1
MUANDAMO WA MWEZI
SURA YA KWANZA
Nimesoma makala niliyoletewa na mmoja wa ndugu zetu katika Uislamu kuhusu suala la kuonekana kwa mwezi muandamo na kuhusu je mfungo na mfunguo uwe kwa muandamo mmoja au uwe kwa mujibu wa uoni wa kila mji? Muandishi anasema kwamba muandamo mmoja unatosheleza duniani kote. Baadhi ya hoja za muandishi wa makala hio tayari nimezijadili katika kitabu Ushahidi Ulioekwa Wazi ambacho nitakiambatanisha tena na makala hii ili ikiwa kuna upinzani wa kielimu juu ya nilioyasema nipingwe kwawo kwa faida ya Waislamu.
Hata hivyo, yako baadhi ya mambo ambayo - japokuwa niliyajibu kwa uwazi lakini - muandishi ameyaleta katika sura mpya inayonifanya nami nitoe tena mchango wangu katika kuweka wazi zaidi. Aliyesoma kitabu changu au kusoma vitabu vya wanavyuoni amejua kwamba ushahidi mkubwa wa kimaandishi wa wale wanaosema kwamba kila watu na muandamo wao ni Hadithi ya Ibn Abbaas na Kurayb ambayo utaiona katika kitabu nitachokiambatanisha humu. Hadithi hio nimeielezea kwa urefu na kutoa ushahidi unaopatikana ndani yake na kutoa upinzani wa wale wasiokubaliana na kutoa kwetu ushahidi kwa kutumia Hadithi hio. Pia nilionesha kwa urefu kwamba na sisi tuna jawabu gani juu ya upinzani huo.
Sasa muandishi wa makala niliyemuashiria hapo juu anatwambia kwamba Hadithi ya kurayb tunayoitegemea sisi ni dhaifu, naye - katika kuthibitishi hilo - anatoa maelezo yafuatayo. Anasema: "Hoja kubwa ya wenye kuhalalisha kila nchi kuwa na mwezi wake ni moja tu nayo ni kisa cha Kuraybu mtumwa wa Ibn 'Abbaas walipojadiliyana na Ibn 'Abbaas mwenyewe anasema Kuraybu kuwa "Ummul Fadhli bint Harith [mama yake huyu Ibn 'Abbaas] alinituma kwa Muawiyya katika mji wa Shamu nikafika Shamu na kutekeleza haja zake [zote] na ukaonekana mwezisayari wa mwezi wa Ramadhaan, na mimi nipo Shamu, tukauona mwezisayari usiku wa kuamkiya Ijumaa, baada ya hapo nikarudi Madina mwisho wa mwezi [wa Ramadhaan] akaniuliza Ibn 'Abbaas, kisha akautaja mwezi akasema : lini mliuona mwezi? nikamwambiya usiku wa kuamkiya Ijumaa. Akasema kuniuliza wewe umeuona usiku wa kuamkiya Ijumaa? Nikajibu ndiyo na wameuona watu [wote] na wakafunga, na akafunga Muawiyya [piya] akasema Ibn 'Abbaas lakini sisi tumeuona mwezi usiku wa kuamkiya Jumamosi na tutaendeleya kufunga mpaka tukamilishe siku 30, au tuuone[wenyewe], nikamwambiya [Ibn 'Abbaas] je, hukutosheka kwa kuuona Muawiyya na kufunga kwake akajibu kwa kusema, "hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)."
Ndugu Waislamu hii ndiyo dalili kubwa ya wenye kuhalalisha kila nchi kuwa na mwezi mwandamo wake kwa hakika hawana dalili nyingine zaidi ya kisa hiki, hebu tukichambuwe kwa undani sote ili kila mmoja wetu apate faida je kinafaa kuwa ni dalili ya kutegemeya?
KUMJADILI KURAYBU NA UCHAMBUZI WA KISA HIKI
Kwanza watukufu Waislam kabla hatujasogeya kwenda mbali inabidi mpate faida kumjuwa huyu Kuraybu ni nani? Hili jina la Kuraybu ni la baba yake ambaye na wanachuwoni wa hadith wanamkubali huyu baba yake kuwa alikuwa mtu mkweli sana na anategemewa katika upokezi wa hadithi tazama kitabu 'Tahdhibu' cha Imam Ibn Hajar Al 'Asqalani [jalada la 3 uk 468 chapa ya Beirut tazama mahala pa herufi kaaf] Na tazama vile katika Taqribu Tahdhibu cha huyu huyu Ibn Hajar Al Asqalani jalada la 2, uk 28. Lakini huyu aliye katika kadhiya hii na Ibn 'Abbaas jina lake kamili ni Muhamad Ibn Kuraybu Ibn Abi Muslim Al Hashimiy alikuwa ni mtumwa wa Ibn 'Abbaasi na mama yake Ibn 'Abbaasi Umul Fadhli alikuwa akimtuma sana kwenda Shamu kwa Muawiyya.
Na yeye huyu si Sahaba bali ni katika tabiin na si mtu wa kuaminika katika elimu ya hadith hakubaliki. Hebu tuwasikilize wanachuwoni wetu wa hadith wanavyomchambuwa huyu Muhamad Bin Kuraybu. Amesema Athram toka kwa Ahmad bin Hanbal kuwa, "Huyu Muhammad Bin Kuraybu hadith zake ni 'Munkar" Na amesema Ad Duuriyu toka kwa Ibn Maiyn kuwa "Hadith zake huyu si chochote". Na amesema Ibn Numair; "upokezi wake haufai kabisa ni dhaifu". Na amesema Ibn Hatim toka kwa baba yake kuwa "Huyu Muhamad Bin Kuraybu hazitolewi hoja hadith zake". Na amesema Abi Zur'a kuwa "Hadith zake ni laini mno".
Na amesema Imam Al Bukhaariy kuwa "Hadith zake huyu ni za kuchunguzwa sana". Na akaendeleya kusema Imam Al Bukhaariy kuwa "Hadith zake huyu ni Munkar hazikubaliki". Kumbuka ndugu Muislamu pindi imam Al Bukhaariy anaposema kuwa hadith za mtu Fulani ni munkar basi wanachuwoni wote wa hadith wamekubaliyana kuwa zinawekwa upande wa dhaifu. Na amesema Imam An Nasaaiy "Huyu Muhamad Ibn Kuraybu ni dhaifu". Na vivyo amesema Imam Adaara Qutni. Na amesema Abubakar Al Athram: "Nilimuuliza Imam Ahmad Bin Hanbal kuhusiyana na hadith za huyu Muhamad Bin Kuraybu akasema 'Ni Munkar kwa sababu analeta hadith za ajabu kabisa".
Na amesema Imam Ibn Hibbaan kama alivyonukuliwa katika Mizanul i'tidali ya Imam Adh Dhahabi kuwa "Huyu Muhamad bin Kuraybu alikuwa ni mudalisi [mrongo]". Na amesema Abu Na'im Ad Damishqi kuwa, "Huyu Muhammad Bin Kuraybu alikuwa anachanganya hadith sahihi na dhaifu". Kumbuka ndugu Muislamu hakuna hata mwanachuwoni mmoja wa hadith aliyemtaja huyu Muhamad Ibn Kuraybu kuwa ni mkweli." Mwisho wa kunukuu.
NASAHA
Kabla sijaanza kutoa jawabu juu ya maneno haya, ningependa kutoa nasaha zangu kwa muandishi wa makala. Tunamuomba muandishi wa makala amche Mungu; akumbuke siku ya hisabu; asiseme kitu asichokijua juu ya Mwenyezi Mungu au Mtume wake au dini yake akapoteza watu bila ya elimu. Allah anasema:"Wala usifutilie usichokuwa na elimu nacho." Na anasema: "Sema hakika Mola wangu kakataza maovu na (kakukatazeni nyinyi) kusema musichokijua."
Na akasema"Na ni nani aliyedhalimu zaidi (wa nafsi yake) kuliko anayemzulia Allah uwongo ili awapoteze watu bila ya elimu."
Na halkadhalika Mtume(s.a.w.w)
katoa indhari kubwa katika Hadithi kadha wa kadha kuhusu mtu kusema kitu asichokijua akawapoteza watu. Aya zote hizo zinatupa indhari juu ya kusema kitu katika dini ya Allah bila ya kuwa na ujuzi nacho.
JAWABU
Baada ya nasaha hizo sasa natotoe jawabu juu ya baadhi ya nukta (points) za makala hio, tukianzia na Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas na khususan kuhusu sanad ya Hadithi hio. Jawabu ni kuwa muandishi wa makala kachanganya mambo! Amesema kitu ambacho hata hao wanavyuoni wakubwa wa Hadithi hata waliopinga kutoa ushahidi kwa Hadithi ya Kurayb hawakukisema. Sijui Sheikh umepata wapi kwamba Hadithi hii imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Kurayb!!!!!!!!! Kama yupo basi naye tutamdai ushahidi kama tunavyokudai wewe ewe Sheikh muandishi wa makala. Sanad ya Hadithi hii katika masimulizi ya Muslim na wengine ni: "Yahya bin Yahya (bin Bukair) katupa habari Ismail bin Ja'afar kutoka kwa Muhammad (naye ni Muhammad bin Abi Harmala) kutoka kwa Kurayb." Hii ndio sanad ya Hadithi hii. Sasa sijui ni nani aliye dhaifu katika wapokezi hawa?!
Ama Muhammad bin Kurayb unayemzungumzia wewe, yeye hayumo katika sanad hii wala katika Hadithi hii kamwe. Na ushahidi wa haya ni kwamba Hadithi hii imepokewa na: Muslim Sahihu Muslim, Al-Tirmidhi Al-Sunan, Abu Daud Al-Sunan Al-Nnasai Al-Kubra Al-Bayhaqi Al-Kubra Ibn Khuzaima Al-Sahih. Wakati Muhammad bin Kurayb aliye dhaifu - ambaye ni mtoto wa Kurayb aliyekuwa mtumwa mkombolewa wa Ibn Abbaas: yaani baba na mwana wote walikuwa ni Mawali (Freed slaves) wa Ibn Abbaas - unayemzungumzia wewe yeye ni mpokezi wa Ibn Maja tu katika wapokezi sita: wapokezi wengine hawakupokea Hadithi kutoka kwake; wakati Hadithi hii imepokewa na Muslim na hao wengine niliowataja. Kwa hivyo, Muhammad aliyetajwa katika sanad ya Muslim na wengine si Muhammad bin Kurayb bali ni Muhammad bin Abi Harmala naye ni mmoja wa wanafunzi wa Kurayb , baba mtu. Tafadhali rejea hayo hayo Maraji'u (Referernces) uliyotupa yaani Tahdhibu Al-Tahdhib cha Ibn Hajar. Tazama vizuri mfumo wa Ibn Hajar katika kitabu hicho: utaona kwamba kabla ya kumtaja mpokezi juu hukuekea nani aliyesimulia Hadithi kutoka kwake katika wasimulizi sita wakuu wa Kisuni. Na ukitazama hapo utaona kwamba Muhammad bin Kurayb ni msimulizi wa Ibn Maja: si Muslim na wengine: wakati Hadithi hii imesimuliwa na Muslim na wengine.
Kwa ufafanuzi zaidi, kwa vile utafiti wa sanad za Hadithi huwa hautazamwi kwa mpokezi mmoja, basi tazama sanad ya Al-Tirmidhi utaona sanad inasema kwa uwazi: .."Katuhadithia Muhammad bin Abi Harmala katupa habari Kurayb ". Na katika masimulizi ya Abu Daud: ".Katupa habari Muhammad bin Abi Harmala katupa Habari Kurayb" Na katika masimulizi ya Ibn Khuzaima: "Kutoka kwa Muhammad (yaani bin Abi Harmala) k utoka kwa Kurayb". Na katika masimulizi ya Al-Nasaai: "Katuhadithia Muhammad - naye ni Ibn Abi Harmala - kasema kanipa habari Kurayb". Na katika masimulizi ya Al-Bayhaqi: "Kutoka kwa Muhammad bin Abi Harmala kutoka kwa Kuraib".
Kwa hivyo, dai hilo kwamba Hadithi hii imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Kurayb si dai sahihi bali ni kutaka kulazimisha kuwa Hadithi hii lazima iwe dhaifu na kwa hivyo kama hakuna mpokezi dhaifu katika Sanad yake basi akachukuliwe mwengine ukooo apachikwe ilimradi Sanad iwe dhaifu, lakini ushahidi wa udhaifu haupo hata mukiomba msada kwa binaadamu wote na majini wote. Bali kama tulivyosema kwamba hata wasiokubaliana na kutoa ushahidi kwa Hadithi hii miongoni mwa wanavyuoni wakubwa kama Al-Shaukani, hawasemi kuwa hii ni Hadithi yenye sanad dhaifu wala hawasemi kuwa imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Kurayb, bali wanasalim amri mbele ya usahihi wa Sanad ya Hadithi hii, tafauti ni katika kuifahamu tu: Al-Shaukani - kwa mfano - akadai kuwa hii ni ijtihad ya Ibn Abbaas, nalo ni kosa kama tulivyobainisha katika kitabu Ushahidi Uliowekwa Wazi.
MATN YA RIWAYA YA KURAYB NA IBN ABBAAS
Baada ya muandishi kutupa utafiti wake wa sanad ya riwaya ya Kurayb, alitupa utafiti wake juu ya matn (text) ya riwaya hio, akasema: "Baada ya kumaliza kumkaguwa huyu Kuraybu ebu sasa ndugu Muislamu tuje kukikaguwa kisa chenyewe, tukianza na qauli ya Ibn 'Abbaas kukataa kufunguliya kwa mwezi ulioonekana katika mji wa Shamu kasema Imam Alqarafi katika kitabu cha "Adhakhira" ya kuwa, "Siku ile habari ya mwezi alipopewa Ibn 'Abbaas kutoka kwa Kuraybu kulikuwa hakuna mawingu yaliyotandaa katika mji wa Madina, na wala haukuonekana mwezi siku hiyo, Ibn 'Abbaas akatanguliza kuuona yeye mwezi kuliko ile habari au taarifa alioletewa na Kuraybu, na ndiyo maana akasema: "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa maana tusichukuwe habari za dhana na tukaacha yakini, japokuwa hakuna tafauti ya kuutazamiya mwezi kukiwa kuna mawingu au hakuna mawingu, lakini yeye alihukumu kwa kuuona mwezi. Anasema Imam Alqarafi kuwa "Hiki kisa kishakuwa na utata mkubwa".
Na qauli ya Ibn 'Abbaas ya kukataa kufunguliya mwezi ulioonekana Shamu na kusema hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akaishiya hapo hakuendeleya na wala hakufafanuwa zaidi na kisa hiki kikaishiya hapo. Na utata ukawa mkubwa katika safu za Waislamu kutokana na kutokupatikana ufafanuzi zaidi juu ya kisa hiki." Mwisho wa kunukuu. Tunasema: Habari ya Kurayb alioitoa ilikuwa inahusu mwezi muandamo wa mfungo: si wa mfunguo, kama riwaya yenyewe inavyosema: "Ukaniindamia mwezi wa Ramadhani (si wa Shawali) nami niko Sham" na mwezi muandamo wa mfungo unathibiti kwa ushahidi wa mtu moja muadilifu kama wewe mwenyewe Sheikh ulivyotwambia katika makala yako kwamba: "Akiona mwezisayari mtu mmoja na akatoa habari kwa wengine katika eneo lina kiongozi wa Kiislam itawalazimu watu wote wafunge." Kwa maana hii hakuna maana ya kuiita habari ya Kurayb kuwa ni habari ya dhana kwani habari ya dhana yaani ya mtu mmoja inakubalika katika mwezi Muandamo kama vile Mtume(s.a.w.a)
alivyoikubali habari ya Ibn 'Umar peke yake. Na kauli ya Al-Qarafi aliposema: "Hiki kisa kishakuwa na utata mkubwa" haina uwezo wa kuibatilisha riwaya hii baada ya kuthibiti kwake kwa sanad sahihi.
Anaendelea Sheikh muandishi wa makala kwa kusema: "Sasa basi tujiulize sote kwa pamoja kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nini? Wamekhitilafiyana wanazuwoni katika makundi manane juu ya hii amri anayosema Ibn 'Abbaas kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
1) "Kundi la kwanza la wanazuwoni wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asifunge wala kufunguwa katika siku itakayokuwa mawingu yametanda angani wakamilishe 30 Shaabaan au 30 Ramadhaan."
Tunasema: Nayo hii ni kauli ilio na udhaifu wa wazi. Kwani maudhui ni kuwa mwezi umeonekana Sham kabla ya Madina, ikiwa Ibn Abbaas aliuzingatia muandamo wa Sham basi asingelisema kuwa "Hatutoacha kufunga hadi tutimize siku thalathini au tuuone mwezi," kwani kutimiza siku thalathini Madina ni kutimiza siku thalathini na moja huko Sham. Na kwa vile hakuna mwezi wa siku thalathini na moja, basi kwa vyovyote vile Ibn Abbaas kama aliukubali muandamo wa Sham alikuwa atimize siku 29 tu kwani wakati huo itakuwa Sham mwezi kwa hakika umeshamalizika. Ama dai kwamba "Kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asifunge wala kufunguwa katika siku itakayokuwa mawingu yametanda angani wakamilishe 30 Shaabaan au 30 Ramadhaan" halihusiani na tokeo hili kamwe kwani hapa maudhui ni kuwa mwezi umeonekana Sham lakini haukufatwa Madina: hakuna suala la mawingu hapa.
Anasema muandishi:
2) "Kundi la pili wao wanasema: "Kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asipokee taarifa ya kufunga au kufunguwa kutoka kwa mtumwa kwa sababu wale wote walioleta habari ya mwezi wa kufunga au kufunguwa zama za Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa si watumwa, na Kuraybu alikuwa ni mtumwa wa Ibn 'Abbaas (radhiya Allahu 'anhu)." Tunasema: Na hii pia ni kauli dhaifu, kwani Kurayb hakuwa mtumwa ambaye kamilikiwa, bali ni Maula yaani mtu aliyekombolewa kutoka katika utumwa, na mawla (freed slave) hukumu zake katika Uislamu ni sawa na Muislamu yeyote yule. Anasema muandishi:
3) "Kundi la tatu wao wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asipokee taarifa au habari ya mwezi kutoka kwa mtu mmoja tu mpaka apatikane mwingine mwenye kumshuhudiya huyo mtowa habari." Tunasema: Na hii pia ni kauli dhaifu kwani Mtume(s.a.w.w)
kapokea habari ya bedui peke yake nayo japokuwa ni hadithi yenye sanad dhaifu lakini maana yake ni sahihi kwani katika Hadithi nyengine tunapata kwamba Mtume(s.a.w.w)
pia alipokea habari iliotolewa na Ibn Umar peke yake. Wala lisipingwe hili kwamba hii ilikuwa ni mahususi kwa Mtume(s.a.w.w)
kwani tunasema kwamba matendo ya Mtume(s.a.w.w)
ndio kigezo kwa Umma wake ila ikiwa kutakuwa na ushahidi kuwa kitendo kadha ni kwa ajili yake tu. Bali Ibn 'Umar - kama ilivyo katika riwaya alioisimulia Ibn Abi Shaiba kama utavyoona katika kitabu - kaujuzisha ushahidi wa mtu mmoja peke yake na watu wa Madina wakafunga kwa ushahidi huo.
Anasema muandishi:
4) "Kundi la nne wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yeyote yule atakayesafiri kutoka katika mji ambao haukuonekana mwezi na kuelekeya katika mji ambao umeonekana, basi hukumu yake atafunga pamoja na watu wa mji huo na atakuwa ni mmoja kati ya watu wa mji huwo. Kwa mujibu ya mafundisho haya ya Kuraybu, atatakiwa afunge siku 31."
Ninasema: Nadhani umebirukiza au msemaji kabirukiza: nadhani sahihi ni kusema: "Atakayesafiri kutoka katika mji ambao umeonekana mwezi na kuelekeya katika mji ambao haukuonekana" nadhani hivi ndio sahihi ili rai hii iweze kuwiyana na matokeo yalivyotokea. Nayo pia ni kauli dhaifu kwani haihusiani na mjadala wa Ibn Abbaas na Kurayb kwani msafiri alikuwa ni Kurayb wakati aliyekataa kuufata muandamo wa mbali ni Ibn Abbaas naye alikuwa Madina: hakuwa msafiri. Anasema muandishi:
5) Kundi la tano wao wamesema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asikubali mwezi aliyouona Muawiyya kwa sababu mtazamo wake yeye Ibn 'Abbaas (radhiya Allahu 'anhu) alikuwa hautambui utawala wa Muawiyya na alisimama pamoja na Aliy bin Abi Twalibu dhidi ya Muawiyya. Kwa mafundisho haya asikubali mwezi ulioonekana na kiyongozi asiyetambulika.
: Nayo pia ni kauli dhaifu kwani kama tulivyoeleza katika kitabu:
a) Mwezi wa Sham haukuonekana na Mu'awiya tu, bali Kurayb kasema kwa uwazi: "Na watu wakauona na wakafunga." Na alipoulizwa Kurayb "Wewe umeuona?" Akasema: "Ndio." Kwa hivyo, dai hilo halina muelekeo kwani mwezi umeonekana na Mu'awiya, na Kurayb na watu wa Sham. Wala suala la kuonekana kwa mwezi halina uhusiano na uovu wa utawala ikiwa Waislamu wameuona.
b) Ibn Abbas katoa sababu ya kuukataa muandamo huo, hatuna haja ya kumtilia maneno katika kinywa chake. Sababu yake ni kuwa "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume s.a.w." Kwa hivyo, kudai kwamba Ibn Abbas kaukataa muandamo huo kwa sababu ya uasi wa Mu'awiya, ni kutoa sababu tafauti na ile ambayo Ibn Abbas mwenyewe kaisema kwa uwazi. Anasema muandishi:
6) "Kundi la sita wamesema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asikubali kufunguwa na kulipa siku badala yake ile waliokula mchana na isipokuwa kwa mashahidi wawili kwa hilo kuhofiya kuwalipisha watu funga ya siku moja iliyowapita kutokana na taarifa ya mtu mmoja".
Ninasema: Na hii pia ni kauli dhaifu kwani - kama tulivyosema - Ibn Abbaas kaukataa muandamo wa mfungo wa Ramadhani: si muandamo wa mfunguo wa Shawaal, na muandamo wa mfungo - kama tulivyosema na kama riwaya zinavyonena kwa uwazi - hauhitaji mashahidi wawili, bali shahidi mmoja anatosha kama wewe mwenyewe pia ulivyotuandikia. Anasema muandishi:
7) "Kundi la saba wanasema kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila nchi ina machomozo ya mwezisayari wake na masafa yake, na masafa yanayokusudiwa ni KM 133.056.
Ninasema: Kauli hii ina usahihi na udhaifu na upungufu. Usahihi ni kuwa tafauti za machomozo ya mwezi ni lazima zizingatiwe kwa mujibu wa Qiyas (analogy) sahihi kama zinavyozingatiwa tafauti za machomozo ya jua. Upungufu ni kuwa Illa (sababu) katika tokeo hili ni murakkaba (yaani sababu ni mbili kwa pamoja: si moja: si machomozo tu: ni machomozo na umbali). Udhaifu ni kuukadiria umbali huu kwa KM 133.056. Maelezo zaidi juu ya hili ni katika kitabu. Kundi la nane alilotuahidi Sheikh muandishi wa makala hakututajia.
TANBIHI
Sasa cha kuzingatia hapa ni kuwa tafauti hizi alizotunakilia Sheikh muandishi wa makala katika kuifasiri riwaya ya Kurayb na Ibn Abbaas hazijaifanya riwaya hio kuwa ni dhaifu, vyenginvyo riwaya kadha wa kadha ambazo ni sahihi kwa makubaliano ya Umma basi wanavyuoni hutafautina katika kuzifasiri hadi kufikia makumi ya rai na zaidi. Hadithi Innamaa Al-A'amalu binniyyaat (Hakika ya matendo ni kwa nia) ni sahihi kwa makubaliano ya Umma, lakini w anavyuoni wametafautiana juu ya maana yake. Je tafauti zao juu ya tafsiri sahihi zitabatilisha usahihi wa Hadithi hii? Bali Aya zote za Qur-ani taqriban zina kauli tafauti za wafasirina juu ya tafsiri gani ya Aya hizo ilio sahihi. Je tafauti katika tafsiri hizo zibatilishe uhakika na ukweli na kuthibiti kwa Aya hizo?! Kwa hivyo, tunasema suala la muandishi aliposema: "Sasa basi tujiulize sote kwa pamoja kaamrishwa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nini? Jawabu ni kuwa baada ya kuzikusanya illa (sababu) zote zinazofaa kuwa illa ya hukumu hii, illa pekeye inayofaa kuwa illa ya hukumu hio ni umbali uliopo baina ya nchi mbili hizo - Sham na Madina. Na tafauti ya machomozo zinatokana na umbali na hizi zinathibiti kwa njia ya Qiyas (analogy) sahihi kama tulivyobainisha katika kitabu.
DAI LA PILI
Watu wengi wenye msimamo wa kufunga kwa muandamo mmoja utasikia mitaani wakisema: "Kile cha Kurayb na Ibn Abbaas ni kisa: si Hadithi!" Kwa baahati mbaya watu kama hawa wanapopata watu waliopapasa karatasi mbili tatu za vitabu wakawambia hivyo hivyo basi huzidi kuamini kwamba hile si Hadithi bali ni kisa. Na hapa muandishi wa makala anatwambia hivi: "Hoja yao kubwa siyo Qur-aan wala Sunnah ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambavyo ndiyo dira yetu tunapokhitilafiyana kama alivyosema Allah Taa'ala katika Qur-aan " Na kama mkikhitilafiyana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, hiyo ndiyo kheri nayo ina matokeo b ora kabisa."
Hoja kubwa ya wenye kuhalalisha kila nchi kuwa na mwezi wake ni moja tu nayo ni kisa cha Kuraybu mtumwa wa Ibn 'Abbaas..". Mwisho wa kunukuu.
Jawabu Sasa tukuulizeni enyi muliosoma elimu ya Hadithi kwani Hadithi ni nini? Wataalamu wa Hadithi wana hiki cha kutwambia:
1) "Kauli ya Sahaba (ataposema): tumeamrishwa kadha au tumekatazwa kadha.na iliofanana na hio, basi kilichosahihi ni kuwa zote hizo hupewa hukumu ya (Hadithi) marfu'u (huzingatiwa kuwa ni Hadithi iliotoka kwa Mtume s.a.w.)."
2) "Ikiwa Sahaba ataitaja amri kwa uwazi akasema kwa mfano: 'Mtume (s.a.w.) katuamrisha, basi hakuna khilafu (ya wanavyuoni) ndani yake (hiyo ni Hadithi marfu'u: ni Hadithi ya Mtume(s.a.w.w)
." Al-Suyuti Tadribu Al-Rawi uk. 161.
3) "Ama Sahaba akileta lafdhi yenye uwezekano wa kuwepo mtu mwengine baina yake na Mtume(s.a.w.w)
, kwa mfano akisema: 'Mtume kasema kadha au kaamrisha kadha au kakataza kadha au kahukumu kadha basi Jumhur inasema kuwa (kauli hio) ni hoja (katika hoja za Kisharia)". Al-Shaukani Irshadu Al-Fuhul uk. 92 Faslu Fii Alfadhi Al-Riwaya. Na mfano wake ni maelezo ya Al-Imamu Al-Ghazali katika Al-Mustasfaa uk. 104 Al-Muqaddimatu Fii Bayani Alfadhi Al-Sahaba.
4) "Na katika hio ni kauli ya Sahaba anayejulikana kwa usahaba (wake): (ataposema kwamba) 'Tumeamrishwa tufanye kadha" na"Tumekatazwa kutokana na kadha wa kadha"
na "Tulikuwa tunaamrishwa kadha" na "Tulikuwa tunakatazwa kadha"
.Ikiwa atayasema hayo Sahaba anayejulikana kwa usahaba (yaani anayejulikana kuwa ni Sahaba), basi hio (inazingatiwa kuwa ) ni Hadithi musnad (kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
na zote hizo zimepokewa katika Masanid (Hadithi zilizotoka kwa Mtume(s.a.w.w)
. Tazama Al-Hakim Ma'arifatu 'Ulumu Al-Hadith uk. 22 katika Dhikru Al-Naw'i Al-Sadis.
5) "Sahaba akisema: 'Nimemsikia Mtume(s.a.w.w)
anaamrisha kadha au anakataza kadha".(basi kauli) inayotegemewa na walio wengi ni kuwa hio ni hoja"
. Al-Aamidi Al-Ihkam j. 2, uk. 325.
6) "Na kauli ya Sahaba (ataposema):'Tumeamrishwa kadha' au 'Tumekatazwa kadha'
ni (Hadithi) Marfu'u, Musnad (yaani inazingatiwa kuwa ni Hadithi kutoka kwa Mtume mwenyewe(s.a.w.w)
kwa Wanavyuoni wa Hadithi, nayo ndio kauli ya wanavyuoni wengi." Ibn Kathir 'Ulumu Al-Hadith j. 1, uk. 150. Anasema Sheikh Ahmad Shakir katika maelezo yake ya chini katika kitabu hicho: "Nayo ndio (kauli) sahihi."
Sasa mukhtasar wa haya ni kuwa wanavyuoni taqriban wote wamekubaliana bali wengine wamenukuu makubaliano kwamba Sahaba akisema "Mtume(s.a.w.w)
katuamuru kadha au katukataza kadha," basi hio inazingatiwa kuwa ni Hadithi ya Mtume(s.a.w.w)
wala si lazima kuwa Sahaba huyo ainukuu lafdhi alioitamka Mtume(s.a.w.w)
. Na mifano ya Hadithi za namna hio ziliokubalika iko mingi sana katika vitabu vya Hadithi. Mfano mmoja ni Hadithi alioipokea Al-Bukhari katika Sahihu yake Hadithi na. 578 na Muslim katika Sahihu yake Hadithi na. 378 "Kutoka kwa Anas kasema: 'Bilal aliamrishwa aifanye adhana kuwa ni shafi'i (Even) na Iqama aifanye kuwa ni witr (Odd)". Utaona kwamba Sahaba hapa kasema tu kwamba Bilal kaamrishwa bila ya kuinukuu lafdhi alioitamka Mtume(s.a.w.w)
kumwambia au kumuamuru Bilal kwayo. Na hii imezingatiwa kuwa ni Hadithi ya Mtume(s.a.w.w)
Sasa ukirudi kuitazama riwaya ya Ibn Abbaas na Kurayb, utamkuta Ibn Abbaas anasema:"Hivi (ninavosema au ninavyofanya mimi) ndivyo alivyotuamrisha Mtume (s.a.w.w)".
Kwa hivyo, hii ni Hadithi marfuu yenye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
, na kuitwa kuwa ni kisa haina maana kuwa si Hadithi. Bali Hadithi nyingi ambazo ndani yake muna matokeo fulani huitwa kuwa ni visa wala haina maana kuwa hizo si Hadithi. Kisa cha Sahaba Tha'alaba kwa mfano - nacho ni dhaifu - kinaitwa kisa na kinaitwa Hadithi. Kimeitwa kisa kwa sababu ya matokeo yaliokuwemo ndani yake na kimeitwa Hadithi kwa kuhusishwa nacho Mtume(s.a.w.w)
. Mimi nahofia kuwa hawa watu wenye fahamu kama hizi kesho watakuja kutwambia kwamba baadhi ya Aya za Suratu Al-Qasas (Sura yenye visa vya Musa na Fir'awna na wengine) si Qur-ani bali ni visa tu kwani imeitwa Sura yenye visa!!!!!!!!!!!! Kwa hivyo, kuyaita maneno ya Ibn Abbaas yasemayo "Hivi (ninavosema au ninavyofanya mimi) ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w)
", kuwa ni kisa kwa maana kwamba si Sunna (Hadithi) ya Mtume(s.a.w.w)
ni kwenda kinyume na kanuni za Elimu ya Hadithi na kanuni za Usulu Al-Fiqhi.
DAI LA TATU
Muandishi anasema: "Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe katika maisha yake kafunga Ramadhan 9 kauona mwezi kwa macho yake mara 2 kaletewa habari za mwezi mara 3 toka Madina na mara 4 toka nje".
JAWABU
Sijui ndugu muandishi unakusudia nini kwa kusema "Na mara 4 toka nje". Je ni kutoka Oman, Yemen, Sham au wapi? Mara zote alizopewa habari ilikuwa ni habari kutoka Madina: wakati mwengine ilikuwa ni habari kutoka katika miji ya Madina na mara nyengine ni habari kutoka katika jangwa la Madina. Kwa hivyo, zote ni habari za Madina.
Hizi ndio nukta muhimu zilizokuemo katika makala ya Muandishi. Ama mengine yote alioyasema tumeyajadili katika kitabu ambacho tutakiambatanisha na makala hii ili wale ambao hawakukipata kitabu hicho waweze kuona hoja za pande zote na mdahalo juu ya hoja hizo.