1
ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI
DIBAJI
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu, Sala na Salamu zimshukie mbora wa mitume bwana wetu na mpenzi wetu Muhammad na pia (Sala na Salamu) ziwashukie watu wa kizazi chake walio wema tena waliotakasika. Amma Baad:
Bila shaka kimsingi dini inategemea itikadi ambazo huwa ni mkusanyiko wa misingi na mategemeo ambayo huyaamini waliyoikubali Dini hii au ile, na misingi hiyo ndiyo ambayo hapana budi imani yao isimame kwayo juu ya dalili madhubuti na hoja iliyo wazi ambayo inakubaliana na akili wanayoiamini watu wote ili itoe fursa ya kuwatosheleza kwa yale inayowaitia.
Japo kuwa hali ni hiyo lakini ziko fikra ambazo ni ngumu kwa ulimwengu kuzifasiri kama ilivyo ugumu kwa akili kuzisadiki kwa mara ya kwanza.
Miongoni mwa hizo kwa mfano, moto kuwa baridi na salama wakati elimu na akili zinakubaliana kwamba moto una joto kali linaloangamiza, au ndege kukatwa katwa na kuwa vipande vipande vilivyotawanyika juu ya mlima kisha vikaitwa na kuja haraka wakati ambapo elimu na akili vinapinga hilo, au kuponywa kipofu na mwenye mbaranga au bubu kwa kiasi cha Nabii Isa kumgusa, bali zaidi ya hapo kama kufufua wafu, wakati ambapo elimu na akili havipati tafsiri ya jambo hili... nayo ni a ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka kwenye mikono ya Mitume wake amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao, na miujiza hiyo inapatikana kwa Waislamu na Mayahudi na Wakristo.
Bila shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu aliiweka miujiza hiyo na mambo yaliyo kinyume na maumbile kwa Manabii wake na Mitume wake (a.s.) ili waja wapate kufahamu kwamba akili zao ni fupi kuweza kufahamu na kudhibiti kila kitu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuwapa elimu isipokuwa kidogo tu, na huenda hilo ni kwa ajili ya manufaa yao na ukamilifu wao unaowahusu.
Kwa hakika watu wengi walikufuru kutokana na neema za Mwenyezi Mungu na wengi wakapinga kuwepo kwake Mwenyezi Mungu, wengi miongoni mwao wakajivuna kwa elimu na akili mpaka wakaviabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu. Hali hii ilitokea pamoja na huo uchache wa elimu na akili fupi, hivyo basi hali ingekuwaje lau Mwenyezi Mungu angewapa elimu ya kila kitu?!
Na kwa sababu ya umuhimu wa aqida na ubora wake katika imani ya Muislamu, bila shaka kitabu changu hiki kimeleta mkusanyiko wa itikadi za Kiislamu ambazo zimekuja ndani ya Qur'an Tukufu na Sunna Tukufu ya Mtume na ni itikadi ambazo zimekuwa ndiyo mahala pa tofauti za madhehebu ya Kiislamu. Basi mimi nimetenga mlango maalum unaohusu itikadi za Kisunni na Kishia ndani ya Qur'an na Sunna ya Mtume, kisha nimefuatisha baada ya hapo mas-ala mengine ambayo wametofautiana ndani yake na baadhi yao kuwafedhehesha baadhi nyingine bila ya sababu ya halali.
Nimefanya hivyo nikilenga kubainisha kile ambacho mimi nimekiona kuwa ndiyo haki hali ya kuwa natamani kumsaidia yeyote anayetaka kuutafuta ukweli, pia nikiwa nataraji kutoa mchango kwa hilo katika kusimamisha umoja wa Kiislamu juu ya msingi imara kifikra. Namuomba Mwenyezi Mungu atuwafikishe sote kwa yale ayapendayo na kuyaridhia na aiunganishe kalima ya Waislamu juu ya ukweli bila shaka yeye ndiye mwenye nguvu mwenye uwezo.
QUR'AN KWA UPANDE WA SHIA NA SUNNI
QUR'AN (INAVYOTAMBULIKANA) KWA MASUNNI NA MASHIA IMAMIYYAH
Qur'an ni maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyoteremshwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), nayo hiyo Qur'an haiwezi kutanguliwa (na sheria yeyote) hapo kabla na baadaye nayo ndiyo rejea kuu kwa Waislamu katika hukmu zao na ibada zao na itikadi zao, yeyote mwenye kuitilia shaka au akaitweza basi huyo huwa kajitoa nje ya dhamana ya Uislamu. Kwa hiyo Waislamu wote wamekubaliana waitukuze na kuiheshimu na kufanya ibada (zao) kwa mujibu wa (mafunzo) yaliyokuja ndani yake.
Lakini Waislamu wametofautiana katika kuifasiri na kuifafanua. Rejea ya Mashia katika tafsiri na taawili za Qur'an hurudi kwa Mtume (s.a.w.) na ufafanuzi uliotolewa na Maimamu watokanao na nyumba ya Mtume (s.a.w.). Ama rejea ya Masunni,wao hurudi kwenye hadithi za Mtume (s.a.w.) pia, lakini Masunni huwategemea Masahaba bila ya kuchambua au Maimamu wanne wenye Madhehebu mashuhuri, (wao huwategemea hao) katika kunakili hadithi, ufafanuzi wake na tafsiri yake.
Na kutokana na hali hiyo ndipo ilipoanzia tofauti katika mas-ala mengi ya Kiislamu hasa yale ya Kifiq-hi, na ilipokuwa kuna tofauti iliyowazi baina ya Madhehebu manne ya Kisunni, hivyo siyo ajabu tofauti hiyo kuwa kubwa zaidi baina ya Masunni na madhehebu yanayofuata mafunzo yatokanayo na watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.).
Kama nilivyoeleza mwanzoni mwa kitabu, bila shaka mimi sitaeleza baadhi ya mifano kwa nia ya kufupisha maelezo, na ni wajibu wa yeyote yule atakaye kutafiti na kupata ziada apige mbizi chini ya bahari (atafiti kwa undani zaidi) ili aweze kutoa kile akiwezacho miongoni mwa ukweli uliomo ndani ya johari zilizojificha!!
Masunni na Mashia wote wameafikiana juu ya kauli isemayo kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliwabainishia Waislamu hukmu zote za Qur'an na alizitafsiri aya zake zote, lakini wametofautiana juu ya nani ambaye inapasa kumrejea baada ya kufariki Mtume (s.a.w.) ili kufahamu ubainisho huo aliobainisha Mtume na tafsiri aliyotafsiri.
Masunni wao wamekwenda upande wa kuwategemea Masahaba bila kuchambua (ni Sahaba gani afaaye na yupi hafai kwao wote ni sawa tu) na baada ya Masahaba Masunni wanawategemea Maimamu wanne na wanachuoni wa umma wa Kiislamu. Ama Mashia, wao wamesema kwamba: "Maimamu watokanao na nyumba ya Mtume (s.a.w.) ndiyo wanaostahiki kurejewa na pia Masahaba wateule, kwani Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) ndiyo wale wenye kumbukumbu ambazo Mwenyezi Mungu ametuamuru tuwarejee pale aliposema:
"Waulizeni wenye kumbukumbu ikiwa ninyi hamjui" (Qur'an, 16:43)
Na ndiyo wale ambao Mwenyezi Mungu amewateua na akawarithisha elimu ya kitabu (yaani Qur'an) pale aliposema:
"Kisha tumewarithisha kitabu wale ambao tumewateua miongoni mwa waja wetu". (Qur'an, 35:32)
Na kwa ajili ya yote hayo Mtume (s.a.w.) amewafanya wao kuwa mfano wa Qur'an na ni kizito cha pili ambacho amewaamuru Waislamu kushikamana nacho pale aliposema: "Nimeacha kwenu vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi changu watu wa nyumba yangu, vitu ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea kamwe baada yangu." Taz: Sahih Tirmidhi Juz. 2 uk. 329, pia Annasai na Imam Ahmad.
Na katika tamko la Sahihi Muslim amesema: "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu" alisema hivyo mara tatu.
Taz: Sahih Muslim Juz. 2 uk. 362. Mlango wa Fadhail za Ali Bin Abi Talib Na ni jambo linalofahamika mno kwamba watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) wao walikuwa ni wajuzi na wachamungu na ni wabora mno kuliko watu wengine.
Amesema Farazdaq kuhusu watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.): "Ikiwa watahesabiwa wachamungu, basi wao watakuwa ndiyo viongozi wa wachamungu hao, au pakisemwa ni kinanani walio bora kuliko watu wa ardhini? Patasemwa ni wao". Hapa ninaleta mfano mmoja ili kukumbusha mtiririko wa maungamano yaliyopo baina ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) na Qur'an Tukufu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Basi ninaapa kwa maanguko ya nyota, na hakika hicho bila shaka ni kiapo kikubwa, laiti mngelijua, hakika hii (mnayosomewa) ni Qur'an Tukufu (yenye heshima kubwa) imetolewa ndani ya kitabu kilichohifadhiwa kweli kweli hawawezi kukifahamu (vilivyo maana yake) ila wale waliotakaswa" (Qur. 56:75-79)
Aya hizi zinaashiria bila ya kificho ya kwamba, watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) wakiongozwa na yeye mwenyewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) wao ndiyo wale ambao wanaozifahamu maana za Qur'an zilizo ngumu kufahamika (kwa wengine), kwani lau sisi tutaangalia kwa makini kuhusu kiapo alichokiapia Mwenyezi Mungu Mtukufu, tutayakuta mambo yafuatayo:
Ikiwa Mwenyezi Mungu huapia Alasiri na Kalamu na Mti wa Tini na Mzeituni, basi utukufu wa kuapia maanguko ya nyota uko wazi kutokana na yale yanayoshikamana juu yake miongoni mwa siri na athari zipatikanazo juu ya ulimwengu kwa amri yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na tunaona" utukufu wa kiapo ndani ya mfumo wa Nafyi na Ithba't na baada ya kiapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anaweka mkazo ya kwamba hii ni Qur'an Tukufu iliyotolewa ndani ya kitabu kilichohifadhiwa kweli kweli, kisha Mwenyezi Mungu anasema, "Hawawezi kuifahamu vilivyo maana yake isipokuwa wale waliotakaswa." Na hii "La" iliyopo hapa (La-Yamassuhu) ni yakukanusha, na hii (Yamassuhu) inamaanisha kuifahamu Qur'an, na makusudio yake siyo kugusa kwa mkono kwani kuna tofauti baina ya tamko la "Al-Lamsu"na "Al-Massu".
Mwenyezi Mungu Amesema:
"Hakika wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu shetani anapowatia wasi wasi, hukumbuka na mara huiona haki (na kuifuata)". (Qur'an, 7:201)
Na amesema tena Mwenyezi Mungu:
"Wale wanaokula riba hawasimami ila ni kama asimamavyo yule ambaye shetani amemvuruga kwa kumzuga". (Qur'an, 2:275) Basi tamko "Al-massu" linalopatikana hapa linafungamana na akili na kufahamu na siyo kushika kwa mkono, itakuwaje basi Mwenyezi Mungu Mtukufu aape kwamba Qur'an haiguswi kwa mkono isipokuwa na yule aliyejitwahirisha, na hali ya kuwa historia inatusimulia kwamba baadhi ya mijitu mijeuri iliichezea na kuichana na pia tumeshuhudia Waisraeli wakiikanyaga kwa miguu yao (Mwenyezi Mungu atulinde na shari zao). Pia tumewaona wanaichoma moto pale walipoivamia Beirut katika vurugu zao mbaya walizozifanya, na Televisheni ziliinasa hali hiyo mbaya ya kutisha.
Kwa hiyo maana ya kauli hiyo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kuwa: "Hawezi kufahamu maana za ndani za Qur'an ila wale wateule miongoni mwa waja wake ambao amewateua na akawatakasa sana." Na hilo tamko la "Mutahharu'n" liliomo ndani ya aya hii ni jina la kilichotendewa yaani kule kutahirika kumetuka juu yao. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu amekuondoleeni uchafu enyi watu wa nyumba (ya Mtume) na kukutakaseni sana sana". (Qur'an, 33:33)
Basi kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema, "La Yamassuhu Illal-Mutahharun " maana yake ni kuwa, "Hawezi kufahamu uhakika wa Qur'an isipokuwa Mtume (s.a.w.) na watu wa nyumba yake (a.s.) na kwa ajili hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema kuwahusu Ahlul-Bait kama ifuatavyo. "Nyota ni amani kwa watu wa ardhini (zinawaongoza) wasiangamie (baharini), na watu wa nyumba yangu ni amani kwa umma wangu (wanawaongoza) wasihitilafiane, basi ikiwa kabila fulani miongoni mwa Waarabu litakwenda kinyume (na kizazi changu), basi watahitilafiana na watakuwa kundi la ibilisi".
Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 149, imepokewa toka kwa Ibn Abbas na amesema kuwa Isnad ya Hadithi hii ni Sahih. Kwa hiyo mwendo waufuatao Mashia kuhusu tafsiri na taawili ya Qur'an unategemea Qur'an Tukufu na hadithi za Mtume (s.a.w.) ambazo zimepokelewa pia kwa Masunni kama tulivyokuta.
MTUME KWA MASUNNI NA MASHIAIMAMIYYAH
MTUME (INAVYOTAMBULIKANA) KWA MASUNNI NA MASHIAIMAMIYYAH
Sunna ni kila kile alichokisema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), au alichokitenda au kukithibitisha. Nayo Sunna ndiyo rejea ya pili baada ya Qur'an Tukufu kwa Masunni na Mashia katika hukmu zao na ibada zao na itikadi zao. Masunni huongeza kwenye Sunna ya Mtume, Sunna za Makhalifa wanne ambao ni Abubakr, Umar, Uthman na Ali, na hilo wanalifanya kutokana na hadithi wanayoisimulia isemayo kuwa:
"Shikamaneni na Sunna zangu na Sunna za Makhalifa viongozi walioongoka baada yangu zing'ang'anie kwa magego". Na hilo ni dalili ya wazi kutokana na kufuata kwao Sunna ya Ummar Bin Khattab inayohusu sala ya tarawehe ambayo Mtume (s.a.w.) aliikataza (isisaliwe jamaa). Na baadhi ya Masunni huongeza kwenye Sunna ya Mtume, Sunna ya Masahaba wote (yaani Sahaba yeyote yule awaye) na hulifanya hilo kutokana na hadithi yao isemayo:
"Masahaba zangu ni kama nyota, yeyote mutakayemfuata mtaongoka". Vilevile kuna hadithi nyingine isemayo: "Masahaba wangu ni amani ya umma wangu".
Taz: Sahih Muslim Kitabu Fadhailus-Sahabah na Musnad Ahmad bin HanbalJuz. 4 uk. 398.
Amma ile hadithi ya sahaba zangu ni kama nyota, bila shaka haikubaliani na akili, mantiq na ukweli wa kielimu, kwani Waarabu walikuwa hawaongoki katika safari zao za jangwani kwa kiasi cha kufuata nyota yoyote ile miongoni mwa nyota bali walikuwa wakiongoka kwa kufuata nyota maalum zinazotambulikana majina yake kuhusu safari zao.
Kadhalika hadithi hii haiungwi mkono na matukio halisi ambayo yalidhihirika kutoka kwa baadhi ya Masahaba baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), kwani wako miongoni mwa Masahaba walioritadi, kama ambavyo Masahaba walihitilafiana katika mambo mengi yaliyosababisha kushutumiana wao kwa wao na kulaaniana wao kwa wao na kuuwana wao kwa wao. Kadhalika kuna baadhi ya Masahaba waliadhibiwa kwa makosa ya kunywa pombe, kuzini, wizi na mengineyo. Basi ni vipi mtu mwenye akili ataikubali hadithi ambayo inaamuru kuwafuata watu kama hawa? Na ni vipi mtu ataongoka kwa kumfuata Muawiyah aliyetoka dhidi ya Imam wa zama zake pale alipoamua kumpiga Imam Ali (a.s.) na hali mtu huyo anatambua kwamba Mtume (s.a.w.) alimuita Muawiyah kuwa ni kiongozi wa kundi lenye kuasi.
Na ni vipi mtu atakuwa ameongoka kwa kumfuata Amr bin Al-A's, Mughira bin Shuubah na Bisr bin Ar-Taah. Watu hawa waliwaua raia bila makosa ili tu wauimarishe ufalme wa Banu Umayyah. Nawe Ewe msomaji mwenye utambuzi utapoisoma hadithi isemayo, "Masahaba wangu ni kama nyota" itakubainikia kwamba hadithi hiyo ni ya kuzushwa kwani inaelekezwa kwa Masahaba wenyewe, basi ni vipi Mtume (s.a.w.) atasema kuwaambia hao hao Masahaba "Enyi Sahaba zangu wafuateni Masahaba zangu"? Ama hadithi ya kusema, "Enyi Sahaba zangu shikamaneni na Maimamu watokanao na watu wa nyumba yangu, wao watakuongozeni baada yangu" hadithi hii iko karibu mno na ukweli kwani inao ushahidi mwingi unaoungwa mkono na Sunna ya Mtume (s.a.w.).
Nao Mashia Ithna-Asheriyah wanasema kwamba makusudio ya hadithi isemayo kuwa: "Shikamaneni na Sunna zangu na Sunna za Makhalifa viongozi waliongoka baada yangu" Makhalifa hao ni Maimamu kumi na wawili miongoni mwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.), wao ndiyo wale ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) ameuwajibishia umma wake kushikamana nao na kuwafuata kama wanavyoshikamana na kukifuata kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Taz: 1. Sahih TirmidhiJuz. 5 uk. 328
2. Sahih Muslim Juz. 2 uk. 362.
3. Khasaisun-Nasai
4. Kanzul-Ummal Juz. 1 uk. 44.
5. Musnad Imam Ahmad bin Hanbal Juz. 5 uk 289.
6. Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 148.
7. As-Sawaiqul-Muhriqah ya ibn Hajar uk. 48.
8. At-Tabaqatul-Kubra ya ibn Saad Juz. 2 uk. 194.
9. At-Tabrani Juz. 1 uk. 131.
Na kwa kuwa nilikuwa nimeapa kwamba sitatoa dalili isipokuwa zile ambazo Mashia huzitolea ushahidi kutoka ndani ya vitabu vya Masunni, basi bila shaka nitatosheka kwa hoja hiyo, lakini vinginevyo ndani ya vitabu vya Kishia kuna hoja zaidi ya hizo tena kwa maelezo yaliyo bayana zaidi. Natoa mfano mmoja tu wa hoja hizo; As-Saduq amethibitisha ndani ya Ikmal kwa sanad inayoishia kwa Imam As-Sadiq naye amepokea toka kwa baba yake ambaye naye kapokea toka kwa babu yake amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema, Maimamu baada yangu ni kumi na mbili, wa kwanza wao ni Ali na wa mwisho wao ni "Al-Qaim" (Al-Mahdi) wao ndiyo makhalifa wangu na ndiyo mawasii wangu". Ni lazima ifahamike kwamba, Mashia hawasemi kuwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) wanayo haki ya kuweka sheria kwa maana ya kwamba sunna yao iwe ni ijtihadi itokanayo na wao, bali wanasema kwamba hukmu zao zote zinatokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu alimfundisha Ali, na Ali naye akawafundisha wanawe, na hiyo ni elimu ambayo wanarithiana.Mashia wanazo dalili nyingi walizozinakili kutoka kwa Ahlul Sunna wal jamaah ndani ya Sihah, Masnad na vitabu vya historia juu ya jambo hili.
Swali ambalo siku zote linabakia, Je, ni kwa nini Masunni hawakuyatumia yaliyomo ndani ya hadithi hizi ambazo na kwao pia ni Sahihi? Kisha baada ya hayo, Mashia na Masunni wanahitilafiana kuhusu tafsiri ya hadithi zilizothibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kama ulivyotangulia ufafanuzi wake katika maelezo juu ya kuhitilafiana kwao katika tafsiri ya Qur'an. Wanahitilafiana kuhusu maana ya Khulafaur Rashidun ambayo imekuja ndani ya hadithi yake Mtume (s.a.w.) na pande zote mbili zinakubaliana juu ya usahihi wa hadithi hiyo, lakini Masunni huifasiri kwamba hao ni Makhalifa wanne ambao walikikalia cheo cha Ukhalifa baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, nao Mashia wanaifasiri maana ya Khulafaur-Rashidun kuwa ni Makhalifa kumi na wawili nao ni Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.).
Kwa hali hii basi tunaiona tofauti na hitilafu imeenea katika kitu ambacho kinafungamana na watu ambao Qur'an imewatakasa na Mtume naye ameamuru kuwafuata. Mfano wa jambo hilo ni ile kauli ya Mtume (s.a.w.) aliposema:
"Wanachuoni wa umma wangu ni bora kuliko Manabii wa Bani Israil" au "Wanachuoni ni warithi wa Manabii".
Taz: Sahih Bukhar Juz. 1 Kitabul-Ilmi, na Sahihi Tirmidhi, Kitabul-Ilmi pia. Masunni wao huieneza hadithi hii kwa wanachuoni wote wa umma, wakati ambapo Mashia Ithna-asheriyyah wao huihusisha kwa Maimamu kumi na wawili tu. Kwa ajili hiyo ndiyo maana wao huwaboresha Maimamu hao juu ya Manabii isipokuwa wale Ulul-Azm miongoni mwa Mitume.
Na ukweli ulivyo ni kwamba akili inaelekea kukubaliana na uhusishaji huu. Kwanza: Qur'an imewarithisha elimu ya kitabu wale ambao Mwenyezi Mungu amewateua miongoni mwa waja wake, hivyo huko ni kuhusisha (kitu kwa watu maalum) kama ambavyo Mtume wa Mwenyezi Mungu amewahusisha watu wa nyumba yake kwa mambo mengi ambayo hakuwashirikisha ndani ya mambo hayo mtu yeyote mpaka akawaita wao kuwa ni Merikebu ya uokovu na akawaita kuwa ni Maimamu waongofu, ni taa za kuondosha kiza na ni kizoto cha pili ambacho kinawalinda (Waislamu) wasipotee.
Hivyo basi, inadhihiri kutokana na hali hii kwamba kauli ya Masunni inapingana na kuhusisha ambako Qur'an imekuthibitisha na pia sunna ya Mtume, nayo akili haikubaliani na kauli hiyo kutokana na utata uliomo na kutokufahamika kwa wanachuoni hao ambao Mwenyezi Mungu amewaondoshea uchafu na kuwatakasa, pia Masunni kutokuwapambanua wanachuoni ambao watawala wa Kibanu Umayya na Banu Abbas walilazimisha wafuatwe. Kuna tofauti kubwa mno baina ya hao wanachuoni (waliowekwa na watawala) na baina ya Maimamu kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.), Maimamu ambao historia haielezi habari za mwalimu yeyote ambaye wamesoma kwake isipokuwa wao mtoto hupata kwa baba yake. Pamoja na hayo wanachuoni wa Kisunni katika elimu zao wamepokea riwaya nyingi za ajabu na hasa kwa Imam Al-Baqir na Imam As-Sadiq na Imam Arridha ambaye kwa elimu yake aliwanyamazisha Maqadhi arobaini waliokusanywa kwake na Maamun, hali ya kuwa Imam Ridha akiwa bado mtoto mdogo. Taz:Al-Iqdul-Farid cha ibn Abd Rabih-Al-Fusul-Muhimmah cha ibns-Sabbagh Al-Maliki Juz. uk. 42.
Na miongoni mwa mambo yanayotia nguvu kuwapambanua watu wa nyumba ya Mtume na watu wengine ni ile hali ya kutofautiana Maimam wa Madhehebu manne ya Kisunni katika Mas-ala mengi ya Kifiqhi wakati ambapo Maimamu kumi na wawili katika Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) hawatofautiani hata katika suala moja. Pili: Lau tutaichukua kauli ya Masunni katika kuenea kwa aya hizi na hadithi hizi kwa wanachuoni wote wa umma huu, basi ingewajibika kuwepo maoni na madhehebu mengi kila zama zinavyopita na kungekuwa na maelfu ya madhehebu. Na huenda wanachuoni wa Kisunni walizindukana mapema kutokana na ubovu wa rai hii na kutenguka kwa umoja wakiitikadi, basi haraka wakafunga mlango wa ijtihad tangu hapo zamani za kale.
Amma kauli ya Mashia, inaita kwenye umoja na mshikamano juu ya Maimamu wanaotambulikana, ambao Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamewahusisha kwa maarifa yote ambayo Waislamu wanayahitajia katika nyakati zote.Hivyo basi haiwezekani kwa mzushi yeyote kuzua uongo dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mturne na wala hawezi kuzua madhehebu yatakayowalazimisha watu kuyafuata.
Hivyo basi tofauti yao (Masunni na Mashia) kuhusu mas-ala haya ni kama ilivyo tofauti baina yao juu ya Mahdi ambaye pande zote mbili zinamuamini, lakini Mahdi kwa Mashia anafahamika na kutambulikana (wazazi wake) baba yake na babu yake, na kwa Masunni mpaka sasa hajulikani na (wanasema) atazaliwa zama za mwishoni, na ndiyo maana utaona wengi miongoni mwao hudai kuwa wao ndiye yule Mahdi (aliyeahidiwa) Nami binafsi(nilipokutana na) Sheikh Ismail ambaye ni kiongozi wa Tariqa ya Madaniyyah aliniambia kwamba yeye ndiye yule Mahdi anayengojewa, na aliyasema madai hayo mbele ya rafiki yangu ambaye alikuwa miongoni mwa wafuasi wake lakini(rafiki yangu huyo) baadaye alizindukana.
Ama kwa Mashia wao wanasema, haiwezekani kabisa kwa mtoto atakayezaliwa kwao wao kudai jambo hilo hata kama kuna mtu atamuita mwanawe jina la Mahdi, kwani kufanya hivyo itakuwa ni kwa ajili ya kutabaruku tu kwa jina hilo la Imam wa zama hizi, na ni kama ambavyo mmoja wetu awezavyo kumwita mwanawe jina la Muhammad au Ali kwani kwa Mashia kudhihiri kwa Mahdi ni jambo ambalo kwa dhati yake ni muujiza kwa kuwa Mahdi alizaliwa tangu karne kumi na mbili zilizopita na akawa katika ghaibah. Kisha baada ya yote haya huenda Masunni wakatofautiana juu ya maana ya hadithi sahihi iliyothibiti katika pande zote mbili hata kama hadithi hiyo haifungamani na watu, na kuhusu hilo ni mfano wa hadithi isemayo: "Ikhtilafu katika Umma wangu ni Rehma" hadithi ambayo Masunni wanaifasiri kwamba ikhtilafu za hukmu za kifiqhi katika jambo moja ni rehma kwa Muislamu ambaye anaweza kuchagua ni hukmu ipi inayomnasibu na kukubaliana na ufumbuzi anaouridhia, basi kufanya hivyo ni rehma kwake. Kwa mfano Imam Malik atakuwa ni mgumu katika mas-ala fulani, basi Muislamu anaweza kumfuata Abu Hanifah ambaye amerahisisha hukmu katika jambo hilo.
Ama kwa Mashia, wao wanaifasiri hadithi hiyo kwa maana isiyokuwa hiyo na wanasimulia kwamba, Imam Jaafar As-Sadiq (a.s.) alipoulizwa juu ya hadithi hii isemayo "Ikhtilafu katika umma wangu ni Rehma" yeye alisema, "Amenena kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu", basi muulizaji akasema, "Ikiwa ikhtilafu yao ni Rehma basi mshikamano wao ni balaa"!! Imam As-Sadiq akasema, "Sivyo ulivyofahamu wewe na wanavyofahamu wengine, bali Mtume alikusudia ikhtilifu ya baadhi yao kwa baadhi nyingine yaani baadhi yao kusafiri kwenda kwa baadhi nyingine na kwenda kwa mwanachuoni yule na kumkusudia kwa ajili ya kusoma, na hapo Imam akatolea ushahidi kwa kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Litoke kundi katika kila taifa miongoni mwao ili wakajifunze dini na kisha waje kuwaonya wenzao watakaporudi ili wapate kujihadharisha" (Qur'an, 9:122).
Kisha aliongeza akasema: "Ikiwa watahitilafiana katika, dini basi watakuwa ni kundi la ibilisi". Na hii tafsiri kama tuionavyo ni tafsiri inayokinaisha na kuita kwenye umoja wa itikadi na siyo kuhitilafiana ndani yake. Nayo ni kama tunavyoona tafsiri inayokinaisha ni kwa sababu inaita kwenye umoja wa kiitikadi na siyo mfarakano.[1] Kisha hadithi hii kwa maf-humu ya Kisunni haikubaliki, kwani inapelekea kuleta mgawanyiko na kuhitilafiana, maoni kuwa mengi, madhehebu nayo kuwa mengi na yote haya yanapingana na Qur'an Tukufu ambayo inatuita kwenye umoja na mshikamano juu ya kitu kimoja.
Mwenyezi Mimgu Mtukufu anasema:
"Na kwa yakini huu umma wenu ni umma mmoja na mimi ni Mola wenu, basi niogopeni". (Qur'an, 23:52)
Na anasema tena: "Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala musitengane" (Qur'an, 3:103)
Na anasema tena: "Na wala musizozane mutashindwa na nguvu zenu zitapotea". (Qur'an, 8:46)
Basi ni kuzozana kupi na kutengana kwa aina gani kukubwa kuliko umma mmoja kugawanyika kwenye madhehebu na vikundi vinavyotofautiana baadhi hii na baadhi nyingine na upande huu kuudharau upande ule bali zaidi ya hivyo ni kukufurishana kwa baadhi hii kuikufiirisha baadhi ile kiasi cha upande fulani kuhalalisha damu ya upande mwingine? Na haya yanatokea kwa vitendo siku zote na historia ndiyo shahidi mkubwa wa hayo, mambo ambayo Mwenyezi Mungu alikwisha kutuonya kutokana na matokeo yake mabaya ambayo umma wetu utayafikia iwapo utafarakana akasema:
"Musiwe kama wale waliofarakana na kuhitilafiana baada ya kuwafikia hoja zilizowazi". (Qur'an, 3:105)
"Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote ule". (Qur'an, 6:159)
"Na wala musiwe miongoni mwa washirikina, katika wale ambao waliitenga dini yao na wakawa makundi makundi kila kikundi kinafurahia kilicho nacho". (30:31-32)
Na hapa inapendeza kuashiria kwamba maana ya neno, "Shiyaan" halina uhusiano na "As-shiah" (au Shia) kama ambavyo baadhi ya watu wa kawaida wanavyo dhania hasa pale aliponijia mtu fulani akinipa nasaha juu ya madai yake akasema: "Ndugu yangu nakuapia Mwenyezi Mungu wachana na Ushia kwani Mwenyezi Mungu anaukemea na Mtume wake naye ametutahadharisha tusiwe miongoni mwao." Mimi nikasema, "Ameukemea na kututahadharisha namna gani"? Akasema: "Hakika wale walioifarikisha dini yao na wakawa makundi makundi (Shiyaan) huna nao uhusiano wowote". Mimi nilijaribu kumkinaisha kwamba "Shiyaan" maana yake ni makundi na wala hakuna uhusiano na "Shia", lakini Bwana yule inasikitisha kwamba hakukinaika kwani kiongozi wake ambaye ni Imam wa msikiti ndivyo alivyomfundisha na akamtahadharisha dhidi ya Mashia, basi hawezi kukubali isipokuwa fikra hiyo.
Narejea kwenye maudhui na ninasema kwamba mimi nilikuwa nikichanganyikiwa kabla sijafahamu kila nisomapo hadithi ya "Ikhtilafu katika umma wangu ni Rehma" na nilikuwa nailinganisha na hadithi isemayo:
"Watafarikiana umma wangu makundi sabini na mbili na yote yataingia motoni isipokuwa kundi moja." Basi nilikuwa najiuliza itakuwaje ikhtilafu ya umma kuwa rehma wakati huo huo ni jambo linalowajibisha kuingia motoni? Na baada ya kuwa nimeisoma tafsiri ya Imam Jafaar As-Sadiq (a.s.) inayohusu hadithi hii, basi mushkeli wangu uliondoka na wao ndiyo hasa Maimamu wa uongofu na ndiyo taa zinazoondosha kiza , wao ndiyo wenye haki ya kuifasiri Qur'ani na sunna ya Mtume, na ni sawa kabisa kwa Mtume (s.a.w.) aseme kuhusu haki yao Maimamu hao wa nyumba yake kama ifuatavyo:- "Mfano wa watu wa nyumba yangu kwenu ninyi ni kama Safina ya Nuhu, yeyote mwenye kupanda Safina hiyo ataokoka na atakayeikhalifu (akakosa kupanda)atazama, musiwatangulie mutaangamia na wala musiwakhalifu mutaangamia na wala musiwafundishe kwani wao ni wajuzi mno kuliko ninyi".
Taz: 1). As-Sawaiqul-Muhriqah ya ibn Hajar uk. 136
na uk. 227.
2). Al-Jamius-Saghir ya Suyut Juz. 2 uk. 132. 3). Musnad Ahmad bin Hanbal Juz. 3 uk. 17 na Juz. 4 uk.
4). Hil-Yatul-Auliyaa Juz. 4 uk. 306. 5). Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 151. 6). Al-Muujamus-Saghir ya TabraniJuz.2 uk. 22. Na ilistahiki kabisa kwa Imam Ali (a.s.) aseme kama ifuatavyo:"Waangalieni watu wa nyumba ya Mtume wenu, shikamaneni na kizazi chao na mufuate nyayo zao, hawatakutoeni kwenye uongofu na hawatakurudisheni kwenye maangamivu, basi wakitua nanyi tuweni, wakinyanyuka nanyi nyanyukeni. Na wala musiwatangulie mutaangamia na musiwaache mutaangamia." Taz: Nahjul-Balagha ya Imam Ali Juz. 2 uk. 190.
Na amesema tena Imam Ali (a.s.) katika khutba yake nyingine akitambulisha daraja ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.): "Wao ndiyo uhai wa elimu na wao ndiyo kifo cha ujinga, upole wao utakuelezeni kiwango cha elimu yao, na dhahiri yao itakuelezeni undani wao, na ukimya wao utakuelezeni hekima ya mantiq yao, hawaendi kinyume na haki na wala hawatofautiani ndani yake, wao ndiyo nguzo za Uislamu na ndiyo tegemeo la umoja. Kwao wao haki ilirejea mahala pake na batili ikaondoka mahala ilipokuwa imesimama na ulimi wake ukakatika pale ulipootea, wameizingatia haki kwa mazingatio ya kuhifadhi na siyo mazingatio ya kusikia na kueleza kwani waelezaji wa elimu ni wengi na wanaohifadhi ni wachache." Taz: Nahjul-Balagha ya Imam Ali Juz. 3 uk. 439.
Naam, bila shaka Imam Ali amesema kweli kwa hayo aliyoyabainisha kwani yeye ndiye mlango wa mji wa elimu, kwa kuwa kuna tofauti kubwa kati ya yule aliyeifahamu dini kwa akili ya mazmgatio na kuihifadhi na yule aliyeifahamu dini kwa akili ya kusikia na kueleza tu. Na wasikiao na kueleza wako wengi, kwani ilikuwaje idadi ya Masahaba wengi waliokuwa wakikaa na Mtume (s.a.w.) na kusikiliza hadithi nyingi na wakizinakili bila kufahamu wala kujua? Hivyo basi maana ya hadithi hubadilika na huenda ikapelekea kinyume cha makusudio ya Mtume (s.a.w.), na huenda baadhi ya nyakati ikapelekea kwenye kufru kutokana na ugumu wa Masahaba kuelewa maana halisi ya hadithi hizo.
Mfano wa jambo hili ni ile riwaya aliyoieleza Abuhurairah kwamba: "Mwenyezi Mungu amemuumba Adam kwa Sura yake". Lakini Imam Jaafar As-Sadiq (a.s.) alifafanua jambo hilo akasema, "Hakika Mtume waMwenyezi Mungu (s.a.w.) aliwasikia watu wawili wakitukanana, basi mmoja wao akamwambia mwenziwe, Mwenyezi Mungu na auharibu uso wako na uso wa yeyote afananaye na wewe, hapo ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema, "Hakika Mwenyezi Mungu amemuumba Adam kwa sura yake", yaani wewe kwa tusi lako kumtukana afananaye na huyu hakika umemtukana Adam kwani yeye anafanana naye".
Amma wale wanaoizingatia elimu na kuihifadhi ni wachache mno, na huenda mtu akamaliza umri wake katika kuitafuta elimu na asipate isipokuwa kidogo, na huenda akajihusisha na mlango fulani miongoni mwa milango ya elimu au fani fulani miongoni mwa fani mbali mbali za elimu na asiweze kuidhibiti milango yote.
Lakini jambo linalofahamika ni kwamba Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) walikuwa ni wajuzi wa elimu nyingi za aina mbali mbali, na hili limethibitishwa na Imam Ali kama wanavyolishuhudia wanahistoria. Kadhalika Imam Muhammad Al-Baqir na Jaafar As-Sadiq ambaye maelfu ya masheikh wamesoma kwake elimu mbali mbali na maarifa mengi katika falsafa, utibabu, kemia na elimu za maumbile na nyinginezo nyingi.