7
ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI
HUZUNI NA MAJUTO
Kwa nini nisijute; bali ni kwa nini kila Muislamu asijute wakati asomapo ukweli huu unaohusu hasara waliyoipata Waislamu kutokana na kutengwa kwa Imam Ali kwenye Ukhalifa ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu alimtawalisha, na hivyo kuunyima umma (wa Kiislamu) uongozi wake na hekima, na elimu yake nyingi. Na pindi Muislamu atakapochunguza bila ya chuki wala upendeleo, atamkuta Imam Ali ndiyo mjuzi mno kuliko watu wote baada ya Mtume, kwani historia inashuhudia kwamba wanachuoni wa Kisahaba walikuwa wakimuuliza Ali kwa kila lililowatatiza, na kauli ya Umar bin Al-Khatab aliyoisema zaidi ya mara sabini ya kwamba "Lau kama si Ali basi Umar angeliangamia' wakati ambapo Imam Ali (a.s.) hakupata kamwe kumuuliza Sahaba yeyote miongoni mwao.
Taz: Manaqibul-Khawar Zami uk. 48, Al-Istiabu Juz.3 uk. 39. Tadhkiratus-Sibt uk. 87, Matalibus-Suuli uk. 13, Tafsir Nishapur katika Surat Ahqaf, Faidhul-QadirJuz.4uk.357. Kama ambavyo historia inakiri kuwa Ali bin Abi Talib ni shujaa mno na mwenye nguvu kuliko Masahaba wote, na kuna mashujaa wengi miongoni mwa Masahaba walipata kukimbia vita katika sehemu nyingi tu, wakati ambapo Ali (a.s.) alisimama imara mahala pote palipopiganwa vita, na inatosha kuwa ni dalili ile nishani aliyopewa na Mwenyezi Mungu pale Mtume (s.a.w.) aliposema: "Kesho nitampa bendera yangu mtu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, mkali katika mapambano si mwenye kukimbia, Mwenyezi Mungu amekwisha utahini moyo wake kwa imani". Masahaba wakaitamania (kuipata) bendera hiyo, Mtume akampa Ali bin Abi Talib.
Kwa kifupi, bila ya shaka maudhui ya elimu , nguvu na ushujaa, mambo ambayo Imam Ali amepwekeka kwayo, ni maudhui inayofahamika kwa wote (Sunni na Shia) na ukiachilia mbali maandiko yanayojulisha kwa uwazi wa kuashiria juu ya Uimamu wa Ali, hapana shaka kwamba Qur'an haikubali uongozi na Uimamu isipokuwa kwa mtu mwenye elimu, shujaa tena mwenye nguvu. Mwenyezi Mungu anasema kuhusu wajibu wa kuwafuata wanachuoni (wenye elimu): "Basi aongozaye katika haki ndiye anayestahiki zaidi kufuatwa au (anastahiki) yule asiyeongoka isipokuwa aongozwe, basi mna nini, ni vipi mnahukumu?" (Qur'an, 10:35)
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu wajibu wa kumfuata mwenye elimu, shujaa tena mwenye nguvu: "Wakasema, ni vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema, Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na kiwiliwili na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye, naye Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mwenye kujua". (Qur'an, 2:247) Hapana shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu amemzidishia Imam Ali wasaa wa elimu kuliko Masahaba wote, akastahiki kuwa ni "Mlango wa elimu," akawa ndiye rejea pekee kwa Masahaba baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) nao Masahaba walikuwa kila wanaposhindwa kutatua mambo husema "Mas-ala haya magumu hakuna ayawezaye isipokuwa Abul-Hasan." Taz: Manaqibul-Khawar-Zami uk. 58, Tadhkiratus-Sibt uk. 87 Ibnul-Maghazili Tarjumah ya Ali uk. 79.
Na alimzidishia wasaa wa kiwiliwili, kwa kweli alistahiki kuwa simba wa Mwenyezi Mungu aliye mshindi, na nguvu zake na ushujaa wake ni wenye kupigiwa mfano katika kila zama kiasi kwamba wanahistoria wamesimulia visa vingi kuhusu ushujaa na nguvu zake visa ambavyo vinakurubia kuwa ni miujiza, kama vile kuung'oa mlango wa Khaybar, wakati ambapo Masahaba ishirini walishindwa hata kuutikisa[73] Na pia kuling'oa Sanamu kubwa la Hubal[74] kutoka juu ya paa la Al-Kaabah na kulisogeza jiwe kubwa ambalo jeshi lote lilishindwa hata kulitikisa[75] na mengineyo miongoni mwa riwaya mashuhuri. Na Mtume (s.a.w.) alimsifu na kumtaja kwa ubora mwana wa ammi yake Ali, na akazibainisha fadhila zake mahala mbali mbali na aliyatambulisha mambo yake maalum yanayomuhusu na daraja yake.
Kuna wakati Mtume akisema:
"Hakika huyu ni ndugu yangu na ni wasii wangu na ni Khalifa wangu baada yangu, basi msikilizeni na mumtii" Taz: 1) Tarikhut-Tabari Juz. 2 uk. 319. 2) Tarikhu ibn Athir Juz. 2 uk. 62. Na kuna wakati Mtume humwambia Ali (a.s.): "Wewe kwangu mimi unayo daraja ya Harun kwa Musa isipokuwa hapana Nabii baada yangu". Taz: 1) Sahih Muslim Juz. 7 uk. 120. 2) Sahih Bukhar katika Fadhail za Ali Na kuna wakati mwingine Mtume akisema:
"Yeyote mwenye kutaka kuishi nilivyoishi mimi na kufa mauti (kama) yangu na akae katika bustani ya milele aliyoniahidi Mola wangu, basi na amtawalishe Ali bin Abi Talib, kwani yeye hatakutoeni kwenye uongofu na kamwe hatakuingizeni katika upotofu". Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk.' 128 na At-Tabrani ndani ya Al-Kabir.
Na yeyote atakayefuatilia sera ya Mtume Mtukufu (s.a.w.) atamkuta Mtume hakutosheka kwa kusema maneno tu na hadithi zinazomuhusu Ali, bali maneno yake yakionekana kwa matendo yake, kwani katika uhai wake Mtume katika uhai wake hakupata kumuwekea Ali amiri yeyote juu yake miongoni mwa Masahaba pamoja na kwamba alikuwa akiwawekea maamiri Masahaba wengine wao kwa wao. Hapana shaka kwamba Mtume aliwawekea Abubakar na Umar amiri (wa kuwaongoza) katika vita ya "Dhatus-Salasil" amiri huyo alikuwa Amr bin Al-As.
Taz: Siratul-Halabiyah, Ghaz-Watu Dhatis-Salasil, na Tabaqat ya ibn Saad. Kama ambavyo Mtume (s.a.w.) aliwawekea Masahaba amiri ambaye alikuwa kijana mdogo Usamah bin Zaid na hilo alilifanya katika jeshi la Usamah kabla ya kufariki kwake yeye Mtume (s.w.a.). Amma Ali bin Abi Talib hakuwa katika ujumbe wowote ila yeye ndiye amiri, hata kuna wakati fulani Mtume (s.a.w.) alituma ujumbe wa namna mbili, akampa uamiri Ali kwenye moja ya ujumbe huo na Khalid bin Walid akampa uamiri kwenye ule wa pili kisha akawaambia:
"Mutakapoachana kila mmoja awe amiri wa jeshi lake na mkikutana basi Ali ndiye amiri wa jeshi lote. Kutokana na maelezo yote yaliyotangulia tunakuta kwamba Ali ndiye mtawalia mambo ya waumini baada ya Mtume (s.a.w.) na haifai kwa yeyote yule kumtangulia.
Lakini kwa masikitiko makubwa, Waislamu wamepata hasara kubwa, na ndiyo maana wanapata taabu hadi leo na wanachuma matunda ya kile walichokipanda, na bila shaka waliokuja baadaye wamekwisha yatambua yale yaliyoasisiwa na hao waliotangulia. Hivi kweli inawezekana kwa mtu yeyote kufikiria kuna Ukhalifa ulioongoka zaidi ya ule Ukhalifa wa Ali bin Abi Talib? Lau umma huu ungelifuata kile alichokichagua Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa kuwa Ali alikuwa ndiye mwenye uwezo wa kuuongoza umma (huu) kwa muda wote wa miaka thelathini juu ya mfumo mmoja kama vile alivyouongoza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) bila ya mabadiliko yoyote. Tunasema hayo kwa kuwa Abu Bakar na Umar walibadilisha na wakafanya ijtihadi zao dhidi ya maagizo na matendo yao yakawa ndiyo sunna inayofuatwa. Uthman naye alipokuja kwenye Ukhalifa akabadilisha mengi mno mpaka ikasemwa kuwa alikikhalifu kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake pia Sunna ya Abubakar na Umar, hapo ndipo Masahaba walipompinga na yakafanyika dhidi yake mapinduzi makubwa yaliyoangamiza Maisha yake na kusababisha fitna kubwa katika umma (fitna ambayo) jeraha lake halijapona hadi leo.
Amma Ali bin Abi Talib, yeye alikuwa akifungamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, hakwenda kinyume japo kwa nchi moja, na ushahidi mkubwa wa hilo ni kwamba yeye Imam Ali alikataa kuchukua Ukhalifa pale walipomuwekea sharti ya kuhukumu kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake na sunna ya Makhalifa wawili waliomtangulia.
Huenda akauliza muulizaji: Basi ni kwa nini Ali anashikamana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake wakati ambapo Abubakar na Umar na Uthman walilazimika kufanya ijtihadi na mabadiliko?
Jawabu ni kuwa, yeye Ali anayo elimu ambayo wao hao hawakuwa nayo, isitoshe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alimuhusisha kwa milango elfu moja ya elimu na katika kila mlango anaweza kufungua milango elfu moja. Taz: Kanzul-ummal Juz. 6 uk.392 hadithi Na.6009 Yanabiul-Mawaddah uk. 73,77 Tarekh Dimishq Juz. 2 uk. 483.
Pia alimwambia: "Wewe Ewe Ali utaubainishia umma wangu yale watakayotofautiana ndani yake baada yangu." Taz: Mustadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 122, Tarekh Dimishq Juz. 2 uk. 488.
Amma hao Makhalifa walikuwa hawajuwi mambo mengi katika hukmu za Qur'an za dhahiri licha ya taawili ya Qur'an, hali hii wamethibitisha Bukhar na Muslim ndani ya sahih zao katika mlango wa kutayamamu ya kwamba, kuna mtu fulani alimuuliza Ummar bin Al-Khatab katika zama za Ukhalifa wake akasema yule mtu: "Ewe Amirul-Muuminina hakika mimi nimepatwa na janaba na sikupata maji, basi nifanyeje"? Umar akasema: "Usiswali"!! Kadhalika Umar hakuifahamu hukmu ya watoto wa ndugu wa kiume wa baba (ibnu Ammi) mpaka amekufa na hali ya kuwa anasema, "Natamani lau ningemuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu juu ya watoto wa Ammi".Wakati ambapo hukmu yake imetajwa ndani ya Qur'ani Tukufu, kwa hiyo Umar ambaye Masunni wanasema kuwa alikuwa miongoni mwa wenye kupewa Il-hamu (na Mwenyezi Mungu) hali ya elimu yake ilikuwa katika kiwango hiki, (basi kama Umar ni hivi) hao wengine wala usijisumbue kuuliza, hao ndiyo ambao waliingiza Bid'a (uzushi) ndani ya dini ya Mwenyezi Mungu bila ya kuwa na elimu wala uongofu wala kitabu cha kuwaongoza isipokuwa jitihada zao binafsi.
Na huenda msemaji akasema: "Ikiwa mambo ndiyo yako namna hii, basi ni kwa nini Imam Ali (a.s.) hakuubainishia umma yale ambayo walitofautiana ndani yake baada ya Mtume (s.a.w.)" Jawabu ni kuwa: Imam Ali (a.s.) hakuacha kufanya juhudi katika kubainisha yale yaliyoutatiza umma, na yeye alikuwa ndiye marejeo ya Masahaba kwa kila lililowatatiza alikuwa akija na kufafanua na kutoa nasaha. Hivyo basi walikuwa wakiyachukua yale wayapendayo na yasiyopingana na siasa zao na kuyaacha yasiyokuwa hayo, na historia ndiye shahidi mkubwa kwa haya tuyasemayo.
Kwa kweli lau siyo Ali bin Abi Talib na Maimamu miongoni mwa wanawe, basi watu wasingeyafahamu mafunzo ya dini yao, lakini watu (walivyo) ni kama ilivyotufunza Qur'an yakuwa hawaipendi haki, basi walifuata matamanio yao na kuzusha madhehebu dhidi ya Maimamu wa nyumba ya Mtume ambao serikali zilizokuwa katika wakati wao zilikuwa zikifuatilia kila wasemalo, wala hazikuwapa uhuru wa kushughulika na kufanya mahusiano ya moja kwa moja na watu. Basi Imam Ali (a.s.) alikuwa akipanda juu ya mimbari na kuwaambia watu, "Niulizeni kabla hamjanikosa" Na yatosha kuwa Imam Ali ameacha Nahjul-Balagha, nao Maimam kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) wameacha elimu ambayo imeenea ulimwenguni na hilo wamelishuhudia viongozi wa Kiislamu Masunni na Mashia.
Ninarejea kwenye maudhui na ninasema: "Kwa msingi huu, lau Ali angewezeshwa kuuongoza umma kwa miaka thelathini kwa mujibu wa sera ya Mtume (s.a.w.) basi Uislamu ungeenea na kuimarisha itikadi katika nyoyo za watu zaidi na kwa undani wala pasingekuwa na fitna ndogo au kubwa wala (mauaji ya) Karbala yasingekuwepo wala msiba wa Ashuraa. Lau tutaukadiria uongozi wa Maimamu kumi na moja baada ya Ali, Maimamu ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwataja, na uhai wao uliendelea kwa kipindi cha karne tatu, basi pasingebaki hapa duniani miji isiyokuwa ya Kiislamu, na ulimwengu usingekuwa katika hali tunayoishuhudia leo hii na maisha yetu yangekuwa ya kibinaadamu kwa maana yake ya hakika lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Alif Lam Mim, Je, watu wanadhani kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: "Tumeamini" wasijaribiwe (wakapata Mitihani)? (Qur'an, 29:2) Umma wa Kiislamu umefeli katika mtihani huu kama vile zilivyofeli umma zilizotangulia, kama ambavyo Mtume wa Mwenyezi Mungu[76] alivyotamka katika minasaba mbali mbali na kama ambavyo Qur'an ilivyosisitiza mara nyingi ndani ya aya nyingi.[77]
USHAHIDI MWINGINE KUHUSU UONGOZI WA ALI (A.S.)
Kama kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka Wilayah ya Ali iwe ni mtihani kwa Waislamu, basi kila ikhtilafu iliyotokea imekuwa ni kwa sababu ya Wilayah hiyo, naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mpole kwa waja wake, hawezi kuwaadhibu waliokuja baadaye kwa makosa yaliyofanywa na wale wa mwanzo. Kwa ajili hiyo imetukuka hekima yake, tukio hili la ukhalifa likazungukwa na mfululizo wa matukio mengine makubwa yafananayo na miujiza, ili iwe ni kichocheo kwa umma. Waliinakili hali hii waliokuwepo ili wapate mazingatio wajao baadaye huenda wakaongoka na kuelekea kwenye haki kwa njia ya kufanya utafiti.
Ushuhuda wa Kwanza: Unafungamana na adhabu kwa wale waliokadhibisha Wilayah ya Ali, hilo lilitokea baada ya kuenea kwa habari za Ghadir Khum na kusimikwa kwa Imam Ali kuwa ni Khalifa wa Waislamu kutokana na kauli ya Mtume alipowaambia "Aliyeshuhudia tukio hilo amfikishie habari asiyehudhuria ".
Habari hizo za tukio la Ghadir zilimfikia Harith bin Nuuman Al-Fihri na hakufurahishwa na habari hizo- Hapa kuna dalili kwamba walikuwepo Mabedui waliokuwa wakiishi nje ya Madina ambao walikuwa wakimchukia Ali na pia Mtume (s.a.w.). Basi huyu bwana alimsimamisha mnyama wake mbele ya mlango wa msikiti akaingia kwa Mtume (s.a.w.) akasema: "Ewe Muhammad bila shaka wewe umetuamuru tushuhudie kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, tumekukubalia hilo, na umetuamuru tusali mara tano kwa siku, tufunge Ramadhan, Tuhiji na tutoe zaka mali zetu tukakukubalia, kisha hukuridhika kwa haya mpaka umeinyanyua mikono ya mwana wa ammi yako na umemboresha juu ya watu ukasema: "Yeyote ambaye mimi ni mtawalia mambo yake basi Ali ni mtawalia mambo yake". Jambo hili latoka kwako au latoka kwa Mwenyezi Mungu"?
Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema hali ya kuwa macho yake yamekuwa mekundu: "Namuapa Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola isipokuwa yeye, jambo hilo latoka kwa Mwenyezi Mungu na halitoki kwangu" Akasema maneno hayo mara tatu.!! Harith alisimama huku akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu ikiwa ayasemayo Muhammad ni ya kweli, basi tuletee mawe toka mbinguni au utuletee adhabu kali". Msimulizi wa kisa hiki anasema: "Wallahi hakumfikia ngamia wake bali Mwenyezi Mungu alimpiga kwa jiwe toka mbinguni likaangukia kichwani na kutokea kwenye makalio akafa. Pale pale Mwenyezi Mungu akateremsha aya isemayo: "Muombaji aliomba adhabu itakayotokea (adhabu ambayo) haina wa kuizuia kwa makafiri." (Qur'an 70:1-2) Tukio hili wameliandika wanachuoni wengi wa Kisunni[78] wasiokuwa wale tuliokwisha kuwataja, basi mwenye kutaka ziyada kutoka katika rejea ni juu yake kutazama kitabu kiitwacho Al-Ghadir cha Al-Allamah Al-Amin.
Ushahidi wa Pili: Unahusu adhabu ya yule aliyeficha ushahidi wa tukio la Ghadir na dua ya Imam Ali ikampata. Hilo lilitokea wakati Imam Ali aliposimama katika zama za Ukhalifa wake kwenye siku iliyoshuhudiwa pindi Imam Ali alipowakusanya watu katika msikiti wa Kufah akatangaza akiwa juu ya mimbar akasema: "Namsihi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Muislamu ambaye alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema siku ya Ghadir Khum kwamba, yeyote ambaye mimi ni mtawalia mambo yake basi Ali ni mtawalia mambo yake namnasihi asimame na kushuhudia aliyoyasikia, na asisimame isipokuwa yule aliyemuona kwa macho yake nakumsikia kwa masikio yake." Walisimama Masahaba thelathini, kumi na sita miongoni mwao ni mashujaa wa Badri, wakashuhudia kwamba Mtume (s.a.w.) aliushika mkono wake (Ali) na akawaambia watu kuwa: "Je, mnafahamu kuwa mimi ni bora mbele ya waumini kuliko nafsi zao? Wakasema ndiyo, Mtume (s.a.w.) akasema, Yeyote ambaye mimi namtawalia mambo yake basi huyu hapa Ali ni mtawalia mambo yake, ewe Mwenyezi Mungu mtawalishe atakayemtawalisha na umpinge anayempinga
Lakini baadhi ya Masahaba waliohudhuria tukio la Ghadir, chuki na husuda dhidi ya Imam Ali ziliwakalisha chini hawakusimama kushuhudia, na miongoni mwa hawa ni Anas bin Malik. Imam Ali aliposhuka kutoka kwenye Mimbar alimwambia "Ewe Anas una nini mbona hukusimama pamoja na Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ili ushuhudie yale uliyoyasikia toka kwake siku hizo kama walivyoshuhudia wengine?" Anas akasema, "Ewe Amirul-Muumina umri wangu umekuwa mkubwa (nimekuwa mzee) na nimesahau". Imam Ali (a.s.) akasema: "Ikiwa wewe ni muongo, basi Mwenyezi Mungu akubabue kwa weupe ambao kilemba chako hakitaufunika." Anas hakusimama isipokuwa uso wake ulikwisha kuwa mweupe kwa mbaranga, na baada ya hapo akawa hulia na kusema, "Imenipata dua ya mja mwema kwa sababu nilificha ushahidi wake". Kisa hiki ni mashuhuri, Ibnu Qutaibah amekitaja ndani ya kitabu kiitwacho Al-Maarif uk. 251, pale alipomuweka Anas miongoni mwa waliodhurika (kutokana na dua ya Imam Ali) katika mlango unaozungumzia mbaranga, pia Imam Ahmad bin Hambal ndani ya Musnad yake Juz. 1 uk.119 (amekitaja kisa hiki) aliposema: "Wakasimama isipokuwa watu watatu hawakusimama basi iliwapata dua yake."
Na hapa inafaa tuashirie kwa kuwataja watu hawa watatu ambao Imam Ahmad amewataja kwa riwaya ya Al-Balaadhuri[79] amesema baada ya kuleta nasaha ya Imam Ali kuhusu ushahidi, na chini ya mimbar alikuweko Anas Bin Malik, Al-Bar-raa bin Azib na Jarir bin Abdallah Al-Balli, Imam Ali alirudia nasaha ile lakini hakuna yeyote aliyemjibu miongoni mwao, basi Ali akasema, "Ewe Mwenyezi Mungu, yeyote mwenye kuficha ushahidi huu na hali ya kuwa anaufahamu basi usimtoe katika dunia hii mpaka umuwekee alama atakayotambulika kwayo." Amesema msimuliaji, "Anas bin Malik akapatwa na mbaranga, Al-barraa bin Azib akawa kipofu na Jarir akarudi kuwa bedui baada ya Hijra yake na akaenda Sharaat akafia ndani ya nyumba ya mama yake".[80] Kisa hiki ni mashuhuri wamekinakili wanahistoria wengi. Basi zingatieni enyi wenye akili:
Yeyote mwenye kufuatilia atafahamu kwa kupitia tukio hili[81] pale alipowanasihi Masahaba washuhudie hadithi ya Ghadir, tukio ambalo Imam Ali alilihuisha baada ya kupita na robo karne, na karibu lilikuwa lisahauliwe. Hivyo basi atakayefuatilia atafahamu ni ipi daraja ya Imam Ali na utukufu wake pia kiwango cha azma yake na usafi wa nafsi yake, wakati ambapo subira aliipa nafasi zaidi kuliko haki yake, na aliwapa nasaha kina Abubakr na Umar na Uthman kitu ambacho alifahamu kuwa katika kuwanasihi hao kuna mas-lahi kwa Uislamu na Waislamu. Pamoja na hayo alikuwa amelihifadhi moyoni mwake tukio la Ghadir kwa maana zake zote na lilikuwemo katika dhamira yake muda wote wa uhai wake, hivyo alipata fursa nzuri ya kulitoa na kulihuisha upya mpaka akawataka wengine walishuhudie mbele ya masikio na macho ya watu.
Tazama ni namna gani ilivyokuwa njia ya kuuhuisha ukumbusho huu wenye baraka, na yale yaliyomo miongoni mwa hekima kubwa kwa ajili ya kuisimamisha hoja juu ya Waislamu wale waliohudhuria kwenye tukio lenyewe na wale ambao hawakuwepo, basi lau Imam Ali angesema: "Enyi watu kwa hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu aliusia siku ya Ghadir Khum kuhusu Ukhalifa wangu", basi jambo hilo lisingekuwa na umuhimu katika nafsi za watu waliokuwepo hapo na wangehoji juu ya kunyamaza kwake kwa muda wote huo. Lakini yeye Imam Ali aliposema:"Namsihi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kila Muislamu ambaye alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema aliyoyasema siku ya Ghadir Khum (namsihi) asimame na ashuhudie", basi ikawa tukio hilo limenakiliwa kwa hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kupitia ndimi za Masahaba thelathini, kumi na sita miongoni mwao ni mashujaa wa Badri, kwa ajili hiyo Imam Ali akawa ameziba njia dhidi ya wapinzani na wenye mashaka na wale wenye kuhoji juu ya kunyamaza kwake kwa muda wote huo, kwani kunyamaza kwa watu hawa thelathini pamoja naye hali ya kuwa wao ni miongoni mwa Masahaba wakubwa mno dalili kubwa juu ya msimamo huu, na kwamba kunyamaza huko ndani yake mna maslahi kwa Uislamu jambo ambalo liko wazi.
UFAFANUZI JUU YA MASHAURIANO (SHURAA)
Katika maelezo yaliyotangulia tumeona kwamba Ukhalifa kwa mujibu wa kauli ya Mashia ni uchaguzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ubainisho wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) baada ya ufunuo unaofunuliwa kwake. Kauli hii inakubaliana kabisa na hekima ya Uislamu katika hukmu zake zote na sheria zake, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye yeye ambaye "Anaumba akitakacho na kuchagua, wao (viumbe) hawana hiyari" (Qur'an. 28:68) Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka ummati wa Muhammad (s.a.w.) uwe ni umma bora uliotolewa kwa watu, basi hapana budi uwe na uongozi wenye hekima, uongofu, elimu, nguvu, ushujaa, ucha Mungu na kutosheka katika nyanja za Imani. Jambo hili hawezi kulipata isipokuwa yule ambaye kateuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akamtengeza kwa sifa maalum zinazomstahiki kwa ajili ya utawala.
Mwenyezi Mungu anasema:"Mwenyezi Mungu anachagua wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu, bila shaka Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kuona." (Qur'an, 22:75) Na kama ilivyo ya kwamba Mwenyezi Mungu amewachagua Manabii, ndivyo hivyo hivyo (amewachagua) Mawasii, na bila shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:"Kila Nabii anaye wasii, nami wasii wangu ni Ali bin Abi Talib". Taz: Ibn Asakir As-Shafii Juz. 3 uk. 5, Manaqib Al-Khawarzami uk. 42, Yanabiul-Mawdddah uk. 79. Na katika hadithi nyingine Mtume (s.a.w.) amesema:"Mimi ndiyo mwisho wa Manabii na Ali ndiye mwisho wa Mawasii". Taz:Yanabiul-Mawaddah Juz. 2 uk. 3 akinakili toka kwa Ad-Dailami-Manaqib Al-Khawarzami Dhakhairul-'Uqba. Na kwa msingi huu basi, Mashia wameyasalimisha mambo yao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na hapakubakia yeyote miongoni mwao anayeudai Ukhalifa kwa nafsi yake au kuutamania, siyo kwa njia ya "Nassi" wala kwa kuchaguliwa, kwanza kwa kuwa "Nassi" inapinga uchaguzi na shuraa na pili ni kwamba "Nassi" imekwishapatikana kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuwahusu watu walioandaliwa na kubainishwa kwa idadi na majina yao,[82] hakuna mtu miongoni mwao anayeunyooshea shingo na ikiwa yuko atayefanya basi huyo ni muovu na ametoka katika dini.
Ama Ukhalifa kwa Masunni ni jambo la uchaguzi na makubaliano, na kwa ajili hiyo wamefungua mlango ambao haiwezekani kumfungia yeyote miongoni mwa watu wa umma huu, na akautamania Ukhalifa (baada ya kuufungua mlango huu) kila mtu aliye mbali na aliye karibu, kila mnyonge na mwenye nguvu na hatimaye ukageuka kutoka kwa Maquraishi mpaka kwa watumwa na waliopewa uhuru,Wafursi na wafalme hadi kwa Waturuki na Wamongolia.
Na zile sharti walizoziweka kuhusu Ukhalifa zikatoweka, kwani mtu asiye Maasum amejaa(sifa ya) upendeleo, wema na ubaya, hivyo basi kiasi tu cha yeye kuupata utawala hawezi kusalimika na kisha kugeuka na kuwa mbaya zaidi kuliko alivyokuwa, na historia ya Kiislamu ndiye shahidi bora wa haya tuyasemayo. Nachelea baadhi ya wasomaji watadhani kwamba mimi natia chumvi, basi haiwalazimu ila kuisoma ( na kuichambua) historia ya kizazi cha bani-Umayyah na bani- Abbas na wengineo ili wafahamu kwamba kuna (miongoni mwa hao) yuko aliyejiita kuwa ni Amirul-Muuminina. huyu alikuwa akinywa pombe wazi wazi, akichezea tumbili na kuwavisha dhahabu. Yuko mwingine naye alimvalisha mjakazi wake mavazi yake ya kiume ili awasalishe Waislamu, na kuna mwingine aliyejiita Amirul-Muuminina, mjakazi wake aliyempenda mno alipofariki, akili zake zilimruka, na kuna Amirul-Muuminina mwingine yeye alikuwa akifurahishwa na mashairi kisha anabusu uume wake.
Basi ni kwa nini tuzame zaidi juu ya habari za watu hawa ambao waliwatawala Waislamu, kwani wao hawawakilishi isipokuwa ufalme wenye matatizo na wala hawawakilishi Ukhalifa, na hilo ni kutokana na hadithi ambayo wanaisimulia (wao Masunni) ambayo ni kauli ya Mtume (s.a.w.) isemayo: "Ukhalifa baada yangu ni miaka thalathini kisha utakuwa Ufalme" Na hii siyo maudhui ya uchambuzi wetu (tunaoufanya) basi mwenye kutaka kufahamu zaidi juu ya hilo na arejee Tarikhut-Tabari, Tarikhu Ibn Athir, Abul-Fidaa na ibn Qutaybah na wengineo.
Nami hapa nilitaka tu kubainisha ubaya wa kuchagua na ubaya wa nadharia hii katika misingi yake, kwani tumchaguaye leo huende kesho tukamkosoa na ikatubainikia kwamba tumekosea na hatukuchagua vizuri-kama yalivyomtokea hayo Abdur-Rahman bin Auf wakati alipomchagua Uthman bin Affan kwa ajili ya Ukhalifa na baadaye akajuta, lakini majuto yake hayakuusaidia chochote umma baada ya kuangamia, basi kama sahaba Mtukufu miongoni mwa kundi la kwanza ambaye ni Uthman anashindwa kutekeleza ahadi aliyompa Abdur-Rahman bin Auf, na pia itakapokuwa Sahaba Mtukufu miongoni mwa kundi la mwanzo ambaye ni Abdur-Rahman bin Auf anashindwa kuchagua vizuri, basi haiwezekani kwa mwenye akili baada ya hayo kukubaliana na nadharia hii butu, nadharia ambayo hapakuzalikana kutokana nayo isipokuwa vurugu na kukosekana utulivu na (hatimaye) kumwagika damu.
Hivyo basi ikiwa baia ya Abubakr ilitimia ghafla kama alivyoieleza Umar bin Khatab na kwamba Mwenyezi Mungu aliikinga shari yake kwa Waislamu na waliikhalifu na kuipinga Masahaba wengi, na iwapo pia Baia ya Ali bin Abi Talib baada ya hayo iliyofanyika mbele ya macho ya watu wengi, lakini baadhi ya Masahaba walitengua baia hiyo na ikasababisha jambo hilo kuleta vita vya Jamal, vita vya Siffin na vita vya Nah-rawan, ambapo roho nyingi zisizo na makosa zikateketea, basi ni vipi atairidhia mwenye akili baada ya yote haya hii kanuni ambayo ilijaribiwa na ikashindwa vibaya tena haraka tu mwanzoni mwake na ikawa na matokeo mabaya kwa Waislamu? Na hasa pale tutakapofahamu kwamba hawa wasemao juu ya Shuraa, wanamchagua Khalifa kisha baada ya hapo wanashindwa kumbadilisha au kumuuzulu, na bila shaka Waislamu walijaribu kwa juhudi zao kumuuzulu Uthuman lakini alikataa akasema: "Siwezi kuvua kanzu aliyonivalisha Mwenyezi Mungu".
Na miongoni mwa mambo yanayotufanya tuzidi kuichukia nadharia hii, ni mambo tuyaonayo leo katika madola ya Magharibi yaliyoendelea, yanayodai kuwa na demokrasi katika kumchagua rais wa nchi, utaona vyama vingi vinagombea na kulumbana na kushindana ili kupata kiti cha utawala kwa gharama yoyote ile, na hutumika katika kazi hiyo mabilioni ya mail ambayo huhusishwa kwa ajili ya kampeni kwa kila njia, na hupoteza nguvu kubwa ya wanyonge miongoni mwa raia masikini ambao huenda wakawa na haja kubwa ya mail hizo, na mara mmoja wao anapofikia kwenye cheo cha urais basi upendeleo huwa unamchukua akawatawalisha wasaidizi wake na wajumbe wa chama chake na marafiki zake na nduguze, huwapa vyeo vya uwaziri na majukumu makubwa na sehemu nyeti katika idara, na wengine waliobaki huanza kumpinga katika kipindi cha urais wake ambacho waliafikiana (kumpa) na hapo huwa wanazusha uchochezi na hujaribu kwa juhudi zao kumuumbua na kumuangamiza, na katika yote hayo ni hasara tupu kwa raia wanaotawaliwa.
Basi ni mara ngapi watu wema wameangushwa na ni mara ngapi mashetani waovu wamenyanyuliwa kwa kutumia uhuru wa demokrasia chini ya vielelezo vizuri hatima yake liwat ikawa ni kanuni ya kisheria na zinaa badala ya kuoa ikawa ni maendeleo, na mambo kama haya yasemwe na hapana ubaya. Basi utukufu ulioje wa Aqida ya Shia pale wasemapo kuwa Ukhalifa ni msingi katika misingi ya dini, na ukoje Utukufu wa kauli yao kwamba cheo cha Ukhalifa ni uchaguzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hii ni kauli ya sawa kabisa na rai iliyoongoka inakubaliwa na akili na dhamira (na nafsi) hupoa. Kauli hiyo inaungwa mkono na maandiko yatokayo ndani ya Qur'an na sunna, pia inawakatisha tamaa wengine wenye mabavu, wafalme na masultani na inaeneza utulivu na amani katika jamii.