HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU0%

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU Mwandishi:
: AZIZI NJOZI
Kundi: Wanawake

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi: Allamah Shahid Murtaza Mutahhari
: AZIZI NJOZI
Kundi:

Matembeleo: 46930
Pakua: 4705

Maelezo zaidi:

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 33 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 46930 / Pakua: 4705
Kiwango Kiwango Kiwango
HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

15

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

III - TALAKA

Tumesema kwamba kwa mtazamo wa Uislamu, talaka ni jambo linalochukiza. Uislamu unataka ndoa iwe imara na idumu. Tuliibua swali kuwa ikiwa talaka inachukiza, kwa nini Uislamu haujaipiga marufuku? Je Uislamu haukupiga marufuku vitendo vyote vinavyochukiza kama vile kunywa pombe, kucheza kamari, ukatili n.k? Kama jibu ni ndiyo, sasa kwa nini Uslamu haujaiharamisha kabisa talaka kisheria? Kimsingi inapingana na mantiki kusema kuwa talaka inaruhusiwa na wakati huo huo inachukiza. Kama inaruhusiwa, vipi inaweza kuchukiza? Kama inachukiza vipi inaweza kuruhusiwa? Uislamu kwa upande mmoja unamkunjia uso mtu anayemtaliki mke wake na wakati huo huo haumuwekei kikwazo cha kisheria (cha kutoa talaka), kwa nini?

Ni swali la busara sana, na ni ufunguo wa siri zote za tatizo la talaka. Kwa kusema kweli, ndoa ni uhusiano wa asili na sio uhusiano wa kimkataba. Maumbile yameweka sheria maalum kwa ajili yake. Mikataba mingine ya kijamii kama vile ya mauzo, ya ajira, rehani ya amana, ya uwakili n.k. Si lolote zaidi ya makubaliano ya kijamii. Hayana mkono wa maumbile na silika. Sheria ya maumbile haiingilii mikataba hii. Lakini kinyume chake, mkataba wa ndoa una utaratibu maalum. Umeundwa na matamanio ya asili ya pande mbili.

Kwa hiyo, haishangazi kuona kuwa mkataba wa ndoa una kanuni zake maalum ambazo ni tofauti na zile za mikataba mingine yote. Sheria za maumbile katika ndoa na talaka. Katika jamii ya kiraia, sheria za asili pekee ni sheria ya uhuru na usawa, sheria ambayo juu yake hujengwa sheria nyingine zote za kijamii. Lakini katika mkataba wa ndoa, mbali na kanuni za jumla za uhuru na usawa, maumbile yametoa sheria nyingine pia, ambazo lazima zizingatiwe katika suala la ndoa, mahari, matunzo na mwisho talaka. Hakuna faida yoyote kuyapuuza maumbile.

Kama Alexis Carrel alivyoonyesha, sheria za kibaiolojia na sheria nyingine za maisha (asili) ni ngumu, katili na zisizozuiliwa kama sheria za kinajimu. Ndoa maana yake ni kuambatana na ni muungano, na talaka maana yake ni kutengana. Maumbile yamesanifu sheria ya maumbile katika namna ambayo mwanaume hutenda mambo kwa nia ya kumpata mwanamke, na mwanamke hujiondoa (hukataa kataa) kwa nia ya kumvutia na kumpotosha mwanaume. Mwanaume hutaka kuumiliki mwili wa mwanamke na mwanamke hutaka kuuteka moyo wa mwanaume.

Msingi wa ndoa umejengwa juu ya upendo, muungano na kuhurumiana na ushirikiano na uswahiba peke yake. Katika jengo la familia, jinsia ya kike huchukua nafasi muhimu na jinsia ya kiume huchukua nafasi ya pembeni. Kutokana na yote haya ni dhahiri kuwa maumbile lazima yatakuwa yameweka kanuni maalumu kwa ajili ya uvunjaji wa maisha ya familia pia. Hapo awali tulimnukuu msomi mmoja akisema kuwa kutafuta mwenzi maana yake ni kushambulia (kwa upande wa mwanaume) na kuteka nyara na kujifaragua kwa mwanamke kwa nia ya kumpendeza na kumdanganya.

Kwa mwanaume ambaye yeye kwa asili ni kama mnyama mwindaji, vitendo vyake ni vya kichokozi na kwake mwanamke ni medali ambayo lazima aipate. Kutafuta mwenzi ni mapambano na ndoa ni kunyakua na kumiliki. Mkataba ambao umejengwa juu ya upendo na hisia za umoja hauwezi ukashinikizwa kwa nguvu.

Sheria inaweza kuwalazimisha watu wawili kuuheshimu mkataba wao kwa msingi wa kushirikiana na usawa lakini haiwezi kuwalazimisha kupendana, kuwa waaminifu kila mmoja kwa mwenzake, kila mmoja kujitolea kwa ajili ya mwenzake na kila mmoja kushiriki furaha za mwenzake. Kama tunataka kudumisha uhusiano huu kati ya watu wawili, tunapaswa kutumia mbinu na njia nyingine tofauti na sheria.

Kwa mujibu wa mpangilio wa asili wa ndoa, ambao juu yake ndio sheria za Kiislamu zimejengwa, mke hushika nafasi ya mtu anayestahiki upendo na heshima katika familia. Ikiwa kwa sababu fulani fulani atapoteza nafasi hii na akanyimwa upendo na mapenzi ya mume wake, msingi wa jengo la familia huanguka chini na utaratibu wa asili huparanganyika. Uislamu huiangalia hali hii kwa huzuni, lakini Uislamu hauwezi kuendelea kufikiri kuwa ndoa bado iko hai hata baada ya kusambaratika kwa msingi wake wa asili.

Uislamu umechukua hatua maalum ili kuhakikisha kuwa maisha ya familia yanabaki katika hali yake ya asili, yaani mke atabaki katika hali ya kupendwa na kuhitajika, na mume abaki na hisia za kumpenda mkewe na awe tayari kumhudumia. Uislamu umemhimiza mwanamke ajipambe na kujiremba sana ili kumridhisha mume wake, kuonyesha utimilifu wake kwa ajili ya mumewe, kumkidhia matamanio yake ya asili na kuepuka kumkera kwa ujeuri na kiburi. Pia umemhimiza mwanaume kumpenda mke wake, kuwa mpole kwake na kushikamana naye na asiufiche upendo wake kwa mkewe.

Hatua hizi zimechukuliwa ili kuifanya furaha ya ngono ibakie katika wigo wa familia na kuifanya jamii ya nje ya familia kujishughulisha na kazi na shughuli nyingine badala ya ngono (yaani ngono iwe nyumbani tu, nje ya nyumbani iwe ni sehemu ya kazi na shughuli nyingine). Uislamu unataka mahusiano ya jimai (ngono) yawe masafi na yasiyo na uchafu. Hatua zote hizi zimechukuliwa kwa nia ya kuifanya taasisi ya familia iepukane na hatari ya kuvunjika na kusambaratika. Nafasi ya asili ya mwanaume katika maisha ya familia. Kwa mtazamo wa Uislamu, ni matusi kabisa kwa mwanamke kwamba sheria imlazimishe kuishi na mwanaume asiyempenda.

Sheria inaweza kumlazimisha mwanamke kuishi na mwanaume fulani lakini haiwezi kumhakikishia kuwa atapata nafasi muhimu kabisa katika familia, nafasi ambayo anastahili. Sheria inaweza kumlazimisha mwanaume kumhudumia mke wake lakini haiwezi kumlazimisha kuwa mume anayejali. Hivyo, upendo wa mwanaume unapopoa, ndoa hupoteza mwelekeo kwa mtazamo wa maumbile. Hapa swali jingine linaibuka. Je, upendo wa mwanamke ukipoa, maisha ya familia yataathirika? Je maisha ya ndoa yataendelea kama yalivyo au yatafikia kikomo. Kama yatabaki salama, sasa inakuwaje kwamba ukose fu wa upendo kwa upande wa mume huvunja ndoa lakini ukosefu wa upendo kwa upande wa mke hauvunji ndoa?

Je, kuna tofauti yeyote kati ya mwanaume na mwanamke? Kama ukosefu wa upendo kwa upande wa mke vile vile huvunja ndoa, basi ni dhahiri kuwa wanawake pia wanapaswa kuwa na haki ya kutoa talaka kama mwanaume. Kwa kusema kweli, mafanikio ya maisha ya familia hutegemea maelewano na masikilizano ya wote wawili, mume na mke. Lakini kama tulivyosema hapo awali kuna tofauti ya tabia ya akili (mentality) ya mwanaume na ile ya mwanamke. Huko nyuma tumeshanukuu maoni ya wanasayansi juu ya hili. Maumbile yamepanga kuwa mapenzi ya kweli na ya dhati ya mwanamke huja tu kama mwitikio wa upendo wa dhati wa mwanaume. Hivyo mapenzi ya mwanamke kwa mwanaume ni matokeo ya upendo wa dhati wa manaume.

Maumbile yamemkabidhi mwanaume funguo za udhibiti wa mapenzi na maelewano yao. Ikiwa mwanaume anampenda mwanamke na ni mwaminifu kwake basi mwanamke pia humpenda na kubaki mwaminifu kwake, kwa kusema kweli uaminifu wa mwanamke ni mwitikio wa uaminifu wa mwanaume. Maumbile yameweka funguo za kuvunja ndoa mikononi mwa mwanaume. Ni kutojali kwa mwanaume na kutokuwa kwake mwaminifu kunakopoozesha mapenzi ya mwanamke.

Kwa upande mwingine, kutojali na kupuuzia kwa mwanamke hakumwathiri mwanaume lakini kinyume chake sio kweli. Mwanaume kupoteza upendo ni mwisho wa ndoa, lakini kwa mwanamke sio hivyo. Ikiwa mwanaume anajali na ni mwaminifu, mara zote anaweza kurejesha upendo wa mke wake kwa kumuonyesha upendo, upole na kujali. Sio matusi kwa mwanaume kumlazimisha kipenzi chake kwa msaada wa nguvu ya sheria, kuendelea kuishi naye, na kumshawishi polepole. Lakini si jambo linalovumilika kwa mke kutumia nguvu ya sheria ili kumrejesha mlinzi na kipenzi chake.

Mambo huwa hivi inapokuwa kutojali kwa mwanamke hakutokani na ukosefu wa maadili na ukatili wa mwanaume. Hawezi kuruhusiwa kutumia vibaya nafasi yake kumtesa au kumtendea vibaya mke wake. Tutaijadili nukta hii baadaye. Ilivyo, mwanaume anahitaji mwili wa mwanamke na mwanamke anauhitaji moyo wa mwanaume. Hiyo ndio tofauti kati ya hawa wawili. Ndoa huwa haina maana kwa mwanamke kama hapati ulinzi na mapenzi ya dhati ya mume wake. Maoni ya mwanasaikolojia wa kike. Hivi karibuni makala moja ilichapishwa na mwanamama mmoja mwanasaikolojia wa Kifaransa, Beatrice Maryo, ambaye ana shahada ya udaktari na anafanya kazi kama daktari wa akili katika hospitali ya Paris.

Yeye mwenyewe ni mama wa watoto watatu. Katika makala hii ameelezea vizuri sana ni jinsi gani mwanamke mwenye mimba au anayenyonyesha anavyohitaji upole na upendo wa mume wake. Anasema kwamba; "Kuanzia wakati mwanamke anapoanza kuhisi kuwa muda si mrefu atakuwa mama, huanza kuutafiti mwili wake. Huutazama kila mara na kuunusa, hasa inapokuwa ni mtoto wake wa kwanza. Huhisi udadisi mwingi juu yake mwenyewe kana kwamba yeye ni mgeni wa mwili wake na hutaka kujijua (kujigundua) kwa mara ya kwanza. Anapohisi kutembea kwa mtoto kidogo katika tumbo lake, huanza kusikilizia kwa uangalifu kila sauti ya mwili wake.

Kuwepo kwa mtu mwingine katika mwili wake humfanya asikie furaha sana kiasi cha kutaka kujitenga na kupumzika. Hutaka abaki peke yake na kitoto chake kidogo, ambacho bado hakijaja katika ulimwengu huu. "Wanaume, katika kipindi cha ujauzito wa wake zao, wana majukumu muhimu ya kufanya, lakini kwa bahati mbaya sana, mara nyingi huyakwepa majukumu haya. Mama mtarajiwa huhitaji kuhisi kuwa mume wake anamwelewa, anampenda, na anamlinda.

Vinginevyo, anapoona tumbo lake limevimba, kuvutia kwake kumetoweka, homa za asubuhi zimeanza, na anaogopa uchungu wa uzazi, atamlaumu mume wake, aliyempa mimba na kumsababishia matatizo na taabu zote. Ni jukumu la mume kujiweka karibu zaidi na mke wake mara nyingi zaidi kuliko kipindi kingine chochote katika miezi yake ya ujauzito. Familia yote inahitaji baba mpole na anayejali ambaye mke na watoto watamweleza matatizo yao, huzuni zao na furaha zao.

Hata kama maongezi yao sio ya maana bado ni muhimu baba kuyasikiliza. "Mwanamke mjamzito hutaka sana watu wote wamuongelee mtoto wake. Mwanamke huona fahari kuwa mama. Lakini anapoona mume wake hamjali mtoto, hisia yake ya fahari hubadilika na kuwa hisia ya dharau. Huchukia kuwa mama na kuwa mjamzito, na huwa ni aina ya udhalilishaji kwake. Inafahamika kuwa akina mama hawa hupata uchungu mkubwa wakati wa kujifungua Uhusiano kati ya mama na mtoto sio wa pande mbili.

Ni uhusiano wa pande tatu; mama, mtoto na baba. Hata kama baba hayupo (ikiwa wamepeana talaka), bado ana jukumu muhimu katika maisha ya ndani ya mama yaani fikra na hisia zake pamoja na hisia ya umama (motherhood)" Haya ndiyo aliyoyasema mwanasaikolojia wa kike ambaye pia ni mama. Jengo lililojengwa juu ya msingi wa hisia za moyoni. Mwanamke hutegemea sana uaminifu, upole na ulinzi wa mume wake kiasi kwamba bila ya ku wepo ushirikiano wake wa dhati, basi hata mtoto mwanamke huyu huwa hamjali sana. Anaweza kuvumilia ugumu wa maisha kwa msaada wake tu (mumewe). Katika hali hii inawezekanaje kumlazimisha, kwa kutumia nguvu ya sheria kubaki ameshikamana na mwanaume ambaye hamtaki?

Je, sio kejeli kwamba kwa upande mmoja tunajenga mazingira ambayo kwayo wanaume wanawajali wake zao kidogo tu na wanamalizia ujana wao sehemu nyingine na kwa upande mwingine tunawatupa wake zao juu yao kwa nguvu ya sheria? Ukweli ni kuwa, Uislamu unataka mwanaume mwenyewe amtafute mwanamke, na ampende. Uislamu hautaki kumtupia mwanamke (yaani kumpatia mwanamke asiyempenda).

Ni kanuni ya jumla kuwa palipo na suala la mapenzi, kujitolea na uaminifu, hapawezi kuwa na kulazimishana kwa nguvu ya sheria. Ikiwa mume hampendi mke wake, linaweza kuwa ni jambo la kusikitisha lakini hakuna nguvu inayoweza kumfanya ampende. Hebu tutoe mfano mmoja. Kama tunavyojua, katika sala za jamaa kuna sharti kwamba kiongozi wa sala anaweza kuwa yule tu ambaye ni mchamungu na ambaye wafuasi wake wana imani juu ya uchamungu wake. Katika hali hii uhusiano kati ya kiongozi na wafuasi wake umejengwa juu ya uchamungu wa kiongozi na imani waliyonayo wafuasi wake juu yake. Ikiwa wafuasi wake watapoteza imani juu yake iwe kwa haki au kwa makosa, uhusiano huu huharibika.

Sheria haiwezi kutumika kuurejesha. Kwa vile ni suala la hisia za moyoni, hakuna yeyote anayeweza kulazimishwa kisheria kuwa na imani na mtu fulani. Hata kama kiongozi wa sala ana kiwango cha juu kabisa cha uchamungu na wema, hawezi kuwalazimisha wengine kusali nyuma yake. Itakuwa ni kichekesho sana kufungua kesi mahakamani kwa sababu watu fulani au wote hawakusali nyuma yake. Inaweza hata kuwa ni matusi kwa nafasi ya kiongozi wa sala kujaribu kuwalazimisha watu kusali nyuma yake. Hali ni hivyo hivyo katika suala la uhusiano kati ya wapiga kura na mgombea katika uchaguzi. Watu watampigia kura mgombea yule tu ambaye wana imani naye. Wasipomchagua mgombea fulani, hata awe na sifa na anafaa kiasi gani, hawezi kuwashitaki wapiga kura.

Kitu pekee kinachoweza kufanyika katika hali hizi ni kuwaelimisha watu juu ya vigezo sahihi na kukuza kiwango chao cha uelewa ili watakapokuwa wakitekeleza jukumu lao la kidini, wampate mtu muongofu kabisa wa kumfuata na wanapotekeleza jukumu lao la kijamii wampigie kura mtu anayestahiki. Lakini ikitokea, kwa sababu yoyote iwayo, watu wakabadilisha maoni yao, linaweza kuwa ni jambo la kusikitisha tu, lakini hakuwezi kuwa na suala la kulazimishana au kuwachukulia hatua za kisheria wapiga kura.

Jukumu la kifamilia ni sawa kabisa na majukumu ya kidini na kijamii tuliyoyataja hapo juu, Uislamu huiona familia kuwa ni jamii ya asili ambayo imewekewa taratibu maalum ambazo zinapaswa kufuatwa kwa ukamilifu ili iweze kwenda vizuri. Ni mafanikio makubwa sana kwa Uislamu kwa kuweza kuuweka utaratibu huu, kwani nchi za Magharibi bado hazijaweza kutatua matatizo yake ya kifamilia. Sio hivyo tu, bali kila siku matatizo yanazidi kuongezeka na kila siku matatizo mapya yanazidi kuongezeka juu ya matatizo ya zamani.

Kwa bahati nzuri, kutokana na uchunguzi wa kisayansi, mambo yanazidi kuwa wazi pole pole. Tunashawishika kwa asilimia zote kuwa ulimwengu wa Kimagharibi pole pole utazikubali kanuni na mafundisho ya Kiislamu juu ya sheria za familia. Hata hivyo hatuamini kuwa mafundisho halisi ya Uislamu yanafanana kabisa na yale yanayofuatwa na kutekelezwa leo hii. (na waislamu - yaani mafundisho hayatekelezwi vilivyo) Kinachoimarisha jengo la familia ni zaidi ya usawa. Ulimwengu wa Kimagharibi wa leo umeleweshwa na neno usawa bila kujua kuwa suala la uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke lilitatuliwa na Uislamu karne 14 zilizopita.

Katika suala la mfumo wa familia, kuna kitu kikubwa zaidi kuliko usawa. Kwa jamii ya kiraia, maumbile yameweka sheria ya usawa tu, lakini kwa jamii ya kifamilia maumbile yameweka sheria nyingine pia. Mahusiano ya kifamilia hayawezi kuongozwa kwa msingi wa usawa peke yake. Sheria nyingine zote za maumbile zinazoyaongoza mahusiano haya, lazima zitambuliwe na zifuatwe. Usawa katika ufisadi Kwa bahati mbaya neno 'usawa' limetumika sana na mara nyingi mno kiasi cha kuwa maana yake halisi imeshaharibika.

Ni mara chache kutokea kwa yeyote kuwa neno usawa linapotumika humaanisha usawa wa haki. Kanuni ya usawa haiwezi kutumika kila sehemu bila kubagua. Inaweza kuwa dhihaka kubwa kusema kuwa kila kitu kimekuwa sawa kwa sababu huko nyuma ni wanaume tu waliowadanganya wake zao. Je, tunaweza kufurahia na kutangaza kuwa sasa usawa umefikiwa kwa sababu huko nyuma ni 10% ya ndoa zilizokuwa zikiishia kwenye talaka na kutengana, na sasa katika baadhi ya sehemu za dunia, 40% ya ndoa zinaishia kwenye talaka, na katika 50% (nusu) ya talaka hizi zilianzishwa (ziliombwa) na wanawake?

Zamani ni wanaume waliowasaliti wake zao kwa kujiingiza katika zinaa na wake zao walikuwa waaminifu sana kwa waume zao, lakini sasa hata wanawake nao wanawasaliti waume zao na hawazingatii tena usafi wa kimaadili (hawajiepushi na zinaa). Je haya ni maendeleo? Je tunaweza kusema kuwa huu ni usawa? Zamani mara nyingi wanaume waliuonyesha ukatili na ugumu (wa hisia) kwa wake zao. Waliwatelekeza wake zao na watoto na kuwakimbilia vimada.

Sasa hata akina mama wenye watoto wengi, baada ya kuwa wameolewa miaka mingi huko nyuma, wanazitelekeleza nyumba zao na kwenda kukidhi tamaa zao, kufuatia utambulisho mfupi aliopewa kwa mtu asiyejua katika hafla ya dansi. Je, hii inamaanisha kuimarika kwa usawa? Hivyo ndivyo ambavyo badala ya kutibu maradhi ya kijamii na kuimarisha maisha ya kifamilia (ndoa), tunadhoofisha mfumo wa familia na kuitikisa misingi yake. Lakini vilevile, tunafurahia kuwa sasa usawa unazidi kuboreka. Kama hali hii itaendelea muda si mrefu mwanamke atamzidi mwanaume kwa ufisadi, upotofu na ugumu wa moyo. Sasa ni dhahiri kuwa kwa nini Uislamu, licha ya kuichukia talaka, haujaiharamisha moja kwa moja. Ni dhahiri kuwa ni vipi kitu kinaweza kuruhusiwa na bado kikawa kinachukiza sana.

16

HAKI ZA WANAWAKE KATIKA UISLAMU

IV - TALAKA

Ni dhahiri kutokana na majadiliano tuliyoyafanya kuwa Uislamu unachukia talaka na kuvunja maisha ya ndoa. Umechukua kila hatua ya kimaadili na kijamii ili kuiokoa ndoa kutokana na hatari ya kuvunjika, lakini haukutumia mbinu ya kulazimisha wala nguvu ya sheria. Uislamu unapinga matumizi ya nguvu ya sheria ili kumzuia mwanaume asimtaliki mkewe na kumlazimisha mwanamke kuendelea kuishi na mume wake.

Uislamu unaona kuwa hatua hizi haziafikiani na nafasi ya mwanamke katika familia, kwani hisia za moyoni na mihemko ndio nguzo za maisha ya familia. Ni mwanamke anayepokea fukuto la hisia za upendo wa mume wake na yeye hulipeleka kwa watoto wake. Ikiwa mwanaume atapoteza upendo wake kwa mke wake, mazingira ya nyumbani huwa baridi na ovyo ovyo.

Hata hisia za kimama kwa watoto wake hutegemea kwa kiasi kikubwa upendo wa mumewe. Kwa mujibu wa mwanasaikolojia mashuhuri, hisia za kimama sio silika kwa maana kwamba haiwi kuwa hisia hizi haziongezeki au kupungua. Upendo na kujali anakokuonyesha mwanaume kwa mkewe kuna athari kubwa kwenye hisia zake za kimama. Kwa kifupi, mwanamke huhamasishwa na kuchochewa na hisia za ndani na upendo wa mumewe katika kuzisafirisha hisia zake kwa wanawe. Mwanaume anaweza kulinganishwa na mlima, mwanamke kama mto na watoto kama mimea. Mto lazima upokee maji kutoka milimani ili uyafyonze na kuyatoa katika hali ya maji yanayotoa uhai kwa ajili ya umwagili aji wa mimea na maua.

Mvua isiponyesha mlimani au yakinyong'onyea ardhini, mto utakauka na mimea itanyauka. Kama ilivyo kuwa ni muhimu kwa rutuba ya ardhi na kwa kustawi kwa mimea, hisia za ndani na upendo wa mwanaume kwa mke wake ni muhimu sana kwa maisha ya ustawi, mafanikio na furaha ya watoto na mama yao.

Inapokuwa hisia za moyoni na upendo wa mume ni muhimu kiasi hicho kwa mafanikio ya maisha ya familia, ni vipi sheria inaweza kutumika kama silaha dhidi yake? Uislamu unapinga vitendo vya aibu na udhalilishaji vinavyofanywa na baadhi ya wale wanaowataliki wake zao wa zamani na kuoa wapya.

Lakini kwa maoni ya Uislamu, sio dawa kumlazimisha mwanaume aliyepoteza mapenzi kuendelea kuishi na mkewe dhidi ya matakwa na utashi wake. Kitendo hicho hakiendani na sheria ya maumbile ya maisha ya familia. Ikiwa mwanamke atajaribu kurudi katika nyumba ya mumewe kwa nguvu ya sheria na kwa msaada wa mamlaka za kiutawala, nafasi yake katika nyumba itakuwa sawa na utawala wa kijeshi. Katika hali hii hataweza kuwa malikia wa nyumba, wala hawezi kuwa kiunganishi cha hisia kati ya mume wake na watoto wake.

Pia hataweza kukidhi hitajio lake la upendo na kutazamwa vyema. Uislamu umechukua hatua ili kuondoa kesi za talaka, lakini Uislamu ukiwa kama mtunga sheria, hautaki kumlazimisha mwanamke ambaye ni kitovu cha mfumo wa familia, kuishi na mwanaume mkorofi asiyemtaka (yaani mwanaume asiyemtaka mwanamke huyo).

Hatua iliyochukuliwa na Uislamu ni kinyume cha kilichofanywa na kinachofanywa na ulimwengu wa Magharibi. Uislamu unapiga vita mambo yote yanayosababisha hali ya kutokuwa na uaminifu na uasherati lakini hauko tayari kumlazimisha mwanamke kuishi na mume asiyekuwa mwaminifu. Lakini kinyume chake ulimwengu wa Kimagharibi unapalilia mambo yanayosababisha kutokuwepo kwa uaminifu, na wakati huo huo unataka kumlazimisha mwanamke kuendela kuishi na mume asiyekuwa mwaminifu na mwasherati.

Uislamu umetumia rasilimali zake zote ili kutunza uhai wa roho ya ubinadamu na uchangamfu na ingawa haumlazimishi mwanaume asiye mchangamfu kwa mkewe kuendelea kuishi na mke wake, kiuhalisia umefanikiwa sana kupunguza kesi za talaka zinazotokana na kutochangamkiana.

Wengine hawazingatii nukta hizi na wanataka furaha kwa nguvu na katika ncha ya sindano na hivyo hawajafanikiwa. Mbali na kesi za talaka zinazotokea katika nchi za Magharibi kwa madai ya wanawake kwa sababu ya kutoshabihiana (incompatibility) na kama ilivyoelezwa na gazeti la Newsweek, kupenda starehe, idadi ya matukio ya talaka kwa sababu ya uasherati wa mwanaume ni kubwa mno kuliko idadi ya matukio kama hayo katika nchi za Mashariki (Asia).

Asili ya Amani ya familia ni tofauti na zile aina nyingine za amani. Hapana shaka yoyote kuwa inapaswa pawepo amani na maeleweno kati ya mume na mke, lakini amani na maelewano yanayopaswa kuwepo katika maisha ya ndoa ni tofauti sana na amani inayopaswa kuwepo kati ya marafiki wawili, wenzi wawili, majirani wawili na nchi mbili majirani.

Amani na maelewano katika maisha ya ndoa ni sawa na amani na maelewano yanayopaswa kuwepo kati ya wazazi na watoto. Yanahusisha uvumilivu, kujitolea, kujali maslahi ya mwenzako, kuvunja ukuta wa uwili (hivyo kuwa mwili mmoja) na kushiriki katika furaha na huzuni ya mwenzi wake.

Lakini kinyume chake, amani na maelewano kati ya marafiki wawili, wenzi wawili, majirani wawili au nchi mbili majirani ina maana kutoingilia haki za mwenzako katika nchi mbili zinazogombana, hata amani iliyopatikana kwa mtutu inatosha. Hata dola ya tatu ikiingilia na kuweka kizuizi ili kuzuia mashambulizi ya moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili, amani itakuwa tayari imepatikana, kwa amani ya kisiasa inamaanisha kutokuwepo vitendo vya uchokozi na migongano (kuparuana). Lakini amani ya familia ni tofauti na amani ya kisiasa. Hapa kutoingilia haki za mwenzako hakutoshi. Amani ya mtutu wa bunduki haifai chochote.

Kinachotakiwa ni muungano wa roho, jambo ambalo ni la juu zaidi na la msingi zaidi. Mambo yako hivyo hivyo katika amani na maelewano kati ya wazazi na watoto. Hapa pia panahitajika kitu kikubwa zaidi kuliko kutokuwepo kwa uchokozi peke yake. Kwa bahati mbaya, kwa sababu za kihistoria na wakati fulani za kimkoa, nchi za Magharibi hazitambui umuhimu wa hisia za moyoni.

Wao hawaoni tofauti yoyote kati ya amani ya familia na amani ya kisasa au amani ya kijamii. Watu wa Magharibi wanafikiri kuwa kwa vile amani kati ya nchi mbili inaweza kufikiwa kwa kurundika majeshi ya dola ya tatu katika mpaka wa nchi hizi mbili, halikadhalika amani kati ya mume na mke inaweza kuimarishwa kwa kuweka nguvu ya kisheria (kimahakama) katika mpaka wa maisha yao.

Wanasahau kuwa mafanikio ya maisha ya familia hutegemea kutoweka au kuondolewa kwa mipaka yote (baina yao). Watu wa Mashariki wenye akili za Kimagharibi, badala ya kujivunia mfumo wao na kuwaonyesha watu wa Magharibi ubovu na mapungufu ya mfumo wa Kimagharibi, wamebobea katika kuiga kibubusa kiasi cha kushindwa kutofautisha kati ya wema na uovu. Lakini muda si mrefu nchi za Mashariki zitaondokana kabisa na minyororo ya magharibi, zitaigundua haiba (Shaksia) yao na zitajifunza kujitegemea.

Hapa ni muhimu kutaja nukta mbili. Uislamu unakaribisha jambo lolote litakaloondosha hatari ya talaka. Kutokana na tulivyoyaandika baadhi ya watu wanaweza kwa makosa kuhitimsiha kuwa tunaunga mkono wazo la wanaume kuwataliki wake zao kwa ridhaa zao na kwa raha zao. Kwa hakika hivi sivyo. Tunachomaanisha 183 ni kuwa Uislamu hautaki kutumia nguvu ya sheria dhidi ya mume. Uislamu unakaribisha jambo lolote litakalofanikiwa kumshawishi mume kuachana na wazo la kutoa talaka, na zaidi ya hayo talaka sio sahihi mpaka itamkwe mbele ya watu wawili waadilifu, ambao wanatarajiwa kutumia jitihada zao zote kuwapatanisha wanandoa. Mila ya sasa ambayo mara nyingi talaka inatolewa mbele ya watu wawili waadilifu, ambao hata hawafahamu wanandoa zaidi ya kuyajua majina yao, sio ya Kiislamu kabisa.

Ulazima wa kuwepo mashahidi wawili wajuzi ni moja ya mambo yanayoweza kumshawishi mume kuachana na mpango wa kutoa talaka, ikiwa sharti hili litazingatiwa kikamilifu kwa maana iliyokusudiwa. Uislamu hauchukulii kuwepo kwa mashahidi wawili kuwa ni jambo la lazima wakati wa ndoa (ili ndoa isihi), ambayo ni mwanzo wa mkataba wa ndoa, kwa sababu hautaki kuchelewesha amali njema. Lakini unaona kuwa ni sharti la lazima kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu na wajuzi ili talaka iweze kusihi (kuwa sahihi), jambo ambalo ni mwisho wa mkataba wa ndoa.

Halikadhalika kwa mujibu wa Uislamu talaka sio sahihi (valid) kama itatolewa wakati mwanamke yupo hedhini ingawa hakuna kikwazo cha kufunga ndoa katika kipindi hicho. Ilivyo hedhi kwa vile ni kikwazo cha kufanyika tendo la ndoa, ilipaswa kuwa ni kikwazo cha ufungaji wa ndoa sio talaka. Lakini kwa vile Uislamu unahimiza usalama wa ndoa na unakataza utengano, umeruhusu ndoa ifungwe hata kama mwanamke yupo hedhini na umekataza talaka katika kipindi hicho. Katika baadhi ya hali, ni lazima kusubiri kwa miezi mitatu kabla ya talaka kuruhusiwa kutolewa. Vikwazo vyote hivi vinakusudiwa kutoa muda wa kutosha wa kuruhusu hasira, iliyosababisha uamuzi wa kutoa talaka, ipoe na kuwawezesha mume na mke kurejea maisha yao ya kawaida.

Aidha, katika talaka rejea mume anaruhusiwa kumrejea mke wake ndani ya kipindi cha eda. Uislamu umemuwekea mwanaume kikwazo kingine kwa kumtaka azikabili gharama za ndoa pamoja na matunzo ya mke na watoto katika kipindi chote cha eda. Ikiwa mwanaume anataka kumtaliki mke wake na kumuoa mwanamke mwingine, kwanza anapaswa kulipa gharama za matunzo ya mke wa kwanza, na kubeba gharama ya matunzo ya watoto na kulipa mahari ya mke mpya. Na pia anapaswa kubeba jukumu la matunzo ya mke wa pili pamoja na watoto atakaomzalia. Mbali na jukumu la kuwalea watoto, majaaliwa yao yenye mashaka humhofisha na kumzuia mume kuchukua uamuzi wa kutoa talaka.

Pamoja na yote haya, Uislamu unaona kuwa ni lazima pindi ndoa inapovunjika mahakama ya familia yenye wasuluhishi wawili, mmoja kutoka upande wa mume na mwingine upande wa mke, hupaswa kuwasuluhisha wanandoa. Wasuluhishi wanapaswa kufanya kila liwezekanalo kusuluhisha ugomvi baina ya mume na mke na ikibidi wanaweza kuwataka ushauri wanandoa ili kufikia lengo hili. Wanaweza tu kuvunja ndoa ikiwa wataona kuwa usuluhishi hauwezekani kabisa. Ikiwa kuna uwezekanao, wasuluhishi wanapaswa kuwa ni ndugu wa wanandoa, ikiwa upo uwezekano wa kupatikana watu wenye ujuzi miongoni mwa ndugu zao. Qur'ani Tukufu inasema:"Ikiwa mna hofu ya kuvunjika kwa ndoa baina yenu wawili (mke na mume), chagueni msuluhishi mmoja kutoka kwa mume na mwingine kutoka kwa mke. Ikiwa wote wanataka mapatano, Mwenyezi Mungu atawawezesha. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yote, Mwenye habari." (Suratul Nisa, 4:35).

Mwandishi wa Kashshaf, neno 'msuluhishi' anasema kuwa ni mtu anayechaguliwa kusuluhisha anayepaswa kuwa mwaminifu, fasaha na mwenye uwezo wa kuleta maelewano na kuzitendea haki pande mbili. Anasema pia kuwa inafaa zaidi kuteuwa msuluhishi kutoka miongoni mwa ndugu zao kwa vile wanatarajiwa kujua sababu za mgogoro vizuri zaidi na pande zote zinaweza kuzungumza nao kwa uhuru zaidi na wanaweza kuwa na imani nao zaidi.

Mafakihi wanatofautiana juu ya suala la usuluhishi, iwapo usuluhishi ni wajibu au unapendekezwa tu. Wazo lililo mashuhuri zaidi ni kuwa ni jukumu la serikali kuteuwa wasuluhishi. Shaheed Thani, katika kitabu chake, 'Masalik' ametoa rasmi rai ya kisheria kuwa usuluhishi ni wajibu na unapaswa kuratibiwa na serikali. Sayyid Muhammad Rashid Riza, mwandishi wa Tafsiri ya Qur'ani, AlManar, baada ya kutoa rai kuwa usuluhishi ni wajibu, anazungumzia khitilafu ya maoni ya mafakihi (wajuzi wa sheria za Kiislamu) juu ya suala hili na anasema kuwa, kivitendo, Waislamu hawafuati kanuni hii ya busara na hivyo wanakosa fursa ya kufaidika na faida zake nyingi.

Wanavyuoni wanapoteza nguvu zao katika kubishana tu, wakati hakuna anayechukua hatua kuitekeleza. Kama kanuni haitekelezwi, kuna tofauti gani ikiwa kanuni hiyo ni wajibu au inapendekezwa tu? Juu ya sharti ambalo wasuluhishi wanaweza kumuwekea mume ili kufanikisha usuluhishi, Shahid Thani anasema kuwa wanaweza kwa mfano, kumlazimisha mume kumweka mke wake katika mji fulani au nyumba fulani na asimuweke mama yake au mke wake mwingine katika nyumba hiyo hata kama ni kwenye chumba tofauti; kulipa malipo yote ya mahari aliyopangiwa wakati wa ndoa kwa mkupuo na kulipa mkopo wote kwa mkupuo mmoja kwa mke wake.

Kwa kifupi, hatua yoyote inayofaa kumshawihsi mume kuachana na mpango wa kutoa talaka inafaa na inakaribishwa. Hili ni jibu kwa swali tuliloliibua awali kuwa mahakama inayoiwakilisha jamii ina haki ya kuingilia kati na kuzuia kuvunjika kwa ndoa au haina. Mahakama inaweza kuingilia kati kwa sababu uamuzi wa mume wa kumtaliki mke si mara zote unakuwa ni dalili ya kuvunjika kabisa kwa ndoa.

Anaweza kutoa uamuzi huo kwa sababu ya hasira au hali ya kutoelewana. Hatua yoyote itakayochukuliwa na jamii kuzuia utekelezaji wa uamuzi huo inakaribishwa na Uislamu. Mahakama ya usuluhishi, ikiwa ni mwakilishi wa jamii, inaweza kuziamuru ofisi zinazohusika na utoaji wa talaka kutohitimisha kesi ya madai ya talaka, mpaka mahakama iwahakikishie kuwa imeshindwa kuwapatanisha na kuleta amani na maelewano kati ya mume na mke.

Huduma alizotoa mke katika familia Talaka, mbali na kuvunja maisha matakatifu ya familia, husababisha matatizo mengine makubwa kwa mke, matatizo ambayo hayawezi kupuuzwa. Jaalia mke ameishi katika nyumba na mumewe kwa miaka, ameichukulia nyumba kuwa ni yake na kwa dhati na uaminifu mkubwa, anafanya bidii kubwa kuijenga na kuitengeneza. Anapunguza bajeti ya chakula na mavazi, ukiachilia mbali wanawake wa mijini (ambao hawafanyi hivi), kiasi cha kumkera hata mumewe (kwa jinsi anavyobana matumizi), na anasita hata kuajiri msaidizi wa kumsaidia kazi za ndani. Anajitolea ujana wake, nguvu zake, afya yake kwa ajili ya mumewe na nyumba yake. Sasa mume wa mke huyu, baada ya miaka ya kuishi pamoja, anataka kumtaliki na kumuoa mwanamke mwingine, sio tu kuwa anataka kuziharibu jitihada zote za mke wake, bali pia anataka kujiingiza katika raha za mapenzi kwa kutumia maumivu ya mke wake (anayemuacha).

Huku sio kuvunjika tu kwa ndoa, na haiwezi ikadaiwa kuwa, kwa asili ni jambo la aibu kwa staha ya mwanamke kung'ang'ania kwa mwanaume huyu ambaye hampendi. Hapa maswala mengine pia huibuka - suala la kutokuwa na nyumba kwa mke, suala la kuikabidhi nyumba yake kwa hasimu wake na suala la kupoteza jitihada zake zote na huduma alizozitoa huko nyuma katika nyumba yake. Kila mwanadamu anataka kuwa na nyumba yake na huhisi kushikamana na nyumba aliyoijenga kwa mikono yake mwenyewe hasa.

Ukijaribu kumfukuza ndege katika kiota alichokijenga, bila shaka atakataa na kujilinda. Kwa maoni yetu, tatizo hili linastahili kujadiliwa kwa umakini. Katika hali hizo, talaka inakuwa sio kuvunjika kwa ndoa peke yake, bali huwa ni kuangamia kabisa kwa mwanamke. Hata hivyo, suala la nyumba ni tofauti na lile la talaka, na haya masuala mawili yanapaswa kujadiliwa tofauti tofauti.

Kwa mtazamo wa Uislamu, tatizo hili halipaswi kutokea. Linatokea kutokana na kutojua kanuni za Kiislamu na taratibu zake na wanaume kuzitumia vibaya dhamira njema za wake zao. Watu walio wengi wanadhani kuwa matunda yote ya jasho la mwanamke ni mali ya mume wake. Wanafikia hata kufikiri kuwa mume ana haki ya kumlazimisha mke wake kumfanyia kazi na kwamba anapaswa kutii amri zote kama mtumwa. Fikra hii potofu ndio chanzo cha matatizo yote.

Kama tulivyosema mwanamke ana uhuru kamili kuhusiana na kazi na shughuli. Chochote anachopata huwa ni mali yake peke yake. Uislamu umempa uhuru wa kiuchumi. Na bado umemuwajibisha mume kubeba gharama zote za mke na watoto wake. Hivyo Uislamu umempa mwanamke fursa nyingi za kujipatia fedha za kumwezesha kuishi maisha ya heshima na yasiomtegemea mwanaume (baada ya kuachika). Talaka na kutengana hakukupaswa kumhofisha kwa upande wa uchumi. Vitu vyote ambavyo anaweza kuwa amekusanya ili kuijenga nyumba yake ni mali yake na mume wake hana haki ya kuvichukua. Mwanaume kuvichukua vitu hivyo kunaweza tu kuhalalishwa na mifumo ambayo inamlazimisha kufanya kazi katika nyumba ya mumewe.

Masaibu yanayowapata watu wetu huenda yanasababishwa na kutojua kwao sheria. Sababu nyingine ya tatizo hili ni tabia ya baadhi ya wanaume kuunyonya uaminifu wa wake zao. Baadhi ya wanawake wanajitolea sio kwa sababu hawaielewi sheria ya Kiislamu, bali kwa sababu wanawaamini waume zao kupita kiasi. Hawataki kuitumia fursa waliyopewa na Uislamu.

Ghafla huzinduka usingizini na kukuta kwamba wamepoteza maisha yao kwa kujitolea kwa mwanaume asiyekuwa mwaminifu na wamepoteza fursa waliyopewa na dini yao. Ikiwa mke atasamehe haki yake ya kisheria ya kujiwekea akaunti yake tofauti ya fedha na mapato mengine, mume pia anatarajiwa kwamba, kwa kuzingatia kujitolea na huduma alizotoa mke wake atatoa zawadi na hidaya kwa mkewe. Qur'ani inasema;"Mnaposalimiwa kwa salamu, itikieni kwa salamu iliyo bora kuliko hiyo au angalau kama hiyo.' (Suratul Nisa, 4:86). Imekuwa ni mila ya watu wema kumpa mke zawadi za vitu vya thamani kama vile nyumba au mali nyingine kama hidaya.

Hata hivyo, tunachomaanisha ni kuwa suala la kutokuwa na nyumba (makazi) halihusiani na talaka na haliwezi kutatuliwa kwa kurekebisha sheria. Tatizo hili linahusiana na suala la uhuru wa kiuchumi wa mwanamke na tatizo hilo tayari limeshatatuliwa na Uislamu. Tatizo hili limeibuka kutokana na ujinga (kutojua) wa baadhi ya wanawake na wengine kwa sababu ya kuwaamini mno waume zao, tatizo hili litamalizika kabisa ikiwa wanawake watayajua mafundisho ya Uislamu juu ya jambo hili na kuacha kuwaamini mno waume zao.