NENO LA AWALI
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu Mahitaji ya zama zetu hizi yanalazimisha kutathmini maswali mengi yenye umuhimu na sio kuridhika na tathmini zake za awali. Mfumo wa haki za ndoa na majukumu ya kifamilia ni miongoni mwa masuala haya. Kwa sababu mbali mbali, ambazo tutazieleza baadaye, imedhaniwa kuwa katika zama hizi, suala la msingi ni uhuru wa mwanamke na haki zake ziwe sawa na za mwanamume, na kwamba maswala mengine yote yapo chini ya suala hili kuu. Hata hivyo kwa mtazamo wetu, suala la msingi kabisa, au angalau tuseme moja ya masuala ya msingi kabisa, juu ya haki za kifamilia, ni iwapo mfumo wa ndoa unajitegemea na hautangamani na mifumo mingine yote ya kijamii na una vigezo na mantiki yake maalum, au ni moja tu ya mifumo mingi ya kijamii na kuwa vigezo na falsafa zile zile ndizo zinazotumika kulishughulikia suala hili kama ilivyo kwa mifumo mingine ya kijamii.
Kiini cha shaka yetu ni kuwa, kwa upande mmoja, katika mfumo huu makundi makuu yanayohusika yapo katika jinsia mbili tofauti, na kwa upande wa pili, inahusisha ongezeko na muendelezo wa vizazi. Maumbile yamefanya tabia za kimaumbile na viungo vya uzazi vya makundi haya mawili kuwa tofauti. Jamii ya wanandoa ni nusu-asili na nusu -mkataba. Ni njia ya kati na kati baina ya jamii ya silika kama ile ya nyuki na siafu ambayo haki na majukumu yake yameshaamuliwa na maumbile na hakuna uwezekano wa kuvunja sheria, na pia baina ya jamii ya kimkataba kama jamii ya wanaadamu, ambayo ina umbile la asili au silika. Kama tunavyojua, wanafalsafa wa kale walilichukulia suala la maisha ya familia kama tawi linalojitegemea la busara za kivitendo, na waliamini kuwa sehemu hii (maisha ya familia) ya maisha ya mwanadamu ina vigezo vyake tofauti.
Plato katika kitabu chake 'The Republic', Aristole katika kitabu chake, 'The politics,' na Abu Ali bin Sina (Avicenna), katika kitabu cha al-Shifaa, wamelizungumzia suala hili katika mtazamo huu pia. Ni suala lenye utata iwapo haki za asili za mwanaume na mwanamke zinafanana au hazifanani; kwa maneno mengine, iwapo haki kwa mujibu wa maumbile ya mwanadamu, ni ya jinsia moja au jinsia mbili, na iwapo kuwa na jinsia ya kike au ya kiume kunaathiri haki na majukumu ya mwanadamu. Katika ulimwengu wa Magharibi, harakati za haki za binadamu zilianza katika karne ya 17, kipindi cha mwamko wa harakati za kisayansi na kifalsafa. Waandishi wanafalsafa wa karne ya 17 na 18 walifanya jitihada zinazostahili sifa kwa kueneza mawazo yao juu ya haki za msingi za asili na zisizoondosheka za binadamu.
Jeans Jacques Rousseau, Voltaire na Montesquieu, ambao ni miongoni mwa wanakundi hili la waandishi na wanafalsafa, ni wafadhili wakubwa wa jamii ya mwanadamu, na inafaa kusema kuwa mchango wao kwa maisha ya wanaadamu haukuwa mdogo kuliko wa wagunduzi na wavumbuzi wakubwa, vilikuwa na thamani sawa. Wazo lao kuu lilikuwa kwamba wanaadamu wana mfululizo wa haki za asili walizozaliwa nazo pamoja na uhuru - vyote ambavyo haviwezi kuondosheka wala kuhamishwa na yeyote kwa visingizio vyovyote. Watu wote, ikiwa ni pamoja na watawala na watawaliwa, weupe na weusi, matajiri na maskini, wote ni sawa. Matokeo ya harakati hizi za kijamii na kisomi zilionekana kwanza Uingereza na kisha Marekani na baadaye Ufaransa. Yakaja yakatokea mapinduzi hapa na pale, mifumo ikabadilishwa na mikataba ikasainiwa. Polepole, harakati zilienea katika nchi nyingine.
Katika karne ya 19, mawazo mapya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa juu ya haki za binadamu yaliibuka. Maendeleo mapya yalipelekea kutokea kwa ujamaa, ushiriki wa wafanyakazi katika faida za viwanda, na kuhamishwa kwa serikali kutoka kwa jamii ya mabepari kwenda kwa watetezi wa wafanyakazi (wavuja jasho). Mpaka kufikia mwishoni mwa karne ya 19, mazungumzo yote na hatua zozote za kivitendo zilizochukuliwa katika anga ya haki za binadamu, zilikuwa zimejikita tu katika haki za mataifa juu ya serikali na haki za waajiriwa dhidi ya waajiri. Katika karne ya 20, suala la haki za wanawake liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka wa 1948, Umoja wa mataifa ulitangaza Azimio la Dunia la Haki za Binadamu ambapo ulitoa mbiu ya usawa wa haki kati ya mwanamke na mwanaume kwa wazi kabisa.
Harakati zote za kijamii huko Magharibi toka karne ya 17 zimekuwa zikizunguka kwenye uhuru na usawa, kwa vile harakati za haki za wanawake zilikuja mwisho kabisa, na historia ya masaibu ya wanawake Ulaya, kutokana na mtazamo huu, ilikuwa mbaya sana, Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu halikuzungumzia chochote zaidi ya uhuru na usawa.
Wanaounga mkono harakati hizi wanashikilia kuwa harakati hizi zinakwenda pamoja na harakati za haki za binadamu. Wanasema kuwa bila kuhakikisha uhuru na haki za wanawake hakuna maana yoyote kuzungumzia uhuru na haki za mwanadamu. Pia walidai kuwa sababu kubwa ya migogoro ya kifamilia ilitokana na mwanamke kunyimwa uhuru na usawa wake dhidi ya mwanaume, na kwamba matatizo yote haya ya kifamilia yatatatuliwa mara tu tatizo hili litakapoondolewa Kilichosahauliwa katika hili kilikuwa ni kile tulichokieleza kama suala la msingi kuhusiana na mfumo wa haki za familia, hii ni kuwa, iwapo mfumo huu unajitegemea au unategemea mifumo mingine ya kijamii, na ikiwa una vigezo na mantiki tofauti au la.
Msisitizo uliwekwa tu kwenye kanuni za jumla za uhuru na usawa na nukta pekee iliyozingatiwa ilikuwa ni ile ya haki za asili na zisizoondosheka za binadamu. Ilidaiwa kuwa mwanamke, kama binadamu, alikuwa na stahili ya kupata haki zote anazozifurahia na anazozipata mwanaume. Katika sura fulani za kitabu hiki, tumejadili vya kutosha juu ya suala la vyanzo ambavyo kutokana navyo haki za asili zimechukuliwa au zimetengenezwa. Huko, tumeonyesha kuwa misingi ya haki zote ni maumbile yenyewe.
Ikiwa mwanadamu ana haki maalum, ambazo farasi, kondoo, ndege na samaki hawana, hii inatokana na maumbile yake na jinsi alivyoumbwa. Ikiwa wanaadamu wote ni sawa katika haki za asili na wote lazima waishi maisha huru, hii ni kwa sababu mfumo huo ndio walioumbwa nao. Wasomi wanaounga mkono wazo kuwa uhuru na usawa ni haki aliyozaliwa nayo mwanadamu, hawana hoja nyingine zaidi ya hii. Hivyo katika suala la haki za familia pia, tunapaswa pia kuongozwa na maumbile. Sasa hebu tuangalie kwa nini mazingatio ya kutosha hayakuwekwa kwenye suala tulilolielezea kama la msingi.
Je imeshathibitika kisayansi kwamba tofauti kati ya mwanaume na mwanamke ni ya kioganiki tu (kimaumbile) na haiwaathiri kiumbo na kiroho au haki na majukumu yao, na ndio maana imepuuzwa katika falsafa ya kisasa ya jamii? Kusema kweli, ilivyo ni kinyume kabisa na swali hili. Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi na ugunduzi wa kibaiolojia na kisaikolojia imethibitika kuwa kuna tofauti muhimu kati ya hizi jinsia mbili. Katika kitabu hiki, tumejadili suala hili na tumenukuu maoni ya wanabaiolojia na wanasaikolojia juu ya hili. Inashangaza kwamba licha ya yote haya, suala hili la msingi lilipuuzwa.
Labda kutolijali suala hili la msingi kumetokana na maendeleo ya haraka mno ya harakati za ukombozi wa mwanamke. Ndio maana, wakati harakati zikirekebisha hali ya mambo kuondoa taabu za wanawake, katika baadhi ya maeneo zimewasababishia maafa wao na jamii nzima kwa ujumla. Tutaangalia baadaye katika kitabu hiki, kwamba mwanamke wa Kimagharibi, hadi mwishoni mwa karne ya 19, alinyimwa haki zake za msingi za binadamu. Ilikuwa ni juzi tu hapa katika karne ya 20 ambapo watu wa Magharibi walifikiria kurekebisha hali ya mambo.
Hii harakati ilipoanza, katika kipindi cha mwamko wa harakati nyingine, kudai usawa na uhuru, walitegemea miujiza kwa maneno haya mawili tu. Walisahau kuwa usawa na uhuru ulihusiana na uhusiano baina ya watu, kama wanadamu tu. Hakuna shaka yoyote kuwa mwanamke ni mwanadamu na amezaliwa huru kama mwanadamu mwingine yeyote na kwa sababu hiyo anastahili haki sawa. Lakini mwanamke ni mwanadamu mwenye sifa fulani za kipekee. Mwenendo wa tabia zao ni tofauti (na wanaume) na mfumo wa akili zao ni wa kipekee.
Tofauti hii sio matokeo ya sababu za kijiografia, kihistoria au kijamii, bali ni ndio maumbile yao. Maumbile kwa makusudi kabisa yamewafanya wawe tofauti (na wanaume) na jitihada zozote zitakazochukuliwa dhidi ya malengo ya maumbile zitakuwa na matokeo mabaya. Kama tulivyochukuwa hamasa zetu kutoka kwenye maumbile juu ya usawa na uhuru wa mwanadamu, basi vivyo hivyo ndivyo tunavyopaswa kupata mwongozo kutoka kwenye maumbile ili tuweze kuamua iwapo haki za mwanamke zinafanana na za mwanaume au hazifanani na iwapo jamii ya kifamilia ni angalau nusu-asili (semi-natural society).
Ni jambo linalofaa kutafakari iwapo kuwepo kwa jinsia mbili katika wanyama, ikiwa ni pamoja na binadamu kumetokea kama ajali au ndio muundo wa maumbile uliokusudiwa; yaani iwapo tofauti za jinsia ni za juu juu tu, au ni kama Alexis Carell alivyoonyesha kuwa kila seli ya mwili ya mwanadamu ina jinsia, iwapo mwanaume na mwanamke wanayo, au hawana, kazi tofauti za kufanya, na kama haki ni za jinsia moja au za jinsia mbili. Swali kama hilo pia linaweza kuulizwa juu ya maadili, elimu adhabu, majukumu na ujumbe. Wakati wa harakati za ukombozi wa mwanamke, haikuzingatiwa iwapo, mbali na usawa na uhuru, kuna maswali mengine pia. Hapana shaka kuwa uhuru na usawa ni mambo muhimu. Lakini mambo sio haya tu. Usawa wa haki ni jambo moja, lakini kufanana kwa haki ni jambo jingine tofauti kabisa. Usawa wa haki za mwanaume na mwanamke kwa mtazamo wa thamani ya kimaada na maadili ni tofauti na kufanana kwa haki zao.
Wakati wa harakati hizi, kwa makusudi au kwa bahati mbaya, usawa umetumika kumaanisha kufanana, na hivyo ubora umefunika uwingi. Ilisisitizwa kuwa mwanamke ni binadamu, lakini ilisahauliwa kuwa ni mwanamke pia. Kwa kusema kweli, kutokujali huku hakukutokana na haraka peke yake, kulikuwa na sababu nyingine pia, ambazo zilimfanya mwanamke anyonywe kwa jina la uhuru. Moja ya sababu hizo ni tamaa iliyopindukia ya wamiliki wa viwanda waliotaka kumuondoa kutoka nyumbani kwenda kiwandani ili kuvuna uwezo wake kwa maslahi yao ya kiuchumi.
Wakiwa na malengo haya, walitetea haki za mwanamke, uhuru wake wa kiuchumi na uhuru wa usawa wa haki kama zile za mwanaume. Ni wao waliokazia utambulukaji rasmi wa madai haya. Will Durant katika sura ya tisa ya kitabu chake 'The pleasure of philosophy,' baada ya kutaja baadhi ya nadharia zenye kumdhalilisha mwanamke zilizokuwa zimebuniwa na Aristole, Neitzsche, Schopenhauere na baadhi ya maandiko (matakatifu) ya kiyahudi na kuonyesha ukweli kuwa wakati wa mapinduzi ya Ufaransa japo kulikuwa mazungumzo ya uhuru wa mwanamke, kivitendo hakukuwa na mabadiliko yoyote, anasema kuwa hadi mwishoni mwa karne ya 19 mwanamke hakuwa na haki yoyote iliyopaswa kuheshimiwa, na ambayo mwanaume angepaswa kuizingatia au ingemfanya abanwe na sheria.
Kisha anajadili mambo yaliyoleta mabadiliko katika karne ya 20. Anasema kuwa uhuru wa mwanamke ni matokeo ya ziada ya mapinduzi ya viwanda. Anaongeza kuwa wafanyakazi wa kike walikuwa ni wa gharama nafuu na waajiri walipenda kuwatumia hawa zaidi kuliko wanaume waliuokuwa jeuri (wabishi) na walikuwa ghali zaidi. Katika karne moja iliyopita ilikuwa vigumu sana kwa wanaume kupata kazi, lakini kulikuwa matangazo yaliyokuwa yanawaomba wanaume wawapeleke wanawake wao na watoto viwandani.
Hatua ya kwanza ya kumkomboa mwanamke ilichukuliwa mwaka wa 1882, ambapo sheria ilipitishwa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, wanawake wa Uingereza walipata fursa na haki ambayo haikuwahi kutokea kabla, haki ya kujiwekea fedha zozote walizopata.1 Sheria hii iliyoelezewa huafikiana na maadili matukufu ya kikristo, ilipitishwa na wamiliki wa viwanda na Bunge, ili kuwashawishi wanawake wa Uingereza kwenda kufanya kazi viwandani. Tokea mwaka huo, hamu isiyozuilika ya kujichumia fedha imewalazimisha kuhenyeka katika maduka na viwanda, na imewaondolea mzigo wa kufanya kazi za nyumbani (The pleasure of philosophy, uk. 155-159). Kutokana na maendeleo ya mitambo na ongezeko la uzalishaji ilionekana ni muhimu kwa mabepari, ili kulazimisha bidhaa zao za ziada juu ya walaji wanapaswa kutumia mbinu zote za kusikia na kuona (TV), kiakili, kihisia, kisanii na hata ngono.
Katika kuwabadilisha walaji (wanunuzi) kuwa vipengele vya utumiaji na kuwafanya wawe kama zana zisizo na nguvu katika soko la walaji, waliamua kuwatumia wanawake, lakini hawakuwatumia kama wafanyakazi tu katika mchakato wa uzalishaji pamoja na wanaume. Wao, kwa upande mwingine walitumia urembo wao, uchangamfu na mvuto wa kingono na kuwashawishi kujitolea muhanga heshima na kujistahi kwao ili kuweza kuwapotosha hao wateja na kuwalazimisha hiari zao wenyewe juu yao.
Ni dhahiri kwamba yote haya yalifanyika katika jina la uhuru kwa ajili ya wanawake na usawa wao na wanaume. Kisiasa vile vile haikurudi nyuma katika kutekeleza kipengele hiki. mara kwa mara utakuwa unasoma taarifa kama hizo katika magazeti na majarida. Mwanamke ananyonywa na huduma zake hutumiwa kutekeleza malen1. Dr. Ali Shayagan, katika kusherehesha sheria ya Iran ya kiraia, anaandika kuwa uhuru wa kumiliki mali, ambayo mwanamke anayo sasa na ambayo imetambuliwa na sheria ya Shia'h toka awali kabisa, haikupata kuwepo siku za kale huko Ugiriki, Urumi, Ujerumani na mpaka hivi karibuni hali imekuwa hivyo katika nchi nyingine nyingi. Alionekana kama mtu mdogo tu na kama kichaa, hivyo alizuiwa kumiliki mali. Huko Uingereza, ambapo mwanamke alihesabiwa kuwa sehemu ya mume wake hivyo si mtu anayejitegemea, sheria mbili zilipitishwa, moja mwaka 1870 na nyingine mwaka 1882, ambazo ziliondoa kizuizi cha mwanamke aliyeolewa kumiliki mali.
go ya wanaume chini ya joho la uhuru na usawa. kwa dhahiri kijana (wa kiume) wa karne ya 20 hawezi kukosa fursa hii ya thamani. Ili kumzuzua (mwanamke), bila kumbebesha dhamana za kawaida, na kucheza na akili yake kwa uhuru yeye (mwanaume) zaidi kuliko mtu yeyote yule, hutoa machozi ya mamba kwa ajili ya kutojiweza kwa wanawake na uonevu usio na maana dhidi yake (huyo mwanamke). ili kuwa na uwezo wa kutoa mchango mkubwa kwenye 'mwenendo huu mtakatifu' huenda mpaka kiasi cha kuchelewesha ndoa yake mwenyewe mpaka kufikia umri wa miaka 40 au hata kubakia kapera maisha yake. Hapana shaka, karne ya sasa imerekebisha malalamiko mengi ya mwanamke, lakini imeleta shida nyingi kwake. Kwa nini? Je, ameangamia daima milele na hana njia ya kufanya katika mzunguko huu?
Je, haiwezikani yeye kuondokana na shida zake zote hizi za zamani na za sasa kwa mara moja na wakati huo huo? Je, wanawake wamewekwa (kutaabika) kwenye shida hizi mbili na kwamba lazima alazimike kuchagua moja ya njia hizi mbili? Kwa kweli sio muhimu kiasi hicho kwamba apaswe kuendelea kuteseka. Alitaabika huko nyuma, zaidi hasa kwa sababu ilisasahauliwa kuwa yeye ni binadamu. Anataabika sasa hivi kwa sababu ya uwanamke wake, mahitaji yake aliyozaliwa nayo, haki zake na madai ya kawaida na vipawa vyake maalum vimepuuzwa kwa makusudi au vinginevyo.
Kinachoshangaza zaidi ni kuwa kila zinapozungumziwa tofauti za mwanamke na mwanaume, baadhi ya makundi yana tabia ya kuzichukulia tofati hizo kama kutokuwa mkamilifu kwa mwanamke na ukamilifu wa mwanaume. Fikra kama hizi zimewafanya waamini kuwa wana upendeleo fulani wa kipekee, ambao wanawake wamenyimwa. Hawaelekei kuelewa kuwa hakuna suala la ukamilifu na kutokuwa kamilifu.
Haikuwa nia ya Muumba kumfanya mmoja mkamilifu na aliyependelewa, na mwingine kuwa mbovu na aliyenyimwa. Watu wa aina hii wakiegemeza hoja zao hizi juu ya dhana zao za kushangaza za kimantiki na za busara, wanadai kwamba kwa vile maumbile yamekuwa katili kwa mwanamke, tusiongeze tusi kwenye jeraha na kwa hiyo itakuwa ni wema zaidi kuupuuza uwanauke wake! Lakini, kwa kweli ni kupuuzia nafasi ya asili ya mwanamke ambayo inasababisha yeye kunyimwa haki zake. Ikiwa wanaume wataungana dhidi ya wanawake na kusema, "Kwa vile sisi wote ni sawa, kazi zetu, majukumu yetu malipo na adhabu ziwe sawa.
Lazima mshiriki pamoja nasi katika kazi ngumu na nzito, mlipwe kutokana na kiasi cha kazi mliyofanya na msitarajie kuhurumiwa, kuheshimiwa wala kulindwa. Bebeni gharama zenu wenyewe na tutachangia gharama za matunzo ya watoto sawa kwa sawa na muweke utaratibu wa kujilinda dhidi ya hatari zote.
Mnapaswa mtugharamie kama tunavyowagharamia." Hali kama hii ikitokea, wanawake ndio watakaoumia, kwa sababu kimaumbile hawana nguvu za kuzalisha kama wanaume, wakati wao wanatumia fedha zaidi kuliko wanaume. Hedhi zao, taabu za mimba, uchungu wa kuzaa na malezi ya watoto vinawaweka katika nafasi ya kuhitaji ulinzi wa wanaume. Wanahitaji haki zaidi na hawawezi kumudu gharama kidogo. Hali hii sio kwa binadamu tu. Hata kwa wanyama wote, madume kwa silika huyalinda majike yao.
Mazingatio sahihi ya nafasi ya asili ya mwanamke na mwanaume na usawa wao na haki zao zinazofanana kama wanaadamu yanamuweka mwanamke katika nafasi hii ya raha ambapo utu wake haudharauliwi wala haiba yake haiathiriki. Ili kupata picha ya matokeo ya kupuuza nafasi asili ya mwanaume na mwanamke, hebu tuangalie wanachosema na kuandika wale ambao wamepitia njia hii kwa ukamilifu. Siku za nyuma kuna makala moja iliandikwa katika gazeti la Marekani liitwalo 'Coronet'. Linafaa kusoma. Linaelezea kisa cha mwanamke ambaye, kwa ajili ya haki sawa kati ya mwanaume na mwanamke alipoteza tahafifu aliyokuwa anapewa hapo awali. Mwanzo wanawake hawakutakiwa kunyanyua zaidi ya ratili 25, wakati kikomo hiki hakikuwepo kwa ajili ya wanaume.
Anasema sasa mazingira ya kazi katika kiwanda cha General Motors, katika jimbo la Ohio, ambapo takriban wanawake 2500 wanamenyeka, yamebadilika. Sasa anajikuta akihudumia injini yenye nguvu sana au kusafisha oven yenye uzito wa ratili 250, iliyowekwa hapo na mwanaume wa miraba minne. Anahisi kuchoka kabisa na anaona amepigika. Anasema pia kuwa kila dakika analazimika kutumia kulabu yenye kishikio cha inchi 25 mpaka 50 chenye uzito wa ratili 35. Mikono yake mara zote imevimba na inauma.
Makala baadaye inasimulia mashaka na masaibu ya mwanamke mwingine ambaye mume wake ni baharia katika jeshi la wanamaji. Hivi karibuni, Afisa wa jeshi (Admiral) aliamua kuwaingiza wanawake 40 na wanaume 480 na akawatuma kazini. Meli iliporudi baada ya safari ya kwanza, wasiwasi wa wake wa wanamaji ulithibitika. Muda si mrefu ikajulikana kwamba sio tu kwamba walifanya mapenzi ndani ya meli, lakini wanawake walio wengi walifanya mapenzi na wanaume zaidi ya mmoja.
Makala inasema kuwa katika jimbo la Florida, wajane wana wasiwasi sana tangu ukombozi wa mwanamke ulipoanza kwa vile Jaji wa jimbo hili ameitangaza sheria inayoruhusu ruzuku ya dola 500 kwa wajane kuwa inakwenda kinyume na katiba kwa vile inawabagua wanaume. Makala inaongeza kuwa wanawake ni wa kwanza kuumia. Wengine pia, wakati wa zamu yao, wataonja ladha ya ukombozi.
Kwa walio wengi swali ni iwapo wanawake wamepoteza zaidi kuliko walivyopata. Haina maana kulilia maziwa yaliyomwagika. Onyesho limeanza na watazamaji wameshachukua viti vyao. Mwaka huu marekebisho ya 27 ya katiba yanakusudiwa kupitishwa na kwa mujibu ya marekebisho hayo, marupurupu yote yanayohusiana na ngono yatafutwa. Hivyo, hofu iliyoelezwa na Profesa Ruscobound, wa chuo cha sheria cha Harvad, kwamba ukombozi wa mwanamke ni chanzo cha machungu yasiyoelezeka katika medani ya sheria ya mwanamke wa Marekani yatadhihirika.
G. Irvin, Seneta wa North Carolina, baada ya kuisoma jamii ya Marekani, ambapo wanawake na wanaume wana haki sawa, anapendekeza zirekebishwe na wanaume wasiwajibike tena kutunza familia. Kwa mujibu wa makala hii, Mrs. Macdaniel anasema kuwa, kutokana na kunyanyua vitu vizito baadhi ya wafanyakazi wa kike katika kiwanda chake walipatwa na tatizo la kuvuja damu ndani kwa ndani (hemoreji).
Wanawake hawa wanataka kurudi katika nafasi zao za awali. Wanataka watendewe kama wanawake na sio kama wafanyakazi tu. Kwa wapiga kampeni wa usawa linaweza kuwa jambo rahisi. Wanakaa katika nyumba zao za fahari na kuzungumzia usawa, lakini hawajawahi kufanya kazi viwandani, ambako wanawake wengi walioajiriwa katika viwanda katika nchi hii wanafanya kazi. Mrs.
Macdeniel anasema hataki usawa huu, kwa sababu hawezi kufanya kazi za kiume. Wanaume wana nguvu zaidi kuliko wanawake. Ni bora aache kazi kuliko kushindana na wanaume. Faida ambazo wanawake wa Ohio wamezipoteza ni nyingi sana kuliko faida wanazopata chini ya sheria ya wafanyakazi.
Wanawake wamepoteza haiba yao. Haifahamiki ni nini wamekipata baada ya kukombolewa. Hali ya wanawake wachache inaweza kuwa imeboreka, lakini si wanawake wote. Hiki ndio kilikuwa kiini cha makala. Ni dhahiri kutokana na yaliyomo ndani yake kuwa wanawake hawa wamechoshwa mno na matatizo waliyosukumiwa kwa jina la uhuru na usawa kiasi kwamba wamepatwa na mzio (allergy) wa maneno haya mawili. Wanasahau kuwa maneno haya hayapaswi kulaumiwa.
Mwanaume na mwanamke ni nyota mbili kila moja ikiwa na obiti yake. "Jua halipiti njia ya mwezi wala usiku hauuzidi mchana Kila kimoja kinaelea katika Obiti (njia) yake." (36:40). Furaha yao, na pia furaha ya jamii nzima ya wanaadamu inategemea sharti kuwa kila mmoja anatembea katika obiti yake. Uhuru na usawa unaweza kuwa n a maana tu ikiwa jinsia zote mbili zitafuata njia zake za asili.
Tunaposema kwamba suala la haki za wanawake nyumbani na katika jamii litathminiwe upya na lisibakie katika uzito wa tathmini ya awali, tunamaanisha kuwa tuongozwe na maumbile na tuzingatie uzoefu uchungu na utamu tulioupata huko nyuma, hasa wa karne hii. Hapo tu ndipo harakati za wanawake zitakapokuwa na maana. Inakubaliwa na kila rafiki na adui kuwa Qur'ani Tukufu ilifufua haki za wanawake. Hata maadui wanakiri angalau kwamba Qur'ani wakati wa kuteremshwa kwake ilichukuwa hatua kubwa katika kuboresha hali ya wanamke na kurejesha haki zao za binadamu.
Qur'ani ilifufua haki za mwanamke kama mwanadamu na kama mwenzi wa mwanaume katika utu na haki za binadamu lakini haikupuuza uwanauke wake wala uwanaume wa mwanaume. Kwa maneno mengine Qur'ani haikupuuza maumbile ya mwanamke. Ndio maana kuna kuwafikiana kikamili kati ya kanuni za maumbile na kanuni za Qur'ani. Mwanamke katika Qur'ani ni sawa na mwanamke katika maumbile. Vitabu hivi viwili vitakatifu, kimoja kikiwa kimeumbwa na kingine kikiwa kimekusanywa, vinakubaliana na kuafikiana kabisa. Nia ya kitabu chetu ni kuangazia na kuelezea kuafikiana huku.