MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 46681
Pakua: 4315

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 46681 / Pakua: 4315
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

UTANGULIZI WA MTUMISHI WA SITE

Kitabu hichi kimeandikwa na wanachuoni wa Madhehebu ya Kisunni, kwa hiyo yaliomo ndani ya kitabu hichi ni masuala ya kielimu yanayoendana na Madhehebu hayo, hivyo basi wafuasi wa madhehebu mengine wanatakiwa kusoma ili kufaidika zaidi, na hapa hakuna lengo la kutoa ushawishi wa aina yeyote ile. Na lengo hasa la kuweka kitabu hichi ni kutaka ndugu zetu wa Kisunni nao waweke makala na vitabu vyetu katika site zao bila ya kuvutia upande wowote, jambo ambalo litawasaidia ndugu zetu wa Madhehebu mengine kuzielewa itikadi zetu bila ya chuki ya aina yeyeote, jambo ambalo litasaidia katika kueneza elimu na tamaduni za Kiislamu.

Asanteni sana.

Ngugu yenu:

SALIM SAID AL-RAJIHIY.

SURA YA KWANZA

MAANA YA ELIMU

Elimu ni ujuzi ulioambatanishwa na utendaji. Wanataaluma wamejitahidi kutoa maana ya elimu kuwa ni mabadiliko ya tabia yanayotokana na ujuzi. Kwa maana hii Elimu haiishii kwenye kuijua tu bali elimu hukamilika inapomwezesha mwenye kujua kutenda kwa ufanisi zaidi kuliko yule asiyejua.

Nani aliye elimika? Kutokana na maana ya elimu tuliyojifunza hapo juu, mtu aliyeelimika ni yule ambaye ujuzi alioupata humuwezesha kutenda kwa ufanisi zaidi kuliko pale alipokuwa hajapata ujuzi huo. Mtu aliyesoma hatachukuliwa tu kwa kirahisi kuwa kaelimika, bali kuelimika au kutoelimika kwake kutathibitika katika matendo na mwenendo wake wa kila siku. Matarajio ni kwamba mtu aliyesoma anapaswa aelimike kwa kutenda kwa ufanisi zaidi kuliko asiyesoma.

Na katika kuzingatia hili Allah (s.w) anatukumbusha katika Qur-an:

﴿قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ﴾

"...Sema, Je! wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu." (39:9)

Jibu la swali hili ni wazi. Mjuzi na asiyejua hawawezi kuwa sawa kiutendaji na kitabia. Endapo mtu atajiita msomi kwa kusoma vitabu vingi au kupewa shahada nyingi lakini kitabia na kiutendaji akawa hatofautiani na wale wasiosoma atakuwa bado hajaelimika na mfano wake ni ule unaopigwa katika Qur-an:

﴿مَثَلُ الَّذِينَ حُمِّلُوا التَّوْرَاةَ ثُمَّ لَمْ يَحْمِلُوهَا كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا بِئْسَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ﴾

"Mfano wa wale waliopewa Taurati kisha hawakuichukua (kwa kuitia katika matendo) ni kama punda aliyebeba (mzigo) wa vitabu vikubwa (bila ya kufaidika kwavyo) ni mbaya kabisa mfano wa watu waliokadhibisha aya za Mwenyezi Mungu.Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu." (62:5).

NAFASI YA ELIMU NA WENYE ELIMU KATIKA UISLAMU

Nafasi ya elimu na mwenye elimu katika uislamu inaonkana katika maeneo yafuatayo:

Kwanza: Elimu ndio takrima ya kwanza aliyokirimiwa mwanaadamu na Mola wake.

Tunajifunza katika Qur-an kuwa jambo la kwanza alilotunukiwa Adam(a.s) mara tu baada ya kuumbwa kwake ni kupewa elimu.

﴿وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا﴾

"Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha Adam majina ya vitu vyote..." (2:31).

katika aya hii inaashiria fani zote za elimu ambazo anahitajia mwanaadamu hapa duniani ili afikie kwa ufanisi lengo la kuumbwa kwake.

Pia tunajifunza katika Quran kuwa mwenye elimu na hekima amepewa kheri nyingi.

﴿يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَن يَشَاءُ وَمَن يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ﴾

(Mungu) humpa hikma amtakaye, na aliyepewa hikma bila shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili. (2.269).

KUTAFUTA ELIMU

Kutafuta elimu (kusoma) ni amri ya kwanza kwa mwanaadamu. Tunajifunza kutokana na historia ya kushushwa Qur-an kuwa Wahay wa kwanza kumshukia Mtume(s.a.w.w) ambao ndio ulimtawazisha rasmi kuwa mtume ni ule unaopatikana katika aya tano za mwanzo za Suratul-'Alaq:

﴿اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ ﴿١﴾ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ ﴿٢﴾ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ ﴿٣﴾ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ ﴿٤﴾ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ﴾

"Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba.Ambaye amemuumba mwanaadamu kwa 'Alaq (kitu chenye kuning'inia).Soma na Mola wako ni karimu sana. Ambaye amemfundisha mwanaadamu kwa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu (chungu ya) mambo aliyokuwa hayajui" . (96:1-5)

Kutokana na aya hizi, kwa muhtasari, tunajifunza yafuatayo:

1. Kusoma kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni jambo la kwanza waliloamrishwa wanaadamu na Mola wao.

2. Kusoma kwa jina la Mola wako ni kusoma kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu au ili kuweza kumwabudu Allah(s.w) inavyostahiki na kusimamisha Uislamu katika jamii.

3. Radhi za Mwenyezi Mungu zitapatikana pale mwanaadamu atakapoweza kufikia lengo la maisha yake la kumuabudu Allah (s.w) kwa kuzingatia maamrisho na mipaka ya Mwenyezi Mungu katika kila kipengele cha maisha.

4. Amri hii ya kusoma hailengi fani maalum tu ya elimu; bali kila fani itakayomuwezesha mwanaadamu kufikia lengo la maisha yake kwa ufanisi.

5. Chanzo au chimbuko la fani zote za elimu ni Allah (s.w). Hivyo kwa Muislam mlango wa kwanza wa elimu ni kusoma kwa mazingatio Qur-an na hadithi sahihi za Mtume(s.a.w.w) na kusoma maarifa ya Uislamu kwa ujumla kutokana na vyanzo hivi viwili.

KWANINI UISLAMU UMEIPA ELIMU NAFASI YA KWANZA?

Elimu imepewa nafasi ya kwanza katika Uislam kwa sababu zifuatazo:

Kwanza : elimu ndio nyenzo pekee inayomuwezesha mwanaadamu kumtambua Mola wake vilivyo na kumuabudu ipasavyo kwa unyenyekevu kama Qur-an inavyothibitisha:

﴿ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴾

"...Kwa hakika wanaomuogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalam (waliozama katika fani mbali mbali)" (35:28).

Pili : elimu iliyosomwa kwa mrengo wa Qur-an ndio nyenzo pekee inayomuwezesha mwanaadamu kuwa Khalifa wa Allah (s.w) hapa Ulimwenguni. Khalifa ni mja anayetawala ulimwengu kwa niaba ya Allah (s.w) kwa kufuata kanuni na sheria zake. Nabii Adam(a.s) aliwathibitishia Malaika kuwa ana uwezo wa kuutawala ulimwengu kwa niaba ya Allah (s.w) baada ya kuelimishwa fani zote za elimu (majina ya vitu vyote) na kuahidiwa mwongozo kutoka kwa Allah (s.w).

Tatu : kutafuta elimu ni Ibada maalumu ya hali ya juu kuliko Ibada zote. Kwa mujibu wa Qur-an Swala ni Ibada maalumu ya hali ya juu na ni dhikri kubwa au zingatio kubwa juu ya Allah (s.w):

﴿ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ﴾

"Hakika swala humzuilia (mja) na mambo machafu na maovu na ni dhikri kubwa kwa Allah (s.w)" (29:45).

Pia katika Hadith Mtume(s.a.w.w) amesisitiza:

"Nguzo kubwa ya Dini (Uislamu) ni swala, mwenye kusimamisha swala kasimamisha Dini na mwenye kuacha swala kavunja Dini."

Hivyo kwa mujibu wa Qur-an na Hadith sahihi za Mtume(s.a.w.w) , swala ni Ibada yenye hadhi ya juu kuliko Ibada zote mbele ya Allah (s.w); lakini bado Ibada ya kutafuta elimu inachukuwa nafasi ya juu zaidi kuliko swala kwani swala haiwezi kusimama bila ya kuwa na ujuzi stahiki. Nne, mwenye elimu ananafasi bora ya kumuabudu Mola wake inavyostahiki katika kila kipengele cha maisha yake kama inavyosisitizwa katika Qur-an:

﴿ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴾

"... Kwa hakika wanaomuogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalamu" (35:28)

Pia Qur-an inasisitiza juu ya umuhimu wa elimu kwa kuuliza:

﴿قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ﴾

"Je,waweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu." (39:9)

Kimsingi wanaojua wanatarajiwa wafanye mambo kwa ufanisi zaidi kuliko wasiojua. Kwa msingi huu Allah (s.w) anasisitiza tena katika aya ifuatayo:

﴿يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴾

"Mwenyezi Mungu atawainua (daraja) wale walioamini miongoni mwenu, na waliopewa elimu watapata daraja zaidi. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda yote" (58:11)

Hivyo, kutokana na aya hizi (35:28, 39:9 na 58:11) tunajifunza kuwa; waumini wenye elimu wana daraja zaidi kuliko waumini wengine kwa sababu wanao uwezo zaidi wa kuona dalili za kuwepo Allah (s.w) na utukufu wake kwa undani zaidi, jambo ambalo huwapelekea kumuogopa Mola wao na kumuabudu inavyostahiki katika kukiendea kila kipengele cha maisha yao kama inavyobainika katika aya zifuatazo:

﴿إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴾

"Katika kuumbwa mbingu na ardhi na mfuatano wa usiku na mchana, ziko hoja (za kuonesha kuwepo Allah (s.w) kwa wenye akili (3:190)

Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima, wakiwa wamekaa na wakiwa wamelala. Na hufikiri (tena) umbo la mbingu na ardhi (wakasema) Mola wetu! Hukuviumba hivi burebure tu. Utukufu ni wako. Basi tuepushe na adhabu ya moto." (3:191).

Pia kutokana na aya hizo tunajifunza kuwa waumini wenye elimu wanao uwezo mkubwa wa kufanya mambo kwa ufanisi, jambo litakalowapelekea kusimamisha ukhalifa wa Allah (s.w) katika jamii.

CHANZO CHA ELIMU

Chanzo cha Elimu ni Allah (s.w) Kama tunavyojifunza katika surat 'Alaq (96:4-5), chanzo cha elimu au mkufunzi wa binadamu ni Allah (s.w). Allah (s.w) huwasiliana na binadamu na kuwaelimisha kwa kutumia mojawapo ya njia zifuatazo zilizoainishwa katika aya ifuatayo:

﴿ وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ ﴾

"Na haikuwa kwa mtu kwamba Mwenyezi Mungu anasema naye ila kwa il-hamu (anayetiwa moyoni mwake) au kwa nyuma ya pazia au humtuma mjumbe (Malaika) naye humfunulia kiasi anachotaka kwa idhini yake (Allah), bila shaka yeye ndiye aliye juu mwenye hekima." (42:51).

Aya hii inatufahamisha kuwa binaadamu hupata habari kutoka kwa Allah (s.w) kwa njia tatu zifuatazo:

(a) Il-hamu (Intution).

(b) Nyuma ya pazia.

(c) Kutumwa Malaika na kufikisha ujumbe kama alivyotumwa. Pia katika Qur-an tunafahamishwa njia mbili nyingine anazozitumia Allah (s.w) katika kumfikishia binaadamu ujumbe kutoka kwake:

(d) Ndoto za kweli (ndoto za Mitume).

(e) Maandishi (mbao zilizoandikwa tayari).

(a) Il-hamu.

Ni mtiririko wa habari au ujumbe unaomjia mwanaadamu bila ya kufundishwa na mtu yeyote au kuona mfano wake katika mazingira yoyote. Mambo mengi mwanaadamu huyafahamu kwa Il-hamu. Wagunduzi wa fani mbali mbali za elimu kama vile Hisabati, Fizikia, Jiografia, n.k. na Wavumbuzi wa vitu mbali mbali katika taaluma mbali mbali za kisayansi wameweza kufanya hivyo kwa kupata Il-hamu kutoka kwa Allah. Hivyo hakuna fani yoyote ya elimu isiyotoka kwa Allah (s.w).

﴿عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ ﴾

"Amemfundisha mwaanadamu mambo yote aliyokuwa hayajui" (96:5)

(b) Kuongea na Allah (s.w) nyuma ya Pazia Hii ni njia ambayo mwanaadamu huongeleshwa moja kwa moja na Allah (s.w) kwa sauti ya kawaida pasina kumuona. Kutokana na ushahidi wa Qur-an njia hii imetumika kwa Mitume na wateule wengine wa Allah (s.w).

Nabii Mussa(a.s) ni miongoni mwa Mitume waliosemeshwa na Allah (s.w).kama tunavyofahamishwa kisa chake katika Qur-an:

﴿فَلَمَّا قَضَىٰ مُوسَى الْأَجَلَ وَسَارَ بِأَهْلِهِ آنَسَ مِن جَانِبِ الطُّورِ نَارًا قَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا لَّعَلِّي آتِيكُم مِّنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ جَذْوَةٍ مِّنَ النَّارِ لَعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ ﴿٢٩﴾ فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ مِن شَاطِئِ الْوَادِ الْأَيْمَنِ فِي الْبُقْعَةِ الْمُبَارَكَةِ مِنَ الشَّجَرَةِ أَن يَا مُوسَىٰ إِنِّي أَنَا اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ﴾

Basi Musa alipotimiza muda, akasafiri pamoja na ahali zake (watu wake kurejea kwao Misri). Aliona moto upande wa mlimani akawaambia ahali zake; 'Ngojeni, hakika nimeona moto, labda nitakuleteeni habari za huko au kijinga cha moto ili muote! (28:29) Basi alipoufikia aliitwa kutoka upande wa kuliani wa bonde hilo katika kiwanja kilichobarikiwa, kutoka mtini: "Ewe Mussa! Bila shaka mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu." (28:30)

Kwa njia ya nyuma ya pazia, Nabii Mussa(a.s) aliongea na Allah mara nyingi na mara zote hizo hakuweza kumuona. Alipoomba amuone alijibiwa kama inavyooneshwa katika aya zifuatazo:

﴿وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ﴾

Na alipofika Mussa katika miadi yetu na Mola wake akazungumza naye, (Mussa) akasema: "Mola wangu! Nionyeshe (nafsi yako) ili nikuone" Akasema (Mwenyezi Mungu): "Hutaniona, lakini tazama jabali (lililoko mbele yako) kama litakaa mahali pake utaweza kuniona".

Basi Mola wake alipojionyesha katika jabali, alilifanya liwe lenye kuvunjika vunjika na Mussa akaanguka hali ya kuzimia. Alipozindukana akasema "Utukufu ni wako.Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa wanaoamini (haya)" (7:143).

Pia tunafahamishwa katika Qur-an kuwa Bibi Maryam, mama wa Nabii Issa(a.s) naye aliongeleshwa nyuma ya pazia wakati wa kumzaa Issa Bin Maryamu kama ilivyo katika aya zifuatazo:

﴿فَأَجَاءَهَا الْمَخَاضُ إِلَىٰ جِذْعِ النَّخْلَةِ قَالَتْ يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَـٰذَا وَكُنتُ نَسْيًا مَّنسِيًّا ﴿٢٣﴾ فَنَادَاهَا مِن تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا ﴿٢٤﴾ وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا ﴿٢٥﴾فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا﴾

"Kisha uchungu ukampeleka katika shina la mtende, (akawa anazaa na huku) anasema:"Laiti ningelikufa kabla ya haya, na ningekuwa niliyesahaulika kabisa.Mara ikamfikia sauti kutoka chini yake ikamwambia usihuzunike.Hakika Mola wako amejaalia kijito cha maji chini yako.na litikise kwako shina la mtende, litakuangushia tende nzuri, zilizo mbivu. Basi ule na unywe na litulie jicho (lako). Na kama ukimuona mtu yeyote (akauliza habari juu ya mtoto huyu), sema:"Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa Rehma ya kufunga, kwa hiyo leo sitasema na mtu" (19:23 - 26).

(c) Kuletewa Ujumbe na Malaika kutoka kwa Allah (s.w) Kutuma ujumbe wa Malaika ni njia nyingine anayoitumia Allah (s.w) katika kuwaelimisha wanaadamu hasa katika mambo ya msingi ya maisha ya mwanaadamu hapa ulimwenguni. Hii ni njia maalum aliyoitumia Allah katika kuwasiliana na Mitume na miongoni mwa watu wengine wema. Kuhusu jinsi Mtume(s.a.w.w) aliyofundishwa na Allah (s.w) tunafahamishwa katika aya zifuatazo:

﴿وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ ﴿١﴾ مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ ﴿٢﴾ وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾ عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ﴿٥﴾ ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ ﴿٦﴾ وَهُوَ بِالْأُفُقِ الْأَعْلَىٰ ﴿٧﴾ ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ ﴿٨﴾ فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ أَوْ أَدْنَىٰ ﴿٩﴾ فَأَوْحَىٰ إِلَىٰ عَبْدِهِ مَا أَوْحَىٰ ﴿١٠﴾ مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ ﴿١١﴾ أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ﴾

Naapa kwa nyota zinapoanguka.(Zinapokuchwa). Kwamba mtu wenu (huyu Muhammad) hakupotea kwa ujinga wala hakukosa. (na hali ya kuwa anajua); wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake. Hayakuwa haya (anayosema) ila ni wahyi (ufunuo). Uliofunuliwa (kwake).Amemfundisha (malaika) mwenye nguvu sana mwenye uweza. Na yeye yu katika upeo wa kuona (Horizon) katika mbingu kwa juu kabisa. Kisha (ukaribu wao) ni kama baina ya upinde na upinde au karibu zaidi. Na akamfunulia huyo Mtumwa wake (Mwenyezi Mungu) aliyoyafunua. Moyo haukusema uwongo uliyoyaona.(Moyo wake ulisadikisha haya yaliyotokea). Je! Mnabishana naye juu ya yale anayoyaona (daima)? (53:1-12).

Katika mafunzo ya Qur-an na Hadithi tunafahamishwa kuwa malaika Jibril ndiye malaika mkuu aliyehusika na kupeleka ujumbe kwa Mitume wa Allah (s.w). Lakini pia kutokana na aya za Qur-an sio yeye pekee aliyehusika tu na kupeleka ujumbe wa Allah kwa Mitume bali wajumbe wengine pia walihusika. Katika aya zifuatazo tunafahamishwa juu ya wageni (wajumbe) wa Nabii Ibrahim(a.s) ,waliomletea habari njema ya kumpata mtoto Is-haqa na habari ya kuhuzunisha ya kuangamizwa kwa watu waovu wa Kaumu ya Lut(a.s) aliyekuwa mpwawe:

﴿وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ ﴿٥١﴾ذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿٥٢﴾ قَالُوا لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ ﴿٥٣﴾ قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَىٰ أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ ﴿٥٤﴾ قَالُوا بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ ﴿٥٥﴾ قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ﴿٥٦﴾ قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿٥٧﴾ قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿٥٨﴾ إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥٩﴾ إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٦٠﴾ فَلَمَّا جَاءَ آلَ لُوطٍ الْمُرْسَلُونَ ﴿٦١﴾ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ ﴿٦٢﴾ قَالُوا بَلْ جِئْنَاكَ بِمَا كَانُوا فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٦٣﴾ وَأَتَيْنَاكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٦٤﴾ فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَاتَّبِعْ أَدْبَارَهُمْ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ وَامْضُوا حَيْثُ تُؤْمَرُونَ ﴿٦٥﴾ وَقَضَيْنَا إِلَيْهِ ذَٰلِكَ الْأَمْرَ أَنَّ دَابِرَ هَـٰؤُلَاءِ مَقْطُوعٌ مُّصْبِحِينَ﴾

"Na uwaambie khabari za wageni wa (Nabii) Ibrahim. Walipoingia kwake na wakasema:"Salaam" (Salaamun Alaykum, akawajibu; kisha) akasema (alipoona wamekataa kula chakula alichowawekea). "Kwa hakika sisi tunakuogopeni".Wakasema: "Usituogope, Sisi tunakupa khabari njema ya (kuwa utazaa) mtoto mwenye ilimu kubwa".Akasema: "Oh! Mnanipa khabari hii, na hali ya kuwa uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanipa khabari njema hiyo? Wakasema: Tumekupa khabari njema iliyo haki: basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa. Akasema: "Na nani anayekata tamaa ya rehema ya Mola isipokuwa wale waliopotea? Akasema: (Tena) kusudi lenu (jingine) ni nini enyi mliotumwa?" Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa wale watu wakosaji (tukawaangamize).(watu wa Nabii Lut.)Isipokuwa waliomfuata Lut.Bila shaka sisi tutawaokoa wote hao (waliomfuata Lut)Isipokuwa mkewe.Tunapimia ya kuwa atakuwa miongoni mwa watakaokaa nyuma (waangamizwe).Basi wajumbe walipofika kwa watu wa Lut (kwa sura za kibinaadamu). (Lut) alisema:"Hakika nyinyi ni watu msiojulikana (na mimi; sikujueni)". Wakasema:"Basi sisi tumekuletea yale ambayo walikuwa wanayafanyia shaka, (nayo ni maangamizo yao).Na tumefika kwako kwa (hilo jambo la) haki (la kuangamizwa) na hakika sisi ni wenye kusema kweli. Basi ondoka na watu wako katika kipande cha usiku (pingapinga la usiku), na wewe ufuate nyuma yao; wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma (na mwende upesi upesi) mnakoamrishwa.Na tukamkatia (Nabii Luti) jambo hili; la kwamba mizizi yao itakatwa asubuhi (yaani wataangamiziliwa mbali asubuhi)" (15: 51-66).

Zakaria(a.s) mlezi wa Maryamu mama wa Nabii Issa(a.s) aliletewa habari na malaika ya kumzaa Yahya(a.s) kama tunavyofahamishwa katika aya zifuatazo:

﴿هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾ فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٣٩﴾ قَالَ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَقَدْ بَلَغَنِيَ الْكِبَرُ وَامْرَأَتِي عَاقِرٌ قَالَ كَذَٰلِكَ اللَّـهُ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ﴿٤٠﴾ قَالَ رَبِّ اجْعَل لِّي آيَةً قَالَ آيَتُكَ أَلَّا تُكَلِّمَ النَّاسَ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ إِلَّا رَمْزًا وَاذْكُر رَّبَّكَ كَثِيرًا وَسَبِّحْ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ﴾

Pale pale Zakaria akamwomba Mola wake, akasema: "Mola wangu! Nipe kutoka kwako mtoto mwema.Wewe ndiye usikiaye maombi (ya wanaokuomba).Mara Malaika wakamlingania hali amesimama akiswali chumbani, kwamba Mwenyezi Mungu anakupa khabari njema za (kuwa utazaa mtoto; umwite) Yahya, atakayekuwa mwenye kumsadikisha (Mtume atakayezaliwa) kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu (Naye ni Nabii Issa) na atakayekuwa bwana kabisa na mtawa na Nabii anayetokana na watu wema (Nao ni nyinyi). Akasema (Zakaria): "Mola wangu! Nitapataje mtoto, na hali uzee umenifikia,na mke wangu ni tasa?" Akasema (Mwenyezi Mungu),Ndiyo vivyo hivyo; Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo)". Akasema:Mola wangu! Niwekee alama (ya kunitambulisha kuwa mke wangu kishashika mimba nipate kufurahi upesi).Akasema: Alama yako ni kuwa hutaweza kusema na watu kwa siku tatu isipokuwa kwa ishara tu. Na mtaje Mola wako kwa wingi na umtukuze (kwa kuswali) wakati wa jioni na asubuhi" (3:38 - 41)

Pia Bibi Maryamu aliletewa ujumbe na malaika kutoka kwa Allah kama inavyodhihirika katika aya zifuatazo:

﴿ وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مَرْيَمَ إِذِ انتَبَذَتْ مِنْ أَهْلِهَا مَكَانًا شَرْقِيًّا ﴿١٦﴾ فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا ﴿١٧﴾ قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا ﴿١٨﴾ قَالَ إِنَّمَا أَنَا رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَامًا زَكِيًّا﴾

"Na mtaje Maryamu Kitabuni (humu).Alipojitenga na jamaa zake, (akaenda) mahali upande wa mashariki (wa msikiti).Na akaweka pazia kujikinga nao.Tukampelekea Muhuisha Sharia yetu (Jibrili) - akajimithilisha kwake (kwa sura ya) binaadamu aliye kamili. (Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema (Aniepushe) nawe.Ikiwa unamuogopa Mungu (basi ondoka nenda zako). (Malaika) akasema: Hakika mimi ni Mjumbe wa Mola wako: ili nikupe mwana mtakatifu" (19:16-19).

Pamoja na Malaika kuleta ujumbe kwa Mitume na miongoni mwa watu wema, pia kuna Malaika waliokuja kufundisha elimu ya uchawi kama sehemu ya mtihani kwa wanaadamu. Malaika waliotumwa na Allah kufundisha uchawi kama mtihani kwetu ni Haruta na Maruta kama inavyobainishwa katika Qur-an:

﴿وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ﴾

Wakafuata yale waliyoyafuata mashetani, (wakadai kuwa yalikuwa) katika ufalme wa (Nabii) Suleiman, na Suleiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru,wakiwafundisha watu uchawi na (uchawi) ulioteremshwa kwa Malaika wawili, Haruta na Maruta, katika (mji wa) Babil. Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: "Hakika sisi ni mtihani (wa kutazamwa kutii kwenu); basi usikufuru". Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo hayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe (na mengineyo). Wala hawakuwa wenye kumdhuru yoyote kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa. Na kwa yakini wanajua kwamba aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika akhera.Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia (starehe za) nafsi zao (za akhera).Laiti wangalijua,(hakika wasingefanya hivi)". (2:102).

Aya hii inazidi kututhibitishia kuwa hapana chochote ambacho anakijua mwanaadamu ila itakuwa amefundishwa na Allah (s.w).

(d) Ndoto za kweli Njia nyingine ya kupata ujumbe kutoka kwa Allah ni njia ya ndoto za kweli. Historia inatuonyesha kuwa ndoto za Mitume daima zilikuwa zikitokea kweli; kwa hiyo ulikuwa ni ujumbe moja kwa moja kutoka kwa Allah (s.w). Ndio maana Nabii Ibrahim(a.s) alipoota kuwa anamchinja mwanawe, hakusita kutekeleza hilo kwa kuwa yeye na mtoto wake Ismail(a.s) walikuwa na uhakika kuwa ni amri kutoka kwa Allah kama inavyobaini katika Aya ifuatayo:

﴿فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ﴾

"Ewe mwanangu!Hakika nimeona katika ndoto ya kwamba ninakuchinja.Basi fikiri, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Fanya unayoamrishwa, utanikuta Insha-Allah miongoni mwa wanao subiri" (37:102)

Kutokea kweli kwa ndoto ya Nabii Yusuf(a.s) kama inavyobainishwa katika Qur-an ni miongoni mwa ushahidi kuwa ndoto za Mitume ni ujumbe wa kweli na wa moja kwa moja (kama ndoto yenyewe ilivyo) kutoka kwa Allah (s.w). Hebu turejee kisa cha ndoto ya Nabii Yusuf(a.s) katika aya zifuatazo:

﴿إِذْ قَالَ يُوسُفُ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ إِنِّي رَأَيْتُ أَحَدَ عَشَرَ كَوْكَبًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ رَأَيْتُهُمْ لِي سَاجِدِينَ ﴿٤﴾قَالَ يَا بُنَيَّ لَا تَقْصُصْ رُؤْيَاكَ عَلَىٰ إِخْوَتِكَ فَيَكِيدُوا لَكَ كَيْدًا إِنَّ الشَّيْطَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوٌّ مُّبِينٌ﴾

"Kumbuka Yusuf alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Hakika nimeona katika ndoto nyota kumi na moja na jua na mwezi. Nimeviona vyote hivi vinanisujudia.Akasema (babaake): Ewe mwanangu! Usiwasimulie ndoto yako (hii) nduguzo wasije wakakufanyia vitimbi (kwa ajili ya husda itakayowapanda). Hakika shetani kwa mwanaadamu ni adui aliye dhahiri (atawatia uchungu tu). (12:4 - 5)

Kutokea kweli kwa ndoto hii kunabainishwa katika aya ifuatayo:

﴿فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَبَوَيْهِ وَقَالَ ادْخُلُوا مِصْرَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ ﴿٩٩﴾ وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا وَقَالَ يَا أَبَتِ هَـٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا وَقَدْ أَحْسَنَ بِي إِذْ أَخْرَجَنِي مِنَ السِّجْنِ وَجَاءَ بِكُم مِّنَ الْبَدْوِ مِن بَعْدِ أَن نَّزَغَ الشَّيْطَانُ بَيْنِي وَبَيْنَ إِخْوَتِي إِنَّ رَبِّي لَطِيفٌ لِّمَا يَشَاءُ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ﴾

"Na walipoingia kwa Yusuf, aliwainua wazazi wake na kuwaweka katika kiti (chake) cha ufalme.Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na (Yusuf) akasema: "Ewe babaangu!Hii ndiyo (tafsiri) hakika ya ndoto yangu ya zamani.Bila shaka Mola wangu ameihakikisha. Na amenifanyia ihsani akanitoa gerezani na akakuleteni nyinyi kutoka jangwani; baada ya shetani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni mwenye kulifikia alitakalo. Bila shaka yeye ni mjuzi na mwenye hikima" (12: - 10).

Kutokea kweli kwa ndoto ya Mtume(s.a.w.w) kuwa Waislamu watangia Makka kuhiji kwa salama bila ya kuzuiliwa na mtu yeyote. Ndoto hii ilitokea kweli kama tunavyofahamishwa katika aya ifuatayo:

﴿ لَّقَدْ صَدَقَ اللَّـهُ رَسُولَهُ الرُّؤْيَا بِالْحَقِّ لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ فَعَلِمَ مَا لَمْ تَعْلَمُوا فَجَعَلَ مِن دُونِ ذَٰلِكَ فَتْحًا قَرِيبًا﴾

Kwa yakini Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ndoto yake ya haki.Bila shaka nyinyi mtaingia katika Msikiti Mtukufu Insha-Allah kwa salama; mkinyoa vichwa vyenu na mkipunguza nywele (kama ilivyowajibu kufanya hivyo wakati wa Hija).Hamtakuwa na khofu.Na (Mwenyezi Mungu) anajua msiyoyajua.Basi kabla ya haya atakupeni kushinda kuliko karibu. (48:27).

(e) Njia ya Maandishi: Njia nyingine anayoitumia Allah (s.w) katika kuwasiliana na waja wake ni njia ya maandishi, yaani maandishi yaliyoandikwa tayari. Nabii Mussa(a.s) aliletewa ujumbe kutoka kwa Allah (s.w) kwa maandishi yaliyoandikwa tayari katika mbao kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo: "Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha (ya kila namna) na maelezo ya kila jambo.

﴿ فَخُذْهَا بِقُوَّةٍ وَأْمُرْ قَوْمَكَ يَأْخُذُوا بِأَحْسَنِهَا﴾

"Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako wayashike vema haya" (7:145)

﴿وَلَمَّا سَكَتَ عَن مُّوسَى الْغَضَبُ أَخَذَ الْأَلْوَاحَ وَفِي نُسْخَتِهَا هُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ هُمْ لِرَبِّهِمْ يَرْهَبُونَ﴾

"Na Musa zilipotulia ghadhabu zake, aliziokota zile mbao.Na katika maandiko yake (hizo mbao) ulikuwamo uwongofu na rehema kwa wale wanaomuogopa Mola wao" (7:154).

Kwa ujumla tumeona kuwa chanzo cha elimu ni "Allah (s.w). Lolote tunalolifahamu tumefunzwa na Allah kwa njia mojawapo katika njia tano tulizoziona.