13
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SABA
﴿وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ قَالَ أُوحِيَ إِلَيَّ وَلَمْ يُوحَ إِلَيْهِ شَيْءٌ وَمَن قَالَ سَأُنزِلُ مِثْلَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ﴾
93.Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye uwongo Mwenyezi Mungu. Au mwenye kusema: Nimeletewa Wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote Na yule asemaye: Nitateremsha kama alivyoteremsha Mwenyezi Mungu. Na lau ungewaona madhalimu watakapokuwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamewanyooshea mikono. Zitoeni roho zenu; leo mtalipwa adhabu ifedheheshayo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyokuwa haki, na mlikuwa mkizifanyia kiburi ishara Zake.
﴿وَلَقَدْ جِئْتُمُونَا فُرَادَىٰ كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَتَرَكْتُم مَّا خَوَّلْنَاكُمْ وَرَاءَ ظُهُورِكُمْ وَمَا نَرَىٰ مَعَكُمْ شُفَعَاءَكُمُ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ أَنَّهُمْ فِيكُمْ شُرَكَاءُ لَقَد تَّقَطَّعَ بَيْنَكُمْ وَضَلَّ عَنكُم مَّا كُنتُمْ تَزْعُمُونَ﴾
94.Na hakika mtatujia wapweke kama tulivyowaumba kwanza. Na mmeacha nyuma yenu yale tuliyowapa. Na hatuwaoni waombezi wenu pamoja nanyi ambao mlidai ni washirika.
KUMZULIA UWONGO MWENYEZI MUNGU
Aya 93-94
MAANA
Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye uwongo Mwenyezi Mungu.
Kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo ni kumtengenezea mambo ambayo hayana chimbuko katika Qur’an wala Hadith au katika misingi ya akili. Na hayo yanakuwa kwa mambo yafuatayo:
• Kuhalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu au kuharamisha aliyoyahalalisha.
• Kumsingizia Mwenyezi Mungu, kwa makusudi, yale asiyokuwa nayo au kumfanyia washirika au kuwa ana watoto na mabinti.
• Kudai Utume kwa asiyekuwa Mtume. Hilo ameliashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kauli yake: Au mwenye kusema: Nimeletewa Wahyi; na hali hakuletewa Wahyi wowote. Jumla hii inaungana na ile ya ‘Amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo.’ Ni katika mlango wa kuunganisha mahsusi kwenye ujumla.
• Na yule asemaye: Nitateremsha kama alivyoteremsha Mwenyezi Mungu.Yaani mlaanifu huyu anadai kuwa ana uwezo wa kutunga Kitab kitakachofanana na Qur’an katika utukufu wake. Imesekana kuwa mtu huyo ni Abdullah bin Sa’d bin Abu Sarh. Wengine wamesema ni Nadhr bin Harith.
Kwa ufupi ni kwamba kila mwenye kumnasibishia Mwenyezi Mungu kitu chochote bila ya kutegemea kauli ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume au misingi ya akili basi huyo ni mzushi, mwongo mkubwa na anayestahiki shutuma na adhabu.
Na lau ungewaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamewanyooshea mikono.
Mahangaiko ya mauti ni maumivu ya kukata roho, Wafasiri wametofautiana katika makusudio ya kunyoosha mikono ya Malaika. Je, makusudio ni kunyoosha kiuhakika wakati mtu anapokata roho, au ni fumbo tu la kufananisha vituko vya mauti?
Sisi hatuoni haja yoyote ya mzozo huu, Kwa sababu akili haikatai kuweko Malaika wala kuwa na mikono wanaoinyoosha au ndimi za kuzungumzia. Kwani Wahyi umelieleza hilo, kwa hiyo ni wajibu kuamini. Msingi huu wanautegemea Maulama wote Waislamu katika kuthibitisha itikadi na sharia.
Zitoeni roho zenu; leo mtalipwa adhabu ifedheheshayo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkisema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyokuwa ya haki, na mlikuwa mkizifanyia kiburi ishara zake.
Haya yote ni maneno ya Malaika wakiwaambia wazushi wakati wa kufa. Nayo ni lawama na shutuma kwa uzushi wao na kukana kwao haki. Kuna Hadith isemayo: "Anayekufa kiyama chake kimesimama." Kwa sababu hii wamesema baadhi ya wajuzi kwamba mtu ana viyama viwili, kidogo ambacho ni mauti na kikubwa, ufufuo.
Shutuma za Malaika kwa anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, katika Kiyama kidogo, ni onyo la vituko vya Kiyama kikubwa atakavyokumbana navyo. Imam Ali anasema: "Kifo kwa Mumin ni kama kuvua nguo chafu na kufungua minyororo na kuvaa kanzu ya kifahari na kushukia kwenye maliwazo. Ama kwa kafiri, ni kama kuvua kanzu ya kifahari na kuvaa gwanda chafu, na kutoka kwenye maliwazo kwenda kwenye vitisho na adhabu kubwa."
Na hakika mtatujia wapweke kama tulivyowaumba kwanza.
Yaani mwanadamu atakutana na Mola wake kesho, kama alivyotoka tumboni mwa mamake hana chochote.
Afadhali angeliingia ardhini kama alivyotoka - haulizi wala haulizwi, lakini atarudi akiwa ni mwenye kuulizwa. Alhamdulilah, mwenye kuuliza ni mwadilifu hamdhulumu yeyote na atamfanyia mtu vile alivyowafanyia watu alipokuwa katika uhai wake wa kwanza. Ikiwa ni kheri basi itakuwa kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.
Wametofautiana wanavyuoni kuhusu kufufuliwa kuwa je, ni kwa roho tu, au ni kwa roho na kiwiliwili pamoja. Dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu: kama tulivyowaumba kwanza, inafahamisha kufufuliwa kwa roho na kiwiliwili kwa sababu vyote viwili vimeumbwa pamoja.
﴿كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ وَعْدًا عَلَيْنَا إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ﴾
"Kama tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena, Ni ahadi iliyo juu yetu, hakika sisi ni watendaji"
(21:104)
Na mmeacha nyuma yenu yale tuliyowapa.
Mtu atarudi ardhini akiwa ameacha watu wake, marafiki mali na ufalme.
Na hatuwaoni waombezi wenu pamoja nanyi ambao mlidai ni washirika (wa Mwenyezi Mungu) kwenu.
Kama vile masanamu, nyota na mengineyo mliyokuwa mkiyaabudu na kuwatawalisha wafisadi na wapotevu.
Kwa hakika yamekatika (mahusiano) baina yenu.
Yaani hamna mawasiliano yoyote ya duniani.
Na yamewapotea mliyokuwa mkidai
katika madai ya uwongo kwa wale mliowafikiria kuwa ni washirika au waombezi mbele yake, na yamepotea matumaini yenu baada ya kufichuka uhakika; na mwema ni yule atakayefuzu kupata radhi za Mwenyezi Mungu na maghufira yake.
﴿إِنَّ اللَّـهَ فَالِقُ الْحَبِّ وَالنَّوَىٰ يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَمُخْرِجُ الْمَيِّتِ مِنَ الْحَيِّ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ﴾
95.Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa. Humtoa aliye hai katika maiti na ni mtoaji wa maiti katika aliye hai. huyo ndiye Mwenyezi Mungu basi mnageuzwa wapi?
﴿فَالِقُ الْإِصْبَاحِ وَجَعَلَ اللَّيْلَ سَكَنًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ حُسْبَانًا ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ﴾
96.Ndiye mpambazuaji wa asubuhi; ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi (kwenda) kwa hesabu, Hayo ndiyo makadirio ya Mweye nguvu, Mjuzi.
﴿وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ النُّجُومَ لِتَهْتَدُوا بِهَا فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴾
97.Na yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaojua.
﴿وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ فَمُسْتَقَرٌّ وَمُسْتَوْدَعٌ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَفْقَهُونَ﴾
98.Na Yeye ndiye aliyewaanzisha nyinyi kutokana na nafsi moja. Pako mahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.
﴿وَهُوَ الَّذِي أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ نَبَاتَ كُلِّ شَيْءٍ فَأَخْرَجْنَا مِنْهُ خَضِرًا نُّخْرِجُ مِنْهُ حَبًّا مُّتَرَاكِبًا وَمِنَ النَّخْلِ مِن طَلْعِهَا قِنْوَانٌ دَانِيَةٌ وَجَنَّاتٍ مِّنْ أَعْنَابٍ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُشْتَبِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ انظُرُوا إِلَىٰ ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَيَنْعِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكُمْ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴾
99.Naye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo tunatoa mimimea ya kila kitu, Kisha tukatoa kutokana nayo kijani, Tukatoa ndani yake punje zilizopandana, Na katika mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo karibu. Na bustani za miza bibu na mizaituni na mikomamanga. Yanayofanana na yasiyofanana. Angalieni matunda yake yanapozaa na kuiva kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.
HUTOA ALIYE HAI KATIKA MAITI
Aya 95-99
MAANA
Katika Aya hizi kuna mifano ya ajabu katika viumbe ambavyo anayemiliki utengenezaji wake ni Mwenyezi Mungu peke yake. Vilevile kufahamisha kuwepo Mwenyezi Mungu na utukufu wake. Mifano imetajwa kwa mpango ufuatao:
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa.
Ukiweka mbegu ya ngano au kokwa ya tende katika ardhi itapasuka chini na juu. Upande wa chini itatoka mizizi na kushuka ardhini, na upande wa juu utatoka mti utakaorefuka hewani. Kisha ile mbegu au kokwa itapotea na mchanganyiko wote kuwa kitu kimoja, sehemu moja itakuwa ardhini na nyingine itakuwa kwenye hewa.
Hakuna mwenye shaka kwamba kazi yote hii inategemea sababu zake za kimaumbile; kama vile mchanga, maji, jua na hewa, lakini vyote hivyo vinaishia kwa Mwenyezi Mungu peke yake, kwa sababu yeye ndiye aliyeumba maumbile, msababishaji wa sababu na mpatishaji wa mada ya kwanza kwa neno 'Kuwa' na ikawa.
UHAI UMETOKA WAPI?
Humtoa aliye hai katika maiti na ni mtoaji wa maiti katika aliye hai.
Si ajabu kuzalika kitu hai kutoka kwa kilicho hai mfano wake; na kisicho na uhai kutoa kisicho na uhai. Vilevile chenye uhai kuzaa kisicho na uhai, au kinyume chake. Msemaji mmoja alisema: "Uhai unazalikana kutokana na nguvu ya asili ya maumbile." Tumwulize msemaji huyu:
Ni nani aliyeifanya ipatikane asili hiyo, nguvu zake na utendaji kazi wake? Ikiwa msukumano tu unatosha kuleta uhai bila ya kuweko msaada wa Mwenyezi Mungu, basi kwa nini wanasayansi wameshindwa kutengeneza uhai kama vile watengenezavyo vyombo vya jikoni na mengineyo; pamoja na kuwa wamejaribu wakaleta msukumano; lakni baada ya kukata tamaa walisema kwamba kutengeneza uhai ni kuzito kuliko kumrudisha mzee utotoni.
Hebu tuchukulie kuwa wao wanajiona watafaulu katika kutengeza chembehai, je, wamefaulu kutengeza mdudu mdogo tu?.
Tuache binadamu na ubongo wake na wanyama na maumbile yao ya ajabu na tupige mfano wa hawa wadudu tunaowaogopa na kupiga madawa kuwauwa. Baadhi ya wataalamu wa wadudu wanasema hivi: "Baadhi ya wadudu wanaishi katika nyuzi joto 50 chini ya sifuri; wengine wanaishi nyuzi joto hizi hizi juu ya sifuri, wengine katika hewa ya sumu na wengine katika visima vya mafuta, na wana utaratibu mzuri sana katika maisha yao na kazi zao."
Ikiwa mwanaadamu anaweza kugundua satalaiti, maroketi na akili za Elktroni, lakini hawezi kabisa kutengeza bawa la mbu au chembe moja ya mbawa zake. Akili ya binadamu ni kubwa lakini ukubwa wake ni wenye kuhemewa mbele ya uweza wa ajabu ulioumba mbu na chungu na nyuki!
Yote hayo yako wazi, Lakini msiba mkubwa ni kuwa tumejisahau, hatujiangalii sisi wenyewe na uwazi wa uweza wa Mwenyezi Mungu mwenye hekima. Kama tukiangalia tutazidi imani kwa kiwango kikubwa kwa muumba aliye mkubwa. Tunachohitajia ni imani na imani yetu inahitajia akili kwa sababu imani bila ya akili ni kama uso bila macho.
Ndiyo, tunahitaji kuamini uweza wa Mwenyezi Mungu ili tufasiri yale yaliyoshinda akili za mabingwa, ambazo zimeshindwa kufasiri maumbile ya uhai. Na wengi wenye akili hizo wanakimbilia kwenye kitu kilicho nyuma ya maumbile, Uwezo wenye hekima na ujuzi, wanaufasiri kwa kusema kuwa ni asili ya uhai,huyo ndiye Mwenyezi Mungu basi mmegeuzwa wapi?
Anaema Enstein: "Hakika uoni wetu wa kidini ndio unaloelekeza uoni wetu wa kielimu". Ustadh Tawfiq Al-Ahkim aliongeza katika kitabu chake Fannul-adab: 'Huku bila shaka ni kukiri dini. Hakuna mtaalamu yeyote katika waliopiata aliyesema kuhusu dini kama alivyosema huyu."
Nasi twaongeza juu ya kauli ya Al-Hakim, kwamba siri pekee ya kukubali wataalamu wa karne ya ishirini ni kuwa uoni wa dini ndio chimbuko la uoni wa kielimu, ni kuendelea kwa elimu katika karne hii na kuwa ilikuwa nyuma katika zama zilizopita. Kila inapopiga hatua elimu ndipo dini inapozidi kupata watetezi; kama Einstein anayekubali ukuu wa dini na kuamini kuwa ni haki ambayo haiingiliwi na batili mbele yake wala nyuma yake.
Ndiye mpambazuaji wa asubuhi; ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi (kwenda) kwa hesabu.
Mwenyezi Mngu (s.w.t) ametaja katika Aya zlizotangulia mifano ya utukufu wake kwa kupatikana uhai kwenye ardhi; na katika Aya hii ametaja mifano mitatu ya mbinguni:
Kwanza
: kuwa ameitoa asubuhi kwenye usiku, hilo ni fumbo la kupatikana mchana ambao watu wanahangaikia riziki na kupanga mambo yao.
Pili
: kwamba yeye Mwenyezi Mungu ameuleta usiku kwa ajli ya kutulia na kupumzika kutokana na machovu za kazi ya mchana kutwa.
Tatu
: kwamba ameweka Jua na Mwezi kwa kiasi mahsusi cha haraka na polepole kwa namna ambayo ardhi inakuwa na harakati mbili: Harakati za masaa 24, hisabu ya siku moja, na harakati za mwaka, ambazo ndani yake mna misimu mine ambayo ni hisabu ya mwaka mmoja. Mwenyezi Mngu (s.w.t) amesema:
﴿هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ﴾
"Yeye ndiye aliyelijaalia Jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu'
(10:5)
Utauliza
: kwa hiyo basi kupatikana usiku na mchana ni natija ya mzunguko wa ardhi , basi kuna wajihi gani wa kutegemeza kwa Mwenyezi Mungu?
Jibu
: kwa sababu yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi na kwake yeye ndio mwisho wa sababu zote , kwa hali yoyote ni kuwa makusudio ya kwanza ya kila yaliyokuja katika Aya hizi ni kuwa hakuna kitu katika vitu vya ulimwengu vilivyopatikana kwa sadfa na kibahati, isipokuwa kumetokana na aliye Mjuzi, Mwenye hekima aliyekipa kila kitu umbile lake na kukikadiria.
Hayo ndiyo makadirio ya weye nguvu, Mjuzi, Na Yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaojua.
Nyota hapa ni kutoa Jua na Mwezi kama inavyofahamika kutokana na mpangilio wa maneno. Katika kitabu Qur-an walilmul-hadith anasema bingwa wa falaki James Jentis: "Tunapotaka kujua nyumba fulani katika mji iko wapi tunauliza jina la mtaa kisha namba yake, basi ni hivyohivyo katika nyota, kwani katika hizo kuna zilizo maarufu kwa majina yake mahsusi nazo ni alama muhimu wanazozifuata mabaharia katika majahazi yao na waendeshao vyombo na wapanda wanyama. Ni misafara mingapi inyokwenda kwa ramani ya mbinguni na nyota wakati dira inapoacha kufanya kazi?"
Na Yeye ndiye aliyewaanzisha nyinyi kutokana na nafsi moja. Pako mahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.
Nafsi iliyoumbwa kila moja kutokana nayo ni mtu wa kwanza ambaye watu wote wametokana naye ambaye ni Adam.
Tumezungumzia kwa ufafanuzi tulipofasiri Juz.4 (4:1) Razi ametaja kauli sita katika kufasirimahali pa kutulia na pa kupita njia
.
Wafasiri wengi wamesema 'kutulia' ni kutulia manii katika migongo ya wanaume na 'pa kupita njia' kuwa katika matumbo ya uzazi ya wanawake. Katika Aya hakuna linalofahamisha hilo, wala lolote katika maana sita alizozinukuu Razi.
Imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq
kwamba: yeye amegawanya waumini katika mafungu mawili; mwenye kuamini imani ya kweli inayotulia mpaka kufa, ambaye maneno yake yanaafikiana na vitendo vyake, na mumini ambaye imani yake inalegalega iko kwa muda tu, inamwondoka kabla ya kufa; maneno yake yanatofautiana na vitendo vyake.
Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.
Na asiyefahamu dalili hizi za ulimwengu juu ya ukuu wa muumbaji, mwanzilishi, basi huyo ni katika wale waliokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ﴾
"Ni viziwi ni mabubu ni vipofu kwa hivyo hawafahamu"
(2:171)
Naye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo tunatoa mimea ya kila kitu.
Mvua ndio chimbuko la maji tamu, lau si hiyo ardhi ingelikuwa kame isiyo na uhai. Mwenyezi Mungu ametegemeza kushuka maji kwake yeye, kwa sababu yeye ndiye msababishaji wa sababu, kwake huanza kila kitu hata kama mzunguko utakuwa mrefu kiasi gani.
Kisha tukatoa kutokana nayo kijani.
Dhamiri ya 'nayo' inarudia kwenye mimea. Makusudio ya kijani ni ubichi, yaani kutokana na mmea huchipua matawi mabichi. Inasemekana kuwa maana ya kijani hapa ni ubichi zaidi.
Tukatoa ndani yake punje zilizopandana.
Dhamiri ya 'ndani yake' ni ndani ya hiyo kijani, yaani tunatoa mashuke katika matawi kama vile ya ngano nk, na kama mfano wa, tunda la komamanga ambalo tembe zake zinapandana.
Na katika mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo karibu.
Yaani ni rahisi kuyachuma au kuwa kukurubiana kwa wingi wake.
Na bustani za miabibu na mizaituni na mikomamanga.
Yaani tunatoa katika mimea aina hizi tatu. Mwenyezi Mungu amezitaja kwa njia ya kupigia mfano ambayo kutokana nazo itajulikana mingine.
Yanayofanana na yasiyofanana.
Katika mimea kuna inayofanana katika umbile na ladha na mingine haifananai.
Angalieni matunda yake yanapozaa na kuiva kwake.
Yaani zingatieni vipi linatoka tunda mwanzo, linakuwa dogo lisilo na manufaa kisha linabadilika badilika mpaka kuiva na kuwa na ladha tamu.
Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.
Makusudio ya wanaoamini siyo wale wanaoamini tu, bali ni wale wanaotikia mwito wa imani na kunufaika na dalili na hoja. Ama wenye nyoyo zilizofungwa wanazipita kama wanyama.
Kwa ufupi makusudio ya kwanza ya mifano hii ya ardhini na mbinguni ni kuleta uzindushi kuwa vitu vya ulimwengu huu na vilivyomo ndani yake vinatokana na uanzilishi na upangiliaji.
Ni muhali kuwa vimekuja kisadfa katika mtazamo wa kiakili na kimaumbile.
Hizo mbili zinahukumu kwa mkato kwamba kila liliopo limepatikana kwa matakwa na makusudio na kwa hekima ya hali ya juu anayoijua mjuzi na mjinga, wala hakuna kitu kinachobatilisha sadfa kama vile kukaririka tukio moja kila zinapokaririka sababu zake.