9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA
﴿قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَخَذَ اللَّـهُ سَمْعَكُمْ وَأَبْصَارَكُمْ وَخَتَمَ عَلَىٰ قُلُوبِكُم مَّنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِهِ انظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ ثُمَّ هُمْ يَصْدِفُونَ﴾
46.Sema: Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akichukua kusikia kwenu na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni nani Mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu awezaye kuwaletea tena? Tazama jinsi tunavyozikariri ishara, kisha wao wanapuuza.
﴿قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ بَغْتَةً أَوْ جَهْرَةً هَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الظَّالِمُونَ﴾
47.Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla au kwa dhahiri nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu?
﴿ وَمَا نُرْسِلُ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ فَمَنْ آمَنَ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾
48. Na hatutumi Mitume ila niwabashiri na waonyaji. Na wenye kuamini na wakafanya wema, basi haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika. 49. Na wale waliokadhibisha ishara zetu itawagusa adhabu kwa sababu ya walivyokuwa mafasiki.
AKICHUKUA MWENYEZI MUNGU KUSIKIA NA KUONA
Aya 46-49
MAANA
Sema: Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akichukuwa kusikia kwenu na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni nani Mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu awezaye kuwaletea tena?
Mtu ni usikizi, uoni na moyo. Lau haya yanamwondokea, basi hatakuwa ni chochote, mnyama atakuwa ni bora kuliko yeye. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuvichukua hivyo, kwa sababu Yeye ndiye aliyeviumba.
Makusudio ya ishara hii ni kuwakumbusha Mwenyezi Mungu Makafiri kuwa wanaowafanya waungu asiyekuwa yeye hawatawakinga na madhara wala hawatawaletea manufaa:
﴿وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ﴾
"Na Mwenyezi Mungu anapowatakia watu adhabu hakuna cha kuzuia"
(13:11)
Tazama jinsi tunavyozikariri ishara, kisha wao wanapuuza.
Yaani tumesimamisha hoja juu yao zinazofuatiwa na hoja kwa mifumo mbali mbali, ili wawaidhike na wazingatie. Tukawaondolea nyudhuru zote ili waamini. Lakini dalili hizo mkato hazikuwadishia ila kuendelea na ukafiri, dhuluma na inadi.
Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla au kwa dhahiri nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu?
Mara ya pili anawapa mawaidha na kuwatishia kuwaletea adhabu ambayo hawataweza kuikinga; ni sawa ingewajia ghafla kwa namna wasiyoijua au kwa wazi wazi kwa namna ya kuwa tayari nayo. Mara hii katika Aya hii anawaonya Mwenyezi Mungu na kuwapa onyo ili waiogope adhabu kabla ya kutukia kwake, na waelekee kwenye uongofu wao, lakini nyoyo zao zikasusuwaa na wala wasipondokee kwenye haki na uongofu.
Na hatutumi Mitume ila na waonyaji.
Hii ndiyo kazi ya Mtume, anawapa bishara watiifu na kuwaonya waasi. Kazi hii, pamoja na urahisi wa ufafanuzi wake na kueleweka kwake, lakini ndiyo kazi yenye mashaka makubwa na nzito. Kwa sababu inagusa maisha ya mataghuti moja kwa moja, na kuyaingilia masilahi yao na manufaa yao.
Mwishilio wa kazi ya Mtume ni kulipwa wema mwenye kuamini na kufanya matendo mema, na kuadhibiwa mwenye kukufuru na kuzikadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu.
Na wenye kuamini na wakafanya wema, basi haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.
Kwa sababu mwenye makosa ndiye anayehofia na kuhuzunika. Ama asiye na hatia huwa katika amani na utuvu.
Na wale waliokadhibisha ishara zetu itawagusa adhabu kwa sababu ya walivyokuwa mafasiki.
Ufasiki ni zaidi ya ukafiri. Kila kafiri ni fasiki, sio kila fasiki ni kafiri. Makusudio ya ufasiki hapa ni ukafiri, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Waliokadhibisha ishara zetu.
﴿قُل لَّا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَفَلَا تَتَفَكَّرُونَ﴾
50.Sema: Siwaambii kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu, wala sijui ghaibu; wala siwambii mimi ni Malaika; sifuati ila ninayopewa Wahyi. Sema: Je, kipofu na mwenye kuona wako sawa? Je, hamfikiri?
﴿وَأَنذِرْ بِهِ الَّذِينَ يَخَافُونَ أَن يُحْشَرُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ لَيْسَ لَهُم مِّن دُونِهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ﴾
51.Na waonye kwayo wale wanaoogopa kwamba watakusanywa kwa Mola wao. Hawana mlinzi wala mwombezi isipokuwa yeye ili wapate kuwa na takua.
﴿وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ﴾
52.Wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake; si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, kwamba uwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu.
﴿وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لِّيَقُولُوا أَهَـٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّن بَيْنِنَا أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ﴾
53.Na namna hii tumewajaribu wao kwa wao ili waseme: Je, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewafadhili miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanaoshukuru?
﴿وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِن بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾
54.Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Amani iwe juu yenu (Assalam alaykum), Mola wenu amejilazimisha rehema. Ya kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea. Basi yeye ndiye mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
﴿وَكَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ وَلِتَسْتَبِينَ سَبِيلُ الْمُجْرِمِينَ﴾
55.Namna hii tunazieleza ishara na ili njia ya wakosefu ibainike.
SIFUATI ILA NINAYOPEWAWAHYI
Aya 50 -55
MAANA
Sema: Siwaambii kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu, wala sijui ghaibui, wala siwambii mimi ni Malaika; sifuati ila ninayopewa Wahyi.
Washirikina walimtaka Mtume(s.a.w.w)
awaambie mambo ya siri, awatolee chemchem, awaletee Malaika, apande mbinguni na awaangushie hiyo mbingu na mengineyo ambayo hayana uhusiano wowote na Utume. Ndipo akateremsha Mwenyezi Mungu Aya hii na akamwamrisha Mtume kuwaambia, kuwa yeye si Mungu wala Malaika; isipokuwa yeye ni mtu anayepewa wahyi tu.
Kwa maneno mengine ni kuwa Mungu ana sifa zinazomhusu yeye tu; kama vile kuwa ni muweza wa kila kitu, mwenye kujua kila kitu. Vilevile Malaika ana sifa zinazomhusu; kama vile kupanda mbinguni na kuwa yeye hali wala hatembei sokoni. Ama Mtume ni mtu kama watu wengine; tofauti ni kuwa yeye analetewa wahyi tu kutoka kwa Mola wake, akimpa bishara ya malipo mazuri yule atakayemwitikia, na kumuonya kwa adhabu yule atakayempa kisogo.
Wala si mambo yanayohusu Utume, kutoa habari za siri na kuleta mambo yasiyokuwa ya kawaida. Kwa hiyo kuchanganya sifa za Malaika na Mitume yake ni ujinga na upofu.
Sema: Je, kipofu na mwenye kuona wako sawa?
Tofauti ilioje baina ya mjinga mpotevu ambaye hatofautishi baina ya sifa za Mwenyezi Mungu na sifa za Mtume, na yule anayefahamu kuwa Mtume ni mtu aliye na yale waliyo nayo watu wengine, isipokuwa yeye anapewa wahyi.
Je, hamfikiri? Kuwa Mtume siye Mungu wala Malaika na kwamba yeye ni mtoaji bishara na muonyaji, ili mzifanyie haki nafsi zenu na muamini Lailaha ila Ilah Muhammadur rasulullah? (Hakuna mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu)
Na waonye kwayo wale wanaoogopa kwamba watakusanywa kwa Mola wao.
Dhamir katika kwayo inarudia Qur'an, iliyotanguliwa kuashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Sifuati ila ninayopewa Wahyi."
Wametofautiana wafasiri kuhusu wanaoogopa kukusanywa kwa Mola wao kuwa je ni waumini au makafiri, kwa kuangalia kuwa baadhi yao walikuwa wakiathirika kuhofishwa na Mtume na maonyo yake; kama ilivyoelezwa katika Tafsir ya Razi?
Tuonavyo ni kuwa baada ya Mtume(s.a.w.w)
kuwaonya watu kwa hoja zinazowasimamia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha, katika Aya hii, kuendelea na kufuatishia kuwaonya waumini kwa Qur'an ili wazidi imani, na waijue dini na hukumu zake.
Vilevile kuwaonya wasiokuwa waumini katika wale ambao kuna matarajio ya kuongoka kwao kwa kufuatisha kuonya na kukaririka.
Hawana mlinzi wala mwombezi isipokuwa yeye ili wapate kuwa na takua.
Yaani wakati unapowaonya wanakusikiliza na kunufaika na unavyowaonya na kujua kuwa hawana mlinzi wa kuwanusuru isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala mwombezi yeyote atakayeombea mbele yake ila kwa idhini yake.
Wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake; si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisTafsir abu yako si juu yao hata kidogo, kwamba uwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu.
Asubuhi na jioni ni fumbo la kuendelea kumtaja kwao Mwenyezi Mungu na kumwabudu; kama kusema "Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni."
Dhamiri ya Hisabu yao na juu yao inawarudia waumini wanaomwomba Mola wao. Maana ya si juu yako hisabu yao ni kuwa hisabu yao na hisabu ya wengineo, haihusiani na Utume wala si katika mambo yake. Hisabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu tu peke Yake; sawa na ilivyo hisabu yako ewe Muhammad.
Mwislamu, kwa hakika, anaamini moja kwa moja kwamba Muhammad(s.a.w.w)
ni Mtukufu wa viumbe vyote na wakati huo anaamini kuwa utukufu wa Muhammad haumwezeshi kumhisabu yeyote au kumwadhibu au kumpa thawabu. Hakika hisabu na malipo ni ya Mwenyezi Mungu na yanatokana na Mwenyezi Mungu pekee bila ya kuwa na mshirika.
Kwa fadhila hii ndipo Uislamu ukatofautiana na dini zote kwa kukanusha uwezo wa mtu kwa mtu mwingine vyovyote atakavyokuwa. Na kwa hali hiyo tunajifaharisha na kujitukuza kuliko Wajamaa, Wakomunisti, Mabepari, Wademokrasia na watu wa dini zote na madhehebu yote.
Wafasiri wametaja sababu za kushuka Aya hii, kuwa mamwinyi wa Kikuraish walimpitia Mtume(s.a.w.w)
akiwa na Ammar bin Yasir, Khabbab, Bilal na wengine katika Waislamu wa hali ya chini, wakasema: "Ewe Muhammad umewaridhia hawa? Unataka tuwe pamoja na hawa? Hebu waondoe tuwe sisi tu peke yetu na wewe; kisha tukimaliza warudishe ukae nao ukitaka" Imesemekana kuwa Mtume(s.a.w.w)
alitaka kuwakubalia, ndipo ikashuka Aya.
Dhahiri ya maneno hapa haiikatai hilo hasa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kwamba usiwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu." Kwa kuwadhulumu hao, ambao ni bora hasa kukaa nao na wapate faida kutoka kwako.
Kwa maneno mengine ni kwamba Mtume alitaka kuwakaribisha matajiri, ili afaidike nao, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia mafukara ni bora kufaidika nao, Ukiacha ubora huu, basi umewadhulumu mafukara waumini katika kufaidika.
Utauliza
: Je, kuacha lililo bora hakupingani na Isma?
Jibu
: Kuacha lililo bora zaidi kunajuzu na wala si haramu, mpaka kupingane na Isma. Zaidi ya hayo ni kwamba Mtume hakujaribu kuwafukuza mafukara kwa kuwadharau kutokana na ufukara wao, bali ni kwa kupupia na kuwa na tamaa ya kusilimu viongozi. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamfahamisha kuwa Uislamu hauna haja na hawa wenye kutakabari mataghuti; na kwamba iko siku watakuja silimu wakiwa madhalili walio chini; kama ilivyotokea baadaye.
Na namna hii tumewajaribu wao kwa wao ili waseme: Je, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewafadhili miongoni mwetu?
Kujaribu Mwenyezi Mungu mja wake ni kumdhihirisha kwa watu hakika yake kwa njia ya vitendo vyake na kauli zake; kama tulivyofafanua katika kufasiri Juz hii (5:94)
Maana ni kuwa tumewajaribu matajiri kwa mafakiri, ili wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaneemesha, lakini hilo likawapeleka kuwa na kiburi na kujitukuza. Imam Ali
anasema:"Msizingatie mapenzi na chuki kwa mali na watoto tu, mkasahau fitina na mtihani katika utajiri"
Amekwisha sema Mwenyezi Mungu (s.w.t):
﴿أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾ نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ بَل لَّا يَشْعُرُونَ﴾
"Je, wanafikiri kuwa yale tunayowapa mali na watoto ndio tunawaharakishia katika heri? Bali hawatambui"
(23: 55)
Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawajaribu waja wake wenye kutakabari katika nafsi zao kwa mawalii wake wanyonge machoni mwao. Musa bin Imran na nduguye Harun waliingia kwa Firaun wakiwa na majuba ya sufi na mikononi wameshikila fimbo.
Wakampa sharti la kusilimu ikiwa anataka ufalme wake na cheo chake kibakie. Akasema: Hamwoni ajabu eti hawa wananipa masharti yakubakia ufalme na cheo na wao wenyewe mnawaona walivyo na hali ya ufukara na udhalili?"
ASSALAMU ALAYKUM WA RAHMATULLAH
Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Amani iwe juu yenu (Assalam alaykum), Mola wenu amejilazimisha rehema. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
: "Mola wangu amenifundisha adabu, akaifanya nzuri adabu yangu." Ni adabu gani iliyo kama adabu ya Muumbaji wa mbingu na ardhi. Ni nafsi gani inayokuwa na kuleta matunda ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu kuliko nafsi ya Muhammad?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameifundisha nafsi hii njema na takatifu, ili kuiandaa na risala yake, risala ya rehema kwa viumbe ambayo kwayo na kwa mwenye nayo, zimetimia tabia njema.
Mwenyezi Mungu amemfundisha adabu Muhammad katika Aya kadhaa; ikiwemo Aya hii tuliyo nayo, ambayo inafundisha Mtume wa Mwenyezi Mungu na bora ya viumbe vya Mwenyezi Mungu, namna ya kufuatana na kuamiliana na wanyonge masikini.
Alikuwa akiwakabili kwa bashasha na makaribisho na kuwambia: Assalamu alykum (Amani iwe juu yenu), Mola wenu amejilazimisha rehema, Na alikuwa akiifunga nafsi yake kukaa nao maadamu wako mpaka waondoke wao.
Ikiwa Mtume ndiye aliyekusudiwa na Mwenyezi Mungu kwa mafunzo haya, basi sisi ndio tuliokusudiwa kufuata nyayo zake. Usimtukuze yeyote kwa mali au jaha au jinsi na rangi. Isipokuwa tumheshimu na kumtukuza kwa dini na tabia nzuri.
Baadhi ya wafasiri wapya wanasema: "Maisha ya watu kabla ya Muhammad(s.a.w.w)
yalikuwa chini yenye kuwayawaya na Muhammad akayapandisha juu hadi kileleni; na hivi sasa yameondoka kwenye kilele kirefu na kuanguka huko New York, Washington na Chicago kwenye ubaguzi wa rangi."
Ndio! katika Usilam hakuna jinsia, rangi, jaha wala utajiri. Hakuna ubora katika Uislamu ila kwa takua. Kwa misingi hii ndipo inapopatikana siri ya kunyenyekea kwa wanavyuoni wa Kiislamu wanaofuatwa katika fatwa zao (marjaa). Mdogo na mkubwa anaweza kumfikia kwa njia ya usawa tu, bila ya kuweko bawabu au kizuizi na wanazungumza naye vile wanavyotaka na bila ya taklifu.
Ama baba mtakatifu (Papa) na wengineo katika viongozi wa dini, hakuna anayeota kukaa naye na kuzungumza naye ila waziri na wakubwa, tena amwekee wakati maalum na muda atakaozungumza naye.
Turudie kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: 'Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Assalamu alaykum (Amani iwe juu yenu), Mola wenu amejilazimisha rehema.'
Assalamu alaykum warahmatullah, (Amani na rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu).
Haya ndiyo maamkuzi ya Kiislam, kumwombea unayemwamkua kuokoka na kila maovu na aishi kwa amani na utulivu na kwa rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake, Kwani hakuna amani wala kuokoka ikiwa kuna ghadhabu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ama ukiongozea Wa barakatuh (na baraka zake), utakuwa umemwombea mwenzako riziki pana.
Wapi na wapi maamkuzi ya marahaba, sabalkher na 'good night' na maamkuzi haya ya Mungu ya Kiislamu? Imetangulia kauli yake Mwenyezi Mungu; amejilazimisha rehema katika Aya 12 ya Sura hii. Na tukaeleza katika Tafsir yake kuwa rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu haiepukani na dhati yake tukufu, sawa na uweza Wake na elimu Yake.
Ya kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea.
Kuhusu toba, tumeweka mlango mahsusi kwa anuani ya toba na maumbile, katika kufasiri Juz.4 (4:18).
Basi yeye ndiye mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
Huyu ndiye Mola tunayemwabudu, husamehe mwenye kutubia na hurehemu waja. Kila mwenye kuwahurumia watu na akafanya kazi kwa ajili ya utengenevu wao, basi atakuwa amemwabudu Mwenyezi Mungu katika matendo yake; hata kama atapinga kwa ulimi wake. Na kila mwenye kuwaingilia watu katika haki zao, basi atakuwa amemkufuru Mwenyezi Mungu kivitendo, hata kama ataleta takbira na tahlili.
Namna hii tunazieleza ishara na ili njia ya wakosefu ibainike.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Kitab chake sifa za watu wema, Vilevile ametaja sifa za wenye makosa ili lidhihirike kila kundi na alama yake. Zaidi ya hayo ni kwamba kujua moja ya vikundi viwili husababisha kujua kundi jingine; sawa na uongofu na upotevu.
﴿قُلْ إِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَعْبُدَ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ قُل لَّا أَتَّبِعُ أَهْوَاءَكُمْ قَدْ ضَلَلْتُ إِذًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُهْتَدِينَ﴾
56.Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu. Sema: Sifuati hawaa zenu, maana hapo nitapotea na sitakuwa miongoni mwa walioongoka. Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria njia ya wenye makosa, Katika Aya hii anaibainisha njia hiyo; kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
﴿قُلْ إِنِّي عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَكَذَّبْتُم بِهِ مَا عِندِي مَا تَسْتَعْجِلُونَ بِهِ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ يَقُصُّ الْحَقَّ وَهُوَ خَيْرُ الْفَاصِلِينَ﴾
57.Sema: Hakika mimi ninayo dalili wazi itokayo kwa Mola wangu, nanyi mmeikadhibisha. Mimi sina haraka kwa mnayoyataka. Hapana hukmu ila ya Mwenyezi Mungu. Anasimulia yaliyo kweli; naye ni mbora wa wanaohukumu.
﴿قُل لَّوْ أَنَّ عِندِي مَا تَسْتَعْجِلُونَ بِهِ لَقُضِيَ الْأَمْرُ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِالظَّالِمِينَ﴾
58.Sema: Lau ningelikuwa nayo mnayotaka haraka, basi shauri lingekwisha baina yangu. na baina yenu Na Mwenyezi Mungu anawajua zaidi madhalimu.
SIFUATI HAWAA ZENU
Aya 56-58
MAANA
Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria njia ya wenye makosa. Katika Aya hii anaibainisha njia hiyo; kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Sema: Sifuati hawaa zenu, maana hapo nitapotea na sitakuwa miongoni mwa walioongoka.
Kwa sababu kuomba kwao hakuna asili yoyote ila hawaa na upotevu, sasa vipi atafuata Mtume Mtukufu?
Sema:Hakika mimi ninayo dalili wazi itokayo kwa Mola wangu, nanyi mmeikadhibisha.
Yaani ninamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ujuzi na nyinyi mnamkanusha; na mnaabudu masanamu kwa ujinga, Kwa mantiki gani mjuzi amfuate mjinga? Na mwenye batili amwongoze mwenye haki?
Sina haraka kwa mnayoyataka.
Mtume alipowatolea mwito wa kuamini walisema: "Tuletee mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu kali."
Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha aseme: Sina haraka. Bali yako kwa Mwenyezi Mungu anaiteremsha wakati anaotaka wala mimi sina uwezo wa kuitanguliza au kuichelewesha.
Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu
katika kuteremsha adhabu na kuitanguliza au kuiahirisha.
Anasimulia yaliyo kweli.
Yaani anasema kweli:Naye ni mbora wa wanaohukumu, hadhulumu
yeyote katika hukumu yake.
Sema: Lau ningelikuwa nayo mnayotaka haraka katika adhabu, basi shauri lingekwisha baina yangu na baina yenu
kwa kuangamizwa mwenye kudhulumu katika nyinyi
Na Mwenyezi Mungu anawajua zaidi madhalimu.
Huharakisha au kuchelewesha adhabu kulingana na vile inavyopitisha hekima yake.