8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA
﴿قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ﴾
33.Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema, Basi hakika hao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu wanakataa ishara za Mwenyezi Mungu.
﴿وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا وَأُوذُوا حَتَّىٰ أَتَاهُمْ نَصْرُنَا وَلَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِ اللَّـهِ وَلَقَدْ جَاءَكَ مِن نَّبَإِ الْمُرْسَلِينَ﴾
34.Na hakika walikadhibishwa Mitume kabla yako, wakavumilia juu ya kukadhibishwa na kuudhiwa, mpaka ikawafikia nusura yetu. Na hakuna wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu, Na bila shaka zimekujia baadhi ya habari za Mitume hao.
﴿وَإِن كَانَ كَبُرَ عَلَيْكَ إِعْرَاضُهُمْ فَإِنِ اسْتَطَعْتَ أَن تَبْتَغِيَ نَفَقًا فِي الْأَرْضِ أَوْ سُلَّمًا فِي السَّمَاءِ فَتَأْتِيَهُم بِآيَةٍ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَمَعَهُمْ عَلَى الْهُدَىٰ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْجَاهِلِينَ﴾
35.Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza kutafuta njia ya chini kwa chini katika ardhi au ngazi kwendea mbinguni na kuwaletea ishara. Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka, bila shaka angeliwakusanya kwenye uongofu. Basi usiwe miongoni mwa wajinga
﴿إِنَّمَا يَسْتَجِيبُ الَّذِينَ يَسْمَعُونَ وَالْمَوْتَىٰ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ ثُمَّ إِلَيْهِ يُرْجَعُونَ﴾
36.Hakika wanaokubali ni wale tu wanaosikia, Na wafu Mwenyezi Mungu atawafufua kisha watarejeshwa kwake.
﴿وَقَالُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ قُلْ إِنَّ اللَّـهَ قَادِرٌ عَلَىٰ أَن يُنَزِّلَ آيَةً وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ﴾
37.Na husema: Kwa nini hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake? Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza wa kuteremsha ishara yoyote, lakini wengi wao hawajui.
TUNAJUA KUWA YANAKUHUZUNISHA
Aya 33 - 37
MAANA
Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema.
Msemo unaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w)
, Dhamir ya 'wanayoyasema' inawarudia wale waliomkadhibisha Mtume(s.a.w.w)
. Ama yale wanayoyasema bali waliyasema hasa, ni yale yaliyoashiriwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t):
﴿ثُمَّ تَوَلَّوْا عَنْهُ وَقَالُوا مُعَلَّمٌ مَّجْنُونٌ﴾
Kisha wakampa mgongo na wakasema: Amefunzwa (na) ni mwendawazimu."
(44:14)
"Wakasema Makafiri: Hakika huyu ni mchawi dhahiri."
(10:2) Na mengineyo.
Basi hakika hao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu wanakataa ishara za Mwenyezi Mungu.
Kila mwenye kumpiga vita mwenye haki, basi ameipiga vita haki yenyewe, na kila mwenye kumdharau Mtume kwa kuwa yeye anachukua risala ya aliyemtuma, basi atakuwa amemdharau yule aliyemtuma na sio Mtume mwenyewe.
Washirikina wa Makka walikuwa wakimwita Muhammad(s.a.w.w)
mkweli mwaminifu, kabla ya Utume. Alipowaletea risala ya Mwenyezi Mungu na kuwasimamishia hoja, walimpiga vita na wakamwita mwendawazimu, mchawi nk.
Kwa hiyo kumkadhibisha kwao huku na hali hii, ni kukadhibisha risala ya Mwenyezi Mungu na hoja zake. Hakuna linalofahamisha hilo kwa dalili zaidi ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّـهَ يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ﴾
"Hakika wale wanaokubai, kwa hakika wanambai Mwenyezi Mungu; mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao"
(48:10)
Na hakika walikadhibishwa Mitume kabla yako, wakavumilia juu ya kukadhibishwa na kuudhiwa, mpaka ikawafikia nusura yetu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake ikiwa watakukadhibisha, basi wamekadhibishwa Mitume kabla yako na wakaudhiwa katika kufikisha risala yake, wakavumilia juu ya maudhi mpaka ikawajia nusura. Kwa hiyo nawe vumilia kama walivyovumilia; na Mwenyezi Mungu atakunusuru kama alivyowanusuru.
Huu ndio mzunguko wa maisha - mvutano baina ya kheri na shari na haki na batili. Ni muhali kwa mpigania haki asipate maudhi kutoka katika maadui wa haki. Vilevile haki haiwezi kushinda ila wapatikane watakaoinusuru wavumilivu katika jihadi ya haki na wainunue kwa nafsi zao, watu wao na mali zao.
Ni desturi ya Mwenyezi Mungu, wala huwezi kupata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na hakuna wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu.
Wala sijui wakati ambao wabatilifu wamekuwa na nguvu kuliko wakati huu tunaoishi. Wameweka vituo vya kijeshi kila mahali, vituo vya kuharibu, silaha kali za kumaliza watu na kubomoa. Wanatawala nyenzo za wananchi wadhaifu, mabenki, magazeti, uchapishaji na usambazaji, Mpaka yule mtu aliye mwaminifu mwenye ikhlasi anajikuta ametupwa hawezi kutoa makala huru au kutangaza haki kupitia kwenye Idhaa. Lakini mhaini, popote atakapoelekea atapata mapokezi na kutukuzwa [7]
.
Na bila shaka zimekujia baadhi ya habari za Mitume hao.
Yaani tumekusimulia kabla yale yaliyowapata Mitume kutokana na watu wao na jinsi walivyovumilia katika kukadhibishwa na maudhi, na kwamba mwisho ushindi ulikuwa wao.
Na desturi hii itakupitia wewe, kama iliyowapita wao, wala hakuna mwenye kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu.
Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza kutafuta njia ya chini kwa chini katika ardhi au ngazi kwendea mbinguni na kuwaletea ishara.
Aya hii ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake Mtukufu:
﴿فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ﴾
"Basi roho yako isitoke kwa majonzi juu yao; hakika Mwenyezi Mungu anayajua yote wanayoyafanya."
(35:8)
Aya zote hizi mbili zinatoa picha jinsi Mtume(s.a.w.w)
alivyokuwa akipata jakamoyo na uchungu kutokanana upinzani wa washirikina kwa mwito wake.
Yaliyompata Mtume kutoka kwa watu wake ni yale yanayoondoa upole wa mpole. Lakini yeye akavumilia na kuwa na matumaini; wala hakuwaapiza bali aliwaombea, akisema:"Ewe Mola wangu! Wasamehe watu wangu, hakika wao hawajui"
Pamoja na hayo yote alikuwa akihisi uchungu kwa kufuru zao. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia kwa Aya hii, ili kumpoza na kumwondolea matumaini na aachane nao; kisha angoje kidogo, aone vile utakavyokuwa mwisho wa wakadhibishaji.
Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka, bila shaka angeliwakusanya kwenye uongofu.
Razi anasema kuwa: "Hii inafahamisha kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hataki makafiri waamini, bali anataka kuwabakisha kwenye ukafiri.
Lakini hii itakuwa ni dhuluma hasa, na Mwenyezi Mungu hawadhulumu waja. Usahihi wa maana ya jumla hii, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hataki kumlazimisha yeyote katika kumwamini, bali anamwachia hiyari yake baada ya kumsimamishia hoja kwa dalili na ubainifu. Lau angelitaka waja wake waamini kwa kusema 'kuwa ikawa', basi asingelikufuru yeyote katika wao. Lakini hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ilitaka ajiingize katika mambo ya watu kama mwamrishaji na mwenye kutoa nasaha, si kama Muumba mwenye nguvu, Umetangulia ufafanuzi katika Juz. 1 (2:26)
Basi usiwe miongoni mwa wajinga.
Atakuwaje Mtume Mtukufu miongoni mwa wajinga na hulka zake ni hulka za Qur'an? Msemo huu umefaa kuelekezwa kwa mtukufu wa viumbe, kwa vile unatoka kwa Muumba wa viumbe na sio kwa kwa aliye kama yeye.
Wanaokubali ni wale tu wanaosikia, Na wafu Mwenyezi Mungu atawafufua kisha watarejeshwa kwake.
Aya hii ni mfano wa Aya isemayo:
﴿إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ﴾
"Hakika huwezi kuwasikilizisha wafu wala huwezi kuwasikilizisha viziwi mwito wanapogeuka kurudi nyuma"
(27:80)
Maana ni kuwa: Ewe Muhammad! Wale unaopupia waonyeke hawakusikii kwa kufahamu na kuzingatia. Kwa sababu kupenda dunia kumewafanya kama wafu, na wafu haitakikani kuwaambia chochote; bali wanaachwa na mambo yao mpaka siku ya kiyama, watakapoiona adhabu ambayo hawataweza kuikimbia.
Na husema: Kwa nini hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake?
Utauliza
: vipi wanasema hivi na hali Mwenyezi Mungu amemteremshia Muhammad(s.a.w.w)
ishara na hoja kadhaa na ubainifu.
Jibu
: Makusudio ya ishara hapa ni muujiza ule walioutaka wao kuwa ni sharti la wao kumwamini Muhammad(s.a.w.w)
; hawakusudii muujiza unaomkinaisha mwenye kuitafuta haki, Lau wangeliutaka huo wasingelisema hivyo.
Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza wa kuteremsha ishara yoyote
, ile wanayotaka, lakini yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu haiteremshi kwa kuitikia matakwa na hawaa zao; isipokuwa anateremsha miujiza kulingana na inavyopitisha hekima yake.
Lakini wengi wao hawajui
, kuwa anateremsha miujiza kulingana na hekima Yake na sio hawa za watu.
﴿وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُم مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يُحْشَرُونَ﴾
38.Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi, Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha watakusanywa kwa Mola wao.
﴿وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا صُمٌّ وَبُكْمٌ فِي الظُّلُمَاتِ مَن يَشَإِ اللَّـهُ يُضْلِلْـهُ وَمَن يَشَأْ يَجْعَلْهُ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴾
39.Na wale waliokadhibisha ishara zetu ni viziwi na mabubu wako gizani. Amtakaye Mwenyezi Mungu humpoteza na amtakaye humweka katika njia iliyonyooka.
WANYAMA NA NDEGE NI UMMA
Aya 38-39
LUGHA
Mnyama, ni kila anayetembea katika ardhi wakiwa ni: Watu, wanyama na wadudu.
MAANA
Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anabainisha katika Aya hii kwamba baina yetu na wanyama kuna aina ya kufanana, lakini hakufafanua aina yenyewe. Je, tunafanana katika kuwa wao ni viumbe wa Mwenyezi Mungu; au katika kumwamini Mwenyezi Mungu na kumsifu kwa sifa zake njema? Au tunafanana katika kuwa wao ni aina zinazojulikana kwa majina; kama zinavyojulikana koo na kabila? Au ni katika kupanga maisha yao na kufanya mambo kulingana na masilahi?
Kwa hali yoyote iwayo ni kuwa wataalamu wengi wamechunguza tabia na kazi za wanyama, wadudu na ndege na wakafikia kwenye siri za ajabu zinazoshuhudia kuweko mpangaji mwenye hekima, Tutataja baadhi ya mifano.
Ndovu huweka mahakama kwa mhalifu na ndovu aliyekosea huhukumiwa kwa kutengwa na kundi la wengine ili aishi peke yake katika upweke.
Kunguru anapohisi hatari itakayowapata wenzake huwaonya kwa sauti maalum. Ama katika hali ya furaha hutoa sauti iliyo karibu na kicheko.
Utauliza
: Kuna faida gani katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kusema arukaye kwa mbawa zake ambapo kumtaja Ndege kunafahamisha moja kwa mja kuruka kwa mbawa?
Jibu
: Hakuna faida, tuijuayo, isipokuwa ufasaha wa maneno.
Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote.
Imesemekana kuwa makusudio ya Kitab hapa ni lawhim-mahfudh (ubao maalum wenye kuhifadhiwa) wenye kukusanya yaliyokuwa na yatakayokuwa.
Kauli ya pili, inasema ni fumbo la ujuzi wa Mwenyezi Mungu kujua makusudio ya mtu, na kauli zake na vitendo vyake.
Kauli ya tatu, inasema ni Qur'an na kwamba Mwenyezi Mungu amebainisha ndani yake kila yapasayo kubainishiwa watu, miongoni mwa misingi ya dini na matawi yake na yanayofungamana nayo, Nasi tumeichagua kauli hii katika kufasiri Aya ya (2:2) Juz. 1, kifungu Qur'an na sayansi.
Kisha watakusanywa kwa Mola wao.
Dhahiri ya maneno inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu atawakusanya wanyama na ndege siku ya Kiyama, kama atakavyowakusanya watu. Vilevile Aya isemayo:"Na wanyama mwitu watakapokusanywa."
(82:5)
Maulama wengi wamesema hivyo kwa kutegemea Aya hizo mbili na Hadith isemayo: "Hakika Mwenyezi Mungu atawachukulia kisasi watu kutokana na wenye pembe."
Sisi tuko pamoja na Ibn Abbas aliyesema kuwa makusudio ya kukusanywa wanyama ni mauti yao; kama ilivyopokewa katika Hadith: "Anayepatwa na kifo ndiyo kiama chake." Kwa sababu hisabu na adhabu ni baada ya kukalifiwa na sharia na kuzihalifu. Wala hakuna kukalifiwa na sharia ila pamoja na akili; na wanyama na ndege hawana akili, kwa hiyo hawakalifiwi na sharia.
Kwa sababu hizo basi, hawatakusanya kwa ajili ya hisabu. Lau wanyama wangelichukuliwa hisabu basi ingefaa zaidi watoto wadogo wachukuliwe hisabu. Ama Hadith ya 'kuchukua kisasi', ni fumbo la uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kwamba yeye hataacha kidogo wala kikubwa ila atakidhibiti.
Ikiwa Mwenyezi Mungu atawaadhibu wenye pembe wakimpiga mtu, basi vizuri zaidi ni kutuharimishia sisi kuwachinja wanyama. Ama kauli ya anayesema kuwa Mwenyezi Mungu atayabadilisha maumivu ya mtu kwa mnyama, hiyo ni kumsemea Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi wowote.
Na wale waliokadhibisha ishara zetu ni viziwi na mabubu wako gizani.
Yaani wao ni kama viziwi, kwa sababu wao hawasikii mwito wa haki, na ni kama mabubu kwa sababu wao hawaitamki haki waliyoijua na wako katika giza la kufuata na giza la ushirikina, ukafiri, ufasiki na dhambi.
Amtakaye Mwenyezi Mungu humpoteza na amtakaye humweka katika njia iliyonyooka.
Yametangulia maelezo kuhusu uongofu na upotevu katika Juz.1 (2:26) na Juz.2 (4:88).
﴿قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ أَوْ أَتَتْكُمُ السَّاعَةُ أَغَيْرَ اللَّـهِ تَدْعُونَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴾
40.Sema: niambieni, kama ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu au ikiwafikia ile saa, je, mtamuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni wakweli?
﴿بَلْ إِيَّاهُ تَدْعُونَ فَيَكْشِفُ مَا تَدْعُونَ إِلَيْهِ إِن شَاءَ وَتَنسَوْنَ مَا تُشْرِكُونَ﴾
41.Bali yeye tu ndiye mtakayemuomba, Atawaondolea mnayomuomba akitaka, Na mtawasahau mnaowashirikisha
.
﴿وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ أُمَمٍ مِّن قَبْلِكَ فَأَخَذْنَاهُم بِالْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ لَعَلَّهُمْ يَتَضَرَّعُونَ﴾
42.Kwa hakika tulipeleka (Mitume) kwa umma zilizokuwa kabla yako; kisha tukawatia katika shida na madhara ili wapate kunyenyekea.
﴿فَلَوْلَا إِذْ جَاءَهُم بَأْسُنَا تَضَرَّعُوا وَلَـٰكِن قَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴾
43.Basi mbona wasinyenyekee ilipowafikia adhabu yetu? Lakini nyoyo zao zilikuwa ngumu na shetani akawapambia waliyokuwa wakiyafanya.
﴿فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ فَتَحْنَا عَلَيْهِمْ أَبْوَابَ كُلِّ شَيْءٍ حَتَّىٰ إِذَا فَرِحُوا بِمَا أُوتُوا أَخَذْنَاهُم بَغْتَةً فَإِذَا هُم مُّبْلِسُونَ﴾
44.Basi waliposahau yale waliyokumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu, mpaka walipofurahia yale waliyopewa tuliwakamata kwa ghafla; na mara wakawa wenye kukata tamaa.
﴿فَقُطِعَ دَابِرُ الْقَوْمِ الَّذِينَ ظَلَمُوا وَالْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴾
45.Ikakatwa mizizi ya watu waliodhulumu; na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote.
SEMA NIAMBIENI
Aya 40 - 45
MAANA
Sema: niambieni, kama ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu au ikiwafikia ile Saa, je, mtamuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni wakweli?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwamrisha Mtume wake awaambie washirikina: Niambieni kama ikiwafikia adhabu, kama ile iliyoteremshiwa wale waliokadhibisha Mitume yao; au yakiwafikia maumivu makubwa ya mauti na vitisho vya Kiyama, je katika hali hii, mtayaita masanamu na mizimu mliyokuwa mkiabudu na kudai kuwa itawaondolea fazaa na adhabu?
Makusudio ya Aya hii ni kuwa Makafiri kesho watajivua na yale waliyokuwa wakiyaabudu na kukimbilia kwa Mwenyezi Mungu baada ya kuwabainikia kuwa hakuna hila wala nguvu ila kwa msaada wake Yeye tu peke yake bila ya kuwa na mshirika.
MWENYEZI MUNGU NA MAUMBILE
Bali yeye tu ndiye mtakayemuomba.
Baada ya kuwauliza kuwa mtamwomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu siku ya vituko vikubwa, amelithibithisha jibu kwa kusema kwake:(Bali yeye tu ndiye mtakayemuomba)
.
Hilo ndilo jibu linaloaminiwa na kujibiwa na umbile ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu, katika dunia na akhera, Na sio maana ya umbile la Mwenyezi Mungu kuwa mtu atamtambua Muumba hivi hivi tu bila ya dalili. Hapana! Kama ni hivo basi kusingelitokea mtu yeyote wa kumkanusha Mwenyezi Mungu.
Hakika maana ya umbile hili ni kuwa Mwenyezi Mungu amempa mtu maandalizi ya kufahamu dalili zinazofahamisha kuweko Mwenyezi Mungu, na dalili hizi haepukani nazo kwa hali yoyote. Anayekufuru anakufuru kwa kuzembea na kupuuza kwa kuepuka kuchunguza dalili na hoja. Kwa hiyo ndipo akastahiki adhabu kwa kupuuza huko.
Kwani hakuna tofauti kabisa katika mtazamo wa akili, baina ya mwenye kuacha kufanya amali, kwa makusudi, na huku anajua; na yule mwenye kuiacha haki akafuta batili kwa kutojua lakini ana uwezo wa kujua na kupambanua uongufu na upotevu, lakini akaacha kwa kupuuza na kudharau.
Inawezekana maandalizi hayo yakajificha nyuma ya pazia la kufuata maelezo na matamanio; sawa na linavyojificha jua nyuma ya mawingu, ikafikiriwa kwa yule asiyejua sitara hizo kuwa yeye amemkana Mwenyezi Mungu kwa kukosa dalili na dalili iko katika dhati yake na maumbile yale ambayo amemuumbia Mwenyezi Mungu. Na siku ya Kiyama sitara hii iliyozuka itaondoka na kudhihiri hakika iliyo wazi wala hakutasalia nafasi ya shaka na ukanusho.
Atawaondolea mnayomuomba akitaka.
Yaani nyinyi washirikina mtaacha siku ya Kiyama, kuomba masanamu mliyokuwa mkiyaabudu duniani na mtamwomba Mwenyezi Mungu peke yake, wakati hakika ya kila jambo itakapodhihiri.
Na mtawasahau mnaowashirikisha.
Yaani nyinyi washirikina siku ya Kiyama mtaacha kuyaomba masanamu mliyokuwa mkiyaabudu duniani na kumwomba Mwenyezi Mungu peke yake wakati itakapodhihiri hakika ya kila kitu.
Kwa hakika tulipeleka (Mitume) kwa umma zilizokuwa kabla yako; kisha tukawatia katika shida na madhara ili wapate kunyenyekea.
Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawaadhibu waja wake ila baada ya kuwapelekea mjumbe atakayewaongoza kwenye njia ya uongofu. Kama hawakuongoka anawapa fursa ili wajirudi wenyewe, na kuwatia katika mtihani kwa mabalaa ili wanyenyekee na watubie, lakini wao waling'ang'ania maasi; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya inayofuatia hii.
Basi mbona wasinyenyekee ilipowafikia adhabu yetu? Lakini nyoyo zao zilikuwa ngumu na shetani akawapambia waliyokuwa wakiyafanya.
Mwenyezi Mungu, ambaye zimetukuka sifa zake, anasema kuwa wao hawakunyenyekea ilipowafikia shida duniani wala hawakumdhalilikia Mwenyezi Mungu kwa kuacha inadi yao, bali waling'ang'ania ukafiri, na shetani akawa nyuma yao akiwapambia upotevu na ufisadi.
Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamkubali kila anayekimbilia kwake, hata kama kukimbia kwake ni kwa vikwazo vya shida na balaa. Hivi ndivyo alivyo aliye mkarimu na adhimu. Hamnyimi mwenye kuomba wala hamkatishi tamaa, kwa namna yoyote lengo na msukumo wake utakavyokuwa.
Basi waliposahau yale waliyokumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu mpaka walipofurahia yale waliyopewa tuliwakamata kwa ghafla; na mara wakawa wenye kukata tamaa.
Aliwaonya kwanza kwa kauli kupitia kwa Mitume. Pili, kwa vitendo alipowapa mtihani kwa shida na madhara.
Waliponga'ang'ania ukafiri na inadi aliwafungulia milango ya riziki na raha, ili kuwasimamishia hoja na kuwavuta kidogo kidogo kwa neema baada ya mtihani wa nakama.
Walipofurahia raha na kuzidi kiburi na wala wasielekee kwenye uongofu, basi Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa namna wasiyofikiria, wakajuta kwa kuzembea na wakakata tamaa ya kuokoka.
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) mara nyingine aliwapa dhiki na mara nyingine furaha kwa kupenda waongoke; sawa na afanyavyo mzazi kumhurumia mwanawe akitaka atengenekewe.
Lakini wala hawakushukuru raha wala kuwaidhika na balaa. Wakang'olewa wote asibakie yeyote katika wao, ili wapate funzo watakaokuja baada yao.
Ikakatwa mizizi ya watu waliodhulumu; na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote.
Kwa sababu ya kuwaneemesha kwake waumin na kuwanusuru na watu wa kufuru na ufisadi.