wakristo) wako walioujua Uislamu,wakaukubali kwa kutii, kukinai na kwa imani.
Historia inathibitisha hivyo; kama ambavyo inathibitisha chuki ya manaswara kwa Uislam na Waislam. Kwa mfano: Fedheha ya Wataliano huko Tripoli ya Magharibi, na Wafaransa katika Algeria, Tunisia, Morocco na Syria, Vile vile fedheha ya Waingereza katika Misr, Iraq, Sudan n.k.
Na leo hii
Marekani wanaaungana na mayahudi katika kulingamiza taifa la Palestina. Wanawapa silaha za kisasa maharamia hawa, kisha wanafanya uchokozi na kudai kuwa wao ndio waliochokozwa na kuungwa mkono na Marekani katika Baraza la Usalama na Umoja wa mataifa. Hapo Marekani husema: Huu ndio ukweli uadilifu na demokrasia.
Je, baada ya hayo na mengi yasiyokuwa haya, itasemwa kuwa wakristo wote wako karibu kwa urafiki na waislam? Haya hayasemwi ila na mjinga au mwenye kutaka kuwapoteza watu. Kisha mpotezaji huyu atasema nini kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Na kwa nini tusimwamini Mwenyezi Mungu na haki iliyotujia, na hali tunatumai Mola atuingize pamoja na watu wema?."
Haki iliyowajia na kuiamini, ni ile waliyobashiriwa na Isa:
﴿وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ﴾
"Na kutoa Bishara ya Mjumbe atakayekuja baada yangu aitwaye Ahmad"
(61:6)
Hayo, bila shaka, yanatiliwa mkazo na kukanushwa na kauli yake Mwenyezi Mungu aliyoifuatilia bila ya upambanuzi wowote isemayo:
Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyosema, Bustani zipitazo chini yake mito, humo watakaa milele na hayo ndiyo malipo ya wafanyao mema.
Ushahidi wa wema na kulipwa pepo kwa kundi hili la wakristo ni dalili ya mkato ya kusilimu, na kwamba ndilo pekee lililokusudiwa baada ya kusifiwa wema na thawabu.
Ama wakristo ambao wameikana haki baada ya kuijua au wakaipinga bila ya kuangalia dalili zake na ubadhirifu wake, hawa wamekemewa na Mwenyezi Mungu na kuwapa kiaga kwa kusema:
Na wale waliokufuru na kuzikadhibisha Aya zetu hao ndio watu wa Motoni.
Unaweza kuuliza
: kuwa kauli ya waliokufuru na kuzikadhibisha Aya zetu, inamhusu kila mwenye kukufuru na kukadhibisha. Sasa je, kuna wajihi gani wa kuhusisha wakristo?
Jibu
: Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kuahidi pepo wenye kuamini katika wakristo, amewaahidi moto wenye kung'ang'ania ukafiri miongoni mwao. Ameleta neno la jumla, ili kujumuisha kemeo kwa kila mwenye kuihalifu haki na kuipinga, jambo ambao halipingani na yale tuliyoyasema.
Kwa ufupi ni kuwa Aya hii iko wazi kuwa makusduio ni kundi mahsusi katika wakristo - wale waliojua haki na kuiamini. Na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaingiza peponi kwa sababu ya imani yao na amali yao njema.
Tukikadiria kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na utawakuta walio karibu kwa mapenzi na waumin ni wale waliosema sisi ni manaswara," inawakusanya wakristo wote, basi itawajibika tuiache dhahiri ya Aya na tuihusishe na wale walioamini katika wao kwa sababu mbili:
Kwanza
: kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya kadhaa kuwa manswara wamemfanyia Mungu washirika, wakaficha jina la Muhammad(s.a.w.w)
na wakawafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akakataza kuwafanya mayahudi na manswara kuwa marafiki. Na akasema:
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ﴾
"Enyi Mlioamini msiwafanye marafiki mayahudi na manswara"
(5:51)
Tukiunganisha Aya hii, na zilizo mfano wa Aya hii, juu ya kauli yake Mwenyezi Mungu na utawakuta walio karibu zaidi kwa mapenzi na waumin ni wale waliosema sisi ni manswara," maana yanakuwa:
﴿مِّنْهُمْ أُمَّةٌ مُّقْتَصِدَةٌ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ سَاءَ مَا يَعْمَلُونَ﴾
"Miongoni mwao wako watu washikao njia ya wastani, na wengi wao wanayoyafanya ni mambo mbaya"
(5: 66)
Pili
: ni kuwa wafasiri wanasema, Aya hii tunayoizungumzia ilishuka kwa sababu ya Najashi, mfalme wa Uhabeshi
aliyekuwa mnaswara (Mkiristo). Kwani Mtume(s.a.w.w)
alipoona adhabu inayowapata sahaba zake kutoka kwa washirikina, mwanzo mwanzo wa mwito wa Uislam, aliwaamuru kuhamia Uhabeshi na kuwaambia: "Huko kuna mfalme ambaye hadhulumiwi mbele yake yeyote." Wakaenda huko, miongoni mwao akiwemo Jafar bin Abu Talib. Wakapata amani kwa Najashi na ujirani mwema. Hilo lilikuwa mnamo mwaka wa tano wa kutangazwa Utume.
Zimekuja Hadith Mutawatir kuwa Najashi na Baraza lake, la Mambo ya dini na mambo ya kidunia, walisilimu mikononi mwa Jafar bin Abu Talib baada ya kuwasomea Aya za Qur'an Tukufu na kutaja mazuri ya Uislam. Na kwamba walibubujikwa na machozi waliposikia Aya za Mwenyezi Mungu.
Baada ya hayo tunasema kwamba yule anayetolea ushahidi kauli ya Mwenyezi Mungu (Na utawakuta walio karibu zaidi kwa mapenzi na waumin ni wale waliosema sisi ni manswara) kwamba ukristo na wakristo kwa ujumla wote wako karibu zaidi na Uislamu na waislamu kuliko wengine, na kunyamazia Aya zinazokamilisha Aya hii, anayefanya hivyo huyo hakijui Kitabu cha Mwenyezi Mungu au ni mwenye kujionyesha tu kwa kutaka kuongeza chumvi kwa kuutumia Uislamu na Qur'an au anaweza kuwa ni mhaini anayezitia sumu fikra dhaifu katika Uislamu ili zikubali madai ya maadui wa dini, wanaowasaidia Israil na kuwapongeza kwa uchokozi wao kwa Waarabu na Waislam.
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحَرِّمُوا طَيِّبَاتِ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ﴾
87.Enyi mlioamini! Msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu. Wala msipetuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaopetuka mipaka.
﴿وَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ﴾
88.Na kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye nyinyi mnamwamini.
MSIHARAMISHE VIZURI
Aya 87 - 88
MAANA
Enyi mlioamini! Msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu.
Wamesema kuwa Aya hii imeshuka kwa Masahaba waliokuwa na hofu sana na Mwenyezi Mungu wakajiharamishia wanawake, vyakula vizuri na mavazi. Wakawa wanaswali usiku na kufunga mchana. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
akawaita na kuwasomea Aya hii, akasema: Ama mimi ninaswali usiku na ninalala, ninafunga na ninafungua na ninawaendea wanawake. Basi atakayejiepusha na mwenendo wangu si katika mimi."
Na kauli yake Mwenyezi Mungu;Wala msipetuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wapetukao mipaka,
inafahamisha kuwa kuharamisha halali ni sawa na kuhalalisha haramu, yote mawili ni dhulma na ukiukaji mipaka.
Na kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri.
Imetangulia tafsir yake katika Juz.2 (2:168)
﴿لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾
89.Mwenyezi Mungu hawachukuli kwa viapo vyenu vya upuuzi; lakini anawachukulia kwa mlivyoapa kwa nia. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa wastani wa mnavyowalisha watu wenu, au kuwavisha au kumwacha huru mtumwa. Na asiyeweza kupata (hayo), basi afunge siku tatu. Hayo ndiyo kafara ya viapo vyenu. Na vichungeni viapo vyenu. Namna hii Mwenyezi Mungu anawabainisha Aya zake ili mpate kushukuru.
VIAPO VYA UPUUZI
Aya 89
MAANA
Mwenyezi Mungu Hawachukuli kwa viapo vyenu vya upuzi.
Viapo vya upuzi ni kuachia ulimi bila ya kukusudia; kama vile kusema: Hapana wallahi, kumjibu aliyeuliza Je umemwona fulani, au kusema: Sivyo wallah, kumjibu aliyesema: Hutaki hii na Viapo hivi havitiliwi manani wala havina kafara kama mtu akihalifu lile alilo liapia.
Na aliyesema hawezi kuhisabiwa kuwa mwongo, na mtu yeyote hawezi kumwambia umemwapia Mwenyezi Mungu uwongo.
Kwa maneno mengine ni kwamba viapo hivyo havina athari yoyote ya kiapo. Hata hivyo iliyo bora ni kuacha ikiwa mtu hajaghafilika.
Lakini anawachukulia kwa mlivyoapa kwa nia.
Yaani kiapo cha sharia ambacho ni wajibu kukitekeleza na kutiliwa manani, ni kile anachoapa mtu aliyebaleghe mwenye akili timamu, kwa kukusudia, kutaka na kuwa na hiyari.
Wameafikiana kuwa kiapo kinakamilika ikiwa ni kwa kuapa kwa jina la Allah au kwa mojawapo ya majina yake mema, kama vile Khaliq, Razak (Muumbaji na Mruzuku)
Shia na Hanafi wanasema: "Kiapo hakiwi kwa jina la Msahafu na Mtume au Al-Ka'aba, kutokana na Hadith isemayo:Ambaye ataapa, basi na ape kwa jina la Allah au aache."
Shafi, Malik au Hambal wanasema: "Kinakuwa kwa jina la Msahafu. Hambali amekua peke yake katika kusema kuwa kinakuwa kwa Mtume vilevile.
Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa wastani wa mnavyowalisha watu wenu, au kuwavisha au kumwacha huru mtumwa.
Akiapa na akavunja kiapo, yaani akifanya lile aliloliapia kuliacha au kuacha lile aliloapia kulifanya, ni wajibu kwake atoe kafara akihiyarishwa baina ya mambo matatu.
Kwanza
: kuwalisha masikini kumi mlo moja kila mmoja, kwa pamoja au mbali mbali kwa sharti ya kuwa ni mlo wa chakula ambacho aghalabu yeye hula na famlia yake. Inajuzu kumpa masikini kibaba cha chakula badala ya mlo. Makusudio ya masikini, ni yule ambaye ni halali kumpa Zaka, Kibaba ni zaidi kidogo ya 800 gm.
Pili
: ni kuwavisha masikini kumi. Inatosha ile inayoitwa nguo ya kawaida. Kwa sababu sharia haikuhusisha. Kwa hiyo yakachukulia maana yaliyozoeleka bila ya kutofautisha mpya na ya zamani; mradi tu isiwe imechakaa au iliyochanika.
Tatu
: ni kumwacha huru mtumwa; wala hakuna utumwa leo.
Na asiyeweza kupata (hayo), basi afunge siku tatu.
Yaani akishindwa kuyapata hayo matatu yaliyotangulia, atafunga siku tatu. Na akishindwa kufunga, basi ataomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu na kutaraji msamaha wake.
Hayo ndiyo kafara ya viapo vyenu.
Hayo ni ishara ya kulisha, kuvisha, kuacha huru mtumwa na kufunga baada ya kushindwa na mambo matatu.
Na vichungeni viapo vyenu. Kuvifanya ni vya kawaida. Kwani kiapo cha Mwenyezi Mungu kina heshima yake na utukufu wake. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala msimfanye Mwenyezi Mungu ni pondokeo la viapo vyenu" Juz.2 (2:224)
Kuna Hadith isemayo:"Hakika Nabii wa Mwenyezi Mungu, Musa aliwaamuru waongo wasiape kwa Mwenyezi Mungu. Na mimi ninawaamuru waongo na wa kweli wasimwapie Mwenyezi Mungu."
Namna hii Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kushukuru.
Amesema Razi: "Maana yako wazi." Hata hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaka kutukumbusha neema za kujua hukumu zake, ili tusizitoe mahali pengine.