7
MUANDAMO WA MWEZI
SEHEMU YA TISA
UFAFANUZI WA NENO 'AHILLAH'
Katika kitabu changu nilisema yafuatayo: "Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo. Sema: Hivyo ni (vipimo vya) nyakati kwa ajili ya watu na Hija" Hapa kuna nukta mbili tatu ambazo tutazijadili kama zilivyotolewa na Sheikh Nassor Bachoo, katika kitabu chake
UFAFANUZI WA MGOGORO WA KUANDAMA KWA MWEZI"
Kuanzia uk. 8 hadi uk. 9 wa kitabu chake hicho, Sh. Bachoo, anazungumzia kuhusu mas-ala ya kuwepo na kutokuwepo miandamo mingi kwa mujibu wa Qur-an. Katika maelezo yake anaona kwamba katika Qur-an hakuna sehemu yoyote ile ilioeleza kwamba kuna miandamo mingi. Na kwa hivyo baada ya kuinukuu Aya hio ya 189 ya Sura ya 2, alisema:
"Baadhi ya watu wa Afrika ya Mashariki wanadhani kwamba Aya hio inakiri kuwepo kwa miandamo mingi. Dhana hio wameijenga kwenye lile neno "miezi miandamo." Ni kweli nen o hilo limekuja kwa wingi (plural) yaani limetaja "miezi mingi" au "miezi michanga" kwa hivyo watu hao tuliowataja wameona kuwa; kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametaja miezi mingi katika Aya hii basi anakiri kuwepo kwa miandamo mingi.
Kwa kweli dhana ya watu hawa juu ya tafsiri ya neno: Ahilla, yaani 'miezi miandamo' sio sahihi kwani neno hilo lilotajwa katika Aya hii ingawaje lina maana ya wingi lakini halikukusudiwa kumaanisha maana ya 'miezi mingi.' Kilichokusudiwa hapa ni kule kuelezwa 'hali ya miezi' kuwa nyingi yaani kwa kuwa mwezi huonekana kwa sura tafauti ndani ya kipindi kizima cha mwaka, imezingatiwa kuwa kama ni miezi mingi." Mwisho wa kunukuu.
Kisha Sheikh akanukuu mfano wa maneno hayo kutoka katika tafsiri ya Al-qurtubiy, ili kuipa nguvu tafsiri yake. Nami nina maelezo kidogo juu ya tafsiri ya Aya hii kama ifuatavyo: Kwa kuanzia ni kuwa Sheikh hakutoa ushahidi wa kielimu juu ya usahihi wa tafsiri alioitoa, kwani tafsiri inakwenda na ushahidi wake, ama: 1) Tafsiri ya Aya kwa Aya. 2) Au Aya kwa Hadithi. 3) Au kwa mujibu wa fani za lugha na usuli. Kwa ufupi ni kuwa neno Ahilla (miezi miandamo), kama alivyosema Sheikh, lina maana ya miezi mingi miandamo. Na hii ina uwezekano wa tafsiri mbili. Moja ni hio alioiita kuwa ni tafs iri ya watu wa Afrika Mashariki kwamba lafdhi Ahilla (miezi miandamo), ni dalili ya kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja.
Tafsiri hii inapata nguvu kwa mambo mawili: Moja ni kuwa sehemu ya pili ya Aya imeifasiri sehemu ya kwanza na kubainisha muradi wake. Sehemu ya kwanza inasema: "Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo." Halafu ikaja sehemu ya pili ikatoa tafsiri kwa kusema: "Sema hivyo ni (vipimo vya) nyakati kwa ajili ya watu na hija." Kwa hivyo ni wazi kwamba kinachozungumziwa hapa ni miandamo yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za mwezi, kwani vipimo vya nyakati na hija ni miandamo yenyewe: si hali tafauti za mwezi: hali tafauti za mwezi za kuwa mkubwa na mdogo haziwezi kuwa vipimo vya nyakati na hija. Kwa hivyo, tafsiri hio ya watu wa Afrika Mashariki - nao wamekulia katika chemchemu za elimu - ni tafsiri yenye muelekeo madhubuti sana.
Cha pili: chenye kuipa nguvu tafsiri yao hio, ni riwaya yenye kusema: "Kutoka kwa Ibn Umar (r.a.) kwamba Mtume(s.a.w.w)
kasema:'Hakika ya Allah kaijaalia miezi miandamo kuwa ni vipimo vya nyakati: mukiuona fungeni na mukiuona fungueni."
Ni wazi katika Hadithi hii kwamba kilichokusudiwa kwa neno Ahilla (miezi miandamo), ni miandamo yenyewe : si hali za mwezi. Na kwa hivyo, imesema Kaijaalia miezi miandamo kuwa ni vipimo vya nyakati.
Na akasimulia Abu Ghanim Al-khurasani - mpokezi wa Kiibadhi - Hadithi kama hio kutoka kwa Umar bin Al-khattab (r.a.) akisema: "Miezi miandamo ni vipimo vya nyakati, basi fungeni kwa kuuona na fungueni kwa kuuona, ikiwa wingu litauzi ba (au litauzinga kwa lugha nyengine) basi kamilisheni idadi ya siku thalathini." Sasa tukirudi katika tafsiri ya Sh. Bachoo, ambayo kaipa nguvu pia kwa tafsiri ya Al-imamu Al-qurtubiy, ni kuwa Sheikh - labda - hakutanabahi kwamba tafsiri hio alioitegemea kutoka kwa Al-qurtubiy na wengine, imejengeka katika Hadithi maudhui (ya kutunga). Nayo ni Hadithi alioisimulia Al-wahidiy na akainuku Al-suyutiy kutoka katika kitabu "TA-ARIKH DIMASHQ" cha Ibn Asakir na kutoka kwa Abu Nuaim, kwa njia ya Al-suddiy Al-saghir kutoka kwa Al-kalbiy kutoka kwa Abu Salih kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Muadh bin Jabal na Tha'alaba bin Ghanama walisema: 'Ewe Mjumbe wa Allah, kwanini mwezi unadhihiri na kuchomoza hali ya kuwa ni mdogo sana mfano wa uzi kisha unaongezeka mpaka unakuwa mkubwa na unakamilika na kuwa duara kisha unaendelea kupungua na kua mdogo mpaka unarudi kama ulivyokua, haui katika hali moja. Basi ikateremka Aya hio inayosema:"Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo"
.
Na riwaya alioinukuu Al-qurtubiy mwenyewe kabla ya maneno hayo alioyaelezea Sheikh Bachoo, inaeleza kwamba hayo ni maneno ya Mayahudi, japokuwa Muadh ndiye muulizaji. Nayo ni Hadithi dhaifu sana kama alivyosema Sh. Abdul-razzaaq Al-hadi, aliyeitia maelezo tafsiri ya Al-qurtubiy. Na pia kama alivyosema Al-alusi na wengineo. Nao ndio ukweli, kwani katika sanad yake kuna Al-sudiy Al-saghir, naye ni Moh'd bin Mar-wan. Anasema Jarir bin Abdi Al-hamid: "Mwongo." Anasema Al-dawri kutoka kwa Ibn Main: "Si mwenye kuaminika." Anasema Salih bin Moh'd: "Alikuwa dhaifu na alikuwa akitunga (Hadithi)." Anasema Abu Hatim: "Hadithi zake zinaporomoka: Hadithi zake zinaachwa: Hadithi zake haziandikwi kamwe." Anasema Ibn Adey: "Udhaifu katika Hadithi zake uko bayana." Anasema Al-jawzjani: "Hadithi zake zinaporomoka." Anasema Ibn Hibban "Si halali kuandika Hadithi zake ila kwa ajili ya kufatilia (Sanad), na wala hafanywi kuwa ni hoja kwa hali yoyote." Anasema Al-tabari: "Hadithi zake hazifanywi kuwa ni hoja." Anasema Abdullahi bin Numair: "Al-suddiy alikuwa mwongo mkubwa."
Pia katika sanad ya Hadithi hio kuna Al-kalbi, naye ni Moh'd bin Saib bin Bishr. Anasema Mu'utamir bin Sulaiman kutoka kwa baba yake: "Al-kufa palikuwa na waongo wawili: mmoja wao ni Al-kalbi." Anasema Laith bin Abi Sulaim: "Al-kufa palikuwa na waongo wawili: mmoja wao ni Al-kalbi na wa pili ni Al-suddiy." Anasema Yahya bin Main: "Si lolote si chochote." Na akasema katika riwaya ya pili: "Dhaifu."
Na Al-kalbiy kaipokea Hadithi hio kutoka kwa Abi Salih kutoka kwa Ibn Abbas. Anasema Al-suyutiy: "Abu Salih ni dhaif." Anasema Abdul-Razzaq Al-mahdiy katika maelezo yake juu ya tafsiri ya Al-baghawiy: "Abu Salih katika (riwaya zake alizozisimulia kutoka) kwa Ibn Abbas, si mwenye kuaminika. Kwa hivyo, tafsiri hio ya Al-qurtubiy inayosema kwamba maana ya Al-ahilla (miezi miandamo) ni hali zake tafauti, si tafsiri ya kushangiriwa sana kwani imejengeka katika Hadithi maudhui (ya kutunga) au dhaifu sana.
JAWABU NILILOPATA
Ndugu zangu wakanijibu hivi: "Ufafanuzi Wa Neno 'Ahillah' Ufafanuzi wa Aya ya Qur-aan:"Wanakuuliza juu ya miezi. Sema: "Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu (mengine) na ya Hijja (zao)
. (2: 189) Hapa Ndugu yetu Juma katika kosoa kosoa zake anaona kama hivi ifuatavyo kwa mujibu anavyosema katika kitabu chake uk 56 - 57: (Kwa hivyo ni wazi kwamba kinachozungumziwa hapa ni miandamo yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za mwezi, kwani vipimo vya nyakati na hija ni miandamo yenyewe: si hali tafauti za mwezi: hali tafauti za mwezi za kuwa mkubwa na mdogo haziwezi kuwa vipimo vya nyakati na hija.)
SISI TUNAJIBU KAMA IFUATAVYO
Neno 'yas-aluunaka' ambalo tafsiri yake ni "Wanakuuliza" tunaweza kuligawa sehemu tatu zifuatazo:-
1. Wenye kuuliza (waulizaji).
2. Mwenye kuulizwa (muulizwaji).
3. Chenye kuuliziwa (kinachouliziwa).
1. Wenye kuuliza (Waulizaji): Kwa hapa bila shaka ima itakuwa ni Waislamu waliokuwa katika hadhara ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) - yaani Masahaba au kama sio Waislamu watakuwa ni makafiri. Lakini kwa mujibu wa Tafsiri nyingi za Wanavyuoni wengi wenye kutegemewa katika fani hii ya tafsiri na baadhi ya vitabu vyengine - vimeeleza kwamba Masahaba ndio waliomuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)".
2. Mwenye kuulizwa hapa bila shaka yoyote atakuwa ni mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani yeye ndiye aliyeteremshiwa hiyo Qur-aan Tukufu. Na Aya kama hizi zipo nyingi katika Qur-aani Tukufu. Angalia: (2: 215, 217, 219, 220, 222).
3. Chenye kuuliziwa kwa hapa ni zile hali za mwezi kama yalivyobainishwa hayo na Wanavyuoni katika tafsiri zenye kutegemewa katika fani hii ya tafsiri. Ni vyema kuelewa kwamba Qur-aan ina utaratibu wake maalumu wa kuitafsiri, hususan inapokuwa katika mjadala wa kielimu au katika kutoa hoja juu ya hukumu ya jambo fulani, lazima yatolewe madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni wenye kutegemewa. Wala sio busara mtu yeyote kutoa fikra zake binafsi hasa kama mtu huyo hajafikia katika daraja ya "Ijtihaad." Kwa mantiki hiyo, ndio maana ukaona katika kitabu cha "Kuandama Kwa Mwezi" cha Shaykh Naaswir Bachuu kila anapotoa hoja ya jambo fulani huwa anatoa madondoo maalumu hata pale anapotaja tafsiri ya baadhi ya Aya za Qur-aan.
JAWABU
Kwanza
: mumepata wapi kwamba mtu lazima ategemee tafsiri za wanavyuoni? Maneno ya wanavyuoni si hoja za Kisharia ila wakikubaliana, na hapo hoja huwa ipo katika katika ijma'a (makubaliano) yao. Nakukumbusheni kauli yenu muliposema: "Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas b ila ya kuonyesha dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu".
Pili
: ni kuwa wanavyuoni wa tafsiri wametumia riwaya nyingi za kutunga na dhaifu sana katika tafsiri zao. Kwa mfano kisa cha Malaika wanaoadhibiwa huko Iraki hadi leo! Kisa hiki ni katika riwaya za kiisraili. Wakati wanavyuoni wa tafsiri wamekitaja na wengine kwa kukikubali. Na kwa hivyo anasema Al-Imamu Ahmad kuwa riwaya za tafsiri hazina msingi kamwe, ingawa dhahir si kwamba Al-Imamu Ahmad anakusudia kuzikanusha riwaya zote za tafsiri; bali - dhahir ni kuwa - anakusudia kutokuwepo usahihi kwa asilimia kubwa ya riwaya hizo kama alivyosema Al-Zarqani. Chukua kwa mfano tafsiri ya Al-Tha'alabi. Utaona kwamba tafsiri yake ni mashuhuri kwa Hadithi za kutunga. Anasema Abdu-Razzaq Al-Mahdi katika utangulizi wake alioutia katika tafsiri ya Al-Baghawi: "Jua ewe ndugu Muislamu kwamba vitabu vyote vya tafsiri vimekusanya Hadithi dhaifu na za kutunga na riwaya za Kiisraili munkar na visa vibovu havina haja hata ya kuvitaja. Na katika hizo ni Hadithi zilizotungwa kuhusu fadhila za Qur-ani sura moja moja alizozisimulia Al-Tha'alabi katika tafsiri yake.na Maimamu wameeleza kwa uwazi kuwa ni za kutunga."
Anasema Ibn Al-Jawzi baada ya kutaja Hadithi ya kutunga: "Na ameitawanya Hadithi hii Al-Tha'alabi katika tafsiri yake..na akafatiwa na Abu Al-Hasan Al-wahidiy katika hayo, nayo si ajabu kwao kwani wao si watu wa (elimu ya) Hadithi." Hio ni mifano michache katika mingi lau twaikusanya basi tunaandika juzuu nyingi za kitabu. Kwa hivyo, marejeo ni kanuni za tafsiri za lugha, usuli-fiq-hi na Usulil-Hadithi: si mwanachuoni kasema nini. Hadithi ikiwa na sanad dhaifu au ya kutunga hakuna mwenye uwezo wa kuikweza akaifanya sahihi hata akiwa na elimu kiasi gani. Kwa hivyo, nakubaliana na nyinyi muliposema: "Ni vyema kuelewa kwamba Qur-aan ina utaratibu wake maalumu wa kuitafsiri, hususan inapokuwa katika mjadala wa kielimu au katika kutoa hoja juu ya hukumu ya jambo Fulani". Kwa bahati mbaya nyinyi na Sheikh Bachoo taratibu hizo hamukuzifata kamwe. Ama kauli yenu: "Lazima yatolewe madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni wenye kutegemewa" hili nakupingeni, bali ni lazima ujue kanuni za tafsiri kisha tafsiri yako iwe kwa mujibu wa kanuni hizo. Ama wafasirina wamesema kauli sahihi na dhaifu; wametegemea riwaya sahihi na dhaifu na za kutunga kama nilivyokunakilieni maneno ya wajuzi.
Cha pili ni kuwa kauli yenu: "Kwa mantiki hiyo, ndio maana ukaona katika kitabu cha "Kuandama Kwa Mwezi" cha Shaykh Naaswir Bachuu kila anapotoa hoja ya jambo fulani huwa anatoa madondoo maalumu hata pale anapotaja tafsiri ya baadhi ya Aya za Qur-aan" maneno haya si sahihi. Sheikh Bachoo kasema Kuraib hajulikani, haya wapi kayapata maneno haya?!
Tatu
: Ikiwa nyinyi hamuna uwezo wa kuifahamu tafsiri sahihi ya Aya, au hamuwezi kupambanua baada ya kuzitazama hoja tafauti za wanavyuoni juu ya tafsiri kwa kutokuwa na elimu ya nahau, sarfu, balagha na usuli, basi si kwamba kila mtu yuko hivyo. Kwa ivyo, anayeweza kuzitazama kauli za wanavyuoni na kuzipambanua na-afanye: asiyeweza na-aulize. Nyinyi hamuwezi na kuuliza hamutaki, munashikilia msimamo huo huo tu. Hata wale wenye elimu kukushindeni nyinyi kule Saudia akina Sheikh Bin Baz na Sheikh Ibn 'Uthaimin na wanavyuoni wote wa Saudia wamebadilisha msimamo baada ya kuona kuwa hoja sahihi ni zile walizoshikana nazo wale wenye kusema kwamba kila watu na muandamo wao. Nyinyi pamoja na udhaifu wenu mmekaa kupinga tu ilhali hamuna uwezo wa kifani wa kuweza kufikia natija sahihi.
Nne
: ni kuwa mas-ala haya hayahusiani na elimu ya tafsiri; bali ni mas-ala ya riwaya marejeo yake ni wanavyuoni wa Hadithi. Na waliotia maelezo tafsiri za Qur-an na kuielezea riwaya hio wamesema kwa uwazi kwamba riwaya hio si hoja. Anasema Abdul-Razzaq Al-Mahdi katika maelezo yake juu ya tafsir ya Al-Zamakhshari baada ya kuinukuu riwaya hio: "Kaitaja Al-Wahidi katika Asbabu Al-Nuzul bila ya sanad. Na hii haina maana kabisa, kwani mbali na kuwa haina sanad, ni riwaya ya Al-Kalbi na jina lake ni Muhammad bin Al-Saib naye ni mwenye kuachwa mwenye kutuhumiwa (kwa uwongo)." Na katika maelezo yake juu ya tafsiri ya Al-Baghawi, baada ya Al-Baghawi kuitaja riwaya hio, Sheikh Abdul-Razzaq anasema kwamba (ni Hadithi): "Dhaifu sana na sanad hii inaporomoka, Al-Suddiy ni mwenye kuachwa na Al-Kalbi ni mwenye kutuhumiwa (kwa uwongo)." Na hata Al-Alusi - naye ni katika watu wa tafsiri - anasema: "Ameipokea Ibn 'Asakir kwa sanad dhaifu..".
MNASEMA
Kitu cha msingi hapa ni kujua kwamba: Je suala liliulizwa au halikuulizwa? Hata kama waliouliza ni Masahaba au Mayahudi. Bila shaka Aliyesema kwamba paliulizwa suala ni Mwenyewe Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliposema: {{Wanakuuliza}}
JAWABU
Suala liliulizwa. Lakini mimi upinzani wangu haukuwa hapo. Mimi nilichokipinga ni kudai kwa Sheikh Bachoo kwamba: Kwa kweli dhana ya watu hawa juu ya tafsiri ya neno: Ahilla, yaani 'miezi miandamo' sio sahihi kwani neno hilo lilotajwa katika Aya hii ingawaje lina maana ya wingi lakini halikukusudiwa kumaanisha maana ya 'miezi mingi.' Kilichokusudiwa hapa ni kule kuelezwa 'hali ya miezi' kuw a nyingi yaani kwa kuwa mwezi huonekana kwa sura tafauti ndani ya kipindi kizima cha mwaka, imezingatiwa kuwa kama ni miezi mingi. Na mimi nimejibu kwamba:
1) Aya inasema kuwa:miandamo ya mwezi ni vipimo vya nyakati na Hija.
Kwa hivyo ni wazi kwamba kinachozungumziwa hapa ni miandamo yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za mwezi, kwani vipimo vya nyakati na hija ni miandamo yenyewe: si hali tafauti za mwezi: hali tafauti za mwezi za kuwa mkubwa na mdogo haziwezi kuwa vipimo vya nyakati na hija.
2) Tafsiri alioitegemea Sheikh Bachoo tegemeo lake ni Hadithi ya kutunga. Kwa hivyo, ili niwe nimejibiwa, basi thibitisheni kuwa:
1) Hali tafauti za mwezi za kuwa mkubwa na mdogo ndio vipimo vya nyakati na Hija. Na mukanushe kwa hoja kwamba kuandama kwa mwezi sio vipimo vya nyakati na Hija.
2) Thibitisheni kwa hoja za kielimu zinazokubalika katika elimu ya Hadithi kwamba riwaya hio ya kuwa Mtume (s.a.w.) aliulizwa kuhusu hali tafauti za mwezi ni riwaya sahihi. Na hili hamutoliweza mpaka ngamia atapita kwenye tundu ya sindano hata mukiomba msada kwa binaadamu na majini wote.
MNASEMA
Masahaba walitaka kujua kwa kina juu ya hali za miezi, mbona mara unakuwa mkubwa, mara mdogo, mara unapotea hauonekani kabisa, mara hali hii mara hali ile? Bila shaka jawabu ingetarajiwa iwe yenye kufafanua hali halisi ya matokeo hayo lakini jawabu ilikuja kutaja "hikma" ya kupatikana hali hizo nazo ni kujua nyakati za Ibada za watu. Yaani kuweza kujua wakati wa kufunga (Swaum), Hijja, Zakka na shughuli nyengine za kimaisha. Ikumbukwe kwamba utaratibu kama huu wa kuulizwa suala na jawabu ikataja hekima ya jambo lenyewe badala ya kufafanuliwa hilo jambo lenyewe ni jambo maarufu katika fani ya "Balagha" ijulikanayo kwa jina la "Uslubul-Hakiim" Angalia kwa makini baadhi ya madondoo kutoka katika kitabu Al-Balaghal - Waadhihah kama ifuatayo: Masahaba walimuuliza Mtume (S walla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu (hali za) miezi, vipi mwezi huonekana mdogo kisha unakamilika nuru yake (kwa kuwa mkubwa) kisha unakuwa mdogo katika hali ya kutoonekana. Mas-ala haya ni miongoni mwa mas-ala yanayohusu elimu ya nyota yanayohitajia uchambuzi mrefu na wa kina, ndio maana Qur-aan Tukufu ikawacha uchambuzi huo, na badala yake ikabainisha kuwa (hali hizi) za miezi ni njia za kujua nyakati za kazi na ibada mbali mbali".
JAWABU
Uslubu Al-Hakim si kazi yake kusahihisha riwaya dhaifu, bali kazi yake ni kuonesha hekima ya jawbu. Tunachokitaka ni sanad sahihi ya riwaya ya uwongo wa Al-Kalbi na Al-Sudi mulioitegemea. Ivo ndio munawalingania watu kukamatana na riwaya yenye sana za waongo halafu munasema nyinyi ndio munafata Sunna?! Tafadhalini leteni sanad sahihi ya riwaya hii, musibabaishe huku na kule. Kama hamuna musione haya kutangaza ukweli.
Pili
: lazima mujue kwamba sababu iliompelekea mwenye kitabu Al-Balaghal - Waadhihah na wengine kuiita jawabu hio ya Qur-an kuwa imekuja katika mfumo wa "Uslubul-Hakiim" si kuitazama Qur-ani yenyewe; bali waliitazama hio riwaya dio wakatoa natija hio kwamba jawabu "Hiyo ni vipimo vya nyakati na Hija" ni "Uslubul-Hakiim". Sasa kama ni hivyo, basi el eweni kwamba riwaya hio ni dhaifu mno, bali ni ya kutunga haiwezi kujenga hoja.
Munasema Kwa hiyo tukichunguza Aya hiyo"Wanakuuliza"
tutaona kuwa, Aya yenyewe inatuthibitishia wazi kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sa llam) aliulizwa, na waliomuuliza walikuwa ni Masahaba na alichoulizwa ni hali za miezi kama tulivyokwishaelezea.
Jawabu Aya inathibitisha kuwa Mtume (kaulizwa) kuhusu miandamo ya mwezi: si hali tafauti za mwezi. Lakini mumepata wapi madai kwamba: "Aya yenyewe inatuthibitishia kwamba.waliomuuliza walikuwa ni Masahaba na alichoulizwa ni hali za miezi kama tulivyokwishaelezea?". Tupeni ushahidi wa waulizaji walikuwa Masahaba katika Aya. Lakini hili si muhimu natusameheane. Leteni ushahadi wa hali tafauti za mwezi katika Aya hio au katika riwaya sahihi, musilazimishe tafsiri japokuwa ni tafsiri dhaifu kwa ushahidi wa kielimu. Wala musiisahau kauli yenu muliposema: "Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas bila ya kuonyesha dalili zenye kuku balika kifani, huo utakuwa ni udhaifu".
MNASEMA
Kwa vyovyote vile kushikamana na Qur-aan ni jambo bora zaidi (aula) hususan inapotokezea khitilafu juu ya jambo au hukumu fulani. Shaykh Saalimiy katika kitabu chake anasisitiza zaidi katika jambo la kushikamana na Qur-aan hasa pale zinapopatikana ikhtilafu juu ya jambo fulani katika Umma:
Mwenye kushikamana na dhahir (ya manen o) ya kitabu cha Mwenyezi Mungu wakati ambapo Umma (wa Kiislam) umetafautiana juu ya hukumu ya jambo (fulani) au habari (fulani) bila shaka (mtu huyo) atakuwa ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika.
JAWABU
Sasa nyinyi mumeshikana na sehemu gani katika Aya hio kuthibitisha madai yenu?
MNASEMA
Ama kuitolea hoja Aya hiyo (Wanakuuliza) kuwa ni dalili ya kuthibitisha kuwepo kwa muandamo wa kisheria au kuwa ni dalili ya kwamba kila nchi ifunge kwa muandamo wake au kuthibitisha kuwepo kwa 'miandamo mingi' huko ni kushindwa kuifahamu makusudio ya Aya. Vile vile ni kwenda kinyume na maelezo ya Wanazuoni katika vitabu vyao vya tafsiri, kwani Qur-aan ni lazima itafsiriwe kwa kuzingatia misingi yake maalum na kanuni zake zinazokubalika katika hiyo fani ya tafsiri. Shaykh Ahmad Al-Khaliil (Mufti Mkuu wa Oman ) alipokuwa akielezea rai za Wanavyuoni juu ya aina za tafsiri ya Qur-aan- ameeleza haya yafuatayo:
Kauli yenye nguvu ni kuwa inafaa kutafsiri Qur-aan kwa kutumia rai (lakini) kwa yule aliyekusanya sharti ambazo lazima Mfasiri awe nazo. Sharti zenyewe tumeshazieleza katika darsa iliyopita. Wala Mfasiri huyo asitie (katika tafsiri yake hiyo) matamanio ya nafsi yake. Bali rai yake hiyo iwe ni faida itokanayo na madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni zenye kutegemewa katika fani hii ya tafsiri. (Sio kubuni tafsiri isiyoeleweka wala isiyokubalika katika misingi ya Dini) vile vile azingatie vizuri tokeo lililosababisha kuteremshwa Aya hiyo anayoifasiri, (lazima) aangalie "Sababun - Nuzuul"
JAWABU
Kwanza
: rekebisheni ghushi zenu au kusukuma kwenu. Maneno ya Sheikh Al-Khalili yasemayo: nyinyi mumeyafasiri Bali rai yake hiyo iwe ni faida itokanayo na madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni zenye kutege mewa katika fani hii ya tafsiri. (Sio kubuni tafsiri isiyoeleweka wala isiyokubalika katika misingi ya Dini). Masadir Al-Tafsir (vyanzo au sources za tafsiri) anazozikusudia Sheikh si tafsiri za wanavyuoni, bali ni fani za kutafsiria Qur-an. Mwenyewe kalieleza hilo kuanzia ukurasa wa 20 wa juzuu ya kwanza ya tafsiri yake Jawahiru Al-Tafasir. Sasa nyinyi ndugu zangu ikiwa maneno ya wanavyuoni hata kuyafahamu hamuyafahamu; kitu gani kilichokupelekeeni kujitumbukiza katika kulielezea jambo hili?! Na kama Sheikh anaona kuwa lazima mtu arejee katika tafsiri za wanavyuoni, haya ilikuwaje tena aipe nguvu kauli ya kujuzu kufasiri kwa rai kwa yule mwenye zana za elimu?! Hamuji mukisemacho!
Pili
: mimi sikutoa ushahidi kwa kipande cha Aya kisemacho:"Wanakuuliza"
tu kuwa ni dalili ya kuthibitisha kuwepo kwa muandamo wa kisheria, kama mulivyobutuwa nyinyi hapa. Dalili ya muandamo wa kisharia katika Aya hii iko katika neno "Ahilla". Tafsiri ya Ahilla ni mwezi miandamo. Na muandamo wa kis haria ni kuuona mwezi au kuthibiti kwa idadi ya siku 30. Sasa kama huu si muandamo wa kisharia ni muandamo gani? Bali Aya yenyewe imejieleza hivyo. Aya - kiukamilifu - inasema:"Wanakuuliza juu ya miezi miandamo. Sema: "Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na vya Hijja (zao) "
. Sasa ikiwa Aya inasema kwamba Al-Ahilla(miezi miandamo) ni vipimo vya nyakati na hija vipi nyinyi mutasema kwamba kusema kuwa Aya hii hapa ni dalili ya miandamo ya Kisharia ni makosa? Jamani! Lakini muko makini au basi "Kake kanena namiye nanena tu?!"
Ama kauli yenu kwamba Aya hio ni kosa kuifasiri hivyo.Au kuwa ni dalili ya kwamba kila nchi ifunge kwa muandamo wake au kuthibitisha kuwepo kwa 'mian damo mingi.' Inaonesha kuwa hamukunifahamu nilivyosema. Mimi nilisema hivi: Kwa kuanzia ni kuwa Sheikh hakutoa ushahidi wa kielimu juu ya usahihi wa tafsiri alioitoa, kwani tafsiri inakwenda na ushahidi wake, ama: 1) Tafsiri ya Aya kwa Aya. 2) Au Aya kwa Hadithi. 3) Au kwa mujibu wa fani za lugha na usuli. Kwa ufupi ni kuwa neno Ahilla (miezi miandamo), kama alivyosema Sheikh, lina maana ya miezi mingi miandamo. Na hii ina uwezekano wa tafsiri mbili. Moja ni hio alioiita kuwa ni tafsiri ya watu wa Afrika Mashariki kwamba lafdhi Ahilla (miezi miandamo), ni dalili ya kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja. Haya ndio maelezo yamgu. Zingatia maneno Na hii ina uwezekano wa tafsiri mbili. Yaani ni dalili yenye uwezekano wa namna mbili:
1) Inawezekana ikawa maana ni kuwa miandamo iko tafauti. Msingi wa hili ni kuwa lafdhi iliotajwa ni Ahillah (miezi miandamo). Na vitu vikitajwa kwa wingi plural form basi kimoja huwa si cha pili au kwa lugha nyengine huwa ni vitu tafauti, ila kukiwa na Qarina kwamba ni kitu kimoja. Ikitajwa Ash-hur mwezi (ya siku 29-30), makusudio huwa ni mwezi tafauti sio mmoja hule hule; wakitajwa watu basi moja huwa si mwengine, n.k.
2) Au ikawa maana ni miandamo ya mwezi tafauti japo ya mji mmoja, yaani mfunguo mosi, pili tatu. n.k. Maana zote hizi zimo katika lafdhi ya neno "Ahillah (miezi miandamo)".
Pamoja na hayo, niliona kuwa tafsiri ya kwanza ni bora kwa sababu ya kupata kwake nguvu katika riwaya tulizozinuku. Pamoja na hayo, kutumia kwangu neno uwezekano kulitakiwa kukufahamisheni kwamba tafsiri hii si ya mkato kwa vile haiko wazi 100%. Inawezekana ikawa makusudio ni ya pili. Ama tafsiri ya hali tafauti za mwezi, hii ndio niliodai kuwa ni batili kwani lafdhi ya neno Ahillah (miezi miandamo) haliingizi; wala haikutegemea riwaya sahihi ikawa ni tafsiri ya Mtume(s.a.w.w)
, bali ni tafsiri iliosimuliwa na waongo kama walivyosema wanavyuoni wa wapokezi wa Hadithi.
Ama wanavyuoni, nimeshakujibuni kuwa hawana mamlaka ya kusahisha hadithi ya kutunga. Na tunachokitaka katika uwanja wa elimu na mijadala ya dini si fulani kanena, bali nini kimenenwa au fulani ana hoja gani? Ama Maelezo ya Sheikh Al-Khalili, ukizitoa sehemu mulizozikoroga zenye rangi nyekundu - inasema: Kauli yenye nguvu ni kuwa inafaa kutafsiri Qur-aan kwa kutumia rai (lakini) kwa yule aliyekusanya sharti ambazo lazima Mfasiri awe nazo. Sharti zenyewe tumeshazieleza katika darsa iliyopita. Wala Mfasiri huyo asitie (katika tafsiri yake hiyo) matamanio ya nafsi yake. Bali rai yake hiyo iwe ni faida itokanayo na madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni zenye kutegemewa katika fani hii ya tafsiri. (Sio kubuni tafsiri isiyoeleweka wala isiyokubalika katika misingi ya Dini) vile vile azingatie vizuri tokeo lililosababisha kuteremshwa Aya hiyo anayoifasiri, (lazima) aangalie "Sababun - Nuzuul"
Eleweni kwamba makusudio ya kufasiri Qur-ani kwa rai anakokupinga ni kufasiri bila ya kuwa na dalili za kilugha, kiusuli au Hadithi na nyenginezo ambazo zinatumika katika kuifasiri Qur-an: sio kufasiri kwa mujibu wa kanuni. Pili: asbabu nnuzuli hakuna azipingae, na waliozipinga wakasema kuwa hazina maana hakuna muhaqqiq aliyewaunga mkono. Lakini cha kufahamu ni kuwa Sheikh Al-Khalili hapa anahimiza ulazima wa kujua asbabu nnuzuli: si kutegemea Hadithi za kutunga kama hio mulioitegemea nyinyi. Yeye mwenyewe Sheikh katika darsa zake za tafsiri hunukuu baadhi ya riwaya za asbabu nnuzuli kisha akazipinga kwa sababu ya udhaifu. Kwa hivyo, si kila iitwayo sababu nnuzuli ndio ichukuliwe tu, bali ichukuliwayo ni ile iliojengeka katika riwaya sahihi.
MNASEMA
Katika maudhui hii, ndugu yetu Juma amechanganyikiwa kwa kuwa tabia yake anaona ni bora kupinga tu vyovyote iwavyo! Yeye anaona katika Aya hiyo neno 'Ahilla' halizungumzii hali tofauti za mwezi bali linazungumzia miandamo yenyewe - yaan i kama kwamba kusema: Omani itazame mwezi wake, Dubai itazame mwezi wake, Yemen itazame mwezi wake, Saudia itazame mwezi wake na kila nchi itazame mwezi wake. Angalia katika kitabu chake uk 56 - 57. Anasema hivi: (Kwa hivyo ni wazi kwamba kinachozungumziwa hapa ni miandamo yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za mwezi,) Kisha akasema: (lafdhi Ahilla (miezi miandamo), ni dalili ya kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja) Angalia uk 56 ndani ya kitabu chake.
JAWABU
Mumenukuu kipande kidogo sana. Ilikuwa munukuu yote nilioyasema au sehemu yenye kuleta maana kamili. Nimesema: Kwa ufupi ni kuwa neno Ahilla (miezi miandamo), kama alivyosema Sheikh, lina maana ya miezi mingi miandamo. Na hii ina uwezekano wa tafsiri mbili. Moja ni hio alioiita kuwa ni tafsiri ya watu wa Afrika Mashariki kwamba lafdhi Ahilla (miezi miandamo), ni dalili ya kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja.
Tafsiri hii inapata nguvu kwa mambo mawili: Moja ni kuwa sehemu yapili
: ya Aya imeifasiri sehemu ya kwanza na kubainisha muradi wake. Sehemu ya kwanza inasema: "Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo." Halafu ikaja sehemu ya pili ikatoa tafsiri kwa kusema: "Sema hivyo ni (vipimo vya) nyakati kwa ajili ya watu na hija." Kwa hivyo ni wazi kwamba kinachozungumziwa hapa ni miandamo yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za mwezi, kwani vipimo vya nyakati na hija ni miandamo yenyewe: si hali tafauti za mwezi: hali tafauti za mwezi za kuwa mkubwa na mdogo haziwezi kuwa vipimo vya nyakati na hija. Kwa hivyo, tafsiri hio ya watu wa Afrika Mashariki - nao wamekulia katika chemchemu za elimu - ni tafsiri yenye muelekeo madhubuti sana.
Hayo ndio maelezo niliotoa. Sasa nikuulizeni enyi Mashekhe wa msikiti wa Sunna. Ikiwa Aya inasema: "Sema hivyo ni (vipimo vya) nyakati kwa ajili ya watu na hija." Munataka mimi niseme vipi: nisema hali tafauti za mwezi?!
Halafu mukabutua tena maneno yangu, mukasema: "Kisha akasema: (lafdhi Ahilla (miezi miandamo), ni dalili ya kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja.)". Maneno ya nyuma mumeyawacha. Mwanzo wa maneno ni: "Na hii ina uwezekano wa tafsiri mbili. Moja ni hio alioiita kuwa ni tafsiri ya watu wa Afrika Mashariki kwamb a lafdhi Ahilla (miezi miandamo), ni dalili ya kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja. Tazama tafauti ya mantiki unayoipata katika maneno kamili na maneno butu mulioyanukuu nyinyi. Na hii ni kawaida yenu katika sehemu nyingi za kitabu chenu. Ni meeleza kwanini nimetumia neno "Uwezekano" rejeeni mutazame maelezo yangu. Sasa kilichobaki munithibitishie kuwa neno Ahillah halibebi maana ya miandamo mingi tafauti, na kama linabeba kipi kimeitoa maana hio katika Aya hio kutoka katika maana yake hio?
MNASEMA
Jambo jengine; ndugu Juma anaona kazi za mwezi na jua ni sawa sawa na kwamba kwa kuwa mwezi una 'Manazil' basi hivyo hivyo na jua lina 'Manazil'. Pia anaona kwamba kwa kuwa jua lina 'Matlai' basi na mwezi vile vile una Matlai. Angalia katika kitabu chake hicho (uk. 153 - 157).
JAWABU
Hili tumeshalizungumzia hatuhitaji kulikariri mara nyingi.
Munasema Jambo jengine ni kwamba ndugu Juma anaona katika tafsiri ya Aya hiyo"Wanakuuliza"
imetumika Hadiyth 'maudhui' yaani ya uongo katika hilo linalobainishwa kwenye sababu ya kushuka Aya hiyo [3 na kwamba waliouliza hawakuwa ni Maswahaba bali ni Mayahudi.
Sivyo nilivyosema: nilivyosema ni hivi: Na riwaya alioinukuu Al-qurtubiy mwenyewe kabla ya maneno hayo alioyaelezea Sheikh Bachoo, inaeleza kwamba hayo ni maneno ya Mayahudi, japokuwa Muadh ndiye muulizaji. Kwa hivyo, maneno yenu: "Na kwamba waliouliza hawakuwa ni Maswahaba bali ni Mayahudi" tafadhali yarekebisheni katika chapa ya pili au katika kunijibu tena. Hayo si maneno yangu bali ndivyo ilivyo riwaya alioitaja Al-Qurtubi. Ama kusema kuwa hii ni riwaya ya uwongo, kweli nimelisema na nalisema kwani nina ushahidi nanyi mumeshindwa kuupindua wala hamuna njia ya kuupindua.
Munasema Sisi tunamuelimisha hivi ndugu yetu huyu kwa kumwambia kwamba kwa upande wetu tunazithamini sana tafsiri za watu wenye elimu ambao hapana shaka, wao hiyo Hadiyth wameshaiona na wameitumia baada ya kuipima kwa viwango vya kielimu zao. Halafu hapa katika Aya, hapana mjadala wala utatanishi wowote unaohitaji maelezo makubwa ya sababu ya kushuka kwa Aya hiyo, kwani dhahiri ya Aya iko wazi mno kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Mwenyewe Anathibitisha kwamba:"Ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): (watu) wanakuuliza kuhusu (hali za) mwezi
JAWABU
Utatanishi haupo juu ya Mtume(s.a.w.w)
kuulizwa bali upo juu ya kilichoulizwa. Mimi sitaki mupige chenga hii na hile; nataka riwaya sahihi. Na nimekuelezeni kwamba wanavyuoni wote wanakubali kuwa katika tafsiri za Qur-ani kuna riwaya nyingi za kutunga hadi Al-Imamu Ahmad bin Hanbal akasema kuwa tafsiri haina hadithi sahihi. Na nimekunakilieni maneno ya Sheikh Abdul-Razzaq na nimekupeni sanad na wanavyosema wanavyuoni wa wapokezi. Kwa hivyo, tufate misingi au tufate riwaya dhaifu?! Sasa kama munazithamini juhudi za wanavyuoni je munaikubali Hadithi isemayo kwamba tufate kitabu cha Allah na Ahlu Al-Bayt, alioipokea mjuzi kuliko mimi nanyiny, naye ni Muslim. Na munaikubali Hadith Al-Tair alioipokea Al-Hakim kwamba Ali (k.w) ndio awe khalifa baada yake. Zote hizi ni juhudi za wanavyuoni. Au mutachagua kile munachokiona kuwa ni sahihi na kukiwacha kile munachokiona kuwa si sahihi? Ikiwa munathamini juhudi za wanachuoni kwa maana hio, basi nijuilisheni nikunakilieni riwaya zao musizozikubali. Ikiwa munathamini juhudi zao pamoja na kuchagua kilichosahihi, na hivi ndivyo inavyotakiwa, naomba munioneshe usahihi wa riwaya hio, Na natoa changa moto.
Ama kauli yenu: "Kwani dhahiri ya Aya iko wazi mno kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Mwenyewe Anathibitisha kwamba:"Ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): (watu) wanakuuliza kuhusu (hali za) mwezi." si kauli sahihi. Wapi Aya imetaja (hali za) mwezi"
?.
MNASEMA
Hebu tumuangalie mwanachuoni Al- Imam Abil-Hawaary Muhammad Binil - Hawaary Al-Omaniy Al-Ibadhy anayetajwa kama ni mwanachuoni wa karne ya tatu Hijriyah aliyeandika kitabu chake alichokiita: Katika kuitafsiri Aya hiyo ya Qur-aani: Aliandika ifuatavyo kwenye uk 99: Imeteremshwa Aya hii kwa Muadh bin Jabal na Tha'alabah bin Anama ambao ni katika Maansar. Walimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu miezi miandamo. Akasema Muadh: "Ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi w a aalihi wa sallam) wa Mwenyezi Mungu una nini huu mwezi mbona unakuwa (mwembamba) kama uzi kisha unazidi (wembamba huo) tena unajaa (unakuwa mnene) mpaka unakuwa sawa sawa baada ya hapo unapungua unakuwa kama ulivyoanza?" (Baada ya suala hilo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akamteremshia Mtume wake aya hiyo: {{Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo. Sema hiyo ni vielelezo vya nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu}} kama kutaka (kujua) nyakati za eda zao, swaum zao, Mikataba yao (na mambo mengine ) na Hijja - yaani kujua nyakati za Hija zao. Kwa hivyo miezi ni vielelezo vya nyakati kwa mambo hayo". Mwisho wa kunukuu.
JAWABU
Na mimi nakuongezeeni mwanavyuoni wengine wa Kiibadhi naye ni Qutbu Al-Aimma, Muhammad bin Yusuf Utfayyish, katika tafsiri yake Al-Taysir j. 1, uk. 277. Halafu baada ya hapo nipatieni ushahidi wa tafsiri hio katika riwaya sahihi. Nipo nasubiri riwaya.
MNASEMA
Sasa tuangalie Wanavyuoni wetu ambao ni wazaliwa wa Zanzibar wenye kutegemewa ambao wameandika tafsiri zao za Qur-aan tukufu:
1. Shaykh Abdalla Saleh Al-Farsy aliyeandika tafsiri ya Qur-aan Takatifu alikuwa na haya yafuatayo katika kuifasiri (yas-aluunaka), alitoa maelezo yafuatayo: "Maswahaba waliuliza nini sababu ya kukhitalifu sura ya mwezi - mara mdo go, mara mkubwa. Wakajibiwa kwa wepesi tu kuwa 'Ipate kuwa kipimo ili wapate watu kujua kuwa sasa wako katika mwanzo wa mwezi au kati yake au mwisho wake.'
2. Shaykh Said Muusa Muhammad Al-Kindy katika Tafsiri yake ya Qur-aan aliyoiita: "Asili ya uongofu" Katika kuifasiri Aya hiyo; Alikuwa na maelezo yafuatayo:-"Kaulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu namna ya mwezi kwamba ukiandama mwanzo wa mwezi unakuwa mdogo kisha baada ya siku unakuwa nusu, kisha mkubwa, kisha unapunguka urudi kuwa nusu, na mdogo, na kuwa kama uzi; Jee nini hekima yake?"
Waulizaji waliouliza ni Muadh bin Jabal na Thaalabah bin Ghanam. Wakazidi kumuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba: kwa nini unabadilika hivyo mwezi? Na kwa nini jua halibadiliki kama mwezi? Ndio ikateremka Aya hii:"Wanakuuliza juu miezi, sema: "Ewe Nabii Muhammad uwaambie kwamba: 'Hiyo' kuwa mwezi mara mdogo mara mkubwa: "Ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya mambo ya "watu." Yanayohusu mambo yao ya dunia na pia ya Dini. Kwa ajili wajue: madeni yao wanayodaiana, na kodi zao wanazolipana katika mambo mbali mbali, na hesabu zao na za kujua siku na mwezi na mwaka na nyakati."
"Na wajue eda ya hedhi za wake zao, na wajue siku za Swaum yao, na wajue siku za 'Hijja' zao na na Ameulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) sababu ya kubadilika mwezi mara kwa mara. Ndio akawajibu kwamba ingekua mwezi utabaki namna moja tu kama jua, haitajulikana hisabu ya mwezi." "Na muradi wa mwezi yaani ni "Takwimu" au kalenda ya kujua hisabu ya wakati za siku na nyakati za wiki na nyakati za miezi na nyakati za miaka, na mambo mengi ya watu ya maisha yao ya duniani kupeana kama : kodi za nyumba, au mashamba au mfanyakazi au au ...Na mengi mengineyo."
"Na kama mambo ya Dini ambayo tumekwisha kuyataja. Yote hayo ya dunia na ya Dini yamehusika na hesabu ya mwezi kubadilika kwake mara kuwa mdogo na mara kuwa mkubwa."
3. Al -Marhuum Shaykh Ali Muhsin Al-Barwani katika Tafsiri yake ya Qur-aan Tukufu ijulikanayo kwa jina la "Tarjama Ya Al-Muntakhab"katika kuifafanua Aya hiyo ameeleza yafuatayo:- "Na watu wanakuuliza habari za mwezi, unaanza mwezi mchanga kama uzi, kisha unakuwa mpaka unatimia kamili. Tena unapungua mpaka unakuwa kama ulivyoanza. Haukai katika hali moja kama jua. Nini maana ya kugeuka huku hata inakuwa kila siku 29 au 30 unakuja mwezi mpya?"
"Waambie huku kutokea hivi kuandama mwezi na kugeuka yapo ndani yake maslaha ya Dini na dunia pia. Hizi ni alama za kuonyesha nyakati za mambo ya maisha yenu. Zinaonyesha nyakati za Hijja, ambayo ni moja katika nguzo za Dini yenu. Na lau kuwa mwezi ungelibaki namna moja tu kama jua msingelitambua nyakati za maisha yenu na Hijja zenu. Wala huko kutojua hekima ya kugeuka mwezi kusikupelekeeni kutilia shaka hekima ya Muumba"
"Uislamu unahisabu mwezi unapoandama na kugeuka Sura kwa watu kupimia nyakati za ibada, na pia kwa mambo yao ya kidunia, kwa sababu hayo ni mambo ya kuonekana, na kwa hivyo tarehe inajulikana kwa sura ya mwezi. Mwezi kwa hakika ni kama kioo kinachoonyesha mwangaza wa jua huku duniani. Mwezi ukiwa kati baina ya jua na dunia hauonekani, na baadae mwezi mchanga unaandama na wakaazi wa dunia wanajua kuwa mwezi mpya umeanza. Ukifika mwezi katika upande unaokabiliana baina ya jua na dunia ndio unapokuwa wakati wa mbaamwezi, mwezi mpevu. Halafu unaendelea kupungua kama ulivyokuwa kwanza ukizidi kukua. Kwa hivyo tarehe inaanza tangu pale ulipokuwa mwezi mchanga. Pale unapoonekana mwezi mchanga kama uzi ndio mwezi umeandama, huonekana upande wa magharibi, hata kwa dakika chache baada ya kuchwa jua nao hupotea. Hivyo hivyo siku baada ya siku huhisabiwa mpaka zipite siku 29 au 30."
4. Shaykh Al-Amin bin 'Ally Al-Mazrui: "Katika tafsiri yake uk 67 ya Qur-aan Tukufu juu ya Aya isemayo: Alikuwa na haya ya kusema:"Wanakuuliza wewe habari ya miezi
!"
Kisha akaendelea kufafanua: "Baadhi ya Masahaba walimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) habari ya miezi - kwa nini huanzia mwembamba, ukaongezeka kidogo kidogo hata ukakamilika kengee yake, kisha ukaanza kupungua mpaka ukapotea kabisa kabisa? Kama suala hili lingejibiwa kisayansi ingewafungulia watu mlango wa kuuliza mengi ambayo hayahusiani na kazi ya Mitume. Kwani Mitume kazi yao ni kuwaongoza watu na kuwafunza yale ambayo hawawezi kuyajua ila kwa Wahyi. Ama mambo yawezayo kujulikana kwa ilimu, kama Falaki (astronomy), utabibu na kadhalika, si mambo ya kufaa kuulizwa Mitume, wala hayahusiani na kazi yao kamwe. Kwa sababu hii Allaah, badili ya kujibu suala lao, Ameeleza faida ya mwezi iliyofungamana na baadhi ya mambo ya manufaa, Shari'ah na mambo ya ibada. Hili lilitosha kuwafunza Masahaba lifaalo kumuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwakomesha wasiulize suala zisizofaa. Wakaambiwa kuwa mwezi huwajulisha watu nyakati za muamala wao na maslaha yao ya kilimwengu na nyakati za ibada zao kama Hijja, Swaum na kadhalika." Mwisho wa kunukuu.
JAWABU
Haya! Sasa nipatieni ushahidi wa usahihi wa tafsiri hio! Nakukumbusheni maneno yenu muliposema: "Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas bila ya k uonyesha dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu". Kwa ufupi mimi nilijibu hivi kuhusu riwaya hio: Nayo ni Hadithi dhaifu sana kama alivyosema Sh. Abdul-razzaaq Al-Mahadi, aliyeitia maelezo tafsiri ya Al-qurtubiy. Na pia kama alivyosema Al-alusi na wengineo. Nao ndio ukweli, kwani katika sanad yake kuna Al-Sudiy Al-Saghir, naye ni Moh'd bin Mar-wan. Anasema Jarir bin Abdi Al-hamid: "Mwongo." Anasema Al-duri kutoka kwa Ibn Main: "Si mwenye kuaminika." Anasema Salih bin Moh'd: "Alikuwa dhaifu na alikuwa akitunga (Hadithi)." Anasema Abu Hatim: "Hadithi zake zinaporomoka: Hadithi zake zinaachwa: Hadithi zake haziandikwi kamwe." Anasema Ibn Adey: "Udhaifu katika Hadithi zake uko bayana." Anasema Al-jawzjani: "Hadithi zake zinaporomoka." Anasema Ibn Hibban "Si halali kuandika Hadithi zake ila kwa ajili ya kufatilia (Sanad), na wala hafanywi kuwa ni hoja kwa hali yoyote." Anasema Al-tabari: "Hadithi zake hazifanywi kuwa ni hoja." Anasema Abdullahi bin Numair: "Al-suddiy alikuwa mwongo mkubwa."
Pia katika sanad ya Hadithi hio kuna Al-kalbi, naye ni Moh'd bin Saib bin Bishr. Anasema Mu'utamir bin Sulaiman kutoka kwa baba yake: "Al-kufa palikuwa na waongo wawili: mmoja wao ni Al-kalbi." Anasema Laith bin Abi Sulaim: "Al-kufa palikuwa na waongo wawili: mmoja wao ni Al-kalbi na wa pili ni Al-suddiy." Anasema Yahya bin Main: "Si lolote si chochote." Na akasema katika riwaya ya pili: "Dhaifu." Na Al-kalbiy kaipokea Hadithi hio kutoka kwa Abi Salih kutoka kwa Ibn Abbas. Anasema Al-suyutiy: "Abu Salih ni dhaif." Anasema Abdul-Razzaq Al-mahdiy katika maelezo yake juu ya tafsiri ya Al-baghawiy: "Abu Salih katika (riwaya zake alizozisimulia kutoka) kwa Ibn Abbas, si mwenye kuaminika.
Kwa hivyo, tafsiri hio ya Al-qurtubiy inayosema kwamba maana ya Al-ahilla (miezi miandamo) ni hali zake tafauti, si tafsiri ya kushangiriwa sana kwani imejengeka katika Hadithi maudhui (ya kutunga) au dhaifu sana. Hio ndio jawabu yangu kwa riwaya yenu. Nanyi hamukunijibu, mumenambia kuwa wanavyuoni wamesema. Nami nakubali kuwa wanavyuoni wamesema, lakiji je:
1) Wa dalili gani.
2) Je Wamekubaliana?
Nimkunakilieni maelezo ya Sheikh Abdul-Razzaq Al-Mahdi akisema kwamba riwaya hio: "Kaitaja Al-Wahidi katika Asbabu Al-Nuzul bila ya sanad. Na hii haina maana kabisa, kwani mbali na kuwa haina sanad, ni riwaya ya Al-Kalbi na jina lake ni Muhammad bin Al-Saib naye ni mwenye kuachwa mwenye kutuhumiwa (kwa uwongo). Na kwamba (ni Hadithi): "Dhaifu sanana sanad hii inaporomoka, Al-Suddiy ni mwenye kuachwa na Al-Kalbi ni mwenye kutuhumi wa (kwa uwongo).
Na Al-Alusi - naye ni katika watu wa tafsiri - anasema: "Ameipokea Ibn 'Asakir kwa sanad dhaifu..". Anasema Al-Sayyid Muhammad Rashid Ridha: "Hakika ya riwaya hii ya Ibn Abaas ni dhaifu, bali wamesema kwamba riwaya za Al-Kalbi kutoka kwa Abi Salih ndio njia dhaifu zao". Anasema Al-Tabatabai - mfasiri wa kishia - "Na ikapokewa kwamba baadhi yao walimuuliza Mtume(s.a.w.w)
kuhusu hali tafauti za mwezi, ikataremka Aya hio. Na hili ndilo tulilolitaja kabla kwamba ni kinyume na dhahir ya Aya hio basi halina mazingatio". Kwa hivyo, sitaki kurefusha, wanavyuoni wako pia ambao hawakukubaliana na riwaya hio kwa sababu ni ya uwongo. Kilichobaki ni kuwa mutuletee riwaya sahihi ili tukubaliane nanyi.