TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 14163
Pakua: 3217


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 14163 / Pakua: 3217
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SABA Juzuu 7

Mwandishi:
Swahili

Sura Ya Sita: Al-An'am

Imeteremshwa Makka isipokuwa baadhi ya Aya.

Ina Aya 165.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

﴿الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ ثُمَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ﴾

1.Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza. Tena wale waliokufuru wanamlinganisha Mola wao (na wengine).

﴿هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن طِينٍ ثُمَّ قَضَىٰ أَجَلًا وَأَجَلٌ مُّسَمًّى عِندَهُ ثُمَّ أَنتُمْ تَمْتَرُونَ﴾

2.Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo. Kisha akapitisha muda; na muda maalum uko kwake, Tena nyinyi mnatia shaka.

﴿وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ﴾

3.Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini; anaijua siri yenu na dhahiri yenu na anayajua mnayoyachuma.

KUUMBA MBINGU NAARDHI

Aya 1 - 3

MAANA

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya giza na mwangaza.

Aya zote hizi tatu ni Aya za kilimwengu zinazofahamisha umoja wake na ukuu wake Mwenyezi Mungu.

Aya ya kwanza inaashiria kuumbwa mbingu na ardhi na giza na mwangaza.

Aya Ya pili, inaashiria kuumbwa mtu na kufufuliwa kwake baada ya kufa.

Na ya tatu, kuenea ujuzi wake kwa kila kitu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu," anakusudia kufundisha; yaani semeni sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdulillah).

Kumsifu Mwenyezi Mungu ni kuzuri katika hali zote; hata wakati wa madhara. Kwa sababu yeye ndiye afaaye kutukuzwa na kuadhimisha. Ukipatwa na msiba na ukasema Alhamdulillah basi hapo unazingatiwa kuwa mvumilivu (mwenye subira) juu ya shida, na imani yako ni yenye nguvu iliyokita ambayo haiyumbishwi na chochote.

Uzuri wa Alhamdulillah unatiliwa mkazo wakati wa furaha na kuondolewa balaa. Kwa sababu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa aliyoneemesha.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejitaja kuwa ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi na giza na mwangaza ili azizindue akili kwamba Yeye hana mshirika katika uumbaji na Uungu. Kwa hiyo anakuwa Yeye peke yake ndiye mwenye kustahiki kusifiwa na kufanyiwa ikhlasi katika kuabudiwa.

Tena wale waliokufuru wanamlinganisha Mola wao (na wengine). Ajabu ya maajabu ni kwamba ulimwengu huu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, na ubainifu huu ulio wazi na dalili mkato, bado hazikuliondoa giza zito kwenye akili ya mshirikina na kwenye moyo wake mpofu wa haki, na akaleta picha kuwa kuna mwingine mwenye kulingana sawa na Mwenyezi Mungu katika kustahiki kusifiwa na kuabudiwa.

Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo.

Yaani ameumba asili yenu, Adam kutokana na mchanga na maji. Au ameumba mada ya kila mtu kwa udongo, kwa sababu mtu anatokana na nyama na damu; na hivyo viwili vimetokana na mmea na nyama ya mnyama aliyetokana na mmea; na mmea nao umetokana na udongo.

Kisha akapitisha muda; na muda maalum uko kwake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwekea kila mtu muda (ajali) mara mbili: Wa kwanza, unaisha kwa kufa kwake, hapo hujulikana ameishi muda gani. Pili, ni kurudishwa na kufufuliwa kwake baada ya kufa. Ujuzi wa muda huu uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala haujui yeyote katika viumbe vyake; kama lilivyofahamisha neno 'uko kwake'

Tena nyinyi mnatia shaka.

Yaani, baada ya kuweko dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kukubwa, ambako ni ulimwengu, na katika kuumba kudogo ambako ni kuumba mtu na kufa kwake na kufufuliwa kwake. Baada ya haya yote mnatia shaka katika kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na utukufu wake!

Tafsir bora ya jumla hii ni kauli ya Amirul-muminin Ali(a.s) :"Namwonea ajabu anayemtilia shaka Mwenyezi Mungu naye anaona kuumba kwa Mwenyezi Mungu; ninamwonea ajabu anayesahau mauti naye anayaona mauti; na ninamstaajabia anayepinga kufufuliwa kwa mwisho naye anaona kufufuliwa kwa kwanza."

Na yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini; anaijua siri yenu na dhahiri yenu na anayajua mnayoyachuma.

Katika Aya ya kwanza Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja kwamba yeye ni Muumbaji wa mbingu na ardhi. Natija ya hayo ni kuwa yeye yuko mbinguni na ardhini; na maana ya kuweko humo ni kuweko athari zake. Katika Aya ya pili ametaja kuwa yeye ndiye Muumba wa binadamu, na atakayemfisha na atakayemfufua. Linalolazimiana na hilo ni kwamba Yeye ni Mjuzi wa anayoyaficha binadamu na anayoyadhihirisha na anayoyachuma katika imani na ukafiri, ikhlasi na unafiki na vilevile vitendo vinavyomrudia yeye vya kheri au shari.

﴿وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ﴾

4.Na haiwafikii ishara yoyote katika ishara za Mola wao ila wanaipinga.

﴿فَقَدْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ فَسَوْفَ يَأْتِيهِمْ أَنبَاءُ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴾

5.Wameikadhibisha haki ilipowafikia; kwa hiyo zitawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

﴿أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ مَا لَمْ نُمَكِّن لَّكُمْ وَأَرْسَلْنَا السَّمَاءَ عَلَيْهِم مِّدْرَارًا وَجَعَلْنَا الْأَنْهَارَ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ﴾

6.Je hawaoni vizazi vingapi tulivyoviangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyowamakinisha nyinyi, Tukawapelekea mvua nyingi, Na tukaifanya mito inapita chini yao. Kisha tukawaangamiza kwa dhambi zao. Na tukaanzisha baada yao karne nyingine.

KUKANA HOJA ZA MWENYEZI MUNGU

Aya 4-6

LUGHA

Imeelezwa katika Tafsiri Razi: Wamesema baadhi: Karne ni miaka sitini. Wengine wakasema ni sabini. Wengine wakasema ni thamanini. Lililo karibu zaidi na ufahamu ni kwamba si yenye kukadiriwa kwa muda fulani kwa zaidi au kupungua, bali makusudio ni watu wa kila zama. Wakimaliza muda mwingi husemwa: Imekwisha karne. Dalili ya hilo ni kauli yake Mtume mtukufu(s.a.w.w) :"karne bora ni karne yangu"

Misingi ya itikadi ni mitatu, Tawhid, Utume na Ufufuo. Aya tatu zilizotangulia zimeelezea Tawhid na dalili zake, na Aya hii inaelezea Utume na hali ya wanaoukanusha.

Na haiwafikii ishara yoyote katika ishara za Mola wao ila wanaipinga.

Makusudio ya ishara hapa ni hoja mkato ya kuweko Mwenyezi Mungu na umoja wake, ufufuo na Utume wa Muhammad. Maana ni kuwa makafiri wanakataa dalili ya haki na wanaipinga bila ya kuichunguza. Lau wangelikuwa ni watafutaji ukweli wangeliangalia dalili na kuzingatia maana yake. Ama kukataa na kuipinga kabla ya kuichunguza ni inadi na ujuba.

HAKUNA UDIKTETA ARDHINI WALA MBINGUNI

Wametofautiana wafasiri katika kuainisha makusudio ya hoja waliyoipinga na kuidharau. Je, ni Qur'an au muujiza mwingineo katika miujiza ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ? Au ni miujiza ya Mitume wote? Nimegundua wakati nikifuatilia tofauti hizi kuwa Aya hii tunayoifasiri na mfano wake katika Qur'an zimekusanya maana ambayo wafasiri wamejihimu kuisherehesha (kuifafanua).

Aya imekusanya dalili kwamba Uislamu unasimamia uhuru wa akili na kutoa maoni na kwamba si haki kwa yeyote, vyovyote awavyo kumtaka mwingine akubali maneno yake hivi hivi tu kwa upofu na bila ya dalili. Hata Muumba wa ulimwengu, ambaye neno lake ni tukufu, hawalazimishi waja wake kumwamini yeye na vitabu vyake, bila ya dalili.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasimamisha hoja kwa kila anayoyasema na kuyatolea mwito na kumtaka kila mwenye akili kuichunguza na kuangalia vizuri maana yake. Mwenyezi Mungu katika hilo ametukuka kabisa - ni kama kila mjuzi anayechunga haki; hata kama ukiwa mbali mshabaha wa Muumba na kiumbe.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

﴿أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِم مَّا خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ﴾

"Je, hawafikiri katika nafsi zao. Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa haki" (30:8)

Na akasema:

﴿أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ﴾

"Je, hawaangalii mbingu zilizo juu yao, vipi tulivyozijenga na tukazipamba wala hazina nyufa" (50:6)

Na akasema tena:

﴿كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴾

"Namna hii tunazipambanua ishara kwa watu wanaofikiri" (10:24)

Aya hizi na nyinginezo, zinafahamisha kwa dalili mkato kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu huleta dalili na hoja kwenye mwito wa haki na kutoa mwito wa kuzifikiria vizuri na kuzichunguza.

Akipinga yule asiyeamini ila yale anayoyataka yeye, basi yeye peke yake ndiye mwenye jukumu la kukanusha kwake na kupinga kwake.

Wameikadhibisha haki ilipowafikia; kwa hiyo zitawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

Mtu anaweza kujitia kutoijua haki bila ya kuitilia umuhimu, na kutoiamini, lakini akawa haiungi mkono wala kuipiga vita; kama ilivyo kwa mtu asiyejali mambo. Au anaweza kuwa katika msimamo wa mwenye kuikadhibisha.

Huyu ni mwenye kiburi, ikiwa atakadhibisha na huku anajijua. Ama akiikadhibisha na kuidharau, basi huyo ni mwenye kuipiga vita. Wa kwanza kosa lake ni hafifu kuliko wa pili kwa sababu yeye anafanana na mtu asiyepiga kura.Wa pili naye dhambi yake ni hafifu kuliko watatu kwa sababu yeye ameitia kura yake kwa waongo. Ama wa tatu amekadhibisha na akadhihirisha harakati dhidi ya haki, naye ndiye aliyekusudiwa kukemewa na kupewa kiaga, na kwamba yeye atakutana na malipo ya inadi yake na istihzai yake.

Je hawaoni vizazi vingapi tulivyoviangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyowamakinisha nyinyi.

Waarabu wa kijahiliya walikuwa wakijua mengi kuhusu watu wa Ad, Thamud, Lut na wengineo, na katika misafara yao walikuwa wakiona athari zao wakizishuhudia na kuzizungumzia. Walikuwa wakijua kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza kwa sababu wao walikadhibisha haki waliyokuja nayo Mitume yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aya hii inawahusu wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) kuwa wazingatie kuangamia kwa vizazi vilivyo pita. Nao walikuwa na milki na nguvu wasizokuwa nazo hao wanaoambiwa - Waarabu wa kijahiliya, Tukawapelekea mvua nyingi.

Yaani mvua inayoleta mavuno na kuwamiminia riziki. Na tukaifanya mito inapita chini yao. Ni fumbo la rutuba na mavuno mengi. Kisha tukawaangamiza kwa dhambi zao Mali na nguvu hazikuwafaa kitu. Na tukaanzisha baada yao karne nyingine. Mwenye akili ni yule mwenye kupata funzo kutokana na wengine kabla ya mwengine kupata funzo kutoka kwake.

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA

﴿وَلَوْ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ كِتَابًا فِي قِرْطَاسٍ فَلَمَسُوهُ بِأَيْدِيهِمْ لَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ﴾

7.Na lau tungelikuteremshia maandishi katika karatasi na wakayagusa kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema: Haya si chochote ila ni uchawi dhahiri.

﴿ وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ مَلَكٌ وَلَوْ أَنزَلْنَا مَلَكًا لَّقُضِيَ الْأَمْرُ ثُمَّ لَا يُنظَرُونَ﴾

8.Wanasema: Mbona hakuteremshiwa Malaika. Na kama tungeliteremsha Malaika, hakika amri ingekwishahukumiwa kisha wasingelipewa nafasi.

﴿ وَلَوْ جَعَلْنَاهُ مَلَكًا لَّجَعَلْنَاهُ رَجُلًا وَلَلَبَسْنَا عَلَيْهِم مَّا يَلْبِسُونَ﴾

9.Na kama tungelimfanya Malaika, bila shaka tungelimfanya mtu. Na tungeliwavisha yale wanayoyavaa.

﴿وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِّن قَبْلِكَ فَحَاقَ بِالَّذِينَ سَخِرُوا مِنْهُم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴾

10.Na hakika walifanyiwa stihzai Mitume kabla yake, lakini yakawazunguka wale waliofanya mzaha miongoni mwao, yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

﴿ قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ ثُمَّ انظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ﴾

11.Sema: Tembeeni katika ardhi, kisha muone ulikuwaje mwisho wa wa wale waliokadhibisha?

LAU TUNGELIKUTEREMSHIA KARATASI

Aya 7 - 11

MAANA

Na lau tungelikuteremshia maandishi katika karatasi

Mtume(s.a.w.w) alikaa Makka miaka kumi na tatu tangu kuteremshiwa Wahyi mpaka alipohama kwenda Madina. Katika muda wote huu alikuwa akiwalingania watu hapo kwenye Tawhid na uadilifu, na kuwakataza ushirikina na ukandamizaji.

Mfumo wake katika kutoa mwito ulikuwa ni hekima na mawaidha mazuri. Wakamwitikia wachache wao na wengi wao hawakumwitikia.

Isitoshe hawakutosheka kutomwitikia, bali walimpiga vita na kumuudhi kwa mikono yao na mara nyingine kwa ndimi zao. Akawa anavumilia maudhi yao na akijitahidi ili waamini, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia:

﴿وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ﴾

"Na wengi katika watu hawatakuwa wenye kuamini hata ukijitahidi vipi" (12:103)

Na akasema: Na lau tungelikueremshia maandishi katika karatasi na wakayagusa kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema: Haya si chochote ila ni uchawi dhahiri."

Yaani lau tungelikuteremshia maandishi katika ukurasa mmoja, wakayaona na wakayagusa na kuyashuhudia na macho yao wangeliyatia ila na kusema ni uchawi.

Aina hii ya watu iko katika kila kizazi na kila mahali. Wakati wetu huu kuna kundi kubwa la watu wasiotosheka na upinzani wa kuhisiwa na kuguswa, mpaka wakaviita vitu kwa vinyume vyake; mbwa mwitu wakamwita punda na nyoka wakamwita njiwa wa amani.

Hii Amerika inapigana vita vya kuangamiza watu katika Vietnam na huku inasema sisi tunajenga na kutumikia uhai, Na hiyo Israil inachokoza, kisha inasema sisi ndio tuliochokozwa.

Wanasema: Mbona hakuteremshiwa Malaika.

Dhamir ya 'wanasema' inawarudia washirikina wa Kiquraish. Walimtaka Mtume(s.a.w.w) awateremshie Malaika ashuhudie anayoyalingania, na awe na msaada wa kutekeleza risala yake. Mfano wa Aya hii ni kama Aya ile isemayo:

﴿وَقَالُوا مَالِ هَـٰذَا الرَّسُولِ يَأْكُلُ الطَّعَامَ وَيَمْشِي فِي الْأَسْوَاقِ لَوْلَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مَلَكٌ فَيَكُونَ مَعَهُ نَذِيرًا﴾

"Na wakasema: Ana nini Mtume huyu anakula chakula na anakwenda sokoni. Mbona hakuteremshiwa Malaika awe muonyaji pamoja naye." (25:7)

Na kama tungeliteremsha Malaika, hakika amri ingekwishahukumiwa kisha wasingelipewa nafasi.

Yaani lau kama Mwenyezi Mungu angeliwateremshia Malaika wangelikufa mara moja bila kungojea. Sasa hapa utauliza, kuna uhusiano gani kufa kwao mara moja na kuteremshiwa Malaika?

Baadhi ya wafasiri wamejibu kuwa watu wakimwona Malaika roho zao zitatoweka kabisa kutokana na vitisho wanavyoviona, Lakin kauli hii si ya kutegemewa kabisa. Wengine wakasema: Imetangulia katika hekima ya Mwenyezi Mungu kumwangamiza kila anayehalifu Malaika.

Kauli hii nayo ndiyo haifai kabisa kuliko ile iliyotangulia; Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawaangamizi wanaomhalifu katika maisha haya, wala Malaika hawana utukufu zaidi ya Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka sana utukufu wake.

Jibu sahihi ni kuwa: uhusiano uliopo kwenye kufa na kuteremshwa Malaika ni siri ambayo Mwenyezi Mungu hakuidhihirisha kwa waja wake wala siri hii haiwezi kujulikana na akili. Kwa hiyo ni wajibu kunyamaza aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu.

Na kama tungelimfanya Malaika, bila shaka tungelimfanya mtu.

Lau Mwenyezi Mungu angelimtuma Malaika kwa watu, angekuwa na hali mbili tu: Ama abakie na Sura yake au awe katika Sura ya mtu.

Na kubakia katika Sura yake na wakati huo huo kuwa mjumbe kwa watu, ni jambo lisilowezekana. Kwa sababu tabia ya Malaika si kama tabia ya mtu. Na kufikisha ujumbe kunahitajia kutangamana na hao watu, nako hakupatikani ikiwa maumbile na tabia hazilingani. Zaidi ya haya ni kwamba Malaika hawakuumbwa kuishi katika sayari hii.

Na lau angelikuwa katika mfano wa binadamu wangelisema tunataka Mtume wa kimalaika. Kwa hiyo Malaika kwa Sura yake ya kimalaika hawezi kufikisha ujumbe na kwa sura ya mtu hawezi kuaminiwa na washirikina wa Makka.

Kwa hiyo tatizo litabakia hivyo hivyo bila ya ufumbuzi. Kwa hakika ni kwamba Aya hii inaelezea wazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwajadili wakadhibishaji kwa mfumo wa mantiki ambao wenye akili wanautumia kuwanyamazisha wabishani wao.

Na tungeliwavisha yale wanayoyavaa.

Yaani lau Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwajaalia Malaika katika Sura ya mtu, watu wangelidhani kwamba yeye ni mtu hasa.

Na hakika walifanyiwa stihzai Mitume kabla yake, lakini yakawazunguka wale waliofanya mzaha miongoni mwao, yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

Yaani tulia ewe Muhammad kutokana na dharau unazozipata kwa watu wako.! Kwani kudharauliwa Mitume sio jambo lililoanza sasa, bali lilikuwako tangu zamani. Na Mwenyezi Mungu aliwaangamiza waliowafanyia mizaha Mitume wao; na yatawapitia wanaokufanyia mzaha yale yaliyowapitia waliokuwa kabla yao. Hayo yalikuwa, kwani Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza waliomdharau Muhammad(s.a.w.w) ; alipomwambia:

﴿إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ﴾

"Hakika sisi tumekutoshea (dhidi ya) wanaofanya mzaha (15:95)

Sema: Tembeeni katika ardhi, kisha muone ulikuwaje mwisho wa wa wale waliokadhibisha?

Tafsir yake imekwishatangulia katika Juz 4 (3:137).

﴿قُل لِّمَن مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُل لِّلَّـهِ كَتَبَ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ لَيَجْمَعَنَّكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ﴾

12.Sema: Ni vya nani vilivyomo ardhini na mbinguni? Useme ni vya Mwenyezi Mungu, Amejilazimishia rehema, Hakika atawakusanya Siku ya Kiyama. Isiyo na shaka, Wale ambao wamezitia hasarani nafsi zao, basi wao hawaamini.

﴿وَلَهُ مَا سَكَنَ فِي اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴾

13.Ni vyake vilivyotulia katika usiku na mchana; naye ndiye asikiaye na ajuaye.

﴿قُلْ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَتَّخِذُ وَلِيًّا فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ يُطْعِمُ وَلَا يُطْعَمُ قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَسْلَمَ وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴾

14.Sema: Je nimfanye mlinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu; naye ndiye anayelisha, wala halishwi. Sema: Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa mwanzo katika wenye kusilimu, Na wala kabisa usiwe katika washirikina.

﴿ قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ﴾

15.Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya siku kubwa ikiwa nitamwasi Mola wangu.

﴿ مَّن يُصْرَفْ عَنْهُ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمَهُ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ﴾

16.Atakayeepushwa nayo siku hiyo, hakika (Mwenyezi Mungu) amemrehemu na huko ndiko kufuzu kuliko wazi.

AMEJILAZIMISHIA REHEMA

Aya 12 - 16

MAANA

Sema: Ni vya nani vilivyomo ardhini na mbinguni? Useme ni vya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu kuwauliza Washirikina wa Kiarabu: Ni nani anayemiliki mbingu na ardhi? Kisha akamwamrisha kuwajibu kuwa ni Mwenyezi Mungu peke yake, yeye ndiye Mfalme wa wafalme.

Inawezekana kuwa yeye ndiye muulizaji na mwenye kujibu. Kwa sababu mwulizaji na mwenye kuulizwa wanaafikiana na jawabu. Kwani Washirikina wa Kiarabu walikuwa wakiamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Muumba wa ulimwengu na ndiye mwenye kumiliki:

﴿وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ﴾

"Ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Basi wapi wanakogeuzwa?" (29:61)

Unaweza kuuliza : maadamu mambo yako hivyo, basi kuna faida gani ya kuuliza?

Jibu : Makusudio ya swali na jibu lake ni kumvuta mbishani akiri uwezekano wa kufufuliwa, na kusimamisha hoja juu yake. Kwa sababu ikiwa yeye ndiye Muumbaji wa ulimwengu na ndiye mwenye kuumiliki, basi anaweza kuumaliza na kuurudisha tena.

Amejilazimishia rehema.

Ameirudia Mwenyezi Mungu (s.w.t) jumla hii katik Sura hii Aya 54.

Wafasiri wanasema Mwenyezi Mungu amejiwabishia rehema kwa wajibu wa fadhila na ukarimu. Na sisi tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila na ukarimu; wakati huo huo tukiamini kuwa rehema yake ni natija ya kujitosheleza na kila kitu na kuwa kila kitu kinamhitajia yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa sababu kiumbe kwa tabia yake anahitajia usaidizi wa Muumbaji na rehema zake kwa uhitajio wa sababu kwenye ilichokisababisha.

Kwa hiyo basi, rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake haiepukani na dhati yake Mwenyezi Mungu na ukamilifu wake. Hivyo basi maana ya Amejilazimishia rehema yanakuwa kwamba rehema yake inalazimiana na dhati yake takatifu; sawa na ulivyo uweza na ujuzi.

Hakika atawakusanya Siku ya Kiyama.

Mkusanyiko huu vilevile ni lazima; ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akausifu kwa kusema: Isiyo na shaka, kwa sababu Siku hiyo atalipizwa kisasi aliyedhulumiwa kwa aliyemdhulumu na atalipwa mwovu mfano wa uovu wake, na mwema atalipwa zaidi ya mfano.

Lau si Siku hii, haki ingelikwenda bure na mwenye nguvu ndio angelikuwa mwenye amri na wala sio Muumbaji wa ulimwengu.

Wale ambao wamezitia hasarani nafsi zao, basi wao hawaamini hawaamini.

Zamakhshari anasema: "Makafiri wamechagua hasara, kwa hiyo hawataamini." Zamakhshari ni katika Mu'tazila wasemao mtu ana hiyari, halazimishwi.

Razi naye akasema; "Mwenyezi Mungu ndiye aliyejaalia hasara yao kwa hiyo hawakuamini" Razi ni katika Ashaira wasemao mtu analazimishwa hana hiyari. Wengine wamesema hawakuamini Makafiri kwa ajili ya kufuata baba zao.

Tuonavyo sisi ni kuwa Aya inaashiria kwenye hakika ya mtu na kwamba mtu ni nafsi yake na mwili wake, na kila kimoja katika viwili hivyo kinamkamilishia mwenzake na kwamba mtu hatakuwa na maisha sahihi mpaka avitumikie vyote viwili.

Mwenye kufanya amali kwa ajili ya roho tu bila mwili, au kwa mwili tu bila ya roho, basi amepata hasara na mwenye kupata hasara hiyo hawi na amani yoyote.

Ni vyake vilivyotulia katika usiku na mchana; naye ndiye asikiaye na ajuaye.

Yaani yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye mwenye kumiliki kila kitu.Unaweza kuuliza : kuwa maana haya yashafahimishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya iliyotangulia: 'Sema ni vya nani vilivyomo ardhini na mbinguni? Useme ni vya Mwenyezi Mungu.' Kuna wajihi gani wa kukaririka huku?

Wafasiri wamejibu kuwa : Aya ya kwanza imeeleza viumbe kwa wakati na hii ni kwa mahali; navyo ni vyombo viwili vya kila kiumbe, iwe ni kwa kimaada au kimaana (kimwili au kiroho). Kwa hiyo ukapatikana ujumla na maana kwa Aya zote mbili; na akafuatishia Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa sifa mbili za usikizi na ujuzi ili kutilia mkazo mkusanyiko wa maana hii.

Mara nyingi tumeeleza kuwa kukaririka katika Qur'an ni jambo la kawaida, lakini wafasiri wamekuwa wakijaribu kuleta kitu tu, hata kama hakuna haja.

Sema: Je nimfanye mlinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu?

Vipi nimtake msaada mwingine, Naye ni Muumba wa mbingu na ardhi? naye analisha na wala halishwi. Mwingine hawezi kujizuia na madhara wala kujinufaisha.

Sema: Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa mwanzo katika wenye kusilimu.

Kwa sababu Muhammad ni mlinganiaji wa kwanza kwenye Uislamu, basi anakuwa yeye ni Mwislamu wa kwanza katika umma wake. Vinginevyo atakuwa katika wale ambao wanaamrisha na wao hawafuati amri. Hiyo haiwezekani kabisa kwa yule aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu kwa risala yake.

Na wala kabisa usiwe katika washirikina.

Ni muhali kuwa miongoni mwao. Maneno haya yamesihi tu kwa vile ni maelekezo kutoka kwa aliye juu kwenda kwa aliye chini; kama tulivyosema mara nyingi.

Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya siku kubwa ikiwa nitamwasi Mola wangu.

Mtume kufanya maasia haiwezekani kutokana na cheo cha Isma. Lakini 'kukadiria muhali si muhali' Lengo lake hapa ni kuthibitisha au kutilia mkazo msingi wa usawa baina ya watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba yeye ameumba pepo kwa anayemtii, hata kama ni mtumwa wa Kihabeshi; na akaumba moto kwa anayemwasi, hata kama ni sharifu wa Kiquiraish.

Na kumcha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kunakuja kwa kiasi cha kujua ukubwa wake:

﴿إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ﴾

"Kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wenye elimu tu" (35:28) na hasa Mitume.

Atakayeepushwa nayo siku hiyo, hakika (Mwenyezi Mungu) amemrehemu na huko ndiko kufuzu kuliko wazi.

Kila mwenye kuhofia vituko vikubwa, huona uokovu kuwa ni rehema kubwa, na kufuzu ni jambo adhimu.

﴿وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ وَإِن يَمْسَسْكَ بِخَيْرٍ فَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

17.Na kama Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hakuna wa kuyaondoa ila yeye, Na akikugusisha kheri, basi yeye ndiye mwenye uweza juu ya kila kitu.

﴿وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ﴾

18.Naye ndiye mwenye kuwatenza nguvu waja wake; naye ndiye mwenye hekima mwenye habari.

﴿قُلْ أَيُّ شَيْءٍ أَكْبَرُ شَهَادَةً قُلِ اللَّـهُ شَهِيدٌ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ أَئِنَّكُمْ لَتَشْهَدُونَ أَنَّ مَعَ اللَّـهِ آلِهَةً أُخْرَىٰ قُل لَّا أَشْهَدُ قُلْ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ وَإِنَّنِي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ﴾

19.Sema: Ni kitu gani kikubwa zaidi kwa kutoa ushahidi? Mwenyezi Mungu ndiye shahidi baina yangu na baina yenu. Na nimepewa wahyi Qur'an hii ili niwaonye kwayo na kila imfikiayo. Je, kweli nyinyi mnashuhudia kwamba wako waungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu? Sema: Mimi sishuhudii. Sema: Yeye ni Mungu mmoja tu, na hakika mimi ni mbali na hayo mnayoyashirikisha.

HAKUNA MWONDOAJI MADHARA ILA MWENYEZI MUNGU

Aya 17 - 19

MAANA

Na kama Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hakuna wa kuyaondoa ila yeye.

Aya hii inafahamisha kuwa: madhara kama vile ufukara, maradhi n.k. ni kazi ya Mwenyezi Mungu sio ya mtu. Vilevile kuyaondoa na kuepukana nayo ni kazi yake. Kwa hiyo kuna haja gani ya kufanya juhudi na kufanya kazi?

Jibu :Kwanza , kufanya juhudi na kujitafutia riziki ni wajibu kiakili na kinakili (nukuu). Ama kiakili ni kwamba uhai haukamiliki ila kwa kazi. Na kinukuu zimepituka kiwango cha mutawatir. Miongoni mwazo ni:

"Tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila ya Mwenyezi Mungu" (62:10)

﴿هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ وَإِلَيْهِ النُّشُورُ﴾

"Yeye ndiye aliyeidhalilisha ardhi kwa ajili yenu; basi tembeeni katika pande zake na mle katika rizki zake." (67:15).

Katika Hadith ni"Safirini mtapata faida." Nyingine ni:"Fanyianeni dawa enyi waja wa Mwenyezi Mungu, kwani yule ambaye ameteremsha ugonjwa, ameuteremshia na dawa".

Kwa hiyo basi atakayezembea akaacha kuhangaika na akapatwa na madhara, yeye mwenyewe ndiye atakayekuwa na jukumu. Mwenye kuhangaika bila ya kuzembea na akaguswa na madhara, basi jamii yake iliyo mbovu katika hali na hukumu zake ndiyo itakayokuwa na jukumu. Ikiwa jamii yake pia ni nzuri basi atakuwa amedhurika kwa kudura ya Mwenyezi Mungu na majaaliwa yake.

Pili, Hakika Mwenyezi Mungu hamtakii madhara mja wake yeyote. Vipi iwe hivyo, na hali yeye ndiye aliyesema:"Na mimi siwadhulumu waja." (50:29) Na ndiye mwenye kusema:

"Na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa waja" (2:207)

Na katika Hadith imeelezwa:"Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwahurumia zaidi waja wake kuliko mama anavyomhurumia mwanawe."

Kwa hiyo basi makusudio ya madhara katika Aya hii ni yale anayolipwa mja kutokana na amali yake; au ni mtihani kwa ajili ya masilahi yake na mengineyo ambayo hayapingani na uadilifu wake Mwenyezi Mungu na rehema yake, Tumeyafafanua hayo tulipofasiri (5:100).

Na akikugusisha kheri, basi yeye ndiye mwenye uweza juu ya kila kitu.

Yaani hakuna wa kuzuia heri na fadhila zake. Arrazi anasema: "Mwenyezi Mungu katika kheri ametaja kuwa yeye ndiye mwenye uweza juu ya kila kitu na katika madhara ametaja kuwa hakuna wa kuyaondoa ila yeye, ametaja hivyo kwa kufahamisha kuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu kufikisha kheri yanashinda yale matakwa yake ya kufikisha madhara".

Naye ndiye mwenye kuwatenza nguvu waja wake; naye ndiye mwenye hekima mwenye habari.

Kutenza nguvu ni ishara ya uweza wa Mwenyezi Mungu na kuwa na habari ni ujuzi wake. Amewatenza nguvu Mwenyezi Mungu waja wake kwa kuwafanya waweko bila ya kutaka kwao; na amewatenza nguvu vilevile kwa mauti.

Ibnul-Arabi katika Futuhatil-makkiyya anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatenza nguvu waja wake kwa sababu wao wamempinga na wakagombana naye katika kuhalifu hukumu zake na mwenye kugombana na Mwenyezi Mungu basi yeye ni mwenye kutenzwa nguvu na hapana budi kushindwa.'

Sema: Ni kitu gani kikubwa zaidi kwa kutoa ushahidi?

Yako maelezo katika baadhi ya Hadith kuwa Washirikina wa Makka walimwambia Mtume: Mayahudi na Wakristo hawashuhudii Utume wako hebu tuonyeshe anayekushuhudia, Ndipo akateremsha Mwenyezi Mungu (s.w.t) Aya hii.

Yaani waulize Ewe Muhammad ni nani ambaye ushahidi wake uko juu ya ushahidi wote? Kisha akamwamrisha kuwajibu:

Sema: Mwenyezi Mungu ndiye shahidi baina yangu na baina yenu.

Hakuna jawabu halisi kama hili, nalo ni kuwa shahidi baina yetu ni Mwenyezi Mungu.

Na nimepewa wahyi Qur'an hii ili niwaonye kwayo na kila imfikiayo.

Qur'an ni ushahidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu ya Mtume Muhammad, ambayo imewashinda kuleta hata Sura moja mfano wake, wakajaribu wakashindwa. Kushindwa huku ni ushahidi mkubwa wa ukweli wa Mtume katika risala yake.

Kauli yake: 'Ili niwaonye kwayo na kila imfikiayo,' Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemteremshia hii Qur'an ili imuonye kila itakayemfikia mpaka siku ya ufufuo. Sahaba mmoja alikuwa akisema: "Atakeyefikiwa na Qur'an ni kama kwamba amemwona Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) "

Vilevile Aya hii inafahamisha kuwa ambaye haukumfikia mwito wa Muhammad(s.a.w.w) , basi anasamehewa katika kuacha Uislamu. Hayo nimeyazungumza kwa ufafanuzi katika Juz. 4 (3:115).

Je, kweli nyinyi mnashuhudia kwamba wako waungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu?

Swali hapa ni la kukanusha na kuyaweka mbali hayo. Maana ni vipi mtamfanya Mwenyezi Mungu pamoja na waungu wengine baada ya kuwa wazi dalili za umoja wake Mwenyezi Mungu Mtukufu! Kisha Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kujibu kuwa yeye hashuhudii kama wanavyoshuhudia.

Sema: Mimi sishuhudii. Kisha akamwamrisha jambo jingine: Sema: Yeye ni Mungu mmoja tu, na hakika mimi ni mbali na hayo mnayoyashirikisha ya kuabudu masanamu na mengineyo.