2
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
I- UISLAMU NA MAISHA YA KISASA
Suala la dini na maisha ya kisasa ni moja ya mambo ambayo hayawagusi Waislamu peke yao. Dini nyingine pia zilikumbana na tatizo hili. Watu wengi wenye kupendelea mabadiliko duniani, wameikana dini kwa sababu wanaamini kuwa dini na maisha ya sasa haviendi pamoja. Wanafikiri kuwa kudumaa, kutuama na kutobadilika ni sifa za lazima za mtu mshika dini. Kwa maneno mengine, wanafikiri kuwa kudumaa na ukinaifu unatokana na kutokuwepo kwa mabadiliko na kwamba kudumisha hali ya kizamani ndio tabia za dini.
Marehemu Bwana Nehru aliyekuwa waziri Mkuu wa India alikuwa na mawazo ya kisekula na hakuwa akiamini dini yoyote. Inaoinekana kutokana na kauli zake kuwa kilichomfanya asipende dini ni kutobadilika kwake na ukinaifu unaotokana na kutokuwepo kwa mabadiliko. Kuelekea kipindi cha mwisho cha maisha yake Nehru alihisi kuwa na uwazi moyoni mwake na aliamini kuwa uwazi ule ungezibwa na nguvu ya kiroho tu.
Lakini hakuelekea kuiamini dini yoyote kwa sababu aliamini kuwa hali ya ukinaifu na kutokuwepo kwa mabadiliko ilikuwepo katika dini zote. Mwandishi wa habari wa Kihindi, aitwaye Karanjia, alimhoji Nehru katika kipindi chake cha mwisho mwisho cha uhai wake (Nehru) na alivyoonekana haya yalikuwa ni mahojiano ya mwisho ambapo Nehru alitoa maoni yake juu ya matatizo ya jumla ya ulimwengu.
Alipokuwa akimzungumzia Gandhi, Karanjia alisema, "Baadhi ya wanaopendelea mabadiliko (liberals) na maendeleo wanaamini kuwa Gandhiji, kwa kupitia na kwa kutokana na utatuzi wake wa matatizo kwa hisia kali, unyofu na njia za kiroho, zimedhoofisha na kuitia ubaridi imani yako ya asili ya ujamaa wa kisayansi." Katika kulijibu hili, Nehru alisema; "Ni muhimu na vizuri kutumia fursa ya njia za kimaadili na kiroho.
Mara zote nimekubaliana na Gandhiji juu ya hili. Ninaamini kuwa ni muhimu zaidi kutumia fursa ya njia hizi, kwani sasa, kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma, tunahitaji majibu ya kiroho na kimaadili juu ya maswali yanayotokana na pengo la kimaadili linalosababishwa na tamaduni za kisasa, ambazo zinazidi kuwa maarufu." Kisha Kiranjia aliuliza swali juu ya Ukomunisti.
Nehru alikiri mapungufu yake na katika majibu yake alionyesha baadhi ya mapungufu na ubovu wake (wa ukomunisti). Kwa mara nyingine tena alipendekeza suluhisho la kiroho juu ya matatizo ya dunia. Alipofika hapa Karanjia akasema; "Bwana Nehru, je dhana yako ya utatuzi wa matatizo ya kimaadili na kiroho haikufanyi uwe tofauti na Jawahanal wa jana? (Nehru mwenyewe enzi za ujana wake).
Ulichokisema kinaonyesha kuwa Bwana Nehru, katika kuelekea mwisho wa uhai wake, ameanza kumtafuta Mungu." Nehru alisema; "Ndiyo, nimebadilika. Msisitizo wangu juu ya unyofu na maadili ya kiroho na utatuzi wa matatizo sio wa bahati mbaya." Akaongeza kuwa; "Swali sasa ni jinsi ya kukuza maadili na imani ya kiroho katika daraja la juu zaidi.
Hapana shaka kwamba kwa ajili ya hili, dini zipo, lakini kwa bahati mbaya zimechukua mtazamo finyu na matendo yasiyobadilika na zimebaki kuwa taratibu rasmi lakini duni. Ni umbo lake la nje tu lililobaki, lakini ari na dhana yake ya kweli imetoweka." Uislamu na mahitaji ya wakati. Katika dini zote ni Uislamu tu unaojihusisha zaidi na vipengele vyote vya maisha ya mwanadamu.
Mafundisho yake hayajajikita katika matendo ya ibada na sala na mfumo wa ushauri wa maadili peke yake. Uislamu, kama ulivyoshughulikia uhusiano wa watu na Mwenyezi Mungu, ndivyo hivyohivyo ulivyoshughulikia mahusiano baina ya watu. Katika sura mbali mbali Uislamu umeshughulikia haki za watu binafsi na majukumu yao pia.
Hii ndio sababu swali kwamba mafundisho yake yanafaa kutumika au la katika mazingira yanayozidi kubadilika ni thabiti zaidi katika suala la Uislamu kuliko dini nyingine yoyote. Kwa bahati imetokea kwamba, wasomi wengi na waandishi wasiokuwa Waislamu wamezisoma sheria za kijamii na kiraia (za madai na za jinai) na wamezisifu kuwa ni chombo cha kisheria cha kimaendeleo na endelevu.
Wameusifu Uislamu kwa mapana na marefu, kuwa ni dini hai na itakayodumu milele, na wameuelezea uwezo na sifa za sheria hizi za Kiislamu wa kuweza kutumika nyakati zote na katika hali zote. Mwandishi maarufu sana wa Kiingereza aliyekuwa akipendelea msimamo wa wastani (liberal), Bernard Shaw amesema; "Mara zote nimekuwa nikiipa dini ya Muhammad heshima kubwa (daraja kubwa), kutokana na uhai wake wa ajabu.
Ni dini pekee inayoonekana kwangu kuwa na uwezo wa kunyumbulika na hivyo kuweza kutumika katika dunia inayobadilika na katika zama zote. Nimetabiri kuwa imani ya Muhammad itakubaliwa na Ulaya ya kesho, na dalili za hili zinajionyesha hata sasa. Makasisi wa zama za kati aidha kwa sababu ya ujinga au kwa sababu ya kung'ang'ania bila hoja imani zao waliupaka Uislamu rangi mbaya kabisa. Kwa kusema kweli walifundishwa kumchukia mtu huyu, Muhammad na dini yake. Kwao Muhammad alikuwa mpinga Kristo.
Mimi nimemsoma, mtu huyu wa ajabu, na kwa maoni yangu hakuwa mpinga Kristo kabisa na lazima aitwe mkombozi wa wanaadamu. Ninaamini kuwa kama mtu kama yeye angetwaa madaraka /uongozi wa dunia ya sasa angefanikiwa kutatua matatizo katika namna ambayo ingeleta amani na furaha, vitu ambavyo vinahitajika sana kwa sasa. Dr. Shibli Shama'il ni myakinifu wa Kiarabu wa Lebanoni. Kwa mara ya kwanza alitafsiri kitabu cha 'Darwin Kiitwacho 'Origin of Species' kwenda katika lugha ya Kiarabu, pamoja na sharhe ya mwanasayansi wa kijerumani aitwaye Boucher katika kitabu hicho akakipa jina la 'A weapon against religious belief.' ('Silaha dhidi ya imani za kidini.') Ingawa hamwamini Mwenyezi Mungu, haoni aibu kuusifu Uislamu na muasisi wake mtukuka. Ameusifu Uislamu kwa kusema kuwa ni dini hai inayoweza kutumika katika zama zote.
Mtu huyu, katika juzuu ya pili ya kitabu chake kiitwacho, 'Philosophy of Evolution' ambacho amekichapisha kwa Kiarabu, ameandika makala yenye kichwa cha cha habari 'Uislamu na Ustaarabu'. Ameandika makala hii kukanusha madai ya wasio Waislamu kwa kutoa madai kuwa Uislamu ndio uliosababisha kuporomoka kwa hali ya Waislamu. Shibli Shama'il amejaribu kuthibitisha kuwa jambo hasa lililosababisha kuporomoka kwa hali za Waislamu ni wao Waislamu kuyaacha (kuacha kutekeleza) mafundisho ya kijamii ya Uislamu.
Wale wazungu wanaoushambulia Uislamu aidha hawajui au wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kuwafanya watu wa Mashariki (Asia) wazitilie shaka sheria zao na mfumo wao ili kuwafanya wafuate mfumo wa Kimagharibi. Wakati wa zama zetu, suala la iwapo Uislamu unaafikiana na hali halisi ya maisha ya sasa au la limekuwa likiulizwa sana. Tunapata picha ya ndani ya watu hasa wale wanaotoka katika tabaka la wasomi na tunakuta kuwa swali hili linaulizwa zaidi kuliko maswali mengine.
PINGAMIZI
Wakati fulani watu hawa wanatoa hoja za kifalsafa juu ya suala hili kuwa vitu vyote hapa duniani lazima vibadilike. Hakuna kinachobaki vile vile bila kubadilika, na halikadhalika binadamu wanabadilika. Sasa inawezekanaje sheria za Kiislamu zibaki hivyo bila kubadilika kwa zama nenda rudi? Kama tukilitazama swala hili kwa mtazamo wa kifalsafa kabisa, jibu ni rahisi.
Ni vitu (maada) vinavyobadilika kila mara, ambavyo hukua na kuporomoka na ambavyo hupasika katika kugeuka na kuoza. Lakini sheria za ulimwengu hazibadiliki. Kwa mfano, viumbe vyote hai vimegeuka na vimeendelea kugeuka kwa mujibu wa utaratibu na kanuni fulani zilizoelezwa na wanasayansi. Hapana shaka kwamba viumbe hivi vinageuka na kubadilika lakini kanuni zinazotawala mabadiliko haya hazibadiliki. Na sasa tunazungumzia kanuni (sheria) hizi.
Katika hili, hakuna tofauti yoyote iwapo sheria hizi ni za asili au zimetungwa na kukusanywa, kwani inawezekana kwamba sheria ambazo zimetungwa zinaweza kuwa na asili kama chanzo chao na kuafikiana na mchakato wa mabadiliko ya mtu mmoja mmoja na halikadhalika jamii ya wanadamu kwa ujumla.
Hata hivyo, swali kuhusiana na kuafikina au kutoafikiana kwa Uislamu na mahitaji ya muda halina sura ya kiujumla na kifalsafa peke yake. Swali ambalo huulizwa zaidi ni kuwa kwa vile sheria huundwa kukidhi mahitaji ya wanaadamu na mahitaji yenyewe yanabadilika kila mara inawezekanaje sheria hizo za kijamii zibaki hivyo hivyo bila kubadilika? Ni swali zuri.
Na imetokea kuwa tabia za kimiujiza za Uislamu zimewezesha sheria zisizohitaji kubadilishwa kukidhi mahitaji yasiyobadilika ya mtu mmoja na jamii na sheria zinazobadilika badilika kwa mahitaji ya muda mfupi na yanayobadilika. Hii ni sifa ya kipekee ambayo Waislamu wote wajuzi wa mambo ya sheria za kiislamu na waliozisoma sheria zake wanajivunia. Tutalielezea hili vizuri zaidi baadaye. Je mabadiliko ya kijamii yanakwenda na wakati? Kabla ya kuliendea swali hili tungependa kuibua nukta mbili. Nukta ya kwanza ni kuwa watu wengi wanaoongelea maendeleo na mabadiliko ya hali wanadhani kuwa mabadiliko yoyote ya kijamii, hasa kama yametokea nchi za Kimagharibi, basi ni matokeo ya maendeleo.
Hili ni moja ya mawazo potofu liliyoendekezwa na kizazi hiki. Watu wanadhani kuwa kwa vile njia za maisha hubadilika siku hadi siku, zilizo duni hubadilishwa kwa zilizo bora zaidi na sayansi na viwanda vinaboreka kila siku, mabadiliko yote katika maisha ya binadamu ni aina ya maendeleo na kwa hiyo yanafaa kukaribishwa na kupokelewa kwa mikono miwili. Wanafikiri pia kuwa mabadiliko haya hayaepukiki na huja baada ya muda fulani.
Kwa kusema kweli sio kwamba mabadiliko yote ni matokeo ya maendeleo ya sayansi na viwanda wala sio kwamba hayaepukiki. Huku sayansi ikiendelea kukua, asili ya ubinafsi na unyama wa mwanadamu nayo hubaki bila kubadilika. Ujuzi (elimu) na busara humpeleka mtu katika ukamilifu na asili ya unyama wa mwanadamu humsukumia kwenye ufisadi na upotofu.
Asili ya unyama wa mwanadamu mara zote hujaribu kutumia ujuzi kama njia ya kupatia matamanio yake. Kwa kadiri muda unavyokwenda, kwa kadiri maendeleo na mabadiliko yanavyotokea, ufisadi na upotofu ndivyo unavyozidi kukua na kukomaa. Tunapaswa kwenda na wakati lakini wakati huo huo lazima tupige vita ufisadi pia. Mleta mabadiliko (mema) na mpinga mabadiliko (mema) wote wanapigana dhidi ya muda, tofauti yake ni kuwa mleta mabadiliko mema hupigana dhidi ya upotofu unaoletwa na mabadiliko ya muda na mpinga maendeleo (mabadiliko) hupigana dhidi ya mabadiliko (maendeleo halisi) yanayoletwa na mabadiliko ya muda.
Kama tunauchukulia muda na mabadiliiko yake kama kigezo cha mema yoyote na maovu yote, sasa ni kigezo gani cha kuupimia muda wenyewe? Kama kila kitu kitakwenda na wakati sasa je wakati wenyewe unapaswa kwenda na nini? Kama mwanadamu ataufuata muda na mabadiliko yake kwa utii mkubwa, sasa nini kitafanyika juu ya majukumu na nafasi ya utashi wa mwanadamu? Mwanadamu anaendesha gari la wakati, ambalo liko kwenye mwendo.
Lazima awe mwangalifu na aliongoze vyema gari lake. Vinginevyo atakuwa kama mtu aliyepanda farasi na akamwachia farasi wake aende popote atakapo. marekebisho au kuondoa kabisa? Nukta ya pili inayofaa kutajwa hapa ni kwamba baadhi ya watu wamelitatua tatizo gumu la Uislamu na mahitaji ya wakati kwa namna rahisi sana.
Wanasema kuwa Uislamu ni dini ya milele, na inaweza kurekebishwa ili kuafikiana na mahitaji ya kila zama na wakati. Lakini wanapoulizwa marekebisho haya yanafanyikaje na kanuni yake ni nini, mara moja wanasema kuwa hali ya maisha inapobadilika, sheria zilizopo hubatilishwa na kuwekwa nyingine. Wanatoa hoja kuwa sheria za msimu (muda mfupi) za kidini lazima ziwe na uwezo wa kurekebishwa na ziafikiane na maendeleo ya elimu na sayansi pamoja na kupanuka kwa utamaduni na ustaarabu. Kwa mujibu wao, uwezo huo wa sheria wa kuweza kurekebishwa ili kuafikiana na mahitaji ya wakati haupingani na Uislamu na sio kinyume na mafundisho yake.
Wanadai kuwa, kwa vile mahitaji ya wakati yanabadilika kila mara, basi kila zama huhitaji sheria mpya. Wanaendelea kudai kuwa sheria za kiraia na kijamii za Uislamu zinaafikiana na maisha rahisi ya Waarabu waliokuwa wakiishi kabla ya Uislamu, na ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa ni kwa mujibu wa mila na desturi zao.
Sasa kwa kuwa haziafikiani na maisha ya zama hizi zinatakiwa ziondolewe na ziwekwe nyingine mpya za kisasa. Watu hawa wanapaswa kuulizwa: Kama uwezo wa sheria kuweza kurekebishwa maana yake ni uwezo wa kubatilishwa na kufutwa, basi ni sheria gani ambayo haina sifa hii? Kuna sheria basi yeyote ambayo haiendi na wakati kwa mtazamo huu?
Tafsiri hii ya uwezo wa sheria kurekebishwa na kuweza kutumika katika zama zote ni sawa na kusema kuwa vitabu vyote na maktaba ndio njia bora kabisa za kufurahia maisha kwa sababu muda wowote mtu atakapotaka starehe, anaweza kuviuza na kutumia fedha zitakazopatikana kwa ajili ya kukidhi matamanio yake. Mwandishi wa Kiirani anasema kuwa mafundisho ya Uislamu yamegawanyika katika sehemu tatu.
Sehemu ya kwanza ina imani za msingi kama vile tauhidi (imani kuwa Mungu ni mmoja tu), Utume, Ufufuo n.k. Sehemu ya pili inahusiana na matendo ya ibada kama vile sala, saumu, udhu, tohara, hija n.k sehemu ya tatu ina sheria zinazohusiana na maisha ya watu. Kwa mujibu wake yeye ni sehemu mbili tu za mwanzo ambazo ni za lazima katika dini na ambazo zinafaa kuhifadhiwa milele.
Lakini sehemu ya tatu sio sehemu ya lazima ya dini kwa kuwa dini haihusiani na maisha ya kila siku ya watu. Mtukufu Mtume mwenyewe hakuamuru kuwa sheria hizi ziwe sehemu ya dini kwa vile hazikuhusiana na ujumbe wake yeye kama Mtume. Ilitokea tu kwamba akawa ni mkuu wa Dola, kwa hiyo akalazimika kuweka sheria pia. Vinginevyo dini haina lolote la kulazimisha katika maisha ya kidunia ya watu. Ni vigumu kuamini kuwa mtu anayeishi katika nchi ya Kiislamu anaweza kuwa mjinga wa mafundisho ya Uislamu kiasi hiki. Je, Qur'ani haijaelezea lengo la kuleta Mitume na Manabii? Je, Qur'ani haisemi wazi wazi kuwa:
(Suratul Hadidi; 57:25). 35 Qur'ani imeuelezea uadilifu katika jamii kama lengo kuu la Mitume wote.
Kama unataka unaweza usiyafuate mafundisho ya Qur'ani, lakini kwa nini unatenda dhambi kubwa zaidi kwa kuusingizia na kuuzushia Uislamu na Qur'ani? Bahati yetu mbaya zaidi inatokana na ukweli kwamba maadili yetu na sheria vimepoteza chanzo pekee cha nguvu yake, yaani dini. Ni katika nusu karne tu tulipoanza kusikia watu wakipiga kelele kuwa Uislamu ni mzuri, ili muradi tu ubakie ndani ya majumba ya ibada, na usishughulike na jamii.
Kelele hii imepigwa kutoka ndani ya mipaka ya nchi za Waislamu na imeenezwa katika ulimwengu wote wa Kiislamu. Ili kuliweka lengo la kelele hizi wazi tunaweza kusema kuwa nia ni kuufanya Uislamu ubaki kuwa ni kikwazo cha kuzuia kuenea kwa ukomunisti lakini kama huu huu Uislamu utagongana na maslahi ya Magharibi basi upingwe vikali.
Kwa mtazamo wa watu wa Magharibi, matendo ya Uislamu lazima yaendelee, ili pindi ikitokea haja, Waislamu wahamasishwe kuupinga mfumo wa kikomunisti ambao hauamini mambo ya dini na Mungu, lakini sheria za kijamii za Uislamu ambazo zinatoa falsafa ya maisha ya Uislamu lazima ziondoshwe, kwa vile sheria hizi huwapa Waislamu uhuru fulani na kuwafanya wawe watu tofauti wanaojitegemea katika mfumo wao, jambo ambalo litawazuia kumezwa na nchi za Magharibi zenye tamaa kali. Kwa bahati mbaya, watetezi wa hoja kuwa Uislamu haujihusishi na maisha ya kila siku ya watu, wamesahau baadhi ya ukweli wa msingi. Awali miaka 1400 iliyopita, Uislamu ulipinga kanuni kuwa tunaamini baadhi ya mambo (baadhi ya mafundisho ya Uislamu) na tunayakataa mengine, na ukatamka kuwa kanuni na sheria za Uislamu hazibadiliki.
Pili tunaamini kuwa muda umefika ambapo Waislamu hawapaswi kupotoshwa na mbiu za uongo. Watu sasa pole pole wameanza kuamka na wameanza kutofautisha kati ya maendeleo ambayo ni matokeo ya kuchanua kwa vipaji vya kisayansi na kiakili, na kudhihiri kwa ufisadi na upotofu, kutoka nchi za Magharibi. Watu wa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa, kuliko kipindi kingine chochote, wameanza kufahamu thamani ya mafundisho ya Uislamu na wametambua kuwa wanaweza tu kuishi maisha huru kwa kuyafuata. Hawatayaacha, kwa gharama yoyote.
Waislamu makini wanafahamu kuwa propaganda dhidi ya sheria za kiislamu si chochote bali udanganyifu wa mabepari. Tatu, watetezi wa hoja hii wanapaswa kujua kuwa Uislamu unapokuwa na nguvu, hushinda mifumo mingine yote, iwe ya kikafiri au vinginevyo. Uislamu unataka kutawala maisha ya jamii kama falsafa ya maisha, na hautaki kubakia misikitini tu na sehemu nyingine za ibada. Uislamu ambao utabakia kwenye nyumba za ibada, utaacha nafasi kwa ajili ya mawazo ya Kimagharibi na halikadhalika mawazo yanayopingana na umagharibi na itikadi zake. Adhabu ambazo nchi za magharini zinatumikia, katika baadhi ya nchi za Waislamu ni matokeo ya kutoujua ukweli huu.