15
ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI
AR-RAJ-A' (KUREJEA KWENYE UHAI)
Kauli inayohusu mas-ala haya, wanayo Mashia peke yao, nami nimetafiti ndani ya vitabu vya Masunni sikukuta athari yoyote inayotajwa juu ya mas-ala haya. Mashia katika kuithibitisha "Ar-Raja'h" wametegemea khabari na riwaya walizozipokea kutoka kwa Maimamu watakatifu (a.s.) ya kwamba, "Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafufua baadhi ya waumini na baadhi ya watu waovu ili waumini wawaadhibu maadui zao ambao pia ni maadui wa Mwenyezi Mungu hapa duniani kabla ya akhera. Riwaya hizi zikisihi na ni sahihi tena kwa daraja ya mutawatiri kwa upande wa Shia, basi haziwalazimu Masunni iwapo hawataamini kusihi kwake na kwa ajili hiyo wao hawalazimiki kuziitakidi, kwani Maimau wa nyumba ya Mtume wamezisimulia toka kwa Babu yao Mtume Muhammad (s.a.w.) hivyo basi siyo sawa kabisa (kuwalazimisha waziitakidi) kwani sisi tumejilazimisha wenyewe kuwa waadilifu na kutokuwa na chuki katika utafiti (tuufanyao) hivyo hatutawakalifisha kitu isipokuwa kile walichojilazimisha wenyewe na wakakithibitisha ndani ya vitabu vyao.
Na kwa kuwa riwaya za "Ar'Raja'h" kwao hazikuja, basi wao wako hum kutozitumia riwaya hizo na wako huru kuzipinga, na hali hii itakuwepo kama kuna Shia fulani anataka kuwalazimisha kuzikubali riwaya hizo. Ama Mashia wenyewe hawakumlazimisha yeyote akubaliane na itikadi ya Ar-Raja'h wala hawamkufurishi anayeipinga. Hivyo basi hapana sababu yoyote inayopelekea kukebehi na vitisho dhidi ya Shia hasa ikiwa wao wanazifasiri baadhi ya aya kwa namna inayokubaliana na itikadi hiyo, kama vile kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Na siku tutakapowafufua katika kila umma makundi ya wale wanaopinga aya zetu nao watawekwa mafungu mafungu". (Qur'an, 27:83) Imekuja ndani ya Tafsiri Al-Qummi kutoka kwa ibn Abi Umair kutoka kwa Hammad naye toka kwa Abu Abdillah Jaa'far As-Sadiq (a.s) amesema:
"Watu wanasema nini kuhusu aya isemayo, Na siku tutakapowafufua katika kila umma makundi? Nikasema, wanasema hiyo ni katika siku ya Kiyama, akasema: Sivyo kama wasemavyo hakika hiyo ni katika Ar-Raja'h, basi je, Mwenyezi Mungu atafufua siku ya Qiyama kundi katika kila umma na kuwaacha wengine? Bila shaka aya ya Kiyama ni ile isemayo: "Na siku hiyo tutawafufua (viumbe wote) wala hatutamuacha hata mmoja miongoni mwao". (Qur'an, 18:47)
Kama ilivyokuja ndani ya kitabu kiitwacho, A'qaidul-Imamiyyah cha Sheikh Muhammad Ridha Al-Muzaffar aliposema: "Hakika kile ambacho Mashia Imamiyyah wanakubaliana nacho kwa mujibu wa mapokezi yaliyokuja toka kwa watu wa kizazi cha Mtume (s.a.w.) ni kwamba; Mwenyezi Mungu Mtukufu atawarejesha duniani watu fulani miongoni mwa watu waliokufa kwa sura zao zile zile walizokuwa nazo. Kisha atawapa nguvu kikundi cha watu fulani na kuwadhalilisha kikundi kingine na atawalipizia kisasi wenye kutenda haki dhidi ya wale waliokuwa wakitenda batili na wenye kudhulumiwa dhidi ya madhalimu, na hilo litakuwa zama zile atakaposimama Mahdi wa kizazi cha Muhammad (s.a.w.).
Na hatarudi isipokuwa yule ambaye daraja yake katika imani ilikuwa ni ya juu au yule aliyefikia' upeo wa juu katika maovu kisha baada ya hapo watarudishwa kwenye mauti, na baada ya hapo ndiyo itakuwa Kiyama na kulipwa wanayostahiki miongoni mwa thawabu au adhabu, kama alivyoeleza Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur'an yake juu ya kutamani kwa watu hawa wenye kurejea ambao hawakujirekebisha kwa kurejea (bali) wakapata adhabu ya Mwenyezi Mungu (watatamani) kurudi mara ya tatu huenda wakajirekebisha: "Wakasema Ewe Mola wetu, umetufisha mara mbili na umetuhuisha mara mbili nasi tukakiri makosa yetu. Basi je, iko njia ya kutoka (tukarejezwa duniani)? (Qur'an, 40:11) Taz: Aqaidul-Imamiyyah uk. 80, (Aqidah No. 32).
Mimi nasema ikiwa Masunni hawaamini Raja'h wanayo haki kikamilifu, lakini hawana haki yoyote ya kuwakebehi wanaoamini Raja'h kutokana na kwamba kwa wale wanaoamini yamethibiti maandiko. Hivyo basi asiyejua hana hoja dhidi ya ajuwaye na wala mjinga hana hoja dhidi ya mwanachuoni na siyo kwamba kukosa kukiamini kitu ni dalili ya kuwa kitu hicho ni batili, kwa sababu kuna hoja chungu nzima zenye nguvu walizonazo Waislamu lakini Ah-lul-Kitab miongoni mwa Wayahudi na Wakristo hawaziamini. Na kuna itikadi nyingi tu na riwaya nyingi hasa kuhusu Mawalii na watu wema ambazo ni muhali na mbaya lakini watu wa Tariqa za kisufi wanaziamini, lakini zote hizo hazilazimu ikebehiwe na iumbuliwe itikadi ya Kisunni. Na ikiwa Raja'h inayo Sanad ndani ya Qur'an na Sunna ya Mtume na ni kitu ambacho siyo muhali kwa Mwenyezi Mungu ambaye ametupigia mifano kuhusiana nacho ndani ya Qur'an kama pale aliposema: "Au kama yule aliyepita kwenye mji uliokuwa umekufa, akasema ni lini Mwenyezi Mungu ataufanya hai mji huu baada ya kufa kwake, basi Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia kisha akamfufua". (Qur'an, 2:259)
Au kama ile kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Je, huzingatii habari ya wale waliotoka majumbani mwao nao wakiwa maelfu wakiogopa mauti, Mwenyezi Mungu akawaambia kufeni kisha akawafufua" (Qur'an, 2:243) Na wako watu fulani miongoni mwa Wana wa Israel, Mwenye Mungu aliwafisha kisha akawapa uhai tena, amesema Mwenyezi Mungu:
"Na kumbukeni pale mliposema, Ewe Musa hatutakuamini mpaka tumuone Mwenyezi Mungu wazi wazi, yakakunyakueni mauti ya ghafla (ya moto wa radi) na hali mnaona, kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru" (Qur'an, 2:55-56) 'Na amesema Mwenyezi Mungu kuhusu As-Habul-Kahf ambao walikaa katika pango lao hali ya kuwa wamekufa kwa zaidi ya miaka mitatu:
"Kisha tukawafufua ili tujuwe ni lipi katika makundi mawili liwezalo kukadiria vyema muda waliokaa (humo pangoni)". (Qur'an, 18:12)
Basi hiki ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kunasimulia kwamba Raja'h ilikwisha tokea katika nyumati zilizotangulia hivyo siyo muhali kutokea katika umma wa Muhammad (s.a.w.) na hasa hasa jambo hilo litakapokuwa limesimuliwa na Maimamu wa Ahlul-Bait (a.s.) kwani wao ni wakweli na ni wajuzi. Ama kauli ya baadhi ya watu wenye mawazo ya kitoto kwamba Raja'h ni kauli ya "Tanasukh" (kuwa Roho huingia ndani ya kiwiliwili kingine) kauli ambayo inaaminiwa na baadhi ya makafiri, basi hiyo ni wazi kabisa kuwa ni ufisadi na ni batili, na lengo la kauli hiyo ni kuwakejeli na kuwatukana Mashia. Izingatiwe pia kuwa wanaoamini "Tanasukh" wao hawasemi kwamba mtu atarudi duniani akiwa na mwili wake na roho yake na sura yake kama jinsi alivyokuwa.
Bali wao wanasema kuwa roho huhama toka kwa mtu aliyekufa kwenda kwa mtu mwingine ambaye huzaliwa upya au hata kwenda kwa wanyama. Na kauli hii kama tunavyofahamu iko mbali mno na akida ya Waislamu wanaosema kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua waliomo makaburini kwa miili yao na roho zao. Hivyo basi "Raja'h" siyo miongoni mwa "Tanasukh" kwa namna yoyote ile, na hiyo Tanasukh ni miongoni mwa kauli za watu wajinga ambao hakuna wakijuacho au ni makundi ya watu wasio na utambuzi.
KUVUKA MIPAKA KATIKA KUWAPENDA MAIMAMU
Kuvuka mpaka kwa hapa hatukusudii kuwa ni kutoka katika haki na kufuata matamanio kiasi cha kuwa huyo mwenye kupendwa huwa ni Mungu mwenye kuabudiwa. Kwani kufanya hivyo ni kufru na ni shirki, hapana Muislamu yeyote anayeitakidi ujumbe wa Kiislamu na Unabii wa Muhammad (s.a.w.) anayesema hivyo. Na kwa hakika Mtume (s.a.w.) ameweka mipaka ya pendo hili pale aliposema kumwambia Imam Ali (a.s.). "Wameangamia kwa sababu yako wewe watu wawili, mwenye kukupenda kupita kiasi na mwenye kukuchukia." Na kauli yake tena Mtume (s.a.w.) "Ewe Ali bila shaka unao mfano wa Isa mwana wa Maryam, Mayahudi walimchukia mpaka wakamsingizia mama yake machafu na walimpenda Wakristo mpaka wakampa daraja ambayo haistahiki" Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 123, Tarikh Dimishq cha Ibn 'Asakir Juz. 2 uk. 234, Tarikhul-Kabir cha Bukhar Juz. 2 uk. 281, Tarikhul-Khulafai cha Suyuti uk. 173, Khasaisun-Nasai uk. 27, Dhakhairul-Uqba uk. 92, As-Sawaiqul-Muhriqah cha ibn Hajar uk. 74.
Na hiyo ndiyo maana ya kuvuka mpaka inayopingwa, na kuvuka mpaka katika kupenda mpaka huyo mwenye kupendwa afanywe Mungu na apewe daraja asiyokuwa nayo au kuvuka mpaka katika kumchukia kiasi ikafikia daraja ya kuzua uongo na tuhuma batili. Mashia katika kumpenda Ali na Maimamu miongoni mwa wanawe hawakuvuka mpaka, isipokuwa wamewaweka kwenye daraja inayokubalika kiakili. Daraja ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu amewatawalisha nayo ni kwamba wao ni mawasii wa Mtume na ni Makhalifa wake, na hapana yeyote aliyesema kwamba wao ni Manabii sembuse Uungu. Hebu zitupilie mbali kauli za wazushi ambao wanadai kwamba Mashia wamemfanya Ali kuwa ni Mungu, na kama itasihi habari hii kwamba (kuna wanaodai hivyo) basi hilo halikuwa kundi fulani wala Madhehebu wala Mashia wala Khawarij. Sasa basi,ni lipi kosa la Mashia ikiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Waambie sikutakeni malipo yoyote isipokuwa kuwapenda Qaraba zangu."
Ni jambo linalofahamika ya kwamba "Mawaddah" yana daraja ya juu kuliko kupenda. Na ikiwa Mtume (s.a.w.) amesema: "Hawezi kuwa Muumini mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake kile anachokipendelea nafsi yake." Kwani upendo (Mawaddah) unakulazimisha wewe kuinyima nafsi yako kitu fulani ili umpendelee kwacho mwenzako". Na liko wapi kosa la Mashia iwapo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: "Ewe Ali, wewe ni Bwana (Mtukufu) duniani na ni Bwana (Mtukufu) akhera, basi yeyote mwenye kukupenda, bila shaka amenipenda mimi, na yeyote mwenye kukuchukia bila shaka amenichukia mimi, na mpenzi wako ni mpenzi wa Mwenyezi Mungu, na mgomvi wako ni mgomvi wa Mwenyezi Mungu, na ole wake mwenye kukuchukia." Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 128, amesema hadithi hii ni sahihi kwa sharti zinazokubalika kwa Bukhar na Muslim, pia Taz: Nurul-Absar cha Ash-Shablanji uk. 73, Yanabiul-Mawaddah uk. 205, Ariyadhun-Nadhrah Juz. 2 uk. 165. Pia Mtume anasema:
"Kumpenda Ali ni imani na kumchukia ni unafiki."
Taz: Sahih Muslim Juz. 1 uk. 48, As-Sawaiqul-Muhriqah uk. 73, Kanzul-Ummal Juz. 15 uk. 105. Na anasema Mtume (s.a.w.): "Yeyote atakayekufa hali yakuwa anakipenda kizazi cha Muhammad, atakufa hali ya kuwa ni shahidi, .fahamuni yakuwa yeyote atakayekufa hali yakuwa anakipenda kizazi cha Muhammad atakufa hali ya kuwa amesamehewa, fahamuni kwamba, yeyote atakayekufa hali ya kuwa anakipenda kizazi cha Muhammad atakufa hali ya kuwa ametubia, fahamuni ya kwamba, yeyote atakayekufa hali ya kuwa anakipenda kizazi cha Muhammad atakufa hali yakuwa ni muumini mwenye imani iliyokamilika, fahamuni ya kuwa yeyote atakayekufa hali yakuwa anakipenda kizazi cha Muhammad, Malaika wa mauti atambashiria pepo..." Taz:
1) Tafsiri Atha'alabi iitwayo Al-Kabir katika Ayatul-Mawaddah.
2) Tafsiruz-Zamakhshari iitwayo Al-Kash-Shaf.
3) Tafsiru Fakhrir-Razi Juz. 7 uk. 405.
4) Ihqaqul-Haq cha At-Tustari Juz. 9 uk. 486.
Ni lipi kosa la Mashia ikiwa wao wanampenda mtu ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema kumuhusu mtu huyo kwamba: "Kesho nitampa bendera yangu mtu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Mwenyezi Mungu na Mtume wake (nao) wanampenda mtu huyo". Taz: Sahih Bukhar Juz. 4 uk. 20 na Juz. 5 uk. 76, Sahih Muslim Juz. 7 uk. 12. (Babu Fadhail All bin Abi Talib). Basi mpenzi wa Ali ni mpenzi wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na mtu huyo ni muumini, na mgomvi wa Ali ni mgomvi wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na mtu huyo ni mnafiki. Naye Imam Shafii amesema kuhusu kuwapenda kizazi cha Mtume: "Enyi watu wa nyumba ya Mtume, kukupendeni ninyi ni faradhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu ameteremsha ndani ya Qur'an." Yakutosheni kuwa na ubora mkubwa kwamba yeyote asiyekusalieni ninyi hana sala. Naye Far-Zadaq amesema kuhusu kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume: "Katika kuwapenda wao hiyo ndiyo dini na kuwachukia ni kufuru, kuwa karibu nao ni jambo linalookoa na kuhifadhi.
Wakihesabiwa wachamungu wao watakuwa ndio Maimamu au isemwe nani aliye mbora hapa ardhini jibu litakuwa, Ni wao!" Basi Mashia wamempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na pendo lao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndilo lililo faradhisha pendo la watu wa nyumba ya Mtume ambao ni Fatmah, Ali, Hasan na Husein. Hadithi zinazohusu maana hii ni nyingi hazina idadi, na wamezithibitisha wanachuoni wa Kisunni ndani ya vitabu vyao na baadhi yake tumevitaja kwa ajili ya kufanya mukhtasari. Hivyo basi ikiwa kumpenda Ali na Ahlul-Bayt kwa ujumla ni kumpenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) basi tunawajibika kufahamu ukomo wa pendo hili linalotakiwa kutoka kwa Waislamu ili tufahamu kama kuna kuvuka mpaka kama wanavyodai.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Hawezi kuwa muumini mmoja wenu mpaka mimi niwe mpendwa mno kwake kuliko mwanawe na mzazi wake na watu wote." Taz: Sahih Bukhar Juz. 1 uk. 9 (Babu Hubbir-Rasul Minal-iman), .Sahih Muslim Juz. 1 uk. 49, (mlango unaowajibisha kumpenda sana Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuliko jamaa, mtoto, mzazi na watu wote). Na kwa msingi huu basi Muislamu hanabudi kumpenda Ali na wanawe ambao ni Maimamu watakatifu (awapende) zaidi kuliko watu wote wakiwemo mke na watoto, na wala haitimii imani isipokuwa kwa kufanya hivyo, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema, "Hawi muumini mmoja wenu mpaka mimi niwe ni mpendwa mno kwake ..."
Hivyo basi Mashia hawavuki mpaka bali wanampa haki kila mwenye haki yake, na Mtume wa Mwenyezi Mungu amewaamuru wampe Ali daraja kama ile ya kichwa kwenye kiwiliwili, na daraja ya macho katika kichwa, basi je, kuna mtu anayepuuza macho yake au kichwa chake? Lakini kinyume chake ni kwamba kuna wanaovuka mpaka katika Masunni kwa kuwapenda Masahaba na kuwatakasa zaidi kuliko wanavyostahiki. Bali ukweli unaodhihiri ni kuwa tendo hilo' la Masunni kuvuka mpaka katika kuwapenda Masahaba ni kisasi dhidi ya Mashia ambao hawaitakidi juu ya uadilifu wa Masahaba wote, hali hii ni kwa kuwa Banu Umayyah walikuwa wanazipandisha daraja za Masahaba na kuporomosha heshima ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.), wakafikia kuwa kila wanapomsalia Muhammad na kizazi chake huwaongezea juu yao Masahaba wote, kwani ndani ya sala hiyo ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) kuna ubora ambao hakutangulia kuupata yeyote na hatoupata yeyote basi wakataka kuwanyanyua Masahaba wafikie daraja hiyo ya juu na wakasahau kwamba Mwenyezi Mungu amewaamuru Waislamu wakiwemo hao Masahaba wote wamsalie Muhammad, Ali, Fatmah, Hasan na Husein, na yeyote asiyewasalia sala yake haikubaliwi, Mwenyezi Mungu hataikubali ikiwa atamsalia Muhammad peke yake kama ilivyothibiti ndani ya Sahih Bukhar na Muslim.
Na tutaposema kwamba kufanya hivyo ni kuvuka mpaka, hiyo ni kwa sababu Masunni wanavuka mipaka ya kiakili pale wanaposema kwamba Masahaba wote ni waadilifu wakati Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameshuhudia kwamba miongoni mwao Masahaba wamo Mafasiqq na wenye kutoka katika dini na wengine wamepotoka na ni wanafiki. Kuvuka kwao mpaka (Masunni) kuko wazi wakati wanaposema kwamba, "Mtume wa Mwenyezi Mungu anakosea na kusahihishwa na Sahaba, au kwamba shetani anacheza na kurukaruka mbele ya Mtume, lakini shetani huyohuyo anamkimbia Umar. Pia wanavuka mpaka pale wanaposema kwamba, "Lau Mwenyezi Mungu angewashushia msiba Waislamu akiwemo Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, basi asingeokoka isipokuwa Ibn Al- Khatab." Na huko kuvuka mpaka kuko wazi mno kutokana na kupuuza kwao sunna ya Mtume (s.a.w.) na kufuata sunna ya Masahaba na hasa Khulafaur-Rashidina. Na bila shaka tumekubainishia baadhi ya hayo na kama utataka ziyada, basi huna budi kutafiti na kuzingatia ili ufahamu zaidi kuhusu mifarakano hii.
MAHDI ANAYENGOJEWA
Jambo hili pia ni miongoni mwa maudhui ambazo Masunni wanafanya kebehi dhidi ya Mashia. Wako baadhi ya Masunni ambao wamefikia mpaka kudharau na kukejeli, kwani wao wanapinga au unaweza kusema wanaitakidi kuwa haiwezekani mtu kubakia muda wa karne kumi na mbili akiwa hai amejificha haonekani machoni mwa watu. Imefikia hadi, baadhi ya waandishi wa zama hizi wakasema kwamba "Mashia wamezusha fikra ya Imam aliyeghaib (aliyejificha) ambaye atawaokoa, na hiyo ni kutokana na dhulma nyingi na ujeuri waliopambana nao toka kwa watawala kwa muda mrefu, basi wakajifariji nafsi zao kwa tarajio la kuja Imam Mahdi anayengojewa ambaye ataijaza ardhi uadilifu na usawa na kulipiza kisasi kwa maadui zao".
Katika miaka ya hivi karibuni na baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu Mahdi anayengojewa, Waislamu na hasa vijana wasomi kila mahali wamekuwa wakiulizana juu ya ukweli wa Mahdi, kuwa je, jambo hilo linao ukweli na linapatikana katika itikadiza Kiislamu au ni miongoni mwa uzushi wa Mashia? Pamoja na kuwepo yaliyoandikwa na wanachuoni wa Kishia wa hapo zamani na wa sasa hivi-Kama vile Shahid Muhmmad Baqir As-sadr ndani ya kitabu chake kiitwacho Bah-thun haulal-Mahdi-kuhusu suala la Mahdi, pia bila kujali mawasiliano (ya Masunni) na ndugu zao Mashia ambayo ni ya miaka mingi katika mikutano mingi na mazungumzo baina yao yanayohusu maudhui mbali mbali za kiitikadi, maudhui hii ya Mahdi wao hawajazowea kusikia riwaya kama hizi. Basi ukoje ukweli kuhusu Mahdi ndani ya itikadi za Kiislamu?
Utafiti juu ya maudhui hii unagawanyika sehemu mbili: Sehemu ya kwanza itahusika na utafiti kuhusu Mahdi ndani ya Qur'an na Sunna. Na sehemu ya pili, itahusu utafiti juu ya maisha yake na ghaiba yake kutoonekana na kudhihiri kwake. Ama katika utafiti wa mwanzo, Mashia na Masunni wameafikiana kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimbashiri Mahdi na akawajulisha Masahaba ya kwamba Mwenyezi Mungu atamdhihirisha katika zama za mwisho. Na hadithi zinazomuhusu Mahdi (a.s.) wote Mashia na Masunni wamezithibitisha ndani ya vitabu vyao na Musnad zao, nami kwa upande wangu kama ilivyo kawaida kwa namna nilivyo jilazimisha katika kila utafiti, sitoi dalili isipokuwa ile iliyothibiti na ni sahihi kwa Masunni.
Hivyo basi, imekuja ndani ya Sunan Abi Dawud: Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Lau kama haitabaki katika dunia isipokuwa siku moja Mwenyezi Mungu atairefusha siku hiyo mpaka amtoe mtu kutoka katika watu wa nyumba yangu jina lake linalingana na jina langu, na jina la baba yake ni jina la baba yangu, ataijaza ardhi usawa na uadilifu kama ilivyojazwa dhulma na ujeuri." Taz: Sunan Abi Dawud Juz. 2 uk. 422. Na imekuja ndani ya Sunan ibn Majah Juz. 2. hadithi na. 4082 na 4087, Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Sisi Ahlul-Bait Mwenyezi Mungu ametuchagulia akhera dhidi ya dunia, hapana shaka watu wa nyumba yangu baada yangu watakumbana na balaa kubwa na kufukuzwa mpaka waje watu fulani toka upande wa mashariki wakiwa na bendera nyeusi, wataomba amani hawatapewa, basi watapigana na watashinda, hivyo watapewa walichokiomba lakini hawatakikubali mpaka wakitoe kwa mtu miongoni mwa watu wa nyumba yangu, basi yeye atakijaza usawa kama kilivyojazwa ujeuri".
Na amesema ibn Ma'jah ndani ya Sunan yake: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Mahdi ni kutokana nasi Ahlul-Bait, Mahdi ni miongoni mwa watoto wa Fatmah" Na amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) "Katika Umma wangu atakuwepo Mahdi (atabaki) kama ni miaka midogo basi ni saba kama sivyo ni tisa Umma wangu utaneemeka humo neema ambayo haukupata kuneemeka mfano wake, utajiwa na chakula chake wala hawatokuwa wanahodhi kitu, mali zitakuwa tele siku hizo, mtu atamwambia Mahdi, Ewe Mahdi! nipe, atamwambia chukuwa."
Taz: Sunan ibn Majah Juz. 2 hadithi No. 4086. Na imekuja ndani ya Sahih Tirmidhi: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: "Atatawala mtu toka katika watu wa nyumba yangu, jina lake linalingana na jina langu, na lau haitabaki katika dunia isipokuwa siku moja, basi Mwenyezi Mungu atairefusha siku hiyo mpaka atawale". Taz: Al-Ja'mius-Sahih Juz. 9 uk. 74-75. Na amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): "Duniya haitaondoka mpaka awamiliki Waarabu mtu kutoka katika watu wa nyumba yangu, jina lake linalingana na jina langu". Taz: Sahih Bukhar Juz. 4 uk. 143, (Babu Nuzuli I'sa ibn Maryam).
Na ameandika Imam Bukhar ndani ya sahih yake amesema: "Ametusimulia bin Bakir, ametusimulia Al-Laith kutoka kwa Yunus naye toka kwa ibn Shihab naye kutoka kwa Nafii1 huru wa Abi Qatadah Al-Ansari ya kwamba, Abu Hurairah (r.a.) amesema, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema, mtakuwa na hali gani ninyi pindi mwana wa Maryam atakapokushukieni na Imamu wenu atatoka miongoni mwenu."? Na amesema mwenye Gha-yatul-Maa'mul: "Imekuwa (ni jambo) mashuhuri miongoni mwa wanachuoni wa hapo mwanzo na waliokuja baadaye kwamba hapo zama za mwisho ni lazima adhihiri mtu kutoka katika watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) aitwaye Mahdi."
Hadithi za Mahdi wamezisimulia jamaa miongoni mwa Masahaba wema na wakazithibitisha wanahadithi wakubwa kama vile Abu Dawud, Tirmidhi, ibn Majah, Tabrani, Abu Yaa'la, Imam Ahmad bin Hanbal na Al-Hakim, Mwenyezi Mungu awawiye radhi wote, na kwa hakika amekosea aliye zikosoa hadithi zote za Mahdi. Amesema Al-Hafidh ndani ya Fat-Hul-Bari: "Zimeenea kwa njia ya Mutawatir Khabari zisemazo kwamba Mahdi atatokana na umma huu, na kwamba I'sa mwana wa Maryam atashuka na ataswali nyuma yake." Taz: Fat-Hul-Bari Juz. 5 uk. 362. Na amesema ibn Hajar Al-Haithami ndani ya As-Sawa'iqul-Muhriqah: "Na hadithi ambazo zimekuja na ndani yake muna utajo wa kudhihiri Mahdi ni nyingi tena mutawatir."
Taz: As-Sawai'qul-Muhriqah ya ibn Hajar Juz. 2 uk. 211. Naye Shaukani ndani ya Risalatul-Musammat, akibainisha juu ya (hadithi) mutawatir zilizokuja kuhusu (Mahdi) anayengojewa na Dajjal na Masih na baada ya kuziorodhesha hadithi za Mahdi akasema: "Na hadithi zote tulizoleta zimefikia kiwango cha mutawatir kama isivyofichikana kwa mwenye ubora wa kuchunguza". Na amesema Sheikh Abdul-Haq ndani ya Lum-a'-t: "Kwa hakika hadithi ni nyingi mno zilizofikia kiwango cha mutawatir kuhusu Mahdi kwamba yeye ni kutoka katika watu wa nyumba ya Mtume miongoni mwa watoto wa Fatmah". Taz: Hashiyatu Sahih At-Tirmidhi, Juz. 2 uk. 42.
Naye As-Sabban amesema ndani ya kitabu chake kiitwacho Is-'afur-Raghibina: '"Kwa hakika khabari mutawatir (zimekuja) kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kuhusu kutokea kwake (Mahdi) na kwamba atatokana na watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) na kwamba ataijaza ardhi uadilifu". Taz: Is-A'fur-Raghibina Juz. 2 uk. 140. Na As-Suwaidi amesema ndani ya kitabu chake kiitwacho, Saba-Ikud-Dhahab uk. 78. "Kauli waliyoafikiana wanachuoni ni kwamba Mahdi ndiye atakayesimama zama za mwisho, na kwamba ataijaza ardhi uadilifu, na hadithi zinazohusu kudhihiri kwake ni nyingi". Naye ibn Khaldun ndani ya Muqaddimah yake amesema: "Fahamu ya kwamba (kauli) iliyo mashuhuri baina ya Waislamu kwa zama zote ni kuwa katika zama za mwisho, hapana budi adhihiri mtu kutoka katika watu wa nyumba ya Mtume atakayeitia nguvu dini na atadhihirisha uadilifu na anaitwa Mahdi". Taz: Muqaddimatu Ibn Khaldun uk. 367.
Kama ambavyo amezithibitisha hadithi za Mahdi mwanachuoni wa zama hizi mufti wa Ikhwanul-Muslimina Sayyid Sa-biq ndani ya kitabu chake kiitwacho, "Al-A 'qaaidul-Islamiyyah " na amesisitiza kwamba fikra ya Mahdi ni miongoni mwa itikadi za Kiislamu ambazo ni wajibu kuziamini. Na vitabu vya Kishia pia vimethibitisha hadithi zinazomuhusu Mahdi kwa wingi mpaka ikasemwa kwamba, hapakupokelewa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu hadithi nyingi kuliko zilizopokelewa toka kwake kuhusu Mahdi. Na ametoa mtafiti aitwaye Lutfullahis-Safi ndani ya Mausuat yake iitwayo, "Muntakhabul-Athar" rejea zaidi ya sitini toka vitabu vya Kisunni hadithi zinazomuhusu Mahdi (a.s.) ndani yake zimo sihah sita, na zaidi ya rejea tisini toka vitabu vya Kishia ndani yake vimo vitabu vinne.
Ama kuhusu utafiti wa sehemu ya pili ambao unahusu kuzaliwa kwa Mahdi, maisha yake, ghaibah yake na kwamba hajafa, sehemu hii pia baadhi ya wanachuoni wa Kisunni wanaoheshimika hawakuipinga, na ndiyo ambao wanaitakidi kwamba Mahdi ni Muhammad bin Al-Hasan Al-A'skari, ambaye ni Imamu wa kumi na mbili miongoni mwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) amekwisha zaliwa na yungali hai na atadhihiri zama za mwisho na kuujaza ulimwengu uadilifu na usawa na Mwenyezi Mungu atainusuru dini yake kupitia kwake (Mahdi), hivyo basi wanachuoni hao wa Kisunni wanaafikiana na kauli za Mashia Imamiyyah.
Miongoni mwa wanachuoni hao ni hawa wafuatao: 1. Muhyid-din bin Al-Arabi-ndani ya Futuha'til-Makiyyah.
2. Sib-ti bin Al-Jauzi ndani ya kitabu chake kiitwacho,
3. Tadh-Kiratul-Khaw-was.
3. A'bdul-Wahab Ash-Shaa'rani ndani ya kitabu chake kiitwacho Aqaidul-Akabir.
4. Ibnul-Khash-Shab ndani ya kitabu chake kiitwacho,"Tawarikh Mawalid Al-Aimmah Wawafiyya-tihim."
5. Muhammad Al-Bukhari Al-Hanafi ndani ya Kitabu chake Faslul-Khitab.
6. Ahmad bin Ibrahim Al-bala-dhuri, ndani ya kitabu chake kiitwacho, Al-Hadithul-Mutasal-sal
1. Ibnus-Sabbagh al-Maliki, ndani ya kitabu chake kiitwacho, Al-Fusulul-Muhimmah.
8. Al-A'rif A'bdur-Rahman ndani ya kitabu chake Mir- atul-as-rar.
9. Kama-lud-din bin Tal-hah ndani ya kitabu chake kiitwacho Matalibus-suul Fi Manaqib Alir-Rasul. l0. Al-Qanduzi Al-Hanafi ndani ya kitabu chake kiitwacho, Yanabiu'l-Mawaddah.
Na lau mwenye kutafiti atafuatilia atawakuta wanachuoni wa Kisunni zaidi ya hawa tuliowataja ambao wanazungumzia kuzaliwa kwa Mahdi na kubakia kwake hai mpaka Mwenyezi Mungu amdhihirishe. Na baada ya haya hakuna wanaobakia miongoni mwa Masunni isipokuwa wale wanaopinga kuzaliwa na kubakia kwake hai baada ya kukiri kwao kusihi kwa hadithi, na hawa siyo hoja dhidi ya wengine wanaokubaliana na suala hili. Nayo Qur'an Tukufu haikanushi wazo hili, na ni mara nyingi Mwenyezi Mungu ametoa mifano juu ya jambo hilo kwa watu wenye akili ngumu ili wajikwamue na kuzipa uhuru fikra zao na akili zao ili ziyakinishe na kukubali kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muweza juu ya kila kitu.
Kwa hiyo basi Muislamu ambaye moyo wake umejaa imani haoni ajabu kuwa Mwenyezi Mungu kumfisha Uzair kwa muda wa miaka mia moja kisha akamfufua ili akiangalie chakula chake na kinywaji chake ambavyo havijaharibika, na punda wake namna gani Mwenyezi Mungu anavyoinyanyua mifupa yake na kuivisha nyama na kuirudisha kama ilivyokuwa baada ya kuwa mifupa yake hiyo imechakaa, basi pindi ilipombainikia akasema: "Nimefahamu kwamba Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu". Sub-hanallah!! alibadilika kwa haraka mtu huyu, wakati hapo kabla ya tukio hili alipopita kwenye kijiji kilichokufa alishangaa na kupinga akasema: "Ni vipi Mwenyezi Mungu atakifufua kijiji hiki baada ya kufa kwake"?
Na Muislamu anayeisadiki Qur'an Tukufu hashangai kuwa Bwana wetu Ibrahim kumkatakata ndege na kuvitawanya viungo vyake na manyoya yao juu ya jiwe kisha akaviita vikamjia mara moja. Pia Muislamu hashangai moto kupoa usimuunguze wala kumuudhi Bwana wetu Ibrahim wakati alipotupwa ndani ya moto huo na Mwenyezi Mungu akauambia, "Ewe moto kuwa baridi na salama ". Si hivyo tu Muslamu hashangai kwamba Bwana wetu I'sa amezaliwa bila mbegu ya kiume yaani bila baba na kwamba yu hai hakufa na atarudi ulimwenguni. Kadhalika Muislamu hashangai ya kwamba Bwana wetu I'sa alikuwa akiwafufua watu na kuwaponya vipofu na wenye mbaranga, na pia Muislamu hashangai juu ya kufunguka bahari kwa ajili ya Bwana wetu Musa na wana wa Israeli wakapita bila kulowana na fimbo ya Musa kugeuka nyoka na maji ya mto Nile kugeuka na kuwa damu.
Vile vile Muislamu hatoshangaa ya kwamba Bwana wetu Sulaiman alikuwa akizungumza na ndege na majini na kuchukuliwa kiti chake kubebwa kwenye busati la upepo, na kukisimamisha (mbele yake) kiti cha Bal-Qis kwa muda mfupi. Wala Muislamu hashangazwi juu ya Mwenyezi Mungu kwamba aliwafisha As-Habul-Kahfi kwa karne tatu na wakazidisha tisa kisha akawafufua basi kipindi hicho mjukuu wa mjukuu alikuwa ni mkubwa kwa umri kuliko Babu wa Babu. Wala hatoshangaa Muislamu ya kwamba Sayydina Al-Khidhr (a.s.) yu hai hakufa na alikutana na Bwana wetu Musa (a.s.). Na pia Muislamu hatoshangaa ya kwamba Ibilisi aliyelaaniwa na Mwenyezi Mungu yu hai hajafa naye ni kiumbe aliyeumbwa kabla ya Adam (a.s.) mpaka sasa angali anafuatilia nyendo za mtu tangu mwanzo wa kuumbwa kwake mpaka kufa kwake. Pamoja na hayo Ibilisi amejificha licha ya matendo yake machafu na kazi zake mbaya, na yeye anawaona watu wote. Kwa hakika Muislamu anaamini yote haya wala hashangai kutokea kwake. Basi je, hivi Muislamu atashangazwa na kuwepo kwa Mahdi ambaye amefichikana kwa kipindi fulani kutokana na hekima aitakayo Mwenyezi MunguMtukufu?
Basi yote yaliyotajwa na Qur'an ambayo ni mengi mno kuliko tuliyoyataja sisi katika ufupisho huu ni miongoni mwa mambo yaliyo nje ya mazowea yanayofahamika, wala si katika mambo waliyoyazowea watu, wala hawawezi kuyafanya hata kama watashirikiana. Bali ni miongoni mwa uumbaji wa Mwenyezi Mungu ambaye hapana kinachomshinda duniani wala mbinguni, na Waislamu wanaamini hilo kwani wao wameamini yote yaliyokuja ndani ya Qur'an tukufu bila kuchagua wala kupinga. Na kwa kuwa Mashia wao ndiyo wanayafahamu zaidi mambo ya Mahdi (a.s.) kwa kuwa ni Imam wao na wameishi naye yeye na wazazi wake. (Kuna mithali husemwa): "Watu wa Makkah ndiyo wanaovifahamu mno vichochoro vyake". Mashia wanawaheshimu Maimamu wao na kuwatukuza na wameyatengeneza na kuyajengea makaburi ya Maimamu wa nyumba ya Mtume na wamejilazimisha kuyatembelea (kuyazuru) na kutabaruku kwayo. Basi lau Imam wa kumi na mbili ambaye ni Mahdi (a.s.) angekuwa amekufa basi kaburi lake lingekuwa linatambulikana, na wangeweza kusema kuwa inajuzu kufufuka baada ya kufa maadamu jambo hili linawezekana, kama ilivyoeleza Qur'an na hasa kwa kuwa wanaitakidi Raja'h. Lakini utawaona Mashia wanakazia kusema kwamba Mahdi (a.s.) yu hai na anaruzukiwa na amejificha kwa hekima aliyotaka Mwenyezi Mungu Mtukufu hekima ambayo wanaweza wakaifahamu wale waliobobea katika elimu na Mawalii wake.
Kadhalika Mashia huomba ndani ya Sala zao Mwenyezi Mungu aiharakishe Faraja yake tukufu kwani katika kudhihiri kwake ni heshima kwa waislamu na ni mafanikio yao na ushindi wao na kwa kupitia kwake Mwenyezi Mungu ataitimiza nuru yake japokuwa makafiri watachukia. Kwa hiyo tofauti iliyopo baina ya Sunni na Shia' juu ya suala la Mahdi (a.s.) siyo tofauti ya msingi maadam wote wanaitakidi juu ya kudhihiri kwake hapo zama za mwisho na kwamba I'sa (a.s.) ataswali nyuma yake. Pia Mahdi ataijaza dunia usawa na uadilifu kama ilivyojazwa dhulma na ujeuri, na Waislamu wataimiliki dunia yote katika zama zake na neema zitaenea asibakie hata masikini mmoja.
Tofauti pekee inayobakia ni kuhusu kauli ya Mashia juu ya kuzaliwa kwake na kauli ya Masunni kwamba atazaliwa hapo baadaye na kauli za makundi haya zinakutana kwenye kudhihiri kwake katika zama za mwisho. Hivyo basi Waislamu na washikamane kwenye neno la kweli na kuimarisha umoja wa umma ambao umesambaratika na wote wamuombe Mwenyezi Mungu kwa ukweli kabisa katika maombi yao na katika kila sala zao ili Mwenyezi Mungu amdhihirishe kwa haraka, kwani kudhihiri kwake ni faraja na ni ushindi kwa umma wa Mtume Muhammad (s.a.w.). Na maombi yetu ya mwisho ni kumshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu, na sala na salamu zimshukie Mtukufu wa Mitume na Manabii Bwana wetu na msimamizi wetu Muhammad na pia kizazi chake (watu) walio wema tena watakatifu. Muhammad Tijani As-Samawi