MUANDAMO WA MWEZI

MUANDAMO WA MWEZI 0%

MUANDAMO WA MWEZI Mwandishi:
Kundi: Midahalo na majadiliano kielimu

MUANDAMO WA MWEZI

Mwandishi: Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui, Al-Zenjibari.
Kundi:

Matembeleo: 61225
Pakua: 6144

Maelezo zaidi:

MUANDAMO WA MWEZI
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 23 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 61225 / Pakua: 6144
Kiwango Kiwango Kiwango
MUANDAMO WA MWEZI

MUANDAMO WA MWEZI

Mwandishi:
Swahili

8

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA KUMI

MASIMULIZI YA KURAIB

Kuhusu Hadithi hii mimi nilisema yafatayo:

"Kutoka kwa Kurayb (kasema) kwamba Ummu Al-fadhli bint Al-harith alimtuma Sham (Syria) kwa Muawiya. Akasema: 'Basi nikaenda Sham nikamkidhia haja yake.' Na ukaniindamia (mwezi wa) Ramadhani na mimi niko Sham. Basi nikauona mwezi usiku wa (kuamkia) ijumaa. Kisha nikaja Madina mwishoni mwa mwezi. Basi Abdullahi bin Abbas (r.a.) akaniuliza. Kisha akataja (habari za) mwezi muandamo akasema: 'Lini mumeuona mwezi muandamo?' Nikasema: 'Tumeuona usiku wa (kuamkia) Ijumaa.' Akasema: 'Wewe umeuona?' Nikasema: 'Ndio. Na Watu wameuona na wakafunga na Muawiya akafunga.' Akasema: 'Lakini hakika ya sisi tumeuona usiku wa (kuamkia) Juma Mosi, basi hatuachi kuendelea kufunga mpaka tutimize (siku) thalathini au tuuone.' Nikasema: 'Kwani wewe hutosheki na kuonekana na Muawiya na kufunga kwake?' Akasema: 'Laa' (Sio): Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w )."

SANAD YA HADITHI.

Tunatoa Sanad ya Muslim. Muslim kaipokea Hadithi hii kutoka kwa:

1) Yahya bin Yahya bin Bukayr. Naye ni mwalimu wa Al-bukhariy na Muslim na kasifiwa bila kifani. Kaitwa Imamu wa dunia wa zama zake, mkweli, muaminifu, mwenye elimu kubwa sana na mcha Mungu sana, wala hakuna aliyemjeruhi hata mmoja. Naye kaipokea kutoka kwa:

2) Ismail bin Ja'afar. Naye ni mkweli mwenye kuaminika, bila khilafu.

Naye kaipokea kutoka kwa:

3) Muhammad bin Abi Harmala, naye ni mwenye kuaminika wala hakuna aliyemjeruhi.

Naye kaipokea kutoka kwa:

4) Kuraib, naye ni Kuraib bin Abi Muslim, naye ni mwenye kuaminika bila khilafu.

Naye kaipokea kutoka kwa:

5) Ibn Abbas. Yeye hahitaji maelezo.

Kwa hivyo, Hadithi hii ni thabiti bila ya wasiwasi wowote. Na - natarijia - kwamba hakuna khilafu yoyote juu ya usahihi wake: khilafu iko juu ya maana yake.

FIQ-HI YA HADITHI.

Fiq-hi ya Hadithi hii, na ushahidi tunaopata ndani yake, ni kuwa Ibn Abbas (r.a), alipopewa habari kwamba mwezi umeonekana usiku wa (kuamkia) Ijumaa huko Sham (Syria) alikataa kuufata muandamo huo, na akasema "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) ." Tukafahamu kwa mujibu wa matamshi haya ya Hadithi kwamba Mtume(s.a.w.w) kafundisha kwamba kila mji kufata muandamo wake. Vyenginevyo hakuna maana ya Ibn Abbas kuukataa mwezi uliothibiti Sham, baada ya kuthibiti kwa habari iliotolewa na mtu muaminifu. Na Kuraib alipomuuliza Ibn Abbas "Kwani wewe hutosheki na kuonekana (huo mwezi) na Muawiya." Akajibu "Laa" (Sitosheki): hivi (ninavyofanya mimi) ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) . Kwa hivyo, amri ya Mtume (s.a.w.) ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali.

UPINZANI NA MAELEZO YA AL-IMAMU AL-SHAUKANIY

UPINZANI WA KWANZA

Anasema Al-imamu Al-shaukaniy - akipinga kutoa hoja kwa Hadithi hio ya Kuraib na Ibn Abbas - : "Na jua kwamba hoja iko katika Al-marfu'u katika riwaya ya Ibn Abbas si katika ijtihadi yake ambayo watu wameifahamu kutoka kwake. Na chenye kuashiriwa kwa kauli yake (Ibn Abbas aliposema): 'Hivi ndivyo Mtume alivyotuamrisha,' na kauli yake 'Hatuachi kufunga mpaka tukamilishe (siku) thalathini.' Na amri yenyewe kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) ni ile (Hadithi) walioipokea Mashekhe wawili (Al-bukhariy na Muslim) na wengineo (yenye kusema): 'Musifunge mpaka muuone mwezi muandamo wala musifunguwe mpaka muuone, ikiwa wingu litakuzibeni basi kamilisheni idadi ya (siku) thalathini." Mwisho wa kunukuu.

Natarajia kwamba maneno haya ya Al-shaukaniy hayako wazi kwa kila mtu, labda yanahitaji kushereheshwa na kuwekwa wazi kabla ya kujibiwa. Anachokisema Al-imamu Al-shaukaniy ni kuwa hoja imo katika Hadithi ya Ibn Abbas alioipokea kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) : wala haimo katika ijtihadi yake, na alichokipokea kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) , ni Hadithi inayosema: "Musifunge mpaka muuone mwezi wala musifungue mpaka muuone, ikiwa wingu litakuzibeni basi kamilisheni idadi ya (siku) thalathini." Na kwa hivyo, Ibn Abbas - katika Hadithi hio ya Kuraib tunayoijadili hapa - alipoukataa muandamo uliothibiti Sham na kusema "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) " amri yenyewe alioikusudia Ibn Abbas ndio Hadithi hio yenye kusema: "Musifunge mpaka muuone mwezi wala musifungue mpaka muuone, ikiwa wingu litakuzibeni basi kamilisheni idadi ya (siku) thalathini." Sasa kama ni hivyo, basi ukiitazama Hadithi hii, utakuta kwamba haiwahusu watu fulani pasi na wengine. Hivi ndivyo anavyosema Al-imamu Al-shaukaniy. Natarajia kwamba - kwa kusherehesha huku - maelezo yake yako wazi.

AL-IMAMU BADRU AL-DIN, AL-KHALILIY AJIBU

Lakini maelezo haya yakajibiwa na Sheikh Al-khaliliy kwamba, dai la Al-shaukaniy kwamba Ibn Abbas kuukataa muandamo wa Sham ilikuwa ni ijtihadi yake (Ibn Abbas) na kwamba aliposema (Ibn Abbas): "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) " amri yenyewe alioikusudia ni Hadithi inayosema: "Musifunge mpaka muuone mwezi." Anasema Sheikh Al-khaliliy: "Hio pia n i ijtihadi ya Al-shaukaniy mwenyewe katika kujaribu kubainisha alichokitegemea Ibn Abbas. Na ilivyo ni kuwa kauli ya Sahaba (ataposema kwamba) Mtume(s.a.w.w) alikuwa akituamrisha kadha na akitukataza kadha basi inapewa hukumu ya raf'ibali Jumhuri inasema kwamba kauli ya Sahaba: 'Tulikuwa tukiamrishwa kadha na tukikatazwa kadha inapewa hukumu ya raf'i." Mwisho wa kunukuu.

Anachokisema Sheikh Al-khaliliy katika kumjibu Sheikh Al-shaukaniy, ni kuwa Ibn Abbas katika Hadithi yake hio aliukataa muandamo wa Sham na kusema "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) ." Na maneno haya ya Ibn Abbas yalikuja baada ya kuulizwa na Kuraib: "Kwani wewe hutosheki na kuuona Muawiya?" Ndio Ibn Abbas akajibu hivyo. Kwa hivyo, ni wazi kwamba kutokutosheka na mwezi wa mbali ndio mafunzo ya Mtume(s.a.w.w) . Sasa kudai kwa Al-shaukaniy kwamba Ibn Abbas alitumia ijtihadi yake, ni kinyume na kanuni za Usulu Al-hadith (Elimu ya Hadithi). Kwani - kwa mujibu wa elimu hii - ni kuwa Sahaba anaposema kuwa "Mtume katuamrisha kadha au katukataza kadha," basi maneno haya yanapewa hukumu ya Hadithi yenye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) . Na hivi ndivyo walivyokubaliana wanavyuoni wote wa Hadithi. Tafauti ipo pale Sahaba anaposema: "Tulikuwa tukiamrishwa kadha," bila ya kumtaja Mtume(s.a.w.w) . Hapa Jumhuri inayapa maneno haya hukumu ya Hadithi inayotoka kwa Mtume(s.a.w.w) na wachache miongoni mwa wanavyuoni hawayapi hukumu hio. Sasa hapa Ibn Abbas kasema: "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) ." Kwa hivyo, kukataa kwake muandamo wa Sham ni hukumu ya Mtume(s.a.w.w) .

Ama kudai kwamba Ibn Abbas - kwa kusema kwamba Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) - alikusudia kuiashiria Hadithi inayosema: "Musifunge mpaka muuone mwezi," ni dai lisilo na ushahidi katika riwaya nyengine, wala halifahamiki katika Hadithi ya Ibn Abbas na Kuraib. Kwa hivyo, hio ni ijtihadi ya Al-shaukaniy, na kauli ya Ibn Abbas ndio mafunzo ya Mtume(s.a.w.w) . Huu ndio mukhtasari wa jawabu ya Al-imamu Badru Al-din Al-khaliliy kwa Al-imamu Al-shaukaniy.

UPINZANI WA PILI

Anaendelea Al-imamu Al-shaukaniy na upinzani wake kwa kusema: "Hata tukikubali (kwamba) muelekeo wa ishara katika maneno ya Ibn Abbas (inaonesha) katika kutokulazimika (kufata) kuonekana (kwa mwezi) wa watu wa mji (mmoja) kwa watu wa mji mwengine, basi ingekuwa kutokulazimika huko kumefungamanishwa na dalili ya kiakili, nayo ni kuwa pawe baina ya miji miwili hio umbali ambao kwawo (hupatikana) tafauti za matalai. Na Ibn Abbas kuacha kuutendea kazi uonekanaji (wa mwezi) wa watu wa Sham - pamoja na kutokuwepo (baina ya miji hio) umbali ambao kwao inaweza kupatikana tafauti (ya matalai) - kulifanyika kwa ijtihadi (yake tu) nayo si hoja." Mwisho wa kunukuu.

Anachokisema Al-imamu Al-shaukaniy ni kuwa hata tukikubali kwamba Ibn Abbas aliposema "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) " tukikubali kwamba Ibn Abbas kwa maneno haya kakusudia kwamba kila mji na muandamo wake, basi hilo haliwezi kuwa sahihi ila lifungamanishwe na hoja ya kiakili, na hoja ya kiakili yenyewe ni kuwa baina ya miji hiyo iliotokea miandamo tafauti basi pawe na umbali wa kutosha baina yake ambapo kwa sababu ya umbali huo, basi matalai (machomozo ya mwezi) yanaweza yakatafautiana baina ya miji hio. Sasa Sham (Syria) na Madina hakuna masafa hayo ambayo yanasababisha kutafautika kwa matalai baina ya miji hio. Kwa hivyo, ikabainika kwamba hili lilikuwa si jengine bali ni ijtihadi ya Ibn Abbas, na ijtihadi ya Sahaba si hoja katika hoja za kisharia.

Huo ndio upinzani wa pili wa Al-imamu Al-shaukaniy, lakini kama unavyoona jawabu yetu ya kwanza inajibu baadhi ya nukta zilizomo katika upinzani huu. Na hii ni kudai kwamba ile ilikuwa ni ijtihadi ya Ibn Abbas. Kwa kweli ilivyo ni kuwa hii ni ijtihadi ya Al-imamu Al-shaukaniy, na msingi ni kurudi katika elimu ya Hadithi, ndio itayohukumu Hadithi ni ipi na ijtihadi ni ipi. Na tumeona kwamba kauli ya Ibn Abbas inasema: "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume s.a.w." Tumesema sigha (form) hii ya Hadithi inaipa Hadithi hukumu ya kuzingatiwa kuwa ni Hadithi ya Mtume Mwenyewe(s.a.w.w) .

Ama kudai kwamba hata ikithibiti kwamba muelekeo wa kauli ya Ibn Abbas ni kuwa muandamo wa mji mmoja hautendewi kazi kwa watu wa mji mwengine, kwamba hata ikithibiti kuwa huo ndio muradi, ni lazima kuufungamanisha muradi huo na miji yenye tafauti ya matalai, si dai sahihi. Maneno haya ya Al-imamu Al-shaukaniy - kama yalivyo maneno ya watu wengi wa kawaida - chimbuko lake ni kuchanganya pale penye kujuzu ijtihadi na pale isipojuzu. Penye andiko huwa hakuna ijtihadi: ijtihadi mahala pake ni pasipo andiko. Sasa ukirudi kuitazama riwaya hio ya Ibn Abbas, utakuta kwamba kinachoelezwa ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali. Hivi ndivyo andiko linavyoonesha.

Sasa je umbali huu uwe kiasi gani, andiko halikubainisha. Kwa hivyo, "Muandamo wa mbali si hoja kwa walio mbali" ndio andiko ambalo lazima tusalim amri kwa hilo; na je "Umbali huu uwe kiasi gani," huu ndio uwanja wa ijtihadi. Sasa mas-ala ya ulazima wa kutokuuzingatia muandamo wa mji mmoja katika mji mwengine kwa kutafautika matalai, ambayo anayazungumzia Al-imamu Al-shaukaniy, ni mas-ala ya ijtihadi. Hakuna ulazima wa kuwa watu wazingatie ijtihadi hio, wanaweza wakashikana na ijtihadi hio na wanaweza kupitisha ijtihadi nyengine. Lakini kilicho lazima na ambacho tunatakiwa tukubaliane ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali.

Pili : ni dai la Al-imamu Al-shaukaniy kwamba Sham na Madina hakuna umbali ambao kwawo inawezekana kupatikana tafauti za matalai. Lakini akajibiwa na Sheikh Al-khaliliy kwamba masafa yaliopo baina ya Sham na Madina ni zaidi ya meli 500 na katika mikutano iliofanyika kwa ajili ya kulitafiti suala hili la muandamo wa mwezi, na ambayo ilihudhuriwa na wataalamu wa falaki, basi ramani zilichorwa na kubainishwa kwamba masafa ambayo inawezekana mwezi kuonekana sehemu moja na kutokuonekana sehemu ya pili, ni masafa ya meli 500 baina ya sehemu mbili hizo. Kwa hivyo, dai la Al-imamu Al-shaukaniy kwamba Madina na Sham hakuna umbali ambao kwawo inawezekana kupatikana tafauti za matalai, si dai sahihi, kwani baina ya miji miwili hio ni zaidi ya meli 500, na meli 500 zinatosha kusababisha tafauti ya matalai kama wataalamu wa falaki walivyosema.

UPINZANI WA TATU

"Lau tutakubali kutokuwepo ulazima wa kuifungamanisha (Hadithi hio ya Ibn Abbas) na akili, basi (mtu) mwenye elimu (yake) hatii shaka kwamba dalili (ushahidi) zinahukumu kwamba watu wa miji (tafauti) huwa wanazitendea kazi habari na ushahidi wake wanaopeana katika hukumu zote za Kisharia. Na kuonekana kwa (mwezi) ni miongoni mwake." Mwisho wa kunukuu.

JAWABU

ni kuwa hakuna upinzani kwamba watu wa nchi moja watendee kazi ushahidi unaotolewa na watu wa nchi nyengine, ikiwa yatakamilika masharti yake. Lakini tunakubaliana kwamba hio ni hukumu ya ujumla, na kwamba ujumla kinapopatikana kitu cha kuuhusisha basi chenye kuhusisha ndio kinachotangulizwa. Kwa hivyo, kanuni inasema kwamba Hadithi ya Ibn Abbas imeuhusisha ujumla wa kuutendea kazi kila ushahidi unaotolewa na watu wa nchi moja kuwapa nchi nyengine. Na natija ni kuwa ushahidi wote unaotolewa na watu wa nchi moja kuwapa watu wa nchi nyengine - ikiwa umekamilisha masharti yake - basi utendewe kazi isipokuwa ushahidi wa kuonekana mwezi. Kwani ushahidi huu umehusishwa na riwaya hio, na kanuni ni kuwa:

"Andiko la ujumla linakwenda katika ujumla wake mpaka lipatikane andiko lenye kuhusisha." Kwa hivyo, ujumla wa kuutendea kazi kila ushahidi au kila habari, umehusishwa katika ushahi di au habari ya kuandama kwa mwezi, kwani hii ni khaas (specific) na ile ni Aam (general).

Pili : - kama alivyojibu Sheikh Al-khaliliy - ni kuwa Ibn Abbas hakumwambia Kuraib kwamba nina wasi wasi na habari yako ulionipa, bali kamwambia: "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume s.a.w." Kwa hivyo, Ibn Abbas hakukataa kuutendea kazi ushahidi unaotolewa na watu wa mji mwengine, lakini kabainisha kwamba ushahidi huo haulihusu suala la kuandama kwa mwezi.

UPINZANI WA NNE

"Na ni sawa sawa, ikiwa baina ya miji miwili kuna umbali ambao kwawo kuna tafauti ya matalai au hakuna, basi kuhusisha (baadhi ya sehemu) haikubaliki ila kwa dalili (ushahidi)." Mwisho wa kunukuu. Jawabu ni kuwa ushahidi wenye kuhusisha sehemu moja pasi na nyengine ni Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbas, ambapo aliukataa muandamo wa Sham. Na akasema kwamba hivi ndivyo Mtume(s.a.w.w) alivyoamuru.

UPINZANI WA TANO

"Hata tukikubali kwamba Hadithi hii ya Kuraib inafaa kuihusisha (sehemu fulani pasi na nyengine), basi inatakiwa iishie katika sehemu ya andiko tu, ikiwa andiko linajulikana au katika kinachofahamika kutokana na hio (Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbas) ikiwa (andiko) halijulikani, kwa sababu ya kuja kwake (Hadithi hio ya Ibn Abbas na Kuraib) kinyume na Qiyas (Analogy)." Mwisho wa kunukuu. Anachokisema Sheikh Al-shaukaniy hapa, ni kuwa Hadithi hio ya Kuraib ni kinyume na Qiyas, na kitu ambacho kiko kinyume na Qiyas basi huwa kitu chengine hakipimwi juu ya kitu hicho, kama kanuni inavyosema: "Kila ambacho hukumu yake imethibiti kinyume na Qiyas basi kitu chengine ha kipimwi (hakilinganishwi na kupewa hukumu moja) na kitu hicho." Kwa ufafanuzi zaidi, ni kuwa maelezo ya Sheikh Al-shaukaniy ni kuwa Hadithi hio ya Kuraib na Ibn Abbas ni kinyume na Qiyas, kwa hivyo hata kama itafaa kuuhusisha ujumla uliomo katika Hadithi inayosema: "Fungeni kwa kuuona," basi uhusisho huo wa Hadithi hio ya Kuraib na Ibn Abbas uishie Madina na Sham, yaani itendewe kazi na watu wa Sham na watu wa Madina tu: si watu wa miji myengine kwani ni kinyume na Qiyas na kanuni - kama tulivyosema - ni kuwa: "Kila kilicho tafauti na Qiyas basi kitu chengine hakipimwi (hakilinganishwi na kupewa hukumu moja) na kitu hicho." Kwa hivyo, watu wa nchi nyengine hukumu hii haiwahusu!!!

Nasi tunajibu kwamba kanuni inayosema: "Kila kilicho tafauti na Qiyas basi kitu chengine hakipimwi (hakilinganishwi na kupewa hukumu moja) na kitu hicho" hapa si mahala pake, kwani Sham na Madina katika hukumu hio hazikutoka nje ya Sunanu Al-qiyas (njia za kufanya Qiyas). Na kwa hivyo, kuzikisia nchi nyengine kwa kuzipa hukumu sawa na hukumu hio ya Madina na Sham, ni Qiyas sahihi kabisa. Ama kusema kwamba kwa hukumu hio, Sham na Madina hazikutoka nje ya Sunanu Al-qiyas (njia za kufanya Qiyas), ni kutazama ukweli kwamba jua - kwa mfano - likitua Sham, watu wa Madina hawasali magharibi wala hawafuturu; jua likitenguka upende mmoja katika nchi mbili hizo, watu wa upande wa pili hawasali; alfajiri ikichomoza upande mmoja watu wa upande wa pili hawalazimiki kusali wala kuanza kufunga mpaka na kwao alfajiri ichomoze. Sasa vipi atasema Sheikh Al-shaukaniy kwamba hukumu ya kutozingatiwa muandamo wa Sham huko Madina ni kinyume na Qiyas (Analogy)? Bali hukumu hio imo katika Sunanu Al-qiyas (njia za kufanya Qiyas), na kwa hivyo kuikisia miji myengine kwa kuipa hukumu sawa na hukumu ya Madina na Sham ni Qiyas sahihi kabisa, kwani Miji Shina, nayo ni Sham na Madina, haikutoka katika Sunanu Al-qiyas (njia za kufanya Qiyas).

Ama njia ya kuiingiza miji myengine katika hukumu hio, ni kutazama kwamba illa (sababu) ziko za namna mbili kuu: Moja: ni "Sababu ilioelezwa kwa uwazi."

Pili : ni "Sababu ya kutolewa katika maandiko (yaani ambayo haikuelezwa kwa uwazi)." Sasa njia moja ya kujua "Sababu ya kutolewa katika maa ndiko (yaani ambayo haikuelezwa kwa uwazi), ni ile wanayoita: (Kupima na kugawa). Njia hio imeitwa hivyo kwa sababu mwenye kufanya Qiyas kwa kutumia njia hio, huwa anazikusanya sifa tafauti, kisha anatazama ipi inafaa kuwa illa (sa babu) ya hukumu. Njia hii pia huitwa (Kusafisha vyenye kufungamanishiwa). Vyenye kufungamanishiwa ndio illa (sababu) zenyewe.

Sasa njia ya illa (sababu) hapa ni njia hii ya (Kupima na kugawa). Nayo ni kutaza ma kwamba Ibn Abbas alipokataa kuufata muandamo wa Sham na kusema "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume s.a.w.," ni kuwa Mtume (s.a.w.) atakuwa kawaamrisha hivyo kwa illa (sababu) moja katika mbili: hakuna zaidi: Moja ni kuwa: iwe hivyo ndivyo walivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.) kutokuuchukua mwezi wa Sham, kwa sababu huko ni Sham. Kwa hivyo, Sham iwe ndio illa (sababu) ya kutokuuzingatia muandamo. Hii inamaanisha kwamba lau Kuraib alikuwa anatoka Misri au Pemba wangeukubali muandamo huo. Illa (sababu) hii ni dhaifu, haifai kuifanya kuwa ndio illa (sababu) ya hukumu hio ya Mtume (s.a.w.) iliomo katika Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbas. Kwani:

a) Ni (It is an intrasitive cause as opposed to a transitive one). Yaani ni sababu ambayo haivuuki mahala pake, nayo inapingwa na sababu nyengine yenye kuvuuka mahala pake.

b) Ni "Kulifanya jina kuwa ndio sababu." Na inavyotakiwa sifa iwe ndio sababu: sio jina. Naam! Jina linaweza wakati mwengine ku fanywa illa (sababu) ikiwa lina maana ya sifa. Katika jina "Sham" maana hii haipo. Pili ni kuwa: iwe Mtume(s.a.w.w) kawaamrisha hivyo kwa sababu Sham ni mbali. Illa (sababu) hii, ni sahihi na imekamilisha masharti ya utoaji wa illa (sababu).

Kwa hivyo, natija ni kuwa Mtume(s.a.w.w) kawaamrisha hivyo kwa sababu Sham ni mbali, sio kwa Sababu kule ni Sham. Baada ya haya tazama maelekezo katika jaduweli inayofata: Al-aslu ( Shina), ni mji wa Madina na mji wa Sham. Al-far'u (T awi) ni miji myengine ya dunia. Al-illah (sababu) ni kuwa mbali mbali. Al-hukmu (hukumu) ni wajibu wa kutokuzingatiwa muandamo wa mji mmoja katika mji wa pili. Kwa hivyo, tunasema kwamba hiki ni Qiyas sahihi, hakina vumbi, na kimetimiz a masharti yake yote. Na hii inabomowa dhana ya Sheikh Bachoo aliposema maneno yafuatayo:

"Kwa hapa: 1) Asili (shina) ni ijtihad ya Ibn Abbas.

2) Hukumu ya Asili: watu wa madina hawakuukubali mwezi ulioonekana Sham.

3) Illa: haipo.

4) Tawi linalozalika halipo." Mwisho wa kunukuu.

Hivyo ndivyo alivyosema, nalo ni jambo la kusikitisha, kwani - kwanza - hivyo alivyopanga Sheikh Nassor Bachoo vyote sivyo (ni wrong). Asili (shina) si ijtihadi ya Ibn Abbas, bali ni ile miji miwili (Madina na Sham) ambako muandamo wa upande mmoja haukuzingatiwa upande wa pili. Tena hii kuita ijtihadi ni kosa la kielimu, kwani Ibn Abbas kasema "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume(s.a.w.w) "Tumesema zaidi ya mara moja kwamba sigha (form au namna) hii ya maneno inaifanya Hadithi kuwa marfu'u (yaani kuwa ni Hadithi yenye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) mwenyewe kama fani zinavyoeleza). Al-illa (sababu): Sheikh Nassor Bachoo anasema: "Haipo." Natarajia ujuzi zaidi wa fani ya usuli unahitajika, kwani illa (sababu) ipo kama tulivyobainisha. Lakini labda Sheikh anadhania kuwa illa (sababu) zote ni "Sababu zinazoelezwa kwa uwazi." Bali Al-ilal (Sababu) - kwa mujibu wa usuli - zinakuwa hizo na zinakuwa: "Sababu z a kutolewa katika maandiko (yaani ambazo hazikuelezwa kwa uwazi)." Na njia zake za kuzijua ni nyingi, moja ni hio tulioitumia hapa nayo ni (Kuzikusanya sifa zinazoelekea kuwa illa (sababu) halafu kuzipima na kuchukua iliokuwa sahih i).

Kuhusu Al-far'u (Tawi), Sheikh anasema: "Tawi linalozalika halipo." Inaonesha Sheikh tawi kalitaja tu bila kulifahamu. Tawi ni nchi nyengine au miji myengine ukiitoa Madina na Sham ambayo ndio miji shina, yaani miji ya asili. Kuhusu Al-hukmu (Hukumu), Sheikh anasema: "Hukumu ya Asili: watu wa Madina hawakuukubali mwezi ulioonekana Sham." Nayo pia si maneno madhubuti, bali hukumu ya asili ni wajibu unaopatikana kutoka katika amri ya Mtume (s.a.w.) ya kuamrisha kutokuufata muandamo wa mbali. Tunakariri kwamba Ibn Abbas - baada ya kuukataa muandamo huo - kasema: "Hivi ndivyo alivyotuamrisha Mtume." Kwa hivyo, kuyaita maneno haya kuwa ni maneno ya watu wa Madina ni kinyume na Mustalahu Al-hadith (Elimu ya Hadithi).

UPINZANI WA SITA

Anasema Al-imamu Al-shaukaniy - akiendelea kutoa upinzani wake juu ya hoja ya kutokuzingatia muandamo wa mbali kwa kutegemea riwaya ya Ibn Abbas - :

"Hata tukikubali usahihi wa kufanya Qiyas, na kuuhushisha ujumla kwayo (kwa riwaya ya Ibn Abbas) basi kipeo chake ni kuwa iwe katika mwahala ambamo umbali baina yake, ni (sawa na umbali) wa Madina na Sham au zaidi." Mwisho wa kunukuu. Katika kitabu chake, Sheikh Bachoo kaongezea upinzani huo kwa kusema: "Jambo la kushangaza hapa, mbona hapatumiwi masafa kama haya? Tena hapafuatwi hata mwezi ulioonekana katika nchi jirani au iliyo na masafa punguzu ya haya. Je hoja hapa bado itakuwa ni kisa cha Kurayb na Ibn Abbas (r.a.)?

Huo ndio upinzani wa sita na wa mwisho, nao ndio upinzani dhaifu kuliko wote, kwani umejengeka katika "MAFHUMU AL-LLAQAB," nayo ni batili - taqriban - kwa makubaliano ya Umma mzima. "MAFHUMU AL-LLAQAB" - kama tulivyoeleza katika kitabu chetu "MEZANI YA HAKI - ni kama mtu kusema: "Muhammad ni Mjumbe wa Mungu." Mwengine akasema "Basi Mussa si Mjumbe wa Mungu!" Huyu wa pili kajenga hoja yake kwa kutumia "MAFHUMU AL-LLAQAB," nalo ni kosa kwani kusemwa kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allah, haimaanishi kwamba hakuna Wajumbe wengine. Sasa msingi huu ndio ambao hoja ya Al-shaukaniy imesimama juu yake: iliposemwa kwamba umbali wa Sham na Madina ndio illa (sababu) ya kuzingatia tafauti za miandamo, yeye akasema: "Basi kama katika miji hakuna umbali wa Sham na Madina miandamo tafauti isizingatiwe!"

Sasa tahariri ni kuwa, tumefahamu kwamba illa (sababu) ya kutokuuzingatia muandamo wa Sham, ni umbali: umbali ndio illa (sababu). Sasa je umbali huu uwe masafa gani? Hapa hakuna andiko, kwa hivyo hapa ndio mahala pa ijtihad: ama muandamo wa mbali kutozingatiwa mbali, hili limethibiti kwa Hadithi, kwa hivyo si suala la ijtihadi: ijtihadi iwe katika umbali gani. Hapa wanavyuoni watatoa rai zao, na sisi tutatazama iliokuwa munasib zaidi au iliokuwa na nguvu zaidi.

UPINZANI WA SH. NASSOR BACHOO KWA HADITHI YA KURAIB NA IBN ABBAS

UPINZANI WA KWANZA

Katika maelezo yake, Sheikh Nassor Bachoo aliifasiri na kuielezea Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbas kama ifuatavyo: "Kwanini Kurayb alimuuliza Ibnu Abbas (r.a.): "Je hutosheki na kuona (mwezi) kwa Muawiya na kufunga kwake?" Bila Shaka suali hili linaonesha kuwa lilikuwa ni jambo linaloeleweka kuwa: mwezi ukionekana pahala mbali - Waislamu wa sehemu nyengine watosheke na habari watakazopewa ikiwa zitakuja kwa njia ya kuaminika. Inaelekea kuwa hivyo, ndivyo walivyofahamu watu kama Kurayb ndio maana akamuuliza Ibnu Abbas ili apate uhakika." Mwisho wa kunukuu.

Kwa ufupi ni kuwa, huo alioutaja Sheikh Bachoo ni uwezekano (ihtimal), mmoja. Na inawezekana ikawa Kuraib aliuliza hivyo kwa sababu hakupata kuisikia Hadithi alioitolea Hoja Ibn Abbas. Kwa hivyo jambo hilo linawezekana kuwa hivi na linawezekana kuwa hivi, na kwa hivyo - kama kanuni inavyo sema: "Dalili ikiwa na maana nyingi basi ushahidi wake huporomoka." Kwa hivyo, uwezekano huo alioutoa Sheikh hauwashi wal a hauzimi katika suala hili. Na wala hili la kuisikia Hadithi baadhi ya Masahaba - wachilia mbali Kuraib ambaye ni mfuasi wa Sahaba - pasi na kuisikia wengine si jambo geni. Mifano ni mingi sana juu ya suala hili. Tosheka na ukweli kwamba Abu Bakr (r.a.) na Umar (r.a.) walikuwa wakitaka kutoa hukumu ya kitu nao hawakumbuki Hadithi juu ya suala hilo wanalotaka kulihukumu, basi kwanza huuliza kama yuko aliyehifadhi Hadithi juu ya jambo hilo. Akiwepo basi wanaitumia katika hukumu hio.

Pili : ni kama tulivyosema kwamba, huo alioutoa Sheikh Nassor Bachoo ni uwezekano, lakini Ibn Abbas amesema kwa mkato kwamba: "Hivi ndivyo Mtume s.a.w. alivyotuamrisha." Kwa hivyo, hakuna mazingatio kwa uwezekano huo mbele ya andiko.

UPINZANI WA PILI

Anaendelea Sheikh Nassor Bachoo kuichambua riwaya hio kwa kusema: "Naye Ibnu Abbas (r.a.) akamjibu (Kuraib) kuwa ametosheka, kwani namna hivyo - yaani kuamini habari za mbali juu ya suala la mwezi - ndivyo alivyoamrisha Mtume(s.a.w.w) ."!!!! Mwisho wa kunukuu.

JAWABU

ni kuwa: hii ni ajabu katika ajabu za dunia! Na huku ni kubadilisha maana ya Hadithi ambako wanavyuoni wakubwa wenye kujua lugha ya Kiarabu na fani za tafsiri hawakukusema. Ibn Hajar - alipokuwa akizungumzia mas-ala haya - kaiashiria Hadithi hio ya Kuraib kwa kusema: "Na katika Sahihu Muslim kiko chenye kutoa ushahidi huo (wa kwamba kila watu na muandamo wao). Kwa ufupi ni kuwa Hadithi inasema:

Wau ni wau al-atfi na asil i yake - herufi hio - ilikuwa ikae mwanzo, lakini ilipokuja Hamzat Al-istifham, (Hamza ya kuulizia), ilibidi hamza ikae mwanzo kwani herufi za kuulizia kwa kawaida hukaa mwanzo. Kwa hivyo tafsiri sahihi ya maneno haya ni:

"Wala hutosheki na Muawiya kuuona (mwezi) na kufunga kwake?" Ibn Abbas akajibu (sio). Watu wa Nahau wanajua kwamba jawabu namna hii ikitolewa huwa kuna kitu kimeondoshwa; na kilichotajwa kabla huwa ndio kinakifasiri kile kilichoondoshwa na kutotajwa, na kina kibainisha ni kitu gani hicho kilichoondoshwa. Yaani jumla (sentensi) huondoshwa kwa ulazima au kwa kujuzu ikiwa inafahamika katika Qarina (context). Kwa hivyo, makadirio ya jawabu ya Ibn Abbas ni sentensi ile ile alioitumia Kurai b kumuuliza Ibn Abbas kwayo, na kwa hivyo maana ni:

"Je hutosheki?"

JAWABU

(si) yaani "si-tosheki Sentensi (kutosheka) imeondoshwa na inabainishwa na ile ilio kabla yake, na ni lazima pakae kabla ya sentensi hio, herufi (si) ili maana iwe (si-tosheki)."

Neno "Si" hapa ndilo lililotajwa, na neno "Tosheki" ndilo lililoondoshwa katika jawabu ya Ibn Abbas. Baada ya makadirio ya neno hilo, maana inakuwa: "Si-tosheki."

Herufi "laa" hapa imefasirika hivyo kwa maana ya (si), kwa sababu ni herufi iliokuja baada ya jumla (sentensi) iliondoshwa, ambayo ni lazima iunganishwe na sentensi hio ilioondoshwa - na ambayo inafahamika katika qarina (context) - ili maana iwe sawa. Sasa ukitazama Qarina (context) hapa huwezi kuyafasiri maneno ya Ibn Abbas kwa tafsiri hio ya Sh. Bachoo, kwani Qarina (context) katika maneno yaliotangulia inaonesha kwamba Ibn Abbas alikataa kuufata muandamo wa Sham.

Na hii ni kwa sababu yeye Ibn Abbas alisema: "Hatuachi kufunga mpaka tukamilishe idadi ya siku thalathini au tuuone mwezi." Sasa kama aliukubali muandamo wa Sham, basi asingelisema maneno hayo, kwani kwa hali yoyote ile ikifika siku ya mwezi 29 ya muandamo wa Madina ni lazima watu wa Madina wale idi siku ya pili, ((halafu ikiwa itawathibitikia kwamba Sham mwezi uliandama tarehe thalathini wao watu wa Madina wailipe siku moja)) kwani siku hio ya mwezi 29 wa Madina ni lazima Sham itakuwa ni siku ya tarehe 30 au tarehe mosi. Ikiwa ni tarehe 30 itakuwa Sham wamefunga siku 30, wakati Madina wamefunga siku 29, na Ikiwa Sham ni tarehe mosi siku hio, basi watakuwa wamo ndani ya siku kuu - kwa hali zote mbili, kama Ibn Abbas aliukubali muandamo wa Sham, basi ni lazima watu wa Madina waishie kufunga tarehe 29.

Lakini tunamkuta Ibn Abbas anasema "Hatuachi kufunga mpaka tutimize (siku) thalathini au tuuone mwezi." Kusema "Mpaka tutimize (siku) thalathini" kunabomowa dhana hio ya Sheikh Bachoo, kwani maana ya maneno hayo ni kuwa mwezi wa Sham hakuukubali, kwani thalathini ya Madina ni thalathini na moja ya Sham - kwa mujibu wa miandamo miwili hio - na hakuna mwezi wa siku thalathini na moja kama Hadithi zilivyobainisha. Kwa hivyo, tafsiri hio ya Sheikh Nassor Bachoo haina msingi madhubuti.

Na sijui ni nani katika wanavyuoni wakubwa wenye fani za tafsiri na lugha ya Kiarabu aliyefasiri hivyo? Kama yupo basi jawabu yetu kwake ni hio. Hata Al-shaukaniy, ambaye ana rai kama hio ya Sheikh Bachoo, basi kubwa alilolisema ni kuwa hio ni ijtihadi ya Ibn Abbas, wala hakusema kwamba Ibn Abbas hapa kakubali kuufata muandamo wa Sham, bali maelezo yake yote ni jawabu yenye kuonesha kwamba Ibn Abbas hakuukubali mwezi wa Sham. Al-tirmidhiy naye alipoisimulia riwaya hio alisema: "Mlango wa tisa: kilichokuja kwamba kila mji una uoni wao (wa mwezi muandamo)." Kisha akasema: "Hadithi hii ni hasan sahihi gharib, na kinachotendewa kazi na watu wa elimu ni Hadithi hii, kwamba kila watu wa mji wana uoni wao."

Na Anasema Ibn Khuzaima: "Mlango wa dalili (ushahidi) kwamba kilichowajibu juu ya watu wa kila mji ni kufunga Ramadhani kwa uoni wao (wenyewe wa muandamo) si uoni wa wenzao." Na Al-nnawawi katika Sherehe yake kasema: "Mlango (kuhusu) ubainifu kwamba kila mji una muandamo wake na kwamba wao wakiuona mwezi muandamo katika mji, haithibiti hukumu yake kwa walio baada (yao) kutoka kwao.".

Hivi ndivyo wanavyuoni walivyoifahamu riwaya hio, tafauti ni katika kuifasiri tu, Al-shaukaniy akadai kuwa hio ni ijtihadi, nalo ni kosa kama tulivyobainisha.

UPINZANI WA TATU

Anaendelea Sheikh Bachoo na uchambuzi wake wa riwaya hio, anasema: "Pili kama ingalikuwa hakuna dhana ya kuwa mwezi ukionekana popote watu wafunge, Ibnu Abbas (r.a.) asingekuwa na haja ya kumuuuliza Kurayb juu ya habari za mwezi wa Sham kwa kusema: "Kisha (Ibn Abbas) akataja (habari) ya mwezi na akasema: "Ni lini mliuona mwezi?...akasema: "Wewe um euona?"

Hio ndio hoja nyengine ya Sheikh Bachoo, kwamba lau hakuna dhana ya kuwa mwezi ukionekana popote watu wafunge, basi Ibn Abbas asingekuwa na haja ya kumuuliza Kuraib "Lini mumeuona mwezi!!!" Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja, mulikuwa hamuwaulizi watu wanaotoka nchi nyengine masuala kama hayo wanapokuja kwenu na nyinyi muko kati kati ya mwezi pamoja na kwamba nyote zamani mukifata muandamo wenu? Sasa kama nyinyi mulikuwa mukiuliza suala hilo hilo kwanini Ibn Abbas na yeye asiulize hata kama dhana hio haipo? Mimi binafsi nina kawaida ya kuwauliza wageni walioko nchi hii ninayoishi suala hilo, na natarajia kwamba pia nimewasikia watu wengi wenye kuwauliza wageni suala hilo. Kwa hakika shubuhati kama hizi hazifai katika kujadili mambo ya kielimu. Kwa ufupi ni kuwa hata kama dhana hio ilikuwepo, dhana hio inabomolewa na kukataa kwake - Ibn Abbas - kuukubali mwezi wa Sham, na kujenga hoja kwa Hadith marfu'u kwamba hayo ndio mafunzo ya Mtume (s.a.w.) kwao.

Bali tunasema kwamba suala la Kuraib aliposema: "Je hutosheki kwa kuuona Muawiya na kufunga kwake" inawezekana ikawa na maana kinyume kabisa na fikra ya Sheikh Nassor, kwani inaweza ikawa ndio hasa inayomaanisha kwamba watu enzi hizo walikuwa hawazingatii muandamo wa mbali, au ikawa jambo hilo lilikuwa halijulikani kamwe, kwa sababu lau ingelikuwa Mtume(s.a.w.w) kafundisha kutendewa kazi muandamo wa mbali au ingelikuwa katika enzi hizo wanazingatia muandamo mmoja tu basi Kuraib asingelikuwa na haja ya kumuuliza Ibn Abbas suali hilo, bali angelimwambia: "Lipeni siku moja iliokupiteni ya muandamo wa Sham." Kwa hivyo, kumuuliza kwake suali hilo ni dalili ya wazi kwamba hakukuwa na dhana ilioenea kuwa mwezi ukionekana popote watu wafunge. Na kwa hivyo, Kuraib alikuwa hajui kamwe nini hukumu ya tokeo hilo.

UPINZANI WA NNE

Upinzani wa nne - ninafupisha - unaeleza kwamba riwaya ya Kuraib inasema kwamba yeye alikuja Madina mwishoni kwa mwezi. "Mwishoni kwa mwezi" inawezekana ikawa ni tarehe 26-27-28-29, au ikawa ni tarehe 30.

Sasa tuchukulie ni moja katika tarehe za mwanzo (26-27-28-29), hii ina maana kwamba mwezi ulikuwa bado unaendelea: bado haujakwisha. Kwa hivyo Ibn Abbas aliposema kwamba "Hatuachi kufunga mpaka tutimize siku thalathini au tuuone mwezi" ni sawa kwa sababu Mtume (s.a.w.) ndivyo alivyofundisha kwamba tusifunge mpaka tuuone mwezi na tusifungue mpaka tuuone mwezi, na mwezi Madina ulikuwa haujaonekana.

Hio ndio hoja yake - kwa kujaalia kwamba Kuraib karejea Madina tarehe 26 au 27 au 28 na 29. Lakini kama unavyoona kwamba upinzani huu unajibiwa na majibu tuliotoa katika sehemu zilizotangulia. Tumesema kwamba kipengele kinachosema: "Mpaka tutimize siku thalathini" kinabomowa hoja hii. Na hii ni kwa sababu kutimiza siku thalathini kwa watu wa Madina, ni kutimiza siku thalathini na moja kwa watu wa Sham. Na kwa vile hakuna mwezi wa siku thalathini na moja, basi Ibn Abbas alikuwa hana haja ya kutimiza siku thalathini huko Madina, kwani ikifika ishirini na tisa Madina, Sham hakika ni mwezi thalathini au ni mwezi mosi, lazima kwa hali yoyote watu wa Madina waishie kufunga siku ya tarehe ishirini na tisa kama Ibn Abbas aliukubali mwezi wa Sham. Lakini kusema kwamba "Mpaka tutimize siku thalathini" ni andiko la wazi juu ya maudhui hii kwamba muandamo wa Sham Ibn Abbas hakuukubali.

UPINZANI WA TANO

Upinzani wa tano na wa mwisho wa Sheikh Nassor Bachoo, ni kuwa tukijaalia kwamba Kuraib kafika Madina tarehe 30, basi Ibn Abbas alikuwa na sababu madhubuti ya kuukataa ushahidi wake kwani utakuwa ni ushahidi uliotolewa na mtu mmoja, na ushahidi wa mtu mmoja haukubaliki katika mwezi muandamo wa Shawaal (mfunguo mosi).

Hapa ukitazama upinzani wa Sheikh Nassor aliotangulia kuutoa huko nyuma, utaona kuna kitu mgongano baina ya maneno yake ya awali na maneno yake katika sehemu hii. Katika sehemu ziliotangulia upinzani wa Sheikh unasema kwamba Ibn Abbas aliukubali ushahidi uliotolewa na Kuraib, wakati hapa Sheikh anajenga hoja yake kwamba Ibn Abbas hakuukubali ushahidi uliotolewa na Kuraib!!!

Kwa ufupi ni kuwa - tukijaalia kuwa upinzani hapa ni huo basi - jawabu ni kuwa Ibn Abbas hakuukataa Muandamo wa mwezi wa Shawwal (mfunguo mosi): bali alioukataa ni mwezi muandamo wa Ramadhani uliothibiti huko Sham. Na mwezi muandamo wa Ramadhani hauhitaji mashahidi wawili, bali shahidi mmoja anatosha kama tulivyotangulia kueleza katika sura ya kwanza. Sasa cha kufanya - kama Ibn Abbas aliukubali mwezi huo - ilikuwa ikifika mwezi ishirini na tisa, basi lazima iwe ni siku yake ya mwisho ya kufunga, kwani Sham itakuwa hakika mwezi wa Ramadhani umekwisha siku hio, na kufunga siku ya Siku Kuu haijuzu. Badae watu wa Madina watatafuta habari, ikiwafikia kwamba Sham walifunga siku 30, basi watu wa Madina wailipe siku moja yao. Lakini tunamuona Ibn Abbas anatumia lugha yenye kuonesha kwamba hakuukubali muandamo wa Ramadhani (si wa M/mosi) uliothibiti Sham na akasema: "Hatuachi kufunga mpaka tutimize siku thalathini au tuuone mwezi."

Na vipi mtu aseme kwamba Kuraib tukijaalia kuwa kafika Madina mwezi 30, basi Ibn Abbas hakuukubali ushahidi wake kwa sababu ni ushahidi wa mtu mmoja na ushahidi wa mtu mmoja haukubaliki katika kuthibitisha muandamo wa mfunguo mosi? Vipi mtu aseme hivyo? Kwani Kuraib kauona wapi na kauona lini mwezi huo muandamo wa mfunguo mosi hata afike Madina mwezi 30 Ramadhani na kutoa habari ya muandamo huo? Je inaingia akilini kwa zama hizo kwamba Kuraib kaondoka Sham baada ya kuushuhudia mwezi muandamo wa mfunguo mosi kisha akafika Madina mwezi 30 Ramadhani wakati mapishano yao ya muandamo ni siku moja tu? Kwa hivyo, habari ya Kuraib ilikuwa ni ya muandamo wa Ramadhani kama Hadithi yenyewe inavyosema: "Ukaniandamia mwezi wa Ramadhani nami niko Sham." Na muandamo wa Ramadhani ni muandamo ambao unathibiti kwa mtu mmoja.

Pili : Ina maana gani kauli ya Ibn Abbas aliposema kwamba hatutaacha kufunga mpaka tuuone mwezi au tutimize siku thalathini, ikiwa Ibn Abbas kaendewa na Kuraib katika siku ya mwezi 30? Jawabu hii ya mwisho, inaufanya upinzani mzima wa Sheikh Bachoo kuwa hauna maana yoyote. Mwisho wa kunukuu nilioyaeleza kuhusu Hadithi hio ya Kuraib na Ibn Abbaas.