HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU15%

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU Mwandishi:
: AZIZI NJOZI
Kundi: Wanawake

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
  • Anza
  • Iliyopita
  • 33 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 48284 / Pakua: 5928
Kiwango Kiwango Kiwango
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

5

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

MWANAMKE KATIKA QUR'ANI

Sasa tunataka kujibu swali iwapo Uislamu unamtazama mwanamke kuwa ni sawa na mwanaume kama binadamu au unamuona ni wa hadhi ya chini kuliko mwanaume. Falsafa maalum ya Uislamu juu ya haki za kifamilia. Kuhusiana na haki za mwanaume na mwanamke, Uislamu, una falsafa yake maalum ambayo ni tofauti, yale yaliyotokea miaka 1400 iliyopita na yanayotokea hivi sasa. Uislamu hauamini kuwa katika mambo yote mwanaume na mwanamke wana haki na majukumu yanayofanana.

Katika mambo fulani haki na majukumu yao ni tofauti na matokeo yake ni kuwa katika baadhi ya mambo nafasi yao inafanana na ya wanaume na katika baadhi ya mambo haifanani na ya wanaume. Hii sio kwa sababu Uislamu, kama falsafa nyingine, unamtazama mwanamke kwa dharau au jinsia yake sio bora kama ya mwanaume.

Uislamu unazitofautisha jinsia hizi mbili kwa sababu nyinginezo za msingi. Unaweza kuwasikia wafuasi wa mifumo ya Kimagharibi wakitaja kanuni za Kiislamu kama vile mahari, matunzo, talaka, ndoa za mitala na mengineyo, kuwa haya yote ni kama matusi kwa mwanamke na yanashusha hadhi yake. Wanawapotosha watu kuwa sheria na kanuni hizi hazina maana na ulazima na zinamfanya mwanaume aonekane ni bwana mkubwa. Wanasema kwamba katika kipindi chote cha historia, kabla ya karne ya 20, sheria na kanuni zote duniani ziliwekwa kwa kuzingatia kuwa mwanaume ni mwenye jinsia bora zaidi na kwamba mwanamke aliumbwa kwa maslahi na starehe ya mwanaume. Sheria zilizopitishwa na Uislamu pia ziko hivyo hivyo, zinampendelea mwanaume.

Wanadai kuwa Uislamu ni dini ya jinsia ya kiume. Hawamtambui mwanamke kuwa ni binadamu kamili. Hii ndio sababu haujampa haki sawa na mwanaume. Ungekuwa unamtambua kuwa ni binadamu kamili usingeruhusu ndoa za mitala (mke zaidi ya mmoja), usingehesabu ushahidi wa wanawake wawili kuwa ni sawa na wa mwanaume mmoja, usingeamuru gawio la mwanamke liwe nusu ya gawio la mwanaume, usingeamrisha papangwe bei ya mwanamke chini ya kivuli cha mahari na usingemfanya mwanamke awe tegemezi kwa mwanaume kwa upande wa matunzo, badala ya kufanya ajitegemee kiuchumi na kijamii.

Kwa kuzingatia yote haya ni dhahiri kuwa mafundisho ya Uislamu yanamtazama mwanamke kwa jicho la dharau. Uislamu unadai kuwa dini ya usawa lakini, katika mahusiano ya kifamilia hakuna usawa wowote uliozingatiwa. Wanashikilia kuwa katika suala la haki, Uislamu wazi wazi unampendelea mwanaume na ndio maana umempa miliki zote hizi. Tukipenda tunaweza kuweka hoja yao katika muundo wa kimantiki kuwa: Kama Uislamu unamhesabu mwanamke kuwa ni binadamu kamili ungekuwa umempa haki sawa na zinazofanana na zile za mwanaume, maadamu haujafanya hivyo basi haumhesabu kuwa ni binadamu kamili.

Usawa au kufanana? Hoja hii imejengwa juu ya msingi kwamba kwa vile heshima ya binaadamu ni sawa kwa mwanaume na mwanamke, hivyo lazima wote wapate haki zinazofanana bila kujali majukumu yao katika maisha. Hapana shaka, utu na heshima yao ni sawa kwao wao wote; wote wanapaswa kuwa na haki sawa. Lakini vipi kuhusu kufanana kwa haki zao?

Ikiwa badala ya kufuata kibubusa mawazo ya Kimagharibi tutaamua kufikiri sisi wenyewe, swali la kwanza linalokuja akilini ni iwapo kweli haki sawa zinamaanisha haki zinazofanana. Kwa kweli hayo ni mambo mawili tofauti. Usawa ni haki ya kuwa na daraja sawa kithamani na hadhi ambapo kufanana maana yake ni kulandana. Inawezekana baba akagawa mali zake kwa watoto wake watatu kwa usawa lakini sio kwa kulingana. Jaalia mali yake inajumuisha vitu mbali mbali kama vile maduka, mashamba na badhi ya mali zilizokodishwa. Baba kwa kuzingatia vipaji vyao na mambo ambayo kila mmoja anapenda, anaamua kumpa mmoja duka, mwingine shamba na wa tatu mali zilizokodishwa.

Anazingatia kuwa thamani ya mali aliyopewa kila mmoja wao ni sawa na wengine na kila mmoja amepewa kutokana na kipaji chake. Hivyo aligawa mali yake kwa usawa lakini sio kwa kulingana. Uwingi ni tofauti na ubora, na usawa ni tofauti na kufanana. Uislamu hauamini juu ya kulingana (uniformity) kwa mwanaume na mwanamke. Lakini wakati huo huo hauwapendelei wanaume katika maswala ya haki. Umezingatia kanuni ya usawa kati ya mwanamke na mwanaume lakini haukubaliani na kufanana kwa haki zao. Usawa ni neno linalifurahisha, kwa sababu linaashiria hali ya kutobagua. Lina utukufu maalum. Linaamsha na kuleta heshima, hasa linapohusiana na haki. Ni neno zuri lilioje 'Usawa na Haki.' Mtu yeyote mwema atafurahishwa na uzuri wake. Lakini hatuwezi tukaelewa ni kwa jinsi gani mambo yalifika hatua hii kiasi cha kuwa wengine ambao walikuwa vinara wa sayansi na falsafa nao wanataka kuingiza mawazo yao juu ya kufanana kwa haki kati ya wanawake na wanaume huku kwetu.

Hii ni sawa na mtu kuuza viazi vitamu kwa jina la mapeasi. Hapana shaka kuwa Uislamu haujatoa haki zinazofanana kati ya mwanaume na mwanamke katika mambo yote. Lakini pia haujaamuru majukumu na adhabu zinazofanana kwa jinsia hizi mbili. Yote kwa yote ni kuwa thamani ya jumla ya haki za mwanamke sio ndogo kuliko ile ya mwanaume. Tunataka kuthibitisha nukta hii. Hapa linazuka swali, kwa nini haki za mwanaume na mwanamke hazijafanana katika mambo yote. Je isingekuwa vizuri zaidi kama haki zao zingekuwa zinafanana katika mambo yote? Ili kulijadili hili swali kikamilifu, tutajadili chini ya vichwa vya habari vitatu. Mtazamo wa Uislamu juu ya nafasi ya mwanamke kutokana na maumbile yake. Athari za tofauti za kimwili kati ya mwanaume na mwanamke. Je, hili linasababisha tofauti ya haki zao pia? Ni nini falsafa ya sheria za Kiislamu, ambazo wakati fulani zinatofautisha kati ya mwanaume na mwanamke? Je falsafa hii bado ni thabiti?

Nafasi ya mwanamke katika utaratibu wa Kiislamu.

Qur'ani sio mkusanyiko tu wa sheria. Sio chombo cha sheria na kanuni kavu bila maelezo ya madhumuni yake. Ina sheria na pia ina historia, mawaidha ya kidini, maelezo ya malengo ya maisha, na maelfu ya mambo mengine katika sehemu mbalimbali, Qur'ani huelezea mambo yenye sura ya kisheria na katika sehemu nyingine hueleza lengo la maisha. Hufunua siri za dunia, mbingu, mimea, wanyama na wanaadamu. Huelezea siri za maisha na kifo, heshima na aibu, kupanda na kushuka, mali na umaskini.

Qur'ani sio kitabu cha falsafa, lakini kimeelezea kwa ufasaha sana maoni yake (Qur'ani) juu ya falsafa ya masomo matatu ya msingi; Ulimwengu, mwanadamu na jamii. Haiwafundishi wafuasi wake sheria peke yake, na haijishughulishi na mawaidha na nasaha (maonyo) peke yake, bali kwa kupitia tafsiri yake ya maisha (maumbile), huwapa wafuasi wake mtazamo maalum na namna pekee ya kufikiri. Msingi wa kanuni za Kiislamu juu ya masuala ya kijamii kama vile umiliki, serikali, haki za kifamilia n.k ni tafsiri ya maisha na mambo mengine tofauti tofauti.

Moja ya mambo yaliyoelezwa katika Qur'ani ni kuumbwa kwa mwanaume na mwanamke. Qur'ani haijakaa kimya juu ya jambo hili. Haijaacha mwanya kwa wadukuzi wa kifalsafa kuibua falsafa yao juu ya kanuni za mwanaume na mwanamke. Uislamu umetoa maoni yake juu ya mwanamke. Ili kujua maoni ya Uislamu juu ya mwanamke, tutazame Qur'ani inachosema juu ya tabia yake ya ndani. Dini nyingine pia zimelizungumzia suala hili, lakini ni Qur'ani peke yake ambayo katika Aya kadhaa inaelezea wazi wazi kuwa mwanamke ameumbwa kutokana na spishi za mwanaume, na wote mwanamke na mwanaume wana tabia za ndani zinazofanana.

Akimzungumzia Adam, Mwenyezi Mungu anasema;"Yeye (Allah) aliwaumba nyinyi wote kutokana na nafsi moja, na kutokana nayo (hiyo nafsi moja) akamuumbia mwenza wake (Suratun-Nisaa 4:1). Na juu ya mwanadamu kwa ujumla, Qur'ani inasema; "Amewaumbieni wake zenu kutokana na nyinyi. ' (Suratul Nisaa, Suratul Aali Imran na Suratul Ruum). Tofauti na vitabu vingine vya kidini hakuna sehemu yoyote katika Qur'ani ambapo imetajwa kuwa mwanamke ameumbwa kwa kutumia vitu duni au kuwa ana asili ya ukupe au ni wa asili ya upande wa kushoto. Uislamu hauungi mkono dhana ya kibiblia kuwa mwanamke ameumbwa kutokana na ubavu wa kushoto wa Adam. Uislamu hauna mtazamo wa dharau juu ya asili ya mwanamke na tabia zake za ndani.

Kuna nadharia nyingine ya dharau kwa wanawake iliyokuwa imeenea sana siku za nyuma, na imeacha alama mbaya katika siku za nyuma, na imeacha alama mbaya katika fasihi ya dunia. Kwa mujibu wa nadharia hiyo mwanamke ndio chanzo cha madhambi yote. Kuwepo kwake tu kunahamasisha uovu. Mwanamke ni shetani mdogo. Inasemekana kuwa katika kila dhambi na uhalifu uliotendwa na mwanaume kuna mkono wa mwanamke. Wanaume wenyewe hawatendi madhambi, ni wanawake wanaowasukumia kwenye madhambi. Pia inasemekana kuwa shetani hawezi kumwendea mwanaume moja kwa moja. Ni kupitia mwanamke ndio huwapotosha wanaume.

Shetani humchochea mwanamke na mwanamke humchochea mwanaume. Adam aliondolewa peponi kwa sababu ya mwanamke. Shetani alimshawishi Hawa, na ni Hawa aliyemshawishi Adam. Qur'ani imesimulia kisa hiki cha peponi lakini hakuna iliposema kuwa shetani au nyoka alipompotosha Hawa na Hawa akampotosha Adam. Haimlaumu Hawa wala haimuondoi katika hatia. Qur'ani inasema;"Tulimwambia Adam, 'Kaa Peponi; wewe na mke wako, na kuleni humo matunda popote mpendapo lakini msiusogelee mti ule msije kuwa miongoni mwa madhalimu ." (Suratul Baqara, 2:35). Inaweka kiwakilishi cha watu wawili. Pia Qur'ani inasema; "Kisha Shetani aliwatia wasiwasi." "Naye akawaapia (kuwaambia) kwa hakika mimi ni mmoja wa watoao shauri njema kwenu . (Suratul Aaraf 7:20-21).

Hivyo Qur'ani inapinga vikali dhana ya uongo iliyokuwa imeenea sana wakati wa kuteremshwa Qur'ani na miwangwi ambayo bado inasikika katika sehemu mbali mbali za dunia hii leo. Ilimuondoa mwanamke katika mashitaka kwamba yeye ni mchochezi wa dhambi na kwamba yeye ni shetani mdogo. Nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ambayo imekuwepo ni juu ya nafasi ya kiroho ya mwanamke.

Ilidaiwa kuwa mwanamke hawezi kuingia peponi. Hana uwezo wa kiroho na msaada wa Mungu kumuwezesha kufanya hivyo. Hana uwezo wa kufikia ukaribu wa Mwenyezi Mungu kama mwanaume anavyoweza kufanya. Lakini Qur'ani katika Aya mbali mbali imesema wazi wazi kuwa malipo ya pepo na ukaribu na Mwenyezi Mungu havitegemei jinsia ya mtu.

Inategemea na imani na amali (vitendo), na hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume juu ya hili katika Qur'ani, wametajwa watakatifu wa kiume na watakatifu wa kike. Qur'ani imewatukuza wake wa Adam na Ibrahim na mama yake Nabii Isa na Musa. Imewataja wake wa Nuhu na Lut kuwa hawakuwa stahili ya waume zao na haijamshahau mke wa Firauni ambaye ametajwa kuwa ni mwanamke mtukufu aliyekuwa mikononi mwa mwanaume muovu. Katika visa vyake Qur'ani imeweka mizania. Mashujaa wake ni wa kiume na wa kike. Wakati, ikimzungumzia mama yake Nabii Musa, Qur'ani inasema, "Tulimjulisha mama yake Musa kwa kumwambia;'Muweke katika sanduku na mtupe katika mto. Mawimbi yatamfikisha ufukweni . (Suratul Taha; 20:39). Juu ya mama yake Issa, Qur'ani inasema kuwa alifikia daraja tukufu ya kiroho kiasi kwamba malaika walikuwa wakiongea naye wakati anasali. Alikuwa akipokea chakula kutoka peponoi. Daraja la kiroho lilimshangaza hata Zakaria, Mtume wa wakati huo.

Kumekuwa na mifano mingi ya wanawake mashuhuri na watakatifu katika historia ya Uislamu. Ni wanaume wachache tu wanaweza kufikia daraja la Khadija, mke kipenzi wa Mtume(s.a.w.w) na hakuna mwanaume anayefikia daraja la bibi Fatima Zahra, binti kipenzi wa Mtume isipokuwa Mtume mwenyewe na Imam Ali(a.s) . Ana daraja kubwa kuliko hata la watoto wake ambao ni Maimamu, na hata la Mitume wote isipokuwa Mtume wa mwisho.

Uislamu hauwabagui wanawake dhidi ya wanaume katika 'safari ya kumuendea Allah' isipokuwa humuona mwanaume kuwa mwenye kufaa zaidi kuchukua jukumu la utume, ambalo yaweza kuelezewa kama safari ya kurudi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa watu. Nadharia nyingine ya dharau kwa wanawake inahusiana na kujihini na kutooa/kutoolewa. Baadhi ya dini zinaona kuwa tendo la ndoa ni kitu kichafu, kwa mujibu wa imani ya wafuasi wake, wanaoweza kufikia kilele cha juu cha daraja la kiroho ni wale tu ambao watamaliza maisha yao yote bila kuoa/kuolewa. Kiongozi mmoja wa dunia wa kidini anasema, "Kateni mti wa ndoa kwa shoka ya ubikira.' Viongozi hawa wa kidini wanavumilia ndoa tu kama uovu wenye nafuu.

Kwa maneno mengine wanashikilia kuwa kwa kuwa watu wengi hawawezi maisha ya bila kuoa/kuolewa na inaeleweka kwamba hawataweza kujidhibiti na hivyo kujiingiza katika zinaa za wanawake/wanaume wengi, basi ni bora waoe ili wasije kukutana na mwanamke zaidi ya mmoja. Watu hawa wanatetea kukaa bila kuoa au kuolewa na kujihini kwa sababu wanaona tendo la ndoa si kitu kizuri. Wanaona upendo kwa mwanamke kuwa ni uovu mkubwa wa kimaadili.

Uislamu unapinga vikali upuuzi huu. Unaiona ndoa kuwa ni taasisi tukufu na kukaa bila kuoa/kuolewa kuwa ni uchafu. Kumpenda mwanamke ni sehemu ya tabia ya Mtume. Mtukutu Mtume amesema; "Napenda vitu vitatu, manukato, mwanamke na swala." Bertrand Russel anasema, "Dini zote, isipokuwa Uislamu, zinalitazama tendo la ndoa kwa jicho baya. Uislamu unalitazama kwa maslahi ya kijamii, umeliwekea utaratibu maalum na kulidhibiti, lakini haulitazami kama uchafu." Nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ni kuwa mwanamke ameumbwa kwa maslahi ya mwanaume. Uislamu hausemi hivyo. Umeeleza malengo ya maisha kwa uwazi kabisa. Imeeleza kuwa dunia, mbingu, hewa, mawingu, mimea na wanyama vyote vimeumbwa kwa ajili ya mwanadamu. Haijasema mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanaume. Kwa mujibu wa Qur'ani mwanaume ameumbwa kwa ajili ya mwanamke na mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanaume.

'Wao (wanawake) ni nguo zenu na nyinyi (wanaume) ni nguo zao (2:187). Ingekuwa Qur'ani imeeleza kuwa mwanamke ni nyongeza (kiambatanisho) ya mwanaume na aliumbwa kwa ajili ya starehe yake (mwanaume) mtazamo huu ungekuwa umetazamwa katika sheria za Kiislamu, lakini Qur'ani haijasema hivyo. Hauyaelezei malengo ya maisha hivi. Haumuoni mwanamke kuwa ni kiambatanisho tu cha mwanaume. Ndio maana mtazamo huu haujazingatiwa katika sheria za Kiislamu. Nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ni kuwa mwanamke ni uovu usioepukika. Katika siku za nyuma, watu walimtazama mwanamke kwa dharau sana na walimuona kuwa ni chanzo cha mikosi na aina zote za matatizo.

Kinyume chake Qur'ani imesisitiza kuwa mwanamke ni baraka kwa mwanaume na ni chanzo cha raha na faraja kwake. Kwa mujibu wa nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ni kuwa hawakuthamini mchango wa mwanamke katika uzazi. Waarabu wa kabla ya Uislamu na baadhi ya jamii nyingine waliomuona mwanamke kama mfuko tu wa kukuzia mbegu ya mwanaume.

Sehemu mbali mbali ya Qur'ani imesema:'Tumewaumba kutokanana na mwanaume na mwanamke. ' Wazo hili limeelezwa katika Aya nyingine za Qur'ani. Hivyo Uislamu ulikomesha fikra hiyo kuwa mwanamke ni mfuko tu wa kukuzia mbegu ya mwanaume. Ni dhahiri sasa kuwa Uislamu hauna kabisa mitazamo yoyote ya kumdharau mwanamke. Sasa muda umefika wa kueleza kwa nini haki za mwanaume na mwanamke hazifanani. Ni kufanana, hapana, Ni kulingana, sawa.

Tayari tumeshasema kuwa katika suala la mahusiano ya kifamilia na haki za mwanamke na mwanaume, Uislamu una falsafa yake ambayo ni tofauti kabisa na ile iliyokuwa ada (kawaida), miaka 1400 iliyopita na ilivyo sasa. Pia tumesema kuwa hakuna ubishi wowote kuwa mwanaume na mwanamke ni sawa kama binadamu na haki zao za kifamilia zinapaswa kuwa sawa kithamani. Kwa mtazamo wa Uislamu wao wote ni binadamu na hivyo wana haki sawa. Nukta inayopaswa kuangaliwa hapa ni kuwa mwanaume na mwanamke, kwa sababu ya tofauti zao za kijinsia, wanatofautiana katika mambo mengi. Asili yao haitaki wafanane.

Nafasi hii inataka wasifanane katika haki nyingi, majukumu, wajibu na adhabu. Katika nchi za Magharibi jitihada inafanyika sasa kuzifanya haki na majukumu yao kufanana, na kupuuza tofauti zao za asili na za ndani. Hapa ndio kuna tofauti kati ya mtazamo wa Kiislamu na mfumo wa Kimagharibi katika nchi yetu, nukta inayobishaniwa ni suala la kufanana kwa haki sio usawa wa haki kati ya mwanamke na mwanaume. Usawa wa haki ni nembo tu ambayo imewekwa kwa makosa katika zawadi hii ya Kimagharibi.

Mwandishi wa kitabu hiki katika vitabu na hotuba zake mara zote amejiepusha kutumia nembo hii ya uongo na kamwe hajakubali kulipa jina la usawa jambo ambalo kiuhalisia ni kufanana kwa haki. Ulaya ya kabla ya karne ya 20 ni mfano dhahiri wa dhulma kwa mwanamke. Mpaka mwanzoni mwa karne ya 20 mwanamke wa Ulaya alinyimwa haki za kibinadamu katika maisha ya kila siku na kisheria. Hakuwa na haki sawa wala zinazofanana na mwanaume.

Ni katika muongo uliopita ambapo kutokana na harakati za pupa, wameanza kumpa haki zake za msingi, lakini bado hajaweza kupata haki zinazochukuana na maumbile yake na mahitaji yake kimwili na kiroho. Kama mwanamke anataka haki na usawa na furaha katika familia lazima alitupilie mbali wazo la kufanana kwa haki. Hiyo ndio njia pekee ya kuimarisha uchangamfu kati ya mwanaume na mwanamke.

Katika hali hiyo, sio tu kwamba mwanaume atazikubali haki za mwanamke, lakini pia atakuwa tayari kumpatia, na katika baadhi ya mambo atatoa haki nyingi zaidi tena bila kumdanganya. Halikadhalika hatudai kuwa katika jamii ya Kiislamu mwanamke anapata haki sawa na mwanaume. Mara nyingi tumesema kuwa ni muhimu kwamba nafasi ya mwanamke iangaliwe upya na apewe haki lukuki ambazo Uislamu umempatia, na ambazo amekuwa akinyimwa katika kipindi chote cha historia. Hata hivyo, haifai kuiga staili na mifumo ya Kimagharibi kibubusa, mifumo ambayo imesababisha madhara makubwa huko Magharibi kwenyewe.

Tunachodai ni kuwa kutofanana kwa haki kati ya mwanaume na mwanamke, kwa mujibu wa mipaka ya maumbile na tofauti zao ndio kutenda haki zaidi. Hukidhi mahitaji ya haki za asili vizuri zaidi, hutoa hakikisho kwa furaha ya familia na huisukuma jamii mbele katika njia ya maendeleo bora zaidi. Inaweza kukumbukwa kuwa tunadai kuwa haki ya asili inataka kwamba, katika baadhi ya mambo, kuwe na kutokufanana kwa haki ya mwanaume na mwanamke.

Kwa vile linahusiana na falfsafa ya haki, suala hili lina sura ya kifalsafa asilimia mia moja. Linahusiana pia na kanuni ya haki na usawa, kanuni kuu za sheria ya Kiislamu na falsafa ya uanazuoni wa Kiislamu. Ni kanuni ya usawa iliyoleta mafundisho ya kukubaliana kati ya akili na sheria ya Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa elimu ya sheria ya Kiislamu au tuseme ya Kishia, kama ikithibitika kuwa usawa unataka kuwa katika hali fulani, basi sura hiyo ndiyo itachukua sura ya kisheria bila kujali hoja zozote nyingine dhidi yake, kwani kwa mujibu wa mafundisho ya msingi ya Uislamu, sheria lazima katika hali yoyote isivunje au kuhalifu uadilifu wa asili na haki na za msingi.

Wanazuoni wa Kiislamu kwa kufafanua kanuni za usawa waliweka msingi wa falsafa ya haki, ingawa kufuatia matukio fulani ya kihistoria yasiyofurahisha, hawakuweza kuiendeleza kazi nzuri waliyoianza. Walikuwa ni Waislamu ambao, kwa mara ya kwanza walilitupia macho suala la haki za kibinadamu na kanuni za usawa, na walizitoa katika haki yake ya asili na kama kanuni zinazojitegemea bila kuathiriwa na sheria za kimikataba. Waislamu walikuwa vinara katika fani ya haki za asili za binadamu. Lakini hawakujaaliwa kuiendeleza kazi yao na hatimaye, baada ya karne nane, iliendelezwa na wasomi na wanafalsafa wa kizungu na wakajichukulia sifa hiyo.

Wazungu walileta falsafa za kijamii, kisiasa na kiuchumi na walijulisha watu, jamii na mataifa juu ya thamani ya maisha na haki za binadamu. Kwa maoni yetu mbali na sababu za kihistoria kulikuwa na sababu za kisaikolojia na kimkoa pia, ambazo ziliwazuia Waislamu wa Mashariki (Asia) kuendeleza suala la haki za msingi za binadamu.

Ni moja ya tofauti kati ya hulka ya nchi za Mashariki (Asia) na zile za Magharibi. Nchi za Mashariki zinazingatia maadili na za Magharibi zinazingatia haki. Mtu wa Mashariki ana upendo zaidi na anaamini kuwa lazima asamehe awe na moyo wa ubinadamu. Lakini mtu wa Magharibi anaamini kuwa kama binadamu lazima azijue na kuzilinda haki zake na lazima asiruhusu wengine wazipore. Utu unahitaji maadili na haki pia. Utu unahusiana na haki na maadili. Moja tu katika hizi haitoshi kuwa kigezo cha sifa bora za binadamu. Uislamu ulikuwa na hadi sasa unazingatia yote mawili haki na maadili.

Katika Uislamu, dhati, kusamehe, na matendo mema ni sifa takatifu na za kibinadamu. Lakini wakati huo huo mtu kujua haki zake na kuwa tayari kuzitetea, ni jambo takatifu na la kibinadamu. Hata hivyo, nchi za Mashariki kwa kiasi kikubwa zimekaliwa na Waislamu, na kwa hiyo, japokuwa awali yote yalikuwa yakizingatiwa maadili na haki lakini pole pole walijikuta wanabaki kushikilia maadili peke yake. Hivi sasa tunashughulikia suala la haki ambalo pia linaweza kuwa suala la kifalsafa na linafaa kujadiliwa kwa kirefu.

Inahusiana sana na maana halisi ya haki na ukweli halisi wa haki uadilifu na sheria uliokuwepo hata kabla ya kuwepo kwa sheria duniani, na ambao maana zake haziwezi kubadilishwa na sheria yoyote.

Montesquieu anasema, "Kabla ya sheria kutungwa na watu, kulikuwepo mahusiano yenye uadilifu baina ya watu kwa msingi wa sheria ambazo zilitawala mahusiano baina ya vitu vyote vilivyokuwepo. Ni kuwepo kwa mahusiano haya kulikosababisha kuundwa kwa sheria hizi. Kusema kwamba kabla ya watu kutunga sheria hapakuwa na uadilifu au dhuluma katika kuyaongoza na kuyadhibiti mahusiano ya watu ni sawa na kusema kuwa kabla ya mduara kuchorwa, nusu vipenyo vyake havilingani." Herbert Spencer anasema; "uadilifu unachaganganyika na kitu fulani mbali na hisia; yaani haki za msingi za binadamu. Lazima tuheshimu haki za binadamu ili uadilifu uwepo kiuhalisia." Wengi wa wasomi wa Ulaya wana mtazamo kuwa maazimio yote ya haki za binadamu yamechukuliwa kutoka katika haki za msingi za binadamu. Kwa maneno mengine, haki za msingi za binadamu zimechukuwa sura ya maazimio ya haki.

Kama tunavyojua, Montesquieu, Spencer n.k. wamesema kitu kimoja, juu ya uadilifu kama walichosema wanafalsafa wasomi wa Kiislamu juu ya msingi wa razini wa wema na uovu na kanuni ya usawa. Miongoni mwa Waislamu wamekuwepo wasomi ambao wamekana kuwepo kwa haki za asili na wanashikilia kuwa uadilifu ni jambo la kimkataba.

Halikadhalika, imani hii imekuwepo miongoni mwa wazungu. Mwanafalsafa wa Kiingereza, Thomas Hobbes alikana kabisa na akadai kuwa uadilifu sio kitu halisi. Azimio la haki za binadamu ni falsafa sio sheria. Ni kejeli kusema kuwa Azimio la Dunia la haki za binadamu ambalo linatoa hakikisho la usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke, imeidhinishwa na Bunge la nchi fulani, wanaume na wanawake wa nchi hiyo wanapaswa kuwa na haki sawa.

Hata hivyo, si jambo lililo katika mamlaka ya kisheria kwa Bunge la nchi yoyote kuidhinisha au kukataa Azimio kwa vile yaliyomo humo kwenye Azimio, hayana sura ya kimkataba, hivyo hayaangukii kwenye mamlaka yake ya kisheria. Azimio la Dunia hushughulikia haki za asili, zisizoondosheka na zisizobatilishika za binadamu na kama inavyodaiwa na Azimio lenyewe, haki hizi ni sehemu muhimu na ya lazima ya heshima ya mwanadamu na zimebuniwa na mamlaka yenye nguvu ya maumbile yenyewe.

Kwa maneno mengine, haki hizi zimetolewa na kupewa wanaadamu na chanzo kile kile kilichowapa akili, utashi na heshima. Kama ni hivyo, hali ya mambo yaliyomo katika Azimio hili inalazimisha kuwa hakuna mamlaka yoyote ya binadamu inayoweza kuyabuni au kuyafuta. Sasa hapa linakujaje suala la kuidhinisha Azimio hilo katika chombo cha kutunga sheria? Kwa kusema kweli, Azimio la Haki za Binadamu ni falsafa sio sheria. Na kama ni hivyo inafaa kuidhinishwa na wanafalsafa na sio na watunga sheria (wabunge).

Hakuna Bunge ambalo linaweza kutunga falsafa kwa kulumbana na kupiga kura. Vinginevyo kwa nini, muswada unaoelezea nadharia ya Einstein juu ya 'relativity' (kwamba vipimo vya mwendo nafasi na wakati vinawiana) au nadharia nyingine inayosema kuwa kuna maisha katika karne nyingine haijapelekwa Bungeni ili ikaidhinishwe na chombo kitukufu? Kiuhalisia, sheria ya asili haiwezi kupitishwa au kukataliwa kama sheria ya kimkataba.

Kupitisha sheria ya asili (maumbile) ni sawa na kupitisha sheria kuwa kupandikiza chipukizi la mpeasi kwenye muepo (tufaa) kutafanikiwa lakini kupandikiza mpeasi kwenye mforosadi (mulberry) hakutafanikiwa. Kila azimio lolote linapotolewa na kikundi cha wanafalsafa, kila taifa hupeleka kwa wanafalsafa wake, na kama watalipitisha basi ndio wananchi wote wa nchi hiyo wanapaswa kuzingatia maelekezo yake kama ukweli wa ziada wa kisheria. Mamlaka ya kisheria itapaswa kutopitisha sheria inayopingana na maelekezo hayo.

Lakini mataifa mengine hayatalazimika kuyazingatia maazimio haya maadamu hayajathibitishwa, kwa mujibu wa maoni yao, kuwa haki hizo zipo duniani. Na zaidi ya haya, kwa vile suala hili haliwezi kupimwa au kujaribiwa, halihitaji vifaa au maabara n.k Ni suala la kifalsafa ambalo vifaa vyake ni ubongo, akili na nguvu ya hoja. Hata kama mataifa mengine yatalazimika kuwafuata walio wengi katika suala la mantiki na falsafa na wanahisi kuwa hawana uwezo wa kutosha wa kufikiri kifalsafa wao wenyewe, sisi Waislamu hatuwezi kufuata mfano wao.

Tumeonyesha huko nyuma kuwa tuna uwezo mkubwa wa kushughulikia masuala ya mantiki na kifalsafa. Kwanini tuwafuate wengine leo? Inashangaza kwamba wakati wasomi wa Kiislamu walitilia uzito sana kanuni ya uadilifu na haki za msingi za binadamu na wanazikubali kama sheria ya dini, bila kusita wala ubishi wowote, yote haya yakakubaliwa na akili (kuwa ni haki), leo mambo yameharibika kiasi cha kuwa tunataka wabunge waidhinishe kutambuliwa kwa haki za binadamu. Falsafa haiwezi kuthibitishwa kwa kujaza kuponi.

Ni kejeli na dhihaka kubwa kuliko hata hiyo iliyotangulia, kujaribu kuamua suala la haki za binadamu kwa kuandaa kura za maoni kwa wavulana wadogo na wasichana wadogo. Je ni akili kweli kuchapisha kuponi na kuwaambia wavulana na wasichana wadogo waijaze ili kujua asili ya haki za binadamu na kama ni za aina moja au mbili. Hata hivyo, hapa tunataka kulijadili suala la haki za mwanamke kwa utaratibu mzuri na kifalsafa, na kwa kuzingatia haki za msingi za binadamu.

Tungependa kujua kama kanuni zinazotaka wanadamu wote wapate na kufaidi haki zao za msingi walizopewa na Mwenyezi Mungu, zinalazimisha au hazilazimishi kuwa mwanaume na mwanamke wawe na nafasi moja sawa katika haki zao. Tunawaomba wasomi, wanafalsafa na wanasheria wa nchi yetu, ambao wanaweza kuwa ni watu pekee wenye mamlaka ya kutoa maoni juu ya suala hilo na kuziangalia hoja zetu kwa jicho la umakinifu.

Tutawashukuru sana kama watatoa maoni yao ya kimamlaka kukubaliana na hoja zetu au kuzipinga. Katika kulijadili suala hili, ni muhimu kwanza kujadili msingi wa haki za binadamu. Haki za mwanaume na mwanamke zitajadiliwa baadaye. Katika muktadha huu, haitakuwa makosa kuzungumzia kidogo harakati za kutaka mabadiliko katika karne chache zilizopita, ambazo zimeleta wazo la usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke.

Tazamo fupi la historia ya haki za wanawake Ulaya. Mazungumzo ya haki za binadamu yalianza karne ya 17. Waandishi na wanafalsafa wa karne ya 17 na 18, kwa uvumilivu mkubwa, waliyatangaza na kuyaeneza mawazo yao juu ya suala la haki za msingi na zisizobatilishika za binadamu. Jeans-Jacques Rouseau,Voltaire na Montesquieu ni miongoni mwa waandishi na wanafalsafa hawa. Matokeo ya kwanza ya kivitendo ya kuenea kwa mawazo yao yalikuwa ni mapambano ya muda mrefu kati ya watawala na raia wa Uingereza. Mwaka 1688 Waingereza walifanikiwa kumshawishi mfalme akubali kuwapa baadhi ya haki za kisiasa na jamii walizokuwa wameziandika katika hati iliyojulikana kama 'The Bill of Rights.' Matokeo mengine muhimu ya kuenea kwa mawazo haya yalikuwa ni Vita vya Uhuru vya Wamarekani dhidi ya Uingereza.

Makoloni kumi na tatu ya Uingereza huko Amerika ya kaskazini yaliasi, kufuatia kuwekewa kodi kubwa sana, na hatimaye walipata uhuru wao. Mwaka 1776 mkutano ulifanyika Philadelphia, mkutano ambao ulitoa Azimio la Uhuru. Dibaji yake inasema; "Tunauchukulia ukweli huu kuwa dhahiri kwamba watu wote wameumbwa wakiwa sawa na kwamba wamepewa na muumba wao haki fulani zisizoondosheka, na kwamba miongoni mwa hizo ni haki ya kuishi, uhuru na kupata furaha au kufurahia.

Ili kuhakikisha kupatikana kwa haki hizi, serikali zinawekwa na watu, zinapata madaraka yao kutokana na idhini ya watawaliwa; na kwamba wakati wowote serikali ya muundo wowote inapokiuka malengo haya, ni haki ya watu kuibadilisha au kuiondoa, na kuweka serikali mpya, ikijengwa chini ya msingi wa kanuni hizi na kupata madaraka yake kwa utaratibu huu, itawahakikishia wananchi usalama na furaha yao.

Na lile linaloitwa Azimio la Haki za Binadamu lilitolewa baada ya Mapinduzi ya Ufaransa, lina kanuni fulani za jumla zinazoonekana kuwa sehemu muhimu na ya lazima ya katiba ya Ufaransa. Azimio lina dibaji na ibara 17. Ibara ya kwanza inasema kuwa watu wote huzaliwa wakiwa huru na hubaki huru katika maisha yao yote. Haki zao zinafanana. Katika karne ya 19 mawazo mapya yalitokeza katika uwanja wa haki za binadamu kiuchumi, kijamii na kisiasa. Haya yalisababisha kuibuka kwa ujamaa, ushiriki wa wafanyakazi katika faida na kuiondoa serikali kutoka mikononi mwa mabepari kwenda mikoni mwa wavuja jasho (wafanyakazi).

Hadi mwanzoni mwa karne ya 20, majadiliano yote yalikuwa yamejikita juu ya haki ya watu dhidi ya serikali au haki za tabaka la wavuja jasho dhidi ya waajiri na makabaila. Katika karne ya 20, suala la haki za mwanamke dhidi ya haki za manaume liliibuka. Ni juzi tu katika karne ya 20 ambapo Uingereza iliyokuwa ikijulikana kama demokrasia kongwe, ilipotambua usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke. Ingawa Marekani kiujumla ilikuwa imezitambua haki za binadamu katika karne ya 18 katika Hati ya Azimio la uhuru, lakini bado haki ya kupiga kura kwa wote ilitolewa mwaka 1920.

Ufaransa pia ilitoa haki ya wanawake kupiga kura katika karne ya 20. Kwa kiasi fulani, katika karne ya 20 sehemu kubwa ya watu duniani walijitokeza kuunga mkono mabadiliko makubwa katika mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke, katika nyanja za haki na majukumu. Kwa mujibu wao lengo la uadilifu wa kijamii halingeweza kufikiwa kwa kufanya mabadiliko baina ya mataifa na kati ya wafanyakazi na waajiri na mabepari bila pia kuleta mabadiliko katika mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke.

Hii ndio maana dibaji ya Azimio la Haki za Binadamu kwa wote, lililotolewa mwaka 1948 linasema kwamba "Ambapo heshima ya utu wa mtu mmoja mmoja na usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke" Machafuko yaliyosababishwa na maendeleo ya kuboreka kwa mashine (mitambo) katika karne ya 19 na 20, na hali mbaya ya wafanyakazi iliyofuatia, hasa kwa wafanyakazi wa kike, yalisababisha macho yaelekezwe kwenye masaibu ya mwanamke na ndio maana suala la haki zao lilizingatiwa sana.

Mwanahistoria anasema, "Kwa vile serikali ilikuwa haijali, masaibu ya wafanyakazi na tabia ya waajiri wao, mabepari walifanya walivyopenda". Wamiliki wa viwanda walikuwa wakiwaajiri wanawake na watoto kwa ujira mdogo sana, na kwa vile masaa ya kufanya kazi yalikuwa mengi mno, wengi wao waliugua magonjwa mbali mbali na wengine walikufa katika umri mdogo." Hii ilikuwa ni historia fupi ya harakati za Haki za Binadamu Ulaya.

Kama tunavyojua, ibara zote za Azimio la Haki za Binadamu ambazo ni mpya kwa wazungu, zilishawekwa na Uislamu katika karne 14 zilizopita, na baadhi ya wasomi wa Kiarabu na Kiirani katika vitabu vyao wamefanya ulinganisho kati ya mafundisho ya Uislamu na maelekezo (masharti) ya ibara hizi. Bado kuna tofauti katika baadhi ya vipengele vya maazimio haya na mafundisho ya Uislamu. Hili ni somo la kuvutia. Kwa mfano Uislamu unakubali usawa kati ya haki ya mwanaume na mwanamke, lakini haukiubali kufanana kwa haki hizi. Heshima ya mwanadamu na haki za binadamu. Ambapo kuitambua heshima na utu wa mwanadamu na haki zisizoondosheka za wanaadamu wote ni msingi wa uhuru, haki na amani duniani."

"Ambapo kutozingatia na kudharau haki za kibinadamu kumesababisha vitendo vya kishenzi na kuikasirisha dhamira njema ya mwanadamu na kuja kwa ulimwengu ambao ndani yake watu watafurahia uhuru wa kujieleza na imani, na uhuru wa kuondokana na hofu na shida imetamkwa kuwa ni hamu kubwa ya watu wa kawaida." "Ambapo italazimu, ikiwa mwanadamu hana kimbilio, kama njia ya mwisho, ana haki ya kuasi utawala wa kidhalimu, na kwamba haki za binadamu zitapaswa kulindwa na utawala wa kisheria." "Itakapobidi, kukuza maendeleo ya uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa." "Ambapo watu wa Umoja wa Mataifa, katika heshima ya utu wa mwanadamu na katika usawa wa haki za mwanaume na wanawake, na wamedhamiria kukuza maendeleo ya kijamii na kiwango cha ubora wa maisha, katika hali ya uhuru zaidi." "Ambapo Baraza kuu la umoja wa Mataifa linatamka Azimio hili la Haki za Binadamu kwa wote kama kigezo cha wote cha kupimia mafanikio ya watu wote na mataifa yote ili hadi kufika mwisho kila mtu na chombo cha jamii, kwa kulizingatia Azimio akilini mwao walijitahidi kwa kufundisha na kutoa elimu, kukuza tabia ya kuheshimu haki hizi na uhuru na kwa hatua za kimaendeleo za kitaifa na kimataifa, ili kulinda utambulisho na zingatio miongoni mwa nchi wanachama wenyewe na miongoni mwa watu wa nchi zilizo chini ya mamlaka yao ya kisheria" Kama tulivyoona mwanzo, kila neno na kila sentensi katika azimio hili limepigiwa hesabu kali, limechukuliwa kwa uangalifu mkubwa. Hili ni dhihirisho la maw azo ya wanafalsafa na wanasheria wataka mabadiliko wa karne nyingi. Nukta muhimu za dibaji ya Azimio la haki za binadamu.

Azimio hili lina ibara 30, japo baadhi ya ibara zimezidi kiasi na baadhi ya nukta zimerudiwa katika ibara nyingi. Nuktra muhimu za ibara ni kama ifuatavyo: Binadamu wote wana haki za msingi zisizobatilishika na haki ya kutambuliwa utu wao. Utu wa binadamu na haki za binadmau ni kwa ajili ya wote na hivi havigawiki. Vinawahusu watu wote bila kujali rangi, utaifa au jinsia. Binadamu wote ni wanafamilia, hivyo hakuna aliyebora kuliko mwingine. Kuzitambua kikamilifu haki za binadamu na utu wa binadamu ni msingi wa uhuru, haki na amani. Yaliyomo katika Azimio yanaashiria kuwa chanzo cha matatizo yote, vita, vitendo vya kishenzi vinavyofanywa na mtu mmoja mmoja na watu dhidi ya wengine ni kutozitambua haki za binadamu na utu wa binadamu.

Kutozitambua huku huwalazimisha baadhi kuasi dhidi ya wengine na hivyo kuhatarisha amani na usalama. Hitajio na kinachotamaniwa kikubwa zaidi katika kufanikisha azma hii ni kuzaliwa kwa dunia ambayo ndani yake kutakuwa hakikisho la uhuru wa imani, usalama na hali nzuri kimaisha pamoja na hakikisho la kuondokana na ukandamizaji, hofu na umasikini. Azimio lenye ibara 30 limeundwa ili kufikia lengo hili. Imani juu ya heshima kwa utu wa mwanadamu na haki za msingi za kibinadamu lazima ikaziwe na kuingizwa pole pole akilini mwa watu wote, kupitia ufundishaji na elimu.

Heshima kwa utu wa mwanadamu. Kwa vile Azimio la Haki za Binadamu limeundwa kwa msingi wa heshima kwa utu, uhuru na usawa kwa nia ya kufufua haki za binadamu, lazima liheshimiwe na kila mtu makini. Sisi watu wa Mashariki (Asia) tumekuwa tukiamini juu ya kuuheshimu utu wa binadamu kwa muda mrefu. Uislamu umetilia sana mkazo katika kuuheshimu utu pamoja na haki za binadamu, uhuru na usawa. Hao waliyoyahamasisha haya, wanastahiki shukrani zetu.

Hata hivyo, haya ni maandishi ya kifalsafa yaliyoandikwa na mikono ya kibinadamu, sio malaika. Hivyo kila mwanafalsafa anayo haki ya kuyachambua na kuonyesha nukta zake dhaifu. Hapana shaka kwamba Azimio la haki za Binadamu lina udhaifu wake, lakini hivi sasa hatuna nia ya kuonyesha udhaifu huo. Badala yake; tunaonyesha nukta zake nzuri.

Msingi wa Azimio hili ni heshima ya utu wa mwanadamu kwa sababu, kwa kuwa nazo hizo, mwanadamu anapata haki fulani ambazo viumbe wengine hawapati, kwa vile hawana utu huo. Hii ndio nukta nzuri ya Azimio hili. Falsafa ya Kimagharibi inamshusha hadhi mwanadamu. Hapa tena tulikutana na swali kongwe la kifalsafa; Ni nini asili ya utu wa mwanadamu ambao humtofautisha yeye na farasi, ng'ombe na njiwa? Hapa ndipo inapodhirika migongano kati ya msingi wa Azimio la Haki za Binadamu na tathhmini ya Kimagharibi juu ya mwanadamu. Falsafa ya Kimagharibi toka zamani imekuwa ikimshushia hadhi mwanadamu.

Chanzo cha yote ambayo yalikuwa yakisemwa zamani kuhusu mwanadamu na cheo chake kitukufu ilikuwa ni katika Mashariki (Asia). Sasa mifumo mingi ya falsafa ya Ulaya inayakejeli yote hayo. Mwanadamu kwa mtazamo wa Kimagharibi, amekuja (duniani) akiwa na cheo cha mashine. Kuwepo kwa roho na asili ya ukarimu kumekataliwa.

Wazo kwamba ulimwengu una lengo la msingi linaonekana kuwa ni wazo la kupinga maendeleo. Sasa hakuna mtu katika nchi za Magharibi anayeweza kusema kuwa mwanadamu ni mfalme wa viumbe. Kwa mujibu wa nadharia ya sasa ya kizungu, imani hiyo ilikuwa ni chipukizi (tawi) la unajimu wa Ptolem, ambayo ilikuwa inaaminika kuwa dunia ndio kitovu cha ulimwengu na nyota ziliaminika kuwa zinaizunguka dunia. Sasa kwa kuwa nadharia hii imeshakufa na kwa kutoweka kwake, hakuna nafasi tena ya mwanadamu kudai kuwa ni mfalme wa ulimwengu.

Kwa mujibu wa Wazungu, hata zamani ilikuwa ni kwa sababu ya ubinafsi wake ndio maana akajifanya kuwa bora kuliko viumbe wengine. Maisha yake ni ya kiumbo tu. Mtu akishakufa, mwili wake huoza na hapo ndio mwisho wa habari! Mzungu haamini kuwa roho inaweza kuishi peke yake. Kwa mtazamo huu, hajioni kuwa na tofauti yoyote kati yake na mimea na wanyama. Kwa hiyo anaona kuwa hakuna tofauti yoyote ile ya msingi kati ya asili ya vipawa vya kiakili na kiroho vya mwanadamu na sifa nyingine za maada kama vile joto, linalotoka kwenye makaa ya mawe.

Maisha kwa viumbe vyote, ikiwa ni pamoja na mwanadamu, yanamaanisha mapambano yasiyokwisha ya kuweza kuishi. Hii ndio kanuni ya msingi ya maisha. Mwanadamu mara zote amekuwa akipambana ili awe mshindi katika mapambano haya, na ili kuilinda nafasi (hadhi) yake amebuni kanuni za kimaadili kama vile uadilifu, wema, ushirikiano, uaminifu n.k. Kwa mujibu wa baadhi ya matapo yenye nguvu ya kifalsafa ya Kimagharibi mwanadamu ni mashine tu inayosukumwa na maslahi ya kiuchumi. Dini, maadili, falsafa, sayansi, fasihi na sanaa nyingine, vyote ni vikorombwezo tu. Miundo mbinu yake ni mfumo wa uzalishaji mali na ugawaji wa mali, na mambo haya ndiyo yanayotawala nyanja zote za maisha ya mwanadamu.

Sio hivyo tu, baadhi ya wanafalsafa wa Kimagharibi wana mtazamo kwamba vipengele vya kijinsia ndivyo vyenye ushawashi halisi wenye nguvu katika shughuli zote za mwanadamu. Maadili, falsafa, sayansi, dini na sanaa vyote hivyo ni miundo ilyobadilishwa na kurekebishwa ya jinsia. Hatuelewi ni jinsi gani tunaweza kuzungumzia utu wa mwanadamu na haki za msingi na ni jinsi gani tunaweza kuzifanya kuwa msingi wa matendo yetu yote, ikiwa tunakana kwamba maisha hayana lengo lolote la msingi, ikiwa tunafikiri kuwa mapambano ya kuweza kuishi na mapambano yatakayombakisha mwenye nguvu zaidi ndio sheria pekee zinazotawala maisha, ikiwa tunaamini kuwa mwanadamu ni mashine tu kama mashine nyingine (lakini) iliyopewa mikono ya binadamu, ikiwa tunashikilia kuwa hakuna roho na kwamba yote yanayozungumzwa juu ya roho ni kuzidisha chumvi kwa kiroho, ikiwa tunashikilia kuwa maslahi ya kiuchumi na ngono ndiyo yanayosukuma shughuli zote za mwanadamu, ikiwa tunajali kuwa wema na uovu ni dhana linganifu tu, ikiwa tuna maoni kuwa muongozo wa kimungu wa asili na wa kimaono ni upuuzi na ikiwa tutasema kuwa mwanadamu ni mtumwa wa matamanio yake na anaweza kunyenyekea kwa nguvu tu.

Maoni ya Kimagharibi juu ya mwanadamu yanapingana na utu wake na yameiporomosha hadhi yake katika kila pembe katika pembe ya sababu ya kuumbwa kwake, umbile lake, nia yake na dhamira yake. Baada ya kufanya yote haya, nchi za Magharibi zimetangaza Azimio la hali ya juu lenye busara kuhusu utu wa mwanadamu na cheo na haki za msingi zisizoondosheka na takatifu, na wametoa wito kwa kila mtu kulitekeleza hilo. Kabla ya kutoa Azimio hili la hali ya juu zuri na lenye busara, nchi za Magharibi kuhusu utakatifu na haki za asili za mwanadamu, wangeipitia upya tafsiri yao juu ya mwanadamu.

Tunakiri kuwa sio wanafalsafa wote wa Kimagharibi wana mtazamo huu. Wengi wao wanamtazama mwanadamu kama tunavyofanya sisi watu wa Mashariki (Asia). Tuna mtazamo ambao watu wengi wa Magharibi wanaung'ang'ania na ambao unawashawishi watu duniani kote. Azimio la Haki za Binadamu lilipaswa litolewe na wale ambao wanamuona mwanadamu kuwa ni zaidi ya roboti ambao wanafikiri kuwa malengo yake hayaishii kwenye silika za kibinadamu na kinyama na ambao wanaamini juu ya dhamira ya kibinadamu. Azimio la Haki za Binadamu lilipaswa litolewe na watu wa Mashariki ambao wanaamini kuwa mwanadamu ni khalifa wa Mwenyezi Mungu katika dunia. Qur'ani Tukufu inasema:

"Kwa hakika nitamuweka khalifa katika ardhi." (2:30) Ni wale tu wanaoamini kuwa mwanadamu ana lengo na makusudio ndio wanaoweza kuzungumzia juu ya haki za binadamu.

"Enyi watu, bila shaka lazima mjitahidi sana kwa ajili ya Mola wenu, kujitahidi kukubwa kabisa hadi mtakapokutana Naye." (84:6). Azimio la haki za binadamu linaifaa mifumo ile ambayo inaamini kuwa mwanadamu ana muelekeo wa asili wa kutenda mema;"Naapa kwa roho na kwa yule aliyeifanya kuwa timilifu na aliyeipa ujuzi (elimu) juu ya uovu na uchamungu." (91:7-8). Azimio la haki za Binadamu haliafikiani na njia za fikra za Kimagharibi.

Kufikiri kwao kunazifaa tu tabia za watu wa kimagharibi ambao huua hisia za kibinadamu, hucheza na tabia za wanaadamu, hujali fedha zaidi kuliko mtu, huabudu mashine (mitambo), huona mali kama Mungu na huwanyonya wanaadamu wengine. Ubepari umepata nguvu na mamlaka yasiyo na kikomo kiasi cha kuwa ikitokea kuwa milionea mmoja atamrithisha mbwa wake kipenzi mali zake, mbwa huyo ataheshimika kuliko watu, watu wengi tu watamtumikia mbwa huyo kama makatibu muhtasi na makarani na wataonyesha heshima ya hali ya juu kwa mbwa huyo.

Leo hii swali kubwa la kijamii kwa mujibu wa Qur'ani, ni je, mwanadamu amejisahau mwenyewe? Sio tu kwamba amejisahau yeye tu bali amemsahau hata Mungu wake pia. Akili zake zote amezielekeza kwenye maisha ya kidunia na mali na amepuuza kabisa kujifikiria na kujipima. Anafikiri kuwa amepoteza roho yake. Mawazo kama haya ni ya hatari sana na yanaweza kuondoa kabisa thamani ya utu na ubinadamu.

Ustaarabu wa sasa unaweza kuzalisha kila kitu chenye ubora wa juu kabisa, lakini hauwezi kumtengeneza mtu halisi. Gandhi anasema kuwa mzungu anastahili kuitwa bwana wa dunia. Anamiliki raslimali zote za kidunia na anafanya vitu ambavyo mataifa mengine wanaamini kuwa ni Mungu tu anayeweza kuyafanya.

Lakini ni kitu kimoja tu ambacho mzungu hawezi kukifanya nacho ni kujifikiria na kujipima. Hilo peke yake linatosha kuthibitisha kutokuwa na maana kwa kumeremeta kwa ustaarabu wa kisasa. Kama ustaarabu wa Kimagharibi umemtaabisha mzungu kwa ulevi na ngono basi ni kwa sababu ya kujisahau na kujipoteza badala ya kujitafuta. Uwezo wake wa kivitendo wa kuvumbua, kugundua na kuzalisha zana za kivita unatokana na kujikwepa nafsi yake na sio kwa sababu ya uwezo wake wa kipekee wa kujidhibiti. Kuogopa kwake upweke, ukimya wake na tamaa yake ya fedha kumemfanya asiweze kusikia sauti yake ya ndani.

Kushindwa kwake kujitawala ndio kichocheo chake cha kuuteka ulimwengu. Hii ndio sababu kila anakokwenda mzungu hueneza mitafaruku na ghasia. Kama mtu akipoteza nafsi yake mwenyewe, hakuna faida yoyote kuushinda ulimwengu. Wale ambao wamefundishwa na Injili kuwa wamisionari wa ukweli, upendo na amani, wanazunguka kutafuta dhahabu na watumwa. Badala ya kutafuta msamaha wa Mwenyezi Mungu na uadilifu katika ufalme wa Mungu, kama Injili inavyofundisha wanatumia dini yao kama kifutio cha madhambi zao (kwa kumfanya Yesu, Mtume mtukufu wa Mungu kuwa kafara ya dhambi kwa kila amuaminiye). Badala ya kufundisha na kuhubiri ujumbe wa Mungu, wanawadondoshea mabomu watu wasio na hatia. Hii ndio sababu, Azimio la Haki za Binadamu linakiukwa na nchi za Magharibi. Falsafa inayofuatwa na watu wa Magharibi katika maisha yao kivitendo inafanya kushindwa kwa Azimio hili kusiepukike.

2

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

I- UISLAMU NA MAISHA YA KISASA

Suala la dini na maisha ya kisasa ni moja ya mambo ambayo hayawagusi Waislamu peke yao. Dini nyingine pia zilikumbana na tatizo hili. Watu wengi wenye kupendelea mabadiliko duniani, wameikana dini kwa sababu wanaamini kuwa dini na maisha ya sasa haviendi pamoja. Wanafikiri kuwa kudumaa, kutuama na kutobadilika ni sifa za lazima za mtu mshika dini. Kwa maneno mengine, wanafikiri kuwa kudumaa na ukinaifu unatokana na kutokuwepo kwa mabadiliko na kwamba kudumisha hali ya kizamani ndio tabia za dini.

Marehemu Bwana Nehru aliyekuwa waziri Mkuu wa India alikuwa na mawazo ya kisekula na hakuwa akiamini dini yoyote. Inaoinekana kutokana na kauli zake kuwa kilichomfanya asipende dini ni kutobadilika kwake na ukinaifu unaotokana na kutokuwepo kwa mabadiliko. Kuelekea kipindi cha mwisho cha maisha yake Nehru alihisi kuwa na uwazi moyoni mwake na aliamini kuwa uwazi ule ungezibwa na nguvu ya kiroho tu.

Lakini hakuelekea kuiamini dini yoyote kwa sababu aliamini kuwa hali ya ukinaifu na kutokuwepo kwa mabadiliko ilikuwepo katika dini zote. Mwandishi wa habari wa Kihindi, aitwaye Karanjia, alimhoji Nehru katika kipindi chake cha mwisho mwisho cha uhai wake (Nehru) na alivyoonekana haya yalikuwa ni mahojiano ya mwisho ambapo Nehru alitoa maoni yake juu ya matatizo ya jumla ya ulimwengu.

Alipokuwa akimzungumzia Gandhi, Karanjia alisema, "Baadhi ya wanaopendelea mabadiliko (liberals) na maendeleo wanaamini kuwa Gandhiji, kwa kupitia na kwa kutokana na utatuzi wake wa matatizo kwa hisia kali, unyofu na njia za kiroho, zimedhoofisha na kuitia ubaridi imani yako ya asili ya ujamaa wa kisayansi." Katika kulijibu hili, Nehru alisema; "Ni muhimu na vizuri kutumia fursa ya njia za kimaadili na kiroho.

Mara zote nimekubaliana na Gandhiji juu ya hili. Ninaamini kuwa ni muhimu zaidi kutumia fursa ya njia hizi, kwani sasa, kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma, tunahitaji majibu ya kiroho na kimaadili juu ya maswali yanayotokana na pengo la kimaadili linalosababishwa na tamaduni za kisasa, ambazo zinazidi kuwa maarufu." Kisha Kiranjia aliuliza swali juu ya Ukomunisti.

Nehru alikiri mapungufu yake na katika majibu yake alionyesha baadhi ya mapungufu na ubovu wake (wa ukomunisti). Kwa mara nyingine tena alipendekeza suluhisho la kiroho juu ya matatizo ya dunia. Alipofika hapa Karanjia akasema; "Bwana Nehru, je dhana yako ya utatuzi wa matatizo ya kimaadili na kiroho haikufanyi uwe tofauti na Jawahanal wa jana? (Nehru mwenyewe enzi za ujana wake).

Ulichokisema kinaonyesha kuwa Bwana Nehru, katika kuelekea mwisho wa uhai wake, ameanza kumtafuta Mungu." Nehru alisema; "Ndiyo, nimebadilika. Msisitizo wangu juu ya unyofu na maadili ya kiroho na utatuzi wa matatizo sio wa bahati mbaya." Akaongeza kuwa; "Swali sasa ni jinsi ya kukuza maadili na imani ya kiroho katika daraja la juu zaidi.

Hapana shaka kwamba kwa ajili ya hili, dini zipo, lakini kwa bahati mbaya zimechukua mtazamo finyu na matendo yasiyobadilika na zimebaki kuwa taratibu rasmi lakini duni. Ni umbo lake la nje tu lililobaki, lakini ari na dhana yake ya kweli imetoweka." Uislamu na mahitaji ya wakati. Katika dini zote ni Uislamu tu unaojihusisha zaidi na vipengele vyote vya maisha ya mwanadamu.

Mafundisho yake hayajajikita katika matendo ya ibada na sala na mfumo wa ushauri wa maadili peke yake. Uislamu, kama ulivyoshughulikia uhusiano wa watu na Mwenyezi Mungu, ndivyo hivyohivyo ulivyoshughulikia mahusiano baina ya watu. Katika sura mbali mbali Uislamu umeshughulikia haki za watu binafsi na majukumu yao pia.

Hii ndio sababu swali kwamba mafundisho yake yanafaa kutumika au la katika mazingira yanayozidi kubadilika ni thabiti zaidi katika suala la Uislamu kuliko dini nyingine yoyote. Kwa bahati imetokea kwamba, wasomi wengi na waandishi wasiokuwa Waislamu wamezisoma sheria za kijamii na kiraia (za madai na za jinai) na wamezisifu kuwa ni chombo cha kisheria cha kimaendeleo na endelevu.

Wameusifu Uislamu kwa mapana na marefu, kuwa ni dini hai na itakayodumu milele, na wameuelezea uwezo na sifa za sheria hizi za Kiislamu wa kuweza kutumika nyakati zote na katika hali zote. Mwandishi maarufu sana wa Kiingereza aliyekuwa akipendelea msimamo wa wastani (liberal), Bernard Shaw amesema; "Mara zote nimekuwa nikiipa dini ya Muhammad heshima kubwa (daraja kubwa), kutokana na uhai wake wa ajabu.

Ni dini pekee inayoonekana kwangu kuwa na uwezo wa kunyumbulika na hivyo kuweza kutumika katika dunia inayobadilika na katika zama zote. Nimetabiri kuwa imani ya Muhammad itakubaliwa na Ulaya ya kesho, na dalili za hili zinajionyesha hata sasa. Makasisi wa zama za kati aidha kwa sababu ya ujinga au kwa sababu ya kung'ang'ania bila hoja imani zao waliupaka Uislamu rangi mbaya kabisa. Kwa kusema kweli walifundishwa kumchukia mtu huyu, Muhammad na dini yake. Kwao Muhammad alikuwa mpinga Kristo.

Mimi nimemsoma, mtu huyu wa ajabu, na kwa maoni yangu hakuwa mpinga Kristo kabisa na lazima aitwe mkombozi wa wanaadamu. Ninaamini kuwa kama mtu kama yeye angetwaa madaraka /uongozi wa dunia ya sasa angefanikiwa kutatua matatizo katika namna ambayo ingeleta amani na furaha, vitu ambavyo vinahitajika sana kwa sasa. Dr. Shibli Shama'il ni myakinifu wa Kiarabu wa Lebanoni. Kwa mara ya kwanza alitafsiri kitabu cha 'Darwin Kiitwacho 'Origin of Species' kwenda katika lugha ya Kiarabu, pamoja na sharhe ya mwanasayansi wa kijerumani aitwaye Boucher katika kitabu hicho akakipa jina la 'A weapon against religious belief.' ('Silaha dhidi ya imani za kidini.') Ingawa hamwamini Mwenyezi Mungu, haoni aibu kuusifu Uislamu na muasisi wake mtukuka. Ameusifu Uislamu kwa kusema kuwa ni dini hai inayoweza kutumika katika zama zote.

Mtu huyu, katika juzuu ya pili ya kitabu chake kiitwacho, 'Philosophy of Evolution' ambacho amekichapisha kwa Kiarabu, ameandika makala yenye kichwa cha cha habari 'Uislamu na Ustaarabu'. Ameandika makala hii kukanusha madai ya wasio Waislamu kwa kutoa madai kuwa Uislamu ndio uliosababisha kuporomoka kwa hali ya Waislamu. Shibli Shama'il amejaribu kuthibitisha kuwa jambo hasa lililosababisha kuporomoka kwa hali za Waislamu ni wao Waislamu kuyaacha (kuacha kutekeleza) mafundisho ya kijamii ya Uislamu.

Wale wazungu wanaoushambulia Uislamu aidha hawajui au wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kuwafanya watu wa Mashariki (Asia) wazitilie shaka sheria zao na mfumo wao ili kuwafanya wafuate mfumo wa Kimagharibi. Wakati wa zama zetu, suala la iwapo Uislamu unaafikiana na hali halisi ya maisha ya sasa au la limekuwa likiulizwa sana. Tunapata picha ya ndani ya watu hasa wale wanaotoka katika tabaka la wasomi na tunakuta kuwa swali hili linaulizwa zaidi kuliko maswali mengine.

PINGAMIZI

Wakati fulani watu hawa wanatoa hoja za kifalsafa juu ya suala hili kuwa vitu vyote hapa duniani lazima vibadilike. Hakuna kinachobaki vile vile bila kubadilika, na halikadhalika binadamu wanabadilika. Sasa inawezekanaje sheria za Kiislamu zibaki hivyo bila kubadilika kwa zama nenda rudi? Kama tukilitazama swala hili kwa mtazamo wa kifalsafa kabisa, jibu ni rahisi.

Ni vitu (maada) vinavyobadilika kila mara, ambavyo hukua na kuporomoka na ambavyo hupasika katika kugeuka na kuoza. Lakini sheria za ulimwengu hazibadiliki. Kwa mfano, viumbe vyote hai vimegeuka na vimeendelea kugeuka kwa mujibu wa utaratibu na kanuni fulani zilizoelezwa na wanasayansi. Hapana shaka kwamba viumbe hivi vinageuka na kubadilika lakini kanuni zinazotawala mabadiliko haya hazibadiliki. Na sasa tunazungumzia kanuni (sheria) hizi.

Katika hili, hakuna tofauti yoyote iwapo sheria hizi ni za asili au zimetungwa na kukusanywa, kwani inawezekana kwamba sheria ambazo zimetungwa zinaweza kuwa na asili kama chanzo chao na kuafikiana na mchakato wa mabadiliko ya mtu mmoja mmoja na halikadhalika jamii ya wanadamu kwa ujumla.

Hata hivyo, swali kuhusiana na kuafikina au kutoafikiana kwa Uislamu na mahitaji ya muda halina sura ya kiujumla na kifalsafa peke yake. Swali ambalo huulizwa zaidi ni kuwa kwa vile sheria huundwa kukidhi mahitaji ya wanaadamu na mahitaji yenyewe yanabadilika kila mara inawezekanaje sheria hizo za kijamii zibaki hivyo hivyo bila kubadilika? Ni swali zuri.

Na imetokea kuwa tabia za kimiujiza za Uislamu zimewezesha sheria zisizohitaji kubadilishwa kukidhi mahitaji yasiyobadilika ya mtu mmoja na jamii na sheria zinazobadilika badilika kwa mahitaji ya muda mfupi na yanayobadilika. Hii ni sifa ya kipekee ambayo Waislamu wote wajuzi wa mambo ya sheria za kiislamu na waliozisoma sheria zake wanajivunia. Tutalielezea hili vizuri zaidi baadaye. Je mabadiliko ya kijamii yanakwenda na wakati? Kabla ya kuliendea swali hili tungependa kuibua nukta mbili. Nukta ya kwanza ni kuwa watu wengi wanaoongelea maendeleo na mabadiliko ya hali wanadhani kuwa mabadiliko yoyote ya kijamii, hasa kama yametokea nchi za Kimagharibi, basi ni matokeo ya maendeleo.

Hili ni moja ya mawazo potofu liliyoendekezwa na kizazi hiki. Watu wanadhani kuwa kwa vile njia za maisha hubadilika siku hadi siku, zilizo duni hubadilishwa kwa zilizo bora zaidi na sayansi na viwanda vinaboreka kila siku, mabadiliko yote katika maisha ya binadamu ni aina ya maendeleo na kwa hiyo yanafaa kukaribishwa na kupokelewa kwa mikono miwili. Wanafikiri pia kuwa mabadiliko haya hayaepukiki na huja baada ya muda fulani.

Kwa kusema kweli sio kwamba mabadiliko yote ni matokeo ya maendeleo ya sayansi na viwanda wala sio kwamba hayaepukiki. Huku sayansi ikiendelea kukua, asili ya ubinafsi na unyama wa mwanadamu nayo hubaki bila kubadilika. Ujuzi (elimu) na busara humpeleka mtu katika ukamilifu na asili ya unyama wa mwanadamu humsukumia kwenye ufisadi na upotofu.

Asili ya unyama wa mwanadamu mara zote hujaribu kutumia ujuzi kama njia ya kupatia matamanio yake. Kwa kadiri muda unavyokwenda, kwa kadiri maendeleo na mabadiliko yanavyotokea, ufisadi na upotofu ndivyo unavyozidi kukua na kukomaa. Tunapaswa kwenda na wakati lakini wakati huo huo lazima tupige vita ufisadi pia. Mleta mabadiliko (mema) na mpinga mabadiliko (mema) wote wanapigana dhidi ya muda, tofauti yake ni kuwa mleta mabadiliko mema hupigana dhidi ya upotofu unaoletwa na mabadiliko ya muda na mpinga maendeleo (mabadiliko) hupigana dhidi ya mabadiliko (maendeleo halisi) yanayoletwa na mabadiliko ya muda.

Kama tunauchukulia muda na mabadiliiko yake kama kigezo cha mema yoyote na maovu yote, sasa ni kigezo gani cha kuupimia muda wenyewe? Kama kila kitu kitakwenda na wakati sasa je wakati wenyewe unapaswa kwenda na nini? Kama mwanadamu ataufuata muda na mabadiliko yake kwa utii mkubwa, sasa nini kitafanyika juu ya majukumu na nafasi ya utashi wa mwanadamu? Mwanadamu anaendesha gari la wakati, ambalo liko kwenye mwendo.

Lazima awe mwangalifu na aliongoze vyema gari lake. Vinginevyo atakuwa kama mtu aliyepanda farasi na akamwachia farasi wake aende popote atakapo. marekebisho au kuondoa kabisa? Nukta ya pili inayofaa kutajwa hapa ni kwamba baadhi ya watu wamelitatua tatizo gumu la Uislamu na mahitaji ya wakati kwa namna rahisi sana.

Wanasema kuwa Uislamu ni dini ya milele, na inaweza kurekebishwa ili kuafikiana na mahitaji ya kila zama na wakati. Lakini wanapoulizwa marekebisho haya yanafanyikaje na kanuni yake ni nini, mara moja wanasema kuwa hali ya maisha inapobadilika, sheria zilizopo hubatilishwa na kuwekwa nyingine. Wanatoa hoja kuwa sheria za msimu (muda mfupi) za kidini lazima ziwe na uwezo wa kurekebishwa na ziafikiane na maendeleo ya elimu na sayansi pamoja na kupanuka kwa utamaduni na ustaarabu. Kwa mujibu wao, uwezo huo wa sheria wa kuweza kurekebishwa ili kuafikiana na mahitaji ya wakati haupingani na Uislamu na sio kinyume na mafundisho yake.

Wanadai kuwa, kwa vile mahitaji ya wakati yanabadilika kila mara, basi kila zama huhitaji sheria mpya. Wanaendelea kudai kuwa sheria za kiraia na kijamii za Uislamu zinaafikiana na maisha rahisi ya Waarabu waliokuwa wakiishi kabla ya Uislamu, na ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa ni kwa mujibu wa mila na desturi zao.

Sasa kwa kuwa haziafikiani na maisha ya zama hizi zinatakiwa ziondolewe na ziwekwe nyingine mpya za kisasa. Watu hawa wanapaswa kuulizwa: Kama uwezo wa sheria kuweza kurekebishwa maana yake ni uwezo wa kubatilishwa na kufutwa, basi ni sheria gani ambayo haina sifa hii? Kuna sheria basi yeyote ambayo haiendi na wakati kwa mtazamo huu?

Tafsiri hii ya uwezo wa sheria kurekebishwa na kuweza kutumika katika zama zote ni sawa na kusema kuwa vitabu vyote na maktaba ndio njia bora kabisa za kufurahia maisha kwa sababu muda wowote mtu atakapotaka starehe, anaweza kuviuza na kutumia fedha zitakazopatikana kwa ajili ya kukidhi matamanio yake. Mwandishi wa Kiirani anasema kuwa mafundisho ya Uislamu yamegawanyika katika sehemu tatu.

Sehemu ya kwanza ina imani za msingi kama vile tauhidi (imani kuwa Mungu ni mmoja tu), Utume, Ufufuo n.k. Sehemu ya pili inahusiana na matendo ya ibada kama vile sala, saumu, udhu, tohara, hija n.k sehemu ya tatu ina sheria zinazohusiana na maisha ya watu. Kwa mujibu wake yeye ni sehemu mbili tu za mwanzo ambazo ni za lazima katika dini na ambazo zinafaa kuhifadhiwa milele.

Lakini sehemu ya tatu sio sehemu ya lazima ya dini kwa kuwa dini haihusiani na maisha ya kila siku ya watu. Mtukufu Mtume mwenyewe hakuamuru kuwa sheria hizi ziwe sehemu ya dini kwa vile hazikuhusiana na ujumbe wake yeye kama Mtume. Ilitokea tu kwamba akawa ni mkuu wa Dola, kwa hiyo akalazimika kuweka sheria pia. Vinginevyo dini haina lolote la kulazimisha katika maisha ya kidunia ya watu. Ni vigumu kuamini kuwa mtu anayeishi katika nchi ya Kiislamu anaweza kuwa mjinga wa mafundisho ya Uislamu kiasi hiki. Je, Qur'ani haijaelezea lengo la kuleta Mitume na Manabii? Je, Qur'ani haisemi wazi wazi kuwa:'Tumewaletea Mitume wetu na dalili za wazi na tumewaleta pamoja nao kitabu na vipimo, ili watu wahukumiane kwa haki. (Suratul Hadidi; 57:25). 35 Qur'ani imeuelezea uadilifu katika jamii kama lengo kuu la Mitume wote.

Kama unataka unaweza usiyafuate mafundisho ya Qur'ani, lakini kwa nini unatenda dhambi kubwa zaidi kwa kuusingizia na kuuzushia Uislamu na Qur'ani? Bahati yetu mbaya zaidi inatokana na ukweli kwamba maadili yetu na sheria vimepoteza chanzo pekee cha nguvu yake, yaani dini. Ni katika nusu karne tu tulipoanza kusikia watu wakipiga kelele kuwa Uislamu ni mzuri, ili muradi tu ubakie ndani ya majumba ya ibada, na usishughulike na jamii.

Kelele hii imepigwa kutoka ndani ya mipaka ya nchi za Waislamu na imeenezwa katika ulimwengu wote wa Kiislamu. Ili kuliweka lengo la kelele hizi wazi tunaweza kusema kuwa nia ni kuufanya Uislamu ubaki kuwa ni kikwazo cha kuzuia kuenea kwa ukomunisti lakini kama huu huu Uislamu utagongana na maslahi ya Magharibi basi upingwe vikali.

Kwa mtazamo wa watu wa Magharibi, matendo ya Uislamu lazima yaendelee, ili pindi ikitokea haja, Waislamu wahamasishwe kuupinga mfumo wa kikomunisti ambao hauamini mambo ya dini na Mungu, lakini sheria za kijamii za Uislamu ambazo zinatoa falsafa ya maisha ya Uislamu lazima ziondoshwe, kwa vile sheria hizi huwapa Waislamu uhuru fulani na kuwafanya wawe watu tofauti wanaojitegemea katika mfumo wao, jambo ambalo litawazuia kumezwa na nchi za Magharibi zenye tamaa kali. Kwa bahati mbaya, watetezi wa hoja kuwa Uislamu haujihusishi na maisha ya kila siku ya watu, wamesahau baadhi ya ukweli wa msingi. Awali miaka 1400 iliyopita, Uislamu ulipinga kanuni kuwa tunaamini baadhi ya mambo (baadhi ya mafundisho ya Uislamu) na tunayakataa mengine, na ukatamka kuwa kanuni na sheria za Uislamu hazibadiliki.

Pili tunaamini kuwa muda umefika ambapo Waislamu hawapaswi kupotoshwa na mbiu za uongo. Watu sasa pole pole wameanza kuamka na wameanza kutofautisha kati ya maendeleo ambayo ni matokeo ya kuchanua kwa vipaji vya kisayansi na kiakili, na kudhihiri kwa ufisadi na upotofu, kutoka nchi za Magharibi. Watu wa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa, kuliko kipindi kingine chochote, wameanza kufahamu thamani ya mafundisho ya Uislamu na wametambua kuwa wanaweza tu kuishi maisha huru kwa kuyafuata. Hawatayaacha, kwa gharama yoyote.

Waislamu makini wanafahamu kuwa propaganda dhidi ya sheria za kiislamu si chochote bali udanganyifu wa mabepari. Tatu, watetezi wa hoja hii wanapaswa kujua kuwa Uislamu unapokuwa na nguvu, hushinda mifumo mingine yote, iwe ya kikafiri au vinginevyo. Uislamu unataka kutawala maisha ya jamii kama falsafa ya maisha, na hautaki kubakia misikitini tu na sehemu nyingine za ibada. Uislamu ambao utabakia kwenye nyumba za ibada, utaacha nafasi kwa ajili ya mawazo ya Kimagharibi na halikadhalika mawazo yanayopingana na umagharibi na itikadi zake. Adhabu ambazo nchi za magharini zinatumikia, katika baadhi ya nchi za Waislamu ni matokeo ya kutoujua ukweli huu.

3

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

- II UISLAMU NA MAISHA YA KISASA

Mwanadamu sio kiumbe pekee anayeishi maisha ya kijamii. Wanyama wengi, na hususan wadudu hupenda kuishi pamoja na kushirikiana. Wanafuata kanuni za mgawanyo wa kazi, uzalishaji na ugavi na kutoa na kupokea amri. Nyuki, na baadhi ya wadudu jamii ya mchwa wana mfumo huu bora wa maisha, mfumo ambao utamchukua mwanadamu, anayejiona kuwa ni mfalme wa viumbe vyote, miaka au hata karne ili kufikia kiwango hicho cha ufanisi.

Ustaarabu wao (wadudu hawa) haujapitia vipindi kama vile zama za mwituni, zama za mawe na zama za nyuklia. Toka mwanzo wamekuwa na ustaarabu na mfumo wa namna moja kama tu walivyo leo. Ni mwanadamu aliyeanzia sifuri. Tazama : "Mwanadamu aliumbwa dhaifu ."Suratul Nisaa 4:28 Kwa upande wa wanyama, mahitaji yao ya maisha hayabadiliki. Kwao usasa na fasheni mpya havina maana. Ulimwengu wa kale na ulimwengu wa sasa kwao hauna tofauti yoyote.

Kwao sayansi haifanyi ugunduzi wowote ule. Bidhaa mpya kabisa nyepesi na nzito za viwanda hazikuingia katika soko lao; kwa nini? Kwa sababu wanaishi kwa silika na sio kwa akili (mantiki). Maisha ya kijamii ya mwanadamu mara zote yanabadilika. Kila karne ulimwengu unabadilika. Hapo ndio kuna siri ya mwanadamu kuwa mfalme wa viumbe vyote.

Mwanadamu ni mtoto wa maumbile aliyekomaa na kustahili heshima. Amefikia hatua ambayo hahitaji muongozo wa moja kwa moja wa ile nguvu ya ajabu iitwayo silika. Maumbile yanafahamu kuwa mwanadamu ni kiumbe aliyekomaa, na ndio maana yamemuacha huru. Yale ambayo wanyama wanayatekeleza kwa silika na kwa kufuata kanuni za maumbile ambazo hawawezi kuzivunja/kukiuka, wanaadamu wanatakiwa kuyatekeleza kwa kutumia akili na elimu na kwa kufuata sheria zilizopitishwa na zinazoonekana. Mwanadamu akiwa ni mwamuzi wa mwisho wa majaaliwa yake mara zote anaweza kupotoka na kuiacha njia ya maendeleo, na hapa ndio kuna siri ya kuteleza kwake, vipingamizi vyake (anavyokumbana navyo) kupotoka na kushindwa kwake.

Kama tu ilivyo kuwa maendeleo yapo wazi kwake, halikadhalika njia ya kuelekea upotofu, ufisadi na kushindwa haijafungwa. Wanaadamu wamefikia hatua ambayo kwa mujibu wa maneno ya Qur'ani wanaweza kubeba dhamana ambayo mbingu, ardhi na milima haviwezi kubeba; kwa maneno mengine, wanaweza kuishi maisha huru na wanaweza kuchukua majukumu ya kisheria, kitaalamu na mengineyo. Hii ndio sababu hawana kinga ya makosa, ubinafsi, ujinga na dhulma. Pale Qur'ani inapouelezea uwezo huu wa ajabu wa binadamu, mara moja unamtaja kuwa ni 'dhalimu na mjinga'.

Uwezo na sifa hizi mbili za mwanadamu, uwezo wa kuboreka (kuwa bora zaidi) na uwezo wa kupotoka havitenganishiki. Mwanadamu sio kama mnyama ambaye katika maisha yake ya kijamii, huwa haendi mbele wala nyuma, hageukii kulia wala kushoto. Lakini mwanadamu kwa upande wake, katika maisha yake wakati fulani huenda mbele na wakati fulani nyuma. Katika maisha ya wanadamu kama kuna mwendo na kasi, basi kuna kusimama na kupumzika pia. Kama kuna maendeleo na kubadilika kwenda katika hali bora zaidi basi kuna ufisadi na upotofu pia. Kama kuna haki na wema, basi kuna udhalimu na ushari pia.

Kama elimu na busara vimedhihiri basi ujinga na matamanio duni yamedhihiri pia. Inawezekana kwamba mabadiliko yanayotokea na hali mpya zinazoonekana vikawa ni vya kundi la pili (la mabaya). Wasiotaka kubadilishwa na waliopotoshwa. Ni moja ya tabia za mwanadamu kwamba wakati fulani hufanya jambo kupita kiasi na wakati fulani hufanya jambo kwa kiasi kidogo zaidi kuliko inavyohitajika. Kama akichagua kundi la kati na kati hufanya jitihada kutofautisha kati ya mabadiliko ya aina sahihi na mabadiliko ya aina potofu.

Hujaribu na hufanya jitihada kuusukuma muda mbele kwa msaada wa elimu na ubunifu wake na kujinasibisha na maendeleo huku akijaribu kuudhibiti upotofu na kuepuka kutangamana nao. Lakini kwa bahati mbaya, si mara zote mwanadamu huchagua njia hii. Anaandamwa na magonjwa mawili ya hatari, ugonjwa wa kutotaka kubadilika na ugonjwa wa ujinga. Ugonjwa wa kwanza matokeo yake ni kubaki bila mabadiliko na kujiepusha na maendeleo na matokeo ya ugonjwa wa pili ni upotofu wa kuangamia. Asiyetaka kubadilika huchukia kila jambo jipya na hawezi kuafikiana na kitu chochote isipokuwa cha zamani.

Kwa upande wa pili, limbukeni huona kila kitu kipya kuwa ni cha kisasa na maendeleo na hukiaona kuwa ndio hitajio la wakati. Kwa yule asiyetaka mabadiliko (rigid) kila maendeleo mapya kwake anaona ni ufisadi na upotofu wakati limbukeni anaona mambo yote mapya bila kubagua yote yana maana kupanuka kwa utamaduni na elimu. Asiyetaka mabadiliko hatofautishi kati ya pumba na kiini safi na kati ya njia na malengo. Kwa maoni yake kazi ya dini ni kuhifadhi yale yote ya kale na kuukuu hata kama hayatumiki.

Anafikiri kuwa Qur'ani iliteremshwa ili kudhibiti mwendo wa wakati na kuibakiza hali ya dunia iwe vile vile siku zote. Kwa mujibu wa mtazamo huu, mila za zamani na zilizopitwa na wakati, kama vile kuanza kusoma Qur'ani kuanzia mwisho, kuandikia kalamu za matete na wino wa kuchovya kunawia kwenye beseni la kituruki; kula kwa mikono, kutumia taa ya mafuta ya taa na kubakia bila ya kujua kusoma na kuandika ni mambo ya kidini ambayo lazima yahifadhiwe na kudumishwa. Kwa upande mwingine limbukeni huelekeza macho yake yote nchi za Magharibi ili aweze kuiga mtindo wowote mpya utakaotokea na kila mila mpya. Huiita hali hii kuwa ni kisasa na jambo la lazima kufuatwa lililoletwa na wakati. Wote wawili, wasiotaka mabadiliko na waliopotoka (wajinga) wanaamini kuwa mila na desturi zote za zamani ni kanuni/matendo ya kidini, tofauti ni kuwa asiyetaka mabadiliko anataka kuzihifadhi wakati mjinga anaona kuwa dini ni sawa na kudorora (bila mabadiliko yoyote).

Katika karne chache zilizopita suala la migongano kati ya dini na sayansi limekuwa likibishaniwa sana miongini mwa watu wa nchi za Magharibi. Wazo la migongano liliibuka kutokana na mambo mawili. Kwanza kanisa lilikuwa limezikubali baadhi ya dhana za kisayansi na kifalfasa kuwa ni imani za kidini, lakini maendeleo ya sayansi yakathibitisha uongo wa dhana hizo. Pili, sayansi imebadilisha muundo na hali za maisha. Wale wasiotaka mabadiliko, ambao wana muonekano wa kushika dini, wanataka kuufanya muonekano wa nje wa maisha ya kimaada kuwa sehemu ya dini, kama tu, bila ulazima wowote walivyoyapa sura ya kidini baadhi ya masuala ya kifalsafa.

Limbukeni nao wanaamini kuwa dini imeamuru muundo fulani wa maisha ya kimaada, na kwa vile sayansi imeamuru kuwepo kwa mabadiliko katika muundo huu, dini inapaswa kutupiliwa mbali. Kupinga mabadiliko kwa kundi moja, na ujinga wa kundi jingine, kumezua wazo la kubuni la mgogoro kati ya sayansi na dini. Hadith ya mafumbo katika Qur'ani Uislamu ni dini ya kimaendeleo na inataka wafuasi wake waendelee. Qur'ani imetumia hadith ya mafumbo (yenye mafundisho) kuwashawishi Waislamu wasonge mbele, chini ya nuru ya Qur'ani. Inasema kuwa wafuasi wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ni kama mbegu iliyopandwa katika ardhi. Kwanza matawi yake hutokeza kama majani laini ya mbegu. Kisha hukua na kuimarika sana kiasi cha kuweza kusimama katika kikonyo chake. Hakua haraka mno kiasi cha kuwashangaza sana wakulima.

Huu ni mfano wa jamii ambayo Qur'ani inaukusudia. Qur'ani inachokikusudia ni kukua. Qur'ani inataka kuweka msingi wa jamii ambayo mara zote itakuwa ikikua, ikiendelea na kupanuka. Will Durant anasema hakuna dini iliyowataka wafuasi wake kuwa na nguvu kama Uislamu ulivyofanya. Historia ya Uislamu wa awali inaonyesha ni kiasi gani Uislamu ulivyo na nguvu ya kuijenga upya jamii na kuisukuma mbele kimaendeleo. Uislamu unapingana na vyote viwili kutaka mabadiliko na ulimbukeni (ujinga) na unaviona vyote hivi viwili kuwa ni hatari. Uchakavu wa kiakili wa wasiotaka mabadiliko na kung'ang'ania kwao mila za zamani ambazo hazina uhusiano wowote na Uislamu, kumetoa kisingizio kwa limbukeni kuuona Uislamu kuwa unapingana na maisha ya kisasa (usasa).

Kwa upande mwingine kufuatana na kuiga mitindo mipya zaidi na namna za maisha za Magharibi kunakofanywa na limbukeni, imani yao kwamba kufuata utaratibu wa Kimagharibi kimwili na kiroho, kukubali kwao tabia, adabu na desturi za Magharibi, na kuiga kibubusa sheria za kiraia na kijamii kutoka katika nchi za Magharibi, kumetoa kisingizio kwa wasiotaka mabadiliko kukitazama kila kitu kipya kwa mashaka na kukiona kama tishio kwa dini yao, uhuru wao na kwa haiba ya kijamii ya jumuiya yao. Kwa sasa, Uislamu unagharamikia makosa ya makundi yote mawili.

Ung'ang'anizi wa wasiotaka mabadiliko umeacha uwanja wazi kwa limbukeni kufanya uharibifu na ujinga wa limbukeni umewafanya wasiotaka mabadiliko kuwa ving'ang'anizi zaidi katika imani zao. Inashangaza kuona kuwa hawa wanaojiita wameelimika na kustaarabika ingawa kiuhalisia ni watu wajinga, wanafikiri kuwa muda ni maasumu (haubebi dhambi). Ukweli ni kuwa mabadiliko yote yanaletwa na watu, na mwanadamu sio maasumu hata kidogo (hajaepukana na madhambi). Sasa vipi inaweza kufikirika kuwa mabadiliko ya muda mara zote huwa hayana makosa na matatizo. Kama ilivyo tu kuwa mwanadamu ana matakwa ya kupenda sayansi, maadili, sanaa na dini, na mara zote huchukua hatua mpya kwa maslahi ya wanadamu, pia ana baadhi ya tabia mbaya.

Ni mbinafsi, mwenye uchu wa madaraka na mwenye kupenda raha. Anapenda fedha na unyonyaji kama tu alivyo na uwezo wa kugundua mambo mapya na kutafuta njia bora zaidi za kufanya mambo pia ana dhamana ya kutenda makosa. Lakini limbukeni na waliopotoka hawajui mambo hayo. Wanarudia mahadhi yale yale kuwa ulimwengu wa kisasa upo hivi na vile. Kinachoshangaza zaidi ni kuwa wanalinganisha kanuni za maisha na vitu; kama vile viatu, kofia na gauni. Kwa vile vitu hivi hutafutwa na kuhitajika vinapokuwa vipya na kutupwa vinapochakaa, halikadhalika kwa mujibu wao, hali iwe hivyo hivyo kwa ukweli usiobadilika. Kwao, kizuri na kibaya havina maana zaidi ya kipya na cha zamani.

Ukabaila ni mbaya kwa sababu tu ni mfumo wa zamani na umepitwa na wakati. Vinginevyo ulikuwa mzuri kabisa wakati unaanzishwa duniani kwa mara ya kwanza. Halikadhalika unyonyaji wa wanawake ni mbaya tu kwa vile haupendwi na ulimwengu wa kisasa; vinginevyo hadi hivi majuzi, watu hawa hawa walikuwa hawampi mgao wa urithi. Walikuwa hawajaitambua haki yake ya kumiliki mali na walikuwa hawaheshimu ridhaa na maoni yake.

Kwa mujibu wa watu hawa, katika zama hizi, zikiwa ni zama za anga (kuruka na ndege n.k), kama ilivyokuwa tu haiwezekani kusafiri kwa punda na kuacha ndege, kuwasha kibatari na kuacha umeme, kushona nguo kwa mkono na kuandika kwa mkono huku ukiacha mashine kubwa za kisasa za kuchapishia, halikadhalika haiwezekani kuacha kwenda kwenye sherehe za muziki, sherehe ambazo watu wanavaa mavazi ya kuogelea, mialiko ya chakula cha usiku chenye nyama za kubanikwa, kutoshiriki katika vicheko vya ovyo, kutocheza karata, kutovaa visketi vifupu kwani vitu vyote hivi ni mitindo ya karne hii. Wanahofu kuwa wasiposhiriki katika mambo haya watarudi nyuma katika zama za kuendesha farasi. Wanadai kuwa hizi ni zama za nyukilia, zama za sayansi, zama za miezi ya kubuni na zama za makombora ya masafa marefu.

Hili ni jambo zuri! Sisi pia tunamshukuru Mungu kuwa tunaishi katika zama hizi na tunaomba kwamba tufurahie na kufaidika na sayansi na viwanda kwa kiwango cha juu kabisa. Lakini je, mambo yote haya yanasababishwa na sayansi tu? Je, hali zote za karne hii ni matokeo ya maendeleo ya kisasa ya sayansi? Je, sayansi inadai kuwa imedhibiti mambo yote hapa duniani? Sayansi haijawahi kudai hivyo hata siku moja.

Balaa la karne yetu ni kuwa kundi la wanasayansi kwa nia njema kabisa, huitumia sayansi kufanya ugunduzi mpya, lakini kundi jingine la wabinafsi na wenye uchu wa madaraka na wanaoabudu fedha huyatumia vibaya matunda ya jasho la wanasayansi ili kuyafikia malengo yao ya kiovu. Sayansi inalalamika kuwa inatumiwa vibaya na wanaadamu wakorofi na hii ndio bahati mbaya ya kizazi chetu. Sayansi inasonga mbele katika fani za fizikia na inagundua sheria za mwanga na kuakisi na kundi la wakorofi na wabinafsi wanaitumia kutengenezea filamu za bluu (ngono) za uharibifu na uovu. Kemia inaendelea na kugundua tabia za vitu mbali mbali na michanganyiko yake.

Baadhi ya watu wanaamua kutumia ugunduzi huu kutengeneza madawa ya kulevya, heroin ambayo ni laana kwa wanaadamu. Sayansi iligundua chanzo kizuri cha nishati ndani ya atom, lakini kabla ya ugunduzi haujatumika kwa manufaa ya wanaadamu, wenye tamaa ya madaraka walifanya haraka kutengeneza bomu la atomiki, na kuwadondoshea watu wasio na hatia. Mapokezi yalipoandaliwa, kwa ajili ya heshima ya Einstein, mwanasayansi mkubwa wa karne ya 20, yeye mwenyewe alipanda juu ya jukwaa na kusema, "Mnampa heshima mtu ambaye amechangia kwa namna fulani kutengenezwa kwa bomu la atomiki?"

Einsten mwenyewe hakutumia elimu yake kutengeneza bomu. Ni wengine waliotumia ugunduzi wake kwa lengo hili. Matumizi ya heroin, mabomu ya atomiki na filamu za matusi (bluu) haviwezi kuhalalishwa eti kwa madai kuwa ni mambo ya karne hii. Ikiwa ndege za kisasa kabisa za mabomu zinatumika kurushia mambomu bora kabisa kwa watu wa nchi nyingine, na watu walioelimika sana wanaajiriwa kufanya kazi hii, je, usasa huu unaweza kupuguza ushenzi wa kurithi wa tendo hili?

4

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

- III UISLAMU NA USASA

Hoja kuu ya wale ambao wanasema kuwa katika masuala ya haki za kifamilia tunapaswa kufuata mfumo wa Kimagharibi, ni kuwa muda umebadilika na mahitaji ya karne hii yanatutaka tufanye hivyo. Tunaonelea kuwa ni vizuri tuyaweke maoni yetu wazi juu ya nukta hii, kwa sababu bila kufanya hivyo, mjadala juu ya nukta yoyote hautakuwa kamili, ingawa kwa sababu ya uchache wa nafasi haiwezekani kulijadili suala hili kwa mitazamo yake yote, kifalsafa, kisheria, kijamii na kimaadili. Itatosheleza hapa kujadili nukta mbili tu. Nukta ya kwanza ni kwamba kuafikiana kwayo na kukubaliana na mabadiliko ya wakati sio suala rahisi sana kama baadhi ya watu wasiojua wanavyofikiri. Mabadiliko yanayoletwa na wakati, wakati fulani huwa ni ya kurudisha maendeleo nyuma.

Tunapaswa kwenda na mabadiliko ya wakati ya kimaendeleo na tunapaswa kuyapiga vita mabadiliko yanayoletwa na wakati ambayo ni ya kiharibifu. Ili kutofautisha aina hizi mbili za mabadiliko na kujua asili yake, tunapaswa kujua chanzo cha maendeleo (ugunduzi au mabadiliko) haya mapya na yameelekezwa katika mwelekeo gani. Tunapaswa kuangalia ni tabia gani za kibinadamu zimeyaleta (njema au mbaya) na ni matabaka gani ya watu yanatetea mambo haya mapya?

Tunapaswa kuangalia je yameletwa na tabia tukufu za mwanadamu au matamanio duni yanayofanana na wanyama, na kama yamekuja kama matokeo ya uchunguzi usio wa kibinafsi wa wanazuoni na wasomi, au yameletwa na matamanio duni ya wanaotumikia nafsi zao na tabia za kifisadi za jamii.

MNYAMBULIKO WA SHERIA ZA KIISLAMU

Nukta ya pili inayofaa kuwekwa wazi ni kuwa baadhi ya wasomi wa kiislamu wanaamini kuwa Uislamu una uwezo na sifa ambazo zinaupa uwezo wa kutumika zama zote. Kwa mujibu wa wasomi hawa, mafundisho ya Uislamu yanaafikiana na maendeleo ya wakati, kupanuka kwa utamaduni na matokeo ya mabadiliko haya. Hebu tuangalie asili, sifa na uwezo huu ambao Uislamu unao. Kwa maneno mengine hebu tuangalie ni vifaa gani vimewekwa katika jengo hili la dini, na ikiwa vimeipa sifa ya kuafikiana na hali zote zinazobadilika, bila kuwa na haja ya kuacha baadhi ya mafundisho yake na bila mgogoro wowote kati ya mafundisho yake na hali yoyote inayojitokeza ya kupanuka kwa elimu na ustaarabu.

Ingawa suala hili lina sura ya kiufundi, ili kuondoa shaka shaka ya wale wanaotilia shaka ukweli huu kuwa Uislamu una sifa hii, tunalielezea kwa kifupi hapa. Kwa undani zaidi juu ya suala hili, wasomaji wanaweza kusoma kitabu kiitwacho 'Tanbihul Ummah' cha hayati Ayatullah Naini au kitabu kingine kiitacho 'Marjaiyyat Wal Imamat cha mwanazuoni mkubwa wa zama hizi Allamah Tabatabai. Lakini vitabu vyote hivi vipo katika lugha ya kifursi. Kuna nukta nyingi, ambazo zinaunda siri ya Uislamu kuwa na uwezo wa kuafikiana na kupanuka kwa elimu na ustaarabu, na uwezo wa kutumika kwa sheria zake thabiti na imara katika hali mbali mbali za maisha. Hapa tutataja baadhi yake.

Msisitizo katika roho na kutojali sana kiwiliwili. Uislamu haujashughulikia maisha ya nje (kimwili) tu ambayo hutegemea kiwango cha maendeleo ya elimu ya mwanadamu. Mafundisho ya Uislamu hushughulikia roho pia na malengo ya maisha na hutoa njia bora kabisa ya kuyafikia malengo haya. Sayansi haijabadilisha roho na malengo ya maisha wala haijapendekeza njia yoyote nzuri zaidi, fupi zaidi na salama zaidi ya kuyafikia malengo haya. Imetoa tu njia bora zaidi na vifaa vya kukwamisha njia ya kuyafikia malengo haya. Uislamu, kwa kuhifadhi malengo tu katika himaya yake na kuacha muundo na mbinu kwenye himaya ya sayansi na teknolojia, umeepuka migongano dhidi ya utamaduni na ustaarabu.

Sio hivyo tu lakini pia kwa kuhimiza mambo yanayosaidia kupanuka kwa ustaarabu, yaani elimu, kazi, uchamungu, ridhaa, ujasiri na uvumilivu bila kukata tamaa, umejitolea kuwa kigezo kikuu cha kupanua ustaarabu. Uislamu umeweka alama za barabarani katika njia yote ya maendeleo ya mwanadamu. Alama hizi kwa upande mmoja zinaonyesha njia na kituo cha mwisho na kwa upande wa pili zinaonyesha makorongo na sehemu za hatari. Sheria zote za Kiislamu ni alama za barabara, aidha za aina ya kwanza au ya pili. Njia za maisha katika zama hutegemea juu ya kiwango cha elimu ya wanaadamu.

Kwa kadri elimu ya watu inavyopanuka, ndivyo njia bora zaidi za kujipatia kipato zinavyotokea na moja kwa moja zinachukua nafasi ya zile njia duni (za zamani). Mifumo ya nje na ya kimaada ya njia hizi (za kupatia riziki) haina utakatifu katika Uislamu, na Waislamu hawalazimiki kuzidumisha. Uislamu haujasema kifaa hiki na kile kitumike kwa ushonaji, ususi, kilimo, usafiri, vita au kazi nyingine. Hivyo hapawezi kuwa mgogoro wowote kati ya sayansi na Uislamu, pindi kifaa kinapopitiwa na wakati, cha kisasa zaidi kinaweza kutumika badala yake.

Uislamu haujaagiza kutumika kwa mtindo maalum ya viatu au nguo, wala haujapendekeza aina fulani ya ujenzi wa majengo. Halikadhalika hauhimizi juu ya mbinu fulani fulani za uzalishaji na ugavi. Hii ni moja ya sifa hizo za Uislamu, ambazo zimeuwezesha kuweza kutumika katika maendeleo yote ya wakati. Sheria madhubuti kwa mahitaji madhubuti na sheria zinazobadilika kwa mahitaji yanayobadilika. Sifa nyingine ya Uislamu, ambayo ina umuhimu mkubwa ni kuwa umeweka sheria madhubuti (zisizobadilika) kwa ajili ya mahitaji madhubuti (yasiyobadilika) na sheria zinazobadilika kwa mahitaji yanayobadilika. Mbali na mahitaji ya wanaadamu, mahitaji ya mtu mmoja mmoja na vikundi, yote yana asili ya kudumu.

Hayabadiliki kwa mujibu wa wakati. Kanuni za mifumo inayotawala silika za binadamu na mahusiano ya kijamii hazibadiliki. Tunazijua nadharia za 'Maadili husianishi' na 'Uadilifu husianishi' ambazo zina wafuasi wake, na tutatoa maoni yetu kuhusiana nao baadaye. Sehemu nyingine ya mahitaji ya mwanadamu ni ile ya mahitaji yanayobadilika, na hii huhitaji sheria zinazobadilika. Uislamu ulishayaona mahitaji hayo na umeyaunganisha na kanuni fulani ambazo zina sheria ndogo zinazobadilika kila hali inapobadilika. Kufafanua nukta hii hebu tuangalie mifano hii;'Andaeni majeshi kwa ajili yao (maadui)' (Suratul Anfal 8:60.) Wakati huo huo tunasoma hadith kadhaa za Mtume katika vitabu vya sheria za Kiislamu chini ya kichwa cha habari 'Kuendesha farasi na kurusha mishale.' Mtume aliwaelekeza Waislamu wajifunze kuendesha farasi na kurusha mishale na wawafundishe watoto wao pia. Haya yalikuwa ni sehemu ya mafunzo ya Kiislamu katika zama hizo.

Ni dhahiri kabisa hapa kuwa amri ya msingi ni 'Kuandaa majeshi.' Upinde na mshale, jambia na mkuki na farasi sio vya muhimu. Kilicho cha muhimu ni kuwa imara kijeshi dhidi ya maadui. Kuandaa majeshi ni amri ya kudumu ambayo imetokana na hitajio la kudumu. Hata hivyo ulazima wa kupata ujuzi katika kuendesha farasi na kurusha mishale sio wa kudumu, na hubadilika kutokana na wakati.

Kutokana na kubadilika kwa hali, ujuzi wa kufyatua risasi umechukua nafasi ya kurusha mishale. Mfano mwingine ni sheria ya kijamii inayohusu kubadilishana mali, iliyotajwa katika Qur'ani. Uislamu umetambua kanuni ya umiliki wa mali wa mtu binafsi. Hata hivyo umiliki huu unaotambuliwa na Uislamu ni tofauti na ule uliopo katika nchi za kibepari. Tabia ya umiliki wa mali wa watu binafsi katika Uislamu ni kanuni ya kubadilishana. Kwa utaratibu huu Uislamu umeweka sheria fulani.

Mojawapo imeelezwa na Qur'ani Tukufu katika maneno haya'Na msile mali zenu (kila mmoja kula za mwenzake) kwa batili' (Suratul Baqarah, 2:188).

Kwa maneno mengine katika mauzo ya biashara, fedha isitoke mkono mmoja kwenda mwingine isipokuwa kwa kubadilishana na kitu kingine cha halali chenye kuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mali hiyo. Imelezwa na kufafanuliwa katika sheria ya Kiislamu mauzo na manunuzi ya vitu fulani yamekatazwa. Vitu hivyo ni pamoja na damu na kinyesi cha binadamu. Sababu ni kuwa vitu hivi havina thamani inayoviwezesha kuhesabika kuwa sehemu ya mali ya mwanadamu. Kanuni hii ni sawa ya mali ya mwanadamu. Kanuni hii ni sawa na ile iliyo katika Aya iliyonukuliwa hapo juu.

Ubatili wa mauzo na manunuzi ya damu na kinyesi cha binaadamu ni sehemu au mfano tu wa matumizi ya kanuni hiyo. Hata kama hakuna ubadilishaji uliofanyika, (wa bidhaa au bidhaa kwa fedha) fedha au mali inayomilikiwa na mtu fulani haiwezi kufujwa au kuliwa bure. Sheria inayokataza kula mali ya mtu mwingine bure (bila kufanya kazi) au kiwizi ni kanuni madhubuti na inatumika zama zote, na imetokana na hitajio la kudumu la jamii.

Lakini kanuni kuwa damu na kinyesi cha binadamu havihesabiki kama mali na haviruhusiwi kuuzwa, inahuisiana na wakati na kiwango cha ustaarabu. Kanuni hii inaweza kubadilishwa kutokana na mabadiliko ya hali, maendeleo ya sayansi na viwanda na uwezekano wa kuzitumia bidhaa hizi katika namna sahihi na yenye manufaa. Mfano mwingine; "Imam Ali(a.s) hakuwahi kuweka dawa kwenye nywele zake hata siku moja, ingawa zilikuwa zimekuwa za mvi katika miaka ya mwisho ya uhai wake.

Siku moja mtu mmoja alimwambia, 'Je Mtume hakuamrisha nywele za mvi ziwekwe dawa?" Ali alijibu 'Ndiyo aliamrisha' Sasa kwa nini huweki dawa kwenye nywele zako? Yule mtu aliuliza. Ali akasema; "Katika wakati ule ambao Mtume alitoa maelekezo haya, idadi ya Waislamu ilikuwa ndogo na kulikuwa wazee wengi waliokuwa wakishiriki vitani. Mtume aliwaamrisha wazipake dawa ili kuficha umri wao halisi, kwani kama adui angeona kuwa anapambana na kundi la wazee tu, hamasa yake ingeongezeka. Kwa kuwa Uislamu umeenea dunia yote, hali imebadilika. Kila mtu yupo huru kupaka dawa nywele zake au kuacha." Kwa maoni ya Imamu Ali, maelekezo ya Mtume hayakuwa ya kudumu wala haikuwa sheria ya kudumu.

Uislamu unajali muonekano wa nje na roho ya ndani pia. Lakini unataka pumba kwa ajili ya punje yenyewe na unataka nguo kwa ajili ya mwili. Suala la kubadilisha herufi Katika siku za hivi karibuni hapa Iran kumekuwa na ubishani juu ya kubadlisha herufi. Suala hili linaweza kuangaliwa katika pande mbili kwa mtazamo wa kanuni za Kiislamu, na kwa sura mbili. Kwanza ni iwapo Uislamu unapendelea herufi fulani na kuzibagua nyingine.

Je Uislamu unaziona herufi za sasa, ambazo ni za Kiarabu, kama zake, na herufi nyinginezo kama zile za kilatini zinazoonekana ni za kigeni? Uislamu ambao ni dini ya ulimwengu mzima unaziona herufi zote duniani kuwa ni sawa. Sura ya pili ni kuwa kiasi gani kubadilika kwa herufi kutachanganya utamaduni wa Taifa la Kiislamu na watu wengine na kutakuwa na madhara gani kwa utamaduni wa taifa hili. Na zaidi ya hayo, katika karne 14 zilizopita, vitabu vya Kiislamu na kisayansi vilivyozalishwa na Irani vimeandikwa katika herufi za sasa (za kiarabu), je kubadilisha herufi si kutazifuta (haribu) kazi zote hizi?

Swali jingine ni, 'Ni akina nani wanaopendekeza mabadiliko haya, na ni akina nani watakaoyatekeleza? Maswali yote haya ni thabiti.' Kuwategemea wengine ndio kumekatazwa, sio kofia ya kizungu Watu kama mimi mara nyingi wanakumbana na maswali, yanayoulizwa kwa dharau au kejeli. "Sheria ya Kiislamu inasemaje kuhusu kula ukiwa umesimama?' Ni vipi kuhusu kula kwa kijiko au uma?' Je kuvaa kofia ya kizungu kumekatazwa?' Je kutumia lugha za kigeni kumekatazwa?'" Katika kujibu maswali haya, tunasema kuwa Uislamu haujatoa maelekezo yoyote mahsusi juu ya hili. Uislamu haujawaelekeza wafuasi wake kula kwa mkono au kijiko. Ulichowaelekeza ni kuzingatia usafi.

Uislamu haujaelekeza matumizi ya mitindo ya aina fulani ya viatu, kofia au nguo. Kwa mtazamo wa Uislamu lugha zote Kiingereza, Kijapani, Kifursi, zina hadhi sawa. Hata hivyo, Uislamu unasema kitu fulani zaidi. Umesema kuwa imekatazwa mtu kupoteza utambulisho wake. Kuwaogopa wengine bila ulazima kumekatazwa, Kuwaiga wengine kumekatazwa, kuchekeshwa na kuvutiwa na wengine kama sungura anavyovutiwa na nyoka, kumekatazwa.

Kumchukulia punda mgeni aliyekufa kuwa ni farasi kumekatazwa. Kuingiza nchini upotofu na ukosefu wa maadili kutoka nje, kwa madai ni mambo ya kisasa ya karne hii, kumekatazwa. Kuamini kuwa Waislamu wanapaswa kufuata mila na utamaduni wa Kimagharibi ndani na nje, kimwili na kiroho, kumekatazwa. Kwenda nchi ya Kimagharibi kwa siku chache na baada ya kurudi, unaanza kutamka maneno yetu kama wao (wazungu) kumekatazwa. Muhimu na muhimu zaidi. Sura nyingine ya Uislamu inayoufanya uende na mahitaji ya wakati ni kukubaliana kwa mafundisho yake na akili/mantiki.

Uislamu umetangaza kuwa sheria zake zimezingatia maslahi makubwa zaidi. Na wakati huo huo, Uislamu wenyewe umetoa madaraja mbali mbali ya umuhimu wa maslahi haya. Hii inarahisisha kazi ya wataalamu wa sheria za Kiislamu katika fani hizo ambapo maslahi tofauti yanaonekana kugongana. Katika hali hizo, Uislamu umewaruhusu wataalamu wa sheria za Kiislamu kupima uzito wa maslahi tofauti, na kuzingatia mwongozo ambao Uislamu wenyewe umetoa, katika kuangalia ni maslahi gani hilo ni muhimu zaidi. Katika fani ya sheria za Kiislamu, hii huitwa suala la "muhimu na muhimu zaidi." Kuna mifano mingi ambapo kanuni hii ya maslahi ya juu na ya juu zaidi imepata kutumika.

Hata hivyo kwa sababu ya uchache wa nafasi, tunairuka sehemu hii Sheria yenye haki ya Turufu. Sifa nyingine ya Uislamu ambayo imeipa dini hii uwezo wa kuhamishika na kutumika katika hali mbali mbali na imeifanya kuwa dini inayoishi na ya kudumu milele ni kuwa ndani yake kuna chombo cha sheria ambacho kazi yake ni kudhibiti na kurekebisha sheria nyingine.

Mafakihi wanaziita kanuni hizi kuwa ni " kanuni za kuongozea." Kanuni ya 'Hakuna madhara' na 'Hakuna hasara' kwamba sheria haitatumika pale ambapo inaweza kusababisha ugumu au madhara kwa maslahi ya mtu asiye na hatia, imeuenea (imeutawala) mfumo mzima wa kisheria. Lengo la kanuni hizi ni kudhibiti na kurekebisha sheria nyingine. Kwa kusema kweli Uislamu umezipa nguvu ya turufu kanuni hizi ambazo hubadilisha kanuni nyingine.

Madaraka ya mtawala Kwa nyongeza kuna mfululizo mwingine wa kanuni za kuweka mambo katika mizania ambazo Mwenyezi Mungu ameipa dini hii ya mwisho. Ayatullah Na'ini na Allamah Tabatabai, juu ya hili, wametegemea madaraka ambayo Uislamu umeipa serikali ongofu ya Kiislamu. Kanuni ya ijtihadi Mshairi na mwanafalsafa wa Kipakistani anasema kuwa Ijtihadi (kuzalisha sheria kutoka vyanzo vyake vya asili) ni nguvu ya hamasa ya Uislamu. Yuko sawa kusema hivyo. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kuwa Uislamu una sifa maalum ya kuruhusu Ijtihadi. Hakuna dini nyingine yenye sifa hii katika namna hii hii. Jengo la ndani la Uislamu limejengwa katika namna ambayo kwa msaada wa Ijtihadi, unaweza mara zote kwenda na mahitaji yanayobadilika katika maisha.

Abu Ali Ibn Sina (Avicenna) katika kitabu chake Al-Shifa, ameelezea haja ya Ijtihadi kuwa inatokana na kubadilika kila mara kwa mahitaji. Anasema kuwa hali za maisha mara zote zinabadilika. Matatizo mapya yanaibuka kila mara, lakini misingi ya Uislamu haibadiliki. Hivyo katika hali hii, lazima wawepo watu wanaojua sheria za kiislamu vizuri na mafundisho ya Kiislamu vizuri ili waweze kujibu maswali yote yanayoibuka katika kila zama na hivyo kukidhi mahitaji ya wakati. Katiba ya Iran inaamuru kuwa pawepo chombo cha mujtahidi wasiopungua watano (wanazuoni wakubwa wa Theolojia wanaoweza kufanya ijtihadi) kitakachokuwa kikichunguza sheria zinazopitishwa na serikali kila wakati.

Lengo hapa ni kuwa watu hawa (mujtahidi) kwa vile sio wapinga mabadiliko wala hawapingi maendeleo ya kisasa, wala sio limbukeni wala hawawafuati wengine kibubusa, waangalie na kudhibiti mfumo wa sheria wa nchi. Inapaswa kueleza kuwa ijtihad kwa namna halisi ina maana kubobea na inahitaji uelewa wa ndani sana wa misingi ya Uislamu na nguzo zake na elimu kubwa kabisa ya kanuni za fikihi ya Kiislamu, ambayo si kila mtu aliyesoma Uislamu kwa muda fulani anaweza kudai kuwa mujtahid.

Hapana shaka kuwa hii ni kazi ya umri mzima wa mtu ili kubobea katika kanuni na mafundisho ya Uislamu, na mbali na kipaji, nia na akili, inahitaji pia msaada wa Mungu. Mbali na kubobea (kwenye mchepuo maalum) na Ijtihad, baadhi ya watu wanaweza kupata elimu na kufikia kiasi kwamba maoni yao yanaweza kuchukuliwa kuwa ni fatwa. Historia ya Uislamu inawataja watu hao ambao licha ya elimu yao kubwa na maadili yao ya hali ya juu walikuwa na hadhari kubwa, walipokuwa wakitoa maoni yao, juu ya masuala ya kisheria.


3

4

5

6

7

8

9

10

11

12

13