17
MUANDAMO WA MWEZI
SEHEMU YA KUMI NA SITA
LAYLATUL- QADRI
MUNASEMA
Laylatul- Qadri: Maelezo Juu Ya Kupatikana Kwa Usiku Ni vyema kujikumbusha kwamba maelezo ya kisayansi yaliyopatikana kwenye Qur-aan Tukufu yanazingatia kwamba "Nyakati" hupatikana kutokana na mipinduko ya jua, mwezi na dunia. Hapana shaka yoyote dunia ina mizunguko yake miwili. Kwanza kuna ule mzunguko wa dunia kulizunguka jua, ambapo mzunguko huo husababisha mabadiliko ya miongo (seasons) mbali mbali kama vile mchoo, vuli, kipupwe au kiangazi. Pili ni ule mzunguko wa dunia kujizunguka yenyewe katika mhimili wake, mzunguko huu wa pili ndio unaosababisha kupatikana usiku na mchana. Kwa kawaida dunia hujizunguka yenyewe kamili kwa muda wa masaa 24 ambayo hupatikana siku moja yenye usiku mmoja na mchana mmoja.
Ni vyema ikumbukwe kwamba hakuna nchi yoyote duniani iliyotafautiana na nchi nyengine katika kupata usiku kwa masaa 24. Nchi zote duniani zinashirikiana katika usiku mmoja pia zinashirikiana katika mchana mmoja huo huo. Isipokuwa nchi nyengine hutangulia na nyengine zitafuatia nyuma.
JAWABU
Hebu tufahamisheni vipi: "Nchi zote duniani zinashirikiana katika usiku mmoja pia zinashirikiana katika mchana mmoja huo huo. Isipokuwa nchi nyengine hutangulia na nyengine zitafuatia nyuma". Mwisho wa kunukuu. Jamani mbona tunaambiana mabo yasio na ukweli! Nimekupeni mfano wa Hong Kong na U.S.A, bila shaka baadhi ya States zake, ambao nimeuona mwenyewe kwamba usiku na mchana haukutani katika nchi hizo, na ninavyodhani ni kuwa Canada na Hong Kong ni hivyo hivyo.
MNASEMA
Sasa tukirudi nyuma katika maelezo ya ndugu Juma katika kuelezea Laylatul-Qadri kwa kupitia fani hii ya Jiografia anaeleza kama ifuatavyo: (Sasa nchi ambazo zimepishana na Makka kwa masaa 12 au zaidi hazitopata nazo LAILATUL-QADRI, kwani LAILATUL-QADRI mwisho wake ni kuchomoza Alfajiri kama Qur-an ilivyosema, na wakati huu kuna nchi bado ni jioni. Sasa vipi hawa wao hawamo au na wao watapata zamu yao baadae?)
Hayo tumeshayaeleza sana kwamba hakuna nchi iliyopishana na nyengine kwa masaa zaidi ya 12. Wala hakuna nchi ya Kiislamu iliyopishana na nchi nyengine ya Kiislamu kwa zaidi ya masaa 9. Kama kweli ndugu Juma anaelewa mambo, ingekuwa jambo la busara akaeleza kwa mfano nchi zote za Kiarabu zina tofauti gani ya usiku au mchana? Au Ulaya (Europe) nzima ina tofauti gani katika kupata usiku au mchana wao? Huku akizingatia kwamba kuna nchi moja kama Canada iliyo na ukubwa kuliko bara zima la Ulaya.
Mara nyinyi tumekuwa tukimfahamisha ndugu Juma kuwa anapojadili jambo lililoambatana na fani fulani basi alijadili jambo hilo kwa kupitia njia sahihi zenye kukubalika kwa mujibu wa fani hiyo. Hususan anapojadili mas-ala ambayo yanahitaji madondoo muhimu kuliko maneno matupu. Kwa uchunguzi zaidi juu ya maelezo ya ndugu Juma tutakuta kuwa hakuweza kutoa ushahidi wa kina hasa anapoelezea tofauti iliyopo katika kutofautiana na baadhi ya nchi juu ya suala zima la kuingia usiku na mchana.
JAWABU
Haya! Hakuna nchi iliopishana na mwenziwe kwa zaidi ya masaa kumi na mbili, je iko iliopishana na mwenziwe kwa masaa hayo kumi na mbili? Je ikiingia alfajiri huko Makka watu hao kwao itakuwa ni saa ngapi hasa siku za joto ambapo Makka Alfajiri yake inaingia saa 10 za usiku. Kama huku saa 10 za usiku, Alfajiri imeingia kule kwenye tafauti ya masaa 12 itakuwa saa ngapi: si itakuwa bado ni jioni? Sasa kama ni jioni, na LAILATUL-QADRI mwisho wake ni alfajiri sasa hoja yenu iko wapi? Kwa ufupi ni kuwa suala hili nilikuwa nikijibu nukta alioileta Sheikh Nassor. Ni vyema nikanukuu hoja yake na jawabu kamili.
Maelezo kamili ni kama inavyofata. Nilisema: Suala jengine ni suala la LAILATUL-QADRI, nayo ni hoja ya mitaani safi. Ufupisho wa hoja hii ni kuwa usiku huo wa Lailatu Al-qadri ni mmoja na unakuwa katika tarehe za witri (Odd numbers: 21-23-25-27-29) za kumi la mwisho. Wakati tokeo hilo hutokea usiku mmoja tu. Sasa kama kila mji au kila nchi watafata muandamo wao, hii ina maana usiku wa mwezi 27 Saudia ni mwezi 26, kwetu. Sasa ni usiku wa nchi gani? Hayo ndio maelezo ya Sheikh Nassor Bachoo kwa ufupi. Kisha nami nikjibu: Tunasema kwamba: suala hili lingekuwa sahihi lau ingelikuwa tuna hakika kwamba tarehe fulani ndio usiku huo wa LAILATUL-QADRI. Lakini hakuna anayejua, hata Mtume (s.a.w.) katika hio Hadithi kasema kausahau usiku huo. Labda na sisi tuulize kwamba je tukio hili ni la dunia nzima au ni la Makka tu. Nadhani jawabu ni "La dunia nzima." Sasa nchi ambazo zimepishana na Makka kwa masaa 12 au zaidi hazitopata nazo LAILATUL-QADRI, kwani LAILATUL-QADRI mwisho wake ni kuchomoza Alfajiri kama Qur-an ilivyosema, na wakati huu kuna nchi bado ni jioni. Sasa vipi hawa wao hawamo au na wao watapata zamu yao baadae? Kama wao watapata zamu yao baadae basi na sisi Pemba hatutokosa.
Kuanzia hapa utajua kwamba hakuna ulazima wa kuwa tarehe ziwe sawa katika tokeo hilo la LAILATUL-QADRI. Lakini kwa kufahamu zaidi udhaifu wa hoja hii, tazama ukweli kwamba Mtume(s.a.w.w)
anasema kwamba siku ya Ijumaa kuna Saa ambayo mtu akiisadifia naye yumo katika kusali na kuomba basi hupokelewa maombi yake. Ikiwa ni saa moja au mbili au tatu n.k, suala ni saa ya nchi gani? Cha kuzingatia zaidi ni kuwa wakati Makka ni mchana siku hio ya Ijumaa kuna nchi nyengine bado ni mwanzo wa usiku na jua likitua Makka nchi hizo ni asubuhi au alfajiri. Jawabu yako hapa ndio jawabu yetu kule. Hii ndio jawabu na - kimsingi - nadhani iko wazi kwamba tokeo la Lailatul Qadri si hoja ya kuwa na tarehe moja.
Munasema
Kuhusu Laylatul-Qadri: Bila shaka ni usiku mmoja unaotokea mara moja kila mwaka katika mwezi wa Ramadhaan. Hayo yanathibitishwa na Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) pale Anapoeleza asili ya siku yenyewe katika Qur-aan Tukufu pale aliposema:
﴿إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴾
"Hakika tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatul-Qadri (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa Ramadhaan"
. (87: 1) Katika kuifasiri Aya hii, Shaykh Abdallah Al-Farsy ametoa maelezo yafuatayo: "Qur-aan kama ijulikanavyo ilikuwa ikiteremshwa kidogo kidogo, basi siku ile iliyoanza kuteremshwa ilikuwa katika Laylatul-Qadri (usiku wenye heshima kubwa). Ndio ikaambiwa kuwa Qur-aan imeteremshwa katika Laylatul-Qadri, ni usiku mmoja mtukufu umo katika mwezi wa Ramadhaan, ambao umebarikiwa kuliko miezi alfu, yaani mtu akifanya amali njema katika usiku huo hupata thawabu kama za mwenye kufanya amali ile kwa zaidi ya miezi elfu, na mwenye kufanya maovu naye hupata dhambi za mwenye kufanya maovu kama yale kwa zaidi ya miezi elfu.
Na Mwenyezi Mungu Ameuficha usiku huu haujulikani ni upi, ili watu wajitahidi kufanya Ibada katika mwezi mzima wa Ramadhaan; lakini watarajiwa zaidi kuwa katika kumi la mwisho na hasa usiku wa kuamkia mwezi 23, 25, 27 na 29. Basi atakaye kujua yakini kuwa ameupata usiku huu, bila ya shaka, inamlazimu ajipinde na kufanya ibada mwezi mzima. Wala si lazima kwa mwenye kuupata usiku huu kuona alama yoyote." Kisha Shaykh Abdallah Al-Farsy akabainisha maneno kama hayo alipokuwa akiifasiri Suratud-Dukhaan kama ifuatavyo:
﴿إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ * فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ﴾
"Kwa yakini tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa, Katika (usiku) huu hubainishwa kila jambo la hikima"
. (44: 3, 4) Shaykh anaendelea kusema: "Hii 'Laylatin Mubaarakatin Fiyhaa yufraqu Kullu amriin Hakym." Dhahir Shahir hapa kuwa siku hii imo katika mwezi wa Ramadhaan kama yalivyobainishwa haya na Mwenyewe Mwenyezi Mungu katika Aya ya 185 ya Suratul-Baqarah." Ndugu yetu Juma yeye bado anahoji: (Sasa nchi ambazo zimepishana na Makka kwa masaa 12 au zaidi hazitopata nazo LAILATUL-QADRI, kwani LAILATUL-QADRI mwisho wake ni kuchomoza Alfajiri kama Qur-an ilivyosema, na wakati huu kuna nchi bado ni jioni. Sasa vipi hawa wao hawamo au na wao watapata zamu yao baadae?)
JAWABU
Sasa nini uhusiano wa nilioyasema na nakala mulizozitoa za Aya na maelezo ya Sheikh Al-Farisi? Jamani! Munasadiki kuwa hawa watu si watu wa kufahamu: basi wanapenda tu kitu!
MNASEMA
Sisi tunapenda kumuelimisha ndugu Juma kama ifuatavyo: Tunajifunza katika Aya za Qur-aan tulizozitaja kwamba Laylatul-Qadri ni usiku mmoja tu kwa ulimwengu mzima.
JAWABU
Ni sehemu gani ya Aya iliosema hivyo kwamba Laylatul-Qadri ni usiku mmoja tu kwa ulimwengu mzima? Hili ni jambo la ghaibu wala halikufafanuliwa, nyinyi munalisema bila ushahidi unaokubalika. Ikiwa dalilu dhanni haikubaliki katika itikadi, vipi mutasema kitu cha ghaib bila ya ushahidi. Mimi nimekujibuni kwamba ziko nchi ambazo zimetafautiana kwa muda wa masaa kumi na mbili wala hazikutani kamwe katika usiku wala mchana. Sasa kama Laylatul-Qadri ni siku moja katika usiku mmoja na kwa hivyo tarehe iwe moja na mfungo mmoja. Tunauliza Laylatul-Qadri mwisho wake ni wakati gani? Qur-ani imesema mwisho wake ni Alfajiri.
Tuchukulie mwezi mwanzo umeonekana Makka, kwa hivyo usiku wa Laylatul-Qadri Makka, alfajiri ya Makka Laylatul-Qadri itakuwa haipo tena. Sasa wale ambao kwao ni jioni je wao hawatopata Laylatul-Qadri? Kwa sababu hii, ndio maana nikaita hii kuwa ni hoja ya mitaani kwani mwenye elimu hasemi maneno haya kama ni hoja ya muandamo mmoja.
MNASEMA
Mwenyezi Mungu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta'ala) Anauadhimisha usiku huo kila mwaka mara moja ndani ya usiku huo kwa amani na baraka nyingi. Hakuna aliyesema kuwa usiku huo hutokea Makkah pekee au kwamba watu wote waitafute Laylatul-Qadri kwa usiku wa Makkah. Kinachozungumzwa hapa ni kwamba usiku huu ni mmoja kwa dunia yote ingawaje kuna nchi zenye kutangulia kabla ya nyengine. Labda ndugu Juma amechanganyikiwa baina ya usiku wa Laylatul-Qadri na 'Arafah, ambayo ilizungumzwa kwamba ibada ya funga ya 'Arafah ina uhusiano wa moja kwa moja na Uwanja wa 'Arafah ulioko Makkah. Kila eneo lina kupambazukiwa kwake na alfajiri kama ilivyo katika hukmu ya kula daku na kuanza kufuturu linapozama jua. Na hayo tumeshayaeleza sana kwamba hata katika nchi moja kubwa kuna kutafautiana alfajiri zao. Kama Dar es Salaam linazama na kuchomoza jua kwa zaidi ya dakika 40 kabla ya Kigoma.
JAWABU
Sikusema kuwa mumedai kwamba Laylatul-Qadri inatokea Makka tu, bali mimi nimenukuu mfano ule ule alioutoa Sheikh Nassor aliposema: "Pindipo itatokea kuwa Laylatul-Qadri? usiku wa 27 kule nchini S. Arabia". Na kwa ujmla bado hamujatoa jawabu katika suala hili kwamba ziko nchi ambazo tafauti ni masaa 12. Alfajiri ya nchi moja ni jioni ya nchi nyengine. Sasa kama Laylatul-Qadri inatoka usiku mmoja na mwisho wake ni alfajiri, tafadhali - musibabaishe - tuelezeni vipi wataupata usiku huo wale ambao bado kwao ni jioni wakati huku ushamalizika. Au kama watapata wao mwanzo huku itakuwa bado ni mchana; jua huku likitua kule alfajiri imechomoza na Laylatul-Qadri itakuwa haipo tena. Kwa kweli, kila mwenye akili - si mwenye elimu - anajua kuwa hii si hoja ya kuonesha kuwepo kwa muandamo mmoja.
18
MUANDAMO WA MWEZI
SEHEMU YA KUMI NA SABA
KUTUMIA QIYAAS CHA KUINGIA WAKATI WA SWALA KWA WAKATI WA SWAUM
MNASEMA
17. Kutumia Qiyaas Cha Kuingia Wakati Wa Swala Kwa Wakati Wa Swaum Katika kuutetea msimamo wake wa kufunga kwa kuzingatia "matlai", Ndugu Juma amejaribu kutoa hoja ya kutumia "Qiyaas" cha "Ibada ya Swala" kwa "Ibada ya Swaum." Kulinganisha kwake huko, Ndugu Juma anatoa taswira ya kuwa: " Kama ilivyokuwa hatuwezi kuswali kwa kufuata machweo ya jua ya nchi ya mbali, vile vile hatuwezi kufunga kwa kufuata nchi nyengine yoyote ile." Sisi kwa upande wetu tunapenda kumzindua ndugu Juma kwa haya yafuatayo: i). Kwanza hakuna mwanachuoni anayekubalika aliyewahi kutumia "Qiyaas" cha wakati wa Swala kwa wakati wa Swaumu katika mas-ala haya ya kuandama kwa mwezi.
JAWABU
Inaonesha mukisoma hamufahamu. Hao wanavyuoni wote waliofanya Qias, Qias chao ndio hicho - Qias cha jua na mwezi. Someni yafatayo kutoka kwa wanavyuoni wenye kuaminika: Mosi: Anasema Al-Imamu Abu Muslim: Na wakaukisia (muandamo wa mwezi kwa kuulinganisha) na kuchomoza alfajiri na (kuchomoza) jua na kutua kwake.
Pili
: Anasema Sheikh Al-Khalili alipokuwa akielezea suala hili: "Na kutenguka kwa jua (kwa mfano) katika mji fulani, hakupelekei kuingia wakati wa adhuhuri katika kila mji".
Tatu
: Anasema Al-imamu Al-nnawawi: "(Kauli ya) Pili: Haiwalazimu (funga watu wa miji ya mbali) kwani vyenye kuchomoza na vyenye kutua huenda vikatafautika kwa kutafautika miji, hakika kila watu wameamrishwa (kufata) mawio yao na machweo yao. Huoni kwamba alfajiri hutangulia kuchomoza kwake katika mji mmoja na kuchelewa mji wa pili, na vivyo hivyo jua: linatangulia kuzama kwake katika mji na linachelewa katika mji mwengine. Kisha kila mji unazingatia kuchomoza alfajiri yake na kuzama jua lake kuhusu watu wake (mji huo), basi vivyo hivyo mwezi muandamo."
Nne
: Anasema Sheikh Ibn 'Uthaimin: "Wakasema: 'Na vivyo hivyo tunasema kuhusu kauli ya Mtume(s.a.w.w)
:"Mukiuona fungeni na mukiuona fungueni."
Hakika atayekuwa katika sehemu ambayo haiwafikiani na sehemu ya aliyeuona (mwezi) katika matalai ya mwezi basi (mtu huyo anahisabiwa kwamba) hakuuona kwa uhakika wala kihukumu. Wakasema: 'Na wakati wa mwezi ni kama wakati wa siku. Kama vile ambavyo miji inavyotafautiana katika kuanza kujizuia (na kula na kunywa na jimai: yaani kuanza kufunga) na (inavyotafautiana katika) kufuturu kwa siku (daily), basi vivyo hivyo inawapasa watafautiane katika (kuanza) kujizuia na (katika kuanza) kufuturu kwa mwezi (monthly).
Na (kama) inavyojulikana kwamba tafauti za kisiku zina athari zake kwa makubaliano ya Waislamu. Waliyo upande wa mashariki, hakika wao wanaanza kufunga kabla ya waliyo upande wa magharibi na wanafuturu kabla yao. Je ndugu zangu mumewafahamu Maulamaa hawa wanasema nini? Je hakuna mwanachuoni aliyefanya Qias hicho? Hili ndio tatizo lenu: hamuoni tabu kusema kitu bila ya kukijua!
MNASEMA
ii). Pili tunapenda kumfahamisha ndugu Juma kwamba ziko nchi nyingi zinazofuata kama huo msimamo wake ambazo zinashirikiana kufunga siku moja, lakini haziswali wakati mmoja wala hazili daku wakati mmoja. Mfano nchi za Tanzania , Kenya na Uganda zinafunga siku moja lakini haziswali wakati mmoja. Wakati wa Swala kama ya "Adhuhuri" ya Dar es Salaam ni tofauti kabisa na wakati wa "Adhuhuri" ya Kampala .
JAWABU
Hili tumeshalielezea kuhusu suala la Dar na Kigoma, hatuna haja ya kukariri - suala ni moja na jawabu ni moja.
MNASEMA
iii). Wanavyuoni wanakubaliana kwamba kila eneo lina wakati wake wa kuanza kufuturu (kufungua Swaum) wakati wa magharibi linapozama jua, wakati wa kujizuilia kula daku inapokaribia alfajiri na pia kila eneo litatekeleza ibada ya swala zake zote tano kwa kuangalia mipinduko ya jua.
JAWABU
Na hili tushalikariri sana. Ufupisho wake ni kuwa kwa makubaliano hayo, ndio imejuzu kufanya Qias sahihi katika nchi zenye miandamo tafauti. Nayo ni kwamba, kama vile ambavyo watu wenye matalai tafauti ya jua wanavyotafautiana kufunga na kufungua, vivyo hivyo wenye matalai tafauti ya mwezi watafautiane katika kuanza kufunga na kufungua. Na ndio maana ya maneno ya Sheikh Ibn 'Uthaimin: "Na wakati wa mwezi ni kama wak ati wa siku. Na akasema: "Hiki ni Qias sahihi ambacho huwezi kukipinga".
MNASEMA
Na hata kama yupo mwanachuoni aliyesema kuwa Hadiyth fulani inawaruhusu watu wa nchi fulani ambapo wengine haiwaruhusu, maneno hayo pia hayawezi kuchukuliwa kama ni hoja sahihi na yenye mashiko madhubuti kwa sababu zifuatazo: Kwanza: Hadiyth zote zilizotaja wajibu wa kufunga na kufungua zimekuja kwa matamko ya kujumuisha Waumini wote popote walipo. Na kanuni ya Usulul-Fiqhi inatufahamisha tuendelee kushikamana na 'aam mpaka ipatikane Khaas. Pili: Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas bila ya kuonyesha dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu.
JAWABU
Haya yote tumeshayaeleza mara baada ya mara. Tumeeleza ni ujumla gani uliokuwemo katika Hadithi "Fungeni kwa kuuona", na kwamba hakuna dalili ndani yake kuwa watu wafunge kwa muandamo mmoja; bali kuna dalili kwamba watu wote lazima wafunge kwa kuuona, yaani kuuona iwe ndio sababu ya kufungwa. Hadit hi hii inaonesha sababu ya kufunga kwani Lamul Jarri iliokuwemo ndani yake inaitwa Ta'aliliya yaani ya kuonesha sababu ya amri iliotajwa. Hivi ndivyo kufasiri kwa mujibu wa fani. Ama khaas ni Riwaya ya Ibn Abbaas na Kuraib, alipoacha kuufata muandamo wa mbali na akasema "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume s.a.w.". Kwa hivyo, khaas imepatikana. Kwa hivyo, udhaifu uko kwenu kwa kutokuweza kuzifahamu dalili za Kisharia.
MNASEMA
iv). Tunapenda kusisitiza maneno yetu ya nyuma ya kwamba cha msingi ni kufunga Swaum na kufungua siku moja kwa Waislamu wote sio kufunga au kufungua kwa saa au dakika moja.
JAWABU
Hata hili haliwezekani. Kwani usiku wa baadhi ya nchi ni mchana kwengine na mcha wa baadhi ya nchi ni usiku kwengine wala hazikutani kamwe.
MNASEMA
v). Haiwezekani kutumika "Qiyaas" cha Swala na Swaum katika misingi ya Shari'ah kwani kwa hapa patakosekana nguzo za kufanyia "Qiyaas." Ni vyema tuelewe kwamba "Qiyaas" hutumika pale tu ambapo hakuna Aya wala Hadiyth juu ya jambo hilo Shar'iah ya Usulul-Fiqhi inasema ifuatavyo:
1. Angalia Kitabu: Kanuni zote hizo mbili zina maana ya kuwa: "Qiyaas" hakitumiki kwa kuwepo dalili za uwazi (yaani: Qur-aan na Hadiyth). Na jam bo hili la muandamo wa mwezi limetajwa wazi katika Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
JAWABU
Hio sio maana ya kanuni hio. Maana ya kanuni hio ni kuwa hakuna kufanya Qias chenye kugongana na andiko; sio Qias chenye kuwafikiana na andiko. Tegemeo la msingi la wenye kusisitiza kuwepo kwa miandamo tafauti ni Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas. Kwa hivyo, Qias hicho kinakwenda sawa na andiko.
MNASEMA
Wala huwezi kusema kila nchi itaswali wakati mmoja kwani kuna baadhi ya nchi moja kama ambayo ni kubwa sana , yenyewe ina tofauti ya masaa mengi kutoka eneo moja kwenda jengine.
JAWABU
Hili nalo tumeshalielezea zaidi ya mara moja. Mukhtasar wake ni kuwa hapaangaliwi nchi moja au mbili; kinachoangali ni umbali na kutafautiana kwa matalai. Pamoja na hivyo, kama tulivyoeleza, suala la umbali gani linatoa nafasi ya ijtihad kwa kutokuwepo andiko la wazi. Lakini suala la kufunga watu wote kwa muandamo mmoja ndio lililo kinyume na andiko na Qias sahihi pia.