SURA YA PILI
ITIKADI YA KISHIA
Swali: Nini itikadi ya Mashia?
Jawabu: Mashia wanaamini Misingi Mitatu.
Swali: Misingi ipi hiyo?
Jawabu: Misingi yenyewe ni hii:
1- Muumba na sifa zake;
2-Utume na mambo yanayo husiana nao, na
3-Kiyama na mambo yanayopatikana humo.
Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya Muumba?
Jawabu: Mashia wanaamini kuwepo kwa Mungu mmoja, Mwumba wa ulimwengu, mwenye kuruzukum mwenye kuhuisha, Mjuzi, Muweza, Hai, Mdiriki, Mwenyeenzi, Asiye na Mwanzo wala Mwisho, Msemi, Mkweli, Asiye na mwili, Asiyeonekana, Asiyebadilika. Asiye na mshirika, Naye ni mwadilifu katika vitendo, maamrisho na uumbaji, kama anavyosema Mwenyewe katika Qur'an: "hakika mola wako si dhalim kwa waja wake". (Qur'an,3:181). Swali: Nini itikadi ya Maisha juu ya Utume? Jibu:Mashia wanaamini kwamba Mwenyezi Mungu amewatuma mitume na manabii kuwaongoza wanadamu kutoka katika upotovu na ujinga na kuwaita katika njia ya uongofu wa ukweli. Hao mitume walikuwa wengi sana, miongoni mwao ni Muhammad (s.a.w) Mtume wa Uislaam. Vilevile manabii Musa, Isa, Nuh, Ibrahim (amani iwe juu yao) na manabii wengine, wametajwa katika Qur'an na hadithi. Hao wote hawakuwa na dhambi na walitumwa na Mwenyezi Mungu kufikisha ujumbe uliokamilika na usio na upungufu wa mola wao.
Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya Uimamu? Jibu: Mashia wanaamini kwamba Mtume mtukufu (s.a.w) aliwachagua Makhalifa (maimamu) Ithna asharia (12) kwa amri ya Mwenyezi Mungu na akawataja kwa majina yao. Wao wamehifadhika kutokana na kila dhambi na makosa kama Mtume mtukufu (s.a.w) alivyo, ambaye kwa ajili ya sifa zake Mwenyezi Mungu amesema: "Hasemi kwa matamanio yake, ila tu ni Wahyi (Ufunuo) uliofunuliwa". (Qur'an, 53: 3).
Swali: Ni nani hao Maimamu na Makhalifa wa Mtume? Jibu: Wao ni:
1-Ali Amirul Mu'miniin
2-Hassan
3-Hussein
4-Ali bin Huseyni
5-Muhammad Baqir,
6-Ja'far Sadiq
7-Musa Kaadhim,
8-Ali Ridha,
9-Muhammad Taqi,
10-Ali naqi,
11-Hassan Askariy, na
12-Muhammad Mahdi (amani iwe juu yao).
Majina yao na ukhalifa wao vimeandikwa kufuatana na hadithi za Mtume katika vitabu vya kisunni na vya kishia pia. Swali: Hao Maimamu wamezikwa wapi? Jibu: Ali (a.s) amezikwa mjini najaf (nchini Iraq); Hassan, Ali bin Husein, Muhammad Baaqir na Ja'far Sadiq (a.s) wamezikwa madina (nchini Saudi Arabia); Husein (a.s) amezikwa Karbalaa (nchini Iraq); Musa Kadhim na Muhammad Taqi (a.s) wamezikwa Kaadhimaini (nchini Iraq); Ali Ridha (a.s) amezikwa Mashhad (nchini Iran); Ali Naqi (a.s) na Hassa Askariy mjini Samarrah (nchini Iraq).
Swali: Je, makaburi ya Maimamu (a.s) hao yapo hadi hivi sasa? Jibu: Ndio, Waislaam wameyajengea makaburi ya Maimamu (a.s) majengo makubwa, na maelfu ya Waislaam kutoka kote duniani huyazuru kila mwaka kama kuonyesha heshima yao. Swali:Nini itikadi ya Mashia juu ya Imamu Mahdi (a.s). Jibu: Mtume Mtukufu (s.a.w) amebashiri kwamba Imamu Mahdi (a.s) atabaki hai hadi atakapodhihiri baada ya muda mrefu wa kughibu (kutoonekana) kwake, ili kuleta uadilifu na amani duniani baada ya kuwepo dhuluma na maonevu, kama ilivyoandikwa katika vitabu vya Kisunni na Kishia. Swali: Je, ni kweli kwamba Mashia wanavuka mpaka kwa kuwasifu Maimamu? Jibu: Si kweli kabisa! Wao wanaitakidi kuwa hao Maimamu walikuwa waja wanyenyekevu wa Mwenyezi Mungu, na Makhalifa wa Mtume wake (s.a.w).
Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya Bibi Fatimah Zahraa, binti wa Mtume Muhammad (s.a.w)? Jibu: Wao wanaitakidi kuwa yeye ni Mkweli (Siddiqah) na Johari (RTTaahirah); na Mwenyezi Mungu ameteremsha aya ya Tat-hir kwa utukufu wake, na baba yake, na wa mume wake, na wa wanawe. Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya Qur'ani? Jibu: Mashia wanaamini kwamba Qur'ani ni Neno la Mungu, ambalo alimteremshia Mtume wake Muhammad (s.a.w) kuwa mwujiza na mwongozo, nayo ni kitabu chenye ukweli kisichokuwa na uwongo ndani yake, pia ni msingi wa sheria zote, kisicho ongezwa wala kupunguzwa maneno yoyote yale. Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya Uislaam?
Jibu: Mashia wanaamini kwamba Uislaam ni dini iliyofundishwa na manabii na mitume wote, ambayo mafundisho yake yalikamilishwa na Mtume wa Uislaam-Muhammad (s.a.w). Dini hii itaendelea kuwepo mpaka siku ya Kiama, "Na mwenye kufuata dini isiyokuwa ya Uislaam, basi haitokubaliwa kwake, na (siku ya) akhera atakuwa miongoni mwa waliopata hasara". (Qur'an, 3:84). Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya majaaliwa? Jibu: Mashia wanaamini kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu Amemwumba mwanadamu akiwa na uwezo tofauti: Amwmwongoza katika mema na kumfungulia njia zote. Basi yule mwenye kuasi na kukufuru huwa amejifanyia mwenyewe; na mwenye kuamini, akaongoka na akatii basi huwa ni kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na kwa ubora wa hiari yake; kama ilivyoelezwa katika hadithi inavyosema: "Hakuna jambo la kulazimishwa au la uhuru kabisa ila lipo jambo moja kati ya hayo mawili" Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya "Taqiyyah" (kutodhihirisha imani?
Jibu: Itikadi ya KKishia juu ya "Taqiyyah" inaelezwa katika Qur'ani Tukufu na Mwenyezi Mungu: "Anayemkataa Mwenyezi Mungu baada ya imani yake, isipokuwa yule aliyelazimishwa hali moyo wake unatulia kwa imani" (Qur'ani, 16:106). Vilevile anasema "Walioamini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi badala ya wanaoamini, na atakayefanya hivyo, basi hatakuwa na chochote kwa Mwenyezi Mungu, ila ya kwamba mjilinde na maovu yao" Qur'ani, 3:28). Mwislaam anatakiwa ayashike maamrisho ya kiislaam lakini hata hivyo anaweza kwenda kinyume chake (kwa kutodhirisha) katika wakati wa hatari na mashaka, kama anavyosema Mwenyezi Mungu: "Mwenyezi Mungu Huwatakieni yaliyo mepesi wala Hawatakieni yaliyo mazito" (Qur'ani, 2:78) Pia Mtume Mtukufu amesema: "Hakuna madhara wala shida katika Uislaam". Swali: Nini itikadi ya Mashia juu ya ukafiri na Uislaam?
Jibu: Mashia wanaamini kwamba Mwislaam ni yule ambaye anashuhudia shahada mbili, " Hakuna Mungu ila Mwenyezi Mungu mmoja, na Muhammad ni Mtume wake". Isitoshe, anafuata maamrisho yaliyoletwa na Mtume ZMtukufu (s.a.w) kutoka kwa Mola wake. Mtu huyu anastahiki kupewa hifadhi ya nafsi yake, mali na heshima yake na huwa ametakasika. Mambo yanayo wahusu Waislaam yanamhusu yeye pia, vilevile mambo yake yanawahusu Waislaam wote. Kafiri ni yule anayekataa shahada yoyote kati ya hizi mbili, au anakataa jambo lolote katika mambo ya kiislaam ambalo linajulikana kuwa ni miongoni mwa mafundisho ya Mtume (s.a.w). Swali: Nini maana ya "Usmat"
Jibu: "Ismat" (Umaaasumu) maana yake ni kutakasika kabisa kutokana na kila dhambi na dosari iwe ndogo au kubwa. Swali: Ni nani Maasumu (alie takasika na dhambi) kufuatana na itikadi ya Kishia? Jibu: Waliokuwa Maasumu ni Mitume, Manabii, Maimamu, Bibi Fatimah binti wa Mtume na Malaika, kama alivyosema Mwenyezi Mungu kuhusu Malaika: " Hawamwasi Mwenyezi Mungu kwa anayowaamrisha, na wanafanya kama wanavyoamuriwa". (Qur'ani, 66:6)
Swali: Nini itikadi na maelezo ya Mashia juu ya Kiyama? Jibu: Mashia wanaamini kwamba mtu anapotokwa na roho haangamii kama wanavyosema walahidi. Walikini anahamishwa kutoka dunia hii na kupelekwa katika dunia nyingine iitwayo Barzakhi. Hakika kaburi ni bustani katika mabustani ya Peponi kwa mwenye kuamini; na ni shimo la moto katika mashimo ya Motoni kwa mwenye kukufuru na kuasi. Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama atafufua maiti za wote wawili ili kuhesabu vitendo vyao. Yeye aliyekuwa mwema atalipwa kwa kuwekwa katika mabustani ya neema, na yule aliyekuwa mwasiatatupwa katika shimo la Moto. Siku hiyo kutakuwako sirati, Mizani, Kitabu Hodhi, Bustani na Moto. Swali: Nini itikadi ya Mashia kuhusu "Shifaa" (Maombezi)?
Jibu: Mashia wanaitakidi kwamba Mwenyezi Mungu atamruhusu yule amtakaye miongoni mwa Manabii, Maimamu, Maulamaa, na Mashahidi, na watu wema na kadhalika kuwaombea (kuwashafiia) baadhi ya waliotenda dhambi-kama anavyosema katika Qur'ani: "Hawata waombea ila yule aliyemridhia". (Qur'ani, 21:28) Na Mtume Mtukufu (s.a.w)amesema: "Shifaa yangu itakuwa kwa wale wafuasi wangu waliokuwa na madhambi".