13
MUANDAMO WA MWEZI
SEHEMU YA KUMI NA TATU
MAANA YA JAMHURI KATIKA MATUMIZI YA KISHARI'AH
MNASEMA
13. Maana Ya Jamhuri Katika Matumizi Ya Kishari'ahKwanza
: ni vyema kuelewa kwamba mjadala huu wa mwezi katika hukumu ya kufunga na kufungua ni mkongwe wala haukuanza leo. Wala hii si fikra aliyoianzisha Shaykh Naaswir Bachuu kama walivyofahamu hayo baadhi ya watu kama akina ndugu Juma. Ukweli ni kuwa Shaykh Naaswir ni miongoni mwa Mashaykh wanaoendeleza harakati hizi za kufuata muandamo mmoja. Mtazamo huu wa kufunga kwa pamoja uliokuwepo tokea karne nyingi zilizopita umeshaelezwa katika kitabu cha "Kuandama kwa Mwezi" cha Shaykh Naaswir Bachuu uk 129 - 133. Wanavyuoni wakubwa kama Dr. Wahbah Zuhailiy, Shaykh 'Abdur-Rahmaan Al-Juzairy, Alqanuji, Sayyid Saabiq, Ibnu Taymiyah, Ibnu Quddama Almaqdisiy, Shaykh Muhammad 'Aliy Assaabuniy na wengine wengi ni miongoni mwa waliosema kuwa msimamo wa kufunga kwa muandamo mmoja ndio "Rai ya Jamhur."
JAWABU
Hakuna katika kitabu changu sehemu niliodai kuwa Sheikh Nassor Bachoo ndiye aliyeanzisha mjadala huu. Nilichokisema ni hiki: Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya. Mutakumbuka kwamba na jambo hili pia kalizungumzia Sheikh Nassor katika kitabu chake aliposema: Pamoja na kuwa mgogoro wa kuandama kwa mwezi umeanza kuonekana hadharani katika jamii za Waislam wa hapa Afrika ya Mashariki katika miaka ya hivi karibuni.
Ama dai kwamba msimamo wa kufunga kwa muandamo mmoja ni rai ya jumhuri, hatuwezi kukubaliana kwani ukweli unaonekana tafauti na hivyo. Kwa ufupi mimi nimelijibu suala hilo hivi: Wengi katika wale wenye msimamo wa kufunga kwa muandamo mmoja huwa wanapenda kudai kwamba rai yao hio ni rai ya Jumhuri (majority) ya Umma, nalo ni kosa kwani ikiwa wanakusudia Jumhuri ni idadi ya wanavyuoni wengi, basi rai ya kwamba kila watu na muandamo wao bila shaka itakuwa ndio yenye kufatwa na wanavyuoni wengi kwani ni rai ya Mashafi nao ndio walio wengi duniani katika madhehebu za Kisuni. Pia rai hii ni rai ya Mashia Imamiyya nao ni wa pili au wa tatu kwa wingi katika madhehebu za Kiislamu.
Ikiwa tunakusudia Jumhuri kwa idadi ya madhehebu, basi - katika madhehebu zilizoko leo duniani - rai ya kuwa kila watu wana muandamo wao ni rai ya Mashafi, Maibadhi, Mashia Imamiyya, pia - kutokana na aliyoyanukuu Al-shaukaniy kutoka kwa Al-imamu Yahya na Al-hadawiyya miongoni mwa Zaidiyya, inaonesha kwamba hii ndio kauli ya madhehebu hio ya Shia-Zaidiyya. Na ndio msimamo wa sasa wa Madhehebu ya Kiwahabi huko Saudia, na ndio kauli sahihi kwa Mahanafi kwa mujibu wa alivyosema Al-sayyid Saabiq kama tutavyonukuu baadae Inshaa Allah..
Pili
: ni kuwa kauli ya kufunga kwa muandamo mmoja imenasibishwa kwa Al-imamu Malik. Lakini riwaya hio ya Al-imamu Malik imesimuliwa na watu wa Iraq, ama kule Madina alipokuwepo mwenyewe Al-imamu Malik, watu wa Madina wamesimulia kutoka kwake akisema: "Funga haiwalazimu kwa habari isipokuwa watu wa mji (ule ule) ambao (mwezi) umeonekana."
Tatu
: ni kuwa: madhehebu zote ambazo zinajulikana kuwa ndizo zenye msimamo wa kufunga kwa muandamo mmoja zina wanavyuoni si kidogo ambao hawakuiafiki rai hii. Kama Al-kaasaniy, naye ni Hanafi. Na akawanukuu Abu Muslim wanachuoni wengine wa Kihanafi wenye kauli hii. Anasema: "Na alichokichaguwa mwenye kitabu cha "AL-TTAJRID" na wengineo katika Mashekhe wa Mahanafi, ni kuzingatia tafauti za Matalai. Amesema Al-zayla'i naye ni miongoni mwao (Mahanafi): 'Nayo (kauli hio) ndio yenye kuelekea zaidi.' Na amesema Ibn Al-hammam miongoni mwao (Mahanafi) na kushikana na dhahiri ya masimulizi (ya Hadithi ya Kuraib) ni (jambo) lenye hadhari zaidi..na hakuna shaka kwamba hii ni bora kwani ni nassu (andiko la wazi) na ile (Hadithi inayosema: 'Fungeni kwa kuuona') ina uwezekano wa kuwa makusudio ni kuwaamuru watu wa kila matalai kuwa na uoni wao wa mwezi muandamo." Mwisho wa nakala kutoka katika kitabu cha Al-imamu Abu Muslim.
Anasema Al-sayyid Saabiq: "Na akasema Ikrima na Salim na Is-haq na ndio (kauli) sahihi kwa Mahanafi..kwamba watu wa kila mji wanazingatia muandamo wao wala hauwalazimu muandamo wa wenzao." Mwisho wa kunukuu. Ninasema: bila shaka watakuepo wengine wengi ambao vitabu v yao hatujavisoma au hatujaviona kamwe.
Pia ukitazama maneno ya Ibn Rushd Al-qurtubiy - naye ni mwanachuoni wa Kimaliki - utaona hakutoa msimamo wake kwa uwazi, lakini maneno yake yanaonesha kwamba anaelemea katika kauli kwamba kila watu wana muandamo wao. Anasema - baada ya kuinukuu Hadithi ya Kuraib na kutoa maelezo -: "Dhahiri ya Riwaya hii inamaanisha kwamba kila mji una uoni wao (wa mwezi muandamo) ukiwa mbali au karibu. Na Qiyas kinatoa tafauti baina ya miji ya mbali na miji ya karibu."
Mwisho wa kunukuu.
Na Ibn Al-arabiy - naye ni miongoni mwa wanavyuoni wakubwa wa Kimaliki - anasema: "Na wakatafautiana katika kuifasiri kauli hii ya Ibn Abbas (yaani Hadithi ya Kuraib). Ikasemwa: '(Ibn Abbas) Kaikataa (habari hio aliopewa na Kuraib) kwa kuwa ni ya mtu mmoja. Na ikasemwa kwa kuwa miji (miwili hio ya Madina na Sham) matalai yake yametafautiana, nayo ndio (kauli) sahihi..na mfano wake ni lau uliandama usiku wa Ijumaa huko Aghmat (Morocco) na ukaandama huko Ishbiliyya (Mji wa Spain) usiku wa J/mosi, ba si inakuwa kila mji una muandamo wake."
Na mfano wa kauli hii ya kuzingatia tafauti za miandamo kwa kutafautika miji kwa umbali au kwa kutafautika matalai, ndio kauli ya Ibn Majishun na Al-mughira miongoni mwa wanavyuoni wa Kimalik. Anasaema Ibn Rushd Al-qurtubiy: "Na wakakubaliana kwamba hilo halizingatiwi katika miji ilio mbali mbali kama Al-andalus (Spain) na Hijaz (Saudia)." Na kauli hii kaisema pia Ibn Abdil-Barri katika wanavyuoni wa Kimalik. Changanya na ukweli kwamba Al-imamu Malik mwenyewe kuna riwaya mbili juu ya kauli gani aliitegemea, na riwaya ya kwamba kila watu na muandamo wao ndiyo yenye kuelekea zaidi kutoka kwake kwani ndio riwaya iliosimuliwa na watu wa Madina ambako Al-imamu Malik mwenyewe alikuwa akiishi.
Nne ni kuwa: kama tulivyotangulia kusema kwamba mas-ala ya kufunga kwa muandamo mmoja yamo katika vitabu tu: si katika matendo: kimatendo ni Waislamu wachache sana duniani wanaofata rai hio. Kwa mfano nchi za India na Pakistan na Bangladesh - ambazo zina Mahanafi wengi - ukiwauliza wakazi wa nchi hizo wenye kuishi Ghuba: "Kwenu mwezi umeandama lini?" Watakwambia siku tafauti na muandamo wa nchi nyengine ambazo labda zimetangulia. Na nchi hizo zote zina Maulamaa.
Tano
: ni kuwa: kauli ya kuwa kila mji na muandamo wake imesimuliwa kutoka kwa Maimamu wengine wakubwa - ukitoa Maimamu wanne - kama Ikrima miongoni mwa Wafuasi wa Masahaba, na Moh'd bin Al-qasim na Salim na Is-haq bin Rahawaih na Al-tirmidhiy akainasibisha na watu wa elimu (Maulamaa). Kwa hivyo, tunasema kwamba kusema kwamba kauli ya muandamo mmoja ni kauli ya Jumhuri ya Umma, ni jambo la kufikiriwa. Kwa hali yoyote ile, mimi sisemi kwamba kilichosawa ni kinachosemwa na Jumhuri,( laa): sisemi hivyo, bali ninachosema ni kuwa kilicho sahihi ni chenye ushahidi madhubuti uliojengeka juu ya misingi ya kielimu, lakini naona watu hapa wamekuwa wakipiga kampeni kwa kutumia jina Jumhuri nayo si sahihi. Na mas-ala kama haya yako mengi: utasikia hii ndio kauli ya Jumhuri, mara ukisoma kitabu chengine utakuta kauli kinyume na hio kwamba ndio kauli ya Jumhuri!!! Cha kustaajabisha zaidi ni kuwa wakati mwengine utakuta kitu chenye tafauti mashuhuri, basi atatokea mtu anayetaka kuipamba rai yake, anasema: "Umma umekubaliana juu ya jambo hili!" Mwisho wa kunukuu nilioyasema kitabuni.
Bila kusahau kwamba hata leo hii, Jumhur ya Waislamu duniani hawafati miandamo ya nchi nyengine. Kwa hivyo, hiki ni kitu tunakishuhudia hatuhitaji andiko. Lakini - kama nilivyosema - ikiwa Jumhur inasema tufunge kwa muandamo mmoja au inasema kama tunavyosema sisi, yote mawili si hoja katika uwaja wa Sharia, bali hoja ni je wana dalili gani, na wapinzani wao wana dalili gani. Chukua - kwa mfano - walio wengi katika Sunni, wanasema tufunge mikono chini ya kitovu, tukichukulia kwamba Sunni wengi ni Hanafi. Au wanasema tufunge juu ya kitovu, tukichukulia kwamba Sunni wengi ni Shafi. Wakati Salafia wana hoja ambazo ndio sahihi kwao kwamba mikoni inafungwa juu ya kifua. Sitaki kusema kipi ni sahihi, nataka kusema kwamba wingi si hoja ya Kisharia. Bali leo, ukitazama katika madhehebu za Sunni utakuta kwamba Salafiyya ndio wachache. Sasa tuseme ndio dalili zao zitakuwa hazifai? Bila shaka kitachotazamwa ni dalili: si wingi na uchache.
MNASEMA
Msimamo huu kwa kweli umejengeka katika misingi imara uliopokewa moja kwa moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema: (Fungeni kwa kuona mwezi - muandamo..)
JAWABU
Tumeshabainisha sana kwamba (Fungeni kwa kuona mwezi - muandamo..) ni Hadithi na "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w)
" pia ni Hadithi. Na huwezi kuyakataa mafunzo ya Mtume(s.a.w.w)
, bali unaweza kuyatafutia maana sahihi
MNASEMA
Wanavyuoni wa Shari'ah wameieleza "Jamhur" kwa maana ya kukubaliana jambo "Maimamu wanne wa Kisunni" na hata kama ikitokea kujitoa Imamu mmoja katika hao wanne kwenye jambo fulani bado jambo hilo litachukuliwa ni la msimamo wa "Jamhur" midam watatu kati yao wana msimamo mmoja.
Ama tukichunguza katika kitabu cha ndugu Juma tunakuta ameeleza maana ya Jamhur kinyume na hivyo. Ameieleza "Jamhur" katika mtindo usioelezwa katika vitabu vya Shari'ah. Miongoni mwa udhaifu alioutaja ndugu Juma katika kueleza maana ya "Jamhur" ni vile alivyoeleza kuwa (tunasema kwamba kusema kwamba kauli ya muandamo mmoja ni kauli ya Jumhuri ya Umma, ni jambo la kufikiriwa.). Sisi tunasema kwamba kitu cha kwanza cha kufikiriwa ni hii tafsiri ya ndugu Juma katika maana ya neno "Jamhur." Tunamuomba nd ugu Juma asijifanye kama yule kipofu aliyeingia kwenye nyumba ya mtu na kujigonga kwa vitu vilivyokuwemo ndani, kisha akawalaumu sana wenye nyumba. Sasa inafaa kujiuliza ni nani wa kulaumiwa baina ya kipofu na mwenye nyumba? Bila shaka wa kulaumiwa ni yule bwana kipofu kwani vitu vilikwishapangwa akamtupia lawama mwenye nyumba. Kwa hivyo nasi tunamtanabahisha vizuri na mwenye nyumba lakini kwa sababu ya kutokuona kwake ndio ndugu Juma kuwa Wanavyuoni wenye kuaminika wamekwishakuieleza maana halisi ya "Jamhur" katika matumizi ya Shari'ah ingawa yeye kwa makusudi akajitia upofu na kuanza kusema: (naona watu hapa wamekuwa wakipiga kampeni kwa kutumia jina Jumhuri nayo si sahihi.) Kisha akaendelea kusema: (basi atatokea mtu anayetaka kuipamba rai yake, anase ma: "Umma umekubaliana juu ya jambo hili!")[5]
Kama kweli ndugu Juma ni msomi ingekuwa jambo la busara atoe majina ya vitabu vya Wanavyuoni wenye kukubalika waliosema kuwa rai ya kufuata muandamo mmoja sio rai ya Jamhur. Pili tunamuuliza ndugu Juma ni rai ipi aliyoikuta yeye ambayo imetajwa kuwa ni rai ya Jamhur kisha isiwe ni rai ya Jamhur? Ilikuwa ni wajibu wake kama anataka kuikosoa atoe ushahidi wa maandiko na madondoo ili uwe ushahidi. Kwani tunavyojua sisi ni kuwa kila rai iliyotajwa kuwa ni ya Jamhur panakuwa na maandiko yenye kukubalisha jambo hilo , hata kama ipo khitilafu ya baadhi ya Wanazuoni.
Tunamnasihi ndugu yetu Juma kuwa anapojaribu kuelezea mas-ala yoyote ya kielimu, basi ni vyema apite katika njia zake zenye kukubalika kitaalamu wala asidhani kuwa anaweza kufaulu bila ya kupita katika njia hizo. Ni vyema aelewe kwamba asipopita katika njia hizo atapotea. Mshairi mmoja wa kiarabu anasema hivi: "Unatarajia kuokoka (kufaulu) bil a ya kupita katika njia zake (Elewa kwamba) jahazi haiwezi kwenda kwenye nchi kavu." Mshairi mwengine anasema: "Ukiliendea jambo (ukitaka kulifanya jambo) bila ya kupita katika njia zake utapotea (na kuwapoteza wenzako). Na ukiliingia jambo katika njia zake utaongoka (na utaongoza wenzako)."
JAWABU
Ni wanavyuoni wa Sharia gani hio waliosema kuwa Jumhur ni kukubaliana jambo kwa "Maimamu wanne wa Kisunni"?! Yaani mulivyowafahamu nyinyi hao wanavyuoni ni kuwa hawa Waislamu wote tokea Masahaba kauli zao ni mataka tu: Maimamu wane ndio wanye haki ya kuzungumzia dini?!!!
Jumhur linatumika kwa maana tafauti. Inatumika Jumhur ya Umma, na hii ndio Jumhur yenye nguvu. Yaani kitu kilichokubaliwa na waliowengi katika Umma, kuanzia Masahaba hadi Maimamu wa madhehebu zote na hadi leo. Pia linatumika kumaanisha Jumhur ya Kisunni, hii ndio hio mulioitaja nyinyi. Na kuna jumhur ya Mashafi, ya Kiibadhi, ya Kishia n.k, yaani walio wengi katika wanavyuoni wa madhehebu hizo. Kwa hivyo, Jumhur halitumiki kwa maana moja. Ndio maana ukisoma vitabu tafauti vya kifi-qhi utaona ibara kama "Jumhuru ya wanachuoni wa madhehebu fulani au wa fani fulani". Na utakuta Jumhur ya Ummah. Na unaweza kukuta kwamba hii ni kauli ya Jumhur; hapa itabidi umfahamu muandishi je anakusudia Jumhur gani.
Anasema Dr. Al-Zuhaili: "Wamekubaliana Jumhur ya watu wa adab (literature)." Na anasema: "Na wakapinga Jumhur ya Mashafi na Mahanafi". Na akasema: "Wakasema Jumhur ya watu wa Usuli". Anasema Al-Imamu Al-Jitali: "Na hio ni kwa sababu kwa (mtazamo wa) Jumhuri ya watu wa elimu". Na anasema: "..Kwa Mashekhe wetu na Jumhur ya Ummah". Anasema Bakli 'Abdil-Rahman: "Na wakasema jumhur ya Maulamaa wetu (wa Kiibadhi)". Anasema Sheikh Al-Khalili: "Na Jumhur ya Umma wakatoa ushahidii". Haya yako katika kila kitabu unachokisoma taqriban utayakuta, wala mtu mwenye elimu yake hayaulizi.
Ama kama Jumhur ni makubaliano ya Maimamu wane wa Kisuni, basi jumhur haitokuwa hoja kamwe, kwani Maimamu wane wametanguliwa na vigogo wengi katika Masahaba na wafuasi wao na Maimamu wakubwa waliokuwa mabingwa sana. Na wote hawa walikuwa na fikra tafauti na za Maimamu wane: yaani mwengine hukubaliana na mwengine hutafautiana. Wametangulia kabla yao akina Jabir bin Zaid na wanafunzi wake; Al-Hasan Al-Basari na wanafunzi wake; Al-Awzai na madhebu yake; Mafaqihi wa Madina; wa Iraq; wa Sham kwa maelfu. Kwa hivyo, kama jumhur:
1) Ni kauli ya Maimamu wane wa Kisuni, itakuwa haina nguvu kwani Umma uliowatangulia ni mkubwa na ulikuwa na vigogo ambao walisifika kushinda wote waliokuja baada yao.
2) Kama ni idadi ya madhehebu, basi madhehebu zenye kufunga kwa miandamo yao leo na zamani ni watu wa madhehebu zote taqriban. Miji ya Pakistan, Bagladesh na India yenye Mahanafi wengi wanafata miandamo yao. Misri ambako Mashafi - nadhani - ndio wengi wanafata muandamo wao. Nchi za Afrika Magharibi zenye Malik wengi pamoja na nchi za Afrika Kaskazini za Kiarabu zenye Malik wengi, zinafata miandamo yao. Nchi za Ghuba, Iraki, Sham na Al-Yaman, Mashariki ya mbali wote hawa wanafata miandamo yao, na waliowengi katika nchi hizo ni Masunni wa madhehebu nne. Kwa hivyo, bado naendelea kusema kwamba kudai kuwa kauli ya muandamo mmoja ni kauli ya Jumhuri ya Umma, ni jambo la kufikiriwa.
MNAEMA
Tukiendelea kumfahamisha ndugu Juma juu ya kauli zake alizoziandika kwenye kitabu chake ambazo sio za kielimu ni kule kusema kwake kwamba: (kama tulivyotangulia kusema kwamba mas-ala ya kufunga kwa muandamo mmoja yamo katika vitabu tu: si katika matendo: kimatendo ni Waislamu wachache sana duniani wanaofata rai hio.) Tunamfahamisha ndugu Juma kwamba kitu cha msingi kinachofaa kuzingatia katika mas-ala yoyote yale ya Dini ni ule usahihi wake, sio kuangalia wingi au uchache wa wafuasi. Mfano mzuri ni haya madhehebu ya Ibadhi yenye wafuasi wachache mno duniani ukilinganisha na madhehebu mengine kama Hanafi na mengineyo. Je kwa sababu ya uchache wao ndio unataka kusema Ibadhi hawako katika haki?
Kwa hiyo uchache wa wafuasi sio kipimo cha haki au batil. Ni vyema ndugu Juma awe makini katika uandishi hususan katika jambo la kujenga hoja, asikubali kutawaliwa na taasub za aina hizo.
JAWABU
Hapa nakubaliana na nyinyi 100%. Na hilo nilikwisha kulisema katika kitabu na humu kabla yakufika hapa pia nimelisema. Kitabuni nilisema: Kwa hali yoyote ile, mimi sisemi kwamba kilichosawa ni kinachosemwa na Jumhuri,( laa): sisemi hivyo, bali ninachosema ni kuwa kilicho sahihi ni chenye ushahidi madhubuti uliojengeka juu ya misingi ya kielimu. Na humu katika jawabu hii, nimekwambieni hivyo kwamba je uchache wa Salafia unawafanya kuwa hawako sahihi?! Na nyinyi mukaniambia je uchache wa Maibadhi unawafanya kuwa hawako sahihi. Kwa hivyo, nukta hii tumekubaliana. Lakini tumetafautiana katika tafsiri ya neno Jumhur.
Ama kauli yenu: "Pili tunamuuliza ndugu Juma ni rai ipi aliyoikuta yeye ambayo imetajwa kuwa ni rai ya Jamhur kisha isiwe ni rai ya Jamhur?" inaonesha hamutaki kusoma: munataka kukosoa tu. Mara ngapi utakuta vitabuni kuwa hii ndio rai ya Jumhur kisha ukisoma kitabu cha pili utakuta rai kinyume kwamba ndio rai ya Jumhur. Kwa mfano, mas-ala ya kuziletea ta-awil Aya za Sifat. Al-Asha'ira wanadai kuwa huo ndio mwenendo wa Al-Salaf (Masahaba, wafuasi wao na Maimamu wakubwa wakiwemo wane); wakati Salafiyya wanadai kutokuziletea ta-awil Aya hizo ndio mwenendo wa Al-Salaf na Maimamu. Na wote wana ushahidi wao wakimaandiko. Bali utakuta kwamba Umma umekubaliana juu ya hili wakati ni kitu chenye khilafu. Kwa mfano, utakuta mara nyingi kwamba "Umma umekubaliana kuwa Hadithi za Al-Bukhari na Muslim zote ni sahihi". Halafu tunakuta Maulamaa wengi, kama Ibn Taymiyya, Ibn Al-Qayyim, Al-Albanni, Al-Qannubi, Ibn Al-Jawzi na mamia ya Maimamu wa Kisuni, wanazidhoofisha baadhi ya Hadithi hizo. Sasa hayo makubaliano ya Umma yako wapi? Kwa hivyo, ndugu zanguni, kwa ujumla vitabu vya binaadamu vyote vina makosa. Haitoshi mtu kutoa hoja kuwa kuwa fulani kasema; ni lazima utafute ukweli wenyewe ukoje.
MNASEMA
Mukhtasari Wa Nukta Muhimu (1) Msimamo wa kufunga na kufungua kwa muandamo mmoja duniani ndio rai ya Jamhur. Wala si rai itokayo kwa Shaykh Naaswir Bachuu. Ndugu Juma hakuwa makini katika kukisoma kitabu alichokiandika Shaykh Naaswir Bachuu: "Kuandama Kwa Mwezi" uk 162 - 163. Wafuatao ni baadhi ya Mashaykh wa Afrika Mashariki waliowahi kubainisha jambo hilo :-
JAWABU
Si kweli huu si msimamo wa Jumhur ya wanavyuoni wa Umma, bali hata ya wanavyuoni wa Kisunni bali hata ya Maimamu wane wa Kisuni. Ama wanavyuoni wa Umma, leo Umma una madhehebu nane kuu: nne za Kisuni, Salafiyya, Ibadhi, Shia Imamiyya Ithnashariyya na Zaidiyya. Wenye msimamo huu kimatendo ni baadhi ya Salafiyya walio nje ya Saudia. Ama wale wa Saudia walikuwa na msimamo huo na baada ya kuuchunguza kupitia kwa wanavyuoni wao wakuu kama Sheikh Bin Baz na Ibn 'Uthaimin na Bodi ya wanavyuoni wakuu, wameweza kugundua kuwa msimamo huo ni makosa na kwahivyo wamebadilisha msimamo huo na sasa wanafunga kwa mujibu wa muandamo wao. Ama nchi zenye Madhehebu za Hanafi na Malik, Maulamaa wao pia wanafata miandamo ya nchi zao. Bali Al-Imamu Malik mwenyewe kuna riwaya mbili juu ya Msimamo gani alifata na riwaya kwamba kila mtu na muandamo wake ndio riwaya iliopokewa huko Madina ambako yeye mwenyewe Al-Imamu Malik alikuwa akiishi. Kwa hivyo, narejea tena kwamba dai kwamba msimamo wenu ni msimamo wa Jumhur - hata kama yuko aliyeandika hivyo - basi ni dai la makosa na vitabu vimejaa makosa tele, kitu muhimu ni tahqiq: sio kuchukua tu fulani kasema.
Ama kudai kwenu: "Ndugu Juma hakuwa makini katika kukisoma kitabu alichokiandika Shaykh Naaswir Bachuu" kunaonesha kuwa nyinyi hamukuwa makini katika kukisoma kitabu changu wala cha Sheikh Nassor, kwani nilichokisema mimi ni kuwa huu ni msimamo mpya kwa kwetu Afrika ya Mashariki, na hivi ndivyo alivyosema Sheikh wetu Nassor Bachoo pia. Nimekupeni marejeo katika sehemu mbili redieni mutazame. Kwa hivyo, nyinyi munanibandika kitu ambacho sikukisema.
MNASEMA
i) Al-Marhuum Shaykh Juma 'Abdul-Waduud wa Zanzibar katika kuelezea msimamo wa kufunga pamoja alisema ifuatavyo: "Hii ni rai nayo na wengi wamesema (hivyo) kama Imamu Malik, Ahmad na kundi kubwa la Hanafi."[7]
ii) Shaykh Abdillahi Naaswir wa Kenya ameeleza yafuatayo: "Wako wanaosema kwamba mwezi ukionekana mji mmoja, basi Waislamu wengine popote walipo wafunge. Hayo ni maoni ya Hanbali, Maliki na Hanafi" (Imenukuliwa kutoka kitabu chake Swaum--Nguzo Ya Nne uk. 22 - 23 chapa ya 1985.).
JAWABU
Kuhusu Al-Imamu Malik, nimeshakujibuni kwamba hakuna uthibitisho kwani riwaya kutoka kwake zinagongana. Na wanavyuoni wa madhehebu yake wametafautiana, lakini pia kusema kwamba walio wengi ni wenye kusema kuwa tufate muandamo mmoja ni kitu cha kufikiriwa kwani Ibn Rushd Al-Qurtubi - naye ni katika vigogo wa Kimalik - anasema: "Na wakakubaliana kwamba hilo halizingatiwi katika miji ilio mbali mbali kama Al-andalus (Spain) na Hijaz (Saudia)." Na haya pia yamenenwa na Ibn Abdil-Barri - naye ni katika Malik pia. Na wanavyuoni wa Kihanafi wametafautiana - kama tulivyoeleza katika kitabu - lakini hadi leo hii wanachokitendea kazi Mahanafi na Malik ni kufata miandamo yao kama tunavyoshuhudia katika nchi zao.
MNASEMA
iii) Al-Marhuum Shaykh Hemed bin Juma bin Hemed -aliyekuwa Mufti Mkuu Wa Tanzania Katika hotuba yake iliyonukuliwa neno kwa neno na gazeti la Al-Jihaad toleo No: 4 la tarehe 18/03/1994 sawa na 6/Shawaal/1416 lililotolewa na MSAUD. Katika maelezo mengi aliyoyatoa Shaykh Mkuu huyo kwenye kadhia iliyosababisha kuandama mwezi siku iliyo ikiaminika kuwa ni mwezi (tarehe) 28 ya Ramadhaan alikuwa na haya ya kusema:
"Nyinyi Waislamu wezangu, mwaniambia mimi, kwa ile tukio lenyewe lote, kadhia nilivyoeleza, mwaweza nambia nimewafungisha siku ishirini na nane? Basi tumefungua, Alhamdulillah rabbil aalamin. Linalofuata, mimi nitoe shukrani kubwa kwa watukufu, kutusaidia namna hiyo, na kuondosha tatizo hilo Pia nashukuru sana, kwa bahati kubwa tuliyoipata mwaka huu, ya kihistoria, kufungua siku moja, sisi na wa Saudia, Cairo na Muscat Oman na wapi, kufungua siku moja, nadhani kihistoria, mimi mpaka leo, nina miaka, huu wa sitini na sita, lakini sikumbuki kupata bahati hii. Sikumbuki kupata bakhti hii. Nimemuuliza mzee wangu, Mzee Gumsani, una miaka mingapi, ananiambia themanini na nne, sijui themanini na ngapi! Je iko siku umebahatika hivyo, asema bado sijapata. Je, bahati iliyoje hii? Hadhi kubwa tuliyoipata ya kufungua siku moja, wa Saudia, Cairo, Maskati Oman na miji kadha kadhaa ya Kiarabu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Aiendeleze bahati hii, ili kuimarisha umoja huu. Mungu ajaalie 'Arafah pia iwe moja. Ndio zina matatizo, na 'Iyd ya mfunguo mosi iwe moja. Matatizo haya yaondoke InshaAllaah!" Mwisho wa kunukuu.
JAWABU
Haya! Hoja yenu iko wapi hapa?! Anachokizungumzia Sheikh Hemed ni kuwa watu mara hio waliuona mwezi muandamo sawa; wakafunga sawa: si kwamba mwezi ulionekana sehemu moja watu wa miji yote wakafunga.
MNASEMA
(2) Imeshawahi kutokezea mara nyingi dunia nzima (au sehemu kubwa ya dunia) kufunga na kufungua kwa pamoja, yaani katika siku moja. Mfano mzuri uliowahi kutokea ni huo hapo juu alioueleza Mufti Mkuu Shaykh Hemed bin Juma katika tokeo la mwaka 1994. Pia katika mwaka wa 2007 takriban dunia nzima ilifunga siku moja ya tarehe 13/09/2007.
JAWABU
Haijapata kutokea dunia nzima kufunga siku moja, wala hata sehemu kubwa zaidi ya dunia; na hilo haliwezekani kifaki wala kijografia. Lakini inawezekana nchi nyingi zikafunga pamoja. Na huu sio mjadala wetu: mjadala wetu ni je walifunga kwa kufata muandamo wan chi moja au walifunga kwa miandamo yao.