2
MUANDAMO WA MWEZI
SURA YA PILI
JAWABU KWA WANAFUNZI WA BACHOO JAWABU YA UTANGULIZI
Wahusika ndugu zetu wa Masjid Al-Sunna Zanzibar, wameanza kitabu chao hicho kwa utangulizi wenye kumshukuru na kumuhimidi Allah na kumtakia rehema na amani Bwana wetu Muhammad (s.a.w.) kama zilivyo khutuba na vitabu vya kiislamu. Na hayo yote yamefanyika chini ya utangulizi wenye anwani:
UKWELI JUU YA KUANDAMA KWA MWEZI
Na hii ndio sehemu ya kwanza ya kitabu chao. Wakasema katika utangulizi huo: Msisitizo wetu mkubwa katika kitabu hiki ni ile nukta muhimu ya kwamba suala la kufunga na kufungua kwa muandamo mmoja kwa dunia nzima si jambo jipya kama wanavyodhani baadhi ya watu, ni jambo la kale mno ambalo linaweza kutekelezeka na kwamba huo ndio uliokuwa msimamo wa 'Jamhur' ya wanavyuoni.
Jawabu Nakubali kuwa hili ni jambo la zamani, lakini kudai kuwa hii ni kauli ya Jumhuri ni madai hewa: hayana ushahidi. Leo hii duniani hakuna madhehebu yoyote ambayo inaitendea kazi kauli hio kama ni madhehebu nzima, bali kuna baadhi ya watu tu katika kila madhehebu ambao wanafata kauli hio. Hata zile madhehebu ziliotajwa kuwa ni zenye kufata kauli hio kama vile Malik, Hanbal na Hanafi, basi hawaitendei kazi kauli hio ila baadhi yao tu. Libya, Algeria na nchi nyengine za Afrika Kaskazini na Magharibi - kwa mfano - ni nchi za wafuasi wa madhehebu ya Malik, nao wanafata miandamo yao wenyewe. Kwa hivyo, dai kuwa hii ni kauli ya Jumhur ya wanavyuoni, si dai sahihi.
SEHEMU YA PILI
Katika sehemu ya pili, ndugu waandishi wanasema:
2. Si Fikra Za Shaykh Naaswir Bachuu "Ndugu yetu Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui amejitahidi kuandika kitabu alichokiita: "Ushahidi Uliowekwa Wazi Katika Suala La Miandamo Ya Mwezi. Makusudio yake yalikuwa ni kutaka kukijibu kitabu kilichoandikwa na Shaykh Naaswir Abdullah Bachuu kinachojulikana kwa jina la "Ufafanuzi Wa Mgogoro Wa Kuandama Kwa Mwezi."
Jawabu Kidogo na mimi naomba niweke wazi kwamba kitabu changu hakikuwa kabisa na lengo la kujibu kitabu cha Sheikh Nassor Bachoo. Hili la kunukuu maneno yake na kuyajadili lilikuwa ni jambo la kutokea tu baada ya mtu Fulani kuniletea kitabu chake. Kwa havyo, kama mulivyosema nyinyi katika kitabu chenu kwamba: Kitabu hiki ni kama nasaha kwa Waislamu wote ili kuweza kudumisha umoja wetu hususan pale ambapo pamejitokeza misimamo tofauti katika mambo ya ibada. Wala lengo la kitabu hiki sio kuendeleza malumbano baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe hata kwa wale wenye misimamo tofauti. Kutajwa ndugu yetu Juma Muhammad Rashid lilikuwa ni jambo lisilobudi wala hapakuwa na lengo la kumkashifu au kumuumbua bali ni kutokana na kuwa hapakuweza kupatikana njia mbadala kwa vile ameshaandika kitabu ambacho ameshakichapisha chapa ya kwanza na ya pili.
Basi na mimi nakuombeni munielewe hivyo hivyo, kwamba wakati mimi naikubali fikra Fulani na kuikataa fikra Fulani, hakuna budi ninukuu fikra pinzani na kuonesha kwanini siikubali; na kwa upande wa pili ni lazima nioneshe kwanini naikubali fikra ninayoikubali. Na nitaposema kuwa kuna watu wana fikra hii, basi nadhani haitokuwa jambo la busara kama watu hao sikuwataja na nikiwataja ni lazima nitaje marejeo. Kwa sababu hii ndio maana nimekuwa nikinukuu maelezo ya Sheikh wetu Nassor Bachoo na kumjadili mule nisimokubaliana naye. Naomba musihuzunike kwani kujibizana katika kutafuta ukweli ni suala mashuhuri katika uwanja wa elimu. Wanavyuoni wakubwa wa kale na wa sasa wamekuwa wakijibizana ili kutafuta ukweli na hatimae huwabainikia woa pamoja na wasomaji. Kwa hivyo, hamukuwa na haja ya kutumia lugha: "Wala hapakuwa na lengo la kumkashifu": hii si kashfa hata kidogo: hii ni elimu.
Lakini, hakuna haja ya kufichana; kitabu chenu mumeandika kwa kujibu kitabu changu. Hamuna haja ya kusema: "Wala lengo la kitabu hiki sio kuendeleza malumbano baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe hata kwa wale wenye misimamo tofauti. Kutajwa ndugu yetu Juma Muhammad Rashid lilikuwa ni jambo lisilobudi wala hapakuwa na lengo la kumkashifu au kumuumbua bali ni kutokana na kuwa hapakuweza kupatikana njia mbadala kwa vile ameshaandika kitabu ambacho ameshakichapisha chapa ya kwanza na ya pili", kwani kitabuchenu kimeanza kwa kunitaja mimi mwanzo hadi mwisho na kuniaga kwa kunipa nasaha mimi. Ama mimi naandika jawabu hii kukujibuni nyinyi: sikufichini wala sisemi uwongo.
Munasema Kutokana na jambo hilo , sisi kwa upande mmoja tunashukuru kwa juhudi yake hiyo na kwa upande wa pili tunatuma masikitiko yetu kwake kwa kutokuwa makini na muadilifu katika kulifafanua jambo hilo muhimu. Kwani kitabu chake hicho kimeandikwa katika mfumo wa chuki, kibri, kejeli na malumbano huku akisisitiza kwa mara nyingi kauli chafu ambazo muandishi hapaswi kuzitumia katika kitabu au katika mijadala ya Dini. Jawabu Hizi chuki, kibri na kejeli, mimi nimezisoma kwenu, kwa hivyo na iwe kama msemo wa Waswahili: "Papa akipea mafuta huwapa wanawe". Je nyinyi munayakumbuka haya:
1) Munaukumbuka muhadhara wa Sheikh Bachoo ambao alisema kuwa wasionyanyua mikono katika sala wanasali kama mipopoo? Jamani! Hii si kejeli? Je katika nyinyi yuko aliyetoa muhadhara au kuandika kitabu ili kumjibu Sheikh wetu. Sasa uadilifu uko wapi?
2) Je munaukumbuka muhadhara wa Sheikh Bachoo aliozungumzia mas-ala ya udhu kasha akasema: "Wengine wakitia udhu kiungo hiki huomba dua hii na kiungo hiki huoma dua hii; upumbavu mtupu". Je haya si matusi? Je hii si kejeli?
3) Siku moja palikuwa na maziko. Maiti alisaliwa msikiti wa wajiitao "Watu wa Sunna". Kijana mmoja akasimama akasema: "Leo tunataka kukuonesheni vipi Mtume (s.a.w.) kamsalia maiti: si kama wanavyofanya Ibadhi na Shia.
4) La nne ni kuwa ikiwa nyinyi mumethubutu kunita mjeuri, mwenye kibri na kejeli; maneno ambayo mimi sikukwambieni wala kumwambia Sheikh Nassor; mimi nimemtoa makosa tu Sheikh wetu: na hii ni kawaida katika uwanja wa elimu; sasa je na nyinyi pia ni majeuri, wenye kibri na kejeli? Katika uwandishi wenu, pia mumesema: "Hatujui dhana hii potofu ameitoa wapi." Mwenye dhana potufu naye ni mpotufu, kwa hivyo na nyinyi hamukutoa nasaha bali mumetukana. Nakupeni mifano hii mitatu ya Sheikh wetu na mmoja wenu nyinyi wenyewe enyi wenye kuandika Radan mardudan na mifano iko mingi. Inatosha kuwaita kwenu watu wengine kuwa ni watu wa bidaa na nyinyi ndio watu wa Sunna. Kwa hivyo, hii hali mumeiuda nyinyi wenyewe: Zanzibar bali Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla haikuwa hivi. Chuki mumeziunda nyinyi; mukijirekebisha kwa kutumia lugha nzuri nadhani hakuna atayekwambieni jambo kwa lugha nzito.
Mnasema Mfano wa kauli zake mbaya ni kama zifuatazo:
(vuta-nikuvute) [uk. 6]
(hii ni ajabu katika ajabu za dunia!) [uk. 124]
(Kwa hivyo, uwezekano huo alioutoa Sheikh hauwashi wala hauzimi [uk. 124]
(Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja,)
(Utaona kwamba masuala yote haya si yenye kima katika soko la elimu, bali ni masuala ya kuwababaisha watu wasiojua nini cha kujadiliwa katika mas-ala haya ya funga) [uk. 167]
(Hoja nyengine - nayo pia ni hoja ya mitaani - ni kuwa watu wengi wa kawaida wanapouona mwezi mkubwa husema: "E basi ule ndio mwezi wa leo ule?!!!")
(Jawabu hii ya mwisho, inaufanya upinzani mzima wa Sheikh Bachoo kuwa hauna maana yoyote.) [uk. 132]
(Kwa ufupi ni kuwa hicho walichokidai watetezi wa rai pinzan) [uk. 32]
(utaona jinsi gani mwanamume alivyokuwa bingwa wa kubadilika! Na hili si jengine bali ni lile Waswahili wanalolisema: "Mfa maji hukamata maji.") [uk. 128]
(Hakuna hapa kinachoonesha mas-ala ya kufunga kwa muandamo mmoja wala kumi na moja.)) [uk. 125] (haina maana kwamba usiku ukiingia sehemu moja ndio umeingia dunia nzima. Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu.)
Jawabu Sikubaliani na nyinyi kwamba humu muna maneno mabaya. Lakini hata nikikubali basi nasema kwamba lugha ya namna hii sababu ni nyinyi, na kwa hivyo, utaona kwamba ninapojadiliana na watu wengine basi lugha yangu hubadilika. Kwa hivyo, tujirekebisheni sote na tujadili tafauti zetu kwa lugha ya kiungwana. Ama ukinita mpopoo, basi usinilaumu na wewe nikikwita mnazi: unanilaumu nini na wewe unakifanya kile kile nikifanyacho?! Bali hata katika kitabu hiki munachonijibu, basi nanyi mumetumia lugha hizo hizo. Katika baadhi ya sehemu umesema: "Kwa hakika katika kitabu chake hicho kwenye uk 6, anajionyesha alivyo na kauli mbili tofauti..". Na mwishoni mwa kitabu mumesema: "Dhana ya pili ya ndugu Juma imejengeka katika msingi dhaifu wala haina nafasi katika uwanja wa fani (kitaalamu) nao ni kule kusukuma kwake juu ya elimu ya Jiografia". Na yamo mengi katika kitabu chenu. Sasa nyinyi mwasema nini na mwatenda nini?
Munasema "Kwa hakika katika kitabu chake hicho kwenye uk 6, anajionyesha alivyo na kauli mbili tofauti: Kwanza anakubali kwamba suala la muandamo wa mwezi lina ikhtilafu katika kufunga kwa kumuelezea Shaykh Naaswir Bachuu kwamba: (Tunampongeza kwa juhudi) Kisha pale pale anageuka kwa kusema: (madamu hili ni suala la khilafu - basi i likuwa ni kutolizungumza kabisa,) Sasa hebu tumuulize ndio anapongeza nini? Na ni nani aliyemwambia kwamba jambo lenye khitilafu halizungumzwi? Yeye angezungumza nini katika kitabu chake kama si masuala ya ikhtilafu? Pia anatwambia haya ni katika mambo ya furui (matawi) za Kidini, kwa hivyo zisizungumzwe. Kwani ni nani aliyemwambia kuwa furui za Kidini hazizungumzwi?"
Jawabu Ikiwa lugha hii ndogo hamukuweza kuifahamu, vipi mutaweza kufahamu kitu chenye kuhitaji fani za lugha na usuli na mengineo. Ikiwa mimi niliingia msikitini kwenu Raha Leo nikakuta juu ya ubao wenu munawasomesha vijana na katika darsa hio Mubtadaa mumemwita Fa'il (vipi mutaweza kujadili masuala haya?!!! Mimi nimempongeza Sheikh Bachoo kwa juhudi au moyo wake; na sikumpong eza kwa kulikuza suala ambalo:
1) Ni la furuu'i
2) Lina khilafu. Na hii haina maana kuwa Furu'i zisizungumzwe; suala la Furu'i huwa halishadidiwi; bali unawaacha watu kama walivyo tu. Lakini yeye anapenda kushadidia katika mas-ala kama haya; ndio maana akashadidi hata katika suala la kufunga mikono hata kuwaita watu mipopoo bali na kuwambia kuwa hawana Sala. Kwa hivyo, nieleweni kwamba ninachokipinga ni kushadidia au kuwakoroga watu katika kitu ambacho ni furu'i za dini ilhali yeye kawakuta na msimamo tafauti tangu zamani. Katika mas-ala ya furu'i, wanavyuoni huwa hawashadidi juu ya Mas-ala kama haya. Mimi leo nikisimama nikaanza kufanya kampeni kwamba watu wasiitikie amina wa kisali, nalo ni jambo la furu'i, si nitakuwa natia fitna tu? Jambo kama hili huwachwa wasomi wakalitafiti kaiha kila mmoja akafanya vile ilivyombainikia. Lakini kufanya kampeni maalumu na da'awa kana kwamba waliotangulia wote ni wapotovu, hili ndilo jambo la kulaumiwa.
Ama kauli yenu: "Kwanza anakubali kwamba suala la muandamo wa mwezi lina ikhtilafu katika kufunga kwa kumuelezea Shaykh Naaswir Bachuu kwamba: (Tunampongeza kwa juhudi) Kisha pale pale anageuka kwa kusema: (madamu hili ni suala la khilafu - basi ilikuwa ni kutolizungumza kabisa,) Sasa hebu tumuulize ndio anapongeza nini?" Mwisho wa kunukuu. Na mimi nikuulizeni nyinyi mumenishukuru kwa juhudi yangu kisha mwisho wa kitabu mukaniambia: "Mwisho tunachukua fursa hii kumuonya ndugu Juma kuwa amuogope Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu. Akumbuke kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya asilolijua. Aelewe kwamba ataulizwa juu ya hilo. Lingekuwa jambo la busara kama ndugu Juma angalikubali kuuliza na kufanya utafiti zaidi juu ya mas-ala haya kama agizo la Mwenyezi Mungu linavyotutaka". Sasa na nyinyi munanishukuru nini?
Munasema "Sisi tunapenda kumfahamisha kuwa suala hili la kwamba mwezi ukiandama sehemu moja unatosheleza kufuatwa kwa kufunga au kufungua ulimwengu mzima, si suala jipya bali ni jambo la kale. Tunasikitika kwamba hakuangalia vizuri maoni ya Wanavyuoni wakubwa walivyoelezea msimamo huo. Angalia katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu uk 51-58. Hapa tunanukuu baadhi ya kauli hizo:
Imamun-Nawawy aliyekisherehesha Kitabu cha Sahihi Muslim anasema:
"Na jambo lililo sahihi kwa wenzetu (Mashaffi) ni kuwa muandamo mmoja hauwahusu watu wote bali unawahusu wale walio karibu kwa kiasi ambacho hawaruhusiki kupunguza Sala (Sala ya safari). Pia imesemwa kuwa iwapo matlai ni mamoja watalazimika (watu) kufunga pamoja. Pia imesemwa kuwa ikiwa (wanaishi) katika eneo la Iklimu moja (maili 72 au km 89) (watalazimika kufunga pamoja) vyenginevyo kila mmoja atafunga kwa muandamo wake. Na wakasema wenzetu wengine (Mashaffi) kuwa muandamo katika sehemu moja utawahusu wote wa dunia nzima".
Shaykh Jaadul Haq wa chuo kikuu cha Al-Azhar katika kitabu chake "Bayaanullinnas" J. 2 uk 203 - 204 ameandika yafuatayo juu ya kauli hiyo ya Imamun-Nawawy:
"Hapa Imamu An-Nawawy ametaja kwa mukhtasari kauli zilizomo katika madhehebu ya Kishaffi (juu ya kuandama kwa mwezi) na ambazo pia zimo katika madhehebu mengine ya Kiislamu. Kauli hizo tunaweza kuzigawa katika maf ungu matatu makuu: "...Hapo Imamu An-Nawawy ametaja kwa mukhtasar kauli zilizomo katika madhehebu ya Shaffi (juu ya kuandama kwa mwezi) na ambazo pia zimo katika madhehebu nyengine za Kiislam. Kauli hizo tunaweza kuzigawa katika mafungu matatu makuu: Kauli ya kwanza: "Kila nchi iwe na matlai yake, wala muandamo wa nchi moja hautalazimu nchi nyengine ya mbali wala karibu". Kauli ya pili: "Muandamo wa nchi moja unalazimu nchi zote za dunia hata kama ziko mbali".
Kauli ya tatu: "Muandamo wa nchi moja unalazimu nchi iliyo karibu nayo au inayowafikiana kimatlai". Kisha, Shaykh Jaadul-Haq akaendelea kusema kwamba:
"Na (kauli) zote hizo ni maoni yatokanayo na Ijtihaadi ambazo hazikusimama juu ya hoja kat-ii, si sanad wala matni. Kwa hivyo ingefaa ichaguliwe kauli ambayo inakubaliana na maslahi ya (Waislam wote wa) dunia nzima kwa jumla"."
Jawabu Sikubaliani na mtazamo wa Sheikh Shaykh Jaadul Haq wa chuo kikuu cha Al-Azhar, kwamba zote hizi ni rai na itihad kwani kanuni ni kuwa "Hakuna ijtihadi mbele ya andiko" Ijtihad mwahala mwake ni musimo andiko. Wakatika katika suala hili, utaona kwamba asemaye kuwa tufunge kwa muandamo mmoja, hoja yake ni Hadithi "Fungeni kwa kuuona"; na anayesema kuwa kila mahala na muandamo wake, anatoa ushahidi wake ni Hadithi ya Ibn Abbaas na Kuraib. Kwa hivyo, ijtihad ni katika kuyafahamu maandiko: si ijtihad kwa maana ya rai tupu pasi na andiko kama alivyosema Sheikh. Kilichobaki ni kuzijadili riwaya mbili hizi zina maana gani?
Munasema Tungependa kumueleza ndugu yetu kwamba hata hapa Afrika ya Mashariki jambo hili hakulianzisha Shaykh Naaswir Bachuu kama alivyodai mwenyewe (Nd. Juma) kwamba: (Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro)) Inasikitisha hakuweza kuangalia katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu uk 161-163 wametajwa walioonyesha kwa vizuri kabisa misimamo hiyo tofauti. Mashaykh wenyewe ni hawa wafuatao: Al-marhuum Shaykh Juma Abdul Waduud (wa Zanzibar), Shaykh Abdillahi Naaswir ( Nairobi Kenya ), na Shaykh Naaswir Khamis Abdul Rahman ( Mombasa Kenya ).
Jawabu Kwani wapi katika kitabu changu nilisema kuwa Sheikh Nassor Bchoo ndiye aliyeanzisha fikra hii hapo Afrika ya Mashariki hata mukaleta dai hili? Mimi nimeeleza kuwa zamani Afrika Mashariki watu wote wakifata muandamo mmoja. Nilisema: Karne zimepita bila ya sikio la Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro juu ya suala la muandamo wa mwezi. Harakati za elimu zilipobadilika na kuelekea zaidi - kwa kujua au bila kujua - katika mrengu wa Kihanbali na Kiwahabi, pakajitokeza mapinduzi ya ghafla ya fikra na matendo. Dr. Ramadhan Al-butti - miongoni mwa wanavyuoni wakubwa wa ulimwengu wa sasa - anaona kwamba harakati hizi hazisifiki kama ni madhehebu: bali ni hatua (phase) katika mapito ya Historia.
Na katika uk. 97, nimesema:
Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya. Kwa hivyo, ni wazi kwamba mimi nazungumzia Afrika Mashariki. Na mfano wa hilo pia kalisema Sheikh Nassor Bachoo, lakini yeye hamukumjibu. Anasema: "Pamoja na kuwa mgogoro wa kuandama kwa mwezi umeanza kuonekana hadharani katika jamii za Waislam wa hapa Afrika ya Mashariki katika miaka ya hivi karibuni". Inasikitisha kwamba hata maneno yangu mumeyakata na kuchukua yale ambayo hayakamilishi maana nilioilenga. Maneno "Karne zimepita" hamukuyataka kwani hayakufikisheni kule mutakako!
Pili narejea tena kusema kwamba hao wanavyuoni aliowataja Sheikh Nassor, hawajathibitisha habari za kuwa watu wafunge au wakifunga kwa muandamo mmoja Africa Masharik, ukimtoa Sheikh Nassir Khamis wa Mombasa ambaye naye pia ni mtu wa sasa. Ama sheikh Juma Abdu-Wadood yeye, kwa mujibu wa nakala hio ya Sheikh Nassor Bachoo, kasema hivi: Kuona huku kwa mwezi kumekusudiwa kuonekana na Waislam, na kuonekana na Waislamu huko, sio lazima kuonekana na Waislamu wote. Bali inatosha shahada ya mtu mmoja muadilifu".
Pia inampasa mtu mmoja pekee kama ameuona mwezi yeye afunge na kila aliyemuamini; hata akiwa haijakubaliwa shahada yake. Haya ndio maneno ya Sheikh Juma Abdu-Wadood kwa mujibu wa alivyomnukuu Sheikh Bachoo. Sasa ikiwa ndugu zetu mumeshindwa kuyafahamu maneno haya ya Sheikh Juma Abdu-Wadood, bado mutaendelea kupoteza watu bila ya elimu?! Sheikh Juma Abdul-Wadood hapa anazungumzia mas-ala ya ushahidi kwamba si lazima - katika suala la kuonekana kwa mwezi - kwamba kila mmoja auone: bali akiona mtu mmoja basi inatosha kwa wengine kufunga. Hii ndio kauli ya Sheikh Juma Abdul-Wadood na hili nimelieleza kwa urefu katika kitabu changu.
Kisha Sheikh Juma Abdul-Wadood akazungumzia suala la kufunga kwa muandamo mmoja akasema: "Rai za Maimamu wengine wameifasiri hadithi isemayo: (Fungeni kwa kuuona Mwezi) kwamba ukionekana popote mashariki au magharibi (watu) wafunge; hapana kutazama masafa fulani au nini. Hii ni rai nayo na wengi wamesema (hivyo) kama Imamu Malik , Ahmad na kundi kubwa la Hanafi. Inakurubia kuwa n dio rai ya Jamhuri - kufata rai hii ni kuhakikisha umoja wa dunia nzima. Wala hatuwezi kusema kwamba rai ya Shaffiy ndio ya Jamhur". Hapa Sheikh Juma anasimulia rai za Maimamu wengine: si rai za Maulamaa wa Afrika Mashariki. Mimi dai langu nililodai ni kuwa jambo hili la kufunga kwa muandamo mmoja, napenda munifahamu: ni jipya kwa Africa Mashariki. Mimi sikusudii jambo la wanazuoni kuzungumzia rai mbali mbali: bali nazungumzia jambo la watu kufata muandamo mmoja kwamba karne zimepita ya sikio la Muafrika Mashariki wa Kawaida halijiapata kusikia. Na nimetumia maneno "Muafrika wa Mashariki wa kawaida" ili kuwatoa wanavyuoni wao hata kama walikuwa hawafati kauli hio, lakini wanaijua. Kwa hali yoyote ile:
1) Sheikh Juma Abdul-Wadoo hajazungumzia kwamba Afrika Mashariki watu walikuwa wakifunga au wafunge kwa muandamo mmoja, bali kazungumzia rai za wanavyuoni wasio wa Afrika Mashariki - Al-Imamu Shafi, Hanbal n.k. Na mimi sijakanusha tafauti hizi.
2) Kauli yake ilikuwa ni kuhusu suala la mashahidi.
Ama Sheikh Abdillahi Nassir, yeye ni mwanachuoni wa sasa. Na mimi sijasema kuwa sasa hakuna rai hizo. Pili ni kuwa nakala alizotupa Sheikh Bachoo za kitabu cha Sheikh Abdillahi utaona kwamba Sheikh Abdillahi hazungumzii kuwa kauli ya kufatwa ni ile ya muandamo mmoja; bali yeye kasema kuwa hili ni suala la khilafu kwa hivyo tusigombane kila mtu afate rai anayoiona kuwa ni sawa. Sheikh Abdillah kayasema haya baada ya kutokea mizozo hii ya sasa. Kwa hivyo tunarudi pale pale kwamba "Karne zimepita bila ya sikio la Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro juu ya suala la muandamo wa mwezi. Harakati za elimu zilipobadilika na kuelekea zaidi - kwa kujua au bila kujua - katika mrengu wa Kihanbali na Kiwahabi, pakajitokeza mapinduzi ya ghafla ya fikra na matendo". Kwa hivyo, nukta hii hamukuuijibu: na wala sioni kuwa kuna haja ya kuijibu kwani haina umuhimu katika maudhui yetu. Bali kitabu chenu chote, munachagua mambo yasio na umuhimu "Juma kantutukana; Juma kanfanya hivi" nyinyi ndio munajibu baada ya kuzungumzia dalili za kielimu.
Ama Sheikh Nassor: yeye pia ni mtu wa sasa na ni mfuasi wa skuli hio hio munayoifuata nyinyi, kwa hivyo kusema kwake alivyosema hakujapindua nilioyasema kuwa - kimatendo - hili ni suala jipya kwa kwetu Afrika ya Mashariki. Wala mimi sikusema kuwa Sheikh Nassor Bachoo ndiye muasisi wa fikra hio huko kwetu. Naomba munifahamu ninachokisema kwanza kisha ndio munijibu. Na sijui munapinga nini kitu ambacho watu wote wanakijua. Bila ya kusahau kwamba mimi sikusudii kusema kuwa kitu sahihi ni kilichofanywa zamani au kilichofanywa leo: laa! Bali kitu sahihi ni chenye ushahidi sahihi uliojengeka juu ya misingi sahihi ya kielimu. Na kielimu, suala la kuzingatia muandamo mmoja - hamutoweza kulithibitisha.
MNASEMA
Pia Shaykh Ahmad Al Khalil, Mufti wa Omani amethibitisha kwamba Ikhtilaf hii ya muandamo wa mwezi katika hukmu ya kufunga au kufungua ipo na kwamba ni jambo la kale. Kama alivyosema maneno yake yaliyotafsiriwa na Shaykh Muniir Sulayman 'Aziz kwamba: "Hakuna madhehebu iliyokuwa imesalimika na kuwa na Khitilafu baina ya Wanavyuoni wake juu ya suala la kutafautiana miandamo ya mwezi." Jee ndugu Juma anataka kusema kwamba Shaykh Naaswir Bachuu ndiye mwalimu aliyeanzisha madhehebu zote? Au ndiye aliyeanzisha mtafaruku huu kama alivyouita mwenyewe ndugu Juma?
JAWABU
Suala hilo jiulizeni wenyewe; mujijibu wenyewe; kwani nyinyi ndio mulioliunda: mimi sikusema hivyo kamwe bali nilichokisema ni hiki: "Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya". Nami sikusudii kusema kwamba upya huo ni katika kuzungunzwa au kusomwa suala hilo katika vitabu; nakusudia kimatendo sula hili lilikuwa halipo Afrika Mashariki. Sasa ili muwe mumenijibu, twambieni nani alikuwa akifata muandamo mmoja hapa Afrika Mashariki. Jamani! Tafuteni hoja mujadili: musijadili kitu kisichokuwa na umuhimu. Kama hamuna hoja nyamzeni musijitie aibu!
MNASEMA
Katika kudhihirisha udhaifu wake wa kumuandama mtu fulani; Ndugu Juma anasema: (Kama tunavyojua kwamba Sheikh Nassor Bachoo, ni mmoja wa wenye kusisitiza ulazima wa kuwa na muandamo mmoja.) Sisi kwa upande wetu tunasema: Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu hakuna pahala alipolazimisha watu wafuate huo aliouita ndugu Juma (msimamo wa Shaykh Naaswir). Bali yeye ameonesha mitizamo ya Wanavyuoni kwa kutumia Aya za Qur-aan, Hadiythi na vitabu vinavyokubalika. Lugha aliyotumia Shaykh Naaswir katika huo unaonekana ni msimamo wake ni maneno yaliyozimuliwa kilugha (polite language) kama vile: (inawezekana) ((inaonyesha) .
JAWABU
Na mimi hapa sijasema kuwa Sheikh Nassir Bachoo kalazimisha watu wafunge kwa muandamo mmoja. Nimesema "Anasisitiza ulazima" yaani yeye analingania msimamo huo kwani kwake ndio msimamo sahihi na ndio wajibu kuufata. Naomba tena tuelewane musiseme kitu kinyume na nilivyosema. Wala musitafute kitu kisicho na maana mukajadili eti ndio jawabu! Pili maneno yenu: "Katika kudhihirisha udhaifu wake wa kumuandama mtu fulani". Sasa je na nyinyi pia munaonesha udhaifu huo huo kwa kumuandama mtu fulani katika kitabu chenu?
MNASEMA
Aliyelazimisha rai ni ndugu Juma mwenyewe kama anavyosema: (Lakini kilicho lazima na ambacho tunatakiwa tukubaliane ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali) [uk. 112]
JAWABU
Bali hata Sheikh Bachoo pia kalazimisha kwani ukidai kuwa huu ndio msimamo wa haki au ndio msimamo sahihi au ndio wajibu kufatwa, bila kusema kuwa rai zote zinafaa basi na wewe huwa umelazimisha rai yako. Sasa je Sheikh Bachoo anakubali hivyo kuwa rai zote ni sawa? Mimi kweli sisemi kuwa rai zote ni sawa: nasema kuwa nyinyi mumekosea na sahihi ni kinyume na munavyofanya, na kwa hivyo bado nipo katika msimamo wangu huo huo kwamba: "Kilicho lazima na ambacho tunatakiwa tukubaliane ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali".
MUNASEMA
"Kisha katika uk 85 ndugu Juma anataja kwamba msimamo huu wa muandamo mmoja kwa dunia nzima ni ((kitu kipya)) na kwamba jambo hilo halitekelezeki na ni kauli iliyobaki vitabuni tu baada ya kutaja baadhi ya nchi zinazofuata miandamo yao - yaani kila nchi na muandamo wake kama Al-yaman , Oman , Misri na Saudia. Kisha hapo hapo akataja: ((isipokuwa Imarati katika miaka ya mwisho wamekuwa wakifata Saudia.)) Inafaa ndugu Juma aulizwe masuala yafuatayo:
i) Kama ni jambo lisilotekelezeka vipi tena Imarat wanalitekeleza?
ii) Je hawa wa Imarat nao ni wanafunzi wa Shaykh Naaswir Bachuu?
iii) Kwani hiyo sio kauli ya Jamhuur ambayo ndio msimamo wa maimamu wakubwa wakiwemo Ahmad bin Hanbal, Malik na Abu Hanifa? (Angalia pia sehemu ya 11 na 13 za kitabu hiki)
JAWABU
Kwanza mumemefanya ghushi: maneno yangu hamukuyanukuu yote. Mimi nimesema: "Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya". Nyinyi maneno "Kwa kwetu Afrika Mashariki" mumeyatoa ili ionekane kuwa mimi nasema kuwa hili ni suala jipya kila pahala. Watu kama nyinyi vipi tutakuamini katika dini yenu na uadilifu wenu, ikiwa munaghushi maandiko hivi? Hii ndio kamati ya Msikiti Sunna na hii ndio suna yenyewe?! Halafu mukaendelea na tadlis (ghushi) yenu mukasema: "Na kwamba jambo hilo halitekelezeki na ni kauli iliyobaki vitabuni tu". Mimi sikusema hapa kuwa "Halitekelezeki", bali nimesema:
Lakini ukweli ni kuwa hata katika nchi nyengine zote za dunia taqriban kauli kwamba tufunge kwa muandamo mmoja, ni kauli ilioishia katika vitabu tu, kimatendo (practically) kauli hio haitumiwi isipokuwa na mtu mmoja mmoja. Hadi leo hii: watu Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao, Misr wanafata muandamo wao na nchi zote taqriban ni hivyo, isipokuwa Imarati katika miaka ya mwisho wamekuwa wakifata Saudia.
Haya nionesheni hapa maneno "Halitekelezeki". Mimi nimesema kuwa kimatendo kauli hii, hadi leo haitendewi kazi isipokuwa na baadhi ya watu. Nyinyi mumebadilisha na kuweka ghushi yenu mukasema nimesema halitekelezeki. Kwa hivyo, hilo Sula (a na b) jibuni wenyewe kwani mumesema kinyume na nilivyosema. Suala (d), najibu kuwa sio: hio si kauli ya jumhur bali jumhur kauli yao ni kinyume na hivyo na hili nimelithibitisha katika uk. 189-193 wa chapa ya pili ya kitabu changu au uk. 171 wa kitabu hicho chapa ya kwanza. Na Al-Imamu Malik riwaya zake zimegongana na riwaya kwamba kila watu na muandamo wao ndio ilio bora kwani ni riwaya ya Madina aliko kuweko Al-Imamu Malik, wakati riwaya nyengine ni ya watu wa Irak kulikokuwa na viwanda vya kutunga riwaya!
MNASEMA
Na sisi tunamuongezea habari moja ambayo ni vyema kuielewa, kwamba nchi ya Uganda iliyo katika Afrika ya Mashariki pia inafuata rasmi muandamo mmoja wa duniani. Pia aelewe kwamba huo msimamo wa kila nchi na mwezi wake huku Afrika ya Mashariki haukuwepo tokea zamani. Mashaykh wote wa huku wanakubaliana mwezi ukionekana popote katika nchi hizi tatu ( Kenya , Uganda na Tanzania ) wanafunga pamoja. Yeye anaendelea kushika msimamo wake: (Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao). Lile analoliona yeye halitekelezeki, basi ndio linatekelezeka.
JAWABU
1) Kitu rasmi Uganda hakizingatiwi kwani Uganda kimsingi sin chi ya Kiislamu wala ya Waislamu: Waislamu ni wachache ukilinganisha na Wasio Waislamu. Kwa hivyo, hakuna kitu rasmi. Na jambo hilo ni jambo la sasa. Na mimi sijapinga kwamba sasa fikra hio ipo Afrika Mashariki.
2) Ama kauli yenu: "Mashaykh wote wa huku wanakubaliana mwezi ukionekana popote katika nchi hizi tatu ( Kenya , Uganda na Tanzania ) wanafunga pamoja". Ndio maana nikatumia lafdhi "Kwa kwetu Afrika Mashariki" nikijua kuwa wanavyuoni wote wa kwetu Afrika Mashariki wana msimamo huo. Ama kauli yenu: "Yeye anaendelea kushika msimamo wake: ((Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao,)). Lile analoliona yeye halitekelezeki, basi ndio linatekelezeka". Mwisho wa kunukuu. Inaonesha kuwa kitabu changu mumekijibu bila ya kukifahamu. Nilichosema ni kuwa, ijtihadi ifanywe katika kubainisha wapi hadi wapi watu wafunge pamoja. Kwa vile, hakuna andiko lililobainisha hivyo. Ama muandamo mmoja kwa dunia nzima hili ni kinyume na andiko. Kwa hivyo, wakiwa wanavyuoni wa zamani wamefanya ijtihad hio, sisi tunafata ijtihad yao kwa vile hapa ni mahala pa ijtihad na haikugongana na andiko. Ama madai yenu nyinyi ni kinyume na andiko lilivyoonesha.
MNASEMA
"Kuna suala moja la nyongeza tunapenda tumuulize ndugu yetu Juma: Hata kama hizo nchi alizozitaja ( Al-Yaman , Oman , Misri na Saudia) hazijakubaliana kufuata muandamo mmoja, je hakuna uwezekano (japo wa sadfa) unaoweza kutokea kufunga siku moja ijapokuwa kila mmoja ameona mwezi katika nchi yake? Sasa tuseme kila nchi katika hizo imeona mwezi usiku wa Alkhamisi kuamkia Ijumaa - Wote si watafunga siku moja ya Ijumaa? Basi huo ndio utekelezaji aliosema hautekelezeki. Ni wazi kuwa unatekelezeka.
JAWABU
Munaendelea kuuliza masula haya kwa sababu masuala yenu mumeyajenga katika kitu nisichokisema kamwe. Wapi nimesema kuwa "Hilo halitekezeki" hata mukauliza masuala haya?