12
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
MIRATHI
Zama za kale mwanamke alikuwa harithi kitu na, hata aliporithi, alitendewa kama mtoto. Alikuwa hana haiba ya kisheria inayojitegemea. Kwa mujibu wa baadhi ya mifumo ya kisheria ya kale, mtoto wa kike alipata urithi lakini watoto wake hawakupata. Kwa upande mwingine, mtoto wa kiume sio tu anapata urithi yeye mwenyewe, bali pia watoto wake walirithi mali iliyoachwa na mababu zao. Baadhi ya mifumo mingine ya sheria ilimruhusu mwanamke kurithi lakini si kwa kupata asilimia maalum au kwa lugha ya Qur'ani 'gawio lililopangwa.' Walichokifanya ilikuwa ni kumruhusu mzazi kuusia kuwa apewe, kama muusiaji anataka.
Wanahistoria na wachunguzi wameeleza kwa kina aina mbali mbali za sheria zilizokuwepo kale, lakini kwa sasa hatutaki kwenda kwa undani zaidi. Kwa sasa ufupisho tulioueleza hapo juu unatosha. Kwa nini mwanamke alinyimwa urithi? Sababu kuu ya kumnyima mwanamke urithi ilikuwa ni kuzuia kuhama kwa mali kutoka familia moja kwenda nyingine. Kwa mujibu ya imani za kale, mchango wa mwanamke katika uzazi haukuwa wa thamani sana. Akina mama walitumika kama mifuko tu ambamo mbegu ya baba ilikua na kuwa mtoto.
Kwa sababu hii waliamini kuwa watoto wa mtoto wa kiume walikuwa sehemu ya familia lakini watoto wa mtoto wa kike hawakuwa sehemu ya familia yake, kwa vile walikuwa sehemu ya familia ya babu yao mzaa baba. Hivyo kama binti angepata urithi, hiyo ingemaanisha kuhamisha mali kwenda kwa watoto wake (binti), watoto ambao hawahusiani na familia ya marehemu.
Marehemu Dr. Musa Ameed anasema kuwa katika siku za kale dini na sio mahusiano mengine yoyote ya asili, ndio ilikuwa msingi wa uundwaji wa familia. Babu, mbali na kuwa mkuu wa kijamii wa watoto na wajukuu wake, pia alikuwa mkuu wao wa kidini. Utekelezaji wa sherehe za kidini na matendo ya ibada yalikabidhiwa kwa kizazi kinachofuatia kupitia kwa watoto wa kiume tu. Wahenga waliwaona wanaume peke yao kuwa ndiyo njia ya kuhifadhi na kuendeleza kizazi.
Baba wa familia mbali na kumpa maisha mwanaye wa kiume, pia alimkabidhi imani na matendo ya kidini. Kwa mujibu wa Maveda wa Kihindi na Wagiriki na sheria za kirumi, nguvu ya kizazi ilikuwa kwa wanaume tu, na hivyo dini za familia zilikuwa ni miliki ya wanaume pekee, na wanawake hawakuwa na usemi wowote isipokuwa kupitia kwa baba zao au waume zao. Kwa vile hawakuweza kushiriki katika utekelezaji wa sherehe na shughuli za kidini, basi walikosa faida na manufaa yote ya kifamilia. Hivyo mfumo wa urithi ulipokuja wanawake walitengwa.
Kutengwa kwa wanawake katika urithi kulikuwa na sababu nyingine pia, mojawapo ikiwa ni kuwa hawakuwa wakakamavu vya kutosha kuwa askari. Katika jamii ambazo ziliweka umuhimu mkubwa katika matendo ya kishujaa na nguvu ya kupigana, na mpiganaji alionekana kuwa bora kuliko watu laki moja wasio wapiganaji, mwanamke alinyimwa urithi kwa vile hakuwa na uwezo wa kupigana. Kwa sababu hii, Waarabu wa zama za kabla ya Uislamu, walikuwa hawakubali suala la mwanamke kurithi mali, maadamu kulikuwepo wanafamilia wa kiume hata kama kiukoo walikuwa ni ndugu wa mbali.
Hii ndio sababu walishangazwa sana Qur'ani iliposema wazi wazi kuwa;
(Suratul Nisa, 4:32). Ilipata kutokea wakati fulani ndugu yake na Hasan bin Thabit, mshairi maarufu, alifariki katika siku hizo, huku akiacha mke na binti zake wengi. Binamu zao wa mfumo dume waligawiana mali zote na hawakuwapa chochote mjane na binti zake. Mjane alilalamika kwa Mtume ambaye aliwaita ndugu wa mume. Walisema kuwa mwanamke hakuwa na uwezo wa kubeba silaha na kupigana na adui. Ni wanaume waliojilinda wao na wanawake. Hivyo ni wao tu waliokuwa na haki ya kurithi mali.
Walipofikia hapo Mtume akawasomea amri ya Allah, kama ilivyo katika Aya hiyo hapo juu. Urithi wa mtoto wa kiume wa kupanga. Waarabu wa kipindi cha kabla ya Uislamu wakati fulani walimfanya mtu fulani kuwa mtoto wao wa kiume wa kupanga. Mtoto huyu wa kupanga kama mtoto halisi, alichukuliwa kuwa mrithi. Mila ya kujipatia watoto wa kupanga ilikuwepo katika mataifa mengine pia kama vile Urumi na Iran.
Mtoto wa kiume wa kupanga, kama ilivyo kwa mtoto halisi alikuwa na haki zote ambazo mabinti halisi wa kuzaliwa hawakuwa nazo. Haki hizi zilikuwa ni pamoja na haki ya kurithi. Halikadhalika kumuoa mke wa mtoto wa kupanga hakukuwa kunaruhusiwa. Qur'ani Tukufu ilipiga marufuku mila hizi. Urithi wa mshirika Mila nyingine, iliyokuwa ya kawaida miongoni mwa Waarabu wa kabla ya Uislamu ilikuwa ni ile ya ushirika (alliance). Watu ambao hawakuwa na uhusiano wa damu walikula yamini ya undugu kuwa; "Damu yako ni damu yangu, uchokozi wowote dhidi yako utakuwa ni uchokozi dhidi yangu; utarithi mali yangu na mimi nitarithi mali yako."
Kwa mujibu wa ushirika huu, makundi yote yalikuwa yakiwajibika kumlinda mshirika wake katika kipindi chote cha uhai wao, na mmoja wao alipokufa, mshirika aliyebaki alichukua mali za marehemu. Mke kama sehemu ya mirathi. Wakati fulani zama za kabala ya Uislamu, Waarabu walikuwa wakimhesabu mjane kuwa sehemu ya mali ya mume aliyefariki na hivyo, yeye pia alirithiwa.
Ikiwa marehemu alikuwa na mtoto wa kiume kutoka kwa mke mwingine, huyo alikuwa na uwezo wa kumrushia mjane kipande cha nguo kama ishara ya kumrithi. Baada ya hapo alikuwa na uhuru wa kumwamulia atakavyo au kumfanya vyovyote apendavyo kwa raha zake. Alikuwa na hiari ya ama kumuoa yeye mwenyewe au kumuozesha kwa mtu mwingine na yeye kuchukua mahari. Mila hii ambayo haikuwepo miongoni mwa Waarabu peke yao ilipigwa marufuku na Qur'ani.
Kuhusiana na suala hili la mirathi katika madaraja mbali mbali, sheria za jamii za kale za Wahindi, Wajapan, Warumi, Wagiriki (wayunani) na Wairani zilikuwa ama haziruhusu wanawake kurithi au zilikuwa zinawabagua (yaani walikuwa wanapewa kidogo sana). Kutokana na uchache wa nafasi hatuwezi kuyaandika hapa yote yaliyoandikwa na wataalamu wa fani hii. Mila ya kuwarithi wanawake katika kipindi cha Sasania. Hayati Saeed Nafisi katika kitabu chake, 'Social History of Iran from the Sasanian times to the end of the Ummayad period' ameandika kuwa; "Tabia nyingine ya kuvutia au kushangaza ya utamaduni wa Wasasania ilikuwa ya kwamba mvulana alipobaleghe, baba yake alimuozesha mwanae huyo mmoja wa wake zake wengi (wa baba huyo).
Katika zama hizo mwanamke hakuwa na haki yoyote ya kisheria. Baba na mume walikuwa na madaraka makubwa sana juu ya mali ya mwanamke. Lilikuwa ni jukumu la baba au mkuu wa familia kumuoza binti yake alipofikia umri wa miaka 15. Lakini umri wa kuoa kwa wavulana ulikuwa miaka 20. Baada ya kuolewa binti huyo hakuwa na haki ya kurithi mali ya baba yake au mlezi wake.
Hakuwa na haki ya kuchagua mume, lakini alikuwa na hiari ya kufanya ndoa ya haramu ikiwa baba yake alishindwa kumuoza baada ya kuwa amevunja ungo. Katika hali hiyo, pia hakuruhusiwa kurithi chochote kutoka kwa baba yake. Hapakuwa na kikomo cha idadi ya wanawake ambao mwanaume angeweza kuoa. Kumbukumbu za Wagiriki zinaonyesha kuwa mume alikuwa akimiliki mamia ya wanawake katika nyumba yake.
Vitabu vya kidini vya Wazoroastria vinaonyesha kuwa kanuni za ndoa katika zama za Sasania zilikuwa tata na zilizokorogeka. Urithi wa mwanamke katika Uislamu. Sheria ya mirathi ya Kiislamu imeepukana na mapungufu yote ya huko nyuma. Kitu kinachopingwa na wale wanaodai kutetea usawa kati ya mwanaume na mwanamke, ni kwamba gawio la mwanamke ni nusu ya gawio la mwanaume.
Kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu mtoto wa kiume hupata mara mbili ya mtoto wa kike, kaka hupata mara mbili ya dada yake na mume hupata mara mbili ya kile anachopata mke wake. Gawio la baba na mama ndio halifuati utaratibu huu. Ikiwa marehemu ana watoto, na wazazi (wa huyo marehemu) wako hai, kila mmoja wa wazazi wawili atapata moja ya sita ya mali iliyoachwa na marehemu. Ni kutokana na nafasi maalum ya mwanamke katika mahari, matunzo, huduma za kijeshi na baadhi ya sheria za jinai ndio maana gawio lake limefanywa kuwa nusu ya lile la mwanaume.
Kwa sababu zilizotajwa hapo awali, Uislamu unachukulia matunzo na mahari kuwa ni mambo muhimu na ya lazima katika kuiimarisha ndoa. Yanatoa hakikisho la maelewano na masikilizano. Kuyaondoa ni kulitikisa jengo zima la familia na kumsukumia mwanamke katika umalaya. Kwa vile mahari na matunzo ni wajibu wa lazima wa mume, basi ni wazi kuwa majukumu ya kifedha ya mwanamke yamepunguzwa sana na mzigo wa mwanaume umeongezwa. Ili kufidia jukumu zito alilonalo mwanaume, gawio lake la urithi limepangwa kuwa mara mbili ya lile la manamke.
Ni mahari na matunzo yaliyopunguza gawio la mwanamke. Pingamizi la wa-Magharibi. Baadhi ya watu wa Magharibi wanapokosoa udogo wa gawio la mwanamke la urithi na wanapolitumia hili kama silaha ya propaganda dhidi ya Uislamu, wanadai kuwa hakuna ulazima wowote wa kupunguza gawio la mwanamke ili kuja kulifidia kwa mahari na matunzo. Je, kuna haja yoyote ya kupita vichochoroni na kuzunguka vichaka? Kwanini gawio la mirathi la mwanamke lisilingane na gawio la mwanaume ili tusilazimike kulifidia kwa mahari na matunzo?
Hawa mabwana ambao wanaonekana kumpenda mfalme kuliko mfalme mwenywe anavyojipenda wamechanganya habari. Sababisho wamelipeka kwenye matokeo na matokeo wameyapeleka kwenye sababisho. Wanafikiri kuwa mahari na matunzo ni matokeo ya nafasi ya pekee kuhusiani na urithi, wakati ambapo ukweli ni kinyume chake. Aidha, wanaelekea kuwa na mawazo kuwa kipengele cha fedha ndio kitu pekee kinachozingatiwa, kama hiki kingekuwa ndio kigezo pekee basi kusingekuwa na haja ya mfumo wa mahari na matunzo wala mfumo unaotoa tofauti ya gawio kati ya mwanaume na mwanamke.
Kama tulivyoeleza mwanzo, Uislamu umezingatia vipengele vingi, vingine ni vya asili na vingine ni vya kisaikolojia. Umezingatia mahitaji maalumu ya mwanamke, yanayotokana na jukumu lake la uzazi. Kimsingi mwanaume hana mahitaji hayo. Mbali na hayo, kwa upande mwingine, uwezo wa mwanamke wa kuzalisha ni mdogo kuliko wa mwanaume na kwa upande mwingine matumizi yake ni makubwa kuliko ya mwanaume.
Kwa nyongeza, kuna vipengele vingine mbali mbali vya kujirembesha kuhusiana na mfumo wa akili zao. Kwa mfano mwanaume mara zote hupenda kutumia fedha zake kwa ajili ya mwanamke anayempenda. Vipengele vingine vya kisaikolojia na kijamii, vinavyosaidia kuimarisha mahusiano ya kifamilia pia vimezingatiwa. Kwa kuzingatia nukta zote hizi, Uislamu umefanya mahari na matunzo kuwa ni wajibu wa lazima. Hivyo sio suala la pesa, ambalo inaweza kusemwa kwamba kuna haja ya kupunguzwa mgao wa mwanamke sehemu moja na kumfidia sehemu nyingine. Pingamizi la waasi wa kipindi cha awali cha Uislamu. Tumesema kuwa mahari na matunzo ni sababisho na nafasi ya pekee ya mwanamke na tofauti zilizopo katika mirathi ni matokea yake. Nukta hii haijaanzishwa leo. Ilikuwepo hata katika siku za awali za Uislamu.
Katika karne ya pili Hijria alikuwepo mtu mmoja aliyeitwa Ibn Abi alAwja, ambaye hakuwa akiamini juu ya dini. Kwa kutumia fursa ya uhuru wa kidini (imani) ya wakati ule alikuwa akielezea waziwazi mawazo yake ya kikafiri. Wakati fulani alikuwa akija katika Masjid al-Haram (Makka) au Masjid Nabawi (Madina) na alikuwa akijibizana na wanavyuoni wa wakati ule juu ya kanuni za Uislamu.
Moja ya pingamizi lake dhidi ya Uislamu lilihusu mirathi. Alikuwa akisema; "Ana kosa gani huyu mwanamke maskini anayepata sehemu moja wakati mwanaume anapata sehemu mbili." Kwa mujibu wake yeye hii ilikuwa ni dhulma kwa mwanamke. Imam Jafar as-Sadiq
katika kumjibu alisema kuwa:
Na zaidi ya hilo Uislamu umemuamrisha mwanaume kulipa mahari na kumtunza mkewe na katika baadhi ya kesi za jinai ambapo ndugu wa mhalifu walipaswa kulipa fedha za damu (kufidia mtu aliyeuliwa) mwanamke aliondolewa (alisamehewa) katika malipo hayo. Hizi ndio sababu zilizofanya gawio lake lipunguzwe. Hivyo Imam Jafar Sadiq
alieleza wazi wazi nafasi ya pekee ya mwanamke juu ya mirathi, sheria ya mirathi na matunzo, kusamehewa kwake kutoa huduma ya jeshi na malipo ya fedha za damu. Maimamu wengine pia walijibu hivyo hivyo walipoulizwa swali hilo.
13
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
I- TALAKA
Hakuna zama kama hizi za kwetu ambapo uzingativu umefanywa sana kwenye hatari ya kusambaratika kwa familia na madhara yake. Na tena, hakuna zama kama hizi za kwetu ambapo mtu amekabiliana na hatari halisi ya kusambaratika huko. Kuongezeka kwa Talaka katika maisha ya kisasa. Huko nyuma uzingativu sana haukuwekwa katika tatizo la talaka, sababu zake na madhara yake pamoja na mbinu za kulizuia vilikuwa havijadiliwi sana na bado idadi ya talaka ilikuwa ndogo sana. Hakuna shaka kuwa ongezeko la talaka hivi sasa ikilinganishwa na zamani linatokana na kuongezeka kwa sababu za talaka.
Maisha ya kijamii yamebadilika mno kiasi cha kuwa sasa kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kuvurugika kwa familia, na hii ndio sababu jitihada za wasomi na watu wanaoshughulikia masuala ya kijamii zimeshindwa kuzaa matunda. Inasikitisha kuwa kizazi kijacho kinakubaliwa na hatari zaidi. Gazeti la Kimarekani, 'Newsweek' katika makala inayovutia yenye kichwa cha habari 'Divorce in America' (Talaka katika Marekani) linaandika kuwa ukiwa Marekani ni rahisi zaidi kupata talaka kuliko kupata taksii.
'Newsweek' linaandika zaidi kuwa methali mbili kuhusu talaka zinajulikana zaidi miongoni mwa Wamarekani kuliko methali nyingine zozote zile. Mojawapo ni kuwa 'Usuluhishi mgumu kabisa kati ya mume na mke ni bora kuliko talaka.' Methali hii ina umri wa miaka 400 na zaidi. Ya pili ambayo imebeba ujumbe ulio kinyume na hii methali ya kwanza imepata umaarufu katika nusu ya pili ya karne ya 20. Inasema kuwa 'penzi la pili ni tamu zaidi kuliko la kwanza." Makala inaonyesha kuwa methali ya pili ndiyo inayofanya kazi zaidi nchini Marekani. Jinamizi la talaka linajivutia kwake, sio kwa ndoa mpya tu, bali hata za mama zao na za wanandoa waliooana zamani huko.
Tangu wakati wa Vita vya pili vya Dunia na kuendelea, kwa wastani idadi ya talaka kwa mwaka si chini ya laki nne (400,000). Katika hizo ndoa zilizovunjika, 40% zilikuwa zimeweza kudumu kwa miaka kumi na zaidi na 13% ndizo zilikuwa zimeweza kudumu kwa zaidi ya miaka 20. Wastani wa umri wa talaka (umri wa wanawake wanaotalikiwa) wa wanawake milioni mbili ilikuwa ni miaka 45, 62% ya hao walikuwa na watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 wakati ndoa ilipokuwa inavunjika. Wanawake hawa, kwa kusema kweli, wanaunda kizazi maalum.
Ingawa mwanamke wa Kimarekani hujisikia huru kabisa baada ya talaka, lakini bado hao waliotalikiwa, wawe vijana au wa umri wa kati, huwa hawana furaha. Kutokuwa kwao na furaha kunaweza kupimwa kutokana na ongezeko la idadi ya wanawake wanaowaita madaktari wa akili au ambao ni walevi wa kupindukia. Katika kila wanawake wanne, mmoja ni mlevi.
Idadi ya wanawake waliotalikiwa wanaojinyonga ni kubwa mara tatu kuliko ya wale wenye waume. Kwa kifupi ni kuwa mara tu mwanamke anapoibuka mshindi katika mahakama ya talaka hugundua kuwa maisha baada ya talaka sio kitanda cha maua ya waridi. Ni vigumu ulimwengu kuwa na maoni mazuri juu ya mwanamke anayeivunja ndoa yake, nyumba thabiti kabisa ya mahusiano ya mwanadamu. Jamii inaweza kumheshimu mwanamke huyo na pengine kumuonea wivu, lakini haiwezi kumuona kuwa ni mtu aliyeingia katika maisha ya mtu na kumletea furaha (mumewe).
Katika makala hii ya gazeti la Newsweek suali limeibuka kuwa ongezeko hili la talaka linalozidi kukua linatokana na mwenendo usio kubaliana kati ya mume na mke, au sababu nyingine. Mwandishi wa makala hii amesema kuwa hata kama tofauti za tabia na kutopatana zitakubaliwa kuwa sababu ya kutengana kwa wanandoa waliooana hivi punde, nini tunaweza kusema juu ya talaka za wanandoa walioishi ndani ya ndoa kwa muda mrefu?
Tukizingatia msaada wa kisheria unaotolewa na sheria ya Marekani kuhusiana na talaka, tunaweza kusema kuwa kutofautiana kwa mihemko na tabia sio sababu ya kutengana kwa wanandoa walioishi kwa miaka kumi au zaidi. Katika zama za vidonge vya kuzuia mimba, mapinduzi ya ngono (ufuska) na kuboreka kwa hadhi yao ya kisheria, wanawake wengi wametokea kuamini kuwa furaha na raha ni bora kuliko uimara wa maisha ya ndoa.
Mara nyingi unaweza kuona kuwa mume na mke wanaishi pamoja kwa miaka, wana watoto, kila mmoja anashiriki furaha na huzuni ya mwenzake lakini ghafla mke anaomba talaka bila ya kuwepo mabadiliko yoyote ya ki-mali au hadhi na makubaliano ya mume. Sababu ni kuwa, mpaka jana, mwanamke alikuwa tayari kuvumilia uchoshi wa maisha, lakini hayuko tayari kufanya hivyo leo.
Ongezeko la kesi za talaka haliko Marekani peke yake. Sehemu yoyote ambayo utamaduni wa Kimagharibi umejipenyeza kwa kiasi fulani, kiwango cha talaka kiko juu. Hata katika nchi za Mashariki, talaka imekuwa ni jambo la kawaida zaidi katika miji mikubwa ya kisasa kuliko katika miji midogo na vijiji. Mazingira yanayochangia talaka nchini Marekani. Tayari tumeshalinukuu gazeti la Newsweek likisema kuwa mwanamke wa kimarekani hujali zaidi starehe na burudani kuliko uthabiti na uimara wa maisha ya familia.
Sasa hebu tupige hatua moja mbele ili tuone kwanini amechukua mwelekeo huo. Hapana shaka kwamba tabia hii sio ya asili wala ya kuzaliwa nayo. Imetokana na sababu fulani za kijamii. Ni mazingira ya Marekani yaliyosababisha akili hii ya mwanamke wa Kimarekani. Baadhi ya watu wa Magharibi wanafanya jitihada kubwa kumsukumia mwanamke wa Mashariki katika mwenendo wanaoufuata wanawake wa Kimarekani.
Kama wakifanikiwa majaaliwa ya mwanamke wa Mashariki na familia ya Mashariki hayatakuwa na tofauti na yale ya mwanamke wa kimarekani na familia ya Kimarekani. Gazeti maarufu la Ufaranza litolewalo kila siku linaandika kuwa katika migahawa zaidi ya 200 na nyumba za kulala wageni katika jimbo la Califonia, wafanyakazi (wahudumu) wa kike wanavaa nguo za nusu uchi. Nguo hizo ambazo ni za kuogelea zinatambuliwa kuwa ndio sare za kazini katika miji ya San-Fransisco na Los Angeles.
Katika jiji la New York kuna kumbi nyingi za sinema zinazoonyesha filamu za ngono tu, na picha za uchi za wanawake zinaweza kuonekana zikionyeshwa mbele ya milango ya kuingilia kumbini. Majina ya filamu za ngono ni ya aina hii; "Wanaume wanaobadilishana wake zao', 'Wasichana wasio na maadili,' 'Magauni ambayo hayafichi chochote.' Maktaba kuna vitabu vichache sana vya hadithi za kubuni (fiction books) ambavyo katika majalada yake hakuna picha za wanawake walio uchi.
Majina ya vitabu kama vile 'Tabia ya ngono ya wanaume wa kimarekani,' 'Tabia ya ngono ya wanaume wa Kimagharibi,' Tabia ya ngono ya vijana walio chini ya miaka 20,' 'Mbinu mpya za ngono zilizotokana na habari mpya kabisa," vimekuwa maarufu na vingi mno. Mwandishi wa makala katika gazeti hili la Kifaransa anauliza kwa mshangao na wasiwasi; "Marekani unakwenda wapi?' Katika mazingira kama haya ikiwa mwanamke wa Kimarekani amepoteza mizania yake na anajali burudani na raha zaidi kuliko uaminifu kwa mume wake na familia, hawezi kulaumiwa. Ni mazingira ya kijamii ambayo yameharibu kila mzizi wa mfumo wa utakatifu wa familia.
Inashangaza kuwa viongozi wa zama zetu wanazipa nguvu na msukumo zaidi sababu zinazosababisha talaka na kusambaratika kwa maisha ya familia na kwa upande mwingine wanapiga mayowe na kelele kuwa kiwango cha talaka kimekuwa kikubwa mno. Hii ni sawa na kumwambia mtu afagie bohari na kuomba asichafue nguo zake. Nadharia tano. Hebu tuangalie, iwapo kimsingi talaka ni nzuri au mbaya. Swali ni je ni jambo zuri kuuacha wazi mlango wa talaka, hata katika hatari ya kusambaratika kwa maisha ya familia? Ikiwa ni jambo zuri basi hakuna tatizo hata kama kiwango cha talaka kitakuwa kikubwa.
Na ikiwa sio jambo zuri, je talaka ipigwe marufuku kabisa na ndoa ifanywe kuwa ya milele? Wazo la tatu ni kuwa talaka isipigwe marufuku kisheria, kwani katika baadhi ya hali haiepukiki, lakini wakati huo huo jamii ichukue kila hatua inayowezekana kuondosha sababu za mikwaruzano na kutengana kwa mume na mke na hivyo kuwanusuru watoto kukosa familia.
Ni dhahiri kuwa sheria peke yake haiwezi kufanya chochote ikiwa jamii yenyewe inazipalilia sababu zinazosababisha talaka. Ikiwa talaka haifai kupigwa marufuku kabisa, je iruhusiwe katika muundo gani? Je ni nani awe na mamlaka ya kutoa talaka? Mwanaume peke yake, mwanamke peke yake au wote? Na wazo la mwisho ni kuwa je mwanaume na mwanamke wote wafuate taratibu zinazofanana katiksa kutoa au kuomba talaka au kila jinsia iwe na utaratibu wake?
Yote kwa yote, hizi ni nadharia tano zinazohusiana na Talaka: Talaka inayotolewa bila kikwazo chochote cha kisheria au kimaadili. Hawa ni wale wanaoitazama ndoa kwa mtazamo wa kupata raha tu, ambao hawaipi utakatifu wowote, na ambao hawajali thamani ya kijamii ya familia. Wanafikiri kuwa mara tu baada ya ndoa kuvunjika na ndoa mpya kuchukua nafasi ya ndoa ya zamani (iliyovunjilka) wanaume na wanawake walioachana hupata furaha zaidi.
Yule anayesema kuwa penzi la pili ni tamu kuliko penzi la kwanza ndiye huiunga mkono nadharia hii. Katika nadharia hii, sio tu kwamba thamani ya kijamii ya kifamilia imesahauliwa lakini pia furaha na kuridhishana kunakosababishwa na ndoa kumepuuzwa pia. Hivyo nadharia hii ni ya kipuuzi na ya kitoto kabisa. Ndoa ni taasisi takatifu. Ni muungano wa mioyo na roho, taasisi ambayo lazima itunzwe kwa usalama na isiharibiwe.
Neno talaka linapaswa kuondolewa kutoka katika kamusi ya jamii ya wanaadamu. Mwanaume na mwanamke wanaooana lazima wajue kuwa hakuna kitakachowatenganisha zaidi ya kifo. Hii ndio nadharia ambayo imekuwa ikitetewa na Kanisa Katoliki kwa karne nyingi na bado inatetewa. Wanaoiunga mkono nadharia hii wanazidi kupungua dunaini.
Hivi sasa ni Italia na Hispania tu wanoifuata. Ni mara nyingi tu tunasikia kwamba, hata Italia, wanaume na wanawake wanaipinga sheria hii na jitihada zinafanyika ili sheria ya talaka itambuliwe rasmi. Watu wengi hawako tayari kuendelea kutaabika na michosho ya ndoa zao zisizo na mafanikio. Miaka kadhaa huko nyuma, gazeti la 'The Daily Express' lilichapisha makala yenye kichwa cha habari, 'Ndoa Italia ina maana kifungo kwa mwanamke.' Makala hii ilisema kuwa, hivi sasa kutokana na kutokuwepo kwa talaka, watu wa Italia wanajiingiza katika mahusiano ya haramu (zinaa). Zaidi ya Waitalia milioni tano walikuwa wakiamini kuwa maisha yao yamejaa madhambi. Gazeti la Italia litolewalo kila siku liliandika kuwa kuzuia talaka kumesababisha tatizo kubwa sana kwa Waitalia. Wengi wao walilazimika kuukana uraia wa Italia kwa sababu hiyo.
Taasisi fulani ya Italia ilipoitisha kura ya maoni, 97% ya wanawake wa Italia walijibu 'hapana' kwa swali lililoulizwa kuwa iwapo talaka ilikuwa ni jambo linalochukiza katika kanuni za dini. Bado kanisa linashikilia msimamo wake na kuendelea kutoa hoja kuutetea (msimamo huo). Hapana shaka yeyote kuwa ndoa ni taasisi takatifu na inatakiwa idumu. Lakini inaweza tu kudumu iwapo wanandoa wote wawili wanashirikiana. Kuna hali ambapo maelewano kati ya mke na mume huwa hayawezekani.
Katika hali kama hizi nguvu za sheria haziwezi kuwapatanisha na kuwaunganisha kwa jina la muungano wa ndoa. Nadharia ya kanisa imeshindwa kabisa kufanya kazi. Sio ajabu muda si mrefu kanisa lenyewe likabadilisha msimamo wake. Hivyo hatuhitaji kuijadili nadharia hii zaidi. Ndoa inaweza kuvunjwa na mwanaume sio mwanamke.
Katika ulimwengu wa zamani watu wengi walikuwa na mtazamo huu, lakini sasa hatudhani kuwa una wafuasi. Hivyo hatuhitaji kuijadili pia. Ndoa ni taasisi takatifu na mfumo wa kifamilia unaheshimika, lakini mlango wa kutoa talaka kwa masharti fulani, uwe wazi kwa wanandoa wote na taratibu za kuvunja ndoa zinapaswa zifanane kwa jinsia zote mbili.
Watetezi wa kufanana kwa haki za familia ambao kwa makosa walikuita usawa wa haki kati ya mwanaume na mwanamke, wanaiunga mkono nadharia hii. Kwa mujibu wa watu hawa, masharti yanayofanana, mipaka inayofanana na vikwazo vinavyofanana vinapaswa vitumike kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume wakati wa kuvunja ndoa. Wanapinga suluhishi jingine ambalo ni la kidhalimu na linalobagua.
Hapana shaka ndoa ni taasisi takatifu, mfumo wa familia unaheshimika, talaka ni jambo linalochukuza na ni jukumu la jamii kuondoa visababisho vyote vya talaka, lakini bado talaka haiwezi kuzuiwa moja kwa moja na kwamba mamlaka ya kutoa au kuomba talaka yapo kwa wote wawili, mwanamke na mwanaume. Hata hivyo utaratibu wa kufuatwa katika uvunjaji wa ndoa uwe tofauti kati ya jinsia hizi mbili. Talaka ni moja ya haki zisizofanana (lakini zinazolingana) kati ya mwanaume na mwanamke. Hii ndio nadharia inayowakilisha maoni ya Uislamu na nchi za Waislamu zinaifuata.