4
MUANDAMO WA MWEZI
SEHEMU YA SITA
MUANDAMO WA KIFALAKI NA MUANDAMO WA KISHARI'AH
UTANGULIZI MFUPI JUU YA SEHEMU HII
Kabla sijaendelea na kunukuu jawabu niliojibiwa na ndugu zangu kuhusu maudhui ya sehemu hii, ni vyema kwanza ninukuu nilioyasema katika kitabu ambayo wao ndio wanayajadili. Kufanya hivyo, ni kuwawezesha wasomaji kuona udhifu uko wapi. Katika kitabu, chini ya anwani
MUANDAMO WA KIFALAKI NI NINI?
nilisema yafatayo: Ni ukweli usiopingika kwamba ufahamu sahihi wa kitu chochote kile unafungamana mfungano wa nguvu na walazima na ufahamu wa dhana (concept) yake sahihi. Kwa hivyo, ni kawaida kwamba muhubiri anapohubiri juu ya maudhui fulani, kwa mfano jografia, kama hakufafanua tangu mwanzo na kuweka wazi, basi suala la kwanza ataloulizwa ni "Jografia ni nini?"
Maudhui yetu katika sehemu hii ni hii dhana sahihi ya muandamo wa mwezi: je kuandama kwa mwezi ni nini katika dhana yake ya uhakika? Qur-an Tukufu, imeashiria muandamo wa mwezi katika baadhi ya Aya zake. Na hii ni pale Allah Aliposema:"Na Mwezi tumeupimia vituo mpaka ukarejea (kuwa mwembamba) kama karara kongwe (la mtende)
. Na anasema Allah :"Yeye (Allah) Ndiye aliyelifanya jua kua muanga na mwezi kua nuru na akaupimia (huo mwezi) vituo, ili mujue idadi ya miaka na hisabu."
MAELEZO JUU YA AYA HIZI
Aya mbili hizi zinathibitisha kwamba mwezi una Manazil (vituo) ambayo hupitia ndani yake. Watu wa elimu ya falaki wanasema kwamba Manazil haya ni ishirini na nane ambayo yamo katika Buruji (constellations) kumi na mbili. Majina ya buruji hizo ni:
1) Al-hamal (Aries, Kondoo dume).
2) Al-thaur (Taurus. Ngo'mbe dume).
3) Al-jawzaa (Gemini. Mapacha).
4) Al-sartan (Cancer. Kaa).
5) Al-asad (Leo. Simba).
6) Al-sunbula (Virgo. Mashuke).
7) Al-mizan (Libra. Mezani).
8) Al-a'qrab (Scorpio. Nge).
9) Al-qaws (Sagittarius. Upinde).
10) Al-jadyu (Capricon. Mtoto wa mbuzi).
11) Al-dalwu (Aquarius. Ndoo).
12) Al-hut (Pisces. Samaki).
Hayo ndio majina ya buruji kumi na mbili, kwa mujibu wa wanaojihusisha na elimu za falaki. Buruji hizo kumi na mbili zina vituo ishirini na nane (28). Kila Buruji moja ina vituo viwili na thuluth. Vituo hivyo ni:
1) Al-shartan. 2) Al-butain. 3) Al-thurayya. 4) Al-dabran. 5) Al-haq'a. 6) Al-han'a. 7) Al-dhiraa. 8) Al-nnathra. 9) Al-ttarf. 10) Al-jabha. 11) Al-kharatan. 12) Al-sarfa. 13) Al-awaa. 14) Al-simak. 15) Al-ghafr. 16) Al-zubanayan. 17) Al-iklil. 18) Al-qalb. 19) Al-shaula. 20) Al-na'aim. 21) Al-baladda. 22) Sa'adu Al-dhabih. 23) Sa'adu Bula'a. 24) Sa'du Su'ud. 25) Sa'ad Al-akhbiya. 26) Al-far'u Al-muqaddam. 27) Al-far'u Al-muakkhar. 28). Batnu Al-hut.
Haya ndio majina ya manazil ishirini na nane kwa mujibu wa wataalamu wa falaki. Kilichomashuhuri katika vitabu vingi vya kale ambavyo vimezungumzia mas-ala haya ni kuwa buruji ya kwanza ambayo ni Al-hamal (Aries), vituo vyake ni: Al-shartan, Al-butain na thuluthi moja ya Al-thuraya. Miongoni mwa hawa ni Al-qurtubiy kama ilivyo katika tafsiri yake. Na hivyo ndivyo walivyosema wengi wengineo ambao nimebahatika kuona maandishi yao juu ya maudhui hii. Lakini hata hivyo mmoja wa wataalamu wetu waliokuweko Zanzibar, naye ni Sheikh Yusuf alikuwa anasema kwamba buruji haziko thabiti (not constant), bali kila miaka sabiini (70), zinaondoka na kujongea mbele, jambo ambalo linazifanya kuingia katika manazil mengine baada ya miaka. Hatimae nikaikuta kauli hii imo katika kitabu "AHKAMU AL-HAKIM" cha mwanachuoni mashuhuri wa falaki wa Misri Al-ustadh Abdul-fattah Al-sayyid Al-tukhi Al-falaki. Anasema: "Jua kwamba manazil (vituo) ni zile nyota tunazoziona usiku. Na waliotangulia walikuwa wakiziita nyota thabiti (fixed stars), kwa sababu ya kudhani kwao kwamba zimesimama kwa ajili ya kwenda kwake kidogo kidogo. Lakini elimu ya sasa imegundua kwamba zinakwenda lakini kidogo kidogo sana ambapo zinakata daraja moja (one degree) katika (kipindi cha) miaka 66 taqriban." Mwisho wa kunukuu.
Kauli ya Sheikh Yusuf inaashiria kwamba labda yeye anaamini kwamba majina ya manazil ni zile sehemu zilizokaa nyota: si ule mkusanyiko wenyewe wa nyota (constellation). Kwa hali yoyote ile - kumbu kumbu yangu - ni kuwa kwa mujibu wake, Manazil (vituo) hayo tulioyataja kuwa ni ya Al-hamal - nayo ni Al-shartan, Al-butain na thuluth Al-thuraya - kwa sasa yamo katika buruji ya Al-thaur (Taurus. Ngo'mbe dume). Kauli yake hii inawafikiana na kauli ya Al-tukhi katika kitabu chake hicho.
Mwezi unakata kila kituo kimoja kwa muda wa siku moja, ikimaanisha kwamba siku ishirini na nane (28), huwa umekamilisha safari yake. Na hapo hufichika kidogo kwa siku moja au mbili kisha hudhihiri na kuonekana tena duniani. Suala ni kuwa je kukamilika huku kwa mzunguko wa mwezi ndio muandamo wa mwezi Kisharia? Umejua - kutokana na hayo yaliotangulia - kwamba mwezi unakamilisha mzunguko wake kwa muda wa siku ishirini na nane (28), na ili uonekane duniani unahitaji kupitiwa na siku moja au mbili. Kuanzia hapa utaanza kujua tafauti baina ya muandamo wa mwezi kisharia na muandamo wake kifalaki. Pia utaanza kuona namna gani Sh. Nassor Bachoo katika kitabu chake alivyochanganya baina ya hali mbili hizi wakati alipokuwa akizungumzia maudhui hii.
MAELEZO YA SH. NASSOR BACHOO
Sh. Nassor Bachoo ni mmoja wa Wazanzibari waliojitokeza kuzungumzia mas-ala haya. Katika kitabu chake, Sheikh kaizungumzia maudhui hii na akanukuu Aya ya 5 ya Sura ya 10 ambayo ni ya pili katika Aya tulizozinukuu kabla. Baada ya maelezo alisema: "Qur-an inalieleza suala la kuandama kwa mwezi kama ni tukio moja wapo kati ya matukio yaliyopangwa na Mwenyezi Mungu kutukia kila mwezi mara moja duniani kote." Mwisho wa kunukuu.
Ukianzia uk. 5. hadi uk. 8, wa kitabu chake, utaona kwamba Sh. Nassor Bachoo anathibitisha mwenendo wa mwezi kupitia katika Manazil (vituo) yake. Ufupisho wake - kama tulivyotangulia kusema - ni kuwa mwezi unasafiri kwa muda wa siku ishirini na nane (28) kupitia katika vituo hivyo, na siku moja au mbili hupotea kisha kudhihiri na kuweza kuonekana duniani. Sheikh aliishia maneno yake kwa kusema: "Baada ya maelezo haya tunatumai tumeweza kuelewa mtazamo wa Qur-an juu ya kuandama kwa mwezi." Mwisho wa kunukuu. Sasa ukitazama sentensi mbili hizi za Sh. Bachoo, utaona kuwa anakusudia kuthibitisha kitu kimoja kwa Aya ambayo haimpatii malengo yake. Anachokusudia kukithibitisha Sh. Bachoo - kwa inavyoonesha kutokana na maandishi yake - ni kuwa muandamo ni mmoja duniani kote na kwa hivyo - bila shaka anakusudia kusema - kwamba sote tufunge kwa muandamo mmoja huo. Ndio maana akasema: "Qur-an inaeleza suala la kuandama kwa mwezi kama ni tukio moja wapo kati ya matukio yaliopangwa na Mwenyezi Mungu kutukia kila mwezi mara moja duniani kote." Lakini dai kwamba Qur-an inasema kuwa muandamo wa mwezi unatokea mara moja tu dunia nzima - ikiwa anakusudia muandamo wa kisharia nao bila shaka ndio anaouzungumzia - si sahihi. Na sijui wapi Qur-an imesema hivi?!
Qur-an imezungumzia muandamo wa mwezi katika hali mbili: Hali ya kwanza: ni ya muandamo wa kifalaki. Na huu sio ule tunaouita muandamo. Hapa tutatumia tu neno "Muandamo" kwa ajili ya kufahamiana. Huu ndio ambao unazungumziwa na Aya hizo tulizotangulia kuzinukuu. Na ndio unaotokea mara moja duniani kote. Hali ya pili: ni ya muandamo wa Kisharia. Huu umetajwa katika Aya ya 189 ya Sura ya 2, ambapo Allah anasema:
"Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo. Sema hivyo ni vipimo kwa ajili ya watu na Hija."
Sasa katika Aya zote mbili hizi hakuna ufafanuzi wowote wenye kuonesha kwamba muandamo wa mwezi wa kisharia ni mmoja au vipi? Bali Aya hii ya pili, inaonesha tu kwamba katika Sharia kuna kitu miandamo ya mwezi. Lakini vipi miandamo hio: hakuna ufafanuzi wowote ule uliotolewa katika Aya hii. Kwa hivyo madai hayo ya Sh. Nassor Bachoo kwamba Qur-an inasema kwamba muandamo ni mmoja ni kitu kimoja na maelekezo ya Aya ni kitu chengine.
Kwa kufahamu zaidi ni kuwa Aya alioitolea ushahidi juu ya fikra yake, inasema:"Yeye (Allah) Ndiye aliyelifanya jua kua muanga na mwezi kua nuru na akaupimia (huo mwezi) vituo, ili mujue idadi ya miaka na hisabu."
Sasa utaona kwamba Aya hii imetaja vitu viwili: jua na mwezi. Na vyote hivi vinazunguka katika falaki (orbits) zake na vinapita katika manazil (vituo) yale yale na vinapita katika buruji (constellations) zile zile. Sasa cha kustaajabisha ni kuwa vipi Sh. Nassor Bachoo ajenge hoja kwa Aya hii kuthibitisha muandamo mmoja na asijenge hoja kwa Aya hii kuthibitisha wakati (time) mmoja wa kusali?! Ninachokusudia kukisema ni kuwa Aya imetaja kwamba Allah ndiye aliyeumba jua na mwezi. Kisha akataja Illa (sa babu) ya kuumba vitu viwili hivyo. Akasema"Ili mupate kujua idadi ya miaka na hisabu (nyengine)."
Kwa lugha nyengine sababu ya kuumbwa jua na mwezi, ni kutuwezesha kudhibiti hisabu za miaka na hisabu za mambo mengine. Sasa kama sababu hii - kwa mujibu wa Sheikh Nassor Bachoo - ndio iliohalalisha au kuwajibisha kuuzingatia muandamo mmoja wa mwezi duniani kote kwa mujibu wa Aya hii, kipi kimeharamisha kuuzingatia mtenguko mmoja wa jua kuwa ni alama ya kuthibitisha wakati mmoja wa sala duniani kote, wakati Aya hii kama ilivyoutaja mwezi kuwa ni chombo cha kudhibitia wakati ndivyo ilivyolitaja jua kwa lengo hilo hilo?
Ubainifu wa haya ni kuwa kama Mtume(s.a.w.w)
alivyosema kwamba:fungeni kwa kuuona mwezi,
vivyo hivyo ndivyo alivyosema Allah"Salini kwa kutenguka jua."
Na Aya hio aliotunakilia Sh. Nassor Bachoo inazungumzia mambo yote mawili jua na mwezi. Kwa hivyo, ilitakiwa fiq-hi ya Sh. Bachoo iliojengeka juu ya Aya hio, ilihusishe jua kama ilivyouhusisha mwezi, kwani Aya inazungumzia mwenendo wa jua na mwezi. Na kwa hivyo, jua likitenguka Makka watu wa Zanzibar wasali?!
Kuanzia hapa utaanza kuona kwamba Aya hio ni kitu kimoja na fikra ya Sh. Nassor Bachoo ni kitu chengine. Qur-an imeeleza tu kwamba mzunguko wa jua na mwezi ni kwa ajili ya kujua miaka na hisabu, na miandamo ya mwezi ni vipimo vya nyakati na Hija: haikufafanua kwamba mwezi wa kisharia unaandama mara moja au kumi na moja. Ufafanuzi huu unaweza kupatikana baada ya kuzikusanya dalili zote zinazohusu maudhui hii kutoka katika Hadithi. Ama Qur-an Aya zake katika maudhui hii ni Mujmala (hazikufafanuliwa).
Baada ya haya, utaona kwamba tatizo sugu kwa walio wengi ni kutokutafautisha baina ya muandamo wa mwezi kifalaki (astronomically) na muandamo wake Kisharia. Muandamo wa kifalaki ni kutimiza kwa mwezi msafara wake kutoka katika kituo ulichoanzia hadi kufikia kituo cha mwisho. Muandamo huu ndio ambao ni mmoja dunia nzima, nao sio muandamo wa Kisharia: muandamo wa kisharia wa mwezi ni kitu chengine kabisa. Dhana (concept) sahihi ya kuandama kwa mwezi kisharia ni kuuona kwa macho baada ya siku ishirini na tisa au thalathini au kukamilisha idadi ya siku thalathini, kama Hadithi ilivyoeleza kwa uwazi. Sasa muandamo huu wa Kisharia, si lazima kwamba ukithibiti mahala pamoja uwe umethibiti mahala pengine. Kwa hivyo, Sheikh katika maelezo yake kachanganya baina ya muandamo wa kisharia na muandamo wa kifalaki na akaufanya muandamo wa kifalaki unaothibiti mara moja duniani kuwa ni sawa na muandamo wa kisharia ambao unatafautika kwa kutafautiana jografia ya ulimwengu kama tutavyoeleza baadae Inshaa Allah". Mwisho wa kunukuu nilioyasema kitabuni mwangu.
JAWABU NILILIPATA
Wanasema ndugu zetu wakijibu maelezo hayo: "6. Muandamo Wa Kifalaki Na Muandamo Wa KiShari'ah Kama kawaida yake ndugu yetu Juma amezusha dhana mpya katika mas-ala ya mwezi ambayo inakwenda kinyume kabisa na mitazamo ya Wanavyuoni, katika kulihusisha suala hilo na utaratibu wa kufunga na kufungua Ramadhaan. Amejaribu kuugawa muuandamo wa mwezi katika sehemu mbili kama alivyodai mwenyewe katika kitabu chake uk 18 kwa kusema: ((Hali ya kwanza: ni ya muandamo wa kifalaki.)) na (Hali ya pili: ni ya muandamo wa Kisharia.)
Hatujui dhana hii potofu ameitoa wapi kwani hakuweza kuthibitisha hata kauli moja ya Mwanachuoni yeyote aliyegawa muandamo au aliyesema kuna miandamo miwili (ya Kifalaki na ya Kisheria). Hoja sio kusema unavyoona wewe binafsi, kama mara nyingi alivyojaribu kuonya yeye mwenyewe ndugu Juma kwamba pasitumike 'hoja za mitaani' lakini bahati mbaya yeye mwenyewe anakwenda kinyume na kauli zake hizo".
JAWABU
Kwanza
: maneno yenu "Kama kawaida yake" hayaoneshi kuwa muna insafu. Tukichukulia kuwa maneno "Muandamo wa kifalaki" ni istilahi mpya, je kitendo hiki cha kutoa istilahi mpya kimejikariri mara ngapi katika kitabu changu hata iwe "Kama kawaida yake". Ni wazi kwamba lengo lenu si kujadili bali ni kuponda na kutia aibu baada ya kushindwa kukijibu kitabu changu kwa hoja za kielimu zinazokubalika.
pili
: Maneno "Inakwenda kinyume kabisa na mitazamo ya Wanavyuoni" yanaonesha kuwa hamujui mukisemacho, mwaporoja tu! Kwenda kinyume ni kuwa moja anasema "Kaja" mwengine anasema "Hakuja", huku ndio kwenda kinyume. Ama kusema kitu kipya tu ambacho hakijasemwa huko hakuitwi kwenda kinyume. Ingekuwa ni kinyume lau kuna wanazuoni waliokataa kwamba hakuna muandamo wa kifalaki, mimi nikauthibitisha, hapo ndio kwenda kinyume.
Tatu
: Ilikuwa ni wajibu wenu kunukuu maneno yangu yote niliosema kisha mukayajibu: sio kuwambia watu "Amejaribu kuugawa muuandamo wa mwezi katika sehemu mbili kama alivyodai mwenyewe katika kitabu chake uk 18 kwa kusema: (Hali ya kwanza: ni ya muandamo wa kifalaki.) na (Hali ya pili: ni ya muandamo wa Kisharia."
Nnne
: Tazameni maneno yangu vizuri nilisema: "Hali ya kwanza: ni ya muandamo wa kifalaki. Na huu sio ule tunaouita muandamo. Hapa tutatumia tu neno "Muandamo" kwa ajili ya kufahamiana. Huu ndio ambao unazungumziwa na Aya hizo tulizotangulia kuzinukuu. Na ndio unaotokea mara moja duniani kote". Maneno haya yote mumeyaruka ili mupate kufikia lengo lenu; lakini watu hamuwadanganyi kwani wanasoma na kujionea. Kwa hivyo, ni wazi - kwa kila mwenye akili licha ya mwenye elimu - kwamba mimi sikuuita huo kuwa ni muandamo, bali nimetumia lugha hio ili kutaka kuikurubisha maudhii katika fahamu za watu kuwa mwezi unakuwa umekamilisha safari yake baada ya kuvikata vituo ishirini na nane, na hapo huwa umemaliza mzunguko wake. Na huu ndio tuoweza kuuthibitisha kwa Aya zenye kutaja kupita kwa mwezi kwenye manazili.
Tano
: Eleweni kwamba kinachotazamwa katika uwanja wa elimu si istilahat (technical terms), bali ni uhakika (facts) Yaani hali hio ya mw ezi kukamilika safari yake ndio uhakika (facts) na hilo jila nililoupa ni istilah tu. Sasa kama mulikuwa ni watu wa kufahamu mungelijadili uhakika (facts) na kubainisha kwamba nilivyosema sivyo. Ama istilahat (technical terms) mtu anawez a kukikipa kitu jina lolote lile kwani muhimu ni kuwa afahamike anakusudia nini. Na hili ni jambo ambalo wanavyuoni wanalizungumzia sana katika vitabu vyao vya Usuli na Furu'i, na ndio makusudio yao pale wanaposema: Hakuna kuvutana ka tika maneno ya kitaalamu au ya kifani (technical terms). Lakini kwa vile wenzetu walivyokuwa masikini wa elimu, basi wameona kule kutaja muandamo wa falaki - pamoja na kuwa nimebainisha kuwa huo si muandamo, bali natumia neno hilo ili kufahamiana - kuwa hilo ni kosa la jinai kwani ni jina ambalo halikutumiwa na wanavyuoni! Maskini wenzetu!
Sita
: Ni kudai kwenu kwamba sikunukuu kauli za Maulamaa. Sijui munataka Maulamaa gani tena. Rejeeni maandiko yangu nilipozungumzia mas-ala haya muone kauli za Al-Tukhi, Al-Baghawi, Al-Zamakhshari, Al-Qurtubi na wengine wengi. Au hawa si wanavyuoni?! Saba: Ni kuwa nyinyi katika kukipinga Qias cha Sala na funga mumeleta hoja zenu binafsi: hakuna mjuzi yeyote anayetoa hoja hizo. Nazo ni hoja zenye kuonesha uchache au utovu wa maarifa.
MUNASEMA
"Ukiangalia katika kitabu cha "Kuandama Kwa Mwezi" uk 6 - 7 cha Shaykh Naaswir Bachuu, utaona kwamba yeye hakuporoja, bali amenukuu hoja za Wanavyuoni katika vitabu zaidi ya kumi. Baadhi yao ni kama vifuatavyo:- Tafsiri ya Durul-Manthuur: Imam as-Suyuuty katika tafsiri yake iitwayo "Durul-Manthuur" ameandika hivi "Amepokea Al-Khalib katika vitabu vya nyota kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'Anhu) kwamba kauli ya Mungu isemayo: "Na mwezi tumeupanga vituo husafiri (vituoni humo) hadi kurudi ukiwa kama karara la mtende." Amesema: "Ni vituo ishirini na nane ambavyo mwezi hutua humo kwa muda wa mwezi mzima, kumi na nne kati ya hivyo vipo magharibi na kumi na nne vyenginevyo viko mashariki."
Baada ya kuvitaja vituo hivyo akaendelea kusema: "Utakapomaliza (kusafiri katika) vituo ishirini na nane, hurudi ukiwa kama karara la mtende, kama ulivyokua mwanzo wa mwezi." (Durul-Manthuur: J. 5, uk. 495) Tafsiri ya Qurtubiy: Naye Imam Al-Qurtubiy amesema haya yafuatayo: "Na vituo vilivyotajwa katika aya hii ni ishirini na nane...." Akavitaja kwa majina kisha akasema: "Mwezi unapofika katika kituo cha mwiisho hurudi tena katika kituo cha mwanzo, kwa hivyo humaliza mzunguko mmoja katika siku ishirini na nane, kisha hufichika, kisha huchomoza tena katika sura ya uchanga (mwandamo) na kurejea katika safari yake kwenye vituo vilivyotajwa". (Tafsirul-Qurtubiy J. 8, uk. 21)".
Jawabu
Je katika kitabu changu hayamo hayo mulioyanukuu kutoka kwa Sheikh Nassor Bachoo hata langu liwe porojo lake lisiwe? Je mimi pia sikunukuu kauli za wanavyuoni juu ya Haya. Bali mimi nimenukuu kutoka kwa mtu ambaye alimu ya nyota ndio fani yake, naye ni Al-Tukhi, huyu ni bora katika fani hii kuliko hao wafasirina. Hebu rejeeni ukurasa wa 17-22 wa chapa ya pili ya kitabu Ushahidi Uliowekwa Wazi. Bali mimi nimewasiliana na mtaalamu wa falaki anayekubalika na akasema kuwa hakuna makosa katika nilioyaandika, na barua yangu kwake na majibu yake nimeyaweka katika uk. 11-13, wa kitabu changu. Tafadhali rejeeni huko. Pili ni kuwa Sheikhe wenu Bachoo ndiye aliyekosea alipotoa hoja kwa Hadithi ya kutunga. Kama alivyodai kwamba Kuraib hajulikani na wanavyuoni wa Hadithi, na akadai kuwa Al-Imamu Abu Muslim Al-Rawahi (Ibadhi) ni miongoni mwa waliosema kuwa muandamo mmoja unatosheleza duniani kote. Yote haya nyinyi munayafumbia macho na kusema "Sheikh Nassor hakuporoja". Ni wazi kwamba hamutafuti haki, bali ni ushabiki tu.
MNASEMA
Wala haina maana kwamba Shaykh Naaswir Bachuu, kwa kuzinukuu tafsiri hizo anaashiria kuwa watu wafunge kwa kutumia huo alioita ndugu Juma 'Mwezi wa falaki. Jawabu Mimi nilichokisema ni hiki: Sh. Nassor Bachoo ni mmoja wa Wazanzibari waliojitokeza kuzungumzia mas-ala haya. Katika kitabu chake, Sheikh kaizungumzia maudhui hii na akanukuu Aya ya 5 ya Sura ya 10 ambayo ni ya pili katika Aya tulizozinukuu kabla. Baada ya maelezo alisema: Qur-an inalieleza suala la kuandama kwa mwezi kama ni tukio moja wapo kati ya matukio yaliyopangwa na Mwenyezi Mungu kutukia kila mwezi mara moja duniani kote. Mwisho wa kunukuu.
Ukianzia uk. 5. hadi uk. 8, wa kitabu chake, utaona kwamba Sh. Nassor Bachoo anathibitisha mwenendo wa mwezi kupitia katika Manazil (vituo) yake. Ufupisho wake - kama tulivyotangulia kusema - ni kuwa mwezi unasafiri kwa muda wa siku ishirini na nane (28) kupitia katika vituo hivyo, na siku moja au mbili hupotea kisha kudhihiri na kuweza kuonekana duniani. Sheikh aliishia maneno yake kwa kusema: "Baada ya maelezo haya tunatumai tumeweza kuelewa mtazamo wa Qur-an juu ya kuandama kwa mwezi." Mwisho wa kunukuu.
KISHA NAMI NIKANENA
Sasa ukitazama sentensi mbili hizi za Sh. Bachoo, utaona kuwa anakusudia kuthibitisha kitu kimoja kwa Aya ambayo haimpatii malengo yake. Anachokusudia kukithibitisha Sh. Bachoo - kwa inavyoonesha kutokana na maandishi yake - ni kuwa muandamo ni mmoja duniani kote na kwa hivyo - bila shaka anakusudia kusema - kwamba sote tufunge kwa muandamo mmoja huo. Ndio maana akasema: "Qur-an inaeleza suala la kuandama kwa mwezi kama ni tukio moja wapo kati ya matukio yaliopangwa na Mwenyezi Mungu kutukia kila mwezi mara moja duniani kote." Lakini dai kwamba Qur-an inasema kuwa muandamo wa mwezi unatokea mara moja tu dunia nzima - ikiwa anakusudia muandamo wa kisharia nao bila shaka ndio anaouzungumzia - si sahihi. Na sijui wapi Qur-an imesema hivi?!
Kwa hivyo, ni wazi kwamba mimi napinga kutoa kwake (Sheikh Bachoo) ushahidi kwa Aya hio kama ni dalili ya muandamo wa mwezi. Nasema kuwa Aya haina maana ya muandamo wa mwezi bali ina maana ya kukakamilika mzunguko wa mwezi ambako ndiko nimekuita "Muandamo wa kifalaki" yaani the moon has been astronomically born: not judicially. Ama muandamo wa mwezi kisharia ni:
1) Kuuona kwa macho siku ya mwezi 29.
2) Kutimiza idadi ya siku 30.
Huu ndio muandamo wa mwezi kisharia. Ama kukamilika mzunguko, huo si muandamo kisharia kwani mwezi unaweza kukamilika mzunguko na usionekane duniani wala kusiwe na uwezekano wa kuonekana. Kwa hivyo, bado hamujajibu nilivyosema. Nasema kuwa Sheikhe wetu alivyoihusisha Aya hio, basi kakosea. Lakini hamutaki kukiri kwa sababu hamutafuti haki, mwatafuta kumlinda mtu fulani na kumshambulia fulani; na kuisapoti rai fulani na kuipinga nyengine hata kama ushahidi unakusuteni. Kiufupi ni kuwa Sheikh Bachoo aliposema hivyo, alikuwa anathibitisha muandamo mmoja kwa kutumia Aya hio, sasa vipi tena mutadai kuwa: "Wala haina maana kwamba Shaykh Naaswir Bachuu, kwa kuzinukuu tafsiri hizo anaashiria kuwa watu wafunge kwa kutumia huo alioita ndugu Juma 'Mwezi wa falaki."
MNASEMA
"Kwanza ni vyema kuelewa kwamba hakuna hiyo dhana ya muandamo wa kifalaki lakini kitaaluma kuna: "mwezi mpya" usioonekana (the invisible new moon) na "mwezi mchanga" unaonekana (the visible young crescent ). Ndio maana Shaykh Naaswir Bachuu akaandika katika kitabu chake uk 87 - 88 kwa kusema hivi: Tukirejea katika mada yetu ya kuandama kwa mwezi, itakuwa vizuri hapa kama tutamnukuu mtaalamu wa elimu hii ya annga (Astronomy), Dr. S. K. Abdali katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la Al-Ittihad la Mombasa Kenya, litolewalo mwaka mara nne; la kipindi cha Januari - Julai 1979. Amesema: "... Huu 'mwezi mpya' usioonekana (the invisible new moon) ambao majira yake hupatikana katika makalenda na magazeti, usichanganywe na mwezi mchanga unaoonekana (the visible young crescent) ambao (kutokana na mwezi huo mchanga) huanza mwezi mpya katika kalenda ya Kiislam...".
Hapa tunajifunza jambo moja muhimu kuwa 'mwezi mpya' (new moon) ni tofauti na 'mwezi mchanga' (young crescent). Na mwezi mchanga ndio tunaoutumia Waislam kujua kalenda (tarehe) yetu. Kwa hivyo hapa Shaykh Naaswir anasisitiza jambo la kutumika mwezi unaoonekana katika hukumu ya muandamo. Pili: Katika kitabu kizima cha Shaykh Naaswir kimeandikwa kwa msisitizo wa kutosha wa kwamba hukumu ya kufunga na kufungua ni lazima uonekane mwezi muandamo au kukamilisha siku 30 kama patapatikana udhuru wa kutoonekana mwezi siku ya tarehe 29. Ameyasema hayo Shaykh Naaswir akiwa anajua fika kwamba huo mwezi (aliouita ndugu Juma wa Falaki) hauna hukumu ya kufanya mtu afunge au afungue, kwani hauonekani kwa macho ya kawaida (the invisible new moon). Unajulikana kwa mahesabu ya Kitaalamu au kwa kuangaliwa kwa vyombo vya Kitaalamu.
JAWABU 1)
Kwanza nimeshakujibuni kuwa: wanavyuoni wote wanakubali na wamesema kuwa: Hakuna kujadiliana katika maneno ya kitaalamu au ya kifani. Kwa hivyo, je mwezi huo tuuite ni mwezi wa kifalaki kama alivyouita Juma Mazrui au tuuite 'Mwezi mpya' usioonekana (the invisible new moon) kama alivyouita mtaalamu wa falaki, hili si muhimu kielimu. Muhimu je huo aliouita Juma Mazrui kuwa ni muandamo wa kifali upo au haupo? Tena, je makusudio yake kwa kuuita muandamo wa kifalaki ni sawa na makusudio ya yule mtaalamu wa kifalaki alipouita 'Mwezi mpya' usioonekana (the invisible new moon). au Juma Mazrui anakusudia kitu chengine na mtaalamu wa falaki anakusudia kitu chengine? Haya ndio mambo ambayo wenye elimu huyajadili: sio kujadili majina, bali kinachojadiliwa ni uhakika (facts).
2) ni kuwa kama munatoa hoja kama hizo, basi hata hio dhana ya 'Mwezi mpya' usioonekana (the invisible new moon) pia katika Uislamu haipo. Hii Qur-ani na hizo Hadithi za Mtume (s.a.w.) haya nitoleeni palipoandikwa 'Mwezi mpya' usioonekana (the invisible new moon). Ni wazi kwamba jina hilo halipo katika Uislamu, lakini suala ni kuw a je uhakika (facts) wa 'Mwezi mpya' usioonekana (the invisible new moon) upo au haupo.
Wataalamu huwa wanatafiti uhakika (facts ) kisha wakishakugundua kitu wanakipa jina. Jina huwa ni jipya na uhakika hua upo zamani. Na jina la kitaala mu huwa linatafautika katika nchi hadi nchi; zama hadi zama; bali wakati mwengine baina ya mtaalamu au mpekuzi mmoja na mwengine. Lakini ndugu zetu, hamutaki kujiweka katika nafasi yenu aliokupeni Allah ya uchache wa maarifa, kisha munawambia watu wanajikweza, sijui nani anayejikweza. 3) Tatu: Eleweni tena, mimi nilikuwa najibu kitu gani? Mimi nilikuwa napinga kuhusishwa Aya"Yeye (Allah) Ndiye aliyelifanya jua kua muanga na mwezi kua nuru na akaupimia (huo mwezi) vituo, ili mujue idadi ya miaka na hisabu"
na suala la muandamo wa mwezi Kisharia: nasema Aya hii haina uhusiano huo kamwe.