4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا شَهَادَةُ بَيْنِكُمْ إِذَا حَضَرَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ حِينَ الْوَصِيَّةِ اثْنَانِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ أَوْ آخَرَانِ مِنْ غَيْرِكُمْ إِنْ أَنتُمْ ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَأَصَابَتْكُم مُّصِيبَةُ الْمَوْتِ تَحْبِسُونَهُمَا مِن بَعْدِ الصَّلَاةِ فَيُقْسِمَانِ بِاللَّـهِ إِنِ ارْتَبْتُمْ لَا نَشْتَرِي بِهِ ثَمَنًا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ وَلَا نَكْتُمُ شَهَادَةَ اللَّـهِ إِنَّا إِذًا لَّمِنَ الْآثِمِينَ﴾
106.Enyi mlioamini! yanapo mfikia mauti mmoja wenu, wakati wa kuusia ushahidi kati yenu ni wa waadilifu wawili miongoni mwenu. Au Wengine wawili wasio kuwa katika nyinyi mnapokuwa safarini na msiba wa mauti ukawafikia. Mtawazuia wawili hao baada ya swala, na waape kwa Mwenyezi Mungu mkiwa na shaka: "Hatupokei thamani yoyote kwa haya hata kama ni jamaa wala hatufichi ushahidi wa Mwenyezi Mungu, hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi."
﴿فَإِنْ عُثِرَ عَلَىٰ أَنَّهُمَا اسْتَحَقَّا إِثْمًا فَآخَرَانِ يَقُومَانِ مَقَامَهُمَا مِنَ الَّذِينَ اسْتَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْأَوْلَيَانِ فَيُقْسِمَانِ بِاللَّـهِ لَشَهَادَتُنَا أَحَقُّ مِن شَهَادَتِهِمَا وَمَا اعْتَدَيْنَا إِنَّا إِذًا لَّمِنَ الظَّالِمِينَ﴾
107.Ikigundulika kuwa wawili hao wamestahiki dhambi, basi wengine wawili watasimama mahali pao katika wale ambao wamestahiki (kudai). Washike nafasi ya wa mwanzo waape kwa Mwenyezi Mungu: "Ushahidi wetu ni haki zaidi kuliko wa wale; na sisi hatukupita kiasi; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa madhalimu.
﴿ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يَأْتُوا بِالشَّهَادَةِ عَلَىٰ وَجْهِهَا أَوْ يَخَافُوا أَن تُرَدَّ أَيْمَانٌ بَعْدَ أَيْمَانِهِمْ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاسْمَعُوا وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ﴾
108.Hiyo inaelekea zaidi ya kwamba watatoa ushahidi ulio sawa au wataogopa visije vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao. Na mcheni Mwenyezi Mungu na msikie, Na hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi mafasiki.
KUTHIBITISHAWASIA
Aya 106-108
MAANA
Aya hizi tatu ni katika Aya za hukumu, na zinaingia katika mlango wa wasia na ushahidi. Ndani yake mna hukumu zifuatazo:
1.Enyi mlioamini! yanapomfikia mauti mmoja wenu, wakati wa kuusia ushahidi kati yenu ni wa waadilifu wawili miongoni mwenu.
Mwenyezi Mungu anakusudia kuwa atakayehisi kuwa ajali yake imekurubia na akataka kuusia anayoyataka, awalete waadilifu wawili katika Waislamu na awashuhudishe juu ya wasia wake.
Ilivyo ni kuwa wasia ni sunna na wala si wajibu ila kwa ambaye ana haki za watu au za Mwenyezi Mungu na zikamdhihirikia dalili za mauti na akahofia kupotea baada yake.
2.Au Wengine wawili wasiokuwa katika nyinyi mnapokuwa safarini na msiba wa mauti ukawafikia. Mtawazuia wawili hao baada ya Swala, na waape kwa Mwenyezi Mungu mkiwa na shaka: Hatupokei thamani yoyote kwa haya hata kama ni jamaa wala hatufichi ushahidi wa Mwenyezi Mungu, hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi.
Shia na Hambal wamesema kuwa Mwislamu akiusia safarini na asipate Mwislamu, basi anaweza kuwashuhudiza watu wawili katika Ahlul-Kitab (watu wa kitab) kuwa waape baada ya Swala mbele ya watu kuwa wao hawakuhini watu kuficha wala hawakupokea chochote kwa ushahidi au kiapo. Hapo ushahidi wao utakubaliwa kama utakavyokubaliwa wa Waislamu wote, Na itapasa juu ya hao mashahidi kuapa ikiwa kuna shaka katika ukweli wao. Ama mwaminifu hana kiapo, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mkiwa na shaka."
Hivi ndivyo walivyofutu Shia Imamiya na Hanbal kwa kutegemea Aya hii. Ama Abu Hanifu, Malik na Shafi, wamesema kuwa haukubaliwi ushahidi wa asiyekuwa Mwislamu kwa hali yoyote ile, na wameifanyia taawili Aya kwa maana nyingine. Ameongezea Malik na Shafi kuwa haukubaliwi ushahidi wa asiyekuwa Mwislamu kwa hali yoyote hata kama ni kwa wao kwa wao, Hayo yamo katika Kitab Al-Mughni.
3.Ikigundulika kuwa wawili hao wamestahiki dhambi, basi wengine wawili watasimama mahali pao katika wale ambao wamestahiki (kudai). Washike nafasi ya wa mwanzo waape kwa Mwenyezi Mungu: Ushahidi wetu ni haki zaidi kuliko wa wale; na sisi hatukupita kiasi; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa madhalimu."
Imeelezwa katika sahih za Shia na Sunni kwamba: Aya hii ilishuka kwa sababu ya watu watatu waliosafiri kibiashara, mmoja wao akiwa Mwislamu na wawili Wakristo. Njiani yule Mwislamu akaugua na akahisi kuwa ajali yake imekurubia, akaandika wasia wake, akitaja vitu vyote alivyo navyo na akauficha katika baadhi ya mizigo yake bila ya kuwafahamisha wale wenzake; kisha akawausia kuwa mizigo yake waifikishe kwa watu wake.
Alipokufa, wale wawili walichukua kitu kutoka katika bidhaa zile za maiti na wakapeleka zilizobaki kwa watu wake. Walipogundua watu wa marehemu wasia wake, waliona kuwa kuna kitu fulani kilichotajwa hakimo. Hivyo wakawauliza wale wawili, wakakanusha na wakasema wakiapa: "Alichotupa ndicho tulichowapa".
Watu wa marehemu wakakiona kile kitu kwa mtu mwengine. Walipomuuliza umekipata wapi, akajibu kutoka kwa fulani na fulani (wale watuhumiwa wawili). Kesi ikapelekwa kwa Mtume(s.a.w.w.)
. Inasemekana kuwa wale wawili walipoonyeshwa, walisema tulikinunua kwake (yule marehemu), Ndipo ikashuka Aya hii.
Maana yake yakiwa kama alama za kuleta shaka zikidhihiri kwa watuhumiwa basi wajibu wakati huo ni kusimama watu wawili katika warithi wa marehemu na waape kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni wa kweli kuliko watuhumiwa na waseme katika kiapo chao: "Sisi hatukupita kiasi; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa madhalimu" Baada ya kiapo watahukumiwa watuhumiwa.
Unaweza kuuliza
: Maneno ya wafasiri yamekuwa marefu na kugongana kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Katika wale ambao wamestahiki."
Mpaka ikanukuliwa kutoka kwa mmoja wa wakale akisema: "Hii ndiyo jumla yenye mushkeli zaidi kwa muundo katika kitab cha Mwenyezi Mungu."Sasa je tafsir sahihi ni ipi?
Jibu
: Lililowatia wafasiri kwenye shaka ni kuwa dhamir ya wanaostahiki inawarudia nani? Tujuwavyo sisi ni kuwa inawarudia warithi wa marehemu kwa sababu madeni na mambo mengine, yaliyokuwa yakimstahiki marehemu yanawastahiki warithi baada ya kufa kwake.
Kwa hiyo maana yatakuwa: Wataapa wawili katika wale ambao ni wajibu juu yao yale yaliyo wajibu kwa wanayemrithi. Mfumo wa Aya unalitilia mkazo hili.
Kwa sababu wengine wawili watakaosimama mahali pa watuhumiwa katika kuapa, hapana budi wawe ni katika warithi wa marehemu kwa maafikiano ya wafasiri, na haiwezekani kwa hali yoyote kuwa ni wengineo. Kwa hiyo inakuwa dhamiri ya wanaostahiki inawarudia wao hasa.
Hiyo inaelekea zaidi ya kwamba watatoa ushahidi ulio sawa au wataogopa visije vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao.
Hiyo ni ishara ya hukumu iliyotangulia na kuelekea zaidi ni ubainifu wa sababu ya hukumu. Yaani makusudio ya sharia tuliyoiweka ni kutogeuza mashahidi ushahidi wao wakaapa uwongo au kujizuia kuapa kwa kuhofiwa kupingwa viapo vyao na viapo vya warithi.
Unaweza kuuliza kuwa
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipobainisha hukumu aliweka wawili wawili, akasema: Ushahidi wao wawili, watasimama wawili. Lakini aliposihiria sababu ya hukumu amebainisha kwa wengi akasema: Ya kwamba watatoa ushahidi. Je kuna wajihi gani?
Jibu
: mashahidi ni wane: wawili wanashuhudia mwanzo, na wawili watasimama mahali pao ikiwa litadhihiri kosa kwa ushahidi wa kwanza. Zaidi ya haya ni kwamba sababu katika hukumu ni kuenea kwenye maudhui yaliyo tajwa na mengineyo.
﴿يَوْمَ يَجْمَعُ اللَّـهُ الرُّسُلَ فَيَقُولُ مَاذَا أُجِبْتُمْ قَالُوا لَا عِلْمَ لَنَا إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ﴾
109.Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya Mitume awaambie mlijibiwa nini? Watasema: Hatujui, hakika wewe ndiwe mjuzi sana wa ghaibu.
﴿إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ اذْكُرْ نِعْمَتِي عَلَيْكَ وَعَلَىٰ وَالِدَتِكَ إِذْ أَيَّدتُّكَ بِرُوحِ الْقُدُسِ تُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلًا وَإِذْ عَلَّمْتُكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَالتَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ وَإِذْ تَخْلُقُ مِنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ بِإِذْنِي فَتَنفُخُ فِيهَا فَتَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِي وَتُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ بِإِذْنِي وَإِذْ تُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِي وَإِذْ كَفَفْتُ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَنكَ إِذْ جِئْتَهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ﴾
110.Atakaposema Mwenyezi Mungu: Ewe Isa mwana wa Maryam! Kumbuka neema yangu juu yako na juu ya mama yako. Nilipokutia nguvu kwa roho mtakatifu, ukazungumza na watu utotoni na katika utu uzima. Na nilivyokufundisha kitab na hekima na Tawrat na Injil. Na ulipotengeneza kwa udongo kama umbo la ndege kwa idhini yangu, kisha ukapuliza likawa ndege kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wenye mbalaga kwa idhini yangu na ulipowatoa wafu kwa idhini yangu, na nilipokukinga na wana wa Israil ulipowafikia na hoja zilizowazi; wakasema wale waliokufuru miongoni mwao. Haya si chochote ila ni uchawi tu.
﴿وَإِذْ أَوْحَيْتُ إِلَى الْحَوَارِيِّينَ أَنْ آمِنُوا بِي وَبِرَسُولِي قَالُوا آمَنَّا وَاشْهَدْ بِأَنَّنَا مُسْلِمُونَ﴾
111.Na nilipowafahamisha wanafunzi kwamba Niaminini mimi na Mtume wangu, wakasema Tumeamini na ushuhudie kuwa sisi ni wanyenyekevu.
MITUME NA SIKU YA KUKUSANYWA
Aya ya 109-111
MAANA
Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya Mitume awaambie mlijibiwa nini?.
Razi anasema: "Desturi ya Mwenyezi Mungu inayopita katika Kitab chake kitukufu ni kwamba yeye akitaja aina yoyote ya hukumu, huifuatishia ama kwa mambo ya Mwenyezi Mungu, au kufafanua hali za Mitume au hali ya Kiyama, ili kutilia mkazo yaliyotangulia. Na alipotaja hapo hukumu miongoni mwa hukumu za sharia, amefuatisha kwanza kutaja hali za Kiyama kisha hali ya Isa"
Hadhara aliyoyataja Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa ni hadhara ya kutisha, atakayofufulia viumbe kwa ajili ya hisabu na hukumu, kabla ya kutoka hukumu ya msamaha.
Mwenyezi Mungu Mtukufu atawakusanya Mitume wake aliowatawanya katika nchi zake majimbo yake na mabara yake. Ilivyo ni kwamba majimbo yake na mabara yake Mwenyezi Mungu Mtukufu sio kama haya majimbo yetu na mabara yetu. Ni umma jinsi na kaumu.
Kisha atauliza kila umma na kila watu kupitia Mtume wao: "Wamekwambia nini hawa?" Anakusudia kwa swali hili kutoa hoja kwa waja wake, na kuwaandaa kwa hukumu yake. Mitume watajibu mbele ya hadhara hii:Hatujui, hakika wewe ndiwe mjuzi wa ghaibu
, Na ajuaye ghaibu haifichiki juu yake dhahiri.
Unaweza kuuliza kuwa
: Mitume wanawajua waliowapinga na kuwapiga vita katika uhai wao; sasa je, kuna wajihi gani wa kusema kwao hatujui?
Jibu
: Makusudio ya kusema kwao huku sio kukanusha kujua kabisa, bali makusudio ni kwamba elimu yao si chochote kwa upande wa elimu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu wao wanajua yale yaliyodhihirishwa na umma wao naye anayajua waliyoya dhihirisha na kuyaficha.
Atakaposema Mwenyezi Mungu: "Ewe Isa mwana wa Maryam! Kumbuka neema yangu juu yako na juu ya mama yako.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwauliza Mitume wake kwa neno fupi (Mlijibiwa nini), amemhusisha Isa
miongoni mwao kwa maneno marefu akitaja neema yake juu yake na juu ya mama yake.
Nilipokutia nguvu kwa roho mtakatifu
(ambaye ni Jibril)ukazungumza na watu utotoni
ili kumwepusha mama yako na kila dhanana katika utu uzima
yaani maneno ya utotoni yalikuwa kama maneno ya utu uzimani.
Na nilivyokufundisha kitabu
Inasemekana makusudio ya kitab ni kuandika kwa sababu neno Kitabu limechukuliwa kutoka katika neno Kitaba (kuandika)na hekima
sharia naTawrat na Injili.
Na ulipotengeneza kwa udongo kama umbo la ndege kwa idhini yangu kisha ukapuliza likawa ndege kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wenye mbalanga kwa idhini yangu na ulipowatoa wafu kwa idhini yangu.
Umepita mfano wa tafsiri yake katika Juz.3 (3:49) Mwenyezi Mugu amelikariri neno kwa idhini yangu mara nne kwa kutilia mkazo, kwamba kuumba, kufufua na kuponyesha kunatokana na uwezo wa Mwenyezi Mungu, na hakutokani na yeye Isa. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amedhihirisha vitendo hivi mikononi mwa Isa ili iwe ni dalili ya ukweli wake na utume wake.
ISA NA UTUME WA UTOTO
Inaweza ikadhaniwa au kugeuzwa kwamba Isa ni ni mtume mtoto mdogo kwa sababu yeye alizungumza utotoni, huu ni ujinga au kutia sifa. Kwa sababu yeye alisema utotoni kwa ajli ya kumuondolea tuhuma mama yake tu, kutokana na kauli ya wakosaji, si kwa kuwa ni mtume. Ikiwa Mwenyezi Mungu amewaondolea taklifu watoto wadogo je anaweza kuwakalifu na mambo mazito; kama alivyoyataja katika kauli yake:
﴿إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا﴾
"Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito"
(73:5)
Na ni nani atakayemsikia na kumtii na yeye yuko susuni? Je inaweza kuwa hoja ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwa mtoto anayenyonya? Ni mafunzo gani atakayoyafikisha kwa watu akiwa ananyonya matiti ya mama yake?
Injili zinazotiliwa maanani na wakristo zinaeleza kuwa Isa alitumwa akiwa katika rika la miaka thelathini (30). Imeelezwa katika Injili, Luka, ninanukuu: "Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikua amepata umri wake kama miaka thelathini." Luka 3:23.
La kushangaza zaidi ni kuwa Injili za wakristo zinasema kuwa mwito wa Isa ulianza akiwa na miaka thelathini, kisha mwingine mtia chumvi anasema kuwa Isa ni mtume mtoto, kinyume na Muhammad aliyetumwa akiwa na miaka arubaini
, akitoa dalili ya uzushi wake huu kwamba Isa alizungumza akiwa utotoni kwa ushahidi wa Qur'an, na kujitia kutojua kuwa Isa alizungumza utotoni ili kumtakasa mama yake, mkweli mtakatifu na wala sio kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake akiwa ananyonya.
Na nilipokukinga na wana wa Israili ulipowajia na hoja zilizo wazi; wakasema wale waliokufuru miongoni mwao: Haya si chochote ila ni uchawi tu.
Yamekuja maelezo katika Nahjul-balagha: "Isa alikuwa akifanya mto wa kulalia ni jiwe , akivaa magwanda, akila chakula kisicho na ladha, taa yake usiku ilikuwa ni mwezi, kimbilio lake wakati wa kusi ni Mashariki na Magharibi (hakuwa na kimbilio), matunda na manukato yake ni mimea inayoliwa na wanyama, hakuwa na mke wa kumtia msukosuko wala mtoto wa kumhuzunisha wala mali ya kumsumbua wala tamaa ya kumdhalilisha, kipando chake (usafiri) ni miguu yake na mtumishi wake ni mikono yake" Pamoja na hayo yote hakusalimika na mayahudi. Walijaribu kumuua wakamwita muongo na mchawi, mama yake wakamwita malaya, si kwa lolote ila ni kwa kuwa ametamka haki akiwalingania kwenye hiyo haki na kuwaamrisha. Haya hayahusiki na mayahudi tu kwani watu wengi humfanyia uadui anayewaongoza kwenye haki.
Na nilipowapa wahyi wanafunzi kwamba, niaminini mimi na mtume wangu, wakasema: "Tumeamini na ushuhudie kuwa sisi ni Waislamu." Neno wahyi linatumika kwa maana nyingi, ikiwemo ilham (ufahamisho): kama katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿وَأَوْحَىٰ رَبُّكَ إِلَى النَّحْلِ أَنِ اتَّخِذِي مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا﴾
"Na Mola wako akampa whyi Nyuki kwamba jitengenezee nyumba katika mlima"
(16:68)
﴿وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّ مُوسَىٰ أَنْ أَرْضِعِيهِ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ﴾
"Na tulimpompa wahyi mama yake Musa ya kwamba mnyonyeshe na utakapomhofia basi mtie mtoni.."
(28:7)
Maana ya wahyi kwenye Aya zote hizo ni ufahamisho na ndiyo maana yaliyotumika hapa.
Unaweza kuuliza
: kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemkumbusha Isa neema kinyume na mitume wengine pamoja na kwamba fadhila zake na neema zake hazina idadi.
Jibu
: Mwenyezi Mungu amejumlisha msemo pamoja na Mitume na akafafanua pamoja na Isa kwa sababu wafuasi wake walizama sana kwa Isa. Ama wafuasi wengine hawakuwahi kudai uungu kwa mitume wao, ndipo ukaja ufafanuzi kwa kuweka hoja.
﴿إِذْ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ هَلْ يَسْتَطِيعُ رَبُّكَ أَن يُنَزِّلَ عَلَيْنَا مَائِدَةً مِّنَ السَّمَاءِ قَالَ اتَّقُوا اللَّـهَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴾
112.Waliposema Wanafunzi: "Ewe Isa bin Mariyam, Je Mola wako anaweza kuteremshia chakula kutoka mbinguni; akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini.
﴿قَالُوا نُرِيدُ أَن نَّأْكُلَ مِنْهَا وَتَطْمَئِنَّ قُلُوبُنَا وَنَعْلَمَ أَن قَدْ صَدَقْتَنَا وَنَكُونَ عَلَيْهَا مِنَ الشَّاهِدِينَ﴾
113.Wakasema: Tunataka kula katika hicho na ili zitulie nyoyo zetu na tujue ya kuwa umetuambia kweli na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.
﴿قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ اللَّـهُمَّ رَبَّنَا أَنزِلْ عَلَيْنَا مَائِدَةً مِّنَ السَّمَاءِ تَكُونُ لَنَا عِيدًا لِّأَوَّلِنَا وَآخِرِنَا وَآيَةً مِّنكَ وَارْزُقْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ﴾
114.Akasema Isa bin Maryam: Ewe Mwenyezi Mungu Mola wetu! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu na kiwe ishara itokayo kwako na uturuzuku kwani wewe ni mbora wa wanaoruzuku."
﴿قَالَ اللَّـهُ إِنِّي مُنَزِّلُهَا عَلَيْكُمْ فَمَن يَكْفُرْ بَعْدُ مِنكُمْ فَإِنِّي أُعَذِّبُهُ عَذَابًا لَّا أُعَذِّبُهُ أَحَدًا مِّنَ الْعَالَمِينَ﴾
115.Mwenyezi Mungu akasema: Hakika mimi nitakuteremshia lakini atakayekufuru baada ya hapo basi nitamwadhibu adhabu ambayo sijamwadhibu yeyote katika walimwengu.
CHAKULA KUTOKA MBINGUNI
Aya 112-115
MAANA
Maneno yamekuwa mengi kuhusu chakula na waliokitaka kuwa je, walikuwa waumini au watiaji shaka? Na kwamba je, kilishuka chakula au hakikushuka kwa sababu wanafunzi waligeuza maombi yao baada ya kutishiwa na Mwenyezi Mungu aliposema: "Lakini atakayekufuru baada ya hapo basi nitamwadhibu adhabu ambayo sijamwadhibu yeyote katika ulimwengu."
Kama tukikadiria kuwa kilikuja je kilikuwa ni cha aina gani na rangi gani? Kisha je, waligeuzwa manyani au nguruwe baadaye kwa sababu waliiba? Sisi tutaelekea kwenye mazungumzo yetu na tunayofahamishwa na matamko ya Aya na yanayoambatana nayo.
Waliposema Wanafunzi: Ewe Isa bin Mariyam, Je Mola wako anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni; akasema Mcheni Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni waumini.
Aya hii inaashiria kuwa wanafunzi hawakuwa wakimwamini Isa walipomtaka chakula kwa sababu wao hawahitajii chakula ndipo waamini, linalotilia nguvu hilo ni kusema kwao: Je anaweza Mola wako." Huku ni kutambulisha kutia shaka katika uweza wa Mwenyezi Mungu, Hata hivyo Aya iliyotangulia imeshuhudia kuamini kwao. "wakasema tumeamimi" Zaidi ya hayo neno wanafunzi lenyewe linafahamisha kumwamini Isa na sasa je kuna wajihi gani wa kuchanganya Aya mbili hizi?
Wafasiri wengi wamejibu kuwa swali lao hili halipingi imani yao. Kwa sababu makusudio yake ni kuami ni kwa njia za hisia na macho, baada ya kuamini kwa njia ya akili na dalili. Kwa maneno mengine ni kuitia nguvu imani na kuithibitisha; sawa na alivyosema Ibrahim
:
"Lakini upate kutulia moyo wangu"
Juz.3 (2:260)
Na wanafunzi wamelifafanua kusudio lao hili kwa kusema kwao katika Aya inayofuatia:
Na ili zitulie nyoyo zetu
ikiwa ni jibu la walivyoambiwa na Isa"mcheni Mola wenu ikiwa nyinyi ni waumini."
Ama kusema kwao,"Je aweza Mola wako"
maana yake je,atakubali Mola wako tukimuuliza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?
Wakasema: Tunataka kula katika hicho na ili zitulie nyoyo zetu na tujue ya kuwa umetuambia kweli na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.
Wanataka wale ili waamini na wajue au wanataka wale ili waitie nguvu imani katika nyoyo zao na elimu katika akili zao; kama tulivyotangulia kueleza, kisha wampe habari asiyehudhuria chakula katika watu wao aamini mpinzani na utulie moyo wa muumini hata kama hatakula.
WANAFUNZI WA MUHAMMAD (S.A.W.W) NAWA ISA (AS)
Mtume Muhammad naye alikuwa na wanafunzi kama alivyokuwa nao Isa
na Mtume wowote katika Mitume. Lakini wanafunzi wa Muhammad hawakumwomba kuwashibisha kutokana na njaa kwa kutumia miujiza yake, kama walivyofanya wanafunzi wa Isa ambao walisema"Tunataka kula katika hicho", wala hawakutaka awasalimishe na hofu , kama walivyofanya sahaba wa Musa
bali walimwambia katika baadhi ya vita kupitia mdomoni mwa Mikidadi bin Al-Aswadi "Endelea ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa lile alilokutakia Mwenyezi Mungu na sisi tuko pamoja nawe wala hatutakwambia yale waliyosema wana wa Israil kwa Musa: Nenda wewe na Mola wako mpigane na sisi tuko hapa tumekaa. Lakini sisi tunakwambia: Nenda wewe na Mola wako mkapigane na sisi tuko pamoja nanyi.
Walikuwa wakifa mashahidi mbele yake na huku wakisema: "Tumefuzu, naapa kwa Mola wa Al-Kaaba." Masimulizi ya historia yao utafikiri ni vigano tu. Ammara bin Yazid alipigana siku ya Uhud mpaka majeraha yakamzidia. Alipoona sasa anakufa alijitupa miguuni mwa Mtume(s.a.w.w)
, hakuinua kichwa chake hapo mpaka alipomaliza uhai wake kwa muishilio huu mwema.
Alipoanguka Sa'ad bin Rabi, siku ya Uhud, alimwambia mmoja wa wenzake: "Mwambie Mtume wa Mwenyezi Mungu, Saad Bin Rabi anasema umetupa kitu bora cha Mtume alichowapa umma wake na wafikishie salam zangu watu wako uwaambie mwana wa Rabi anawaambia hamtakuwa na udhuru wowote kwa Mwenyezi Mungu kama mkimwacha Mtume wetu hata kidogo."
Amra bin Jumuh alikuwa mlemavu na akataka kutoka pamoja na Mtume kwenda vita vya Uhud. Watoto wake walipojaribu kumzuia akaondoka kumshtakia Mtume(s.a.w.w)
: "Mimi nataraji kuchechemea usiku kwenda peponi" Mtume(s.a.w.w)
akamruhusu. Akauliwa yeye, watoto wake wane na shemeji yake. Baada ya vita mjane wake akaja, akachukua maiti ya mumewe, nduguye na wanawe wane kwenye ngamia na kwenda nao Madina.
Wanawake wakamkabili kumuuliza habari, akasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko salama, ama msiba mwingine zaidi ya Mtume ni mwepesi." Wakamuuliza: "Na hizi maiti ni za nani?" Akawajibu: "Wanangu, mume wangu na ndugu yangu. Mwenyezi Mungu amewakirimu kwa kufa mashahidi ninawachukua nikawazike"
Mifano hii tumeileta kutofautisha baina ya sahaba wa Muhammad na wa mitume wengineo. Wala hatutakuwa tumeongeza chumvi, kama tukisema kuwa hakuna mtume yeyote aliyekuwa na masahaba kama Mtume Muhammad(s.a.w.w)
. Ama siri ya hilo inakuwa katika utu wake utukufu wake na risala yake.
Akasema Isa bin Maryam: Ewe Mwenyezi Mungu Mola wetu! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ishara itokayo kwako na uturuzuku kwani wewe ni mbora wa wanaoruzuku.
Alipoona kuwa wao wanang'ang'ania, aliomba kwa unyenyekevu:Ewe Mola wetu!
Kuondoa shub-ha na kumkadhibisha kila atakayedai kuwa Isa ana uwezo katika hilo. Makusudio ya ishara ni mujiza. Na sikukuu ni furaha.
Mwenyewzi Mungu akasema: Hakika mimi nitakuteremshia lakini atakayekufuru baada ya hapo basi nitamwadhibu adhabu ambayo sijamwadhibu yeyote katika walimwengu.
Mwenyezi Mungu aliitikia maombi ya Isa ili sahaba zake wazidi kumwamini na kuamini utume wake na awe na hoja nao, kama watahalifu na watastahiki adhabu kali ambayo hajamwadhibu yeyote katika waliokanusha na waliokufuru. Kwa sababu wao ndio waliotoa maombi ya chakula na kukitaka; na mwenye kuitikiwa maombi yake amesimamiwa na hoja na hana udhuru wowote wakuhalifu.