19
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
NDOA YA MITALA (MKE ZAIDI YA MMOJA)
Ndoa ya mke mmoja ndio muundo wa asili zaidi wa ndoa. Hali ya kumiliki kitu peke yako, au uhusiano ambao wewe tu ndio unashikilia nafasi hiyo na umiliki binafsi umejikita katika aina hii ya ndoa, japo umiliki huu ni tofauti na umiliki wa mali au utajiri. Katika mfumo huu mume na mke, kila mmoja huhisi hisia za moyoni na faida za ngono za mwenzake kuwa ni zake peke yake. Kinyume na ndoa ya mke mmoja ni ndoa ya mke zaidi ya mmoja (mitala) kwa wakati mmoja na Ukomonisti wa ngono. Jimai ya ngono, kimaana pia inaweza kuitwa mitala.
Ukomonisti wa ngono. Ujimai wa ngono maana yake hakuna kuwa peke yako. Kwa mujibu wa nadharia hii, hakuna mwanaume ambaye anapasa kuwa mali ya mwanamke mmoja tu wala mwanamke kuwa mali ya mume mmoja tu. Maana yake ni kupinga (kuikana) kuwepo maisha ya familia. Historia na nadharia zinazohusiana na zama za kale kabla ya kuanza kuandikwa kwa historia haionyeshi kipindi chochote ambapo mwanadamu hakuwa na familia na ambapo Ukomonisti wa ngono ulikuwa umestawi.
Kinachodaiwa kuwepo katika baadhi ya makabila ya kishenzi (yasiyo na ustaarabu na utamaduni) ilikuwa ni hali ya kati na kati, kati ya maisha ya familia (yaani kila mtu na mke wake au mume wake) na Ukomonisti wa ngono. Inasemekana kwamba katika baadhi ya makabila ilikuwa ni jambo la kawaida kwamba wavulana kadhaa kwa pamoja waliwaoa wasichana kadhaa, au wanaume kadhaa wa ukoo mmoja waliwaoa kwa ushirikiano wanawake kadhaa wa ukoo mwingine.
Will Durant katika kitabu chake, 'History of Culture' Jalada la 1, anaandika kwamba katika baadhi ya maeneo ndoa za ushirikiano zilikuwa mashuhuri kwa maana kuwa wanaume kadhaa wa ukoo mmoja walishirikiana kuwaoa wanawake kadhaa wa ukoo mwingine, kwa mfano imekuwa ni mila huko Tibet kwamba ndugu kadhaa wa kiume wana idadi sawa ya madada (ambao ni ndugu) kama wake zao. Kila kijana huingiliana na yeyote katika wale akina dada anayempenda.
Hapa kuna aina fulani ya Ukomonisti wa ngono. Mila kama hii ilipata kuwepo huko Uingereza enzi za kale. Mila ambayo ilikuwa maarufu miongoni mwa Wayahudi na makabila mengine ya zamani na ambapo kwa mujibu wa mila hiyo, baada ya kufa ndugu mmoja wa kiume, ndugu yake mwingine wa marehemu alimuoa mjane wake, ilikuwa ni masazo ya mila ya kale.
Maoni ya Plato Inaelekea kwamba wakati akiitangaza nadharia yake ya 'wanafalsafa watawala' Plato amependekeza katika kitabu cha 'The Republic,' aina fulani ya ujamaa wa kifamilia kwa tabaka hili. Viongozi kadhaa wa kikomunisti wa karne ya 19 pia walitoa pendekezo kama hilo, lakini kama ilivyoripotiwa na mwandishi wa kitabu, 'Freud and the Prohibition of consanguineuous marriage,' baada ya machungu mengi, dola nyingi za kikomunisti zenye nguvu, zilitangaza rasmi kuitambua sheria ya mke mmoja mume mmoja mwaka 1938. Kuwa na mume zaidi ya mmoja (polyandry).
Muundo mwingine wa mitala ni hali ya mke kuwa na mume zaidi ya mmoja (polyandry) kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Will Durant mila hii inapatikana miongoni mwa makabila fulani ya Tibet na kwingineko. Al-Bukhari katika mkusanyiko wake maarufu wa hadithi, as-Sahihi, anamripoti Aisha kuwa alisema kuwa miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu kulikuwa aina nne za mahusiano ya ngono.
Mojawapo ni ndoa sahihi ambayo bado ipo hadi sasa. Katika muundo huu mwanaume hutoa pendekezo kwa msichana kupitia kwa baba yake na baada ya kupanga mahari, humbeba mke wake. Hapawezi kuwa na utata juu ya watoto waliozaliwa katika ndoa hii. Kulikuwa na aina nyingine ya ndoa, ambayo ilikuwa ikiitwa Istibza. Ili kuzaa (kupata) kizazi kizuri, mume alimchagua mwanaume na kumuomba mke wake aingiliwe na huyo mwanaume kwa muda fulani.
Yeye mwenywe alijitenga na mke wake hadi mwanamke alipopata mimba. Ilikuwa ni ndoa ndani ya ndoa iliyofanywa ili kuboresha kizazi. Kwa mujibu wa mila nyingine, kundi la wanaume kumi au pungufu ya hapo, walishirikiana kufanya mapenzi na mwanamke mmoja. Baada ya kuwa mjamzito, mke aliwaita wote, na kwa mujibu wa mila ya enzi hizo, wote walipaswa kwenda. Hapo alimteua mwanaume mmoja kuwa baba wa mtoto wake na kuwaacha wale wengine ambao nao pia walikuwa tayari kukubali jukumu hilo. Mwanaume huyo baada ya kuchaguliwa, hakuwa na hiari ya kukubali au kukataa kuwa baba wa mtoto.
Aina ya nne ya mahusiano ya unyumba ni umalaya. Malaya walikuwa na bendera juu ya nyumba zao. Hii ilitumika kama alama ya kuwatambulisha. Mwanaume yeyote alikuwa anaweza kuwaingilia wanawake hawa. Mwanamke yule alipozaa, aliwaita wanaume wote waliomwingilia, na kwa msaada wa mtaalamu wa kutambua tabia kwa kuangalia uso, alimteua baba wa mtoto. Mwanaume mhusika alipaswa kukubali uamuzi wa mtaalamu huyu na kummiliki mtoto. Hizi ni aina za mahusiano ya kinyumba zilizokuwepo Arabuni kabla ya Uislamu. Mtume alizipiga marufuku zote na kubakiza moja iliyopo sasa.
Hii inaonyesha kuwa mila ya mke kuwa na mume zaidi ya mmoja ilikuwepo miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu pia. Montesquieu anaripoti kuwa Mwarabu mtembeaji wa dunia nzima, Abu Zahir al-Hassan, aliikuta mila hii China na India alipozitembelea nchi hizi katika karne ya 19 na aliichukulia kama aina ya ufisadi. Pia anaandika: "Katika Pwani ya Malabar kuna kabila liitwalo Nair.
Waume wa kabila hili hawawezi kuwa na mke zaidi ya mmoja lakini wanawake wanaruhusiwa kuchagua waume wengi. Labda sababu ni kuwa Wanair ni jamii ya wapiganaji na wawindaji. Kama tunavyowazuia kuoa askari wetu wa Ulaya ili ndoa isiingiliane na kazi zao za kupigana, makabila ya Malabar pia yameamua kuwa, wanaume wa Nair wajitahidi kadri wawezavyo kuepukana na majukumu ya familia.
Kutokuwa na hali na tabia ya kitropiki ya eneo hili, haiwezekani kuzuia ndoa kabisa, imeamuliwa kuwa wanaume wengi wawe na mke mmoja ili wasielemewe na majukumu ya kifamilia na hivyo kuathiri ufanisi wao." Kasoro za mke mmoja kuwa na waume zaidi ya mmoja. Kasoro kubwa na ya msingi ya mfumo huu wa mke kuwa na mume zaidi ya mmoja ni kuwa ukoo wa baba wa mtoto hubakia haujulikani kwa uhakika (yaani baba halisi wa mtoto huwa hajulikani). Katika mfumo huu uhusiano kati ya baba na mtoto haueleweki na hii ndio sababu mfumo huu hau jafanikiwa kama ilivyo Ukomonisti wa ngono haujaweza kujikita sehemu yeyote, mfumo huu pia haujakubalika katika jamii yoyote ya maana.
Kama tulivyosema awali, maisha ya familia, ujenzi wa nyumba (makazi) ya kizazi kijacho na muunganiko maalumu kati ya vizazi vya zamani na vijavyo ni moja ya mahitaji ya silika za binadamu. Kuwepo kwa mifano michache ya mke kuwa na waume wengi katika baadhi ya jamii hakuthibitishi kuwa uundaji wa familia sio silika ya mwanadamu. Halikadhalika utawa na useja kabisa (kuepuka kufanya tendo la ndoa), kama inavyofanywa na wanaume na wanawake kadhaa, pia ni aina ya upotofu. Mfumo huu si tu kwamba hauafikiani na asili ya mwanaume ya kuhodhi na upendo wake wa mfumo dume, bali pia unapingana na maumbile ya mwanamke pia. Uchunguzi wa kisaikolojia umebaini kuwa mwanamke anapenda zaidi kuwa na mume mmoja kuliko mwanaume anavyopenda kuwa na mke zaidi ya mmoja.
MITALA (MKE ZAIDI YA MMOJA)
Muundo mwingine wa mitala ni mtu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mfumo huu umezoeleka na kuwa na mafanikio zaidi kuliko ule wa mke kuwa na waume wengi na ujima wa ngono. Sio tu kwamba umekuwepo miongoni mwa makabila ya kishenzi, bali pia umetumiwa na watu wengi wastaarabu. Mbali na Waarabu, umetumiwa pia na Wayahudi, Wairani wa zama za Sasania na jamii nyinginezo.
Montesquieu anasema kuwa huko Malaya ilikuwa inaruhusiwa kuwa na wake watatu. Pia anasema kuwa mfalme wa Urumi, Valentinian II aliwaruhusu watu wake kuoa wake wengi, lakini kwa sababu sheria hii ilikuwa haiafikiani na hali ya hewa (tabia) ya Ulaya, ilifutwa na wafalme wengine kama Theodore n.k. Uislamu na mitala. Tofauti na ilivyokuwa kwa mfumo wa mke kuwa na mume zaidi ya mmoja, Uislamu haukukataza moja kwa moja ndoa ya mke zaidi ya mmoja (mitala). Badala yake uliweka idadi maalumu, pia umeweka masharti mengine pia na haukumruhusu kila mtu kujiingiza katika kuoa wake wengi.
Tutaeleza baadaye masharti yaliyowekwa na Uislamu na tutaeleza kwa nini Uislamu haukupiga marufuku ndoa za mitala moja kwa moja. Inashangaza kwamba katika zama za kati, ambapo propaganda za kuupinga Uislamu zilikuwa katika kilele chake, wapinzani wa Uislamu walikuwa wakisema kuwa ni Mtume wa Uislamu ambaye kwa mara ya kwanza alianzisha ndoa ya mitala. Walidai kuwa mila hii ilikuwa msingi wa Uislamu na kwamba kuenea kwa Uislamu kwa haraka haraka sehemu mbalimbali duniani kulitokana na mila hii. Wakati huo huo walidai kuwa mitala hii ilikuwa ndio sababu ya kuporomoka kwa watu wa Mashariki.
Will Durant katika kitabu chake "History of Culture" juz. 1, anasema kuwa mapadri na makasisi wa zama za kati waliamini kuwa ndoa za mitala zilianzishwa na Mtume wa Uislamu, ambapo sio kweli. Kama tunavyojua maisha ya ndoa katika jamii nyingi za kijima yalifuata utaratibu huu wa mitala. Kuna sababu nyingi za kuzuka kwa mfumo huu.
Katika jamii za kijima, sehemu kubwa ya wanaume walikuwa zaidi wakijishughulisha na uwindaji na upiganaji, hivyo kiwango chao cha vifo kilikuwa juu miongoni mwao. Kwa vile idadi ya wanawake ilizidi ya wanaume, hivyo ilikuwa ni lazima kutumia mfumo huu. Haikuwa inawezekana kuwaacha baadhi ya wanawake bila kuolewa, hasa ikizingatiwa kuwa, kwa vile idadi ya vifo katika jamii za kijima ilikuwa juu, kila mwanamke alitarajiwa kuzaa watoto.
Hapana shaka kwamba mfumo huu ulizifaa jamii hizo, sio tu kwa sababu ya uwingi wa wanawake kuliko wanaume, bali pia mfumo huu uliongeza idadi yao na kuwafanya kuwa na nguvu. Katika zama hizi wanaume wengi wenye nguvu na afya huchelewa kuoa na huzaa watoto kidogo tu. Lakini zamani wanaume wenye nguvu walikuwa na nafasi ya kuoa wake bora kabisa na walikuwa wakizaa idadi kubwa ya watoto. Hii ndio sababu desturi hii iliendelea kwa muda mrefu sana si tu miongoni mwa jamii za kijima bali hata katika jami zilizoendelea. Ni hivi karibuni tu kuwa pole pole desturi hii imeanza kutoweka katika nchi za Mashariki. Kilimo kimeimarisha maisha ya wanaume na kimepunguza ugumu wa taabu za kale, ambapo matokeo yake ni kuwa na idadi ya wanaume na wanawake imeanza kulingana.
Hivi sasa mitala imekuwa ni fahari ya kundi dogo la matajiri, hata katika jamii za kijima, na walio wengi wanalazimika kuridhika na mke mmoja, na kwa burudani ya ziada, wanaweza kujiingiza katika zinaa, kila inapowezekana. Gustav Leabeon katika kitabu chake, 'History of Culture' anasema kuwa hakuna mila isiyopendwa Ulaya kama ndoa za mitala, wala Ulaya haijaihukumu kimakosa mila nyingine yoyote kama ilivyofanya kwa ndoa hii.
Waandishi wa kizungu wameamini kuwa ndoa za mitala ni msingi wa Uislamu na ndio sababu kubwa ya kuenea kwake. Pia wanashikilia kuwa mila hii ndio sababu ya kuanguka kwa watu wa mashariki. Pingamizi nyingine mbali na hizi, zinazoonyesha huruma kwa wanawake wa Mashariki, zinadai kuwa wanawake hawa walionenepeana wanafungiwa ndani ya kuta nne za nyumba zao chini ya matowashi (wanaume waliohasiwa) wenye mioyo migumu.
Pia wanadai kuwa kosa dogo ambalo wanaweza kumuudhi mkuu wa familia linaweza kuwafanya waadhibiwe adhabu ya kifo. Fikra kama hizi hazina msingi wowote. Wazungu wasio na upendeleo wanapaswa kujua kuwa ni mila ya ndoa ya mitala ambayo imeyapa nguvu mahusiano ya kifamilia na kuinua maadili ya watu hawa. Ni kutokana na mila hii kwamba mwanamke wa Mashariki anaheshimika zaidi kuliko wa ulaya. Kabla ya kuthibitisha nukta hii, lazima tuweke wazi kuwa mila hii haihusiani na Uislamu.
Hata kabla ya Uislamu, mila hii ilikuwa inafuatwa na watu wa Mashariki wakiwamo Wayahudi, Wairani, Waarabu n.k. Watu waliosilimu huko Mashariki hawakunufaika na lolote katika mila hii. Juu ya hayo, hakuna dini yoyote yenye nguvu kama hii iliyobuni au kuzuia mila hii ya mitala. Mila hii haikuanzishwa na dini yoyote. Ilitokana na hali ya hewa na sababu nyingine zilizohusiana na mfumo wa maisha ya Mashariki. Hata Magharibi, ambako hali ya hewa haiendani na kuweko kwa desturi kama hiyo, lakini ndoa ya mke mmoja inapatikana katika vitabu vya sheria tu.
Katika maisha halisi hakuna dalili ya ndoa ya mke mmoja. Haifahamiki ni kwa namna gani mitala ya halali ya Mashariki ni ya hadhi ya chini kuliko ndoa za mitala ya siri za watu wa Magharibi. Watu wa mashariki, wanapotembelea nchi za Ulaya na kukumbana na shutuma kali za Wazungu dhidi ya mila zao hushangazwa na kuona wameonewa. Ni ukweli kwamba Uislamu haukuanzisha ndoa za mitala. Ulichokifanya ni kuidhibiti tu. Umepanga idadi ya mwisho. Umeweka masharti magumu juu yake.
Mila tayari ilikuwepo katika jamii nyingi ambazo zilikuja baadaye kusilimu. Walilazimika tu kufuata masharti yale yaliyowekwa na Uislamu. Katika kitabu chake 'Iran During the Sassanian Period,' Christenson ameandika: "Ndoa za mitala zilichukuliwa kuwa ni msingi wa familia. Kimsingi, idadi ya wake ambao mtu angependa kuwa nao ilitegemea na uwezo wake.
Watu maskini hawakuwa wanamudu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Mkuu wa familia alikuwa na haki maalum. Mmoja wa wake alichukuliwa kuwa ni mke kipenzi na alipata haki zote. Wake wengine waliwatendea kama wafanyakazi tu. Haki za kisheria kati ya makundi haya mawili zilitofautiana sana. Watumwa wa kike (masuria) walijumuishwa katika kundi la wake wafanyakazi. Haifahamiki ni wake vipenzi wangapi mume angeweza kuwa nao. Lakini limetajwa suala la wake wawili vipenzi katika maandishi ya kisheria.
Kila mmoja wao aliitwa malkia wa nyumba (mama mwenye nyumba). Waliishi katika nyumba tofauti. Mume alipaswa kumhudumia mke wake kipenzi katika maisha yake yote. Kila mtoto wa kiume hadi anapobalehe na kila mtoto wa kike hadi alipoolewa walikuwa na haki sawa. Lakini ni watoto wa kiume tu (wa wake wafanyakazi) walioingizwa katika ukoo wa baba." Katika kitabu, "Social History of Iran from tha fall of the Sassanians to the fall of Umayads", marehemu Sa'id Nafisi anaandika kuwa, "Idadi ya wanawake ambao mwanaume angeoa haikuwa na mpaka na wakati fulani inavyoonekana katika kumbukumbu za Kigiriki mwanaume alikuwa anaweza kuwa na mamia ya wanawake katika nyumba yake."
Montesquieu, akimnukuu mwanahistoria wa Kirumi, anasema kuwa wanafalsafa wengi wa Kirumi ambao walikuwa wanateswa na Wakristo kwa sababu walikataa kuwa wakristo walikimbia Roma na kwenda kwa Mfalme wa Iran, Khusro Parviz. Walishangazwa kuona kwamba huko si tu kwamba ndoa za mitala zilikuwa zinaruhusiwa bali pia wanaume wa Kifarsi walikuwa wakiingiliana na wake za watu wengine pia. Lazima ieleweke hapa kwamba wanafalsafa wa Kirumi walikimbilia kwenye kasri la Mfalme wa Iran, Anushirwan na sio kwenye kasiri la Khusro Parviz. Montesquieu amechanganya majina kutokana na kutoelewa vizuri. Kabla ya Uislamu, Waarabu walikuwa na uwezo wa kuwa na idadi isiyo na mipaka ya wake.
Ni Uislamu ulioweka mipaka. Hii bila shaka iliwasababishia usumbufu wale waliokuwa na wake zaidi ya wanne. Kuna baadhi walikuwa na wake kumi. Walilazimika kuwaacha sita. Kutokana na haya ni wazi kuwa si Uislamu ulioanzisha ndoa za mitala. Uislamu uliziwekea udhibiti tu. Hata hivyo haukuzipiga marufuku kabisa, katika sura zinazofuatia tutataja sababu zilizosababisha mila hii, na tutaelezea sababu ambazo zimewafanya wanaume na wanawake wa zama hizi walazimike kuipiga vita mila hii. Sababu za kihistoria za mitala.
Ni sababu zipi za kihistoria na kijamii zilizosababisha mitala? Kwa nini mataifa mengi ya ulimwengu, hasa mataifa ya mashariki yamekubali mila hii na kwa nini mataifa ya Magharibi, kamwe hayakupata kuitumia mila hii? Imekuwaje kwamba katika miundo mitatu ya mitala ni huu muundo mmoja tu wa mume kuwa na wake wengi ndio uliopata umaarufu? Mke kuwa na waume wengi na Ukomonisti wa ngono ama hazikupata kutumiwa kabisa, au zimetumika kidogo sana na katika maeneo machache sana. Mpaka tuyajadili maswali haya ndio tutaweza kulijadili suala la ndoa za mitala katika Uislamu na kwa mujibu wa mahitaji ya sasa ya mwanadamu.
Tusipoyatumia na kuyazingatia matokeo ya uchunguzi wa kijamii na kisaikolojia yaliyopatikana juu ya mada hii, sisi pia, kama walivyokuwa waandishi wengine wa juu juu, tunaweza kuangukia na kuanza kuimba nyimbo za zamani za kudai kuwa sababu za mitala ziko wazi. Yaani, mila hii imetokana na ukatili wa mwanaume na utawala wake kwa mwanamke. Ni matokeo ya mfumo dume.
Kwa kuwa mwanaume amemtawala mwanamke, ametunga sheria na mila ambazo zitamnufaisha yeye. Hivi ndivyo alivyoipa nguvu mila hii yenye manufaa kwake na madhara kwa mwanamke, na amekuwa akiitumia kwa karne nyingi. Mwanamke alikandamizwa, hakuweza kuutekeleza mfumo wa yeye kuwa na waume wengi. Na sasa muda wa uonevu wa mwanaume umekwisha, mila ya ndoa za mitala lazima iondoke kama ilivyokuwa kwa fursa nyingine za uongo ili kuleta haki sawa kwa wanaume na wanawake. Kufikiri kwa namna hii ni kwa kitoto na kwa juu juu sana.
Sababu ya mitala sio ukandamizaji wa mwanaume kwa mwanamke wala kushindwa kwa mfumo wa mke kuwa na waume wengi sio ukandamizaji wa mwanamke. Kama kivitendo mfumo huu umekufa, hii sio kwa sababu muda wa uonevu wa mwanaume umefikia kikomo. Mwanaume hajapoteza fursa yoyote, kimsingi amepata fursa juu ya mwanamke. Hatukatai kuwa ukandamizaji ni moja ya mambo yaliyobadilisha historia. Pia hatukatai kuwa katika kipindi chote cha historia mwanaume ameyatumia vibaya madaraka yake dhidi ya mwanamke. Lakini tunaamini kuwa ni mawazo finyu kuyaelezea mawazo ya kifamilia kwa kigezo cha dhulma peke yake.
Tukikubali mtazamo huu, lazima pia tukubali kuwa katika kipindi ambacho ndoa za mke kuwa na wanaume wengi zilikuwa maarufu miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu, au kama alivyoripoti Montesquieu, miongoni mwa Wanair katika pwani ya Malabar mwanamke alipata fursa ya kumtawala mwanaume na akawa anakaa na wanaume wengi. Lazima ikubaliwe pia kuwa kipindi hicho kilikuwa ni cha dhahabu kwa mwanamke.
Awali tulimnukuu Montesquieu akisema kuwa mila ya mke kuwa na waume wengi miongoni mwa Wanair haikutokana na utawala wa mwanamke au heshima aliyokuwa akipewa, bali ilikuwa ni uamuzi wa jamii wa kuwaepusha askari dhidi ya mzigo wa majukumu ya familia.
Aidha, kama Mfumo dume ndio ulisababisha mitala, kwa nini mfumo huu haukupata umaarufu Ulaya (Magharibi)? Hata hivyo, mfumo dume haukuwepo Mashariki peke yake. Je, watu wa Magharibi tokea awali wamekuwa Wakristo wachamungu wanaoamini juu ya usawa kati ya mwanaume na mwanamke? Je, kigezo cha kumiliki kimemnufaisha mwanaume wa mashariki na kukuza uadilifu huko Magharibi?
Mpaka kufikia nusu karne iliyopita mwanamke wa Magharibi alikuwa miongoni mwa wenye bahati mbaya kabisa duniani. Hata mali yake ilidhibitiwa na mume wake. Wazungu wenyewe wanakiri kuwa katika zama za kati, nafasi ya mwanamke wa mashariki ilikuwa bora sana ikilinganishwa na mwanamke wa Magharibi.
Gustav Leabeon anasema kuwa Uislamu, katika kipindi cha mwanzo kabisa, ulimpa mwanamke nafasi (hadhi) ambayo mwanamke wa kizungu alipata baada ya muda mrefu sana, yaani baada ya uungwana na ustaarabu wa Waarabu wa Andolusia kuingia Ulaya. Tabia njema kwa mwanamke ni sehemu kubwa ya uungwana ambao Wazungu walijifunza kutoka kwa Waislamu. Ilikuwa ni Uislamu (na sio dini ya Kikristo kama inavyoaminiwa na watu wengi wa kawaida), ulioinyanyua hadhi ya mwanamke. Katika zama za kati machifu wa makabila, licha ya kuwa Wakristo kamwe hawakumpa mwanamke heshima anayostahili.
Uchambuzi wa historia ya kale unaonyesha kuwa tabia ya 235 wafalme na viongozi wengine wa Ulaya ilikuwa ni ya kishenzi sana. Waandishi wengine wa Kizungu, pia wametoa maelezo kama haya kuhusiana na nafasi ya mwanamke katika zama za kati. Japo mfumo dume ulikuwa umeenea sana Ulaya katika kipindi hiki, bado ndoa za mitala hazikuweza kuwa ni desturi. Ukweli ni kuwa ni mfumo wa mke kuwa na waume wengi (popote ulikotumika) hautokani na utawala au nguvu ya mwanamke juu ya mwanaume wala kushindwa kwa mfumo huu hakukutokana na udhaifu wa mwanamke wala ukandamizaji wa mwanaume dhidi yake. Halikadhalika mitala katika nchi za Mashariki haikusababishwa na udikteta na uonevu wa mwanaume wala si kwamba haujaenea huko magharibi kwa sababu ya kuwepo usawa kati ya mwanaume na mwanamke.