JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI
MAKALA NO: (8)
MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR
WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU
Kama tulivyoahidi wiki iliyopita, leo tunaanza kuwajibu Ahlu-Tawheed kwa waliyoyaandika katika makaratasi yao waliyoyapa jina la "Uzushi na Shirk Ndani ya Barzanji na Vitabu Vyengine vya Maulidi".
Katika makaratasi yao hayo, ndugu zetu hao wamenukuu baadhi ya maneno yaliyomo katika Barzanji na Burdah (vitabu viwili vinavyoeleza sifa za Mtume Muhammad s.a.w.w.) na kujaribu, kadri ya ujuzi na uweza wao, kuonyesha kwamba kusema maneno hayo ni shirki. Lakini, kabla ya kutoa majibu yetu, tuanze kwa kuyanukuu maneno yenyewe. Nayo ni mane yaliyotolewa katika Barzanji, na mawili katika Burdah.
Katika Barzanji wameyatoa yanayofuata:
1. "Na kama si yeye (Mtume s.a.w.) asingekuwa Alkhalilu (Ibrahim) na Adam. Na Musa (asingekuwepo) na Issa, bali hata Mulku Suleimani (usingekuwepo)."
2. "Ilisemekana alipotaka Mwenyezi Mungu, Mwenye Ezzi na Alietukuka, kumdhihirisha Mbora wa viumbe vyake, Muhammad, Rehma na Amani za Mwenyezi Mungu zimfikie. Akamuamrisha Jibril achukue Udongo wake (wa kumuumbia nao) kwenye mahali pa kaburi lake karimu".
3. "Alikuwa Mtume akikua mchana mmoja kama anavyokua mtoto mwengine kwa mwezi mzima kwa ajili ya kushughulikiwa na Mwenyezi Mungu".
4. "Akamwonyesha kwa haya macho ya kichwani (ya usoni) aliyomwonyesha. Nayo ni yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu."
Na katika Burdah wameyatoa yanayofuata:
5. "Kama si yeye (Mtume s.a.w.w.) usingetoka ulimwengu (usingeumbwa)."
6. "Haukupata kunipiga vita Ulimwengu, nikataka nusra kwa Mtume, ila huipata tu."
Hayo ndiyo maneno waliyoyanukuu ndugu zetu wa Ahlu-Tawheed kuthubutisha kwamba, katika vitabu hivyo, muna shirki. Wakayaandamiza, pia, na hujja zao za kuyabatilisha hayo.
MAJIBU YETU :
Kwanza; tukumbuke kwamba tunalojadiliana si kuwa, katika vitabu vya maulidi, muna shirki au hamuna; la! Tunalojadiliana ni: maulidi ni bid'a au si bid'a; ni haramu au si haramu? Sisi, kwa upande wetu, katika makala yetu sabaa yaliyopita, kwa kujibu hujja zinazotolewa na wapinga maulidi, tumeonyesha kwamba maulidi si bid'a wala si haramu. Kwa hivyo sasa tunalolingojea kwa wapinga maulidi, wakiwamo Ahlu-Tawheed, ni majibu yao ya hujja tulizozitoa -- kiilimu na kimantiki, kama tulivyofanya sisi.
Pili; hata kama itakubaliwa kuwa hayo maneno waliyoyanukuu ni shirki -- na hilo hatulikubali kwa hujja tunayoitoa hapa chini -- hilo haliwi ni hujja ya kuharamishia maulidi au kuyasusia. La sawa kufanywa hapo ni kuyatoa hayo yanayoonekana ni shirki na / au kuyasahihisha; si kuzuia watu kuyasoma. Hivyo, kwa mfano, ndivyo alivyofanya marehemu Sheikh Abdulla Swaleh Farsy katika Wasila wa Nabahani. Yeye alipoona kwamba "Lawlaahu maa kunnaa walaa baaqiina" si sawa, hakuzuia watu, wala yeye hakuacha kuusoma. Alichofanya ni kukibadilisha kipande hicho na kukisoma alivyoona yeye ni sawa: "Lawlal ilaahu" Hakuutupa wasila wote, wala hakuzuia watu kuusoma kwa sababu tu muna kipande cha maneno asiyoyakubali.
Tatu; tunapoyataamali yote madondoo sita waliyoyanukuu Ahlu-Tawheed, ambayo nasi tumeyanukuu hapo juu, hakuna hata moja liwezalo kusemwa ni shirki kwa hujja ifuatayo:
Shirki ni kusema / kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ana mwenziwe, au ana aliye sawa naye, au ana mfanowe, au ana anayetokana naye. Pia kusema / kuamini kuwa yuko muumbaji mwengine wa ulimwengu asiyekuwa Yeye, au muendeshaji (mudabbir) ulimwengu asiyekuwa Yeye, au mwenye haki ya kuweka sharia asiyekuwa Yeye, au anayelazimika kutwiiwa asiyekuwa Yeye, au kuna mtawala (haakim) asiyekuwa Yeye, au kuna mwenye haki ya kuabudiwa asiyekuwa Yeye.
Kwa kuwa hakuna hata moja, ya madondoo sita waliyoyanukuu Ahlu-Tawheed kutoka katika Barzanji na Burdah, linalosema hivyo, vipi basi mutakuwa muna shirki? Kama lipo, tunaomba watwambie ni dondoo lipi kati ya hayo waliyotutajia, na linaingia wapi katika hiyo taarifa ya shirki tuliyoieleza sisi hapo juu. Kama taarifa yetu imeacha mengine yaliyo shirki, basi tunaomba tukumbushwe. Kwa hakika haikuwa nia yangu kuingia katika masiala ya shirki kwa sababu hilo li nje ya maudhui yetu. Maudhui yetu ni maulidi ni bid'a au si bid'a; ni haramu au si haramu. Na hilo tushalijibu vya kutosha. Lakini, kwa kuwa wafuasi wa madhihabi ya wapinga maulidi hupenda kukibandika jina la bid'a au shirki kila wanachokipinga wao, nimeona japo kwa ufupi niwaeleze wasomaji wangu jamaa zetu hao hupotelea wapi katika kuielewa shirki ni nini, na si nini! Hilo, inshallah, tutalishughulikia wiki ijayo, kabla ya kuwajibu "Wakereketwa wa sunna Malindi".
ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA
8 Jamaadal Uulaa, 1423
19 Julai, 2002
9
JAWABU KWA WAPINGA MAULIDI
MAKALA NO: (9)
MUANDISHI NI: SEHIKH ABILLAHI NAASIR
WANAVYOSEMA WAPINGA MAULIDI NA MAJIBU YETU
Wiki iliyopita tuliyataja maneno ambayo Ahlu-Tawheed wameyatoa katika Barzanji na Burdah ambayo, kwa maoni yao, ni shirki. Tukaahidi kuyajadili maoni hayo leo, baada ya kuieleza shirki ni nini.
Kwa taarifa tuliyoitoa sisi (na tumeomba tuelezwe kama tumeacha kitu katika taarifa hiyo), kati ya madondoo sita yaliyonukuliwa na ndugu zetu hao, matano yametushinda kuelewa vipi yaweza yakawa ni shirki. Kwa hivyo hatutashughulika nayo kwa leo mpaka hapo tutakapofafanuliwa inshallah. Tutakaloshughulika nalo leo ni moja tu lililobaki ambalo, kwa hujja walizozitoa kulipingia, tumeweza kulifahamu lililowafikirisha wao kuwa ni shirki. Nalo ni lile la Buswiri kusema katika Burdah: "Haukupata kunipiga vita Ulimwengu nikataka nusra kwa Mtume ila huipata tu."
Kulikosoa hilo, Ahlu-Tawheed wameitaja Sura 3:126 ambayo wameifasiri hivi: "Na msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Mwenye hikima". Kwa kuitaja aya hii, kwa hivyo, tumeelewa kwamba ndugu zetu hao wameyaelewa maneno ya Buswiri hivi: "Kwa kuwa msaada (nasr) hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kuuomba kwa mtu mwengine yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, hata awe ni Mtume (s.a.w.w.), ni sawa na kumfanya mtu huyo ni Mwenyezi Mungu! Na kufanya hivyo ni shirki; kwa hivyo katika Burdah muna shirki!"
MAJIBU YETU :
Kwanza; katika tafsiri yao ya hiyo Sura 3:126 wameongeza maneno katika pinde, tuliyoyachapa kwa italiki, ambayo hayamo katika aya hiyo, wala hayaipunguzii maana lau yasingeongezwa.
Pili; kama maana ya "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu" ni kwamba haturuhusiwi kutafuta msaada kwa asiyekuwa Yeye, au asiyekuwa Yeye hana msaada wa kuutoa, basi ilikuwaje watu wa Madina wakaitwa answaar (wasaidizi)? Walimsaidia nani? Huyo aliyesaidiwa, aliukosa msaada wa Mwenyezi Mungu hata wakaingia kati wao? Na sisi Waislamu, pamoja na Mtume wetu (s.a.w.w.), tunamshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kuwaita answaar watu wa Madina?
Tunaposoma Sura 3:81 tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyochukua ahadi kwa Mitume Yake kwamba itamsaidia / itamnusuru (latansurunnahuu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu," ilikuwaje hapo, Yeye Mwenyewe, akautaka kwa asiyekuwa Yeye? Jee, kwa kitendo hicho, Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali! -- alikusudia kuifanya Mitume Yake ni miungu?
Katika Sura 7:157, kati ya sifa za waumini ambao "ndio wenye kufaulu", ni wale ambao wamemsaidia / wamemnusuru (wanaswaruuhu) Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa nini akawaagiza waumini wamsaidie Mtume Wake? Kwa sifa hiyo hapo, ndio Mwenyezi Mungu amewafanya waumini kuwa ni miungu? Mwenyezi Mungu -- Mwenyezi Mungu apishe mbali -- hapo amefanya shirki?
Hali kadhaalika; tunaposoma Sura 28:15 tunaona jinsi jamaa yake Nabii Musa (a.s) "alivyomuomba msaada" (fastaghaathahuu) juu ya adui yake. Jee, Nabii Musa (a.s) alimrukia jamaa yake huyo, na kumwambia asilete shirki kwa kumuomba yeye msaada badali ya Mwenyezi Mungu? La! Alimsaidia; na siku ya pili (Sura 28:18) yule aliyeomba msaada jana (istanswarahuu) akamuomba tena! Jee, kama "msaada hautoki (kwa mwengine yoyote) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu", kwa kutoa msaada wake huo, Nabii Musa (a.s) alikuwa Mwenyezi Mungu, au hakujua kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"?
Kwa kutaja mifano hiyo hapo juu, sisi tusomao maulidi hatukusudii kukanusha yaliyomo katika aya iliyotajwa na wapinga maulidi, kuwa "msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu"; hasha! Tunalokusudia ni kufahamisha kwamba: maneno yanapofanana, si lazima na maana yafanane (yawe mamoja). Kwa hivyo, msaada ambao Buswiri aliuomba kwa Bwana Mtume (s.a.w.w.), na sisi huukariri tunapoisoma hiyo Burdah, sio msaada ambao huombwa kwa Mwenyezi Mungu. Ni majina tu kufanana -- kama ulivyokuwa ule ambao Mwenyezi Mungu alimtakia Mtume Wake kwa Mitume mengine, na aliotutaka sisi waumini tumpatie Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na ambao watu wa Madina walimpatia Bwana Mtume (s.a.w.w.) hata wakaitwa answaar (wasaidizi wake), na ule ambao Nabii Musa (a.s) alimpatia jamaa yake.
Msaada wa Mwenyezi Mungu unatokana na Yeye Mwenyewe; hakupawa na yoyote uweza huo wa kusaidia. Lakini wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, akiwamo Mtume Muhammad (s.a.w.w.), si wake mwenyewe; ni wa kupawa (kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu). Na hapo ndipo palipo na tafauti baina ya shirki ni nini, na si nini.
Ukiamini kwamba Mtume (s.a.w.w.) -- yeye mwenyewe, bila ya kupawa uweza huo na Mwenyezi Mungu -- aweza kusaidia; hiyo ni shirki. Na hilo silo alilokuwa akiliamini Buswiri, wala silo tunaloliamini sisi tusomao maulidi. Lakini ukiamini kuwa msaada uwezao kupawa na Mtume (s.a.w.w.) ni ule aliowezeshwa yeye na Mwenyezi Mungu; hiyo si shirki. Na hilo ndilo alilokusudia Buswiri katika Burdah, na ndilo tunaloliamini sisi tunaosoma maulidi. Kwa hivyo kubwa ambalo wapinga maulidi waweza kutwambia sisi ni kuwa Mtume (s.a.w.w.) hakuwa / hana uweza huo; kwa hivyo ni kazi bure kumuomba hivyo -- jambo ambalo hatulikubali kwa sababu ya hujja tulizonazo. Lakini hawawezi kutwambia ni shirki, kwa mifano mingi tuwezayo kuwatolea katika Qur'ani Tukufu.
Inshallah wiki ijayo tutaeleza kwa urefu ni wapi ambapo wapinga maulidi hupotea na kukosea kuielewa shirki. Nataraji baada ya hapo wataweza kuyaelewa yaliyomo katika Barzanji na Burdah.
ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA
15 Jamaadal Uulaa, 1423
26 Julai, 2002
10