MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU 0%

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU Mwandishi:
Kundi: Vitabu mbali mbali

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi: NDUGU ZETU WA KISUNNI
Kundi:

Matembeleo: 46673
Pakua: 4315

Maelezo zaidi:

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 22 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 46673 / Pakua: 4315
Kiwango Kiwango Kiwango
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

Mwandishi:
Swahili

1

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU

KATIKA UISLAMU HAKUNA ELIMU YA DINI NA DUNIA

Makafiri na hata baadhi ya Waislamu kutokana na mtazamo wao finyu juu ya maana ya dini iliyowapelekea kuyagawanya maisha ya binaadamu kwenye matapo mawili; maisha ya dini na maisha ya dunia, wameigawanya elimu kwenye matapo hayo mawili. Kwa mtazamo huu potofu elimu ya dini ni ile inayoshughulikia maswala ya kiroho (spiritual life) ya mtu binafsi inayoishia katika kumuwezesha mtu kuswali, kufunga na kutekeleza Ibada nyingine maalumu kama hizi bila ya kuzihusisha na maisha yake ya kila siku ya kibinafsi, kifamilia na kijamii.Hivyo elimu hii haina nafasi ya kumuwezesha binaadamu kuendea maisha yake ya kila siku ya kijamii.

ELIMU YA DUNIA

Elimu ya Dunia kwa mtazamo huu wa makafiri, ni ile inayojishughulisha na masuala ya kijamii kama vile uchumi, siasa, utamaduni, sheria na maongozi ya jamii kwa ujumla kwa kufuata maelekezo na matashi ya binaadamu bila ya kuzingatia mwongozo wa Allah (s.w). Kwa mtazamo wa mgawanyo huu, elimu ya dini ndiyo iliyofundishwa na Allah (s.w) kupitia kwa Mitume na Vitabu vyake na elimu ya dunia imebuniwa na binaadamu wenyewe kwa msukumo wa matashi na mahitaji yao katika kuendea kila kipengele cha maisha yao ya kimaada (Physical or Material life). Kwa mtazamo wa Uislamu (Qur-an na Sunnah) hapana mgawanyo huu wa elimu kwa sababu za msingi zifuatazo: Kwanza, Nabii Adam(a.s) katika kuandaliwa yeye na kikazi chake kuwa Makhalifa wa Allah (s.w) hapa ulimwenguni alifundishwa majina ya vitu vyote kama Qur-an inavyoainisha:

﴿وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا﴾

"Na (Mwenyezi Mungu) akamfundisha Adam majina ya vitu vyote" (2:31)

Majina ya vitu vyote hapa kama tulivyotangulia kusema inaashiria fani zote za elimu zitakazomuwezesha binaadamu kuendea kila kipengele cha maisha yake na kufikia malengo tarajiwa. Pamoja na kufundishwa majina ya vitu vyote, p ia Adam(a.s) na kizazi chake waliahidiwa na Mola wao kuletewa mwongozo utakaowawezesha kutumia fani mbali mbali za taaluma walizonazo kwa kufuata utaratibu utakaowapelekea kukiendea kila kipengele cha maisha yao kwa furaha na amani:

﴿قُلْنَا اهْبِطُوا مِنْهَا جَمِيعًا فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾

"Tukasema: Shukeni humo nyote; na kama ukikufikieni uwongozi utokao kwangu, basi watakaofuata uwongozi wangu huo, haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika." (2:38).

Lakini wale watakaotumia taaluma mbali mbali walizonazo katika kuendea kila kipengele cha maisha yao ya kila siku ya kibinafsi na kijamii bila ya kufuata mwongozo wa Allah (s.w) kupitia kwa Mitume wake na Vitabu vyake, wataishi maisha ya huzuni na khofu na katika maisha ya akhera watakuwa na adhabu kali:

﴿وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

"Lakini wenye kukufuru na kuyakadhibisha maneno yetu, hao ndio watakaokuwa watu wa motoni, humo watakaa milele" (2:39)

Kwa mujibu wa maelezo haya tunajifunza kuwa fani zote za elimu (majina ya vitu vyote) ambazo amezifundisha Allah (s.w) pamoja na mwongozo maalumu kutoka kwake, vinahitajika kwa binaadamu ili kumuwezesha kuishi maisha ya furaha na amani hapa duniani na huko akhera. Hivyo hapana mwenye uwezo wa kutenganisha maisha ya dini na dunia au elimu ya dini na dunia.

Pili : Amri ya kusoma (kutafuta elimu) aliyopewa Mtume(s.a.w.w) na umma wake, haibagui elimu ya dini na dunia.

Vinginevyo fani yoyote ya elimu inayomuwezesha binaadamu kusimamisha ukhalifa wa Allah (s.w) katika jamii na kufikia lengo la kuumbwa la kumuabudu Allah (s.w) inavyostahiki katika kila kipengele cha maisha yake inapaswa isomwe kwa juhudi zote.

Tatu : chanzo cha fani zote za elimu ni Allah (s.w) kama Qur-an inavyosisitiza:

﴿اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ ﴿٣﴾ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ ﴿٤﴾ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ﴾

"Soma na Mola wako ni karimu sana.Ambaye amemfundisha (Binaadamu fani zote za elimu) kwa msaada wa kalamu.Amemfundisha mwanaadamu (chungu ya mambo) aliyokuwa hayajui". (96:3-5)

Kwa mujibu wa aya hizi hapana fani yoyote ya taaluma iliyoasisiwa na binaadamu. Hivyo suala la kuwa na elimu ya dunia iliyoasisiwa na binaadamu na elimu ya dini ambayo tu ndiyo iliyotaka kwa Allah (s.w), halipo kwa mtazamo wa Qur-an.

Nne : katika Qur-an tunafahamishwa kuwa wanaomcha Allah (s.w) ipasavyo na kumuogopa ni wale wataalamu (ulamaa) waliozama katika fani mbali mbali za elimu. Kwa mujibu wa Qur'an fani hizi mbali mbali haziishii tu kwenye zile fani zinazotazamwa kwa mrengo wa kidini kama vile fiqh, Tawhiid, n.k. bali fani zote za elimu zinazo muwezesha binaadamu kutafakari kwa undani juu ya kuwepo Allah (s.w) na daraja ya utukufu wake, hasa zile fani za kisayansi zinazohusiana na maumbile. Hebu turejee aya zifuatazo:

﴿أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ ثَمَرَاتٍ مُّخْتَلِفًا أَلْوَانُهَا وَمِنَ الْجِبَالِ جُدَدٌ بِيضٌ وَحُمْرٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهَا وَغَرَابِيبُ سُودٌ ﴿٢٧﴾ وَمِنَ النَّاسِ وَالدَّوَابِّ وَالْأَنْعَامِ مُخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ كَذَٰلِكَ إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ ﴾

Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji toka mawinguni!Na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na (mengine) myeusi sana. Na katika watu na wanyama wanaotambaa na wanyama (wengine), pia rangi zao ni mbali mbali. Kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja Wake ni wale wataalamu (wanavyuoni). Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Msamehevu. (35:27-28)

Katika aya hizi tunajifunza kuwa wenye kumcha Allah (s.w) ipasavyo na katika kiwango cha juu cha unyenyekevu ni wale waumini waliobobea katika taaluma mbali mbali (maulamaa). Je, maulamaa waliotajwa katika aya hizi ni wale tu waliobobea kwenye taaluma zinazoitwa za kidini kama vile fiq-h, Qur-an na Hadith? Maulamaa waliopigiwa mfano katika aya hizi ni wale waliozama katika fani ya Hali ya Hewa (Meteorologist), Maulama waliozama katika uchunguzi wa wanyama (Zoologist), maulamaa waliozama katika fani ya matunda (Horticulturist), Maulamaa waliozama katika fani ya Madini (Geologists) na Maulamaa waliozama katika fani ya kuchunguza watu walivyo kimaumbile, rangi, n.k. (Anthropolagist). Pia katika aya nyingi za Qur-an binaadamu amesisitizwa kuyafanyia utafiti mazingira ya mbingu na ardhi ili kumtambua Mola wake na kumuabudu ipasavyo.

Tano : katika Qur-an Allah (s.w) anatufahamisha kuwa waumini waliobobea kwenye elimu wana daraja kubwa zaidi kuliko waumini wengine:

﴿يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴾

"Mwenyezi Mungu atawainua wale walioamini miongoni mwenu; na waliopewa elimu watapata daraja zaidi.Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda yote." (58:11)

Aya hii haijabagua wenye elimu.Hivyo yeyote yule mwenye taaluma inayomuwezesha kumcha Mola wake na kumuabudu inavyostahiki katika kila kipengele cha maisha yake na ikamuwezesha kuchangia katika kusimamsiha Uislamu katika jamii atakuwa na daraja zaidi kuliko wale wasio na taaluma hiyo kama Qur-an inavyozidi kusisitiza:

﴿إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ﴾

"Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mwenyezi Mungu zaidi katika nyinyi." (49:13)

Sita : hatuoni mgawanyo wa elimu katika Hadith mbali mbali za Mtume(s.a.w.w) zinazozungumzia elimu. Kwa mfano Mtume(s.a.w.w) aliposema: "Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu mwanamume na kila Muislamu mwanamke." (Ibn Majah), hakubagua elimu.Pia rejea Hadith zifuatazo: Anas (r.a) ameeleza kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema: Mwenye kutoka nje kutafuta elimu yuko katika njia ya Allah mpaka atakapo rejea. (Tirmidh)

Abu Hurairah (r.a) ameeleza kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema: Yeyote atakayeulizwa juu ya jambo alilojifunza kisha akaficha (akakataa kutoa elimu ile) atavalishwa mshipi (mkanda) wa Moto siku ya Kiyama." (Ahmad, Abu Daud, Tirmidh na Ibn Majah).

Pia tunajifunza katika historia kuwa; Mtume(s.a.w.w) aliwaacha huru mateka wa vita vya Badr kwa yule aliyeweza kujikomboa kwa kuwafunza kusoma na kuandika watoto kumi wa Waislamu.

Hadith hizi zinadhihirisha kuwa Mtume(s.a.w.w) naye hakuigawanya elimu katika elimu ya dini na elimu ya dunia. Bali Mtume(s.a.w.w) amewahimiza Waislamu kutafuta elimu yenye manufaa kwa jamii popote pale inapopatikana. "Tafuteni elimu hata China" (Baihaqi)

Laiti kama pangelikuwepo na mgawanyo wa elimu na kuwa elimu ya lazima kutafutwa na Waislamu ni ile iitwayo "elimu ya dini" kwanini Mtume(s.a.w.w) aliwaamuru waende China wakati wahay ulikuwa unamfuata yeye alipo? Ilikuwa inatosha wao kubaki na Mtume Makkah au Madina na asiwatume tena kwenda China kutafuta elimu. Hivyo, kutokana na hoja hizi sita, Uislamu hautambui mgawanyo wa elimu kwenye tapo la elimu ya dini na elimu ya dunia.

MGAWANYO WA ELIMU KATIKA FARADH

Mgawanyo wa Elimu katika Faradh 'Ain na Faradh Kifaya Faradh ya elimu inaweza kugawanywa kwenye faradhi 'Ain na faradh Kifaya.Faradh 'Ain ni faradh inayomhusu kila mtu binafsi isiyo na uwakilishi. Mfano, kusimamisha swala, kutoa Zakat, kufunga, n.k. ni katika faradh 'ain. Faradh Kifaya ni faradh inayoweza kufanywa kwa uwakilishi.Ni faradhi ya kijamii. Wachache wanaweza kuitekeleza kwa niaba ya jamii. Kwa mfano swala ya maiti na yale yote ya faradh anayostahiki kufanyiwa maiti wa Kiislamu ni katika faradh kifaya.

ELIMU YA MAARIFA YA UISLAMU

Elimu ya Maarifa ya Uislamu, itakayompelekea mja kumtambua, Mola wake, vilivyo na kumuabudu inavyostahiki katika kila kipengele cha maisha ni faradh 'Ain. Kwa maana nyingine ni faradh kwa kila Muislamu kuujua Uislamu vilivyo na kujitahidi kuutekeleza kwa kadiri ya uwezo wake katika kila kipengele cha maisha. Elimu juu ya fani mbalimbali zinazohitajika katika maisha ya jamii ni faradhi kifaya kwa jamii ya Kiislamu. Kwa mfano ni faradhi kwa jamii ya Kiislamu kuwa na madaktari, wahandisi, wanasheria, wanasiasa, wanauchumi, waalimu na wataalamu wengineo katika kila fani ya maisha ya jamii wa kutosha kukidhi mahitajio ya jamii katika kuendea nyanja zote za maisha.

Ikitokezea Waislamu wamezembea kiasi cha kushindwa kutoa wataalamu wanaohitajika kuendesha kila fani ya maisha ya jamii mpaka inapelekea Waislamu kushindwa kumuabudu Mola wao ipasavyo katika kila kipengele cha maisha, jamii yote ya Waislamu itakuwa katika lawama (itapata dhambi) na itaathirika kutokana na dhambi hii.

Hivyo ili Waislamu waweze kusimamisha Uislamu (Ukhalifa wa Allah) katika jamii, kila Muislamu hanabudi kuufahamu Uislamu vilivyo na pawekwe mazingira ya makusudi yatakayomuwezesha kila Muislamu kujielimisha katika fani maalumu ya maisha inayohitajika katika jamii kwa kadiri ya vipaji alivyoruzukiwa na Mola wake.Kwa maana nyingine kila Muislamu mwenye vipaji vya kuwa Daktari au Mhandisi au Mwanasheria au Mchumi au Mwalimu au. ajizatiti kuiendea taaluma hiyo na jamii ijizatiti kumuwezesha. Endapo, kwa mfano Muislamu mwenye kipaji cha kuwa Dak tari, akazembea asiwe Daktari atakuwa mas-uli mbele ya Allah (s.w).Pia endapo jamii ya Waislamu itazembea isitoe Madaktari wanaohitajika itakuwa mas-uli mbele ya Allah (s.w).

ELIMU YENYE MANUFAA

Elimu yenye manufaa ni ile ambayo:

Kwanza : humuwezesha mja kufikia lengo la kuumbwa kwake. Tumeona kuwa elimu imekuwa faradhi ya kwanza kwa waumini kwa kuwa elimu ndio nyenzo kuu ya kuwawezesha binaadamu kufikia lengo la kuumbwa kwao ambalo ni kumuabudu Allah (s.w), ipasavyo katika kila kipengele cha maisha yao. (Qur-an 51:56).

Pia elimu ndio nyenzo kuu ya kuwawezesha waumini kuwa viongozi wa jamii (makhalifa wa Allah) katika ardhi. (Qur-an 2:30 - 31).

Elimu itakayotafutwa kinyume na kumuwezesha mtu kumuabudu Mola wake ipasavyo na kusimamisha ukhalifa wa Allah (s.w) katika ardhi itakuwa si elimu yenye manufaa bali elimu yenye kuhasirisha kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo: Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema:

"Anayetafuta elimu isiyokuwa kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah (s.w), hasomi kwa lengo lolote lile ila la kupata maslahi ya hapa duniani tu.Huyo siku ya kiyama hatapata hata harufu ya Pepo." (Ahmad, Abu Daud, Ibn Majah).

Pia Mtume(s.a.w.w) ametuasa kuwa mwenye kutafuta elimu ili awazidi wasomi wengine au ili kuitumia katika biashara za kijahili au ili kujionesha kwa watu kuwa naye ni msomi, Mwenyezi Mungu atamuingiza motoni. (Tirmidh)

Pili : elimu yenye manufaa kwa binaadamu hapa ulimwenguni na huko akhera ni ile ambayo pamoja na mtu binafsi kuitumia katika kumuabudu Allah (s.w) ipasavyo katika maisha yake ya kila siku, huifundisha au huifikisha kwa wengine pia kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah (s.w). Ni vibaya mno mbele ya Allah (s.w) mtu kukataa au kuacha kufikisha kwa wengine kila anachokijua kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:

"Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w) amesema:

"Atakayeulizwa juu ya jambo alilojifunza kisha akaficha (akakataa kutoa elimu ile) atavalishwa mshipi wa moto katika siku ya Kiyama". (Ahmad, Ibn Majah, Tirmidh na Abu Daud).

Katika hadith nyingine iliyosimuliwa na Abu Hurairah Mtume(s.a.w.w) amesema:

"Mfano wa elimu isiyonufaisha ni sawa na mfano wa mali iliyokusanywa bila ya kutumiwa katika njia ya Allah". (Ahmad, Darini).

Kutokana na hadith hizi tunajifunza kuwa elimu yenye kunufaisha ni ile iliyofundishwa kwa wengine kinadharia na kiutendaji. Kwa kufundisha watu unachokijua bila ya wewe mwenyewe kutenda ni mfano mbaya mno kwa wale wanaofundisha na chukizo kubwa mno mbele ya Allah (s.w):

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ ﴿٢﴾ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ﴾

"Enyi mlioamini mbona mnasema msiyoyatenda?Ni chukizo kubwa mbele ya Allah (s.w) kusema msiyoyatenda" (61:2-3)

ZOEZI

1. Elimu ni nini?

2."Sema, Je wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?.. ." (39:9) Ni kwasababu gani wanaojua hawawi sawa na wasiojuwa?

3. Unatoa maoni gani iwapo wanaojua na wasiojua wakawa sawa kiutendaji?

4. Toa maelezo yenye ushahidi wa Qur-an kuonyesha kuwa:

(a) Elimu ndio takrima ya kwanza aliyokirimiwa binaadamu na Mola wake.

(b) Kutafuta elimu ni amri ya kwanza kwa binaadamu.

5. Onyesha kwa ushahidi wa Qur-an kuwa katika Uislamu mgawanyiko wa elimu katika "elimu ya dini" na "elimu ya dunia" haukubaliki.

6."Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba." (96:1)

Kusoma kwa jina la Mola wako maana yake nini?

7. "....Soma na Mola wako ni karimu sana.Ambaye amemfundisha mwanaadamu kwa kalamu.Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui". (96:3-5)

Orodhesha njia tano anazozitumia Allah (SW) katika kuwasiliana na wanaadamu.

8. Elimu yenye manufaa kwa binaadamu ni ile.................................

9. Eleza sababu tatu zinazopelekea elimu kupewa nafasi ya kwanza katika Uislamu.