2
NGUZO YA UCHAMUNGU
KURUDI MADINA
Baada ya ndoa, Imamu
alikaa Baghdad kwa muda wa mwaka mmoja hivi na halafu Mamun aliwaona wakiondoka kwenda Madina.
TABIA YAKE ADHIMU
Imamu Muhammad Taqi
alikuwa ni mmoja wa watu wa ukoo wa Mtume
na aIikuwa na tabia nzuri kama za wale wengine wa ukoo huo. Kumfanyia kila mtu upole, kutosheleza mahitaji ya kila mhitaji, kuweka maisha rahisi na usawa kuwa ni mambo muhimu zaidi, kuwasaidia maskini kwa siri, kuwatendea mema hata maadui, ukarimu mkubwa na kila wakati kuwakarihisha wale wapendao kujifunza vilikuwa sifa kubwa ziIizomtofautisha lmamu Taqi
.
Watawala wa koo za Bani Umayya na Bani Abbas hawakuwa na jambo Ia kufanya juu ya mtu wa ukoo wa Mtume
maana kwa sifa zao hizo walionyesha tofauti kubwa (iliopo kati yao na watu wengine) na kuonyesha ubaya wa watawala na majeshi yao. Kwa hiyo kila mara walijaribu kuivuruga senta ya Kidini ya Madina na jaribio la Yazid kumfanya Imamu Husain
awe upande wake jambo ambalo baadaye lilisababisha masaibu ya Karbala au tukichukua mfano mwingine, Mamun kumteua Imamu Ridha
kuwa mrithi wake wa kiti cha Ufalme kulikuwa ni njia tofauti ya kudhihirishia msimamo wao ule ule wa siku zote. Wakati fulani nguvu za uovu zilijitokeza kuushambulia UkweIi na mara nyingine walijaribu kuvishinda 'vipingamizi' kwa kumwua lmamu Ridha kwa sumu.
Sasa Mamun aIifikiria kuwa wakati huo ulifaa kwa kumgeuza mawazo mtoto mdogo mwenye umri wa miaka minane au tisa ambaye ametengwa na baba yake miaka mitatu iliyopita na hivyo hatari iliyokuwepo kila mara kwa utawala wa Bani Abbas itaondolewa. Mamun hakukuchukulia kushindwa kwake Imamu Ridha
kuwa iwe ndicho chanzo cha kukata tamaa kwake. Alifikiria kuwa haikuwa lazima kuwa ikiwa Imamu Ridha
hakuweza kushawishika (kwa sabahu alikwisha kuwa na tabia za kiutu uzima) mwanawe asingeliweza kufikiriwa kuwa si wa kumtumainia.
Lakini Mamun na watu wote wale ambao macho yao hayakuweza kuuona ukweli wa mambo, walistajaabu kuona kuwa mkwewe Mfalme wa ukoo wa Bani Abbas mwenye umri wa miaka tisa alikataa kukaa katika jumba la kifalme. Walimuona anashikilia kuendelea na tabia ya watu wa ukoo wake na walishangaa kuona kuwa alipokwenda Baghdad alikodisha nyumba ya kuishi badaIa ya kuishi katika majumba ya kifalme. Si hivyo tu, bali baada ya muda mfupi tu alikataa kuishi mjini Baghdad na kabla ya mwaka mmoja kwisha baada ya ndoa yake na binti wa mfalme, ilimbidi mfalme atengane na binti wake na kumruhusu aondoke na mumewe ambaye ilibidi matakwa yake yatiliwe na huyo mfalme mkuu na tena aliye baba mpenzi.
Huko Madina, Imamu
alirudia maisha yake ya zamani. Wakati wake mwingi aliutumia katika msikiti wa Mtukufu Mtume
ambamo wanafunzi wa Hadithi za Mtume
na Elimu ya dini walikwenda na kukuta kiti cha Imamu Ja'far al-Sadiq
kikiwa kimekaliwa tena na kiu yao ya kujifunza ikazimishwa.
Katika maisha yake ya faragha alikuwa na kawaida hiyo hiyo. Alimwekea mkewe Bibi UmmuI Fazl (bintiye Mamun) amri hizo hizo katika maisha yake kama alizowawekea wakeze wengine; baadaye kidogo alimwoa mwanamke mmoja tajiri wa ukoo wa Bwana Ammar bin Yasir (Mwenyezi Mungu na aiweke roho yake mahali pema Peponi) ambaye baadaye alikuwa mama wa lmamu Ali Naqi
. Ummul Fazl alimuandikia baba yake akimlalamikia juu ya jambo hilo. Hakika Mamun alikasirishwa sana kusikia hivyo lakini ilimbidi ajikaze. Kwa hiyo alimjibu akisema, 'sikukuoza kwa Abu Ja'far ili nimzuie asifanye yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu. Usinilalamikie juu ya mambo kama hayo tena.
b Jibu hili lilikuwa la kusawazisha mambo hasa. La sivyo, pamekwishakutokea mifano ambayo kuwapo mwanamke bora (kufuatana na imani) kuliweza kuzuia kufanyika kwa ndoa ya pili. Mtume
hakuoa mke mwingine wakati wa uhai wa Bibi Khadija na wakati wa uhai wa Bibi Fatimah
, Hadhrat Ali
pia hakuoa mke wa pili. Sasa Imamu Muhammad Taqi
aliona kuwa kwa vile Bibi Ummul Fazl akiwa binti wa Mfalme, alihitaji kutendewa tofauti na wake wengine. Imamu
alitaka kumuonyesha Bibi huyu kuwa mwenendo wa Uislamu haukutaka kuendekeza jambo hilo.
IMAMU MUHAMMAD TAQI [a.s] AKIWA MWALIMU WA DINI
Hotuba zake zilikuwa zinapendeza sana. Wakati mmoja wa Hija huko Makka alitoa hotuba juu ya amri za Dini kwa namna nzuri mno kiasi ambacho wanachuoni wakuu waliokuwepo walishangaa na walikubali kuwa walikuwa hawajapata kusikia hotuba nzuri kama hiyo. Wakati wa Imamu Ali
ilizuka madhehebu mpya ambayo ilikomesheza Uimamu kwa Imamu Musa Kadhim
na hawakuamini Uimamu wa Imamu Ali Ridha
.
Madhehebu haya yalijulikana kwa jina Ia "Wazifiyyah". lmamu Muhammad Taqi
alifaulu vizuri kuhubiria dhidi ya imani yao kiasi ambacho karibu kila mmoja wao alikubaliana naye na karibu wale wote walioifuata madhehebu hayo waliyotoka. Idadi kubwa ya wanavyuoni wakawa wanafunzi wake. Kama alivyoacha mhenga wake Hadhrat Ali
, Imamu Taqi
nae ameacha idadi kubwa ya Hadithi za kuaminika na zinazojulikana sana. Pia ameacha hotuba fulani nzuri sana.
SAFARI YAKE YA MWISHO KWENDA IRAQ
Katika mwaka wa 218 Hijiriya mfalme Mamun alifariki na nduguye Mu'tamin alirithi kiti cha ufalme akitumia jina Ia Mu'tasim Billah. Mara moja barua za malalamiko ambazo Bibi Ummul Fazl alimuandikia baba yake sasa zilianza tena kummiminikia baba yake hakuzitia maanani barua hizo kwa kuwa mwenyewe alimuozesha kwa Imamu
ingawa watu wa ukoo wa Bani Abbas walipinga, sasa huyu baba mdogo alianza kuzisikiliza.
Wakati wa ndugu yake Mamun, Mu'tamin aliwahi kukiwakilisha kikundi kilichopinga kuozwa kwa binti wa nduguye, Bibi Ummul Fazl kwa Imamu
. Zaidi ya hayo, alikuwa akiiogopa na kuihesabu sifa ya Imamu
ya uongozi wa dini kuwa si isiyokuwa na haki, chanzo cha hatari kwa utawala wake kama vile baba zake walivyofanya wakati wa enzi zao.
Kwa hiyo mnamo mwaka wa pili wa utawala wake alimwagiza Imamu
aende kwake na alimwandikia barua Gavana wa Madina, aitwaye Abdul Malik kuhusu jambo hiIo. Hivyo Imamu
alimuacha mkewe, mama yake Imamu Ali Naqi
akae na Abdul Malik na yeye akaondoka kwenda Baghdad.
KUFARIKI KWAKE
Kwa muda wa mwaka mmoja hivi baada ya kwenda Baghdad Imamu
hakusumbuliwa na Mu'tasim isipokuwa maisha ya Baghdad yalikuwa ya namna ya kifungo". Halafu silaha ile ile ya zamani (yaani ya kuuwa kwa sumu) ilitumika kwake na akapewa sumu akafa mnamo tarehe 22 Dhul-Qa'dah mwaka 220 Hijiriya. Alizikwa karibu na kaburi la Imamu Musa Kadhim
. Na mahali hapo pakajulikana kwa jina Ia Kadhimain (mji wa Kadhim wawili) na sasa kituo hicho kinaitwa Jawadain (mahali pa Jawad). Kimoja kati ya vyeo vya Imamu Muhammad Taqi
ni "Jawad".
MASAYYIDI WA UKOO WA RIDHAWI
Masayyidi (Masharifu) ambao wanajulikana kwa jina la Ridhawi wote wametokana na kizazi cha Imamu Muhammad Taqi
na wangekuwa wameitwa Taqawi kama pangekuwepo mfuatano wa ukoo wa Imamu Ridha
zaidi ya kupitia kwa Imamu Muhammad Taqi
ambao ungejulikana kwa jina Ia Ridhawi kwa kutofautishwa na wale wa ukoo waTaqawi. Lakini kizazi cha Imamu Ali Ridha
ni kile tu kilichotokana na lmamu Muhammad Taqi
na kwa kuwa Imamu Ali Ridha
alijulikana sana katika ulimwengu wa Kiislamu kwa sababu ya kuteuliwa kwake kuwa mrithi wa mfalme Mamun wa kiti cha ufalme, kizazi cha Imamu Muhammad Taqi
chote kiliitwa Ridhawi badala ya Taqawi.
HADITHI ZA IMAMU MUHAMMAD TAQI [a.s]
1. Yeyote yule amsaidiaye mshari (kwa namna yoyote ile) katika vitendo vyake ni mshiriki wake.
2. Siku ya "Uadilifu" (mdhuIumiwa kulipiziwa kisasi) ni ngumu zaidi kwa mshari (huyo aliyedhulumu) kuliko siku aliyomfanyia shari mdhulumiwa.
3. Mtu afanyaye kitu bila ya elimu ya kukifanyia kitu hicho, hukiharibu badala ya kukitengeneza.
4. Uchamungu huleta heshima, kujifunza ni hazina, ukimya humpa mtu hekima.
5. Hakuna kitu kibaya kwa dini kupita 'bid'at' (uzushi wenye maana mbaya) na hakuna kitu kiharibucho heshima kama tamaa.
6. Kuwatengeneza raia hutokana na mtawala na dua huzuia maovu.
7. Anayetumia maneno mabaya hulipwa maneno mabaya na afanyaye jambo bila akili huumia.
8. Mkarimu huwa mwangalifu kwa ukarimu wake kuliko wale wafaidikao kwa ukarimu huo. Ukarimu wake humlipa na humletea heshima na utukufu.
9. Yeyote ategemeaye upendeleo fulani toka kwa mtu mwingine pia humuogopa mtu huyo. Na yeyote asiyekielewa kitu fulani hukiona ni kibaya.
10. Kuachwa kwanza (kutoadhibiwa mara moja) ni kitu kipoteacho mara moja tu.
11. Anayetaka kuokoka lazima awe na moyo wa uvumilivu katika shida.
12. Ampandaye farasi wa uvumilivu huipata barabara ya kwendea kwenye uwanja wa ushindi.
13. Vitu vinne humuongoza mtu kwenye matendo mazuri, afya, utajiri, elimu na Neema za Mwenyezi Mungu.
14. Kumwamini Mwenyezi Mungu ni kuokokana na maovu yote na ni kinga kutokana na kila adui.
MAELEZO MACHACHE KUHUSU KABURI LA KADHIMAIN
Mtu yeyote anayeukaribia mji wa Baghdad kutokea upande wa Kaskazini au Magharibi atapendezwa kuona minara minne ya dhahabu katika mji wa Kadhimain, Kuba la Kadhim wawili ambao ni Maimamu Musa bin Ja'far
na Muhammad Taqi
. Kwenye lango kubwa lenye umbo la nusu mduara, kwenye ukuta unaolizunguka Kuba hilo pametundikwa mikufu mikubwa ambayo inaonyesha kwamba sehemu ile ni Takatifu.
Jengo la sasa lilijengwa mnamo mwanzoni mwa karne ya kumi na sita (ya zama za Ukristo), na limekuwa likitarizwa kwa nakshi nzuri nzuri. Jengo hili linakumbusha kujengwa kwake na Shah Isma'ili wa kwanza (tangu mwaka 1502 hadi 1524 Masihiya), ingawaje sultani wa Kituruki, Suleiman Mkuu aliyeuteka mji wa Baghdad na akakaa humo kwa muda wa miezi minne katika mwaka wa 1534 Masihiya alikwenda sehemu takatifu za Mashia na inasemekana aliyatia nakshi zaidi yale Makuba ya Kadhimain. Hata hivyo, vigae vya zege, viliwekwa mnamo mwaka 1796 Masihiya na Shah Muhammad Khan aliyekuwa Mfalme wa kwanza wa ukoo wa Qachar.
Mnamo mwaka 1870 Masihiya, mfalme Nasiruddin Shah Qachar aliviweka hivi vigae vya dhahabu katika Kuba moja na kwenye minara. Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba tarehe zote za mabadiliko hayo zimeandikwa waziwazi. (Soma Kitabu cha maarifa yote kiitwacho "Encyclopaedia of Islam", chini ya kichwa cha habari "Kadhimain".
Hivyo ni wazi kwamba kuna miaka mia saba ya historia ya Kuba hili, kabla ya muda wa kutengenezwa kwa sasa kulikofanywa na Shah Ismail wa Kwanza. Maimamu wawili waliishi katika siku za awali za mji wa Baghdad ambapo kuta za Mji wa Mviringo wa mfalme Mansur katika upande wa Magharibi wa mto Tigris zilipokuwa bado zimesimama. Palikuwa na sehemu ya makaburi upande wa Kaskazini na Kaskazini ya magharibi zilizokuwa na majina kadhaa; likiwemo lile la Lango la Shamu, Ukoo wa Bani Abbas na lile la Lango la Majani Makavu, (Soma kitabu kiitwacho 'Tabaqat' cha Bwana Ibn Saad).
Maimamu hao wawili walizikwa karibu sana na kaburi la mwisho la upande wa Magharibi lakini wakati Bwana Ya'qubi, alipoandika kitabu chake cha Historia, sehemu yote ya Kaskazini ilikuwa imetengwa kwa ajili ya makaburi ya Maquraishi (Soma kitabu kiitwacho 'Tarikh') cha Bwana Yaqubi.
MWISHO