24
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
KWA NINI KUNA WANAWAKE WENGI WA UMRI WA NDOA KULIKO WANAUME?
Ingawa idadi ya wasichana wanaozaliwa sio kubwa kuliko ile ya wavulana, lakini bado kuna idadi kubwa ya wanawake wengi wa umri wa kuolewa kuliko idadi ya wanaume. Sababu iko wazi. Kiasi cha vifo vya wanaume ni kikubwa. Vifo hutokea katika kipindi ambapo mwanamume alipaswa kwa kawaida kuwa mkuu wa familia. Tukizingatia vifo vinavyotokea katika ajali, vita, kufa majini, kuanguka, kugongana kwa magari n.k. tutakuta kwamba wengi wa waathirika ni wanaume. Ni mara chache sana kukutwa kwamba mwanamke ni moja wa waathirika. Iwe ni migongano (ajali) kati ya wanaadamu au kati ya mwanadamu na maumbile, wengi wa waathirika huwa ni wanaume watu wazima.
Ili kujua kwa nini idadi ya wanawake wanaopaswa kuolewa ni kubwa kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa, inatosha kufahamu kuwa tokea mwanzo wa historia ya mwanadamu hakuna hata siku moja ambayo imewahi kupita bila kupigana vita na wanaume kupoteza uhai. Vifo vinavyotokea kutokana na vita katika hizi zama za viwanda ni vingi mara mia kuliko vile vilivyokuwa vinatokea katika zama za uwindaji na zama za kilimo. Katika vita vya Pili vya Dunia, idadi ya vifo vilivyotokea inafikia milioni saba. Utakubaliana na sisi ukihesabu vifo vinavyotokea katika vita vya kimkoa huko Mashariki ya Mbali, Mashariki ya Kati na Afrika katika miongo miwili iliyopita.
Will Durant anasema kwamba sababu nyingi zimechangia kudondoka kwa mila hii ya mitala. Maisha thabiti ya kilimo yamepunguza ugumu na hatari za maisha ya wanaume, ambapo matokeo yake ni kuwa idadi za wanawake na wanume zinakaribia kulingana. Anachosema Will Durant kinashangaza sana. Kama ingekuwa kupotea kwa maisha ya watu kunatokana na mapambano ya wanaume dhidi ya muambile tu, kungekuwa kuna tofauti kati ya zama za uwindaji na zama za kilimo.
Lakini kadri muda unavyokwenda, vita vimeendelea kuchukua idadi kubwa zaidi ya uhai wa wanaume na idadi ya vifo vinavyotokana na vita haijapata kupungua katika zama zozote. Pia sababu kubwa kwa nini wanawake hawajakumbwa na ajali nyingi ni kwamba wakati wote wanaume wamekuwa wakiwalinda, na wao wanaume ndio wamekuwa wakifanya kazi za hatari zaidi. Hivyo kama ilivyokuwa katika zama za uwindaji, uwiano usio sawa wa idadi ya wanaume na wanawake umeendelea pia katika zama za kilimo. Will Durant hajasema lolote juu ya zama za viwanda, ingawa hiki ndio kipindi ambacho kimeshuhudia mauaji makubwa zaidi ya wanaume na kipindi ambacho uwiano kati ya idadi ya wanaume na wanawake umepishana mno.
MWANAMKE ANA UWEZO ZAIDI WA KUJIKINGA DHIDI YA MARADHI.
Imegunduliwa hivi karibuni kuwa mwanaume ana uwezo mdogo zaidi wa kujikinga dhidi ya maradhi kuliko wanawake. Hii ni sababu nyingine kwa nini idadi ya vifo vya wanaume ni kubwa zaidi. Miaka kadha iliyopita, Tume ya Takwimu ya Ufaransa iliripoti kuwa nchini Ufaransa, wavulana 105 huzaliwa dhidi ya wasichana 100 lakini cha ajabu idadi ya wanawake ilikuwa ni kubwa kuliko wanaume kwa 1,758,000 (milioni moja na laki saba na elfu hamsini na nane). Inaaminika kwamba tofauti hii inatokana na uwezo mkubwa wa mwanamke wa kujilinda dhidi ya magonjwa.
Si muda mrefu umepita, makala moja ilichapishwa kwenye jaria la UNESCO liitwalo Courier. Kwa mujibu wa makala hii, mwanamke ana uwezo mkubwa zaidi wa akili kuliko mwanamume. Wastani wa kinga yake ni kubwa zaidi. Kwa kawaida, ana afya nzuri zaidi kuliko mwanaume na ana uwezo zaidi wa kustahamili maradhi. Hupona haraka kuliko mwanaume. Katika kila mwanamke mmoja mwenye kigugumizi, kuna wanaume watano wenye kigugumizi. Katika kila mwanamke mmoja asiyeweza kutofautisha rangi, kuna wanaume kumi na sita wasioweza kutofautisha rangi. Na kwa kawaida ni ugonjwa wa wanaume tu. Wanawake wana mfumo bora zaidi wa kinga ya ajali.
Wakati wa vita vya Pili vya Dunia ilithibitika kuwa katika mazingira ya aina moja, mwanamke alikuwa na uwezo zaidi wa kustahamili ugumu wa vizuizi, magereza, na kambi za wafungwa wa vita kuliko wanaume. Takribani katika nchi zote, idadi ya kesi za wanaume kujinyonga ni kubwa mara tatu zaidi kuliko wanawake. Ashley Montague ameitaja nadharia yake ya uwezo mkubwa zaidi wa mwanamke kustahamili maradhi, katika kitabu chake kiitwacho, "Woman, the Superior Sex."
Ikiwa siku moja itatokea mwanaume ataamua kumpeleka mwanamke katika kazi za hatari na za kifo au kama atamsukumia katika uwanja wa vita kukabiliana na bunduki na mabomu, bado idadi ya wanawake itaendelea kuwa kubwa kwa sababu yeye ana uwezo zaidi wa kustahamili maradhi. Haya tuliyoyasema yanahusiana tu na uwingi wa wanawake wanaofaa kuolewa dhidi ya wanaume wanaofaa kuoa. Tunajua kwamba uwingi huu ni ukweli halisi. Pia tunajua sababu zake. Na sababu zake, zile zilizokuwepo tokea mwanzo wa historia ya mwanadamu bado zipo mpaka sasa.
HAKI YA MWANAMKE KATIKA MITALA
Nukta ya pili ni kuwa uwingi wa idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa sio tu kwamba hufanya haki kwa ajili yao, bali pia na wajibu kwa ajili ya mwanaume na mwanamke aliyeolewa. Hapana shaka kwamba ndoa ni moja ya haki za asili na ni moja ya haki za msingi za binadamu. Kila mtu awe mwanaume au mwanamke, ana haki ya kuishi maisha ya familia na kupata watoto. Haki hii ni sawa na haki ya kufanya kazi, kuwa na nyumba, kupata elimu na huduma za afya na haki ya kufurahia uhuru na usalama. Ni jukumu la jamii kuhakikisha kwamba hakuna kizuizi kinachowekwa katika upatikanaji wa haki ya asili na ya msingi ya binadamu. Badala yake, jamii inapaswa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha lengo hili.
Ni maoni yetu kuwa moja ya dosari kubwa za Amizio la Haki za Binadamu kwa wote ni kutoipa umuhimu wowote haki hii. Azimio limeitambua haki ya uhuru na usalama, haki ya kupata huduma bora za kimahakama, haki ya kuwa na uraia na kuubadili, haki ya kuoa au kuolewa bila vipingamizi vya rangi au dini, haki ya kumiliki mali, haki ya kukusanyika na haki ya kupumzika na kupumbaa, lakini azimio hili halijaitaja haki ya mtu kuishi maisha ya ndoa halali.
Kwa mwanamke, haki hii ni yenye umuhimu mkubwa sana, kwani anayahitaji maisha ya kifamilia zaidi kuliko mwanaume. Kwa mwanaume kilicho muhimu zaidi, katika ndoa ni ngono na kwa mwanamke kilicho muhimu zaidi ni hisia za moyoni na roho. Kama mwanaume hana familia, angalau anaweza kukidhi sehemu ya mahitaji yake kwa kujiingiza katika ngono holela na ufuska. Lakini kwa mwanamke, familia ina umuhimu mkubwa zaidi. Ufuska hauwezi kukidhi japo sehemu tu ya mahitaji yake ya kimwili na kimhemko (hisia ya moyoni).
Kwa mwanaume, haki ya kuwa na familia ina maana kukidhi tamaa zake za ngono, haki ya kuwa na mwenzi maishani na haki ya kuwa na watoto halali. Lakini kwa mwanamke, ndoa inamaanisha pia kuwa na mlinzi na mwangalizi na ambaye anaweza kumpa msaada wa kimaadili. Baada ya kuzielezea nukta hizi mbili, kwamba kwanza idadi ya wanawake wanaofaa kuolewa ni wengi kuliko idadi ya wanaume wanaofaa kuoa, na pili kwamba ni haki ya asili ya binadamu kuwa na familia, ni rahisi kutoa hitimisho kwamba ikiwa ndoa ya mume kuwa na mke mmoja itafanywa kuwa ndio ndoa pekee iliyo halali, idadi kubwa ya wanawake itakuwa katika hatari ya kunyimwa haki yao ya asili, na hivyo ni ndoa za mitala tu ndio zinaweza kuwarejeshea wanawake hao haki hii iliyo hatarini.
Ni jukumu la wanawake wa Kiislamu, kwamba kama njia ya kutetea haki za wanawake, waitake na kuishinikiza tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kuutambua rasmi mfumo wa ndoa za Kiislamu wa kuwa na wake wengi kama haki ya binadamu, na hii itakuwa ni neema kubwa kwa mwanamke na maadili. Ukweli kwamba kanuni hii imetoka Mashariki na nchi za Magharibi zinapaswa kufuata usionekane kuwa ni dhambi.
NADHARIA YA RUSSEL
Kama ilivyoonyeshwa hapo awali, Bertrand Russel alikuwa anaufahamu ukweli kwamba ndoa za kuoa mke mmoja kufanywa kuwa ndio ndoa pekee zilizo halali kungewanyima wanawake wengi haki ya kuolewa. Amependekeza suluhisho rahisi sana la tatizo hili. Alitaka wanawake waruhusiwe kuwashawishi wanaume na kuzaa watoto wasio na baba. Kama ambavyo baba huwa anasaidia katika matunzo ya watoto, serikali inapaswa kuchukua nafasi ya baba na watoe ruzuku kwa wanawake ambao hawajaolewa.
Russell anasema kwamba hivi sasa nchini Uingereza kuna zaidi ya wanawake milioni mbili waliozidi idadi ya wanaume ambao kamwe hawatarajii kuolewa na kupata watoto kutokana na sheria iliyopo inayotaka mwanaume awe na mke mmoja tu. Hii ni dhulma kubwa. Anasema kwamba mfumo wa mume mmoja mke mmoja umejengwa juu dhana kwamba idadi ya wanaume inalingana na idadi ya wanawake, lakini pindi idadi hizi hazilingani, hawa wanawake waliozidi huwa hatarini kubakia bila kuolewa katika umri wao wote. Aidha, ikitokea haja ya kuongeza, idadi ya watu, aina hii ya ndoa sio tu kwamba haina maslahi na umma, achilia mbali maslahi ya mtu mmoja mmoja. Hili ni suluhisho la tatizo hili la kijamii, kama lilivyopendekezwa na mwanafalsafa mkubwa wa karne ya 20.
Lakini kwa mujibu wa Uislamu, tatizo lote hutatuliwa ikiwa idadi ya kutosha ya wanaume wenye uwezo wa kifedha, wa kimaadili na kimwili watakubali kuoa mke zaidi ya mmoja na kuwatendea uadilifu na kutoonyesha upendeleo baina ya watoto wa wake hawa wawili. Mke wa kwanza anapaswa kumpokea na kumkubali kwa ukunjufu mke wa pili kwa nia na lengo la kutekeleza jukumu la kijamii ambalo ni muhimu sana na ni namna bora ya maadili.
Kinyume na kifra za Uislamu, mwanafalsafa huyu anawashauri wanawake walionyimwa haki ya kuolewa, wawaibe waume wa wanawake wengine na anatoa wito kwa serikali kuwasaidia na kuwatunza watoto hawa waliozaliwa katika mahusiano haramu. Inaonekana kwamba mwanafalsafa huyu wa karne ya 20 anadhani kuwa mwanamke anahitaji ndoa kwa sabau tatu: kukidhi tamaa zake za ngono, kupata watoto na kukidhi mahitaji yake ya kiuchumi. Haja mbili za mwanzo zinaweza kukidhiwa kwa ulaghai na haja ya tatu itekelezwe na serikali. Anasahau kwamba mwanamke ana haja za hisia za moyoni pia. Anataka awe chini ya uangalizi wa mume anayempenda na kwamba mkataba wake na mwanaume huyo usiwe ni wa kingono peke yake. Nukta nyingine ambayo mwanafalsafa huyu hajaipa umuhimu ni hadhi ya watoto walioza liwa katika mahusiano haramu.
Kila mtoto huhitaji wazazi wanaoeleweka vizuri na upendo wao wa dhati. Uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi mwanamke huwa haonyeshi upendo kwa mtoto wake ambaye baba yake hajulikani. Ni vipi ukosefu wa upendo huu unaweza kufidiwa? Je serikali inaweza kufanya chochote katika hili? Bertrand Russell anasikitika kwamba wanawake wengi watabaki bila watoto mpaka pendekezo lake lipewe sura ya kisheria. Lakini anapaswa kujua kuwa wanawake wa kiingereza hawawezi wakasubiri sheria yoyote. Wao wenyewe tayari wameshatatua tatizo hili, wanaiba waume za watu na wanapata watoto wasio na baba.
Katika ripoti ya mwaka ya 1958, iliyoandaliwa na Dr. Z.A. Scott, Mkuu wa Idara ya Utabibu ya Halmashauri ya London, ilionekana kwamba katika watoto kumi waliozaliwa mwaka uliopita, mtoto mmoja ni wa nje ya ndoa. Ripoti hiyo pia ilisema kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa inazidi kuongezeka. Idadi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa ilipaa kutoka watoto 33,838 mwaka 1957 hadi 54,433 katika mwaka uliofuata. Inaonekana kwamba Waingereza wameamua kutatua tatizo lao bila kuwa na haja ya kusubiri kupitishwa kwa pendekezo la Bertrand Russell kuwa sheria.