7
MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA ELIMU
KUAMINI SIKU YA MALIPO
Kuamini siku ya Malipo ni miongoni mwa Nguzo Muhimu katika Nguzo za Iman ya Kiislamu. Kwa hakika ndiyo Msingi wa nguzo nyinginezo za Iman. Mtu hawezi kuwa muumini wa kweli mpaka awe na yakini kuwa pana maisha mengine baada ya kufa. Katika sehemu mbalimbali katika Qur'an Allah (s.w) ameiambatanisha nguzo hii ya "Kuamini Akhera" na "Kumuamini Allah" ambayo ni nguzo ya kwanza.
Allah (s.w) anatuambia:
﴿وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا﴾
"Na mwenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume wake na siku ya mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali (na haki)
(4:136)
Pia anasema:
﴿لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا﴾
"Bila shaka mnao mfano mwema (ruwaza nzuri) kwa mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa Mwenye kumwogopa Mwenyezi mungu na Siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyezimungu sana"
(33 :21)
Pia anasema:
﴿لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ﴾
"Sio wema (peke yake tu) kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, bali wema hasa ( ni wale) wanaomwamini Allah na Siku ya Mwisho"
(2:177)
Muislamu wa kweli anaamini kuwa maisha haya ya duniani ni maisha yana mwisho, yatakoma na kuna siku nyingine ambayo hakuna siku baada ya siku hiyo, kisha yanakuja maisha ya pili ambayo ndiyo maisha halisi ya kweli ya nyumba ya Akhera. Kupatikana kwa siku hiyo ambayo hakuna siku baada ya siku hiyo, kutakuja baada ya Ulimwengu wote kutoweka na kubaki ufalme wa Allah (s.w) tu yeye peke yake, Aliye dhati ya kweli. Malaika, Milima, Majini, Binaadamu, maji na kila kilicho na uhai kitatoweka kipende kisipende. Allah anatutanabahisha hili kwa kusema:
﴿كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ﴾
"Kila aliye juu ya ardhi atakufa na atasalia Mola wako Mwenye Utukufu (wa kweli) usio na mahitaji na fadhila kamili"
(55:26 - 27)
Baada ya kila kilicho hai kutoweka na kubaki Ufalme wa Allah (s.w) kama Alivyokuwa kabla ya kuumba chochote, hapo Allah atawafufua viumbe na kuwakusanya kwake wote ili apate kuwalipa kwa lile walilolifanya katika ardhi hii, wapate Pepo kama walikuwa watiifu kamili kwa Mola wao au wastahili Moto kwa kuwa walishika miungu mingine badala ya Allah (s.w) katika kuendesha maisha yao. Maisha hayo ndiyo maisha halisi na yenye kudumu daima! Allah (s.w) anatubainishia kuwa:
﴿أَلَا يَظُنُّ أُولَـٰئِكَ أَنَّهُم مَّبْعُوثُونَ ﴿٤﴾ لِيَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥﴾ يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ﴾
"Kwani hawaelewi kuwa wao watafufuliwa ? Ndani ya Siku tukufu, Siku watasimama watu kwa amri ya Bwana wa viumbe vyote? (83: 4-6).
Pia anasema:
﴿زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴾
"Makafiri wanadai kuwa hawatafufuliwa!, (sema Kwanini msifufuliwe?!) Naapa kwa Mola wangu Wallah!: Mtafufuliwa na kisha wallah! Mtaelezwa mlichokifanya duniani, hayo kwa Allah ni sahali (64:7)
Muislamu wa kweli anaamini kuwa Qiyama kitasimama na kila mja atalipwa kwa kila tendo alilolifanya, dogo au kubwa kama Allah (s.w) anavyotubainishia katika Qur'an:
﴿فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ﴾
"Basi atakayefanya (jambo lolote) la kheri lenye uzito mfano wa Dharra (Atom) ataliona jaza yake. Na atakayefanya (jambo lolote) la shari lenye uzito mfano wa Dharra (Atom) ataliona jaza yake".
(99: 7 - 8)
Pia Allah (s.w) anamkumbusha Mtume(s.a.w.w)
juu ya wasia wa Mzee Luqmaan kwa kijana wake ambao kwa hakika ndio wasia bora wa kila mzazi kumpa kijana wake, anasema:
﴿ يَا بُنَيَّ إِنَّهَا إِن تَكُ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ فَتَكُن فِي صَخْرَةٍ أَوْ فِي السَّمَاوَاتِ أَوْ فِي الْأَرْضِ يَأْتِ بِهَا اللَّـهُ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴾
"Ewe mwanangu, jambo lolote lililo na uzito wa chembe ya Hardal (au ndogo kuliko hiyo) ikiwa katikati ya jabali, au juu mbinguni au chini ardhini Allah Atalileta (amlipe aliyelifanya) Hakika Allah ni mwingi wa habari na mwenye ujuzi (hasa)"
(31: 16)
Dalili (Alama) za Qiyama Ingawa hakuna ajuaye Kiyama kitakuwa lini, kupitia Aya mbali mbali za Qur'an na Hadith kadhaa za Mtume (s.a.w) zinabainisha kwa uwazi juu ya dalili mbali mbali za kusimama kwa kiyama. Ziko Dalili kubwa na Dalili ndogo, na zipo ambazo tayari zimekwishadhihiri nyingine zinaendelea na ambazo bado kudhihiri kwake; Kama Allah Aliyetukuka anavyotubainishia:
﴿فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ﴾
"Kwani wanangoja jingine ila kiyama kiwajie kwa ghafla?Basi alama zake (hicho kiyama) zimekwishakuja.Kutawafaa wapi kukumbuka wakati kitakapowajia?"
(47:18)
Pia anasema
﴿وَالذَّارِيَاتِ ذَرْوًا﴾
"Saa ya Kiyama imekaribia; na mwezi umepasuka" (54:1)
Dalili Ndogo za Kiyama:
(i) Watu kumiliki mali na hali ya kuwa ni madhalimu wasio na uadilifu
(ii) Kuenea mno kwa riba kiasi cha kila mtu kuathiriwa nayo
(iii) Kuenea kwa kila aina ya Ulevi
(iv) Wanawake kukithiri katika kuvaa nguo zinazochochea zinaa (nguo nyepesi za kuangaza,fupi na za kubana)
(v) Wanawake watawaiga wanaume katika mavazi kadhalika wanaume watawaiga wanawake katika mavazi. Leo wanaume wanavaa hereni, shanga, bangili,na mengineyo yanayojulikana kuwa mapambo ya kike.
(vi) Kuenea kwa Liwati (kujimai baina ya jinsia mojawanaume kuwaendea wanaume wenzao na wanawake kuwaendea wanawake wenzao) Homosexuality and Lesbiansm. Jambo hili leo limehalalishwa na watu wa Magharibi, pia hapa kwetu Afrika na hasa Kenya na Afrika kusini ni halali Mwanaume kuolewa na mwanamume mwenzake! Subhaanallah!
(vii) Kuenea sana kwa zinaa na itafanyika hadharani.
(viii) Watu hawatawajali tena wazazi wao, ndugu zao na jamaa zao badala yake watawathamini na kuwasaidia rafiki zao.
(ix) Watu watachukia sana kulea watoto.
(x) Unafiki utaenea sana.
(xi) Mauaji yataenea sana, kwa kutoka Taifa moja kwenda kulivamia Taifa jingine na watu baadhi kuwaua wengine kwa maslahi yao binafsi
(xii) Watu wataona uzito sana kutoa sadaka
(xiii) Watawala watakuwa wengi sana lakini hakuna atakayekuwa mkweli na mwadilifu
(xiv) Mtu ataheshimiwa kwa shari yake na si kwa uadilifu na wema wake.
(xv) Kujifaharisha kwa misikiti
(xvi) Pamoja na haya yote,bado kutakuwepo na kundi dogo tu la waislamu ambalo litadumu katika njia iliyonyooka na halitatetereka kwa lolote.
Dalili Kubwa za kukaribia Siku ya Kiyama Mtume(s.a.w.w)
pia ametutajia dalili kubwa za kukaribia kwa siku ya Mwisho. Dalili hizo zinapatikana katika Qur'an na Hadith kama inavyobainishwa hapa chini:
Allah (s.w) anasema:
﴿وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ﴾
"Na kitakapokaribia Kiyama, tutawatolea mnyama kutoka ardhini atawaeleza (watu) kwa kuwa watu walikuwa hawaziamini aya zetu" (27:82)
Pia anasema:
﴿حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍ يَنسِلُونَ ﴿٩٦﴾ وَاقْتَرَبَ الْوَعْدُ الْحَقُّ فَإِذَا هِيَ شَاخِصَةٌ أَبْصَارُ الَّذِينَ كَفَرُوا يَا وَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا بَلْ كُنَّا ظَالِمِينَ﴾
"Mpaka watakapofunguliwa Ya'juj na Ma'juj nao wataporomoka kwa kasi, na ikakaribia ahadi ya kweli kufunguliwa, hesabu na malipo, basi wakati huo macho ya makafiriyatatokeza mno juu" (21:96 - 97)
Katika hadith aliyoipokea Imam Ahmad, na kusimuliwa na Khudhaifa Ibn Usaid Al - Ghifaar (r.a) amesema; Alitutokea Mtume (s.aw) kutoka chumbani kwake na sisi tukikumbushana jambo la kiyama, Mtume (s.a.w) akasema: Hakitosimama Kiyama mpaka muone alama kumi;
1. Kuchomoza jua Magharibi 2. Kutokea moshi mkubwa utakaochafua mazingira (pollution)
3. Mnyama atatokeza na kuwasemesha watu (27:82)
4. Kufunguliwa Ya'juj na Ma'juj (21:96 97)
5. Kurudi kwa Issa mwana wa Maryam Kuamini siku ya mwisho ni kuamini kuwa kuna maisha ya milele baada ya maisha haya ya hapa duniani. Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur-an, maisha hayo yatakuwa na hatua kuu nne zifuatazo:
(i) kutokwa na roho
(ii) Maisha ya kaburini - Barzakh.
(iii) Kufufuka na kuhudhurishwa mbele ya Allah (s.w) na kuhesabiwa.
(iv) Maisha ya kukaa Peponi milele kwa watu wema au kukaa motoni kwa watu waovu. Aidha kwa kuzingatia matukio yatakayotokea katika hatua nne za maisha yajayo, siku ya mwisho katika Quran imepewa majina mengi yafuatayo:
(i) Siku ya Qiyama (21:47, 75:1, 75:6, 79: 42)
(ii) Siku ya mwisho (2:4, 2:8, 58:22)
(iii) Siku ya malipo (1:4, 82:9, 95:7, 107:1, 83:11)
(iv) Msiba ugongao nyoyo (101:1)
(v) Siku ya hukumu (77:13-14)
(vi) Wakati maalumu (56:49-50)
(vii) Siku ya makamio (50:20)
(viii) Siku ya makutano (40:15)
(ix) Siku iliyokaribu sana kufika (40:18)
(x) Siku ya kuitana (40:32)
(xi) Siku ya kutoka makaburini (50:42)
(xii) Tukio lilokaribu, limesogea
(xiii) Siku zitakapotikisika mbingu mtikisiko wake
6. Kuja kwa Masih Dajal (False Messayah)
7. Kutoka Moto (Volcano) katika pango la Aden
ukiwaendesha watu
8. Dunia kugawika mapande matatu (Three Blocks); Pande la Mashariki (Eastern Block)
9. Pande la Magharibi na (western block)
10. Bara Arab (Mashariki ya kati - Middle East)
Kwa hakika Qur'an imetaja dalili nyingi mno, Rejea Suratul qiyaamah (75:6 - 9) na nyinginezo nyingi zilizotajwa katika hadith mbali mbali.
(xiv) Siku ya kukaa daima (50:42)
(xv) Siku zitakapofichuliwa siri (86:9)
(xvi) Tukio la Haki (69:1-3)
(xvii) Siku ya Haki (78:39)
(xviii) Tukio kubwa (56:1-2)
(xix) Siku iliyokadiriwa (85:2)
(xx) Msiba ukumbao (88:1)
(xxi) Siku iliyokuu (83:5)
(xxii) Siku ya mkusanyiko (64:9)
(xxiii) Siku ya Hisabu
HOJA ZA WAPINZANI WA SIKU YA MWISHO
Wengi wa makafiri wapingao kuwepo siku ya mwisho wanatoa hoja kubwa mbili zifuatazo:
1. Hapana uwezekano wa kupatikana uhai baada ya mtu kuoza na mifupa yake kusagika sagika
﴿يَقُولُونَ أَإِنَّا لَمَرْدُودُونَ فِي الْحَافِرَةِ ﴿١٠﴾ أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا نَّخِرَةً ﴿١١﴾ قَالُوا تِلْكَ إِذًا كَرَّةٌ خَاسِرَةٌ﴾
"(Makafiri) wanasema (kwa stihizai) Je! Tutarudishwa katika hali yetu ya kwanza (tutafufuliwa)?Hata tukiwa mifupa mibovu (iliyooza)? (kwa stihizai wanasema):- Basi marejeo haya ni yenye hasara (kwetu)" (79:10-12)
﴿وَكَانُوا يَقُولُونَ أَئِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ﴾
"Na walikuwa wakisema: "Tutakapokufa na kuwa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa? (56:47)
UDHAIFU WA HOJA
Allah (s.w) ameonyesha udhaifu wa hoja hii katika aya zifuatazo:
﴿أَوَلَمْ يَرَ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ ﴿٧٧﴾ وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ ﴿٧٨﴾ قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ ﴿٧٩﴾ الَّذِي جَعَلَ لَكُم مِّنَ الشَّجَرِ الْأَخْضَرِ نَارًا فَإِذَا أَنتُم مِّنْهُ تُوقِدُونَ ﴿٨٠﴾ أَوَلَيْسَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُم بَلَىٰ وَهُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ ﴿٨١﴾ إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾ فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴾
Je, mwanaadamu hatambui ya kwamba tumemuumba kwa tone la manii? Amekuwa hasimu yetu aliye dhahiri (Sasa)! Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake (kwa manii) - akasema: "Nani atakayeihuisha mifupa na hali imesagika?" Sema: "Ataihuisha yule aliyeiumba mara ya kwanza, naye ni Mjuzi wa kila (namna ya) kuumba. Ambaye amekufanyieni moto katika mti mbichi, mkawa nanyi kwa (mti) huo mnauwasha. Je, yule aliyeziumba mbingu na ardhi (mnaona) hana uweza wa kuumba (mara ya pili) mfano wao (wanaadamu)?Kwa nini? Naye ni Mwumbaji mkuu, Mjuzi (wa kila jambo).Hakika amri yake anapotaka chochote (kile kitokee) ni kukiambia:'Kuwa,' basi mara huwa. Ametukuka yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake mtarejezwa nyote. (36:77-83)
﴿أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَلَّن نَّجْمَعَ عِظَامَهُ ﴿٣﴾ بَلَىٰ قَادِرِينَ عَلَىٰ أَن نُّسَوِّيَ بَنَانَهُ﴾
Anadhani mtu ya kuwa sisi hatutaikusanya mifupa yake?Kwa nini! Sisi tunaweza (hata) kuzisawazisha ncha za vidole vyake (tutakapomfufua mara ya pili,ziwe kama zilivyokuwa duniani)
(75:3-4)
﴿أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ ﴿١٧﴾ وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ ﴿١٨﴾ وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ ﴿١٩﴾ وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ﴾
Je! Hawawatazami ngamia jinsi walivyoumbwa? Na mbingu jinsi zilivyoinuliwa. Na milima jinsi ilivyothubutishwa? Na ardhi jinsi ilivyotandazwa? (Basi aliyeyafanya hayo kutamshinda kufufua Binaadamu)?
(88:17-20)
﴿وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴾
Na yeye ndiye aliyeanzisha viumbe na ndiye Atakayevirudisha (mara nyingine), na (jambo) hili ni rahisi zaidi Kwake; naye ndiye mwenye sifa nzuri mbinguni na katika ardhi, naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(30:27)
﴿أَفَعَيِينَا بِالْخَلْقِ الْأَوَّلِ بَلْ هُمْ فِي لَبْسٍ مِّنْ خَلْقٍ جَدِيدٍ ﴾
Je! Tulichoka kwa kuumba kwa mara ya kwanza (hata tushindwe kuumba umbo la pili)? Basi wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya! (50:15)
2. Waliokufa hawajarudi wakatoa ushahidi
﴿وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ مَّا كَانَ حُجَّتَهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴾
"Wanaposomewa aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila husema waleteni baba zetu (wazee wetu waliokufa) ikiwa nyinyi ni wasemao kweli (kuwa watu watafufuliwa)" (45:25)
Udhaifu wa Hoja Kutofufuka waliotangulia kufa sio hoja ya kutokuwepo ufufuo, kwani katika utaratibu wa Allah (s.w) watu hawatafufuliwa mmoja mmoja, bali watafufuliwa wote kwa pamoja, wa mwanzo na wa mwisho katika siku hiyo maalumu:
﴿قُلْ إِنَّ الْأَوَّلِينَ وَالْآخِرِينَ ﴿٤٩﴾ لَمَجْمُوعُونَ إِلَىٰ مِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴾
"Sema "Bila shaka wa kwanza na wa mwisho watakusanywa kwa wakati (uliowekwa) katika siku maalum. (56:49-50).
Ulazima wa kuwepo Siku ya Mwisho Kimantiki kuwepo siku ya malipo (siku ya hukumu) ni jambo lisilo budi ili:
1. WALE WALIOFANYA WEMA HAPA DUNIANI BILA YA KUPATA UJIRA UNAOSTAHIKI, WALIPWE FADHILA YA WEMA WAO.
﴿هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ﴾
"Hakuna malipo ya ihsani ila kulipwa ihsani" (55:60)
2. WALE WALIODHULUMU HAKI ZA WATU HAPA DUNIANI, WARUDISHE HAKI ZA WENYEWE MBELE YA HAKIMU WA MAHAKIMU.
﴿أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ ﴾
"Je!Mwenyezi Mungu si Hakimu muadilifu kuliko mahakimu wote? (95:8)
3. WALE WABABE WALIOFANYA UOVU ULIOKITHIRI HAPA DUNIANI
bila ya kupata adhabu inayostahiki, wahukukumiwe na kupewa adhabu inayolingana na makosa yao mbele ya Mfalme wa Wafalme.
﴿مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ﴾
"Mwenye kumiliki siku ya malipo" (1:4)
4. WATU WAULIZWE VIPI WALISHUKURU JUU YA NEEMA NA VIPAJI MBALI MBALI WALIVYOTUNUKIWA NA MUUMBA WAO.
﴿ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴾
"Kisha kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema (mlizopewa mlizitumiaje)? (102:8)
5. WABAINIKE NI AKINA NANI WALIOFUATA NJIA SAHIHI YA MAISHA, WAISLAMU AU MAKAFIRI?
﴿وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَا يَبْعَثُ اللَّـهُ مَن يَمُوتُ بَلَىٰ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٨﴾ لِيُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي يَخْتَلِفُونَ فِيهِ وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّهُمْ كَانُوا كَاذِبِينَ﴾
"Nao (wakaapa) kwa jina la Mwenyezi Mungu kwa kiapo chao cha nguvu (kwamba Mwenyezi Mungu hatawafufua wafao.Kwanini (asiwafufue)? Ni ahadi iliyolazimika kwake,(kuwafufua na kuwalipa) lakini watu wengi hawajui.(Atawafufua) ili kuwabainishia yale waliyohitalifiana ili wajue waliokufuru ya kwamba wao walikuwa ni waongo.(16:38 - 39)
Ushahidi wa Ufufuo kutokana na Historia Tukirejea Qur-an tunafahamishwa matukio kadhaa ya kihistoria yanayotudhihirishia kuwa ufufuo ni jambo jepesi kwa Allah (s.w). Matukio haya ni pamoja na:
1. Kufufuka msafiri na punda wake
﴿أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّـهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالَ بَل لَّبِثْتَ مِائَةَ عَامٍ فَانظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ وَانظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ آيَةً لِّلنَّاسِ وَانظُرْ إِلَى الْعِظَامِ كَيْفَ نُنشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾
"Au kama yule aliyepita karibu na mji uliokuwa umekufa akasema:"Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu (na watu wake) baada ya kufa kwake?" Basi Mwenyezi Mungu alimfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua akamwuliza:"Umekaa muda gani?" Akasema: "Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku." (Mwenyezi Mungu) akasema: "Bali umekaa miaka mia; nawe tazama chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na mtazame punda wako (amekuwa mifupa mitupu iliyolikalika).Na ili tukufanye uwe hoja kwa watu (ndio tumekufufua hivi). Na itazame mifupa (ya punda wako) jinsi tunavyoinyanyua,kisha tunaivisha nyama."Basi yalipombainikia (haya yule aliyefufuliwa) alinena: 'Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu." (2:259)
2. KUFUFUKA NDEGE WA NABII IBRAHIMU
﴿وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِّنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِّنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴾
Na (kumbuka) Ibrahimu aliposema:"Mola wangu!Nionyeshe jinsi utakavyofufua wafu"(Mwenyezi Mungu) akasema:"Huamini?"Akasema: "La, (naamini), lakini (nataka kuona hayo) ili moyo wangu utulie (zaidi)" Akasema: "Basi chukua ndege wanne na uwazoeshe kwako (uwadhibiti vizuri sura zao hata wasikupotee popote unapowaona), kisha (wachinje) uweke juu ya kila jabali sehemu katika wao.Kisha waite, watakujia mbio. Na ujue ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima". (2:260)
3. KUAMKA AS-HABUL-KAHF
﴿ وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا ﴾
"Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha (miaka) tisa" (18:25)
4. KUFUFUKA KWA WATU WA NABII MUSSA
﴿ وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَىٰ لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْكُمُ الصَّاعِقَةُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ﴾
Na (kumbukeni habari hii pia:) Mliposema:"Ewe Mussa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu wazi wazi" Yakakunyakueni mauti ya ghafla), na hali mnaona. Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru. (2:55-56)
5. KUFUFUKA KWA YULE MTU ALIYEULIWA KWA DHULUMA WAKATI WA NABII MUSSA
﴿ وَإِذْ قَتَلْتُمْ نَفْسًا فَادَّارَأْتُمْ فِيهَا وَاللَّـهُ مُخْرِجٌ مَّا كُنتُمْ تَكْتُمُونَ ﴿٧٢﴾ فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا كَذَٰلِكَ يُحْيِي اللَّـهُ الْمَوْتَىٰ وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ﴾
Na (kumbukeni khabari hii inayotajwa sasa hivi:) Mlipoiua nafsi, kisha mkakhitilafiana kwa hayo; (wengine wanasema kauawa na Fulani na wengine wanasema Fulani mwingine). Na Mwenyezi Mungu ni Mtoaji wa hayo mliyokuwa mkiyaficha.(Basi akayatoa akajulikana huyo aliyemwua). Tukasema: "Mpigeni kwa baadhi (sehemu) yake (huyu ng'ombe)." Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Dalili zake ili mpate kufahamu.(2:72-73)
6. NABII ISSA
ALIFUFUA WAFU KWA IDHINI YA ALLAH (S.W)
﴿ وَرَسُولًا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنِّي قَدْ جِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ أَنِّي أَخْلُقُ لَكُم مِّنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ فَأَنفُخُ فِيهِ فَيَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِ اللَّـهِ وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّـهِ وَأُنَبِّئُكُم بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴾
"Na (atamfanya) Mtume kwa wana wa Israili, (kuwaambia): 'Nimekujieni na hoja kutoka kwa Mola wenu, ya kwamba nakuumbieni, katika udongo, kama sura ya ndege, kisha nampuliza, mara anakuwa ndege, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.Na ninawaponesha vipofu na wenye mbalanga, na ninawafufua (baadhi ya) waliokufa,kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na nitakwambieni mtakavyovila na mtakavyoweka akiba katika nyumba zenu. Bila shaka katika haya imo hoja kwenu ikiwa nyinyi ni watu wa kuamini'!" (3:49)
Uthibitisho wa Ufufuo kutokana na maisha ya kila siku Allah (s.w) pia anatupigia mifano kutokana na maisha yetu ya kila siku inayotuyakinisha juu ya ufufuo. Miongoni mwa mifano hii ni:-
1. Kufufuka kwa ardhi wakati wa mvua baada ya kufa kwake wakati wa kiangazi
﴿ وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾
"Na katika ishara zake ni kwamba unaona ardhi imedhalilika (kwa kukosa mvua) lakini tunapoiteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka; bila shaka aliyeihuisha ndiye atakayehuisha waliokufa. Hakika yeye ndiye mwenye uweza juu ya kila kitu" (41:39)
2. Kufufuka kutoka usingizini
﴿وَمِنْ آيَاتِهِ مَنَامُكُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَابْتِغَاؤُكُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ﴾
"Na katika ishara zake ni kulala kwenu usiku na kuamka mchana ,na kutafuta fadhila Yake.Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanaosikia(30:23)
3. Kufufuka kutoka kwenye kuzimia. Mtu aliyezimia ni kama mtu aliyekufa kwani hajitambui wala hajiwezi kwa lolote, na anapozindukana hajui lolote lililoendelea katika kipindi cha kuzimia kwake.
MAZINGIRA YA MAISHA YA AKHERA
Qur-an Karimu imechukua sehemu kubwa kuelezea maisha ya akhera kuanzia pale roho ya mtu inapokaribia kutoka mpaka katika hatua ya mwisho ya kuingia peponi kwa watu wema au kuingia motoni kwa watu waovu. Hakika iliyowazi ya kufahamishwa maisha ya akhera yatakavyokuwa ndani ya Qur'an ni kumtahadharisha binaadamu na maisha hayo ili aishi kwa uangalifu kwa kuzingatia maisha hayo yajayo.
Muumini baada ya kupewa picha kamili ya maisha ya akhera na Mola wake atajitahidi kufuata mwenendo mwema wa maisha utakaompelekea kupata radhi za Allah na kustahiki kupata mwisho mwema na kuingizwa katika neema za peponi na kujitahidi kujiepusha na mwenendo mbaya wa maisha ili kuepukana na ghadhabu za Allah (s.w) na kuepukana na adhabu kali ya motoni watakayostahiki kupata watu waovu waliomkufuru na kumuasi Mola wao. Ili tupate picha kamili juu ya maisha ya akhera katika sehemu hii tumenukuu na kurejea aya chache za Qur-an na Hadith sahihi za Mtume(s.a.w.w)
juu ya kila hatua ya maisha ya akhera kama ifuatavyo:
(i)Wakati wa Kukaribia kufa Mtu anapokaribia kufa na hasa baada ya kumuona malaika aliyehudhurishwa kuchukua roho yake huwa na yakini juu ya maisha ya akhera. Watu wema watafurahia kufa kwa yale maliwazo watakayopewa na malaika:
﴿ يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ﴿٢٧﴾ ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً ﴿٢٨﴾ فَادْخُلِي فِي عِبَادِي ﴿٢٩﴾ وَادْخُلِي جَنَّتِي ﴾
"Ewe nafsi yenye kutua! Rudi kwa Mola wako hali ya kuwa utaridhika (kwa utakayoyapata), na (Mwenyezi Mungu) aridhike na wewe. Basi ingia katika (kundi la) waja wangu (wazuri) uingie katika pepo yangu" (89:27-30)
Watu waovu watajuta kwa kupoteza muda wao nje ya lengo la kuumbwa kwao na wataomba wacheleweshwe kidogo ili wafanye mema. Juu ya hili Allah (s.w) anatutahadharisha:
﴿ وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠﴾ وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴾
"Na toeni katika yale tuliyokupeni kabla ya mmoja wenu hayajamfika mauti; kisha akasema: Mola wangu: Huniakhirishi muda kidogo (tu) nikatoa sadaqa na nikawa miongoni mwa watendao mema! Lakini Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapokuja ajali yake; Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda" (63:10-11)
﴿ حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴾
"Hata yanapomfika mmoja wao mauti husema: "Mola wangu! Nirudishe (katika uhai) ili nifanye mema sasa badala ya yale niliyoyaacha"
(23:99-100)
Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa muda (wakati) ambao ndiyo rasilimali ya uhai wa binaadamu unahitajika utumike wote katika kuendea lengo la maisha ya binaadamu hapa ulimwenguni. Muda wote uliotumika nje ya lengo utakuwa ni wenye kujutiwa. Lagh-wi (mambo ya upuuzi yanayopoteza muda wa kuendea lengo) ni haramu katika Uislamu. Rejea sifa za waumini Qur-an 23:2) na (25:72).
Hebu turejee hadith za Mtume(s.a.w.w)
juu ya hali wanayokuwa nayo watu wanao karibia kufa"Ubaidah bin Swamiti amesimulia kuwa Mtume wa Allah(s.a.w.w)
amesema: Yeyote anayependa kukutana na Allah (s.w), naye Allah (s.w) anapenda kukutana naye; na yeyote yule asiyetaka kukutana naye, pia Allah (s.w) hana haja ya kukutana naye. Aisha, au baadhi ya wake zake Mtume(s.a.w.w)
wakasema: Hakika ni kweli hatupendi kifo. Alifafanua Mtume(s.a.w.w)
"Sio hivyo, bali wakati kifo kinapomjia Muumini, anapewa habari njema juu ya ridhaa ya Allah (s.w) na neema zake. Baada ya habari hizi hatakuwa na kitu chochote atakachokipenda zaidi kuliko kifo (kinachomkaribia). Kwa hiyo atataka kukutana na Allah (s.w) na Allah (s.w) atataka kukutana naye.Na asiye muumini, kifo kinapomkaribia anapewa habari mbaya juu ya adhabu kali ya Allah (s.w). Na hapati kuwa na kitu kisichopendeza mbele yake kuliko hicho kinachomngojea mbele yake.Kwa hiyo Allah pia hataki kukutana naye. (Bukhari na Muslim).
Katika Hadith nyingine: "Anas amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) alikwenda kumuona kijana ambaye alikuwa katika hali ya ulevi wa mauti (Mtume(s.a.w.w)
alimuuliza: Unajisikiaje? Alijibu (kijana): "Ewe Mtume wa Allah!Ninamtumainia Allah (s.w) na ninaogopa madhambi yangu." Ndipo Mtume(s.a.w.w)
. Hivi viwili haviungani pamoja katika moyo wa mja kama hivi kwa wakati mmoja, isipokuwa Allah (s.w) anampa (mja wake) kile anachokitumaini na kumkinga na kila anachokiogopa" (Ibn Majah na Tirmidh)
Katika hadithi hizi tunajifunza kuwa watu wema watapata maliwazo na matumaini wakati wa kukaribia kufa na watu waovu watakata tamaa na kuhuzunika wakati huo.
(ii) Kutolewa roho (kufikwa na kifo) Kifo ni katika ishara kubwa ya kuwepo Allah (s.w) na siku ya mwisho. Binaadamu pamoja na mamlaka yake hana uwezo wa kuzuia kifo kisimfike. Wafalme pamoja na kuzungukwa na walinzi wenye silaha na zana za ulinzi madhubuti wanakufa kila uchao. Zingatia kuondoka kwa wafalme mbalimbali unaowafahamu katika historia kuanzia enzi za Fir'aun mpaka kwa hawa wafalme waliofutika katika uso wa dunia hivi karibuni. Allah (s.w) anatutanabahisha:
﴿ فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ ﴿٨٣﴾ وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ ﴿٨٤﴾ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾ فَلَوْلَا إِن كُنتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ ﴿٨٦﴾ تَرْجِعُونَهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴾
"Basi mbona (roho) ifikapo kooni, na nyinyi wakati ule mnamtazama,nasi tunakaribiana naye zaidi (huyo anayetokwa na roho) kuliko nyinyi wala nyinyi hamuoni. Kama nyinyi hamumo katika mamlaka (yangu) ,kwanini hamuirudishi (hiyo roho) ikiwa mnasema kweli?" (56:83-87)
Kama tulivyojifunza katika Hadith, watu wema baada ya kupata bishara za kuridhiwa na Mola wao watafurahia kufa na roho zao zitatolewa kwa upole. Kinyume chake, watu waovu baada ya kuona dalili za ghadhabu za Allah juu yake hatapenda kufa na kuwalazimu Malaika husika wachukue roho zao kwa nguvu. rejea kazi za malaika.
(iii) Maisha ya Barzakh (Kaburini)
﴿ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴾
"na mbele yao kuna Barzakh (maisha baada ya kufa) mpaka siku ya kufufuliwa". [23:100]
Kwa mujibu wa aya hii Barzakh ni kipindi cha maisha ya kaburini kinachodumu kwa kipindi chote ba ada ya mtu kufa mpaka siku ya kufufuliwa watu wote. Hiki ni kipindi ambacho roho za watu zinakuwa zimetengana na miili husika. Ambapo roho zitakuwa hai ima katika starehe au katika adhabu kama tunavyojifunza katika Hadithi zifuatazo: Anas amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w)
amesema: Hakika mja anapolazwa kaburini na jamaa zake wakawa wanarejea nyumbani anasikia sauti ya miguu yao. Malaika wawili humjia na kumkalisha na kumuuliza: Ulikuwa ukisemaje juu ya huyu Muhammad? Kama ni muumini atajibu: "Ninashuhudia kuwa yeye ni mja wa Allah (s.w.). Ataambiwa kuwa angalia sehemu yako ya motoni uliyobadilishiwa na sehemu katika pepo. Kisha ataziona sehemu zote mbili
Kwa Mnafiki au Kafiri ataulizwa: ulikuwa ukisema nini juu ya huyu mtu (Muhammad)? Atajibu:"Sijui, nilikuwa nikisema kama watu walivyokuwa wakisema. Ataambiwa hukuwahi kujua wala kusoma. Kisha atapigwa dharuba na rungu la kipande cha chuma, kwa kiasi kwamba atapiga kelele ambayo itasikiwa na kila kitu isipokuwa viumbe wa aina mbili (watu na majini)".
[Bukhari na Muslim]
Pia katika hadithi nyingine tunafahamishwa: Abdullah bin Umar umesimulia kuwa: Mtume wa Allah (s.w.) amesema:"Hakika wakati miongoni mwenu anapokufa. Mahali anapokwenda huwekwa mbele yake asubuhi na usiku. Kama ni miongoni mwa wakaazi wa peponi (roho yake) itakuwa ni miongoni mwa wakaazi wa peponi. Ikiwa yeye ni miongoni mwa wakazi wa motoni, (pia roho yake) itakuwa ni miongoni mwa wakaazi wa motoni. Kisha ataambiwa: "Hii ndio sehemu yako mpaka utakapofufuliwa siku ya kiyama"
. [Bukhari na Muslim]
Aysha amesimulia kuwa mwanamke wa Kiyahudi alimuendea na kumsimulia adhabu ya kaburini. Akamwambia: "Allah akukinge na adhabu ya kaburini.Aysha akamuuliza Mtume(s.a.w.w)
juu ya adhabu ya kaburini Mtume(s.a.w.w)
akajibu: "Ndio. Adhabu ya kaburini ni jambo la kweli". Aysha alisema: Sikumuona Mtume(s.a.w.w)
baada ya hapo kuswali swala yoyote bila ya kumuomba Allah amkinge na adhabu ya kaburini. [Bukhari na Muslim]
Ibn Abbas amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w)
alikuwa akiwafundisha (kwa msisitizo) dua (ifuatayo) kama alivyokuwa akiwafundisha sura ya Qur'an kwa kuwaambia:"Sema, Ee Allah! Nakijinga kwako na adhabu ya Jahannam na najikinga kwako na adhabu ya kaburi,na najilinda kwako na majaribu ya Dajjal mwenye jicho moja, na najikinga kwako na majaribu ya maisha ya kifo"
[Muslim]
Hadithi zote hizi zinatuthibitishia kuwa Roho, katika kipindi cha Barzakh, zitakuwa katika raha au taabu, kulingana na yale mja aliyoyatanguliza kutokana na matendo yake hapa duniani. Ndio maana Mtume(s.a.w.w)
akatufundisha dua hiyo na akatusisitiza tumuombe Allah (s.w.) atukinge na adhabu katika maisha ya akhera na atuwezeshe kufaulu mitihani ya majaribio ya maisha ili tuweze kupata maisha ya salama na amani katika makazi ya akhera. Hebu tuzidi kuzingatia hadithi zifuatazo:
Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w)
wa Allah amesema: Baada ya maiti kuzikwa malaika wawili, mmoja mweusi na mwingine mwenye rangi ya kibluu, watamjia. Mmoja wao anaitwa Munkar na mwingine Nakiir. Watauliza: Unasemaje juu ya huyu mtu? Kama (maiti huyo alikuwa Muumini atajibu).Ni mja wa Allah (s.w.) na ni Mtumwa wake. Ninashuhudia kuwa hapana Mola ila Allah (s.w.) na kwamba Muhammad ni Mtume(s.a.w.w)
wake na Mjumbe wake.
Watasema: Tulijua kuwa utajibu hivyo baadaye (baada ya swali). Kaburi lake litafanywa pana kiasi cha dhiraa sabiini kwa kila upande na kisha patakuwa na mwanga na ataambiwa: Lala kama usingizi wa Bwana arusi ambaye hakuna anayeweza kumuasha isipokuwa wapenzi wake katika familia. Mpaka Allah (s.w.) atakapomuinua kutoka kwenye kitanda chake. Kama (maiti) alikuwa Mnafiki, atajibu: Nimesikia watu wakisema neno kama hili linalosema: Simjui. (Malaika) watasema: Tulijua kuwa utasema hivyo.Kisha ardhi itaambiwa M'bane. Kisha itam'bana mpaka pande mbili (ubavu wa kulia na kushoto) zibadilishane.
Hatapumzika na adhabu ya hapo mpaka Allah atakapomuinua kutoka kwenye kitanda chake hicho. [Tirmidh] Katika hadithi nyingine: Abu Hurairah amesimulia kutoka kwa Mtume (s.a.w) wa Allah ambaye alisema: Hakika maiti hupelekwa kaburini na hukaa kaburini bila ya khofu wala fadhaa. Baada ya hapo ataambiwa: Ulikuwa katika nini? Atajibu: "Nilikuwa katika Uislamu". Kisha ataulizwa: Huyu ni nani? Atajibu: Muhammad, Mtumwa wa Allah.
Alitujia na hoja zilizowazi kutoka kwa Allah (s.w.) na kwa hivyo tulimuamini. Ataulizwa tena: Umemuona Allah? Atajibu: Si katika uwezo wa yeyote kumuona Allah.Kisha patawekwa uwazi utakaomwezesha kuona moto unaofoka. Ataambiwa: Angalia kile ambacho Allah amekuokoa (amekukinga) nacho. Kisha patawekwa uwazi utakaomuwezesha kuiona pepo na vile vilivyomo ndani yake. Ataambiwa: Hii ni sehemu yako kutokana na uthabiti wa imani uliyoishi nayo na ukafa nayo na ambayo utafufuliwa nayo, InshaAllah.
Mtu muovu, atakuwa katika kaburi lake kwa khofu na fadhaa.Ataulizwa ulikuwa katika nini? Atajibu: Sijui. Kisha ataulizwa tena: Ni nani huyu? Atajibu: Nilisikia watu wakisema kama ninavyosema. Kisha atawekewa uwazi wa kumuwezesha kuiona pepo. Ataangalia na kuona uzuri wake na vilivyomo ndani yake. Ataambiwa angalia kile ambacho Allah amekukosesha (kutokana na imani yake mbovu). Kisha utawekwa uwazi wa kumuwezesha kuona moto. Ataungalia na ataona muwako wake ulio mkali. Kisha ataambiwa.Hii ndio sehemu yako ambayo uliendesha maisha yako kwa kuwa na mashaka nayo, na umekufa ukiwa na mashaka nayo na utafufuliwa katika hali hiyo hiyo, InshaAllah. [Ibn Majah]
Hadithi hizi zimetuweka wazi juu ya hali zitakazokuwa nayo Roho za waja katika kipindi cha kukaa kaburini.Patakuwa na maswali yatakayoulizwa mara tu mtu anapokufa. Maswali haya yatakuwa ni mtihani kwa mja. Waumini tu ndio watakaoweza kujibu maswali haya kwa usahihi na ndio pekee watakaofaulu na kupewa bishara nzuri ya kupata pepo na neema zake. Kwa hawa kaburi huwa ni Bustani miongoni mwa bustani za peponi. Makafiri, Washirikina na Wanafiki hawataweza kujibu maswali watakayoulizwa, na watashindwa mtihani huu na kuahidiwa adhabu kali ya motoni na wataendelea kupata adhabu kali katika kipindi chote hiki cha maisha ya kaburini kama ujira wa imani yao mbovu juu ya Allah (s.w.) iliyosababisha matendo yao kuwa maovu. Kwa hawa kaburini huwa ni mashimo miongoni mwa mashimo ya motoni. Jambo muhimu linalotubidi tulifahamu kwa uwazi ni kwamba uwezo wa kujibu maswali haya haupatikani kwa kusoma na kukariri majibu kama tufanyavyo katika matayarisho ya mitihani yetu ya kila siku au mahojiano, bali uwezo wa kujibu maswali hayo hupatikana kutokana na uthabiti wa imani katika maneno na matendo ya kila siku. Wanafiki, wenye kuamini kinadharia tu, hawatakuwa na uwezo wa kujibu maswali hayo, hata kama walikuwa ni Masheikh wa kuwasomea watu talakini katika maisha yao yote.
Hivyo si talakini anayosomewa mtu wakati wa kuzikwa itakayomuwezesha kujibu maswali ya Munkar na Nakiir, bali kitakachomsadiia mtu ni ule uthabiti wa imani yake iliyofuatiwa na matendo mema katika utendaji wa maisha yake yote ya hapa ulimwenguni. Kwa ukweli huu Mtume(s.a.w.w)
kila baada ya kumaliza kumzika mtu alikuwa akiwaambia Maswahaba wamtakie maghfira ndugu yao na wamuombee uthabiti wa imani ili aweze kujibu maswali yale inavyostahili. Hivi ndivyo tunavyofahamishwa katika hadithi ifuatayo: Uthman amesimulia kuwa Mtume(s.a.w.w)
alipomaliza kumzika mtu aliyekufa alikuwa akisimama pale (kaburini) na kusema: "Mtakie maghfira ndugu yenu na muombeeni awe thabiti kwani ataulizwa sasa hivi". [Abuu Daud]
Kwa ufupi maisha Barzakh huwa kama mt aliyelala na kuota ndoto, mtu mwema, kwa kipindi chote atakacholala kaburini humo. ataota ndoto nzuri na muovu ataota ndoto mbaya zitakazoudhi nafsi yake kwa kipindi chote atakacholala kaburini humo. Kutokana na Hadith hii hakuna mtu yeyote wa kumuwezesha mtu kufaulu mtihani huu wa Allah (s.w.) mbali na uthabiti wa imani yake na matendo yake katika maisha ya dunia.