6
DALILI ZA KIAMA
KUANGAMIA KWA MIJI MIKUU:
Vita na majanga Miongoni mwa mambo aliyoyasema Mtume kuhusiana na zama za mwisho ni hili:
Miji mikuu itaangamia na itakuwa kana kwamba haikupata kuwepo hapo kabla (Al-Muttaq Al-Hindi Al Burhan fi Alamat Al Mahadi Akhir al Zaman)
Kuangamia kwa miji mikuu iliyozungumzwa katika hadithi hii kunatukumbusha maangamizi ambayo yanatokea hivi leo kutokana na vita na majanga mbali mbali ya asili. Silaha za kisasa za Nyuklia, Madege ya Kivita, Mabomu, Makombora na Zana nyingine za kisasa zimesababisha maangamizi yasiyosemeka.
Zana hizi za hatari zimeleta kiwango kikubwa cha maangamizi ambacho dunia haijapa kukiona hapo kabla. Kwahakika miji mikuu ndio imekuwa malengo makuu ya mashambulizi na imekuwa ikiathirika zaidi kutokana na maangamizi haya. Maangamizi yasiyo na mfano ya vita ya pili ya dunia ni kielezeo cha haya. Kwa kutumika bomu la Atomic katika vita kuu ya dunia, miji ya Hiroshima na Nagasaka iliangamizwa kabisa.
Kutokana na Mabomu mazito, miji mikuu ya Ulaya na miji mingine mikubwa imepata kiwango kikubwa cha hasara. Buku la marejeleo (Encylopedia Britannica) linaelezea hasara iliyosababishwa na vita kuu ya pili ya dunia katika miji ya Ulaya: Maangamizi yaliyotokea yameigeuza sehemu kubwa ya Ulaya kuwa kama taka taka na ilimalizwa na mabomu ya moto, bara bara zilijaa mashimo matupu, sura ya nchi ilikuwa giza tupu njia za reli zikaharibiwa na kutofanya kazi, madaraja yalibomolewa na bandari zilijaa Meli. Berin, anasema Jenerali Lusias D. Clay, Naibu Gavana wa Jeshi katika ukanda wa Post war German, lilikuwa kama jiji la wafu.
Kwa kifupi maangamizi ambayo yalisababishwa na vita ya pili ya dunia yanashabihiana kabisa na hadithi ya Mtume (s.a.w.w) Sababu nyingine ya maangamizi ya miji mikuu ni majanga ya asili. Ni ukweli wa kitakwimu kuwa zama tunazoishi hivi leo zimeshuhudia kuongezeka kwa idadi na madhara ya majanga ya asili. Katika miaka kumi iliyopita, majanga ya asili yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yalikuwa ni mambo ambayo hayakuwahi kutokea.
Maangamizi, Umasikini, mauaji, machafu kuongezeka Sababu nyingine ya maangamizi katika miji ni majanga ya asili. Kulingana na takwimu, zama zetu zimeshuhudia ongezeko la idadi na ukubwa wa majanga ya asili. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kulikuwa na majanga yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Haya yalikuwa ni majanga ya aina yake.
Hatari kubwa ya uchafuzi wa hali ya hewa unaosababishwa na viwanda ni tishio kwa dunia nzima. Viwanda vinavuruga urari wa angahewa ya dunia na kuongeza mabadiliko ya hali ya hewa. Mwaka 1998 ulikuwa ni mwaka wa joto kali sana duniani tangu rekodi za hali ya hewa zianze kuwekwa. Kwa mujibu wa maelezo ya kituo cha taarifa za hali ya hewa cha Marekani, idadi kubwa ya majanga yaliyotokana na hali ya hewa ilikuwa mwaka huo wa 1998.
Kwa mfano, Kimbunga kimeelezewa na wachunguzi wengi kuwa ndio janga baya mno la kimaumbile lililoikumba Amerika ya kati. Katika miaka michahe iliyopita vimbunga, dhoruba, tufani na majanga mengine yameleta maangamizi katika bara la Amerika na katika sehemu nyingine kadha wa kadha za dunia. Mbali na hayo mafuriko nayo yameleta maangamizi katika maeneo kadhaa ya watu. Aidha mitetemeko ya ardhi, Volkeno nayo pia yamesababisha maangamizi makubwa. Hivyo basi maangamizi yote haya yaliyotokea katika miji ni ishara muhimu.
Mitetemeko ya ardhi Hapana shaka kuwa katika historia, hakuna majanga ya asili ambayo yamewaathiri watu kwa kiasi kikubwa kama mitetemeko ya ardhi. Mitetemeko ya ardhi hutokea mahali popote na wakati wowote. Kwa karne zote mitetemeko ya ardhi imesababisha maafa na hasara kubwa ya mali. Kwa sababu hii tetemeko la ardhi ni janga linalohofiwa mno. Hata teknolojia ya karne ya Ishirini na Ishirini na moja imeweza kwa kiasi kidogo sana kuzuia uharibifu wa tetemeko la ardhi.
Tetemeko la ardhi la mwaka 1995 kule Kobe laweza kuwa somo kwa wale wanaodhani kuwa teknolojia itaweza kudhibiti maumbile. Itakumbukwa kuwa tetemeko hili la ardhi lilitokea bila kutarajiwa kwenye eneo kubwa la viwanda na usafirishaji. Licha ya ukweli kwamba lilidumu kwa sekunde ishirini tu, kama lilivyoripoti gazeti la Time, bado lilisababisha hasara ya dola bilioni 100. Kadhalika tetemeko la ardhi ndani ya bahari lililofahamika kama Tsunami fukweni mwa nchi za Indonesia, Thailand na ukanda mzima wa Pwani ya Asia, lilikuwa la aina yake kupata kutokea katika historia ya mwanaadamu.
Katika miaka michache iliyopita mitetemeko mikubwa ya ardhi imetokea mara kwa mara na ndio matishio makubwa ya maisha ya watu duniani kote. Tukiangalia takwimu zilizokusanywa na kituo cha taarifa za matetemeko ya ardhi cha Amerika mwaka 1999 tunaona kuwa mitetemeko ipatayo 20, 832 ilitokea sehemu mbali mbali duniani. Matokeo yake watu wanaokadiriwa kufikia 500,000 walikufa. Matukio yote haya yanakumbushia maneno ambayo Mtume (s.a.w) aliyasema miaka 1400 iliyopita: Kiama hakitasimama mpaka pale mitetemeko ya ardhi itakapotokea mara kwa mara. (Bukhari).
Katika Qur'an kuna aya kadhaa zinazobainisha uhusiano kati ya mitetemeko ya ardhi na zama za mwisho. Sura ya 99 inaitwa suratil Zil Zaala ambayo maana yake ni mtikisiko au tetemeko la ardhi. Sura hii yenye aya nane inaelezea mtetemeko mkubwa wa ardhi na inasema kuwa kufuatia mtetemeko huo siku ya hukumu itakuwa imefika. Watu watafufuliwa makaburini na kutoa hesabu ya amali zao kwa Mwenyezi Mungu na kupata malipo yao hata kwa jambo dogo sana walilolifanya:
Itakapotetemeshwa ardhi kwa mtetemesho wake mkubwa. Na itakapotoa ardhi mizigo yake, na binadamu akasema (wakati huo) (oh!) ina nini leo ardhi? Siku hiyo itatoa habari zake zote kwa kuwa Mola wake ameifunulia (ameiamrisha kufanya hayo). Siku hiyowatu watatoka (makaburini) vikundi vikundi ili waonyeshwe vitendo vyao. Basi anayefanya wema hata kwa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jazaa yake na anayefanya uovu hata kwa kiasi cha uzito wa mdudu chungu ataona jazaa yake. (99:1-8).
7
DALILI ZA KIAMA
UMASIKINI
Inafahamika kuwa umasikini ni ukosefu wa chakula, makazi, mavazi, huduma za afya na mahitaji mengine ya msingi kwa sababu ya kipato duni. Licha ya fursa zinazopatikana kutokana na maendeleo ya teknolojia, umasikini hivi leo ni moja kati ya matatizo makubwa kabisa yanayoukabili ulimwengu. Katika mabara ya Afrika, Asia, Amerika Kusini na Ulaya Mashariki watu wengi wanahangaika na njaa kila siku. Kwa sababu ya mgao mbaya wa rasilimali za ulimwengu umasikini umesababisha uwepo mgawanyiko kati ya nchi za kaskazini ya jangwa la sahara ambazo ni za ulimwengu wa kwanza na nchi za kusini maskini ambazo ni za ulimwengu wa tatu.
Ubeberu na Ubepari usio na mipaka unazuia mgawanyo wa kipato ulimwenguni kote na unakwaza maendeleo ya nchi changa na nchi zinazoendelea. Wakati ambapo kuna watu wachache wanaofurahia kipato kinachozidi mahitaji yao, kuna idadi kubwa ya watu wanaohangaika na matatizo ya umasikini na ufukara. Katika Ulimwengu wa leo umasikini umefikia hatua mbaya au kiwango kibaya sana.
Ripoti ya mwisho ya UNICEF ilieleza kuwa mmoja kati ya kila watu wanne duniani anaishi katika tabu na shida isiyoelezeka. Watu bilioni 1.3 duniani wanaishi kwa wastani wa chini ya dola moja kwa siku. Watu bilioni 3 duniani wanaishi kwa dola mbili kwa siku. Takribani watu bilioni 1.3 hawapati maji safi. Watu bilioni 2.6 hawapati maji salama.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la chakula duniani, (FAO) , Mwaka 2000, watu milioni 826 duniani kote hawapati chakula cha kutosha. Kwa maneno mengine mmoja katika kila watu sita ana njaa. Katika miaka kumi iliyopita dhulma katika mgawanyo wa kipato imeongezeka kwa kiwango kisichosemeka.
Ripoti za umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika mwaka 1960 asilimia 20 (20%) ya watu wanaoishi katika nchi tajiri kabisa duniani walikuwa na pato lilozidi mara thelathini pato la nchi 20 masikini kabisa. Hadi kufikia mwaka 1995 iliongezeka mara 82. Kikiwa ni kielezeo cha kutoweka kwa haki ulimwenguni, mali za matajiri 225 wakubwa kabisa ulimwenguni ni sawa na pato la mwaka la asilimia 47 (47%) ya nchi masikini ulimwenguni.
Takwimu za sasa zinaonyesha yale ambayo Mtume (s.a.w.w) aliyasema juu ya kuongezeka kwa umasikini. Katika hadithi inabainishwa kuwa umasikini na njaa ni miongoni mwa dalili za kipindi cha kwanza cha zama za mwisho:
Masikini wataongezeka (Amal Al Diin Al Qazwin, Mufid Al Ulum wa Mubid Al humum) Kipato kitagawanywa kwa matajiri tu, hakuna mafao kwa masikini. (Tirmidhi). Ni dhahiri kuwa kipindi hicho kilichobashiriwa na Mtume (s.a.w.w) kinawiana na hali ya wakati wetu wa leo. Tukiangalia karne zilizopita tunaona kuwa shida na tabu zilizoletwa na ukame, vita na majanga mengine zilikuwa za muda mfupi na ziliishia katika eneo moja moja. Lakini umasikini na shida za leo ni za kudumu na sugu. Kwa hakika Mola wetu ni Mwingi wa Rehma, yeye hadhulumu watu lakini kwa sababu ya ukosefu wa shukurani wa wanadamu na maovu wanayoyafanya, umasikini na tabu vimeongezeka. Kwa hakika hali ya mambo ya kusikitisha inaonesha wazi kuwa dunia imetanzwa na uchoyo na ubinafsi.
Kuporomoka kwa maadili, kushamiri kwa ushoga na ukahaba Katika zama zetu za leo kuna janga kubwa linalohatarisha uhai wa jamii ulimwenguni. Mithili ya virusi vinavyoua mwili, janga hili linasababisha msiba mkubwa wa kijamii. Janga hilo ni mmomonyoko wa maadili ambayo husaidia kustawisha jamii. Ushoga, Ukahaba, uhusiano haramu wa kijinsia kabla ya ndoa na nje ya ndoa, Filamu za ngono, Picha za ngono, unyanyasaji wa kijinsia na ongezeko la maradhi ya zinaa, mashindano ya kukaa uchi maarufu ulimbwende, uuzaji na utumiaji wa vileo na dawa za kulevya miongoni mwa vijana ni miongoni mwa ishara kubwa za kuporomoka kwa maadili.
Mambo haya ndiyo yamekuwa yakizishughulisha jamii. Idadi kubwa ya watu haijali hatari hii inayozidi kuwa kubwa na wanaiona kama jambo la kawaida tu. Lakini takwimu zinaonesha kuwa kila siku ipitayo kiwango cha hatari kinazidi kuongezeka. Ongezeko la maradhi ya zinaa ni kigezo kikuu cha kusaidia kuonesha ukubwa wa matatizo yanayomkabili mwanadamu. Kwa mujibu wa rekodi za Shirika la Afya ulimwenguni magonjwa yanayotokana na zinaa yanachukuwa sehemu kubwa ya maradhi. Ripoti zinaonesha kuwa kati ya kesi mpya za magonjwa ya zinaa zinazokadiriwa kufikia milioni 333 kila mwaka ulimwenguni kote, Ukimwi ndio tatizo kubwa zaidi.
Takwimu za Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) zinaonesha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi tokea pale ulipoanza imefikia watu milioni 18.8. Ripoti za shirika hilo kwa mwaka 2000 zinaielezea hivi hali ya mambo: "Ukimwi una nafasi ya kipekee katika kuleta athari mbaya za kijamii, kiuchumi na katika mipango ya sensa ya maendeleo".
Miongoni mwa mambo mabaya kabisa yanayozidi kushamiri ni ushoga. Katika baadhi ya nchi jambo hili limehalalishwa kama ndoa, linapewa heshima zote za ndoa na limeundiwa vyama na jumuiya. Duniani kote uovu huu unapingwa. Kushamiri kwa ushoga hivi leo kunatukumbusha hatima ya watu wa Lut waliokithiri katika uovu huu. Kama isemavyo Qur'an walipoukataa wito wa Lut kuiendea njia sahihi, Mwenyezi Mungu aliuangamiza mji na watu wake kwa maangamizi makubwa.
Ni dhahiri kuwa zile hadithi zinazoelezea zama za mwisho na mporomoko wa maadili zinathibitika hivi leo. Hadithi moja inasema kuwa kutoweka kwa aibu katika dhambi ya ukahaba ni dalili ya kiama:
Kutashitadi maingiliano haramu ya kijinsia wazi wazi (Bukhari). Saa hiyo itafika wakati uzinzi utakapokuwa umeenea sana (Al-Haythami, kitab al fitan) Kufifia kwa maadili na hisia ya aibu kunaelezwa kwa maneno haya:
Saa ya mwisho haitasimama hadi pale watu watakapofanya uzinzi njiani (njia wanazopita watu) ( Ibn Iban na Bazzar). Yafaa kukumbuka kuwa hivi sasa matukio ya ukahaba yanayochukuliwa na kamera za siri yamekuwa yakioneshwa katika Internate, vituo vya Televisheni na katika magazeti yanayoitwa ya ngono na udaku. Makahaba wanaingiliana na wateja wao wazi wazi katikati ya mitaa. Hali kadhalika kuna Filamu na picha nyingi zinazosambazwa ulimwenguni kote ambazo zinaonesha uzinzi unavyofanyika wazi wazi. Takriban katika miji mingi duniani makahaba wamekuwa wakisimama na wateja wao na kufanya mambo ya ajabu barabarani hasa nyakati za usiku.
Hii ni dalili nyingine ya kiama iliyobainishwa katika hadithi. Mamilioni ya watu wanaishuhudia wenyewe dalili hii duniani kote. Hadithi zifuatazo zinaonyesha kuwa kuibuka kwa ushoga kuwa jambo la kawaida la maisha ni ishara kuu ya zama zinazokaribia siku ya mwisho:
Wanaume watawaiga wanawake na Wanawake watawaiga wanaume. (Allama Jalaluddin Swiyuti, Durre- Mansuri). Watu watazama katika ushoga na usagaji (Al Mutaqi al Hindi, Muntakhab, Kanzul Ummaal).
Vitendo vya wanaume kuwaiga wanawake na wanawake kuwaiga Wanaume vimekuwa vingi hivi leo. Tunashuhudia Wanaume wanaosuka nywele zao na pia tunashuhudia Wanaume wanaowasuka nywele wanawake kwenye Masaluni na majumbani. Imekuwa ni aina ya ajira kwa wanaume hawa hasa Wamasai kupita mitaani kusuka nywele akina Mama.
Pia tunashuhudia Wanaume wakivaa hereni masikioni na vidani shingoni. Tunashuhudia teknolojia ikitumika vibaya kubadilisha maumbile ambako kumeleta kiroja cha mwanaume kubeba uzazi na kujifungua! Kwa upande mwingine tunashuhudia Wanawake wakivaa mavazi ya Wanaume, wakijaribu kuiga usemaji wa kiume. Wakioa wanawake wenziwao na wakifanya kazi za mitulinga. Tunashuhudia wanawake wakivaa mavazi yenye kuonesha vivazi vyao vya ndani na maungo mateke ili kushawishi uzinzi.